Ijumaa, 18 Aprili 2025

Ufahamu kuhusu njia ya Msalaba! (Via Dolorosa)


1Wakorintho 1:18-24 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa.Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”




Utangulizi:

Leo ni siku ya ijumaa kuu, wakristo wote nchini wanaungana na wakristo wenzao duniani kuadhimisha na kukumbuka Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuuawa kwake msalabani kwaajili ya ukombozi wa wanadamu kulikotokea huko Yerusalem zaidi ya miaka 2000 iliyopita, Katika siku hii ya leo nataka kuzungumzia Ufahamu kuhusu njia ya Msalaba.

Huenda wewe umewahi kusikia au kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika ibada iitwayo ibada ya njia ya Msalaba! Na huenda umewahi kujiuliza ibada hii ni ibada ya namna gani, asili yake ni nini na je ni mapokeo au ni mafundisho ya kibiblia, ina kweli gani na ina dosari gani ni mambo gani mazuri tunaweza kujifunza kutoka katika ibada hii, yepi ya kibiblia na yepi sio ya kibiblia, kwa wakristo wa makanisa ya kikatoliki na Anglican ya High Church njia ya msalaba inaweza kuwa sio kitu kigeni, Hususani katika wakati ule wa Kwaresma na katika siku ya leo ya ijumaa kuu – Kwaresma maana yeke ni (40), lakini kwa makanisa ya kipentekoste inaweza kuwa kitu kigeni, vyovyote iwavyo vile kuna mambo ya kujifunza kwa kila mmoja wetu uwe ni mpentekoste au mkatoliki na muanglikan na wengineo, yako mambo ambayo Roho Mtakatifu anataka tujifunze kwa msingi huo basi Leo basi Mwalimu Mkuu Mungu Roho Mtakatifu ametupa neema ya kujifunza maswala muhimu katika ibada hii ya njia ya msalaba na tutajifunza kwa kina na mapana na marefu kwa kusudi tu la kuelewa yale yaliyoko katika njia ya msalaba na kufaidika. Kwa ufahamu na maarifa. Tutajifunza somo hili Ufahamu kuhusu njia ya msalaba kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo:-

 

·         Historia ya njia ya Msalaba.

·         Mafundisho Muhimu katika njia ya msalaba.

·         Mambo yasiyo ya kibiblia katika njia ya Msalaba.

·         Faida ya mafundisho ya njia ya Msalaba.

 

Historia ya njia ya Msalaba

Ni muhimu kufahamu kuwa ibada ya njia ya msalaba asili yake ilitokana na ibada ya kutafakari kwa kina na kujifunza maswala mbali mbali kuhusu mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo tangu alipohukumiwa na Pilato hadi wakati alipokufa Msalabani na alipozikwa, ibada hii huadhimishwa kwa kirefu aidha wakati wa Kwaresma (40) ama wakati wa sikukuu ya ijumaa kuu, Katika wakati huo watu waliomwamini Yesu hujumuika kwa pamoja katika kujifunza na kutafakari Mateso ya Yesu na hivyo kujiimarisha kiroho, kiimani,toba na kiufahamu, wakati wa kutafakari mateso hayo lakini lengo kuu likiwa ni kupandikiza fundisho hilo Muhimu kuhusu kuteswa kusulubiwa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo fundisho ambalo ni msingi mkuu wa ukombozi wa Mwanadamu, na Imani yetu, kwani kama Kristo asingelisulubiwa na kufa na kufufuka katika wafu Imani yetu ingelikuwa ni bure.

1Wakorintho 15:13-20 “Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.”

Ibada hii ilianza mnamo karne ya 4 baada ya Yesu Kristo, kama matokeo ya wakristo waliokuwa na tabia ya kutembelea Yerusalem na kupita katika njia ile halisi aliyopitia Yesu Kristo kutoka jumba la hukumu la Anthonio akielekea Golgotha au Kalvari mahali ambako alisulubiwa, wakristo hao wa kale walikuwa na tabia ya kutembelea Yerusalem (Kufanya hija) na kupita hatua kwa hatua na kusimama katika kila eneo la kihistoria kwa kutafakari kujifunza na kufanya maombi kwa kukumbuka mateso ya Yesu Kristo.

Moja ya watu mashuhuri waliokuwa wakifanya ibada hii na baadaye kuyatambua maeneo hayo muhimu ya mateso ya Yesu ni pamoja na mama wa Mfalme Constantine aliyejulikana kama Malkia Hellena ambaye alikuwa ni Mkristo kabla ya mwanae kumuamini Bwana Yesu Baadaye.

Mnamo karne ya 13-14 watawa wa Kifransisko (Franciscans) walipewa jukumu la kuyahifadhi maeneo hayo ya njia ya Msalaba huko Yerusalem chini ya utawala wa Sultan wa Ottoman 1342 na wao walifanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kuieneza ibada hii katika maeneo mbali mbali ya ulaya, mpaka karne ya 18 Papa Clement XIV alikubali kupitisha vituo 14 rasmi katika ibada hii ya njia ya msalaba vinavyotambulika mpaka leo, hata hivyo baadhi ya wakristo waliongeza kituo cha 15 kuzungumzia kuhusu kufufuka kwa Yesu na wengine huona kuwa wakati ibada ya njia ya msalaba hufanyika ijumaa kuu, basi kituo cha 15 kinaweza kuadhimishwa sikukuu ya pasaka. Vituo tisa tu kati ya vituo vile 14 ni matukio ya kweli ya kibiblia wakati vituo vitano 5 matukio yake si ya kibiblia bali yanatokana na masimulizi ya kale yaliyoaminiwa na watu kwa miaka na kwa taarifa za kimapokeo.

Ibada hii ya njia ya Msalaba ilipewa umuhimu mkubwa katika nyakati za pasaka kwa sababu ilikuwa ikiwasaidia wakristo kupata nafasi ya kutafakari kwa undani mateso ya Yesu Kristo kama njia ya kujiimarisha kiimani katika maisha ya kiroho. Katika lugha ya kilatini njia hii ya Msalaba inajulikana kama “Via Dolorosa” kwa kiingereza “Sorrowful Way” au “Way of Suffering” au “The Painful Path” yaani njia ya huzuni au njia ya mateso, au njia ya maumivu, hapa tunaiita njia ya msalaba, njia hii iko katika mji wa zamani wa Yerusalem na inaaminika njia hiyo ndiyo ile aliyoipitia Yesu kuelekea mahali alikosulubiwa.

Isaya 53:3 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; MTU WA HUZUNI NYINGI, AJUAYE SIKITIKO; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.”  


Mafundisho Muhimu katika njia ya msalaba

Kutokana na mwamko mkubwa wa kiinjili tulio nao leo, Njia ya msalaba inaweza kuonekana kuwa ni ibada ya kimapokeo, lakini ukiichunguza kwa undani utaweza kugundua kuwa kulikuwa na nia njema ya kutaka kuwafundisha watu kwa kina sana kuhusu mateso ya Yesu Kristo, japo kutokana na ufinyu wa kiufahamu uliokuwako nyakati hizo, na upungufu mkubwa wa Elimu na maarifa ya wakati ule, uwezo wa kufikisha mafundisho hayo ulikuwa duni, na wa kitoto hata pamoja na kuhusisha picha, lengo kuu lilikuwa halijafikiwa na sasa Roho Mtakatifu aliniamuru kuwa wakati wa kuweka sawa fundisho hili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho umewadia nami kwa neema ya Mungu niliyopewa kama mkuu wa wajenzi ninafanya kazi hii leo ya kuliweka wazi fundisho hilo kwa maarifa yake katika msingi wa kimaandiko.

Ni ukweli ulio wazi na usiopingika kuwa katika kufuatilia yale yaliyomo katika ibada ya njia ya msalaba utaweza kugundua kuwa yako mafundisho muhimu sana na mazuri na ya kweli ya kujifunza katika maswala kadhaa lakini vile vile yako maswala machache ambayo tunaweza tusiyape kipaumbele kwa sababu hayana ushahidi wa kimaandiko na sio ya msingi kwa sababu hiyo ingawa Papa Clement XIV alikubali kupitisha vituo 14 vya kimafundisho, Mimi nitajadili vifungu tisa tu na kuweka pembeni vile visivyo na ushahidi wa kimaandiko na vilivyo na asili ya kimapokeo lakini vinakubalika katika masimulizi ya wakristo wa kale. Baada ya maelezo hayo sasa tunangalie yale tunayoweza kujifunza kutoka katika njia ya Msalaba:-


1.       Yesu Kristo Mbele ya Pilato: # 1

 

Katika eneo la kwanza tunapotafakari kuhusu mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, utagundua hukumu iliyo mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani, ni hukumu ya kifo kwa mtu ambaye kimsingi hakuwa na hatia, Watu, wakuu wa makuhani pamoja na Pilato waliyaacha maisha ya mtu mwenye haki kuingia hukumuni na kuuawa pasipo hatia kwa ujumla ilikuwa ni hukumu ya uonevu mkubwa usioweza kusimuliwa, hii inathuthibitishia kuwa uovu wa mwanadamu ulikuwa umefikia ngazi ya juu kabisa ambapo mtu mwema alionekana kuwa mbaya na mtu mbaya alionekana kuwa mwema, jamii ilikuwa ikishabikia uovu kuliko wema.

 

Mathayo 27:22-25 “Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe. Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe. Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”

 

Yohana 19:6-8 “Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. Basi Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa.”

 

Hukumu hii ya Yesu Kristo ina maswala kadhaa ya kujifunza

 

a.       Inatufundisha jinsi ambavyo Yesu asiye na hatia alivyokubali adhabu mbaya zaidi ya kwenda kufa msalabani kwaajili ya makosa yetu na dhambi zetu,- Hukumu hii ya Yesu inadhihirisha jinsi wanadamu walivyo waovu na walivyooza na kupotoka katika kutenda dhuluma, tunajifunza jinsi dhambi ilivyo mbaya na jinsi ilivyoweza kusababisha majeraha makubwa katika moyo wa mwana wa Mungu, Hata hivyo kwa sababu ya upendo wake kwa wanadamu Yesu kristo anaonekana kukubali kuiachia dhuluma ishinde.

 

Isaya 53:3-8 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.”

 

b.      Inatufundisha jinsi Yesu alivyohukumiwa kwa makosa ya uongo.- Kimsingi hukumu hii ilikuwa ya dhuluma, isiyo ya haki na ambayo haikuzingatia sheria ya kiyahudi wala za kirumi, Mashitaka ya Yesu Kristo kwa kweli yalitolewa na watu waliokuwa wamepikwa na wakuu wa makuhani ili kutoa ushahidi wa uwongo, wala hakimu mwenyewe hakupata ushahidi wa wazi ambao ungeweza kumtia Yesu hatiani na kupelekea kupata adhabu ya kifo kibaya kuliko maelezo aidha hakukuwa na nafasi ya upelelezi wa kina kuhusu makosa anayosingiziwa Yesu Kristo badala yake kwa kupitia ushahidi wa kuunga unga tu yakafanyika maamuzi mabaya na ya kusikitisha sana !

 

Luka 23:1-4 “Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato.Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.”

 

Mathayo 26:59-61 “Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.”

 

Yohana 18:38 “Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.”

 

c.       Tunajifunza kwamba hukumu yake ni matokeo ya wivu na uhasama na sio haki – Wakuu wa makuhani na viongozi wa dini walimuonea Yesu wivu, kwa sababu alikuwa anafanya wanafunzi wengi kuliko wao, alikuwa maarufu kuliko wao, alikuwa na huduma yenye nguvu na upako kuliko wao, alikuwa akifanya miujiza mingi na mikubwa wakati wao hawakuwa na kitu, mafundisho yake yalijaa amri na mamlaka, Yesu alikemea sana dhambi ya unafiki ambayo kimsingi ilikuwa ikiwatafuna mafarisayo na viongozi wa dini na kwa sababu hizo walifanya njama za wazi za kutaka kumuua, na ni ukweli ulio wazi kwamba  hukumu hii ya kifo likuwa ni mauaji ya makusudi na haikuwa haki.

 

Yohana 11:47-50 “Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi.Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima.”

 

Mathayo 23:13-16 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. [Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.] Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.”

 

d.      Tunajifunza ya kuwa hukumu hii ilikuwa ya kinafiki na ya uovu – kimsingi haikuwa hukumu iliyozingatia sheria wala utaratibu, Kesi iliendeshwa usiku, hii ilikuwa kinyume cha utaratibu na kudhihirisha kuwa lilikuwa swala la njama  na uovu, hakukuwa na muda wa kujitetea, kesi ilihukumiwa kwa kura, ambapo jambazi na mashuhuri Baraba aliachiwa huru na Yesu Mwalimu na mtenda miujiza alichaguliwa kufa, hakimu aligundua kuwa Yesu hakuwa na hatia lakini hakuzingatia haki kwa sababu ya hofu ya fitina za kiyahudi na kwa unafiki alitoa hati ya hukumu ya kifo.

 

Mathayo 27:16-22 “Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu. Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba. Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe.”

 

Pamoja na kuwa kuhukumiwa kwa Yesu Kristo kwa njia ya uonevu ilikuwa ni njia ya Mungu ya kuleta ukombozi wa mwanadamu, Hukumu hii inatukumbusha wajibu wa watu kuhukumu kwa haki, kuhukumu kwa kuangalia mambo juu juu kunaweza kutuletea gharama kubwa sana na kutukosesha mbele za Mungu, kitendo hiki cha kuhukumiwa vibaya kwa Yesu kinatukumbusha kuwa wakati wa kukumbuka mateso ya Bwana Yesu tunakumbushwa kuhukumu kwa haki na kuacha dhuluma na kufanya upepelezi wa kesi mbalimbali ili kupata ushahidi wa kujiridhisha na sio kukimbilia kutoa uamuzi wa haraka haraka, umewahi kujiuliza ni kwanini Baraba alikuwa amefungwa na haikuwa tatizo lakini kulikuwa na haja gani ya kutokuchelewesha hukumu ya Bwana Yesu hata kwa kifungo tu? Neno la Mungu linatutaka kama tunahukumu basi tuhukumu kwa haki.

 

Yohana 7:24-26 “Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo?

 

Tunajifunza ya kuwa Yesu Kristo ambaye alikuwa na uwezo wa kuagiza malaika waje kumuokoa na hali iliyokuwa ikimkabili alikubali kupoteza haki zake, wakati mwingine katika maisha haya ya uchaji wa Mungu tutadhulumiwa na kupoteza haki zetu, haya yanaweza kutupata na wakati mwingine wenye kukudhulumu wakawa ni wapendwa kabisa, lakini Neno la Mungu linasema ni afhadli kudhulumiwa na ni afhadhali kupoteza wakati mwingine na kule kuachilia kutatujengea heshima mbele za Mungu

 

1Wakorintho 6:6-7 “Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini.  Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu?

 

e.      Njia ya msalaba inatukumbusha wakristo kumuomba Mungu ili watu wema na watenda haki watawale ikiwezekana sisi wenyewe tuwepo madarakani ili kutawala kwa haki, inapendeza sana watu wenye haki wakitawala na inachukiza sana na kuleta kuugua waovu wakitawala.

 

Mithali 29:2 “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.”

 

Kanisa lina wajibu wa kuombea mihimili ya maamuzi katika inchi ili haki iweze kutendeka kila mahali, na wale walioko kwenye maamuzi wanapaswa kujifunza kuwa na ujasiri na kusimama katika haki kwa gharama yoyote ile na kutokuiga mfano wa Pilato katika hukumu hii ya ajabu aliyoifanya. Hata hivyo wote tunakumbuka kuwa ingawa Yesu alionewa katika kesi hii alionewa kwa sbabu yetu na kwaajili ya ukombozi wetu.

       

 

2.       Yesu Kristo anaubeba Msalaba: # 2

 

Kuubeba msalaba ni ishara ya kujitoa dhabihu, kujikana kujitoa sadaka, kuwa tayari kwa majaribu na taabu na masumbufu ya Imani, Msalaba ni ishara ya kuvumilia magumu na sio kubeba mizigo, ni nafasi ya kumfuata Yesu Kristo, njia zake tabia zake na utii, baada ya hukumu ya kifo iliyokuwanya uongo kutolewa Yesu alikabidhiwa Msalaba wake na kukubali kuubeba alifanya hivyo kwa hiyari na kwaajili yetu!

 

Yohana 19:15-17 “Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.

 

Kitendo cha Yesu Kristo kukubali kuubeba msalaba kinatufundisha jinsi ambavyo Yesu Kristo alikuwa tayari sasa kuyatii mapenzi ya baba yake, kumbuka kufa kwake msalabani ulikuwa ni mpango wa Mungu na ni mapenzi yake, kukubali kuubeba msalaba kulikuwa ni ishara ya kwanza kwamba Yesu Kristo sasa anakubaliana na mateso ambayo kimsingi haikuwa rahisi kukubaliana na njia ile aliyoipitia

 

Luka 22:41-42 “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.”

 

Wafilipi 2:6-9 “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;”

 

Yesu kukubali kuubeba msalaba ilikuwa ni ishara ya upendo mkubwa kwa wanadamu self- sacrificial love, Yeye alikuwa tayari kuyapoteza maisha yake kwaajili yetu, alikubali kuabishwa na kuibeba fedhea ya dhambi na kuteketeza maisha yeke kwaajili ya upendo wake kwetu

 

Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”

 

Ni watu wachache sana duniani ambao wanaweza kukubali kutatoa maisha yao kwaajili ya wengine, kuubeba msalaba ilikuwa ni alama kubwa sana ya kuwa Yesu Kristo hakuwa na ubinafsi, wakati huu wa maadhimisho ya pasaka tunapokumbuka mateso yasiyo na kifani ya Bwana Yesu ni muhimu kukumbuka kuwa Mungu alituumba pia kwaajili ya wengine na ya kuwa mtu aliyekomaa kiroho katika ngazi ya juu zaidi ni yule ambaye yuko tayari kuyatoa maisha yake kwaajili ya wengine! Kama sio wengine kujitoa kwaajili yetu huenda tusingelikuwa hapa leo, Lakini wokovu wetu, maisha yetu na kuwepo kwetu kumetokana na watu wengine kutuvumilia na kuyatekekeza aisha yao ili sisi tuwepo!

 

Isidor Straus alikuwa moja ya wafanya biashara wakubwa sana mwenye asili ya kijerumani na alikuwa mbunge pia katika baraza la wawakilishi huko Marekani mtu huyu alikuwa tajiri mkubwa na mwenye mali nyingi sana wakati wa ajali ya meli maarufu ya Titanic ilipokuwa inazama waokoaji walitoa kipaumbele kwa watu wenye uwezo mkubwa na matajiri ili kuokoa maisha yao kwanza watu ambao walijulikana kama VIP. Katika namna ya kushangaza mfanya biashara huyu Isdor Straus aliyekuwa na uwezo mkubwa hata wa kununua Meli kama Titanic mara sita, Yeye alikataa kuokolewa na boti za uokoaji na kuomba waokolewe kwanza wanawake na watoto, Mkewe aliyeitwa Ida pia alikubali kubaki na mumewe na kukataa nafasi ya kuokolewa na boti maalumu na hivyo walikubali kufa kwa kuzama majini anaingia kwenye kumbukumbu ya watu waliokubali kufa kwaajili ya usalama wa wengine huku ni kujitoa kwa hiyari ya hali ya juu sana na kusikokuwa na ubinafsi.

 

Kuubeba msalaba kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatufunza hapa kwamba kila mwanafunzi wa Yesu anapaswa kuelewa kuwa tumeitwa sio kumwamini tu bali pia na kushiriki mateso kwaajili ya kusudi la Mungu, maisha yetu katika Bwana yanapaswa kuwa ni maisha ya kujitoa kwaajili ya wengina na kuwa mbali na ubinafsi.

 

Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”

 

Kila mwanafunzi wa Yesu anapaswa kujua kuwa kuna nyakati utaubeba msalaba wake kwaajili ya wengine na kwaajili ya utii kwa Mungu wetu, kuifuta njia ya Yesu Kristo njia ya msalaba ni pamoja na kujikana na kukataa ubinafsi kwa faida yetu na ya mwili wa Kristo, mambo mengi duniani leo yangefanyika kwa weledi mkubwa kama tu watu wataacha ubinafsi na kujiangalia wenyewe na kwa kufanya hivyo neno la Mungu linatufundisha kuwa tunapoteza badala ya kuingiza.

 

Luka 9:23-25 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?

 

Kukubali kuubeba msalaba kunatufundisha vilevile uwezo mkubwa wa kuvumilia magumu, Mungu ana makusudi na mpango wake mkubwa katika maisha ya kila mwanadamu aliyemuamini na wakati wingine Baraka hizo zimefichwa katika njia ngumu tunazozipitia, kukubali msalaba ilikuwa ni njia ya unyenyekevu ya hali ya juu sana na njia nzito ya kujifunza kuvumilia, wakati wote kuvumilia kunaleta thawabu kubwa sana thawabu zilizojificha, Yesu alistahimili mapingamizi makubwa sana  na kwa uvumilivu huo aliinuliwa juu sana

 

Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”

 

Tendo la Yesu kuukubali Msalaba sio tu la kihistoria lakini linatufundisha wakristo mtindo wa maisha, tunajifunza kutii mapenzi ya Mungu na kuwa waaminifu hata kufa,  Tunajifunza unyenyekevu,  tunajifunza kuvumilia (uvumilivu), na tunajifunza msamaha  na kukubali njia na mpango wa Mungu wa ukombozi wa Mwanadamu.

 

3.       Simon yule Mkirene asaidia kubeba msalaba. # 5

 

Simon Mkirene anajitokeza kama mtu aliyeshurutishwa na Askari katika kusaidia kuubeba msalaba wa Yesu; hata hivyo katika namna ya kushangaza sana Mtu huyu kwa hiyari yake alikubali kuubeba msalaba wa Yesu pamoja naye, angeliweza kukataa kwani halikuwa swala lililomuhusu, lakini alimuhurumia Yesu Kristo, na kwa jambo hili aliweza kuingia katika rekodi ya injili zinazofanana yaani “synoptic Gospel” zote kwa hiyo kuna kitu cha muhimu sana cha kutufunza katika swala zima la njia ya msalaba. Kwanza anatajwa kwa tukio lake hili katika injili zote tatu ona:-

 

a.       Mathayo 27:32 “Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.”

 

b.      Marko 15:21 “Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.”

 

c.       Luka 23:26 “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.”

Simon huyu alikuwa ni mgeni kutoka Kirene (Cyrene) ambako kunajulikana kama Libya leo hizi zilikuwa ni pande za Afrika ya kaskazini, mtu huyu kama alikuwa myahudi basi alikuwa akiishi Afrika na huenda alipanda Yerusalem kwaajili ya maadhimisho ya pasaka, Yeye alilazimishwa kuubeba msalaba wa Yesu, Na kwa hiyari yake alikubali kwani angeweza kukataa lakini alishiriki kuubeba msalaba wa Yesu pamoja naye, kimsingi tunajifunza jinsi mtu huyu alivyokuwa tayari kushiriki taabu pamoja na wengine alimsaidia Yesu kubeba msalaba na kushiriki mateso ya wengine, kwa sababu hiyo yeye alikuwa na moyo wa kuchukuliana na mizigo ya wengine lakini pia alikuwa na uwezo wa kufurahi na wanaofurahi na kulia pamoja na wanaolia, hapa alihuzunika na kulia pamoja na Yesu Katika taabu yake.

Wagalatia 6:2 “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”

Warumi 12:15 “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.”

Simon Mkirene licha ya kuwa mtu aliyekuwa tayari kuchukuliana mzigo na wengine, na kuwa mtu anayelia na wale waliao pia anatukumbusha wajibu wetu wa kuyashiriki mateso ya Kristo, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kukumbuka ya kuwa tumeitwa au tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili ya Kristo, kwaajili ya njia hii ya wokovu wakati mwingine tutapata mateso na changamoto za aina mbalimbali lakini hatuna budi kukubali kupita katika njia hizo:-

Wafilipi 1:29 “.Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”

2Timotheo 2:3-8 “Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu. Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari. Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali. Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda. Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote. Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu.”

Historia ya kanisa inaonyesha kuwa Mzee huyu ambaye alikubali kuyashiriki mateso ya Bwana Yesu hatimaye watoto wake yeye na familia yake waliokolewa na watoto wake wakamuamini Bwana Yesu na kuwa watu maarufu sana nyakati za Kanisa la Kwanza, watoto wa mzee Simeoni Mkirene walikuwa ni (Alexander na Rufus) Iskanda na Rufo na walikuwa wanafunzi waaminifu sana wa Bwana Yesu, tukio la mtu huyu mwenye huruma kutoka Afrika kumsaidia Yesu, kulisababisha muujiza wa yeye kuokolewa pamoja na familia yake na wakawa maarufu sana katika kanisa lakini pia walikuwa waaminifu na mama yao Rufo akawa kama mama wa wakristo wengi na mitume wengi sana baadaye akiwepo Paulo mtume ona

Warumi 16:18 “Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana. Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na mamaye, aliye mama yangu pia.”

Mafundisho ya njia ya msalaba hapa yanatufundisha kuwa kupitia Simeoni kwamba kila mwanadamu anapaswa kuwa na matendo ya huruma kwa wahitaji, tunaposaidia watu kwa namna na jinsi mbalimbali maana yake tunamsaidia Yesu bila sisi kujua, Ingawa Yesu peke yake ndiye mwokozi wa ulimwengu Lakini kitendo cha Simeoni kusaidia msalaba hakumfanyi yeye kuwa mwokozi bali kunamuweka yeye kuwa miongoni mwa watu wanaosaidia wengine, kuokolewa, kumpokea Yesu, kukutana na mahitaji yao na kwa sababu hiyo kushiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuifikisha injili duniani. tunapowatendea mema wengine kwa sababu ya Imani yetu katika Kristo tunamtendea Yesu bila kujua:-

Mathayo 25:34-40 “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”

Aidha Simeoni Mkirene katika picha ya kinabii anatufundisha ya kuwa Mungu ataitumia Afrika katika kuitangaza injili wakati wa uchungu na mateso au wakati mgumu dunia yote itakapokuwa imeharibika kwa uovu na ukatili Mungu ataitumia Afrika kusaidia kuenea kwa injili katika siku za mwisho wakati dunia ikiwa imeharibika kwa sababu hiyo Afrika inakumbushwa kuwa tayari kuihubiri injili wakati wa uharibifu wa dunia.

4.       Huruma kwa wanawake wa Yerusalem! #  8

Akiwa katika njia ya msalaba katikati ya mateso Yesu anakutana na wanawake wa Yerusalem ambao kimsingi walikuwa wakimuhurumia kwa sababu ya mateso yake na hata kumlilia, wao walikuwa wanakumbuka mambo yote mazuri ambayo Yesu aliwatendea watu wasio na shukurani na kuwa sasa kwa wivu wanamuweka matatani wamama hawa wanalia na kuomboleza lakini inaonekana Yesu anawahurumia wao zaidi  na kuwaonya

Luka 23:27-31 “Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Wakati wanawake hawa wa Yerusalem wakiwa wanamsikitikia Yesu Kristo na kumuhurumia na kumuombolezea na kumlilia, Yesu ambaye wakati huu alikuwa kwenye mateso na akiwa amebeba msalaba na maumivu, Yesu anaonyesha kuyajali maisha yao hasa na maisha yao ya baadaye, ingawa alikuwa katika maumivu makali lakini alikuwa na huruma kwa kuwa alikuwa anajua yanayokuja mbeleni kama nabii, Yesu aliwaonya wanawake hao kulia na kuomboleza sio kwaajili yake bali kwaajili yao na watoto wao, Kimsingi Yesu alikuwa anaona hukumu kubwa inayokuja dhidi ya Yerusalem miaka michache baadaye na hii ilikuwa inajumuisha kubomolewa na kuvunjiliwa mbali kwa mji wa Yerusalm na Israel nzima tukio hilo lililotokea mwaka wa 70 baada ya Kristo wakati huu ikiwa ni mwaka wa 33 baada ya Kristo ukweli ni kuwa ilipita miaka 37 tu na Yerusalem ulibomolewa vibaya na watu wengi kuuawa na wayahudi kukimbilia uhamishoni wengi sana na Askari wa kirumi walipita kila mji na kila kijiji wakiua watu na kuchinja kila myahudi, ulikuwa ni wakati wa historia mbaya zaidi kuwahi kutokea, watoto wa wanawakw wale walioonywa na Yesu ndio waliokutana na hukumu ile mbaya!

Jililieni nafsi zenu na watoto wenu yalikuwa ni maonyo ya Yesu aliyekuwa katika mateso akionya juu ya watoto wa Yerusalem ya kuwa watapitia mateso makali na makubwa sana kutokana na kizazi kile kumsulubisha mwokozi, Yesu anaonya kuwa itakuwa dhiki ya hatari ambayo watu watasema heri matumbo yaliyo tasa, kuashiria huzuni kubwa itakayowapata wayahudi kwa kuona watoto wao wakiuawa, Yesu anawaonya wao kuwa tayari kwa hukumu hiyo na kuwataka kuwa afadhali watubu na kujihurumia wenyewe.

Aidha katika somo hili la njia ya msalaba tunaonywa kuwa hatupaswi tu kuhuzunika kwaajili ya kuteswa na kufa kwa Yesu Kristo badala yake tunapaswa kuwa na ufahamu kwanini alikufa na faida ya kifo chake inatuletea wokovu, huzuni kubwa na mbaya zaidi sio kwa sababu Yesu anateswa na kufa bali kama sisi tutakosa nafasi ya kuzifurahia faida za msalaba.

Yesu aliendelea kuonya kuwa ikiwa wanaufanyia hivi mti mbichi itakuwaje kwa mti mkavu,  lilikuwa ni onyo pia kuwa kama mtu mwema kama Yesu anatendewa ukatili kama ule hebu jaribu kufikiri wale wasio na toba, kama Mungu anaruhusu mateso kama haya kwa mtu mwenye haki, kutatokea nini kwa wale wasio haki.

Yesu alionya kuwa ni lazima watu watambue kuwa Mungu ni Mungu mwenye haki na atahukumu kwa dhati, na kamwe watu wasichukulie uvumilivu wake kama nafasi ya kujifanyia wanayoyataka, ni lazima tuwafundishe watoto wetu kuishi maisha ya haki na kuikulia njia ya Bwana, aidha kile alichokisema Yesu kwa wanawake wa Yerusalem alikwisha kukisema kwa kina kwa wanafunzi wake katika Mathayo 24 akiwaonya kuhusu siku za mwisho na pia kuhusu Anguko la mji wa Yerusalem.

Mathayo 24:2-12 “Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.”

Kitendo cha Yesu kukutana na wanawake wa Yerusalem na kuwaonya wajililie nafsi zao na watoto wao kinatukumbusha wajibu wetu kama kanisa kuzingatia na kukumbuka maonyo yote kuhusu unabii wa siku za mwisho, tunakumbushwa kuwa tunaishi katika nyakati za hatari na kwa sababu hiyo kila mtu anapaswa  kuchukua tahadhari na kujikumbusha kuwa kanisa hatuko salama na badala yake ni jukumu la kila mkristo kujitazama na kujihami na kuzipima roho/mafundisho ya watumishi wa Mungu katika nyakati hizi za hatari.

1Timotheo 4:1-2 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

2Timotheo 3:1-5 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.”

Kristo pia anatukumbusha wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa tunajiangalia sisi wenyewe kuwa tukoje na Mungu badala ya kunyoosha vidole kwa wengine, tunafundishwa kuacha kufikiria wengine wanapopitia shida na changamoto kuwa labda huenda wana makosa makubwa kuliko yetu na badala yake tunakumbushwa kujiangalia wenyewe na kutubu kwa sababu kama wenye haki wanateseka ni zaidi sana kwa mtu asiye haki hataweza kustahimili

Luka 6:41-42 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.”

Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”    

Tangu zamani imekuwepo dhana Fulani ya kufikiri kuwa wale wanaopatwa na mabaya labda walikuwa waovu kuliko sisi, au wanaopatwa na ajali, Lakini Yesu anatukumbusha kuwa wao wanaweza kuwa sio waovu kuliko waliobaki na hivyo iko haja ya kuitumia nafasi tuliyo nayo ya Amani na uhai kwaajili ya toba na kujiweka tayari kwaajili ya Mungu wetu

5.       Yesu anavuliwa nguo # 10

Tunajifunza Nini Kupitia Kitendo cha Yesu Kuvuliwa Nguo Kabla ya Kusulubiwa? Kitendo cha Yesu kuvuliwa nguo kabla ya kusulubiwa ni sehemu muhimu ya mateso yake, na kina maana kubwa kiroho na kimaandiko. Tukio hili linatajwa katika Injili zote nne:

·         Mathayo 27:28, 35 – “Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu.35 Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.]

 

·         Marko 15:20, 24 – “Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe... Wakagawana nguo zake, wakizipigia kura waone nani atakaye pata kitu gani.”

 

·         Luka 23:34 – “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wale wakagawana mavazi yake kwa kura.”

 

·         Yohana 19:23-24 – “Askari walipomsulubisha Yesu, walitwaa mavazi yake, wakayagawa mafungu manne, kila askari Fungu Lake; na lile joho lake pia. Na hilo joho halikuwa na mshono, limetengenezwa kwa kipande kimoja tangu juu hata chini. Wakaambiana, ‘Tusilikate, ila tuzipige kura tupate kujua litakuwa la nani.’ Hii ilikuwa ili andiko litimie, lililosema: Wamegawana mavazi yangu kati yao, na nguo yangu wameipigia kura.”

Maana na Mafundisho Tunayopata Kutoka kwa Kitendo hiki

a.       Utimilifu wa Unabii wa Agano la Kale- Kitendo hiki kilikuwa ni utimilifu wa Zaburi 22:18 – “Wamegawana mavazi yangu, na nguo yangu wameipigia kura.”

Hii inaonyesha kuwa mateso ya Yesu hayakuwa ya bahati mbaya bali ni sehemu ya mpango wa Mungu uliotabiriwa tangu zamani. Yesu alikuwa akiyatimiza mapenzi ya Mungu, na kila andiko alilokuwa ameandikiwa, kwa hiyo hakuna kilichotokea Msalabani ambacho kilitokea kwa bahati mbaya hii inadhihirisha wazi kuwa haya yalikuwa ni mapenzi ya Mungu.

 

b.      Yesu alihisi aibu na fedheha kwa ajili Yetu - Kuvuliwa nguo hadharani ni tendo la aibu na fedheha. Kwa Wayahudi, kuona mtu akiwa uchi hadharani lilikuwa jambo la kudhalilisha sana, kitendo cha kuwekwa uchi ni kitendo cha kuaibishwa ni tukio la kudharaulika sana, hili ndio tukio lililomtokea Adamu na Eva katika Bustani ya Edeni walipokula lile tunda walilokatazwa, wakati wote tunapotenda dhambi tukumbuke kuwa tunajiweka katika aibu na tunajivua nguo, Yesu anapovuliwa nguo anatukumbusha wajibu wetu ya kuwa ni yeye pekee anayeweza kutuvalisha vazi lililo bora, kwani pale msalabani alivuliwa nguo kwaajili ya matendo yetu, alifanywa vile kwa sababu dhambi zetu zilizowekwa juu yake na dhambi kwa kweli ni aibu mbele za Mungu.

 

Isaya 47:3 “Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.”

 

Nahumu 3:5-6 “Tazama, mimi ni juu yako, asema Bwana wa majeshi; nami nitafunua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonyesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau.”

 

Isaya 53:3-5 – “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

 

Waebrania 12:2 – “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu

 

Hii inatufundisha kuwa Yesu alikubali fedheha yetu ili sisi tupate heshima mbele za Mungu. Yesu Aliacha Kila Kitu kwa Ajili Yetu-Yesu alipovuliwa nguo, alikuwa hana kitu chochote cha kidunia. Hii inatuonyesha kuwa alijitoa kikamilifu kwa ajili ya wokovu wetu: Hili linatufundisha kuwa hakuna kitu cha kidunia kinachopaswa kutuzuia kumfuata Kristo, lakini pia tubakumbushwa ile kweli ya kuwa hatukuja duniani na kitu na tutaondoka duniani bila kitu.

 

2 Wakorintho 8:9 – “Kwa kuwa mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, ya kwamba alipokuwa tajiri, alikubali kuwa maskini kwa ajili yenu, ili ninyi mpate kuwa matajiri kupitia umaskini wake.”

 

Yesu analishauri kanisa kujificha kwake kwa toba katika ulimwengu wa roho tunapotubu na kucha maovu yetu Yesu hutuvika mavazi meupe na kutuficha dhidi ya aibu yetu na kutuondoa katika mashaka

 

Ufunuo 3:17-19 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”

 

Kama Mungu alivyomfunika Adamu kwa mavazi yaliyo bora katika bustani ya Edeni atatuhifadhi sisi kwa haki yake kwani yeye alifanyika dhambi ili sisi tuwe haki

 

2 Wakorintho 5:21 – “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu ndani yake.”

Dunia ilimnyima Yesu Heshima yake yote, Lakini yeye alituheshimisha, na kutokana na kukubali kudharauliwa kwa kiwango hicho Yesu ameinuliwa juu kuliko mtu awaye yote na amekekirimiwa jina lipitalo majina yote na ameketi mkono wa kuume wa nguvu wa Mungu baba mwenyezi mbinguni.


6.       Yesu anawambwa Msalabani na kusulubiwa # 11

 

Yohana 19:16-18 “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati.”

 

Yesu alifanya kazi nyingi sana za kuponya na kufundisha watu neno la Mungu lakini moja ya kazi muhimu kabisa aliyoifanya na kuikamilisha ni kufa msalabani kwaajili ya dhambi za ulimwengu kupitia njia ya kusulubiwa msalabani

 

Mathayo 1:21 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”

               

Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”

 

Pamoja na tukio hili Mateso yake, kufa kwake na kufufuka kwake msalabani, Yesu ilikuwa sio tu anapaswa kufa lakini pia analipaswa kufufuka kwaajili yetu, kitendo cha yeye kufufuka kinampa nafasi ya kuwa kuhani mkuu na mwombezi na mpatanishi kwaajili yetu huko mbinguni

 

Warumi 8:33-34 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”

 

Warumi 4:24-25 “bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.”

 

Warumi 5:9-11 “Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.”

 

Kusulubiwa kwake msalabani kunatukumbusha upendo mkubwa sana wa Mungu kwa wanadamu ambapo Mungu kwa hiyari yake mwenyewe anaamua kuwakomboa wanadamu kwa adhabu aliyojipa yeye mwenyewe kwa ajili ya upendo wake kwetu

 

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

 

7.       Yesu Kristo anafia msalabani # 12

 

Mathayo 27:45-50. “Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.”

 

Kitendo cha Yesu Kristo kufa msalabani kinathibitisha wazi kuwa Yesu aliikamilisha kazi yote na unabii, hata alipopaza Sauti na kusema imekwisha Yesu alikuwa na maana ya kuikamilisha kazi yote aliyokuwa ameandikiwa aikamilishe, Yesu alihakikisha kuwa kila neno lililonena na Mungu limetimia na hivyo hakukuwa na unabii wowote kuhusu mateso yake ambao ulikuwa haujatimia

 

-          Kazi ya upatanisho kati ya Mungu na wanadamu ilikuwa imekamilishwa Warumi 5:10 “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.”

 

-          Kristo alikuwa amefanyika sadaka kamili ya dhambi kwaajili yetu Waebrania 10:10-14 “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.”

 

-      Kazi ya kuwashinda maadui wakubwa wa mwanadamu, Shetani, dhambi na mauti ilikamilishwa, kwa kifo chake msalabani alilipa deni la dhambi, na kumvua shetani enzi na mamlaka

 

Wakolosai 2:14-15 “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

 

Waebrania 2:14-15 “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.”

 

8.       Yesu anashushwa Msalabani # 13

 

Yohana 19:38-40 “Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.”          

 

Kitendo cha mwili wa Bwana Yesu kushushwa kutoka msalabani na kufanyiwa maandalizi ya kuzikwa kilikuwa ni kitendo kinachotufundisha unyenyekevu mkubwa, Kumbuka yeye alikuwa ni mwana wa Mungu lakini hapa alikuwa amekufa, mtu aliyefariki dunia huwa hajimudu kabisa, anafanyiwa kila kitu anasaidiwa na wanadamu wenzake, huu ndio wakati ambapo tunawahitaji wanadamu wenzetu washughulike na sisi, wawe masikini au matajiri, tunajifunza kuwaheshimu watu na kutembea duniani kwa unyenekevu.

 

Wale waliokuja kumzika Yesu Kristo kama rafiki yao na mwalimu wao, walionyesha upendo wa kweli hata katika wakati mgumu lakini maziko makubwa ya heshima walioyafanya yanatukumbusha kuwa kila mwanadamu duniani hata kama alizarauliwa kiasi gani anapaswa kuzikwa kwa heshima zote, Yesu anatimiza unabii wa Samsoni ambaye alikataliwa na kukosa heshima alipokuwa akali hai, lakini alipofariki nduguze walikuja kuutwaa mwili wake na kumhifadhi, alidharauliwa alipokuwa hai na aliheshimiwa sana baada ya kifo chake.

 

Waamuzi 16:31. “Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.”

 

Ingawa Yesu alishushwa kama maiti isiyokuwa na uwezo wowote yeye bado alijua kuwa atafufuka, Yesu anatufundisha kuwa kifo sio mwisho wa kila kitu, kwani liko tumaini la maisha mapya, mtu akimuamini Yesu hafi bali anapita kutoka mautini na kuingia uzimani

 

Yohana 11:25-16. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

 

9.       Kristo Yesu anazikwa  Kaburini # 14

 

Tendo la kuzikwa kwa Yesu Kristo linathibitisha kuwa Yesu alikufa kweli kimwili kwaajili ya dhambi zetu, Yesu alizikwa pia kama sehemu ya kutimiza unabii kuhusu kuzikwa pamoja na waovu

 

Yohana 19:41-42 “Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye yote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.”

 

Isaya 53:8-9 “Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”

 

1Wakorintho 15:3-4 “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;”   

 

Mathayo 12:39-40 “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.”        

 

Tendo la kukubali kuzikwa linatufundisha unyenyekevu mkubwa aliokuwa nao Bwana wetu Yesu Kristo, unyeyekevu huu hatimaye ulimuinua sana Bwana Yesu, kimsingi tunajifunza hata kuwa njia mojawapo ya juu kabisa ya ukristo ni pamoja na unyenyekevu, unyenyekevu hutupelekea kuinuliwa juu sana na Bwana.

 

Wafilipi 2:5-8 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

 

Mambo yasiyo ya kibiblia katika njia ya Msalaba.

Njia ya msalaba ni fundisho muhimu sana linalohusiana na tafakari ya kile kilichomkuta Bwana wetu Yesu Kristo wakati wa mateso yake, kutafakari kuhusu mateso ya Bwana Yesu hakutufanyi sisi kuwa na huzuni bali kunatufanya kuwa na furaka kwa sababu ndio njia iliyochaguliwa na Mungu kwa ukombozi wetu, kwa hiyo njia ya msalaba ina mambo mengi muhimu ya kutufunza kibiblia, hata hivyo kuna mambo yasiyo ya kibiblia ambayo tunaweza kuyachukulia tahadhari

-          Maandiko hayajaeleza kokote pale kwamba Yesu aliwahi kuanguka na msalaba, tunaweza kuona kuwa ni kweli Yesu alikuwa dhaifu kiasi cha kusaidiwa Msalaba wake na Simeoni Mkirene lakini swala la Yesu kuanguka na msalaba mra ya kwanza na ya pili na ya tatu halina rekodi yoyote katika maandiko na ingawa inaweza kuwa hivyo katika historia na masimulizi ya kale lakini hatuwezi kuwa na msimamo thabiti kwa sababu Biblia iko kimya kuhusu matukio hayo  kwa sababu hiyo kituo cha tatu Yesu kuanguka na msalaba mara ya kwanza  na kituo cha saba Yesu kuanguka na msalaba mara ya pili na kituo cha tisa cha Yesu kuanguka na msalaba mara ya tatu hakiwezi kujumuishwa katika fundisho la kibiblia kwa sababu hakuna mwanafunzi wa Yesu aliyeandika hilo wala waandishi wengine wala mitume hawajawahi kugusia hilo kokote, Penginepo pia hakuwezi kuwepo na fundisho zuri linalohusiana na kuanguka.

 

-          Kuhusu swala la Yesu kukutana na mama yake njiani wakati wa mateso pia linaweza kuwa na utata kwa sababu Biblia iko kimya, lakini tunao uhakika kuwa Mariamu na ndugu za Yesu zake Yesu Kristo walikuwepo wakati Yesu anasulubiwa lakini hatujaelezwa kuwa walikutana mahali fulani njiani isipokuwa kwa masimulizi ya wakristo wa nyakati za kanisa la Kwanza kwa sababu hiyo tukio hili linalotengeneza kituo cha nne  miongoni mwa wakatoliki na Anglican hatukiingizi katika fundisho la njia ya msalaba, maandiko yanaonyesha ni kama Yesu alimuona mama yake na wanafunzi wake akiwa tayari ametundikwa juu ya msalaba hata kama inawezekana mama yake aliongozana na watu waliofuatilia mateso

 

Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”

 

-          Kuhusu swala la Yesu kukutana na Mwanamke aliyeitwa Veronica na kuwa mwanamke huyu alimfuta jasho lake na picha ya Yesu ikasalia katika kitambaa cha mama huyu, pia ni swala la kimapokeo na masimulizi tu na hakuna taarifa za kibiblia, aidha jina Veronica kimsingi sio jina la asili la Kiyahudi jina hilo ni la kilatini, na katika kigiriki labda jina Berenice la Ugiriki au Makedonia lingeweza kutumika, jina Veronika lina asili ya maneno mawili ya kilatini “Vera Icon” ambalo tafasiri yake ni true image kwa hiyo masimulizi kuhusu mwanamke huyu na tukio la picha ya Yesu kubaki katika kitambaa chake halina uthibitisho wa kimaandiko kwa sababu hiyo kituo cha sita kinachohusiana na uwepo wa Veronika hakina uhalali wa kimaandiko kwa hivyo kuanguka wa Yesu mara tatu, kukutana na Mariamu na kukutana na Veronica kunaingia katika kundi la mambo yasiyo ya kibiblia.

 

-          Jambo lingine ni kuwa hakuna sababu ya kutumia picha au sanamu katika kuadhimisha au kujikumbusha kuhusu njia ya msalaba kwani njia hiyo ipo kule Yerusalem na picha za kila kituo zipo kwa hiyo picha za vituo zinaweza kutumika katika kufundisha mafundisho yote ya njia ya malaba kwani siku hizi watu wanaelewa tofauti na miaka ya zamani ambapo watu wengi walikuwa hawajui kusoma na kuandika, mfano picha niliyoitumia mimi katika kielelezo hapo juu ni picha ya njia halisi hiyo aliyoitumia Yesu iitwavyo via dolorosa na njia hiyo ipo hata leo kule Yerusalem nchini Israel

 

-          Fundisho kuhusu njia ya msalaba sio la kikatoliki na Anglican pekee linauhusu mwili wa Kristo na hivyo kila Mwalimu wa neno la Mungu anaweza kulitumia kwa mafundisho sahihi na semina za pasaka katika kuwatafakarisha watu mateso na kifo cha Bwana Yesu na wakato wowote tunapotaka kutafakari au kujikumbusha kuhusu aina ya mauti na mateso aliyokutana nayo Yesu.  Kupitia fundisho hili ni Imani yangu kuwa walimu wa neno la Mungu watapata ufahamu mkubwa zaidi wa kuyaweka sawa mafundizho haya kwa njia iliyo bora zaidi katika siku za usoni.

 

Yohana 8:31-32 “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”


Na Rev. Innocent Samuel Kamote.


Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Ijumaa, 11 Aprili 2025

Neno la Mungu halifungwi!


2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.”

 


      

Utangulizi

Kauli ya kuwa Neno la Mungu halifungwi, ilitamkwa na Mtume Paulo ambaye wakati huu alikuwa kifungoni, Paulo alifungwa na kupitia mateso kwa sababu alikuwa akiihubiri injili na kufundisha watu Neno la Mungu ambalo alikuwa na Imani kwamba litawafungua watu kutoka dhambini na kuwaelimisha, Hata hivyo kutokana na njama za shetani Paulo mtume mara kadhaa aliwekwa kizuizini na kufungwa gerezani shetani akifikiri ya kuwa kwa kufanya hayo ataweza kuzia kasi ya injili na utendaji wa Roho Mtakatifu katika maisha ya muhubiri huyu Mashuhuri wa karne ya Kwanza, Hata hivyo Paulo Mtume alikuwa na ujuzi na uzoefu  ya kuwa Neno la Mungu halifungwi!, vizuizi kwa Paulo mtume kamwe havikuweza kudhoofisha Nguvu ya injili, kwani wakati mwingine aliweza kuhubiri akiwa kifungoni na kuwafikia wengi huko na zaidi ya yote alipata nafasi ya kuandika mafundisho ambayo kimsingi yaliweza kuinua kwa kiasi kikubwa maisha ya waamumini wa makanisa wa nyakati za kanisa la Kwanza hata leo, kwa hiyo tunajifunza ya kuwa licha ya mateso, vikwazo na vifungo mbali mbali ambavyo tunakutana navyo kwaajili ya injili kumbe Neno la Mungu halifungwi!

2Timotheo 2:9 “Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.”                

Kwa Msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani usemi wa Paulo kuwa neno la Mungu Halifungwi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Injili ina nguvu kuliko vifungo vya gerezani

·         Mifano ya watu waliofungwa kwaajili ya injili

·         Neno la Mungu halifungwi!

 

Injili ina nguvu kuliko vifungo vya gerezani

Wote tunafahamu kuwa habari njema za Yesu Kristo zina nguvu kubwa sana ya kuwafungua watu na kuwaweka huru kutoka katika vifungo mbalimbali vya shetani pamoja na utumwa wa dhambi, ni ukweli usiopingika kuwa injili ni uweza wa Mungu uletao wokovu, kwa kila aaminiye bila kujali anatokea katika utamaduni wa aina gani, wala bila kujali hekima au elimu aliyonayo mtu.

Warumi 1:14-16 “Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi. Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”

Kwa utambuzi na uzoefu wa namna Paulo alivyoona injili ikiwasaidia wengi na kuwafungua kutoka katika vifungo vya giza na dhambi, Paulo aliendelea kushikwa na shauku ya kuihubiri injili kila mahali na kila wakati, hata hivyo katika namna ya kushangaza sana Paulo mtume mara kadhaa alikamatwa na kutiwa gerezani, kama muhalifu/au mtenda mabaya kwa sababu ya injili aliyokuwa anaihubiri, Paulo alitamani sana kuwa huru ili aweze kuieneza injili, Lakini Ibilisi alikusudia kumzuia na sio tu kuwa aliwekwa gerezani lakini pia alilindwa na askari na kufungwa kwa minyororo kama moja ya wahalifu hatari sana, kwa hiyo mara nyingine aliwaandikia makanisa mbalimbali wamuombee, ili afunguliwe kinywa na kuihubiri injili kwa ujasiri mkubwa, Lakini hata hivyo alikuwa amefungwa

Waefeso 6:18-20 “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”

Katika hali ngumu kama hiyo, akiwa gerezani, na katika vifungo na chini ya mikatale akiwa mfungwa au mjumbe wa minyororo bado anawaomba kanisa kumuombea ili apewe ujasiri aendelee kulisema neno la Mungu, Paulo alifanya hivyo akiihubiri injili kwa wafalme, wafungwa na wakuu wa magereza ambao kimsingi walifunguliwa na walipata neema ya kusikia habari njema licha ya kuwa Mtumishi wa Mungu alikuwa katika minyororo, aliendelea kuhubiri kwa ujasiri mahakamani, kwa mahakimu na wasikilizaji lakini pia aliendelea kuandika nyaraka mbali mbali ambazo zilikuwa na mafundisho mazuri na ya msingi akiyatia moyo na kuwajenga wale aliokuwa amewahubiri injili pamoja na mwili wa Kristo kokote uliko ulimwenguni.

Matendo 26:27-29 “Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.”

Vifungo havikumzuia Paulo Mtume kuihubiri injili, alihubiri kwa ujasiri wote, alihubiri wafalme mahakamani na wasikilizaji wa kesi wote akiendelea kuwashawishi waijuie injili na kumuamini Mwana wa Mungu, Paulo hakujali injili inahubiriwa wapi, alikuwa gerezani lakini alitamani watu wote wabadilike wawe kama yeye isipokuwa vifungo vyake tu, kwa maneno yake na matendo yake inatufundisha kuwa injili ina nguvu kuliko magereza, magereza ilikuwa shimoni, mwanga ukiwa hafifu sana lakini Moyo wa Paulo uliendelea kumuwaka akiwa na shauku ya kuisema injili, kufungwa kwake kulitumiwa na maadui kama njia ya kuhubiri kwa fitina injili isiyofaa lakini kulitumiwa na watu wazuri kuwapa ujasiri wa kuisema injili kwa nguvu kubwa huku yeye akiendelea kuandika nyaraka za kuwatia moyo makanisa mbalimbali na mwili wa Kristo.

Wafilipi 1:12-13 “Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu.”

Neno la Mungu limedhihirika kuwa na nguvu sana kuliko mipaka ya kibinadamu na utendaji wa shetani, Injili ina nguvu kuliko vifungo vya gerezani, ina nguvu kuliko vizuizi vya shetani, ina nguvu kuliko vifungo vya kidini, ina nguvu kuliko wivu wa wanadamu na husuda zao, injili haiwezi kuzuiwa na mtu yeyote, wala haiwezi kuziwa na vita vya kijinga vya maadui wa injili, Injili itaendelea kuhubiriwa hata kwa kalamu, itapelekwa kwa mitandao ya kijamii, itapenya kwa sauti za Redio na televisheni, hakuna dhehebu, wala dini, wala taifa, wala ufalme, wala bara, wala kisiwa ambacho kitaweza kuizuia injili, nguvu za giza haziwezi, mapepo na majini hayawezi, mila na desturi haziwezi injili ina nguvu kuliko maregeza yoyote ile, inaweza kupenya kwa askari, inaweza kupenya kwa daktari, inaweza kupenya kwa mkulima, inaweza kuwafikiwa wachimba madini, inaweza kuwafikia wanasiasa, inaweza kumfikia yeyote yule kwa njia yeyeote ile, Paulo alitumia mateso yake na vifungo vyake kumkumbusha Timotheo na kumtia moyo kwamba asiogope kwani Yesu aliteseka pia kwaajili ya injili, lakini alifufuka, hakuna mateso yanayoweza kuizuia injili, wala hila, wala vifungo neno la Mungu litaendelea mbele, wapinzani watakufa lakini neno la Mungu halifi, hivyo kila Muhubiri wa injili hapaswi kuogopa kuisema kweli ya Mungu kwa sababu watu wa Mungu watafunguliwa kwa injili ya kweli na sio injili ya hila na uongo hubiri kweli saidia watu kuwa huru na unaweza kwa injili.

Mifano ya watu waliofungwa kwaajili ya injili

Ni muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuihubiri injili katika mazingira yoyote yale yawe magumu yawe laini, bila kujali kwamba kuna vikwazo vya aina gani, kumbuka kuwa kwa kadiri siku zinavyokwenda mbele upinzani wa kiinjili unaendelea kuchukua sura mpya, shetani sasa anaweza kuwatumia viongozi wa kidini na kidhehebu kuhakikisha kuwa wanakuziba kinywa ili usihubiri injili, kumbuka tu kuwa watakatifu waliotutangulia wote waliopewa maagizo ya neno la Mungu walipitishwa katika nyakati ngumu na kufungwa na kuzibwa vinywa vyao kwaajili ya injili hata hivyo bado tunaonyeshwa ya kuwa neno lilisimama na wale waliokuwa huru waliisema injili kila mahali.

1.       Paulo na Sila walipokuwa wakiihubiri injili ambayo ilifungua watu na zaidi sana mwanamke mwenye pepo wa uaguzi, mji ulitaharuki, wakafanyiwa ghasia, wakapelekwa mahakamani, wakisingiziwa kesi ya kuchafua mji, wakavuliwa nguo, wakapigwa kwa bakora, wakatupwa gerezani wakafungwa miguu yao kwa mikatale wakiwa wamepokea mapigo mengi, hawakuweza kutulia walipokuwa ndani gerezani wakifungwa kama wahalifu hawakukata tamaa, wala hawakunyamaza, waliendelea kuisema injili walimwimbia Mungu na kuomba usiku kucha, Na Mungu akatuma tetemeko kubwa gereza na vifungo vyote vya watu wote vikaaachia na hatimaye mkuu wa gereza na nyumba yake wakaokoka, shetani kwa ujinga wake alifikiri kwa kumuweka Paulo na sila kizuizini ataizuia injili na badala yake injili iliwafikiwa wafungwa wote na mkuu wa gereza na familia yake wote waliokoka na kubatizwa

 

Matendo 16:19-34 “Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji; wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi. Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.”

               

2.       Petro na Yohana  - Waliwekwa gerezani na wakuu wa makuhani na masadukayo kwaajili ya wivu walipokuwa wakiihubiri injili na kuijaza Yerusalemu mafundisho yao, wakuu wa makuhani na wazee wa dini waliwakataza wasihubiri kwa jina la Yesu wala nguvu zake za ufufuo na kuamua kuwaweka gerezani, lakini malaika wa Bwana alikuja kwa muujiza na kuwafungua na kuwaagiza tena wakaseme habari njema na kuendelea kuwafundisha watu

 

Matendo 4:1-20 “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano. Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.

 

Matendo 5:18-25 “wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.

 

3.       Yeremia nabii alifungwa lakini neno la Mungu lilienea - Historia na tabia ya Mungu inaonyesha ya kuwa neno lake halijawahi kufungwa wala kuwekwa kizuizini, shetani anaweza kutumia hila kuwatesa na kuwaweka kizuizini watumishi wa Mungu lakini Historia inamuhukumu kuwa hajawahi weza kushidana na Roho wa Mungu na Hekima aliyo nayo Mungu katika kuyahifadhi mapenzi yake, Yeremia yeye alitiwa Gerezani kwa sababu ya kuwaonya watu kuhusu kuharibiwa kwa Yerusalem na hekalu pia, lakini pamoja na kufungwa aliendelea kupenyeza ujumbe wa Mungu kwa mfalme na unabii wa ujumbe wa Mungu kwa watu wake uliendelea

 

Yeremia 37:15-17 “Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza. Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi; ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.”               

 

4.       Yesu Kristo aliuawa kwaajili ya injili – Wakuu wa dini na makuhani walipanga njama za kummaliza Yesu, walifikiri kwa ufupi ya kuwa wakimmaliza basi watakuwa wameondoa ujumbe wake na kupunguza kadhia ya kusikia Yesu akiwa maarufu siku hadi siku, walimsingizia mengi, walimtesa, aliteswa sana alipigwa mijeledi mikali, walimdhihaki na kumsulubisha msalabani, hawakujua ya kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kiinjili, Mwanaume huyu mmbora alifufuka siku ya tatu na habari zake zilihubiriwa mpaka leo na yeye ameamuru habari hizi na mafundisho yake yahubiriwe na kufundishwa kwa wanafunzi wa mataifa yote

 

1Wakorintho 2:6-8. “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.

 

Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.   

 

Kifo cha Yesu Kristo cha mateso, kileleta ukombozi mkubwa sana kwa wanadamu na kusababisha neno la Mungu kuenea kwa kasi kubwa duniani, tunajifunza hapa kuwa neno la Mungu sio tu kuwa halifungwi lakini halizikwi, ni kukosa hekima na ni ujinga mkubwa kujaribu kuizuia injili kwa sababu zozote zile, kila wakati shetani anapojaribu kuleta vikwazo kuizuia injili anakuwa kama mtu anayechochea moto na kusababisha chakula kiive haraka, upinzani mkubwa ulisababisha kazi kubwa na ueneaji mkubwa wa injili, Ndugu haijalishi wanaoizuia injili ni makuhani, au wakuuwa dini au mafarisayo au masadukayo au wanasiasa vyovyote iwavyo Neno la Mungu litaendelea  na hakuna mwanadamu anayeweza kizuia injili. Mtu akiifunga injili malaika wa Bwana watakunong’oneza kwa kukuambia Enendeni mkasimame mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu!

 

Matendo 5: 18-21bwakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha

Neno la Mungu halifungwi!

Tumeona na sasa unaweza kukubaliana na ukweli wa maneno ya Paulo mtume ya kuwa neno la Mungu halifungwi, Katika historia nzima ya dunia tumeona shetani akiwatumia watu na wafalme na mataifa mbalimbali kuzizuia habari za Yesu, lakini pia madhehebu na viongozi wa dini wakiwa sababu ya kuizuia injili lakini daima shetani na maajenti wake wote wamethibitisha kufeli, usikubali kupoa, usikubali moto wa injili uzimike katika maisha yako, ni lazima tuhakikishe ya kuwa tunakirithisha kijiti hiki au mwenge huu au nuru hii kwa kizazi kingine waipeleke injili bila kujali vikwazo wanavyokutana navyo, Mateso, upinzani na vifungo kamwe havijawahi kuwa sababu ya kuizuia injili na badala yake kama upinzani wa upepo kwa ndege inayotaka kupaa ndio ulivyo upinzani wa injili husababisha moto uwake na kukolea zaidi.

2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.”

Tunao ushuhuda ya kuwa mataifa mengi, wafalme wengi na wenye mamlaka wengi wamejaribu kuipinga injili lakini injili imeenea kila mahali ulimwenguni, yako maeneo ambayo Biblia imepigwa marufuku lakini uthibitisho tulio nao leo duniani ni kuwa bado ndicho kitabu kinachoongozwa kwa kusomwa zaidi duniani, Yako makanisa yamefungwa na wako wakristo ambao wako katika mateso ya aina mbalimbali, lakini hayo hajayasaidia kuifanya injili isisonge mbele, wewe nawe mtu wa Mungu unaweza kuwa unapitia vikwazo vya namna mbalimbali, wakuu wa dini wanakukandamizia, hawataki uibuke, wanataka upotee kwa sababu una mafundisho sahihi, una injili iliyo sahihi wewe bado ni wa moto nataka kukutia moyo ya kuwa unayoyapitia hayawezi kukufanya unyamaze neno la Mungu litaendelea  kila kitu duniani kitapia lakini maneno ya Mungu hayatapita kamwe, Kama makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika kumbuka ya kuwa kusudi kubwa la Mungu ni injili hakuna mtu anayeweza kuizuia injili lihubiri neno bila kujali wakati unaofaa na wakati usiofaa hubiri neno!

Isaya 40:7-8 “Majani yakauka, ua lanyauka; Kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.”

Hitimisho;
Neno la Mungu halifungwi, Paulo mtume alikuwa na ufahamu huo ya kwamba hata ingawa yeye yuko kifungoni, hekima ya shetani imeshindwa kwa hekima ya Mungu, shetani hakuweza kuzuia kabisa ujumbe wa kitume usiwafikie watu, watu hawakuweza kuisikia sauti yake lakini mafundisho yenye uzima yaliwafikiwa watu kupitia nyaraka zake, hakuna mwanadamu anayeweza kulifunga neno la Mungu na kufanya hivyo ni upuuzi na hekina ya kibinadamu na ya shetani, Shetani hawezi kuzuia mpango wa Mungu, kila wakati mipango ya giza imehibitisha kufeli vibaya, mateso na vifungo havujawahi kuwa mwisho wa kazi ya Mungu, badala yake imekuwa njia ya kuonyesha utukufu wake na nguvu,  injili itaendelea kuhubiriwa na kufundishwa pasipo hofu hata kama tutakutana na vikwazo, Mungu atafanya kila njia ili kwamba neno lake lizidi kukua  na kuenea Je umekuwa unakabiliwa na hofu kama Timotheo kwaajili ya vikwazo? Usiogope neno la Mungu halifungwi!

Marko 13:31 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Ijumaa, 4 Aprili 2025

Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia!

 

Luka 7:19-23 “Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika ulimwengu tulio nao wakati mwingine wako watu ambao wangependa kujua uko wapi na unafanya nini na ni kitu gani kinaendelea katika maisha yako, wakati wote watu hao watataka kujua unaendeleaje, unafanya nini sasa na mbona siku hizi uko kimya, wao ni kama hawana kazi nyingine lakini kazi yao ni kufuatilia tu maisha ya watu na kutaka kujua uko wapi na unafanya nini na nini kinaendelea katika maisha yako, watu hawa ni kama wasoma nyota tu, wana yao lakini wanataka kujua habari zako, watataka kujua kama nyumba yako uliyojenga umemuachia nani, watataka kujua una gari? Watataka kujua una watoto wangapi? Wanataka kujua mwanao yuko wapi na anasoma shule gani, wanataka kujua hali ya mkeo ikoje, wanataka kujua hata habari za rafiki zako fulani yuko wapi? Je mmewasiliana? Yaani wao ni kutaka kufahamu tu kuwa unaendeleaje? Na kupeleleza kila kinachoendelea katika maisha yako! Sijui kama umewahi kubaini wako watu wa namna hii!. Leo tutachukua Muda kujifunza namna ya kuwajibu watu hao kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, kuna namna Yesu anatufundisha nzuri sana ya kuwajibu wambeya na wapelelezi wanaotaka kujua maisha yako yanaendeleaje! Katika kifungu cha maandiko Luka 7:21-23 Yesu anaufunua moyo wake akionyesha asili yake Yeye ni nani na ametumwa kufanya nini, “He was a man in mission” Yesu alikuwa ni mtu wa kazi, kuna shughuli aliyokuwa ameandikiwa kuja kuifanya na alikuwa akiifanya kwa uaminifu, Maandiko yanaonyesha wazi na mara kadhaa Yesu aliweka wazi kuwa alikuja kufanya nini “He was an man with his assignment” alikuwa ni mtu mwenye shughuli zake!

-          Kutangaza habari njema na kuweka huru walioonewa Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

 

-          Kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

 

-          Kuwa fidia ya wengi kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu Marko 10:45 “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

 

-          Kuishuhudia kweli Yohana 18:37 “Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”

 

-          Kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi Mathayo 28:18-20. “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Kupitia maandiko hayo tunaweza kuelewa kuwa Yesu alikuwa anajitambua yeye ni nani, na yuko duniani kwaajili ya nini na kwa kweli alikuwa akitekeleza lile ambalo kwaajili ya hilo alizaliwa, unapouliza swali kuhusu maisha ya mtu anayejitambua kama ilivyo kwa Yesu Kristo basi ni vema utarajie majibu mazuri kama aliyoyapata Yohana Mbatizaji alipotaka kujua kama Yesu ndiye yule ajae au tumtazamie mwingine?  Tutajifunza somo hili Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?    

·         Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia


Wewe ndiwe yule ajaye au tumtazamie mwingine?

Ni muhimu kufahamu kuwa Yohana Mbatizaji alikuwa amewekwa kizuizini yaani gerezani tena kwa uonevu tu katika taabu zake na mashaka yake ya kuwekwa kizuizini huku akiwa na hofu kama haki itatendeka au la anapatwa na mashaka sio ya kuhusu maisha yake na kufungwa kwake tu bali hata kuhusu Yesu Kristo kama ni Masihi halisi au la?  Yohana ndiye aliyemtangaza Yesu Kristo wazi na kwa ujasiri kwa jamii na kuielezea jamii ya kuwa Yeye ajaye Nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi naye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”

Lakini sasa akiwa gerezani Yoahana anawatuma wanafunzi wake wakaulize kwa Yesu kama kweli yeye ndiye yule ajaye au tumtazamie mwingine?  Swali hili linaonyesha mashaka aliyokuwa nayo Yohana na matatizo aliyokuwa nayo kwenye kichwa chake alipokuwa gerezani, pia swali linaonyesha kuwa Yohana naye hakuwa ameifahamu vema huduma ya Kimasihi kwa wakati ule Yeye alikuwa akimtarajia masihi ambaye atakuwa na nguvu kubwa sana za kisiasa na kijamii na kama masihi ambaye angeleta mapinduzi makubwa  ya kikoloni na kuwaondoa warumi na utawala wao na Israel kupata uhuru wa kweli kutoka kwa wakoloni hao, kama huduma hii ya kimasihi ingelikuwa ya namna hiyo hata Yeye Yohana mbatizaji angeliweza kuwekwa huru kutoka katika magereza iliyokuwa ikimkabili na mauti penginepo iliyokuwa ikimnyemelea. Yohana alikuwa ameingia shaka kama kweli unabii uliosemwa katika maandiko kumuhusu Masihi ulikuwa ndio huu, kwa maana nyingine alikuwa na mashaka na huduma aliyokuwa akiifanya Yesu Kristo kama ilikuwa huduma sahihi au la? Yeye alikuwa anaona mbona huyu jamaa yuko kimya niko gerezani mbona hafanyi kitu anachopaswa kukifanya?  Kwa hiyo alipata mashaka kuhusu utendaji wa kimasihi!

Luka 7:21-20 “Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?

Swali hili lenye utata linajibiwa na jibu lenye utata la Yesu Kristo ambalo kimsingi lina mambo ya kutufunza leo.

Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia

Jibu la Yesu Kristo kwa wanafunzi wa Yohana na Yohana mwenyewe halikuwa la moja kwa moja  Ndio au hapana  na badala ayake kwanza walimkuta akiendelea na kazi ambayo kazi yenyewe ilikuwa ndio ushahidi wa nini Yesu amekuja kukifanya, Yesu kabla ya kujibu swali hilo kwanza alikuwa “busy” BIZE akishughulika na kuhubiri injili, kufundisha lakini kama haitoshi

-          Aliwafungua vipofu na wengi wakafunguliwa na kuona hapo hapo

-          Aliwafungua wenye ulemavu na wengi walitembea hapo hapo

-          Alitakasa wenye ukoma na wengi walitakasika hapo hapo

-          Aliwafungua waliokuwa viziwi na wengi walipata kusikia hapo hapo

-          Alifufua wafu na wengi walioonekana  na Misiba ilikomeshwa, pepo walikemewa na kutoka  na wagonjwa wengi sana walipokea uponyaji wao

-          Alihubiria masikini habari njema na wengi waliipokea injili

Baada ya kazi hii kubwa aliyoifanya Yesu na wanafuzi wa Yohana Mbatizaji waliishuhudia, kwa macho yao yeye mwenyewe ndipo akajibu kwa kuwaambia Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia.

Luka 7:21-23 “Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.”

Swali kubwa la kujiuliza hapa ni kwa nini Yesu alijibu swali la Yohana mbatizaji katika njia aliyoitumia?  Na ya wazi?

1.       Wajibu watu kivitendo – Siku zote watu wanapoingia mashaka na wewe hupaswi kwa namna yoyote ile kujitetea lakini matendo yako na misheni yako uliyopewa na Mungu itajibu kivitendo kwamba wewe ni mtu wa namna gani, Huduma ya kimasihi ilikuwa imefunikwa na utendaji mkubwa wa kimiujiza na uwezo wake wa kuwahurumia watu na kuwafungua kutoka katika vifungo vyao na mateso yao na misiba yao, kimsingi Yesu alikuwa akiutimiza unabii kwa huduma yake vile vile kama manabii walivyokuwa wametabiri na kupitia kazi alizikuwa akizifanya ilikuwa ni udhihirisho wa wazi kuwa alikuwa ni mtu na shughuli zake.

 

Isaya 61:1-2 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;”

 

Yohana 5:36 “Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma.”

 

Yohana 10:37-38 “Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.”

 

Yesu anatufundisha kuwa ni kwa kufanya kazi na kwa kuonyesha kazi zetu tuzifanyazo tutathibitika kwamba tunayatimiza mapenzi ya Mungu, kama mtu ana mashaka na wewe mjibu kwa kazi za Mungu unazozifanya, namna njema ya kuondoa mashaka katika huduma zetu ni kuonyesha kazi, wewe fanya kazi, ooo huyu vilienda vikarudi waambie nionyeshe kazi, kazi zetu zinatushuhudia kama sisi ni wa Mungu au la, wako watu ni hodari sana wa kuchafua wengine na ni kama wameumbwa wawe wataalamu wa kuharibia wengine maisha lakini waambie waonyeshe kazi zao ni kazi gani wanamfanyia Mungu? Wewe uchukiaye sanamu wateka mahekalu? Mungu hataangalia uso wa mwanadamu Mungu ataangalia kazi tutapimwa na kuthibitika kwa kazi, shuhuda zetu hazitegemei wanadamu zinategemea kazi, kazi itakusemea wewe ni nani, kwa hiyo watu wanapokufuata fuata waonyeshe kazi, Yesu alionyesha kazi ili kuondoa mashaka ya Yohana mbatizaji, Mbinguni tutapimwa kwa kazi fanya kazi acha kupiga domo kazi, ee huyu sijui ilikuwa hivi ikawa vile acha upuuzi onyesha kazi, Kazi ambazo wanafunzi wa Yohana waliziona yalikuwa ni majibu tosha Yesu ni nani!

 

1Wakorintho 3:13-15 “Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

 

Uthibitisho wetu kuwa tumeitwa na Mungu tunatembea na Mungu na tunamtumikia Mungu ni kazi, ile neema ya Mungu iliyoko juu yetu inatenda kazi na inatufanya tufanye kazi zaidi ikiwezekana kuliko wote, watu watajaribu sana kukufanya ukose sifa kwa kukukosoa na kukuchukia na kukuuatilia Lakini ifikie wakati kila mtu aonyesha kazi, kwamba unachangia nini katika mwili wa Kristo kwa sababu kazi zetu zitapimwa, watu wengi walikuwa wakimkosoa Paulo mtume na kumuweka katika viwango vya chini na kumuona kama mtume asiye sahihi Lakini Kazi alizofanya ndio zinajibu kuwa yeye alikuwa ni Mtume wa namna gani? Watu wanaokufuata fiata waambie waangalie kazi

 

1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”                

 

2.       Mtu asikutaabishe – Wako watu ambao ukiwa kazini wanadhani hujui unalolifanya kwa hiyo wanataka wakutaabishe, Maswali ya Yohana mbatizaji hayakumtoa Yesu Nje ya Mstari, badala yake aliendelea kuifanya kazi, kutokujibu swali la wanafuzi wa Yohana mbatizaji kwa haraka na kuanza kupiga kazi kwanza kulikuwa kunamaanisha kuwa usikubali kutaabishwa fanya kazi ile uliyoitiwa wako watu wataabishaji sana hapa duniani hawataki ufanye kile Mungu amekuitia au watataka kukubabaisha ili uondoke katika lile uliloitiwa uanze kujibizana nao, achana na magazeti ya udaku, achana na vyombo vya habari acha kujibizana na watu kwenye mitandao ya kijamii, wewe weka uso wako katika kazi, mtu anayeondoa uso wake katika kazi hafai katika ufalme wa Mungu wewe piga kazi usipoteze mwelekeo hata kidogo, Yesu alipiga kazi, kazi zitajibu

 

Luka 9:59-62 “Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”

 

Wagalatia 6:17 “Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.”

 

Luka 13:31-32 “Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.”

 

Mtu anayejua kusudi la Mungu, na kusudi la kuwepo kwake “a man with a mission” hawezi kutikiswa na kuacha kufanya lile aliloitiwa, Kristo Yesu kwa majibu yake kivitendo alikuwa anatukumbusha kuwa na msimamo katika shughuli zetu na wajibu wetu na yale mambo ambayo Mungu ametuitia acha kusikiliza mambo ya pembeni, pembeni wewe angalia yale ambayo ni mapenzi ya Mungu na ile kazi ambayo Mungu amekuitia kuifanya chukua chapa za Kristo, fanya kazi mtu asikutishe! Wala asikutoe nje ya mstari.

 

3.       Heri mtu yule asiye na mashaka nami - Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami, Yesu alikuwa anahitimisha jibu lake kwa kutaka kumtoa shaka Yohana mbatizaji  kwamba asiye na mashaka naye wala asichukizwe naye, utendaji wake na utoaji huduma zake ulikuwa sawasawa na mapenzi ya Mungu, lakini wakati mwingine haungeweza kuwafurahisha wanadamu, kwa hiyo ingekuwa heri kama wangelikuwa na Imani naye, unapofanya lile ambalo Mungu amekuitia wakati mwingine ni vigumu kueleweka kwa ndugu zetu, jamaa zetu na hata marafiki zetu, kuna namna na jinsi ambavyo watu wanatarajia uwe na utrende katika njia wanazozifikiria wao lakini utendaji wa Mungu na mapenzi yake wakati mwingine unaweza usieleweke kwa wanadamu na ukawakwaza Yesu aliwekwa kwaajili ya kuinuka na kuanguka  wengi  katika Israel

 

Luka 2:25-34 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

 

Huduma ya kimasihi ni yenye utata na yenye kufikirisha, na kuwakwaza wengi, utendaji wake na mafundisho yake yangeweza kusababisha mgawanyiko mkubwa na upinzani mkubwa utakaongoza wengi kujikwaa na wengi kuinuliwa katika Imani, Simeoni alimaanisha Yesu angekuwa na huduma yenye utata  na hivyo kuwa ishara itakayonenwa, Matarajio yake Yohana mbatizaji kuhusu huduma ya kimasihi kwake yangeweza kuwa kwazo kama bado angekuwa haelewi maandiko, ilikuwa ni lazima huduma ya kimasihi ilete utata miongoni mwa jamii lakini ana heri mtu yule ambaye angeamini ambaye hangekuwa na mashaka naye ambaye hatakwazwa na yeye, kukwazwa na huduma ya kimasihi ilikuwa ni jambo la kawaida na lilikuwa limetabiriwa na Isaya na pia Mzee Simeoni

 

Isaya 8:14-15 “Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”

 

Yesu alitaka kumsaidia Yohana Mbatizaji asiwe na mashaka naye aendelee kumuamini, hata kama Yesu hatamtoa gerezani lakini hapaswi kuchanganyikiwa kuhusu Yesu, Yesu hakutaka Yohana awe miongoni mwa wale wengi wataakaojikwaa juu yake, lakini alitaka kumpa jibu thabiti kwamba awe na imani njia za Mungu za kiutendaji ziko juu sana kuliko tunavyofikiri, usikwazike ukiona katika maisha yako ni kama Yesu hashughuliki na wewe usimlaumu wala usiwe na mashaka naye endele kupiga kazi, utendaji wa Mungu ni utendaji wa kipekee na wa ajabu na njia zake ziko tofauti na matarajio yetu na utendaji wake.

Hitimisho:

Njia za Mungu za kiutendaji sio njia zetu, utendaji wa Mungu unazidi utendaji wa fikra ya kawaida ya kibinadamu, ni lazima tuwe tayari kufuata njia na mapenzi ya Mungu, wale watu wanaotaka kujua kuwa tuko wapi tunafanya nini, tunaendeleaje, familia zetu zikoje tuna watoto wangapi, tumejenga au la, tuna mashamba au la, tuna magari au la! tuko wapi tuna ishu gani au la, tunamiliki fedha au la watu wanaofuatilia maisha yako waambie Kazi za Mungu zinaendelea, waambie unachukua chapa za Kristo waambie wasiwe na mashaka na wewe!, kuna wale waliokukwamisha pia watatamani kujua uko wapi sasa na unaendeleaje, kuna wale waliokufukuza kazi, kuna wale waliokuwekea fitina wakadhani ya kuwa utakwama, waambie waendelee kutufuatilia katika mitandao ya kijamii wapitie kurasa zetu facebook na kwenye blogu zetu waambie ya kuwa neno la Mungu linaendelea, waambie tunaendelea kuihubiri injili vile vile na hatujawahi kukaa kimya, waambie tunaendelea kufanya wanafunzi waambie kazi za Mungu zinaendelea kamakawaida, waambie watu wanaokoka, waambie tunaendelea na wokobvu na wala hatuna mpango wa kurudi nyuma,  waambie kazi zinaendelea na hakuna wa kutuzuia, pepo wanatoka, habari njema inahubiriwa, wafungwa wanafunguliwa na vipofu wanapewa kuona, Nyaraka zinaandikwa na maisha yanaendelea  heri yake mtu yule asiye na mashaka nami!, Heri yake mtu yule asioyechukizwa nami!

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.