Waebrania 10:32-36 “Lakini zikumbukeni siku
za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya
maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na
wale waliotendewa hayo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo,
tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu
mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una
thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya
Mungu mpate ile ahadi.”
Utangulizi:
Ndugu zangu wapenzi!, Leo nataka
tuchukue muda kutafakari kwa pamoja kifungu hiki muhimu Katika kitabu cha Waebrania 10:32-36, kifungu hiki bila
shaka kinazungumza na moyo wa kila mmoja wetu,
na kina makusudi ya kumtia moyo na kumjenga kila Mkristo kwa ngazi
yoyote ile ya kiroho, kuendelea kuwa na ujasiri katika Kristo, bila kujali ni
aina gani ya mapito unapitia, na bila kujali kuwa mapito hayo yatadumu kwa muda
mrefu kiasi gani, tunapopita katika changamoto nzito, mateso, fadhaa, fedheha,
magumu, hatari na misukosuko ya aina yotote ile, kama tukisimama katika Kristo
hatari hizo haziwezi kufua dafu na zitatuletea thawabu kubwa sana, lakini
hatari kubwa zaidi kuliko hizo ni kuupoteza ujasiri wetu wakati mambo magumu
yanapoendelea hata kutufikisha katika ngazi ya kushindwa kuendelea kujivunia
wokovu tuliopewa na Bwana wetu Yesu Kristo au kujivunia Yesu mwenyewe.
Kitabu cha Waebrania ni kitabu
chenye kuzungumzia theolojia zoefu ya kutembea na Kristo (Experimental Theology) ambapo Mwandishi ametumia uwezo wake
mkubwa katika kuelezea ubora wa Yesu Kristo na kuonyesha hasara kubwa ya
kumpoteza Yesu, au kuupoteza wokovu, kwa hiyo Mwandishi anatumia uzoefu wake
kuwatia moyo wasomaji wake kuendelea kuwa na msimamo katika Kristo, bila kujali
ni aina gani ya mapito wanaipitia kwani kwa kufanya hivyo watajipatia thawabu
kubwa sana. Jambo hili linatuhusu sisi nasi tunaoishi katika siku za leo zilizo
ngumu zaidi na zenye mapito mengi, Tutajifunza somo hili Msiutupe ujasiri wenu
kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Zikumbukeni siku za Kwanza (Mst 10:32-33)
·
Nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi (Mst
34)
·
Basi msutupe ujasiri wenu (Mst 35-36)
Zikumbukeni siku za Kwanza (Mst 32-33)
Waebrania 10:32-33 “Lakini zikumbukeni siku
za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya
maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na
wale waliotendewa hayo.”
Mwandishi anawakumbusha Waebrania
waliomuamini Yesu Kristo kukumbuka siku za Kwanza yaani siku za mwanzoni walipokuwa
wamemuamini Bwana Yesu na kujua habari za wokovu, baada ya kuipokea injili,
watu hawa walikuwa na uwezo mkubwa sana wakustahimili mashindano magumu,
makubwa yaliyowaletea maumivu, wakati walipodhalilishwa yaani kutwezwa na kushutumiwa
na kuteswa, kwa kupitia dhiki kwaajili ya Imani, sio hivyo tu Waebrania pia
walisimama bega kwa bega na ndugu zao wote waliopitia mateso katika Imani wazi
wazi bila kuogopa, hata katika macho ya wengine, walikuwa na umoja, na
waliwahurumia wale ambao waliteseka kwa sababu ya Imani kama wao wakionyesha
moyo mkubwa wa kuwatia moyo japo lilikuwa jambo la hatari sana, lakini walilifanya
huku wakifurahia miyoni mwao sawasawa na
mafundisho ya Kristo na mitume.
Mathayo 5: 11-12 “Heri ninyi
watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili
yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa
maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”
Matendo 5:40-41 “Wakakubali maneno yake;
nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu;
kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa
sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo”
Walikuwa na ujasiri, mmoja
alipoteseka walikubali kuteseka naye, na kumkingia kifua na kuwa tayari hata
kuhatarisha maisha yao, waliishi sawasawa na injili ya Kristo na mitume na
hawakuogopa lolote, walisimama kidete
walikubali kuumia pamoja na ndugu zao katika Bwana kama viungo katika
mwili wa Kristo, Nyakati za agano jipya mtu alipokuwa amefungwa alipata mateso
makali kama mtu anayetafuta kuuawa, kwa hiyo watu walioko gerezani walihitaji
kutiwa moyo sana na kutembelewa na kujaliwa
na ndugu na jamaa na marafiki vinginevyo wangeweza kufa kwa kukata
tamaa, lakini sio hivyo tu ilikuwa ni
hatari sana kama Mkristo angemtembelea mkristo mwenzake gerezani, kwenda kumtia
moyo kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kama unakwenda kujishitaki mwenyewe kwa kosa
lile lile lililomtia ndani mwenzako, na mara kwa mara waamini walikamatwa kwa
tendo hilo tu la kuwatembelea wenzao magerezani, lakini pamoja na changamoto
hizo zote Waebrania hawakuacha kusimama na wenzao waliokuwa magerezani wakikumbuka
maneno ya Bwana kuhusu wafungwa pia
Mathayo 25:34-40 “Kisha Mfalme atawaambia
wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini
ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa,
mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;
nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa
kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini
tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona
u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u
mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin,
nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo,
mlinitendea mimi.”
Hawakupoteza ujasiri wao,
walikuwa na imani kali sana katika Kristo, adui zao walikuwa na nguvu na
walikuwa wengi, watu walipoteza ndugu zao, wengine walipoteza mali, ardhi zao,
nyumba zao, familia zao na urithi wao, kumpokea Kristo katika familia za
kiyahudi ilikuwa ni sawa na kujifuta kabisa katika kabila hilo mila na desturi,
Lakini walikubali kupoteza kila kitu kwaajili ya Imani katika Kristo kwa nini
walifanya hivyo waliamini Kuwa na Kristo ni kuwa na mali njema zaidi, kupoteza
kila kitu kwaajili ya Kristo kungeleta furaha kubwa zaidi katika maisha yajayo.
Nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi (Mst 34)
Waebrania 10:34 “Maana mliwaonea huruma
wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali
zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.”
Kama nilivyodokeza awali kuwa
ilikuwa ni hatari sana kuonyesha matendo ya huruma dhidi ya wale waliokuwa
kifungoni, Lakini Waebrania waliokuwa
wamempokea Yesu walionyesha matendo hayo ya huruma kwa wafungwa na wengine walioteseka,
kuonyesha huruma kwa mtu aliyefungwa au anayeteseka kwaajili ya imani ilikuwa
ni sawa tu na kuianika imani yako wazi wazi jambo ambalo lilipeleka nawe kuwa
hatarini, Lakini hawa jamaa walikuwa tayari kwa lolote, walipokea mateso hayo
kwa Imani na furaha kubwa, furaha yao haikuwa katika kupoteza walivyopoteza
lakini ilikuwa katika Imani ya kuwa wamepoteza kwaajili ya Kristo na kuwa
watapata thawabu iliyokubwa zaidi, walijua nafsini mwao kuwa iko mali mbinguni
iko mali katika ulimwengu wa roho zaidi ya ile waliyopoteza na kuwa hizi
walizopoteza ni za muda tu lakini kile watakachokipata ni cha milele,
walihesabu kuwa mateso ya sasa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa baadaye
kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya
wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”
2Wakorintho 4:17-18 “Maana dhiki yetu
nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa
mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana
vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.”
Waebrania walijawa na imani hii,
Mafundisho haya yalikuwa yamewakolea sana kwa hiyo waliwaza thawabu na malipo
ya umilele watakayopokea kwa Mungu kuliko maswala ya muda mfupi ya dunia hii,
haya ndio yalikuwa mawazo yao ya kwanza, hii ndio ilikuwa Imani yao ya kwanza,
huu ndio ulikuwa ujasiri wao wa kwanza na huu ndo msingi wa Imani yao uliokuwa
umejengwa na mitume nyakati za kanisa la Kwanza, kwa hiyo mwandishi
anawakumbusha siku zile za kwanza! Walivyokuwa na msimamo huu mara baada ya
kuokolewa kwao, kutiwa nuru.
Basi msiutupe ujasiri wenu (Msta 35-36)
Waebrania 10:35-36 “Basi msiutupe ujasiri
wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha
kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.”
Pamoja na mambo mazuri waliyokuwa
nayo na moyo mkubwa wa uvumilivu na subira, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania
anaonya, na kutoa tahadhari kwamba wasije wakautupa ujasiri huu, Ujasiri huu ni
upi? Mstari huu katika Biblia ya
kiingereza unasomeka hivi “ So do not throw away your CONFIDENCE; it
will be richly rewarded” Neno la kiingereza Confidence yaani ujasiri katika Kiyunani linasomeka “Parrhēsia”
ambalo kiingereza tunapata neno Bluntness, assurance, bold, freely na
confidence, sawa tu na neno, Kwa msimamo, kwa kujiamini, kwa ujasiri, kwa
uhuru, kwa uaminifu.
Mwandishi alikuwa anaona wazi
kuwa kama mateso haya yataendelea kwa muda mrefu na hali hii ya kuteseka
itaendelea uko uwezekano wa waamini wa Kiebrania wakaanza kulegea na kupoteza
uaminifu wao, wanaweza kuanza kupoteza ujasiri, kupoteza kujiamini, kupoteza
msimamo na kuanza kulegea kwa hiyo anatoa wito kwamba wasiutupe ujasiri
wao kwa sababu una thawabu kubwa sana, na kuwa waendelee kukaza, kuwa imara na
kuamini.
Hakuna jaribu gumu duniani kama
Kusubiri, kusubiri ndiko kunakowasumbua watu wengi, watu wengi sana wameiacha imani
na kukosea kwa sababu walichoka kusubiri najua unaweza kusema mchungaji wewe
hujui habari ya subira nisikilize najua sana na najua ugumu wa kusubiri na
kuvumilia, yako mambo katika maisha yangu nimevumilia sana na nikamuona Mungu
lakini yako mambo yalinishinda, yaliniumiza na yalinifanya ninung’unike, kwa
hiyo naelewa habari ya subira na uvumilivu najua kilivyo kitu kigumu, hapa
ndipo watu wengi sana wameutupa ujasiri wao, wamefarakana na imani, wamemuacha
Yesu, kwa sababu tu walishindwa kusubiri, Imani yetu pia inajengwa katika
kusubiri, Yusufu alisubiri miaka 13 mpaka ndoto zake kutimia, Mateso ya Ayubu yalidumu kwa miaka 13 mpaka kupona na
kurejeshewa kila alichokipoteza, Daudi aliusubiri ufalme kwa miaka karibu 14
huku akikataa kulazimisha awe mfalme kwa kumuua Sauli, Ibrahimu alimsubiria Isaka
kwa miaka 25 na alishindwa kusubiri akajitafutia Ishamaeli wake, nimeona watu
wengi sana wakishindwa kushika ujasiri wao mpaka mwisho japo mwanzoni walikuwa
na imani, lakini pale Mungu alipoonekana anachelewa walichoka, Mungu leo anakutaka
usichoke, anakutaka uwe na subira, anakutaka uendelee kuvumilia hatimaye
utauona mkono wake yeye atakutokea tu, Mungu ameahidi Baraka kubwa sana za
kimwili na kiroho kwa kila mwenye subira
na wakati tunaposubiri tuendelee kuyatenda mapenzi ya Mungu kwa
uvumilivu mpaka mwisho ili tusipoteze thawabu yetu iliyokusudiwa na zaidi sana tuweze
kuifikia ile ahadi ambayo kwayo Mungu ametuahidi, Mwandishi anaonyesha kuwa
tunaweza kuifikia ahadi tukiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu !
Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na
kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako,
ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako,
nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii
walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa
uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao
waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya
kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Maandiko yanatuonyesha ya kuwa
Mungu ni mwema tena ni mwingi wa rehema, na amejaa huruma hawezi kukuacha kama
ulivyo, kubali kuendelea kuwa somo ili uwe ushuhuda mzuri, ziko baraka zinakusubiri,
kaka zangu na dada zangu, tunakutana na majaribu mengi sana duniani majaribu ya
kutisha na kutikisa yanaweza hata kutuondolea ujasiri wetu, lakini tusikubali
kuibiwa thawabu zetu kumbuka uaminifu wa Mungu, kumbuka Kuwa Mungu ni mwema
katika ahadi zake, watu wengi leo hawako tayari kuteseka kwaajili ya Kristo,
wala hawataki kupoteza, wala kusubiri na kuvumilia Yesu Kristo Bwana wetu ni kielelezo cha
uvumilivu aliweza kuvumilia mapingamizi makuu sana kwaajili ya furaha
iliyowekwa mbele yake, kaka zangu na dada zangu wapenzi natoa wito kwa kanisa
na kila mtu anayesoma ujumbe huu tuvumilie, tuvumilie, tuvumilie, uvumilivu
unalipa, Mungu hawezi kutuagiza kitu ambacho yeye mwenyewe hajawahi kukifanya
tukishindwa kuvumilia na kuwa na subira maana yake tumeutupa ujasiri wetu, Yesu
ni ujasiri wetu mkuu, Imani katika yeye ni ujasiri wetu mkuu hatupaswi
kuupoteza tunapokutana na changamoto za aina mbalimbali, suluhu iko wazi kwamba
tunapaswa kukumbuka imani yetu mwanzoni, ujasiri tuliokuwa nao mwanzoni wakati
tulipomuamini Bwana Yesu, tuendelee kuvumilia na kuendelea kutenda mapenzi ya
Mungu, na kuwa na subira kamwe tusiutupe ujasiri wetu una thawabu kubwa sana,
ahadi za Mungu ni kweli, tuendelee kuamini katika ahadi zake, neno lake na kujua
ya kuwa yeye ni mwaminifu tu naye atatenda lile tunalolisubiri kwa muda.
Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye
kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa
mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume
wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili
mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije
mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”
Maombi!
Baba katika jina la Yesu; tunakushukuru kwa somo zuri la mfano kutoka
kwa Waebrania hawa, waliovumilia magumu kwa furaha wakiendelea kudumu katika
Imani bila kujali ni magumu gani waliyapitia, sisi nasi utupe uvumilivu, na subira
ili tuzione rehema zako na wema wako na baraka zilizofichika katika kipimo cha
uvumilivu, kwa ulimwengu huu wa sasa na ule ujao, wako wanaosubiri watoto, wako wanaosubiri
kuolewa, wako wanaovumilia mateso na changamoto mbalimbali, wako wanaosubiri
kazi, wako wanaoteseka kwa sababu wamekuamini, wako wanaosubiri kutoka kiuchumi
na kufanikiwa katika maeneo mbalimbali, wako pia wanaosubiri kuinuliwa
kihuduma; Baba Mtumwa wako ninawaombea kwa jina la Yesu Kristo, asante kwa
sababu utatupa kuvumilia kwa neema na kila aliyewahi kushindwa kuvumilia
msamehe na utupe neema ya uaminifu wako asante kwa sababu nimekuomba kwa ufupi
nawe utafanya kwa urefu kwa kadiri ya wingi wa rehema zako, asante kwa sababu
utafanya hivyo na kuzidi katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai
ameen!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote