Jumatatu, 10 Juni 2024

Kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu!


Mwanzo 50:24-26 “Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.”



Utangulizi:

Kaka zangu na dada zangu katika Kristo! Leo tunachukua Muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu kutimizwa kwa mojawapo ya agizo la Muhimu sana la Yusufu kwa wana wa Israel, wote tunakumbuka habari za Mtu huyu Muhimu aliyeitendea mema familia yake na mataifa mengi kwa kuyaokoa na njaa kupitia uwezo wake mkubwa wa kiutawala na mipango chini ya Farao iliyoleta wokovu kwa wengi, Pamoja na kuwa ndugu zake walimfanyia vibaya lakini wote tunaukumbuka Moyo wa Yusufu jinsi ulivyokuwa mwema kwani hakuthubutu kulipa mabaya, alihesabu yaliyomkuta kama mapenzi ya Mungu, jambo lililopelekea kuwa mtu wa kuheshimiwa sana katika familia yake, Lakini akiwa anakaribia kufa mtu huyu aliwakusanya Israel wote na akiwa amezungukwa na wana wa Israel pamoja na wanae na wajukuu zake aliwaeleza habari za Muhimu sana na akazisisitiza kwa kuwaapisha kwamba ni lazima Bwana atawatokea tena na Bila shaka atawapandisha kutoka katika inchi hii Misri, na kuwa atawapandisha katika inchi ile aliyowaapia baba zao yaani Ibrahimu, Isaka na Yakobo, na ya kuwa wakati huo utakapowadia wahakikishe wanaipandisha Mifupa yake huko na aliwaapisha kuwa jambo hili ni lazima walitimize.

 Mwanzo 50:24-26 “Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.”

Tunaweza kujiuliza swala la msingi sana kwanini mtu huyu aliyekuwa na mafanikio makubwa sana kule Misri, aliyestawi sana na kuwastawisha ndugu zake wote lakini bado hataki kusahau inchi ya Urithi wa baba zake?  Yusufu alikuwa na ujuzi mkubwa sana kuhusu Mungu wa baba zake ya kuwa hakuna neno ambalo Mungu wetu ataahidi likaanguka bure yaani likapita bila kutimizwa, Yusufu anamjua wazi Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo kuwa hakuna neno linalotoka katika kinywa chake ambalo liliwahi kuanguka bure, Mungu alikuwa ameahidi kwa kinywa chake Tangu zamani ya kuwa atawapa Israel Inchi ya Mkanaani, Nchi iliyojawa na maziwa na asali. Yusufu alikuwa na Imani kuwa neno hilo lazima litakuja kutimizwa, Hivyo hata kama yu katika hali ya kufa anajua kuwa Mungu atatimiza ahadi zake, Yusufu aliendelea kumuamini Mungu kwamba atawaokoa watu wake na kuwaondoa katika inchi ile ambayo wangetumikishwa kwa utumwa mzito ambao kimsingi pia waliujua kuwa utakuja na ya kuwa ni lazima atawaleta tena katika inchi ya ahadi. Nadhani Yusufu alikuwa anakumbuka kile ambacho Mungu alizungumza na baba zake Ibrahimu na Isaka na Yakobo.

Mwanzo 15:13-16 “BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”

Tutajifunza somo hili kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

1.      
  
Kwanini Mifupa ya Yusufu katika inchi ya Kanaani?

2.       Kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu


Kwanini Mifupa ya Yusufu katika inchi ya Kanaani?

Yusufu aliinuliwa sana katika inchi ya Misri, alikuwa maarufu mno? Aliwasaidia wengi na kuheshimika sana na alipata mafanikio makubwa, aliwapa ndugu zake inchi ya Gosheni mahali ambapo Mto Nile unamwaga maji yake katika bahari ya Mediteraniani, ni eneo lenye rutuba na ustawi mkubwa sana kwa wana wa Israel na kwa kweli walifanikiwa sana, walimiliki mali nyingi mpaka wenyeji wao waliona wivu, waliongezeka sana walistawi na walikuwa na Nguvu,  Gosheni lilikuwa eneo lenye kufaa kwa malisho pia, unaweza kujiuliza kwanini Yusufu anawaapisha Israel na kuwahakikishia kuwa watakuja kuondoka na hivyo waikumbuke mifupa yake na kuipeleka katika inchi ya ahadi?

1.       Yusufu alikuwa amejifunza ya kuwa Mungu wa baba zake ni Muaminifu, Hakuna neno hata moja amewahi kuliahidi lisitimizwe bila kujali kuwa itachukua muda gani, Yeye mwenyewe alikuwa amejifunza uaminifu wa Mungu kwani Ndoto zile alizooteshwa na Mungu Japokuwa zilimpitisha katika mapito Mengi lakini zilikuja kutimia, alikuwa amejifunza kivitendo kwamba ni Mungu asiyeweza kusema uongo na ya kuwa neno lake haliwezi kwenda bure, uaminifu wake na fadhili zake ni za milele nazo hudumu kizazi hata kizazi!

 

Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

 

Isaya 55:10 -11 “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

 

Kwa hiyo Yusufu alikuwa na uhakika wa Mungu wa baba zake ya kuwa hakuna kitu anaahidi kisha asikitimize, kwa hiyo tukio la kuagiza mifupa yake kuzikwa katika inchi ya kanaani ni wazi kuwa alikuwa na Imani ya kuwa wana wa Israel watatoka katika inchi ya utumwa na kuwa Mungu atawarejesha katika inchi ya ahadi.

 

Waebrania 11: 22 “Kwa imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake, alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa yake.”

 

2.       Yusufu anatumika kama alama ya kisayuni kwa wana wa Israel, Israel leo wametawanyika kila mahali duniani, na nafahamu na wote tu mashahidi kuwa wengi wamerudi nyumbani, wako pale Israel leo katika inchi ambayo dunia inachanganyikiwa kuhusu mustakabali wa inchi ile, Lakini Yusufu anawakumbusha Wayahudi wote duniani hata pamoja na mafanikio makubwa wanayoyapata kokote waliko duniani, wanaheshimika sana wanafanikisha inchi hizo huko waliko lakini ni lazima wakumbuke kuwa wao ni Wayahudi na kuwa Mungu anatoa wito kwao kurudi Nyumbani, kuchelewa kwao kurudi nyumbani kunachelewesha kutimia kwa unabii na mapenzi mengi ya Mungu, Mungu aliahidi kuwatawanya lakini vile vile Mungu aliahidi kuwa atawarudisha,

 

Kumbukumbu 30:4-6“Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa; atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako. Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.”  

 

Haijalishi vizazi vingapi vimepita, haijalishi wana siasa  wa dunia wanawaza nini Lakini Israel ni Inchi ya ahadi kwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo na Yusufu pia, kila anayeshindana na agizo hili anashindana na agizo la Mungu, Yusufu anaonyesha moyo wa kizalendo, anajitanabahisha kuwa Myahudi halisi nyumbani ni Israel, alijua kuwa Israel watakuwa watumwa, lakini Misri sio inchi salama kiroho wala sio kwao, ina miungu mingi inayoabudiwa, walipitia magumu mengi, watoto wao wa kiume waliuawa na Yusufu anaonyesha kwamba anatamani nyumbani na nyumbani halisi ni Israel sawasawa na Neno la Mungu kwa baba zao.

 

Mwanzo 15: 18-21 “Siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai,na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.”

 

Mwanzo 17:7-8 “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.”

 

Mwanzo 28:11-17 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”

 

Mwanzo 48:3-4 “Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele.”

 

Israel ni ya Mungu, Israel (Kanaani) ni Mungu alimpa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, kila anayetaka Israel isiwepo anashindana na agizo la Mungu, Wayahudi wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa Mbele kutii agizo la Mungu ambalo Ibrahimu, Isaka na Yakobo walilitii, na Yusufu hakutaka kuwa sababu ya wayahudi kubakia Misri hivyo kwa kiapo aliwaapisha kwamba akifa haijalishi watakaa muda gani Misri, lakini Lazima Mungu ataitimiza ahadi yake naye hataki kubaki ugenini, huu ni moyo wa uzalendo mkubwa na nitoe wito kwa kila myahudi kokote aliko duniani wakumbuke Kanaani, kwa sababu Mungu ameagiza hivyo.

 

3.       Yusufu alikuwa ni Mwalimu mzuri sana, alitumia kifo chake na mifupa yake kuwa alama muhimu kwa kizazi na kizazi, kumbuka Tangu walipofika Misri Israel waliishi miaka karibu 430 na Yusufu aliishi miaka 110 tu lakini Fundisho lake na kazi yote ambayo Mungu aliifanya Yusufu alihakikisha kuwa kumbukumbu yake haitafutika alihakikisha kuwa kupitia mifupa yake kila kizazi kitakumbuka umuhimu wake, na uaminifu wa Mungu na unabii wake, Yeye aliagiza siku watakapoondoka Misri aliwaapisha wakumbuke mifupa yake hivyo kizazi na kizazi katika jamii ya wayahudi kila mmoja kabla hajafa alimkubusha mtoto wake kila nyumba kulikuwa na mafundisho ya kuwa Mungu atatutoa utumwani na atakapotimiza hilo kumbukeni mifupa ya Yusufu, kila familia ilionywa jamani jamani msisahau mifupa ya Yusufu, na ndio maana Musa alipotoka Misri  japo alikuwa wa kabila la Lawi hakusahau kamwe mifupa ya Yusufu, na Wana wa Israel hata alipokufa Musa huko jangwani bado wana wa Israel chini ya Yoshua walipewa inchi na walihakikisha wanaizika mifupa ya Yusufu huko Shekemu  nchini Israel yaani inchi ya mkanaani nchi ya ahadi.

 

Kutoka 13:19 “Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.”

 

Yoshua 24:31-32 “Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana, aliyowatendea Israeli. Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu.”

 

Vizazi vingi vilikuwa vimepita Lakini Israel walikumbuka umuhimu wa Yusufu na agizo lake, walilishika walilitii na walilitimiza kama walivyoapishwa na Yusufu!

 

Kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu!

 

Kupandishwa kwa mifupa ya Yusufu katika inchi ya kanaani kunatufundisha maswala kadhaa ya Muhimu sisi kama wakristo, huu ni mfano Muhimu sana wenye vitu vya kutufunza.

 

1.       Lazima tuendelee kumuamini Mungu na ahadi zake – iwe mvua iwe jua, iwe tumefanikiwa iwe hatujafanikiwa bado Mungu ni mwaminifu, Yusufu alikuwa amebarikiwa sana na alikuwa na mafanikio makubwa sana, lakini hii haikumfanya asahau uaminifu wa Mungu. Wala haikumfanya asahau kwao!  Alikuwa amejifunza kuwa Mungu ni mwaminifu na kila alisemalo litatimia aliamini kuwa Mungu atafanya alilolisema, Ni wangapi tunaamini katika kile ambacho Bwana amekisema? Yesu Kristo ni mwaminifu kila neno lake aliloliahidi litatimia kila kitu kitapita lakini maneno yake Bwana wetu Yesu hayatapita kamwe. Ni lazima kila mtu wa Mungu awe na Imani katika Neno la Mungu. Yesu Kristo anaitwa shahidi aliye mwaminifu, ni lazima tuziamini ahadi zake na kujua ya kila alilolisema atalitimiza.

 

Ufunuo 1:4-6 “Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi; tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”     

 

2.       Yusufu alifikiri yajayo – Yusufu hakujifikiri yeye mwenyewe tu, alitaka kizazi na kizazi kimuelewe Mungu, hakuwa anafanya mambo kwaajili yake, tendo lake la kuamuru kwa nguvu na lazima yaani kwa kuwaapisha lilikuwa linaonyesha anawaza maisha zaidi ya maisha haya, kila Mkristo anapaswa kuhakikisha ya kuwa injili inarithishwa kwa kizazi kijacho kwa watu waaminifu ambao watafaa kuwafundisha na wengine, Israel walikuwa waaminifu kurudia tena na tena kiapo cha Yusufu kwao kwa kizazi kilichofuata waliogopa kupata madhara endapo hawatawashirikisha watu wengine, Injili yetu inapaswa kukabidhiwa watu wengine ili kizazi na kizazi kiweze kulijua neno la Mungu vile vile kama tulivyoagizwa tangu enzi za mitume

 

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

 

3.       Umuhimu wa inchi ya kanaani – Wakristo wanapaswa kuwa Mstari wa mbele kuelewa mapenzi ya Mungu kuhusu Israel ile nchi ni lango la Mbinguni, Baraka zote zilizokusudiwa duniani kwa wanadamu wote zinapitia Israel, kwa hiyo kila mmoja anapaswa kuwatendea mema wayahudi na kuwasaidia kurudi kwao na kuisimamia inchi yao, Wamarekani na Waingereza na Wafaransa na Wajerumani wanaijua siri hii, ni afadhali kukaa kimya linapokuja swala la Israel kuliko kuropoka ropoka Israel ni ya Mungu na amewapa wana wa Ibrahimu Milele, Waarabu wanapaswa kulijua hilo, Waafrika wanapaswa kulijua hilo, Wazungu wanapaswa kulijua hilo na zaidi sana Wakristo na kuwa watetezi wakubwa kwa wayahudi, Yusufu aliipa kipaumbele inchi ya Kanaani kwa sababu ni inchi waliyoahidiwa na Mungu, makao makuu ya Bwana wetu Yesu Kristo na serikali ya ufalme wake duniani itatawala kutokea Israel na Yerusalem yakiwa makao makuu yake, linaweza kuwa jambo la kusikitisha na la kushangaza mtu yeyote yule akisimama kinyume na Mapenzi ya Mungu kuhusu Israel, waarabu wanapaswa kukumbuka hilo ya kuwa endapo wanamuheshimu Mungu basi pia wakumbuke kuiacha Israel kwa wana wa Israel na waarabu kubakia katika mataifa mengine, vinginevyo Ibrahimu na Isaka na Yakobo na Yusufu watashangaa sana wakati wa Hukumu kukuta watu wengine wakiidai inchi ya kanaani kuwa yao kinyume na mapenzi ya Mungu mwenye nguvu sana !

 

Mathayo 5:34-35 “lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.”

 

4.       Kuwaza kuhusu uzima wa milele – Swala la mifupa ya Yusufu liatukumbusha kuwa maisha yanaendelea hata baada ya kifo, kila mtu anapaswa kufikiri zaidi ya mazingira ya kawaida kwa sababu hata baada ya uzima huu uko uzima wa milele. Mungu ameahidi uzima wa milele kwa kila anayemuamini Yesu Kristo aliyetolewa pale msalabani kwa niaba ya watu wote watakaoamini ahadi hii ni ya kweli, kwa hiyo katika kuishi kwetu duniani pamoja na mafanikio yetu yote na umaarufu wetu wote tusisahau kujiwekeza katika uzima wa milele, Yusufu hakusahau inchi ya ahadi, Hatupaswi kusahau uzima wa umilele, hatuna budi kuwekeza katika uzima wa milele na kuamini ya kuwa Mungu atatufufua kutika kwa wafu na kutupa neema ya kuketi katika mkono wake wa kuume katika ufalme wake 

 

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”         

 

5.       Imani ni zaidi ya kawaida ya Muda – Ni swala la Muda tu, Yusufu hakujali kuwa Israel wataondoka lini Misri lakini alikuwa na Imani kuwa iko siku Mungu atawatokea, Nasema Mungu atakutokea bila kujali muda, kila mkristo anapaswa kukumbuka kumsubiri Mungu na kuishi kwa Imani, Mwamini Mungu biola kujali Muda, mwamini Mungu kuwa atafanya kitu, mwamini Mungu kuwa atakujibu, mwamini mungu kuwa atatkutokea, mwamini Mungu kuwa atafanya, Yusufu aliishi kwa Imani, aliamini katika maneno ya Mungu wa baba yake na babu zake alihesabiwa haki kwa Imani hii

 

Waebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.”         

 

6.       Agizo kuu – Agizo la Yusufu ambalo ilishikwa na kizazi na kizazi cha wana wa Israel ni fundisho kwa kanisa ya kuwa sisi nasi tunapaswa kulikumbuka agizo la Bwana wetu Yesu Kristo na kuihubiri injili duniani na kwa kila kiumbe, kama wana wa Israel vizazi na vizazi walilishika agizo la Yusufu, wakristo hawana budi kuhakikisha wanalishika agizo la Bwana Yesu, kuhakikisha kuwa kwa nguvu zetu zote tunarithisha injili au habari njema za wokovu  ulioletwa kwetu na Bwana wetu Yesu Kristo kwa kufa kwake Msalabani, Neno la Mungu ni lazima lienee na kurithishwa kwa watu wote Duniani na kwa vizazi vyetu vyote kwa kufanya hizi sisi nasi tutakuwa tumeipandisha mifupa ya Yusufu katika inchi ya kanaani, Musa hakuisahau mifupa, na hata Yoshua na wazee baada ya Yoshua walihakikisha Mifupa ya Yusufu inafika Shekemu inchi ya urithi wa wana Israel Efraimu na nusu ya Manase na Israel wote.  

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”               

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!      

Hakuna maoni: