Jumatatu, 29 Aprili 2024

Uamsho: Upendo wa Kwanza


Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”



Utangulizi:

Nyakati hizi tulizo nazo ni nyakati za mwisho, maandiko yanasema mwisho wa mambo yote umekaribia 1Petro 4:7 “Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.” Katika nyakati hizi za mwisho nabiii nyingi zinazozungumziwa kama dalili za mwisho wa dunia zimekaribia,   Na ndio maana Petro anatukumbusha kuendelea kukesha yaani kudumu katika maombi, kuwa macho na kuongeza umakini. Moja ya unabii mkubwa unaoonyesha kuwa tuko katika wakati wa mwisho Yesu alisema licha ya kuongezeka kwa maasi lakini tunaelezwa kuwa Upendo wa wengi utapoa 

Mathayo 24:10-12 “Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.”

Upendo wa wengi kupoa pia ina maana ya kwamba kutokana na kuongezeka kwa maasi na uwepo wa manabii wengi wa uongo watu wengi watapoteza upendo wa kweli kwa Mungu na wanadamu, au tunaweza kusema upendo kwa Mungu na kwa kanisa lake, na matokeo yake ni kuwa katika nyakati hizi za mwisho ambazo shetani ataongeza kasi ya utendaji wake kazi, moja ya njia kubwa sana atakayo itumia ni kuhakikisha ya kuwa ile hamu na shauku ya kumuabudu Mungu na hata kumtumikia Mungu, kasi hiyo itapoa, na hapo ndipo tunaposema kuwa kanisa limepoa, au kanisa limelala au kanisa limekufa na linahitaji uamsho!

Kwa msingi huo basi katika somo hili lenye jina Uamsho: Upendo wa Kwanza tutachukua muda kujifunza na kutafakari kwa makini na kwa undani sana maswala yahusuyo uamsho na namna ya kuleta uamsho katika makanisa yetu; Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufuatilia somo hili kwa umakini katika jina la Yesu Kristo Amen!, Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya Uamsho

·         Namna ya kujua kama unahitaji uamsho

·         Jinsi ya kurejesha uamsho


Maana ya Uamsho:

Kimsingi sio rahisi kupata neno uamsho moja kwa moja kutoka kwenye Biblia, lakini tunaweza kuliona neno uamsho katika namna isiyokuwa ya moja kwa moja kama tunavyoweza kuona katika mstari wetu wa Msingi ona

Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Neno uamsho kibiblia linaweza kabisa kufananishwa na neno kuurudia upendo wa Kwanza, kama tunavyoweza kuona wito wa Bwana Yesu katika waraka wake kwa kanisa la Efeso kupitia Yohana katika kitabu cha ufunuo, Yesu aliliona Kanisa la Efeso kama Kanisa lililokuwa na uvumulivu, yaani subira, kwa ajili ya jina lake tena anawaona ya kuwa hawakuzimia moyo, lakini aliwaona pia kuwa upendo waliokuwa nao kwanza umepoa na ndio maana anawalaumu kuwa wameuacha upendo wa Kwanza, na kuwataka kufanya matendo yale ya kwanza, vinginevyo watapata adhabu! Wasipogeuka na kutubu, kihistoria kanisa la Efeso lilianza na wanafunzi 12 tu ambao kimsingi walikuwa hawajajazwa Roho Mtakatifu, na Paulo mtume alipofika hapo watu hao waliombewa na kumpokea Roho Mtakatifu, mahali hapo Mungu alimtumia Paulo mtume kwa miujiza mikubwa isiyohesabika, tena miujiza inayoitwa ya kupita kawaida, watu waliokolewa kwa wingi katika mji huu na watu waliotumia mambo ya uchawi na uganga walichoma vitabu vyao kukawa na uamsho mkubwa sana jina la Yesu likatukuzwa

Matendo 19:1-7 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.”

Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”

Matendo 19:17-20 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Unapoyaangalia maandiko hayo yanakuonyesha wazi kuwa Kanisa la Efeso lilikuwa ni moja ya Kanisa lenye nguvu kubwa sana, watu walijazwa Roho Mtakatifu, miujiza ya kupita kawaida ilitendeka, hofu ya Mungu iliushika mji mzima neno la Mungu lilipata nguvu, Kanisa la Efeso lilianzishwa katika mwaka wa 52-54 AD Baada ya Kristo, Lakini unaweza kuona kuwa wakati Yesu anawaandikia waraka katika mwaka wa 95-100 AD ni muda wa miaka kama 40 hivi au 41 Kanisa lilikuwa tayari limepoteza hali yake ya kwanza, yaani limeuacha upendo wa kwanza na Yesu analiita kutubu, kanisa lilikuwa limepoa, kanisa lilikuwa limelala kanisa lilikuwa linahitaji uamsho! Je Kanisa lenu lina miaka mingapi sasa? Kama nyakati za kanisa la kwanza miaka 40 tu watu walikuwa wameanza kupoa je kanisa lenu linahitaji miaka mingapi sasa ili mjue ya kuwa limepoa? Baki na jibu lako moyoni!  Je ni vibaya kuliamsha? je huoni ya kuwa mnahitaji uamsho? Uamsho ni nini Hasa?

-          Neno uamsho  kwa kiingereza linatumika neno REVIVAL ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni Restoration to life, consciousness, vigor, strength  au awakening in the church or community of interest and care for matters relating to Personal religion

-          Kwa hiyo Uamsho kurejesha kwenye uhai, kufufua, dhamiri, au kuamsha nia ya mtu asiyejitambua ajitambue, au kurejesha nguvu zilizopungua au kupotea

-          Uamsho ni kufufua Habakuki 3:2 “Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.” Neno la kiingereza linalotumika kuhusu Fufua ni neno REVIVE katika kiebrania neno hilo linasomeka kama CHAYAH  (  חיק    ) ambalo maana yeke ni REPAIR   sawa na neno UKARABATI katika Kiswahili au kuhuhisha

-          Yesu anatumia neno kurejesha upendo wa kwanza, hii maana yake ni nini hasa?

Wengi wetu tulipompokea Yesu kwa mara ya kwanza, tulijawa na furaha kubwa sana, tulijisikia huru, tulijiona wepesi ni kama Yesu ameondoa mizigo Fulani iliyokuwa inatuelemea, tulijawa na upendo mkubwa sana kwa Mungu na tulihisi kuwa tuko karibu sana na Yesu! Mioyo yetu ilijawa na kiu na  hamu na shauku, ya kutaka kumtumikia Mungu, tulisoma neno la Mungu kwa nguvu na mioyo yetu yote, tulihudhuria ibada bila kukosa huku tukitoa kipaumbele kwa ibada kuliko kitu kingine, tulikuwa waombaji, tulihudhuria mikesha, tulishuhudia habari njema na kuwaleta wengi kwa Yesu, tulikuwa na mijadala ya kidini na ndugu na jamaa zetu,  hatukuweza kutulia, tulijawa na wivu kwa ajili ya Mungu, tulifuatilia watoto wachanga kiroho, tulitembelea magerezani, mahospitalini, wagonjwa, yatima na wajane, tulijali mambo ya Mungu, tulitoa bila kusukumwa, hata ndoto na maono yetu yalikuwa ya kimbingu,  maisha na mwenendo wetu haukuwa na mashaka watu walikuwa na kiu na hamu na shauku ya kuwa kama Yesu Kristo!, Nyimbo zetu zilikuwa nataka kuwa kama Yesu moyo wangu, nataka kuwa kama Yesu maisha yangu!  Hali hii ndio inaitwa upendo wa Kwanza, ni kama Uchumba au ndoa inavyokuwa mwanzoni, kila mmoja anavyojitoa kwa mpenzi wake hali hiyo ndiyo inaitwa upendo wa Kwanza! Kila mmoja wetu alikuwa nayo, na makanisa yetu mengi yalikuwa hivyo, Pepo walikuwa wakiwatoka watu wenyewe wakati wa kusifu, au hata kwa kuwepo tu kanisani, kabla hata ya kukemea kwa nguvu udhihirisho wa Mungu ulikuwa ni kitu cha wazi wazi! huo ndio, watu walikuwa na kiu ya kutenda haki, hakukuwa na majivuno, hakukuwa na kiburi, hakukuwa na ukaidi, utii ulikuwa wa hali ya juu, hakukuwa na upendeleo makanisani, hakukuwa na ukabila, hakukuwa na ugomvi wala mafarakano, hakukuwa na kupindishwa kwa haki, wala dhuluma, wala wivu, wala kubaniana, wala hakukuwa na urasimu, Mungu alikuwa akisema wazi wazi na watu wake hata kwa unabii, karama za Roho Mtakatifu zilidhihirika!  Je mambo hayo yapo? Wakati huo hakukutumika sana mafuta wala visaidizi vya kiroho, hatukujua chumvi, wala maji ya Baraka (sisemi kwamba kutumia vifaa vya kiroho ni vibaya) lakini visaidizi vya kiroho hutumiwa na watu ambao Imani imeshuka sana yaani wenye Imani ya kawaida kwaajili ya kuinua Imani zao, Wakati wa uamsho mkubwa sisi tulilijua jina la Yesu tu! Huo ndio uamsho!  Jina la Yesu lilikuwa ni utoshelevu mkubwa kwa kutamka tu  wakati wa uamsho watu walifanya maamuzi magumu,Watu waliacha kazi Redioni, ili tu wasipige miziki isiyompendeza Mungu, watu walifunga baa zao, watu waliacha kuuza sigara huo ndio ulikuwa uamsho!  Watu waliuza nyumba zao na mali zao kwaajili ya injili, Watu walikuwa wakiokolewa na wokovu ulikuwa una vita kali sana katika ngazi za familia na jamii, watu walikuwa na msimamo mkali hiyo ndio ilikuwa hali ya uamsho, watu walijitenga na dunia wala hawakufuatisha namna ya dunia hii katika usemi, menendo Imani na ufasi, haki ilitendeka kila mahali watumishi walizaa watumishi, watu walikuwa kiroho kwa haraka, kazi ya Mungu ilisonga mbele na Mungu alidhihirika wazi wazi kati ya watu wake!

Ni Muhimu kufahamu kuwa Kanisa linapokuwa na nguvu kubwa namna hii, maana yake ufalme wa Shetani unapata taabu sana, na shetani hawezi kukubali kirahisi ashambuliwe na watu wake kuchukuliwa mateka kwenda upande wa  ufalme wa Mungu, na ndio maana mara baada ya mtu kuokolewa yeye anaanza kuwa na mipango mikakati ya kuhakikisha kuwa anawarejesha nyuma au katika ufalme wake wale wote ambao wametekwa kwenda upande wa ufalme wa Mungu, shetani anajua wazi kuwa ni kazi ngumu kuwarejesha mateka wake katika mikono ya Mungu

Yohana 10:27-29 “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”

Kwa hiyo mbinu kubwa anayoitumia shetani ni kuhakikisha kuwa watu wa Mungu wanapoa, wanakinai, wanachoka, wanapoteza tumaini, wanakosa upendo, shauku na hamu ya kumpenda Yesu, Shetani hatakurudisha nyuma kwenye dini yako ya zamani, lakini anakufanya usiwe na madhara katika ufalme wake huku ukiwa katika ufalme wa Mungu,  atahakikisha kuwa unabaki kama Mtumishi au Mkristo asiye tishio katika ufalme wa ibilisi, hutaomba tena, hutakuwa mshabiki wa mikesha, huoni umuhimu wa kuhudhuria ibada husikilizi nyimbo za injili tena na huna madhara kwa wasiookoka wala kwa shetani mwenyewe huko ndiko kuuacha upendo wako wa kwanza ndio kupoa! Atakuacha shetani uwe vuguvugu, atakuacha ufungiwe nira na wasiamini, atakuacha uwe na urafiki na giza, atakuacha uipende dunia, haijalishi uko katika kanisa gani wala haijalishi kuwa uko na mtumishi wa kiwango gani cha kiroho utapoa tu

2Timotheo 4: 9-10 “Jitahidi kuja kwangu upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.”                 

Kwa msingi huo ni muhimu kila mtu na kila kanisa kujihoji na kujiuliza kama wako salama au la? Na ni vigumu sana kwa kanisa au mkristo aliyepoa kukubali kuwa amepoa au amekufa kiroho, lakini swala la msingi la kujiuliza ni je bado tunampenda Yesu kwa kiwango kile kile?, je tunatafuta ufalme wa Mungu kwanza na haki yake? Je tuna upendo wa kweli na ushirika wa kweli kwa na ndugu zetu katika Bwana? Je tunashuhudia matunda ya Roho katika maisha ya wakristo na watumishi wa Mungu leo? je ziko nguvu za Mungu katika maisha yetu na kanisa letu?, Leo hii imefikia hatua hata wachwi wanaabudu katika makanisa ya kiroho, watu wa Mungu pia wanarogwa! Niliwahi kumsikia Mchungaji mmoja akilalamika kuwa wachawi wanakopera sadaka katika Kanisa Lake! Mpaka aliposimama na kukemea kwa midomo yake kuwa waache tabia hizo ndio sadaka zikaongezeka! Sikumjibu lolote nilikuwa na mke wangu hakua aliyesema kitu pale lakini tulipofika nyumbani tulianza kujiuliza, kama Askofu yule angeliruambia sadaka zinaibiwa angalau akili yangu ingeweza kuwa na Amani, kwamba wako wezi ambao hawana hofu ya Mungu wameingia makanisani, lakini hebu fikiria wachawi wanakopera sadaka katika kanisa la kiroho? Ni jambo la kusikitisha sana, ni lazima kanisa lirejee, lirudi mahali pake mahali ambapo limejengwa na malango ya kuzimu hayataliweza! Na msingi huo ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai!, Je hali ya kanisa lenu wewe na hali yakow ewe mwenyewe na hali ya wenzako na zamani zile ikoje? Yako makanisa ukiokoka leo na ukawa wa moto sana wenzako waliokutangulia utasikia kaka ana moto sana dada ana moto sana aaa ni uchanga tu atapoa sasa hivi Je umewahi kusikia hali kama hiyo?

Marko 12:30 “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.”

Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

1Yohana 1:7 “bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

1Yohana 4:20-21 “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.”

Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Kama maswali yote tuliyojiuliza hapo juu yanatoa jibu hapana au kuna upungufu basi ukweli ni kuwa tunahitaji uamsho! au kwa lugha nyingine ni kuwa tumepoa au kanisa lisilo na hayo au lenye mapoungufu kuhusu hayo limepoa limekuwa la baridi na sio la moto tena moto umezimika au moto umefifia kwa hiyo tunahitaji uamsho!       

Namna ya kujua kama unahitaji uamsho;

Ni vigumu watu, mtu au kanisa lolote lile kukubali kuwa limelala, au limepoa na linahitaji uamsho lakini ni rahisi kujijua kama tuna uamsho au la kwa kujiuliza maswali kadhaa Muhimu, maandiko hayakatazi kujitathimini, na kujijaribu wenyewe ili kujua kama tumekuwa katika Imani au lahasha

2Wakorintho 13:5 “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa.”

Tunawezaje kujua kama tuko vema au la Maswali kadhaa yajayo yatasaidia kujitambua tuko hai kiasi gani au tuko hoi kiasi gani

1.       Je tunampenda Mungu kuliko Kazi zetu, familia zetu, biashara zetu, anasa zetu na mambo yetu?  Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

 

2.       Kumnung’unikia Mungu na watumishi wake katika kila hali unayokutana nayo katika maisha 1Wakorintho 10:10 “Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.”

 

3.       Tunapenda sifa za wanadamu? Tunapenda kusifiwa kwa kila tendo jema?, tunapenda kutukuzwa sisi kuliko Kristo? Yohana 12:42-43 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.”

 

4.       Kuwa na uchungu, kukosa uvumilivu kwa wengine, kukosoa wengine, kuwa mkali sana ukikosolewa, wivu kwa wengine na kutokutaka mafanikio ya wengine, kukomoa wengine na kufurahia tunapoona wanaharibikiwa?  Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”

 

5.       Kukwaza wengine, kupenda mabishano, kujiona uko sawa wakati wote, mkali sana kwa wengine, kujisikia vibaya wengine wakifanikiwa, kuogopa watu watasemaje, kufurahia watu wengine wanapokwama, au kuanguka, kukosa kabisa matunda ya roho na kujaa matunda ya mwili, kutokusemeshana, dhuluma, majungu, hila, fitina, uzushi, husuda yaani ni matunda ya mwili tupu, Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

 

6.       Kukosa uaminifu, kutokuwa mkweli, kusema uongo, kuficha maovu, kujitahidi kujipa raha ili hali huna raha, wala Amani, kuishi maisha ya kinafiki, kuwa na sura mbilimbili, Mathayo 23:27-28 “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”         

 

7.       Kusumbuliwa na mawazo, mgandamizo wa mawazo, kukata tamaa na kuacha kumtumaini Mungu Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”   

 

8.       Kuwa wakavu kiroho, kuwa wa kawaida sana, kutokushuhudia, kutokufanya uinjilisti, kuwa dhaifu kiroho, kuwa vugu vugu, kurudi nyuma Ufunuo 2:4-5 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

               

Ufunuo 3:15-16“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.”

 

9.        Kuanza kuifuatisha namna ya dunia hii, kuupenda ulimwengu, kuanza kufikiri, kusema na kutenda kama watu wa ulimwengu huu tu Warumi 12:1-2 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”       

 

10.   Kuacha kuomba, kuacha kushuhuhudia, kuacha kuhubiri injili, kuacha kuhudhuria ibada, kuacha kujali waliorudi nyuma, kuacha kusoma neno, kupuuzia karama za roho, kutweza unabii, kuwasumbua wenye vipawa badala ya kuwalea, kuacha kufundisha neno la Mungu, kuhubiri mafanikio ya mwilini zaidi kuliko maswala ya rohoni, na mkazo wa matumizi ya vifaa vya kiroho zaidi kuliko jina la Yesu, kukatisha tamaa watu wenye bidi katika bwana, kuwabania watumishi wa Mungu wenye vipawa, kumzimisha Roho Mtakatifu 1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho

 

11.   Kurudi kwa magonjwa mbalimbali makubwa ambayo zamani yalikuwa yakiwasumbua watu wa dunia hii Kutoka 23:25-27 “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.”    

 

12.   Endapo utaanza kuona uovu na uharibifu Habakuki 1:2-4 “Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.”             

 

Endapo kila mmoja na kila kanisa litajifanyia tathimini na kujichunguza kuona mapungufu yetu ukilinganisha na jinsi tulivyoanza wakati tunakutana na Yesu na tukibaini kuwa kuna mapungufu, basi mara moja tunaweza kufahamu kuwa tunahitaji uamsho bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na ufahamu na kuanza kuutafuta uamsho katika maisha yetu katika jina la Yesu Kristo.

 

Jinsi ya kurejesha uamsho

Uamsho ni kurejesha upendo, ule upendo wetu wa kwanza tuliokuwa nao kwa Yesu Kristo,  ni kurejea katika kila jambo ambalo tuliliacha na ambalo limeagizwa katika neno la Mungu, ni kurejesha afya ya kiroho ambayo imepungua katika maisha yetu na katika kanisa, na jambo la kwanza ambalo tunaweza kuanza nalo ni toba, na kuomba rehema za Mungu,  ujumbe wa toba hauna uhusiano na watu walioko nje, watu ambao hawajaokolewa ujumbe wao ni habari njema ya kuwa Yesu Kristo anaokoa, na hivyo wanapaswa kumuamini na kukubali kazi yake aliyoifanya msalabani kwaajili ya ulimwengu mzima, ujumbe wa toba ni ujumbe kwa kanisa  ni ujumbe kwa watu wa Mungu, wanaoambiwa watubu ni makanisa ni watu ambao walimjua Mungu na kisha wakaingia kwenye njia mbaya kwa hiyo unatolewa wito kwao kumrudia Bwana  na Mungu takapoona mioyo yetu iko tayari yeye ndiye anayeleta uamsho, bidi na jitihada za kibinadamu kamwe haziwezi kuleta uamsho!

Mathayo 26:40-43 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.”

Wakati wote wanafunzi walipokuwa wamelala ni Yesu ndiye aliyewaamsha, umasho hauwezi kuletwa na mwanadamu mwenyewe, yako maandalizi ya kawaida ya kufanya lakini mwenye kuamsha hiyo nia na hiyo hari ni Mungu mwenyewe kumbuka yale maombi ya nabii Habakuki. Habakuki 3:2 “Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.” Hata hivyo kama wanadamu tuna wajibu wa kufanya sehemu yetu na haya ndio tunayoweza kuyafanya!

Toba:

Ufunuo 2: 4-6 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia

Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile. Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”

2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

Marekebisho:

Toba haiwezi kuwa kamili bila kufanya marekebisho, au matengenezo, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaweka sawa pale ambapo tuliharibu, mfano kama ulidhulumu watu umetubu na watu hao wapo uerejeshe kile ulichodhulumu, uliazima vitabu Library (maktaba ya shule) na hujavirudisha rejesha, una mume ambaye si wako, au mke ambaye si wako mwachie aende kwa mmewe au mkewe,  swala la toba na malipizo katika makanisa mengi linachukuliwa poa, lakini ni fundisho halali na liko, umemkosea mtu usijikaushe tu nenda kaombe msamaha,  Kumbuka jinsi Yakobo alivyotafuta Amani kwa bidi kwa kaka yake Esau!, hakikisha hauna mtu moyoni mwako samehe, sahau achilia.

Mathayo 5:23-24 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.”

Luka 19:8-9 “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.”

Ezra 10:1-3 “Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana. Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.”

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

Maombi:

Maombi ni funguo muhimu sana katika kutafuta uamsho wa katika kanisa, unaposoma vitabu vingi sana vuinavyozungumzia uamsho huwezi kuona kuna mwandishi amewahi kuacha kuzungumzia maombi kuwa ni moja wapo ya nyenzo muhimu sana katika kuleta uamsho, ndio njia ya Imani, unyenyekevu, na yenye kuchochea mabadiliko, Mungu anatutegemea tumuombe ili aweze kuleta Baraka zake kwetu kwa mtu mmoja mmoja na kanisa zima kwa ujumla, maombi hayo ndiyo yanayohusisha toba,  na kutafuta rehema, na kutimiza kiu yetu ya kukleta uamsho, tunaweza kumuomba Mungu aokoe wengine, kuombea umisheni na uinjilisti, kuhitaji uwepo wa Mungu, karama na vipawa, nguvu za Roho Mtakatifu na mpenyo wa kiroho maombi maombi maombi

Matendo 1:12-14 “Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”    

Kufunga:

Kufunga ni njia ya kujitia nidhamu ya kiroho kwa kusudi la kujiungamanisha na Mungu, kumlingana Mungu, kuutafuta uso wake kwa bidii ili kwamba Mungu aweze kuingilia kati na kuleta badiliko tunalolikusudia, Kufunga kunaongezea nia yetu ya kuonyesha kuwa tunamtafuta Mungu kwa bidi hii ni kwa sababu kufunga huambatana na kuomba, kuomba kunajumuisha unyenyekevu, tafakari, na kutafuta mpenyo wa kirohoni nyenzo muhimu, yasiyowezekana katika hali ya kawaida yanaweza kusawazishwa kwa maombi ya kufunga, kufunga kufunga. Kufunga kulitumika kama njia ya kuonyesha kujidhabihu kama ibada ya kuutafuta uso wa Mungu lakini pia kwaajili au ikama njia ya kumrudia Bwana

Yoeli 2:12-14 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?              

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

Unyenyekevu:  watu wengi sana hawafahamu siri ya kuinuliwa na Mungu, Mungu anapendezwa sana na watu wanyenyekevu, anakaa yeye na watu wanyenyekevu na waliotubu, moja ya sababu ya watu wengi kuachwa na Mungu ni kwa sababu ya kiburi na majivuno, siku hizi hata makanisa ya kipentekoste wachungaji wanaitwa Baba! Na watu wanaona ni jambo la kawaida tu wala hawalikemei, Mungu hakai na watu wenye kiburi, watu wanaojifikiri kuwa bora zaidi kuliko wengine, na hata kujikinai wakiwadharau wengine kama tunataka uwepo wa Mungu na kukubaliwa na Mungu hatuna budi kuweka mbali kiburi na majivuno, na wakati wote tukiri ya kuwa tunahitaji neema ya Mungu

Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”                

1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake

Yakobo 4:5-6 “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

Luka 18:10-14 “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, WATAJINYENYEKESHA, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

Neno la Mungu:

Neno la Mungu ndio kiini kikuu cha uamsho, lenyewe ndilo ambalo hutumika kama nyenzo ya uamsho na mabadiliko, linakazia ukweli na kutuelezea kile kilichopungua kwetu na njia ya kufanya, wakati wa uamsho Kuhubiri na kufundisha huwa ni nyenzo muhimu ya wakati wote inayotumika kusema na mioyo yetu, lenyewe linafunua dhambi zetu, linatuonyesha njia na kutupa tumaini na namna ya kumtafuta Mungu na kudumisha uhusiano na yeye, Ezra alipata uamsho, kwa sababu alirudisha moyo wake kwenye mkazo au msingi wa uamsho huo ambao ndio neno la Mungu. Mitume nyakati za kanisa la kwanza walihakikisha kuwa wanabaki katika kulihudumia neno, hii ni kwa sababu walikuwa na ufahamu wa umuhimu wa kutunza uamsho na uwepo wa Mungu kwa kudumu katika neno

Ezra 7: 10 “Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.”

Matendo 6:3-4 “Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Utii kwa Roho Mtakatifu:

Roho Mtakatifu pekee ni Bwana wa uamsho, yeye nndiye anayeweza kuichochea mioyo yetu, na kutupa nguvu za kuwa mashahidi wa Mungu, kwa ujumla tunaweza kusema ya kuwa Uamshio ni kazi ya Roho Mtakatifu, kwa hiyo hata kama wanadamu watautaka uamsho na kuvaa majoho ya kutaka kuuuketa kamwe bila Roho Mtakatifu kuhusika hakuwezi kuweko kwa uamsho, Uamsho wa kweli unakuja tu mara anaposhuka Roho Mtakatifu, bila Roho wa Mungu kutenda kazi ya kuvumisha upepo mifupa mikavu isingeliweza kuwa hai

Ezekiel 37:1-14 “Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake.  Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli.Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.”

Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.”

Roho Mtakatifu anaweza kuanza na mtu mmoja au wawili tu na akaweka mzigo wa maombi ndani yao na kupitia wao wengine wakaambukizwa, kumbuka kuwa hatuwezi hata kuomba au kufunga bila msaada wa Mungu, ni kazi ya Mungu Roho Mtakatifu, kuamsha roho zetu, kwa hiyo unaweza kuanza peke yako, usitegemee kuwepo kwa uamsho wa ujumla, tegemea kuanza wewe, Roho Mtakatifu hutoa nguvu ya kuomba, huleta mvuto wa toba, nguvu ya kuhubiri na kuokolewa kwa wengi na Mungu kuwatumia wengi, kwa ujumla tunaweza kusema Roho Mtakatifu ndiye wa Muhimu zaidi kwa kazi ya uamsho: Na bado uamsho ni neema ya Mungu mwenyewe kwa kanisa lake na watu wake,sisi tuna sehemu ndogo sana ya kufanya lakini yeye ndiye mshika dau, na ndiye mwenye kuamsha nia na neema ndani yetu, aamshe nia ndani yetu kuombea viongozi wa kanisa wasichoke, kuombea mikutani ya injili, kuamsha nia ya kusifu na kuabudu, kuamsha ibada zenye nguvu,  kuamsha karama na vipawa vya Roho Mtakatifu, kuamsha nia ya vikundi vya maombi, kuamsha nia ya kusoma neno, kuamsha Imani, kuamsha kiu na hamu na shauku ya kutafuta na kudumisha uhusiano na Mungu, na kuhakikisha kuwa upendo unatawala katika kanisa la Mungu.
 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

0718990796.



Jumapili, 21 Aprili 2024

Umponyaye masikini na mtu aliye hodari!

 

Zaburi 35:9-10 “Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”





Utangulizi:

Kwa kawaida katika ulimwengu huu limekuwa ni jambo la kawaida katika mazingira Fulani, wenye nguvu kuwaonea wale wasio na nguvu, au Matajiri, kuwaonea masikini, au mtu aliye hodari kumuonea aliye mnyonge, Hali hii inaweza kuwa imekutokea wewe au familia yako katika mazingira Fulani. Familia nyingi za kiafrika bado ziko katika kipindi cha mpito, kutoka katika hali duni kuelekea katika hali njema kwa hiyo watu wengi sana wamewahi kukutana na uonevu wa namna nyingi, kutoka kwa wenye nguvu, wenye mamlaka, au watu Fulani kulingana na nyadhifa zao, wanaweza kwa namna mmoja ama nyingine kuwa wamekutana na aina Fulani ya uonevu Daudi alikuwa mmoja ya watu waliokutana na hali kama hiyo na kupata maumivu nafsini mwake, Hali hii inamkuta mtu anapokuwa Katika namna au nafasi ambayo hakuna wa kuingilia kati isipokuwa Mungu mwenyewe.

Katika Zaburi ya 35 Daudi anajaribu kumuomba Mungu sasa ili Mungu aweze kuinglia kati kwa haraka na kumtoa katika mazingira magumu aliyokuwa anakabiliana nayo ambayo yalikuwa hayana mtetezi. Na anamuahidi Mungu kuwa endapo atamletea msaada basi yeye ata mfurahia Bwana na kuushangilia wokovu wake!  

Zaburi 35:9 “Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.” Kwa sababu hii sisi nasi leo tutachukua muda mfupi kujifunza na kutafakari kifungu hiki muhimu kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

 

·         Bwana ni nani aliye kama wewe

·         Umponyaye masikini na mtu aliye hodari!

 

Bwana ni nani aliye kama wewe! 

Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”

Daudi akitumia lugha ya kimashairi hapa anaanza kwa kuahidi kuwa atamtukuza Mungu, endapo BWANA ataingilia kati mahitaji yake na maombi yake na kwa kweli yalikuwa ni maombi ya mtu mwenye uchungu mwingi yanayodhihirisha kuwa alikuwa amechoshwa na hali inayomkabili,  Mifupa yangu yote itasema Bwana ni nani aliye kama wewe, Ni Muhimu kufahamu kuwa Waebrania walitumia neno Mifupa kumaanisha nafsi au mtu wa ndani, wao walikuwa wakifikiri kuwa mtu wa ndani kabisa anawakilishwa na mifupa, kwa hiyo hata mtu alipokuwa akimaanisha mtu wake wa karibu au wa ndani  sana au ndugu alitumia neno Mifupa

Mwanzo 2:23 “Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” 

Zaburi 6:2-4 “Bwana, unifadhili, maana ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini? Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.” 

Kwa hiyo Daudi alikuwa akimaanisha nafsi yake imeumizwa na kama Bwana ataingilia kati dhidi ya adui zake ambao kimsingi walikuwa na nguvu au mamlaka au wenye kutisha kuliko yeye au wenye uwezo kuliko yeye au wenye uchumi mzuri kuliko yeye, au wenye nguvu, au uwezo wa kumchukua mateka, na kumuokoa Basi nafsi yake yaani kwa kibrania mifupa yake ingempa Mungu utukufu na kumshukuru sana na atasema Bwana ni nani aliye kama wewe! Mifupa katika lugha ya kiibrania wanatumia neno ETSEM ambalo linazungumzia mtu wa ndani Selfsame yaani nafsi neno hili limejitiokeza katika maandiko mara 126 katika mistari karibu 108.

Usemi huu Bwana ni nani aliye kama wewe ulikuwa ukionekana mara kwa mara katika mashairi ya kiibrania likitumika kama swali la kimashairi  kuhoji kuwa  ni nani mwenye nguvu au anayeweza kuwa na kiburi na jeuri kiasi cha kujilinganisha au kusimama kinyume na Mungu aliye hai anapoamua kuingilia kati mambo yake, wakati Farao alipokuwa na nguvu za kijeshi kuliko taifa lolote duniani na kuamua kusimama kwa ujeuri kinyume na wana wa Israel na hata walipookolewa aliamua kuwafuata ili awarejeshi utumwani, Israel baada ya udhihirisho mkubwa wa Mungu na ukombozi ulio hodari wa Bwana wa majeshi waliimba na kusema Bwana ni nani aliye kama wewe! 

Kutoka 15:10-12 “Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza” 

Israel Walimshangilia Bwana na kumuimbia kwa furaha huku wakihoji ee Bwana katika miungu Ni nani aliye kama wewe huu ulikuwa ni usemi wa kawaida katika Israel wenye kuonyesha ya kuwa Hakuna wa kulinganishwa na Mungu mwenye nguvu wa Israel

Zaburi 89:7-9 “Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.”

Zaburi 71:17-19 “Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

Zaburi 113: 4-5. “Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote, Na utukufu wake ni juu ya mbingu. Ni nani aliye mfano wa Bwana, Mungu wetu aketiye juu;” 

Bwana ni nani aliye kama wewe ni usemi unaoonyesha Mungu ni mwenye nguvu na hakuna mfano wake,ana uwezo kuliko kitu chochote, ana nguvu kuliko nguvu za wachawi na waganga na washirikina, ana nguvu kuliko jeshi lolote duniani, ana mamlaka kuliko mtu yeyote duniani, ana uweza, ulio juu kuliko mungu yeyote duniani, ana utajiri kuliko yeyote duniani na ndiye mkombozi na mtetezi wa wanadamu hasa kwa sababu yeye hapendi uonevu, kwa hiyo wakati tunajiona duni na tumeachwa tukiwa hatuna mtetezi, tumeachwa tupate kudhalilika, tuko katika hali ya unyonge hatuna budi kujiandaa kwa shuhuda, Daudi alikuwa anajiandaa kwa shuhuda alipokuwa anaomba kwamba Mungu akingilia kati na kumsaidia alisema nafsi yangu itakushukuru, atashuhudia jinsi Mungu alivyo mtenda miujiza mikubwa na mwokozi na mtetezi na kimbilio la wanyonge,  na hivyo fadhili za Bwana zina nguvu kuliko majeshi yoyote, mamlaka yoyote na wapanda farasi wake!

Zaburi 33:16-18. “Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.”

Kwa hiyo haijalishi ukubwa wa changamoto zinazokukabili, haijalishi nguvu ya yule unayepambana nawe kama ilivyokuwa kwa Daudi liitie jina la Bwana na Mungu atajifunua kwako kutoka katika pembe ya kile unachokabiliana nacho ukijua wazi ya kuwa hakuna aliye kama yeye  naye atatenda mambo makuu, Nani aliye kama Bwana?


Umponyaye masikini na mtu aliye hodari! 

Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”

Neno Umponyaye  hapa linaweza pia kutumika sambamba ba Uokoaye, Kwamba mtu wa Mungu anaweza kupitia katika hali ngumu na mateso na usumbufu wa mwili, nasfi na roho lakini hatimaye Bwana anaweza kukuokoa nayo yote, na  anaweza kukuponya nayo yote,  Maandiko yanaonyesha wakati wote tunapokabilia na mambo magumu ya kuumiza nafsi zetu, iwe ni magonjwa, iwe ni migogoro ya ndoa, migogoro ya malezi, migogoro ya kazini, migogoro ya maisha, kesi mahakamani, kukosa ada za shule, umasikini, mateso magonjwa ya aina mbalimbali, njaa, madeni, uonevu wa mirathi, uonevu wa mipaka ya shamba, kusalitiwa, kuogombana, vita baridi na kurushiana maneno huku na kule  nataka nikuhakikishie ya kuwa tukimlilia Bwana kwa mapenzi yake akaamua kutujibu atatutoa katika hali zote zinazotukabili.

Zaburi 34: “Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”

Hakuna changamoto ambayo Bwana hawezi kuitatua yeye anayaweza yote yeye ni mponyaji wa nafsi zetu na ni mwokozi wa kila janga linalotukabili  hata kama tunaweza kupita katika hali ngumu kwa sababu ya kuweko Duniani na kuweko kwa shetani, ni Muhimu kufahamu kuwa tutaokolewa katika hayo yote yanayotukabili labda kama Mungu sio Muaminifu kwa neno lake! Jambo ambalo haliwezekani kwa sababu uaminifu wake unadumu kizazi hata kizazi

2Timotheo 3:10-11 Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.”

Jambo kubwa la msingi ni kumtumainia Bwana na kumuweka yeye mbele naye atafanya kitu, yeye ni mwenye nguvu,  na uwezo wa kutukinga na kila kilicho hodari duniani anao kwa msingi huo wakati wote tunapopita katika wakati mgumu tukimtumainia yeye tutasimama tena,  Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.” Masikini katika luga ya kiebrania hapo linatumika neno ANIY ambalo maana yake ni mtu awaye yote ambaye yuko katika hali ya kudhikika, kuanzia kwenye akili mpaka katika mazingira ya kawaida, mtu mnyonge, mwenye uhitaji, masikini, aliyeonelewa, mtumwa, aliyechukuliwa mateka, mtu wa hadhi ya chini, mgonjwa anayeonewa na kitu chenye nguvu kiasi cha kumuumiza Hali zote hizo bwana hawezi kukubali hata kidogo, yeye huingilia kati na kuokoa na kuponya. Jambo kubwa la ziada ni kumtumaini yeye kama asemavyo;

Mithali 3:5-6. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
     



Jumanne, 9 Aprili 2024

Hata saa tisa!

Mathayo 27:45-50 “Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?  Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.”



Utangulizi:

Moja ya matukio muhimu tunayoweza kuyazingatia katika msimu wa kukumbuka Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Kifo chake na kufufuka kwake ni Pamoja na Saa ile aliyokata roho, yaani saa tisa, Karibu kila mwandishi wa Injili anaonyesha tukio hili la kipekee la Yesu kukata roho saa tisa, licha ya kuwepo kwa giza kubwa na la kipekee kuanzia saa sita mpaka saa tisa na kisha saa tisa Ndipo Yesu alikata roho. Tunaweza kuona, tukio hilo likirudiwa tena na tena katika injili nyingine:-

Marko 15:33-34 “Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Luka 23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu

Tukio la Yesu Kristo kufa saa tisa jioni lina umuhimu mkubwa sana kwa mujibu wa injili na ndio maana limeelezwa na injili zote tatu, tunaelezwa kuwa katika muda huo tofauti na kawaida kulikuwa na giza tangu saa sita hata saa tisa, na saa tisa Yesu alipaza Sauti ya kilio Mungu wangu Mungu wangu Mbona umeniacha, na kisha Yesu alifikia hatua ya kutimiza kusudi lote la ukombozi wa mwanadamu kwa kujitoa dhabihu yeye mwenyewe, kwa ukombozi wa Mwanadamu. Lakini labda swali muhimu linaweza kubakia pale pale kwa nini saa tisa? hilo linatupa nafasi ya kutafakari somo hili hata saa tisa kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu yafuatayo:-


·         Saa tisa katika masimulizi ya kale ya tamaduni za kiyahudi

·         Saa tisa kwa mujibu wa maandiko

·         Hata saa tisa!

 

Saa tisa katika masimulizi ya kale ya tamaduni za kiyahudi

Kwa mujibu wa masimulizi ya Kale Wayahudi waliamini kuwa Mungu alikuwa na tabia ya kumtembelea Adamu katika Bustani ya Edeni, Saa ya jua kupunga, Kwa kiingereza “In the cool of the day” Ruach/yom

Mwanzo 3:8-9 “Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?  

Kwa mujibu wa masimulizi ya kiyahudi Muda au wakati wa jua kupunga katika unaitwa YOM ambalo kwa tafasiri wakati wa  jioni ambapo wayahudi walikuwa wanaamini ni mida ya saa tisa, Kwa mujibu wa masimulizi ya kiyahudi Muda huu kwa kawaida Mbingu huwa zinafunguka, na Mungu huwa ana kuwa na shauku ya kuimarisha uhusiano wake na wanadamu, hili ni moja ya jambo la kwanza na muhimu ambalo tunalipata katika Masimulizi ya kiyahudi na ndio maana moja ya saa za maombi katika jumuiya ya kiyahudi ni pamoja na kuomba saa tisa. Meno mawili ya kiebrania yanatumika kuelezea Saa ya jua kupunga in the cool of the day ambalo ni Ruach na Yom yakiwa na maana wakati wa utembeleo wa Roho wa Mungu.

Aidha kweli nyingine ya Masimulizi ya kale ya kiyahudi inasema ni katika muda huu, Mungu alimpa Adamu usingizi Mzito na kuchukua sehemu ya ubavu wake na kumuumba Mwanamke.

Mwanzo 2:21-23 “BWANA Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”

 Usingizi mzito katika lugha ya kiibrania wanatumia neno TARDEMA ambalo maana yake ni hali inayosababishwa na Mungu mwenyewe kwaajili ya kumletea mwanadamu ufunuo muhimu, au kufanya jambo la Muhimu kwa mwanadamu    
          

Masimulizi mengine ni kuwa saa tisa ni muda ambao wayahudi walikuwa wanautumia kwa maombi, kuna vipindi vikubwa vitatu vya maombi katika tamaduni za kiyahudi. Hata manabii na waandishi wa zaburi wana nukuu kadhaa katika maandiko, zinazoashiria kuwa wayahudi walikuwa na vipindi vitatu vya maombi na ambavyo wameendelea kuwa navyo hata siku za leo angalia

Zaburi 55:16-17 “Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa; Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.”

Daniel 6:10-11 “Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake   
  

Vipindi hivyo vitatu vya ibada za maombi, ambavyo Wayahudi wanaendelea navyo mpaka leo kwa lugha ya asili ya Kiibrania vinaitwa SHACHARIT, MINCHA NA MAARIV ambavyo tunavichambua kama ifuatavyo:-

1.       Shacharit: - huu ni muda wa maombi ya alfajiri ambapo Wayahudi husali baada ya kupambazuka kwa jua, Maombi haya hufikiriwa kuwa ni maombi ya muhimu sana ambayo wayahudi huamini kuwa wanapokea Baraka kubwa sana, maombi au sala ya alfajiri huambatana na Kusifu, kusoma maandiko hususani Torati. Na hii inasadikiwa kufanyika kati ya muda wa asubuhi mpaka saa tatu na hasa kilele chake ni saa tatu.

 

2.       Mincha: - huu ni Muda wa maombi ya jioni (afternoon) Maombi haya ndiyo ambayo hufanywa saa tisa, ni maombi mafupi sana, ukilinganisha na Maombi ya alfajiri yaani Sacharit, maombi haya ya saa tisa hujumuisha kuomba, kusoma zaburi na kunyamaza kimyaa (Amidah) kusimama kimyaa, nah ii inasadikiwa kufanyika kati ya saa sita mpaka saa tisa na kilele chake hasa kilikuwa saa tisa

 

3.       Maariv au Arvit: Maariv pia huitwa Maarib au Magharibi kwa Kiswahili, Maombi haya yanafanyika baada ya jua kuzama ni kwaajili ya kuukaribisha usiku na kuuaga mchana, maombi haya hujumuisha Baraka, na ukiri wa SHEMA ukiri wa shema ni ukiri unaopatikana katika Kumbukumbu la torati 6:4-5 nimenukuu hapa:-

 

Kumbukumbu 6:4-5 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”

 

Shema ndio kiini kikuu cha Imani ya kiyahudi, Maombi haya ya Maariv au magharibi kilele chake ni jioni saa kumi na mbili wakati wa kuzama kwa jua.

Kwa hiyo kwa mujibu wa tamaduni za kiyahudi, na dini ya kiyahudi, yanashikiliwa na wayahudi katika maisha yao yote na siku zote, Kwa hiyo kuna saa tatu, kuna saa tisa na kuna saa kumi na mbili, Kwa hiyo  Saa tisa ni moja ya saa nyeti katika tamaduni na dini ya kiyahudi. Wayahudi wengi waliamini kuwa muda huu ni muda mwema sana Saa tisa Muda wa dhabihu ya jioni Mungu husikia kwa haraka sana na hujibu kwa haraka sana, na ni saa ya miujiza mikubwa.

Zaburi 141:1-2 “Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.”                        

Saa tisa kwa mujibu wa maandiko:

Nadhani sasa unaweza kupata picha ya umuhimu was aa tisa, ya kwamba ni saa yenye neema ya ajabu, ni saa yenye faida kubwa sana, kila mtu aliyeokolewa ana neema kubwa na amepewa neema ya kuzijua siri za ufalme wa Mungu, lakini kufunuliwa kwa nguvu za ufalme wa Mungu kunategemeana sana na ujuzi wa kanuni, kama vile ambavyo ziko hesabu huwezi kuzifanya bila kujua kanuni, au huwezi kupata majibu bila kujua kanuni, ufunuo kuhusu kanuni unatofautiana kati ya Mtu na mtu, Kadiri unavyozijua kanuni hizo ndio unajiweka katika nafasi kubwa sana ya mafanikio na siri za ufalme wa Mungu na kufaidika kiroho, kwa hiyo maombi ya saa tisa ni ufunuo wa Muhimu sana kwako leo, lakini ili uweze kuwa na ufahamu sasa tufuatane nani katika maandiko kuweza kuona saa hii kwa mujibu wa maandiko:-

-          Ulikuwa ni Muda ambao Bwana alimtembelea Ibrahimu na kuwa na ushirika naye pamoja na Sarah Na kumuahidi kupata mtoto Mwanzo 18:1-2 “BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, BWANA wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.” Neno Mchana wakati wa Hari katika kiibrania linatumika tena neno YOM ambalo lina maana ya jioni mida ya saa tisa

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao makuhani waliagizwa kutoa dhabihu ya jioni Kutoka 29:38-42 “Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo.”

 

-          Ulikuwa ni Muda wa kuchoma au kufukiza uvumba wakati wa dhabihu ya jioni Kutoka 30:7-8 “Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; KILA SIKU ASUBUHI atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza. Na Haruni atakapoziwasha zile taa WAKATI WA JIONI, ATAUFUKIZA, UWE UVUMBA WA DAIMA mbele za BWANA katika vizazi vyenu vyote.”

 

2Nyakati 13:11 “nao humtolea Bwana kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi twayalinda malinzi ya Bwana, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha.”

 

Luka 1:8-14 “Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.”

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao Eliya alimuomba Mungu dhidi ya manabii wa baali katika mlima Karmel na Mungu akamjibu kwa moto kutoka mbinguni 1Wafalme 18:36-39 “Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.”

 

-          Ulikuwa ni Muda huu ambao Ezra aliomba Maombi ya toba na maombezi yaliyoleta uamsho mkubwa sana miongoni mwa jamii ya Wayahudi waliokuwa wamerudi nyuma Ezra 9:4-8 “Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni. Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu wangu; nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu.”

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao Daniel nabii aliletewa majibu ya maombi yake kupitia malaika Gabriel Daniel 9:20-22 “Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.”

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao Yesu Kristo alikuwa ameimaliza kazi yote Pazia la hekalu lilipasuka na Yesu akakata roho kwa kuikabidhi roho yake mikononi mwa Baba Luka 23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao Petro na Yohana walikuwa wakihudhuria maombi katika hekalu na Kiwete akaponywa na ukawa ndio muujiza wa kwanza katika kanisa la kwanza ulioambatana na uamsho mkubwa na kuokolewa kwa watu wengi zaidi Matendo 3:1-7 “Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.”

 

-          Ulikuwa ni Muda ambao Kornelio  Mmataifa aliyekuwa anaomba na kutoa sana sadaka alipata utembeleo wa malaika akiagizwa na Mungu, kumuita Petro aje kumueleza habari za Kristo Matendo 10:1-6 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.”

 

Hata saa tisa!

Luka 23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu

Nadhani sasa unaweza kuona umuhimu wa saa tisa, kimsingi ilikuwa ni Muda wa kutoa dhabihu ya jioni kwa wayahudi, ilikuwa ni saa ya kinabii, ulikuwa ni muda ambao wayahudi walipiga tarumbeta ya wito wa kwenda hekaluni kusali, Na Yesu yeye ndiye Dhabihu Halisi ya jioni, Alitumia Muda huo huo kukamilisha kazi yake ya ukombozi, Kristo alikuwa amekamilisha mpango wa Mungu wa kurudisha ushirika na wanadamu, ulikuwa ni muda ambao Msimamizi wa Mateso askari yule alimpiga Yesu Mkuki wa ubavuni ili kuthibitisha kama amekwisha kufa, ubavu ule ulitoa maji na damu, ambayo kimsingi ina thamani kubwa sana katika upatanisho wa watu kwa Mungu, Yesu alipewa Mkewe kutoka katika ubavu wake, (ni Kanisa) limezaliwa kutoka katoka moyo wa upendo wa Kristo, tunaona miujiza mingi, muda huo, tunaona watu wakijibiwa maombi muda huo, tunaona ni Muda ambao wayahudi hawakuomba sana walitumia muda mfupi tu, kwanini kwa sababu Mungu ni Mungu aliye karibu anapatikana na zaidi sana ulikuwa ni muda ambao wengi walitembelewa na malaika, kama muda wa usingizi kwa Adamu muda huo watu wengi waliofanya kazi kutwa nzima wanaweza kusinzia kidogo, ni Muda wa muujiza, ni muda wa rehema ni muda wa neema ya Mungu.

-          Mafunuo makubwa kuhusu Mungu yalishushwa saa tisa.

-          Utembeleo mkubwa wa malaika ulifanyika saa tisa.

-          Kupasuka kwa Pazia la Hekalu na watu wakaona patakatifu ilifanyika saa tisa.

-          Ulikuwa ni muda ambao wayahudi walitoa dhabihu ya pili ya mwanakondoo kwaajili ya upatanisho wa dhambi zao, na sasa tukio hilo la kinabii linakamilishwa na Bwana wetu Yesu

-          Dhabihu ya ukombozi wa mwanadamu ilikamilika saa tisa

-          Yesu alitundikwa Msalabani muda wa kutoa dhabihu ya asubuhi na alikufa muda wa kutoa dhabihu ya jioni

-          Ulikuwa muda wa Kujibiwa maombi kwa Eliya na Mungu alijibu kwa Moto.

-          Ulikuwa ni Muda wa Kujibiwa maombi Daniel kwa kutumiwa malaika

-          Ulikuwa ni Muda wa kutembelewa Abrahamu na wageni watatu

-          Ulikuwa Muda wa kufukiza uvumba katika madhabahu ya kufukiza uvumba wakati wa dhabihu ya jioni

-          Ulikuwa ni muda ambao malaika wa Bwana alimtokea Zekaria na kupewa ahadi ya kuzaliwa Yohana

-          Ulikuwa ni Muda wa kusali kwa Petro na Yohana na Muujiza mkubwa kwa kiwete wa miaka 40

-          Ulikuwa ni muda wa utembeleo kwa Kornelio kuona maono ya malaika

-          Miujiza mikubwa ya kubadilika kwa maisha ya watu ilitokea muda huo

-          Ulikuwa ni muda unaowakilisha saa ya kukubaliwa kwa maombi, Maandiko yanaonyesha hakuna mtu aliwahi kukataliwa kujibiwa maombi yake katika muda huo, japo Mungu anatusikia kila wakati.

-          Jambo kubwa la msingi na la Muhimu kuliko yote saa tisa ndio saa ya ukombozi wetu, kwani Yesu alikufa saa tisa na pazia la Hekalu lilipasuka kumpa kila mmoja nafasi ya kuweza kumfikia Mungu moja kwa moja kupitia sadaka iliyotolewa Msalabani na mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo.

Saa tisa ilifanya kazi katika agano la kale na katika agano jipya, siwezi kukufundisha kuwa ufanye kitu saa tisa au uabudu saa tisa au uombe saa tisa,  lakini nataka kusema hivi, kila mtu anayeamini katika mateso, kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu na kuokolewa hapaswi kuwa gizani kuwa anapaswa kufanya nini muda huo na uzuri wake hauchukui muda mrefu, hivyo hata kama uko kazini, fanya kitu kidogo kwaajili ya Uhusiano wako na Mungu, Nyenyekea utaona miujiza mikubwa na utajua kwanini Yesu alikufa muda huo kifo kibaya sana kwaajili yetu, utajua kwanini pazia la hekalu lilipasuka, na patakatifu pakaonekana hii maana yake nini ni muda ambao unaweza kukikaribia kiti cha neema na kujipatia Rehema kutoka kwake aliyekuumba na nataka nikushuhudie ya kuwa utamuheshimu milele kwa sababu Bwana takupa neema ya kukusaidia wakati wa mahitaji yako, Kwa kweli saa tisa ni saa ambayo unaweza kuamuru muujiza wako, saa tisa ni kama saa ambayo Mungu yuko tayari kuamka na kufanya kitu kwaajili ya mwanadamu, ni saa ambayo tunaweza kusema Mzee hufungua ofisi yake ili asikilize watu wake, Hebu itumie saa hiii kwaajili ya kuamuru Baraka zako. neno hili ni kweli ni nani awezaye kulifahamu?

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima