Ijumaa, 2 Mei 2025

Nafasi ya wafanya kazi wa ndani katika nyumba za wachungaji!


2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.” 



  

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba mojawapo ya nafasi ya Muhimu sana katika utumishi wa Mungu ni pamoja na kupata nafasi ya kuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji au mtumishi awaye yote wa Mungu, hii ni nafasi ya kipekee sio tu ya kupata neema ya kuwahudumia watumishi wa Mungu lakini pia ya kupitia kujifunza kwa namna ya kipekee na kushuhudia maisha ya utumishi wa watu wa Mungu na kujiletea baraka  na heshima kutoka kwa Mungu, hii ni kwa sababu neno la Mungu limesema yeye amuhudumiaye nabii kwa kuwa ni nabii atapata thawabu ya nabii.


Mathayo 10:40-42 “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”


Wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanahitaji maelekezo maalumu ili waweze kutambua wajibu wao na baraka ambazo Mungu amezikusudia kwao, wasipoelekezwa vema wanaweza kutumika kinyume na mapenzi ya Mungu na kusababisha changamoto kubwa za kihuduma kwa mtu wa Mungu na hata na kanisa lake kwa ujumla na huduma ya Mchungaji na mama Mchungaji, Ni lazima watumishi wa ndani katika nyumba za wachungaji watambue kuwa kazi yao ni huduma kamili na ni ibada kamili mbele za Mungu na kwa sababu hiyo wanapaswa kuifanya kwa moyo na ni nafasi ya kipekee sana na kwa sababu hiyo hawapaswi kuichukulia kama nafasi isiyo ya heshima, wao wanaweza kuyatumia mazingira ya kiroho yapatikanayo katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kama njia ya Baraka kubwa katika maisha yao.


Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza maswala ya msingi ambayo wafanyakazi wa ndani katika nyumba za watumishi wa Mungu wanaweza kuyaishi ili waweze kuwa Baraka katika mwili wa Kristo na kwa kanisa la Mungu bila kusababisha madhara katika nyumba za watumishi wa Mungu na huduma walizoaminiwa na Mungu katika maisha yao. Huduma ya kichungaji inapaswa kulindwa na kwa sababu hiyi mtenda kazi wa ndani ni moja ya walinzi wa huduma ya kichungaji, ni walinzi wa madhabahu iliyo hai yaani moyo na maisha ya Mchungaji.

1.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni watenda kazi pamoja na mtumishi wa Mungu.

 

Inapotokea kuwa kwa njia yoyote ile umepata nafasi ya kuishi katika nyumba ya Mchungaji au nabii, Mtume na kadhalika kwaajili ya kazi za ndani ni lazima utambue kuwa wewe ni mtumishi wa Mungu katika nafasi uliyo nayo, kwa sababu umepata neema ya kumtumikia Mungu pamoja na mtumishi wake na familia yake, na kwa sababu hiyo kazi yako sio kazi ya kawaida bali ni ibada mbele za Mungu na Mungu atakubariki endapo utaifanya kazi hiyo kwa uaminifu na uchaji wa Mungu, kwa hiyo fanya kazi hiyo kama sehemu ya utumishi wako kwa Mungu na kamwe acha kujifikiri kuwa u mtumwa au mjakazi.

 

Wakolosai 3:23-24 “Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.”    

 

Nimeishi na wasichana wa kazi wengi katika maisha yangu na wengi wa wale waliokaa na mimi vizuri Mungu aliwabariki na waliolewa na sasa wana nyumba zao na wanaishi maisha mazuri na yenye utulivu, nay a kuvutia sana, vijana  wengi waliamini kuwa mambinti hao wako salama  na wote waliooa kutoka katika nyumba za wachungaji hawakuwahi kujutia hii ni moja ya Baraka kubwa, wakati mwingine kutokana na kuishi katika utumishi wa Mtumishi wa Mungu, Mungu amewafanya wafanyakazi katika nyumba za watu wa Mungu kuja kuwa na huduma ya kitumishi vile vile na wengi wameinuliwa kutoka kuwa watumishi wa ndani na hata kuwa mama wachungaji, mama maaskofu na kadhalika  

 

Roho ya utumishi wa Mungu imewahi kuwakalia wale waliokuwa watumishi wa watumishi wa Mungu, hii ni kwa sababu watumishi wa waliokuwa watumishi wa Mungu wanajua mapito na mateso yote ambayo Bwana zao waliyapitia kwa hiyo haishangazi kuona Mungu akijitwalia viongozi kutoka wale waliokuwa wakifanya kazi kama za utumwa tu, kimsingi wakati mwingine huwezi kuwa mtumishi wa Mungu kabla ya kuwa mtumishi wa mwanadamu.

 

Kutoka 3:1-4 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.”  

 

Hesabu 11:28-29 “Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.”

 

Yoshua 1:1-3 “Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.”

 

Ni jambo la kushangaza kuwa Musa alikuwa akifanya kazi ya kulichunga kund la Yethro mkwewe ambaye alikuwa kuhani wa Midian, Lakini Mungu alimuita Musa akiwa katika hali ya kumtumikia mkwewe na kufanya kazi hiyo ambayo kimtazamo ilionekana ni kama kazi ya chini sana, Yoshua alikuwa mtumishi wa Musa na baadaye Musa alipokufa Yoshua ndiye aliyekuwa kiongozi mkubwa aliyewaingiza Israel katika inchi ya mkanaani  hii inaweza isiwe kanuni lakini inatufunza Mungu anajali utumishi wako dhidi ya watumishi wake.               

 

2.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wajifunze kuwaheshimu wachungaji na familia zao.

 

Kila anayefanya kazi katiia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni lazima awe na uelewa kuwa watumishi hao wa Mungu wanahitaji kuheshimiwa sana wao pamoja na familia zao, Mchungaji au nabii au mtume ni mtu aliyeitwa na Mungu na ni mtu anayestahili heshima yeye pamoja  na mkewe pia na watoto wao, kwa sababu hiyo kila anayefanya kazi ndani ya nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kujiheshimu, ni marufuku kuutumia udhaifu wa mke wa Mchungaji kama nafasi ya kutaka kumvunjia Heshima mama Mchungaji na au mchungaji, Moja ya mgogoro mkubwa uliompata Sara na Hajiri hata kufikia ngazi ya kuanza kutesana ni pamoja na Hajiri kuanza kumdharau Bibi yake.

 

Mwanzo 16:6-9 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake.”

 

Wafanyakazi wa ndani watapaswa kuishi na mke wa mchungaji vizuri na kujiepusha na migogoro isiyo na msingi, aidha wao ni waajiriwa wa mwanamke na kamwe halitakuwa jambo lenye kupendeza Mchungaji kujihusisha na malipo ya mshahara wa mfanyakazi, wafanyakazi wa ndani wanapaswa kuheshimu mamlaka ya kiroho ya kichungaji sawa tu na ilivyo Kanisani na nyumbani pia.

 

1Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.”

 

Aidha kila msichana wa kazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa kielelezo kwa kuishi maisha matakatifu na yaliyo kielelezo kwani watu wanaitazamia nyumba ya mchungaji kuwa kielelezo, wako mambinti wengi katika nyumba za watumishi wa Mungu ambao wametia aibu kwa kuishi maisha yasiyokuwa na kielelezo na kwa sababu hiyo kusababisha maswali yasiyoyokuwa na majibu, wengine walipata ujauzito na wakarudhishwa makwao huku washirika wakibaki na maswali kwamba waliwezaje kufanya matukio ya aina hiyo ili hali wanaishi katika nyumba za watu wa Mungu, huku ni kufanya uchafuzi wa kimazingira na kuleta shaka juu ya usimamizi wa huduma ya kichungaji kwani Mchungaji na mama Mchungaji wana wajibu wa kuisimamia nyumba ya Mchungaji ili iwe kielelezo kwa waamini.

 

1Timotheo 3:4-5 “mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

 

3.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe kielelezo katika Uadilifu, Nidhamu na kutunza siri za nyumbani

 

Ukiacha kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji kuishi maisha yaliyo kielelezo na ya uadilifu na nidhamu, pia kila msichana wa kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutunza siri za changamoto zinazojitokeza katika nyumba ya mtumishi wa Mungu, Nyumbani Mchungaji ni Baba, ni Mume  na ni kiongozi wa familia, lakini sio hivyo tu Nyumba ya mchungaji ina mapito mengi, wanaweza kulala na njaa, kufunga, kula vibaya yaani chakula kisicho na hadhi, kupungukiwa na kadhalika pia Mchungaji anao ndugu na jamaa ambao wanaweza kuwa hawajaokoka, hivyo watendakazi nyumbani kwa mchungaji hupita mapito hayo pamoja na familia ya Mchungaji na kwa sababu hiyo wakati mwingine usiri unahitajika kuhusiana na mapito hayo, Ni lazima mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya mchungaji awe mwaminifu kwa kila linaloendelea nyumbani, hupaswi kulianika nje? Usieneze siri ya matatizo au mapito ya ndani ya nyumba ya mchungaji, hakikisha kuwa washirika wengine hawatengenezi nafasi ya udadisi ya kutaka kujua yanayoendelea katika nyumba ya mchungaji wewe endelea kuwa mwaminifu na kufanya kazi kwa heshima, usafi na kwa moyo acha kueneza fitina hususani kati ya nyumba ya mchungaji na washirika wake, waache waguswe wenyewe kuihudumia nyumba ya Mchungaji na usiwaeleze watu kabisa hata kama mmeshinda na njaa. Aidha kama kuna jambo watu wanajaribu kulidadisi kuhusu Mchungaji au mama Mchungaji waelekeze watu kuwaona wasemaji wa familia ya Mchungaji na wewe baki kama mtu usiyejua kinachoendelea!

 

Mithali 11:13 “Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.”

 

Mithali 25:2 “Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.”

 

Aidha ishi na watoto wa Mtumishi wa Mungu sawa na makusudi ambayo kwayo watoto hao wamezaliwa, wewe kama yaya wa watoto wa Mchungaji usijihusishe katika kuwapandikizia watoto wa Mchungaji uharibifu, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kuwa Hajiri yeye alianza kumnyanyasa Isaka na akiwa na mwanae Ishmael walianza kutumiwa na shetani kumdhihaki Isaka na kumfanya mtoto yule wa ahadi asiyafurahie maisha nyumbani kwao jambo lililompelekea Sara kuamuru kutimuliwa kwa mjakazi na mwanae.

 

Mwanzo 21:8-12 “Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”

 

Aidha uzembe uliowahi kufanya na yaya wa Yonathan mwana wa Sauli kwa kijana wake Methiboehseth ulisababisha ulemavu usio wa lazima kwa mtoto wa Mtumishi wa Mungu Yonathan, kwa hiyo hata yaya katika nyumba za watumishi wa Mungu anapaswa kuwa mtu mwangalifu kwa familia ya Mchungaji, watoto wke mkewe na nduguze na kuchukua tahadhari za kutokuwasababishia matatizo au changamoto watumishi wa Mungu zikiwemo changamoto za kiafya!

 

2Samuel 4:4 “Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi.”       

 

4.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waishi kwa kutumia fursa za kiroho zinazopatikana katika nyumba ya mtumishi

 

Kuishi na watumishi wa Mungu kwa uzuri ubora na uaminifu kunaleta Baraka kubwa sana kutokana na utendaji wako uliotukuka wewe unaweza kufanikisha watumishi wa Mungu kuhudhuria ibada kwa wakati huku wakiwa wameshiba, kuwapikia chakula bora, kuitumia nafasi ya kufunga kwao na kuomba kukua kiroho, kuhudhuria ibada pamoja nao na kujifunza maisha ya utumishi, kwa ujumla ni Baraka kubwa sana kuwatumikia watumishi wa Mungu wale waliotumika kwa uaminifu walipata Baraka na wale walioshindwa kuwa waaminifu walipata madhara kwa sababu hiyo wewe itumie nafasi ya kuishi kwa mchungaji kwa nia njema, usikubali kuwaacha watumishi wa Mungu kwa sababu zozote zile hata wanapopitia changamoto wewe ni lazima uwe mtu wa kwanza kusimama nao

 

2Wafalme 2:9-15 “Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”

 

Elisha alikuwa ni mtumishi binafsi wa Eliya, alitumika kwa uaminifu mpaka dakika ya mwisho, jambo hili lilimletea Baraka kubwa sana wakati wa kuagana ulipofika kwa kweli Eliya alikuwa amekusudia kumbariki Elisha na Elisha aliomba sehemu maradufu ya roho ya Eliya imkalie juu yake na kwa kweli Mungu alifanya hivyo na wote waliokuwa wakimtambua Elisha kama mtumishi wa Eliya walimuinamia mpaka nchi wakijua kuwa Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha

 

Wakati Elisha akiwa anafaidika na utumishi wake mambo yalikuwa kinyume kwa Gehazi ambaye aliweka maslahi yake mbele na kutokufuata maelekezo ya Bwana wake na kwa sababu hiyo aliambulia kuwa na ukoma siku zote za maisha yake

 

2Wafalme 5:20-27 “Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama Bwana aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.”

 

Kutokuitumia fursa ya kiroho ya kuishi na watumishi wa Mungu kunaweza kutuletea laana na wazao wetu, lakini tukiwa na akili na kujua mapenzi ya Mungu neema ya Mungu itatuinua na watumishi hao wa Mungu watatuachia Baraka kubwa sana katika maisha yetu, kama ukiitambua siri ya kuishi na watumishi wa Mungu na ukajua Baraka zinazopatikana kwa kweli utasema kama Daudi kuwa siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku 1000, kuitumikia nyumba ya mtumishi wa Mungu ni kuitumikia madhabahu ya Bwana

 

Zaburi 84:10 “Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.”

 

5.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima waitumie nafasi ya kuishi kwa maombi na neno la Mungu

 

Kupata nafasi ya kuishi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu kusikufanye wewe kubweteka na kuishi maisha ya kiburi na majivuno, badala yake lazima uitumie nafasi hiyo kwa kuishi kwa maombi huku ukiwa mtu uliyejaa neno la Mungu, lazima mtu anayeishi katika nyumba ya mchungaji awe msikilizaji na mtendaji mzuri wa neno la Mungu, huku ukiwa kielelezo cha maisha ya kiroho, kushiriki ibada na mafundisho na hata kuandika notes, watu wanaokaa kwa mchungaji hawachukuliwi kuwa watu wa kawaida kwa hiyo ni lazima uwe kielelezo.

 

Kutoka 33:11 “Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.”

 

Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”

 

6.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima kuitumia nafasi ya kuishi kwa Mchungaji kama sehemu ya huduma na Upendo kwa wengine.

 

Kufanya kazi katika nyumba ya Mchungaji kunahitaji hekima, uvumilivu na upendo kwa wengine lakini zaidi sana kwa Mchungaji, wachungaji wakati  mwingine hukosa nafasi ya Mapumziko mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji anapaswa kuwa na hekima sio kila wakati utamwamsha mchungaji au kuwakaribisha wageni katika nyumba yake, utawahoji wageni kwa hekima na upendo iwapo wana ahadi ya kukutana na Mchungaji nyumbani kwake au ofisini, Afya ya Mchungaji ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote, muda wake binafsi na Mungu, muda wake wa kujiandaa kwaajili ya neno la Mungu, utulivu wake kula kwake na mapumziko yake kwa hiyo ni wajibu wa mfanyakazi katika nyumba ya Mchungaji ni kusimamamia ratiba za mtumishi wa Mungu badala ya kumwamsha kila anapokuja mtu yoyote na hata matapeli tu kwa hiyo tunaaswa kuwa na huduma na moyo wa upendo lakini tukiyanusuru na kuyalinda maisha ya mtumishi wa Mungu yasiiingiliwe kama mtu atakavyo

 

Wagalatia 5:13-14 “Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.”

 

7.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wafanyike Baraka katika nyumba ya Mchungaji.     

 

Katika mstari wa msingi wa somo hili nimenukuu habari za binti mmoja kijakazi katika nyumba ya Naamani ambaye alichukuliwa mateka huko Syria, lakini binti huyu aligeuka Baraka kubwa kwa sababu kupitia yeye na imani yake Bwana wake aliponywa ukoma wake, mfanyakazi huyu alichukuliwa mateka kutoka Israel lakini jambo la kushangaza hajawahi kuweka kinyongo chochote alikubali maisha ya ujakazi na utumwa huku akiwa mwaminifu kwa Bwana wake huku akimtakia afya njema na mafanikio zaidi, Naaman tunaelezwa kuwa alikuwa mzuri sana kwani jina Naaman maana yake ni mzuri lakini alipougua ukoma hali yake iliharibika na sasa kijakazi huyu anamtakia bibi yake na bwana wake furaha ya kweli kwa kujali afya ya Naamani

 

2Wafalme 5:1-5 “Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”

 

Kila mfanyakazi katika nyumba ya mtumishi wa Mungu anapaswa kuwa sababu ya Baraka na uponyaji wa nyumba ya mtumishi badala ya kutumika kama ajenti wa shetani na kusababisha maafa na anguko la mtumishi wa Mungu au huduma yake, aidha kuwa na moyo wa shukurani na subira kuacha tamaa, wivu na kutokuyatenda majukumu yako ipaswavyo, binti yule wa kiyahudi alikuwa mwaminifu na mwenye moyo wa kweli kwani licha ya kuwa alikuwa amechukuliwa mateka lakini alikuwa ni mtu aliyethamini utumishi wa Naamani na kutamani kama angeponywa ukoma wake, alikuwa na imani kubwa kwani haijawahi kusikika kokote kuwa mtu amewahi kuponywa ukoma wake lakini yeye alimuamini Elisha na kusaidiki kuwa bwana wake anaweza kupata msaada Endapo angekutana na mtu wa Mungu na ikawa hivyo kwani Naamani aliponywa na sio mwili wake tu na alimuamini Mungu wa Israel hata ushindi wake ulitokana na Mungu wa Israel

 

8.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wavae kwa kujisitiri

 

Kama mtumishi wa Mungu ndani ya nyumba ya mchungaji hakikisha kuwa unavaa kwa heshima na kujisitiri, haiwezekani unakaa katika nyumba ya Mtu wa Mungu kisha ukawa unavaa mavazi ya kikahaba na kutumika kama chombo cha ibilisi kwaajili ya kumaliza huduma ya kichungaji swala hilo halitaleta Baraka kwako na kwa mwili wa Kristo, acha kujifikiri mwenyewe na starehe zako na baadala yake fikiri kuhusu faida za mwili wa Kristo na ufalme wa Mungu.

               

1Timotheo 2:9-10 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”

 

Mithali 7:10-18 “Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.”

 

9.       Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji wasijaribu kuwa mrithi wa mama Mchungaji

 

Hakuna sheria inayokataza Mchungaji kumuoa binti wake wa kazi endapo itatokea Mungu ametaka iwe hivyo, hata hivyo litakuwa ni jambo lenye kuchukiza na kuleta utata mkubwa sana endapo itatokea unaolewa na Mchyhungaji baada ya mama Mchungaji, maandiko yanaonyesha kuwa ni chukizo kwa mjakazi kumrithi bibi yake, Muombe Mungu akupe mumeo na usijihusishe na maisha ya Mchungaji wale mke wake hata kama uliyasoma  madhaifu yake, watmishi wa Mungu tafadhali Mungu akupe hekima usilitupia jicho lako kwa binti wa kazi yeye na awe kama moja ya mabinti zako tu nyumbani, Mwandishi wa kitabu cha Mithali alionyesha kuwa kuoa housegirl ni jambo lisilovumilika na linaweza kutetemesha nchi

 

Mithali 30:21-23 “Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia. Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula; Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.”

 

10.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji Wanaweza kumjua Mchungaji vema zaidi kuliko watu wengine wote

 

Watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanauwezo wa kumjua Mchungaji na mahitaji yake vema zaidi kuliko watu wengine, Nyakati za kanisa la kwanza wakati Mchungaji Yakobo na Petro walipokuwa wamekamatwa, na Yakobo akauawa na Herode ni ukweli uliokuwa wazi kuwa kanisa lilimuomba Mungu kwa bidii sana lakini hata hivyo hawakuwa na Imani kuwa Mungu angefanya muujiza, Hata hivyo Mungu alimtuma malaika akamfungua Petro Gerezani na hata alipokuwa akigonga mlango mtu aliyetambua kuwa Petro anagonga mlango alikuwa ni Roda mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya Mariamu mama yake Yohana, binti huyu kwa furaha aliacha kufungua mlango na kuwapasha wote kuwa Petro anagonga mlango, hata hivyo kila mmoja katika kanisa walifikiria kuwa binti huyo ana wazimu ni kichaa, hayuko sawasawa,  lakini ni ukweli ulio wazi yeye ndiye aliyekuwa sahihi kuliko watu wote, moyo wake upendo na Imani yake kwa Mungu ilimfanya kuwa na mtazamo tofauti na watu wengine wote yeye alimjua Petro vizuri na hata sauti yake na alipogonga pia alikuwa anajua namna Petro anavyogonga mlango wa nyumba

 

Matendo 12:11-16 “Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.”

 

Hii inatukumbusha na kutufundisha kuwa watumishi wa ndani katika nyumba ya Mchungaji wanaweza kuwa na ufahamu mkubwa na wa kina kumuhusu mtumishi wa Mungu nahata kumjua Mungu na utendaji wake kuliko mtu mwingine yeyote na Mungu amewapa wao neema ya kutambua mwenendo na uhitaji wa Mchungaji wakati mwingine kuliko wengine katika kanisa, na tunakumbushwa hapa kuwa hatupaswi kuwafikiria kuwa ni wenye wazimu hata kidogo, na kuwapuuzia au kuipuuzia mitazamo yao ya kiroho

 

11.   Watumishi wa ndani katika nyumba ya mchungaji ni lazima wawe waaaminifu kwa mama Mchungaji

 

Ruthu ni mfano wa kuigwa kwa uaminifu wake aliokuwa nao kwa Mkwewe, alisimama na mkwewe katika mazingira yaliyokuwa magumu sana na kujionyesha kuwa mwaminifu hata kwa gharama yoyote, Yeye alikuwa ni Mmoabu na hakukuwa na kitu cha kupoteza endapo angemuacha Naomi lakini alisimama na mkwewe katika mazingira magumu sana ambo lililomletea sifa za kipekee na faraja kubwa sana hapo baadaye, simama na mama Mchungaji katikamhali zote iwe njema au mbaya usikubali kumuacha mama Mchungaji isipokuwa kama utaolewa na kuwa na majukumu yako mengine yanayokulazimu

 

Ruthu 1:16-18 “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”       

 

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”  
           

Hitimisho:

Wafanyakazi wa ndani hasa katika nyumba za watumishi wa Mungu wameitwa kuwa mabalozi wa Baraka za Mungu, kwa Imani yao, mwenendo na tabia zao, kamwe hatuwatarajii wao kuwa sababu ya kusambaratika kwa huduma za wachungaji au kusababisha kero na ugomvi katika nyumba ya Mchungaji, haipendezi wao kuwa sababu ya dharau, na uchonganishi kati ya huduma ya Mchungaji na washirika wake, somo hili linatoa mwanga tu wa namna na jinsi iwapaswavyo kuishi kwaajili ya Mungu na wala si kwaajili yao, aidha na kuwaonyea ili kwamba waache kutumika kama chombo cha shetani na badala yake waweze kutumika kuiinua huduma ya kichungaji na kuiweka kwenye heshima inayostahili, ni imani yangu kuwa kama unafanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu hutakata tamaa na kujidharau na kujifikiri kuwa huna maana nataka nikutie moyo ili ujue ya kuwa Mungu anakuzingatia sana anajua umuhimu wako katika kuitumikia familia ya mtumishi wake!


Wengi wa waliofanya kazi katika nyumba za watumishi wa Mungu kamwe Mungu hakuwahi kuwapuuzia kwani wengine alijifunua kwao na kuwabariki na wengine walimuona Mungu hata pale walipopita katiia changamoto ngumu Mungu aliwatokea


Wakati Sara alipomtendea vibaya Hajiri malaika wa Bwana hawakumuacha Hajiri na badala yake walimuelekeza njia sahihi ya kufanya na kuyalinda maisha yake na ya mtoto wake, Mungu hajawahi kuwadharau wajakazi na kuwaona kama watu wasio na maana na badala yake aliwahusisha katika Baraka zake alizozikudsudia sawa na nyumba za watumishi wake  


Mwanzo 16:6-11 “Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”


1Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 27 Aprili 2025

Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto!


Mathayo 2:19-21 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.”



Utangulizi:

Malaika wa Bwana alimwambia Yusufu maneno haya alipokuwa akali akiishi Misri, mahali alikokuwa ameelekezwa kwaajili ya kwenda kumficha mtoto Yesu baada ya kutafutwa kuuawa na Mfalme Herode mkuu, kwa hofu ya kutokutaka kuwepo kwa mfalme mpya wa Wayahudi, tabia ya Herode ilikuwa ni matokeo ya wivu wake na mpango wa kishetani wa kutaka kuharibu mpango na mapenzi ya Mungu kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu kwa kutaka kumuua Yesu. Somo hili ni maonyo kwa watu wote wasio na mapenzi mema kwa kazi na mpango wowote wa Mungu, Mungu yuko tayari kuulinda mpango wake na makusudi yake kwa gharama yoyote ile, na hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwa bora kuliko mpango na makusudi ya Mungu!

Mathayo 2:13 – 14 “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;”

Herode ambaye alitafuta kumuangamiza Yesu alikuwa amekwishakufa, Yesu alipaswa kukulia Nazareth katika inchi ya Israel inchi ya utumishi wake na aliyekuwa kipingamizi cha mpango huo alikuwa ameondolewa na Bwana mwenyewe hivyo Kristo angetekeleza mapenzi ya Mungu bila kizuizi, katika inchi ya Israel kwa sababu hiyo sasa malaika wa Bwana anatoa wito wa wao kurejea huku akiweka bayana sababu za kurejea ni kuwa wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto!

Mathayo 2:22-23 “Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.”

Tutajifunza somo hili “Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto” kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

 

·         Hatari ya kuzuia mpango wa Mungu.

·         Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya Mtoto.

 

Hatari ya kuzuia mpango wa Mungu

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo baya na la hatari sana duniani kama kujaribu kuzuia mapenzi ya Mungu au Mpango wa Mungu, mtu awaye yote wa mamlaka ya aina yoyote ile ambaye atasimama kuzuia kusudi la Mungu au kujaribu kusimamisha mpango wa Mungu juu ya kile alichokikusudia Mungu anajiweka katika hatari isiyoweza kusimulika, kuzuia makusudi ya Mungu wakati wowote na kwa sababu zozote zile ni kuingia katika mfumo wa Mungu. Mfalme Herode mkuu kwa ujumla hakufurahia taarifa za kuzaliwa kwa Masihi ambaye kimsingi ni mfalme wa wayahudi, na badala yake alianza mipango mikakati ya kutaka kumuua Yesu na kuharibu mpango wa Mungu wa ukombozi kwa mwanadamu, Kiburi cha kibinadamu na ulevi wa madaraka ulimfanya mfalme huyu mjinga kujifikiri ya kuwa yeye ni Muhimu kuliko mpango wa Mungu, na kwa akili zake ndogo alifanikiwa kusababisha misiba kwa wamama wa Bethelehemu waliokuwa na watoto wadogo chini ya miaka miwili.

Mathayo 2:3-8 “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.”

Mathayo 2:16-18 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.”

Mipango ya Herode na mikakati yake na kughadhibika kwake kunaonyesha Dhahiri nia ya moyo wake ilikuwa ni kuuufutilia mbali kabisa mpango wa Mungu, ni ujinga ulio wazi kuwa Herode aliweza hata kuita wakuu wa makuhani na kuuliza kuwa masihi anazaliwa wapi na akaelezwa kwa mujibu wa maandiko, lakini alikuwa amefanya upumbavu mkubwa sana kwani nadhani alipaswa pia kuwauliza makuhani hao hao kuwa kuna madhara gani anaweza kuyapata mtu anayejaribu kuzuia mapenzi ya Mungu?  Na neno la Mungu lingemjibu hivi:-

Isaya 14:26-27 “Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?

Ayubu 9:4 “Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?

Wakati wote, mahali popote na saa yoyote kila mtu wa Mungu ni lazima ahahakikishe kuwa linapokuja swala ambalo ni mapenzi ya Mungu, sisi kamwe tusiwe sababu ya kuharibu au kuzuia mpango huo kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kujikuta tunapingana na mapenzi ya Mungu jambo ambalo ni hatari na linaweza kuleta madhara makubwa sana, tuache kiburi na kujifikiri ya kuwa sisi ni maalumu sana, umaalumu wetu unaweza kuwa na maana kama tuko kwaajili ya kutimiza mpango wake, lakini umaalumu wetu unaweza kupotea ikiwa tu tunasimama kama kizuizi cha ule mpango halisi wa Mungu neno linaonyeshqa huwezi kuwa mgumu kwa mapenzi ya Mungu kisha ukatoboa! 

Matendo 5:38-39 “Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”

Maandiko yanaonya vikali swala zima la kujaribu kushindana na mapenzi ya Mungu, onyo linatolewa kuwa kama kazi imetokana na binadamu inaweza kuvunjwa lakkini ikiwa imetokana na Mungu huwezi kuvunja  na kinyume chake mtu utakuwa unajiingiza kwenye mfumo wa Mungu, nakumbushia kuwa Mungu habadiliki, Mungu yule yule wa agano la kale ndiye huyu huyu wa Agano jipya, Rehema zake zinadumu hata kizazi na kizazi kwa wamchao, lakini jicho lake li juu ya watenda mabaya aliondoe kabisa kumbukumbu lao duniani.

Zaburi 34:15-16 “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.”

 

Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya Mtoto

Herode alikuwa moja ya wafalme ambaye alishindana na kusudi la Mungu kuhusu Maisha ya Yesu, alikuwa anataka kumwangamiza, alisahahu kujifunza kutoka kwa Farao ambaye mara kadhaa alikuwa akikataa mpango wa Mungu wa kuwaachilia wana wa Israel waende katika nchi iliyokusudiwa na Mungu na matokeo yake Taifa la Misri lilipatwa na mapigo mazito yaliyosababisha hasara kubwa kwa Farao na raia wake na mwishoe msiba wa wazaliwa wote wa kwanza  wa binadamu na wanyama uliwapata Misri nzima na kama haitoshi Farao na majeshi yake wote walifutwa na Mungu katika bahari ya shamu, na hakukuweko mtu aliyesalia hata kupeleka habari ya kile kilichowakuta!

Yeye ni mwenye akili moyoni, na mwenye nguvu nyingi, ni nani aliyemwasi naye akasalimika? Herode aliyaasi mapenzi ya Mungu na hivyo uwezo wake wa kuwa salama uliondolewa, kumbukumbu lake duniani lilifutwa, huwezi kuufunga mpango wa Mungu kwa vizuizi vya kibinadamu, Herode aliyatafuta sana maisha ya Yesu Kristo Mwana wa Mungu ili kuyaangamiza na kwa dhamiri mbaya kabisa aliangamiza watoto wengi kule Bethelehemu ili yamkini ikiwezekana miongoni mwao awe ni Bwana wetu Yesu Kristo, Nini kilimtokea Herode maandiko yanaeleza tu kuwa alikufa ona:-

Mathayo 2:19-21 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.”

Hata hivyo Maandiko hayajaelezea kwa kina yaliyomkuta Herode, lakini kwa taarifa za Mwandishi maarufu wa kihistoria  wa karne ya kwanza Myahudi Flavius Josephus  anaelezea kuwa mara baada ya kuagiza askari kuwaua watoto wadogo wasio na hatia kwa kusudi la kummaliza na Yesu, kule Bethelehemu Mfalme huyo aliandamwa  na maumivu makali sana yasiyokoma, kujinyonga kwa utumbo mwembamba na kupata maumivu makali sana, kubanwa na pumzi mfano wa mtu mwenye pumu, maumivu makali katika kila sehemu ya mwili wake, mashambulizi makali ya figo, kumomonyoka kwa seli za mwili wake (gangrene) na maambukizi mabaya katika via vyake vya uzazi, kwa maelezo ya Mwanahitoria huyu nguli wa kiyahudi anaeleza kuwa pia siku zake za mwisho akiwa na mashaka makubwa sana aliuwa baadhi ya watoto wake wa kiume kwa hofu kuwa wangeweza kumpindua, na  mwisho aliagiza kuwa wakamatwe viongozi muhimu wa kiyahudi na serikali yake na kuamuru kuwa wauawe siku atakayokufa akiwa na mashaka kuwa hakuna mtu atakayeomboleza msiba wake kwa vile alivyokuwa katili, kwa nini haya yalimkuta Herode? Kutokana na kupingana na mapenzi ya Mungu na Mungu alimfutilia mbali ili mpango wa ukombozi kupitia Yesu Kristo uweze kukaa katika njia yake na mapenzi ya Mungu yaweze kusimama!

Hitimisho:

-          Hakuna mwanadamu anaweza kuzuia mpango wa Mungu hata siku moja iwe ndani ya mtu au katika agenda za Mungu  nay ale ambayo watumishi wake manabii wamesema

-          Mungu ataendelea kuweka ulinzi dhidi ya wale anaowatumia kwa mapenzi yake, na kujaribu kuwaharibu au kuharibu kitu cha Mungu kilichomo ndani yao ni kujiweka katika wakati mbaya wa kuharibiwa wewe na Mungu mwenyewe, Mungu huangalia maslahi yake mapana zaidi kuliko tamaa zako finyu, na kutaka kwako kujijengea umaarufu acha kabisa kushindana na makusudi ya Mungu na mpango wake.

-          Mungu akikugundua kuwa wewe ni kikwazo kwaajili ya kazi yake atakuondoa kwa wakati wake ili mpango wake uweze kutimia, Maneno haya wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto  yanadhihirisha wazi kuwa Mungu alisimamamia kifo cha Herode ili mpango wake na agenda yake ndani ya Yesu Kristo iweze kuendelea, Siku zote Mungu ataondoa kila kikwazo kinachosimama mbele ya watoto wake  ili makusudi yake yaweze kutimia, do not mess-up with the G.O.D of Israel, usimkosee Mungu wa Wayahudi hata siku moja 

 

-          Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”

 

-          Tunajifunza kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa neema wanyenyekevu

 

Yakobo 4:6 Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

Mtu yeyote anayezuia mapenzi ya Mungu na kazi ya Mungu na makusudi ya Mungu hatadumu Mungu ana mwisho wa kila Herode anayeitafuta roho ya mtoto aiangamize, ikiwa uko katika mpango wa Mungu usiogope, kwani wanaoyatafuta maisha yako ili kuyaharibu wanaharibu ya kwao na kwa ghafla kama ilivyokuwa kwa Herode kiburi chao kitafikia mwisho.               

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Ijumaa, 25 Aprili 2025

Uwezo wa kuwakubali wengine!


Filemoni 1:9-15 “lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele;”




Utangulizi:

Moja ya kitabu ambacho kinazungumzia vizuri huduma nzima ya wokovu pamoja na upatanishi ni pamoja na kitabu cha Filemoni, Katika kitabu hiki ambacho kinaunganisha watu wakuu watatu, Onesmo ambaye ni mkosaji, Filemoni aliyekosewa na Paulo mtume kama mpatanishi,Paulo mtume ambaye anasimama kama mpatanishi hapa anamtaka Filemoni amkubali Onesmo ambaye alimkosea hapo awali na sasa amejirekebisha baada ya kukutana na Yesu Kristo akiwa gerezani, somo kubwa tunalojifunza hapa ni kuwa je mtu aliyekukosea, au aliyekosea anapokuwa amejirudi, je unaendelea kumuhesabu kama mhalifu? Au utamkubali? wako baadhi ya wapendwa ambao kama mtu alikosea wakati Fulani basi wataendelea kumuhesabu kama mhalifu miaka yake yote na hawako tayari kuachana na stori za zamani kuhusu maisha ya mtu na badala yake wanatumiwa na Shetani kuendelea kugandamiza watu wa Mungu ambao maisha yao yamebadilika. Msimamo wa aina hiyo unapingana kabisa na uwezo na utendaji wa Mungu ambaye hubadilisha maisha ya watu siku hadi siku kwa kadiri watu hao wanavyokubali kujiachia katika neema ya Mungu iwezayo kubadilisha na maisha yetu sote. 

 

1Timotheo 1:12-16 “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.”


Maisha ya kiroho ni Mchakato, ambao unahitaji uvumilivu, ikiwa ni pamoja na kuwavumilia watu ili wabadilike na tena waokolewe na tena wakue kiroho na tena na kuwasamehe na kuamini katika nguvu ya Damu ya Yesu yenye uwezo wa kubadilisha watu, Paulo ni mdau na mfano wa mchakato wa mabadiliko hayo,  katika kitabu cha Filemoni leo yako mambo ya kujifunza kuhusiana na swala hilo hasa kwa mabadiliko aliyoyapata mtumwa wa Filemoni aliyeitwa Onesmo ambaye, Mungu alimuokoa na kuyabadili maisha yake kabisa, tutajifunza somo hili Uwezo wa kuwakubali wengine kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo:-

 


·         Wajibu wa Mkristo anapokosewa

·         Kuendeleza uwezo wa kusamehe

·         Kuendeleza uwezo wa kuwakubali wengine

·         Kuendeleza uwezo wa kupenda kama Yesu

 


Wajibu wa Mkristo anapokosewa

Filemoni 1:10-18 “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili.Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu.”

Onesmo alikuwa ni mtumwa wa Filemoni, Nyakati za Biblia karne ya kwanza kumiliki watumwa kwa watu waliokuwa na uchumi mkubwa lilikuwa ni swala la kawaida, na Onesmo alikuwa ni Mtumwa wa Filemoni, Mtumwa huyu hakuwa mwaminifu na pia alikuwa hajaokoka, hivyo alimtoroka Filemoni na kukimbia mbali huku akimwibia Filemoni na kumsababishia hasara ya fedha nyingi katika wakati ule mtumwa alikuwa ananunuliwa kwa dinari 500, dinari moja kwa kawaida ni sawa na Shilingi za Tanzania  8,575.29/- kwa hiyo Dinari mia 500 ni sawa na shilingi 4,287,645/- kwa hiyo licha ya fedha alizoiba Onesmo yeye mwenyewe alikuwa ni ghali kwa kiwango cha milioni nne na laki mbili na mia sita arobaini na tano za mwaka 1952, hukumu ya mtumwa aliyekimbia katika utawala wa Kirumi ilikuwa ni kifo, Lakini hata hivyo mtumwa huyu aliwekwa gerezani,  na kwa neema ya Mungu lilikuwa ni gereza lile lile alilokuwa amefungwa Paulo mtume, kwa hiyo Paulo alimuhubiri Kristo kwa mfungwa huyu na kumlea kiroho gerezani na akapokea badiliko kubwa sana, Sasa mfungwa huyu alikuwa amepata nafasi ya kutoka na kukubali kurejea kwa Filemoni, na ndipo Paulo anamwandikia Filemoni ili aweze kumsamehe! Je ungelikuwa ni wewe ungeweza kumsamehe? Kukoseana ni jambo la kawaida katika maisha haya, ni ukweli ulioko kama tu sisi nasi tunavyomkosea Mungu mara kadhaa, Lakini hata hivyo kwa upande wa Binadamu uwezo wetu na degree (Viwango) zetu na mitazamo yetu inatofautiana sana  je Neno la Mungu linatuelekeza nini mtu anapokukosea?

Mathayo 18:7 “Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha!

Luka 17:1-3 “Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.”

Biblia haiungi mkono watu kukoseana lakini inaonya pia wale wenye kukosesha hata hivyo kwa watu wa Mungu tunapaswa kusamehe, hatupaswi kuwa kama watu wa ulimwengu huu au wale wa jicho kwa jicho na jino kwa jino, sisi tunapaswa kuhakikisha kuwa Mungu anatukuzwa kwa namna yoyote ile pale watu wanapotukosea, kwa hiyo Onesmo alikuwa amebadilika, injili ilikuwa imembadilisha na Paulo namuomba Filemoni sasa ampokee Onesmo kwa sababu sasa amebadilika, tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa na Rehema na kuwakubali tena watu waliowahi kufanya makosa kana kwamba hawajawahi kukosea kwani hivyo ndivyo Mungu anavyotufanyia na sisi pale tulipokuwa tumewahi kumkosea

Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.”

Mathayo 5:38-41 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.”

Jifunze kuachilia, jifunze kuwa kama Mungu, jifunze kuwakubali kwa upya watu waliokosea na wakajirekebisha, wahesabie kuwa ni wenye kufaa sana kuliko mwanzo, Paulo anaonyesha kuwa Onesmo sasa anamfaa sio tu Filemoni hata na yeye na kama isingelikuwa ni mtumwa wake huenda yeye angemchukua ili amtumikie katika vifungo vyake.  

     

Kuendeleza uwezo wa kusamehe

Filemoni 1:10-12 “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa;”

Kusamehe ni moja ya tabia ya Kikristo, Paulo mtume hapa anaonyesha umuhimu mkubwa na uwezo wake wa kusamehe, na kuonyesha kuwa ana moyo sio wa kusamehe tu bali wa kukubali  na kuwahurumia wengine, anamuombea Msamaha Onesmo, lakini yeye anamkubali kama mwanae aliyemzaa huko gerezani na anasema huyu ni moyo wake hasa, kumbuka ni vigumu sana kwa wachungaji wa leo na wakristo wa leo kumkubali mtu aliyewahi kukosea kwa kiwango kama hiki, Je unaweza kumuita mkosaji aliyetubu na kubadilika na kusema huyu ni moyo wangu hasa? Wakati mwingine tunakosa huruma na kuwakandamiza wengine kupitia makosa waliyowahi kuyafanya, na kuyahubiri kwa kukandamiza ili yamkini wasikubalike tena, wengi wetu ni kama hatuamini katika mchakato wa Mungu kubadilisha mtu aliyekosea, ni muhimu kukumbuka kuwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa wokovu iko rahisi sana kumsafisha aliyeokolewa na akakosea, Mkristo aliyekomaa kiroho ana uwezo wa kuendeleza moyo wa kusamehe na kumuhesabu mwingine kuwa yuko sawa kama hajawahi kukosea, Onesmo hakuwa tatizo tena kwa Paulo mtume Lakini kazi ilikuwa kwa Filemoni, je ataweza kumkubali tena mtumwa yule aliyemuingizia hasara?  Paulo kwa waraka huu anauandaa moyo wa Filemoni kuendeleza uwezo wa kusamehe, tusiwe na uchungu tena, tuwe na huruma na tusamehe.

Waefeso 4:31-32 “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.”

Kama tumeamua kumfuata Kristo, basi ni lazima kuuiga moyo wake, yeye hakuwa mnafiki kama tulivyo leo, leo hii unaweza hata usikaribishwe katika makanisa Fulani kwa sababu tu wana historia yako ya nyuma kwamba uliwahi kukosea na pengine wala hawajawahi kuthibitisha kama yalikuwa makosa hasa, pengine hata ulichafuliwa tu, lakini watu wakakushikia bango kana kwamba wana funguo za mbinguni, dini leo zimejaa watu wanafiki wakubwa sana ambao wamejaa ufarisayo wakimuhubiri Kristo huku wakiwafungia watu mlango huo huo wa Yesu Kristo kwa mioyo yao mizito isiyotaka kuachilia, Paulo Mtume alikuwa tofauti na anamshihi Filemoni ambaye pia alimzaa kiroho na kanisa lilikuwa katika nyumba yake kwamba yeye asiwe mfano wa hao bali ampokee Onesmo, Paulo anasema hata kama unamdai Yeye yuko tayari kulipa, Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini jambo la kushangaza ni kuwa Yesu alipofufuka mtu wa kwanza kumtaja miongoni mwa wanafunzi wake ilikuwa ni Petro tena kwa agizo la malaika

Luka 22:54-62 “Wakamkamata, wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika. Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu. Akatoka nje akalia kwa majonzi.”

Marko 16:6-7 “Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.”

Kwa nini unadhani Yesu aliwaagizia malaika kuwaambia wale wanawake kuwa wakawaambie wanafunzi wake na Petro pia ingawa Petro alikuwa amemkana Yesu mara tatu? Hii inatufundisha kuwa Yesu alimwamini Petro, alimpenda na hakuyahesabu yaliyotokea nyuma kuwa ni kitu cha kushikilia na sasa anaenda mbali zaidi anampa majukumu ya kulisha kondoo zake, jambo kama hili linaweza kufanywa na watu au watumishi wenye moyo mkubwa kama wa Yesu au Paulo mtume watu waliozoezwa kusamehe wengine na kuwaamini kwa upya!

Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”

Maandiko yameamuru kusamehe pale mtu anapokosea na kutubu, na ni muhimu kwetu kuwaamini tena kama Mungu amewaamini tena wewe ni nani usiyewaamini, wakati mwingine tunaweza kukaza shingo zetu kuwakataa kwa sababu ya wivu na uchanga wa kiroho, wako watu kwa uchanga wao hufikiri kuwa wengine hawana mchango tena kwa mwili wa Kristo, wanadhani kama mioyo yao ilivyo ya kifarisayo  basi na Yesu yuko hivyo hivyo, hii ni roho ya kujihesabia haki.

Wakolosai 3:12-13 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.  Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.”


Kuendeleza uwezo wa kuwakubali wengine

Filemoni 1:15-17. “Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.”

Wakati Onesmo alipokuwa anatoroka alikuwa mwenye dhambi, mhalifu na mtumwa, Lakini alipokuwa anarejea sasa ni Mtakatifu na ndugu katika Bwana ni zaidi ya mtumwa anamfaa Filemoni na anamfaa Paulo Mtume, Paulo anamuomba Filemoni amkubali, Paulo anataka Filemoni aendeleze uwezo wa kuwakubali wengine, Je wewe unaweza kumkubali? Mtu aliyekosea na sasa amerudi kwako upya?  Kama wakristo tunapaswa kuwa na moyo wa kuwakubali wengine bila kujali yaliyotokea nyuma katika historia yao, Hakuna kiwango cha kusema unamkubali huyu na huyu unamshusha chini kidogo kwa sababu eti alikuwa hivi au vile kumbuka mfano wa mwana mpotevu

Wagalatia 3:28-29. “Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”

Luka 15:25-32 “Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”                

Ni Imani yangu kuwa utakuwa ka ma Paulo mtume na utakuwa kama Filemon wao bila shaka walimkubali Onesmo, lakini kama wewe hukubali huna tofauti na yule mwana mkubwa ambaye alikasirika wakati baba yake alipompokea mwana wake aliyekuwa amepotea, endeleza uwezo wa kuwakubali wengine. Paulo mtume alitaka Onesmo apokelewe na Philemoni kana kwamba Filemoni anampokea Paulo Mtume hii ni kiwango cha juu sana cha kukubaliwa kwa Onesmo!


Kuendeleza uwezo wa kupenda kama Yesu

Filemoni 1:4-7 “Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.”

Filemoni 1:21 “Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo.”

Paulo alikuwa anamfahamu Filemoni kama lilivyo jina lake maana ya jina PHILEMON  maana yake Mpendwa/Mpenzi Filemoni alikuwa mwanafunzi wa Paulo Mtume alikuwa vizuri kiuchumi kulikuwa na Kanisa nyumbani mwake alikuwa ni mtumishi wa Mungu alikuwa na upendo sana lakini pia alikuwa mtii kwa Paulo mtume, kwa hiyo Paulo hakuwa na shaka juu ya agizo lake kupokelewa na kukubalika kwa Onesmus, Filemoni alikuwa na uwezo huo, wako watumishi hawana uwezo wa kupokea mtu aliyekosea lakini wako watumishi wenye uwezo mkubwa wa kutokuhukumu na kuwapokea kwa mikono miwili wale waliokosea na kuwahesabu kuwa wanastahili, tendo la aina hii linaendeleza na kukuza uwezo wa kupenda kama Yesu Kristo, Yesu alitupenda pasipo sababu, tunapokuwa na upendo kwa wengine bila kujali walifanya nini na historia yao ya nyuma ikoje tunaendeleza kile ambacho Kristo alifanya kwetu, maisha ya aina hiyo ni zaidi ya injili.

1Yohana 2:9-11Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”

Ikiwa katika moyo wako kuna mtu unamchukia basi unajiumiza mwenywe, haujiweki katika nafasi ya kufurahia msamaha na upendo wa Mungu unabaki gizani, kwa hiyo jipime sana na jichunguze kama uko katika upendo wa kweli na kama hauna siku nzuri na saa nzuri ya kuanza ni sasa, anza kujenga mazoezi ya kupenda nje ya mipaka ya kawaida kama Yesu Kristo aliagiza kuwapenda maadui zetu, iweje tushindwe kuendeleza kuwapenda wale tu waliokosea zamani na sasa hawako kama zamani tena? Paulo alimkubali sana Onesmo, na alikuwa anamuamini Filemoni kwamba angeliweza kabisa kubeba agizo la waraka wake kwa kumkubali Onesmo na kumuhesabu kama ndugu

Filemoni 1:8-20 “Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia.    Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima