Jumatatu, 17 Juni 2024

Basi msiutupe ujasiri wenu !

 

Waebrania 10:32-36 “Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.”




Utangulizi:

Ndugu zangu wapenzi!, Leo nataka tuchukue muda kutafakari kwa pamoja kifungu hiki muhimu Katika kitabu cha Waebrania 10:32-36, kifungu hiki bila shaka kinazungumza na moyo wa kila mmoja wetu,  na kina makusudi ya kumtia moyo na kumjenga kila Mkristo kwa ngazi yoyote ile ya kiroho, kuendelea kuwa na ujasiri katika Kristo, bila kujali ni aina gani ya mapito unapitia, na bila kujali kuwa mapito hayo yatadumu kwa muda mrefu kiasi gani, tunapopita katika changamoto nzito, mateso, fadhaa, fedheha, magumu, hatari na misukosuko ya aina yotote ile, kama tukisimama katika Kristo hatari hizo haziwezi kufua dafu na zitatuletea thawabu kubwa sana, lakini hatari kubwa zaidi kuliko hizo ni kuupoteza ujasiri wetu wakati mambo magumu yanapoendelea hata kutufikisha katika ngazi ya kushindwa kuendelea kujivunia wokovu tuliopewa na Bwana wetu Yesu Kristo au kujivunia Yesu mwenyewe.

Kitabu cha Waebrania ni kitabu chenye kuzungumzia theolojia zoefu ya kutembea na Kristo (Experimental Theology) ambapo Mwandishi ametumia uwezo wake mkubwa katika kuelezea ubora wa Yesu Kristo na kuonyesha hasara kubwa ya kumpoteza Yesu, au kuupoteza wokovu, kwa hiyo Mwandishi anatumia uzoefu wake kuwatia moyo wasomaji wake kuendelea kuwa na msimamo katika Kristo, bila kujali ni aina gani ya mapito wanaipitia kwani kwa kufanya hivyo watajipatia thawabu kubwa sana. Jambo hili linatuhusu sisi nasi tunaoishi katika siku za leo zilizo ngumu zaidi na zenye mapito mengi, Tutajifunza somo hili Msiutupe ujasiri wenu kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

 

·         Zikumbukeni siku za Kwanza (Mst 10:32-33)

·         Nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi (Mst 34)

·         Basi msutupe ujasiri wenu (Mst 35-36)

 

Zikumbukeni siku za Kwanza (Mst 32-33)

Waebrania 10:32-33 “Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.”

Mwandishi anawakumbusha Waebrania waliomuamini Yesu Kristo kukumbuka siku za Kwanza yaani siku za mwanzoni walipokuwa wamemuamini Bwana Yesu na kujua habari za wokovu, baada ya kuipokea injili, watu hawa walikuwa na uwezo mkubwa sana wakustahimili mashindano magumu, makubwa yaliyowaletea maumivu, wakati walipodhalilishwa yaani kutwezwa na kushutumiwa na kuteswa, kwa kupitia dhiki kwaajili ya Imani, sio hivyo tu Waebrania pia walisimama bega kwa bega na ndugu zao wote waliopitia mateso katika Imani wazi wazi bila kuogopa, hata katika macho ya wengine, walikuwa na umoja, na waliwahurumia wale ambao waliteseka kwa sababu ya Imani kama wao wakionyesha moyo mkubwa wa kuwatia moyo japo lilikuwa jambo la hatari sana, lakini walilifanya  huku wakifurahia miyoni mwao sawasawa na mafundisho ya Kristo na mitume.

Mathayo 5: 11-12 “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”

Matendo 5:40-41 “Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo

Walikuwa na ujasiri, mmoja alipoteseka walikubali kuteseka naye, na kumkingia kifua na kuwa tayari hata kuhatarisha maisha yao, waliishi sawasawa na injili ya Kristo na mitume na hawakuogopa lolote, walisimama kidete  walikubali kuumia pamoja na ndugu zao katika Bwana kama viungo katika mwili wa Kristo, Nyakati za agano jipya mtu alipokuwa amefungwa alipata mateso makali kama mtu anayetafuta kuuawa, kwa hiyo watu walioko gerezani walihitaji kutiwa moyo sana na kutembelewa na kujaliwa  na ndugu na jamaa na marafiki vinginevyo wangeweza kufa kwa kukata tamaa,  lakini sio hivyo tu ilikuwa ni hatari sana kama Mkristo angemtembelea mkristo mwenzake gerezani, kwenda kumtia moyo kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kama unakwenda kujishitaki mwenyewe kwa kosa lile lile lililomtia ndani mwenzako, na mara kwa mara waamini walikamatwa kwa tendo hilo tu la kuwatembelea wenzao magerezani, lakini pamoja na changamoto hizo zote Waebrania hawakuacha kusimama na wenzao waliokuwa magerezani wakikumbuka maneno ya Bwana kuhusu wafungwa pia

Mathayo 25:34-40 “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”

Hawakupoteza ujasiri wao, walikuwa na imani kali sana katika Kristo, adui zao walikuwa na nguvu na walikuwa wengi, watu walipoteza ndugu zao, wengine walipoteza mali, ardhi zao, nyumba zao, familia zao na urithi wao, kumpokea Kristo katika familia za kiyahudi ilikuwa ni sawa na kujifuta kabisa katika kabila hilo mila na desturi, Lakini walikubali kupoteza kila kitu kwaajili ya Imani katika Kristo kwa nini walifanya hivyo waliamini Kuwa na Kristo ni kuwa na mali njema zaidi, kupoteza kila kitu kwaajili ya Kristo kungeleta furaha kubwa zaidi katika maisha yajayo.

Nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi (Mst 34)

Waebrania 10:34 “Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.”

Kama nilivyodokeza awali kuwa ilikuwa ni hatari sana kuonyesha matendo ya huruma dhidi ya wale waliokuwa kifungoni,  Lakini Waebrania waliokuwa wamempokea Yesu walionyesha matendo hayo ya huruma kwa wafungwa na wengine walioteseka, kuonyesha huruma kwa mtu aliyefungwa au anayeteseka kwaajili ya imani ilikuwa ni sawa tu na kuianika imani yako wazi wazi jambo ambalo lilipeleka nawe kuwa hatarini, Lakini hawa jamaa walikuwa tayari kwa lolote, walipokea mateso hayo kwa Imani na furaha kubwa, furaha yao haikuwa katika kupoteza walivyopoteza lakini ilikuwa katika Imani ya kuwa wamepoteza kwaajili ya Kristo na kuwa watapata thawabu iliyokubwa zaidi, walijua nafsini mwao kuwa iko mali mbinguni iko mali katika ulimwengu wa roho zaidi ya ile waliyopoteza na kuwa hizi walizopoteza ni za muda tu lakini kile watakachokipata ni cha milele, walihesabu kuwa mateso ya sasa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa baadaye kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Warumi 8:18 “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”

2Wakorintho 4:17-18 “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.”

Waebrania walijawa na imani hii, Mafundisho haya yalikuwa yamewakolea sana kwa hiyo waliwaza thawabu na malipo ya umilele watakayopokea kwa Mungu kuliko maswala ya muda mfupi ya dunia hii, haya ndio yalikuwa mawazo yao ya kwanza, hii ndio ilikuwa Imani yao ya kwanza, huu ndio ulikuwa ujasiri wao wa kwanza na huu ndo msingi wa Imani yao uliokuwa umejengwa na mitume nyakati za kanisa la Kwanza, kwa hiyo mwandishi anawakumbusha siku zile za kwanza! Walivyokuwa na msimamo huu mara baada ya kuokolewa kwao, kutiwa nuru.

Basi msiutupe ujasiri wenu (Msta 35-36)

Waebrania 10:35-36 “Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.”

Pamoja na mambo mazuri waliyokuwa nayo na moyo mkubwa wa uvumilivu na subira, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaonya, na kutoa tahadhari kwamba wasije wakautupa ujasiri huu, Ujasiri huu ni upi?  Mstari huu katika Biblia ya kiingereza unasomeka hivi  “ So do not throw away your CONFIDENCE; it will be richly rewarded” Neno la kiingereza Confidence yaani ujasiri katika Kiyunani linasomeka “Parrhēsia” ambalo kiingereza tunapata neno Bluntness, assurance, bold, freely na confidence, sawa tu na neno, Kwa msimamo, kwa kujiamini, kwa ujasiri, kwa uhuru, kwa uaminifu.

Mwandishi alikuwa anaona wazi kuwa kama mateso haya yataendelea kwa muda mrefu na hali hii ya kuteseka itaendelea uko uwezekano wa waamini wa Kiebrania wakaanza kulegea na kupoteza uaminifu wao, wanaweza kuanza kupoteza ujasiri, kupoteza kujiamini, kupoteza msimamo  na kuanza kulegea  kwa hiyo anatoa wito kwamba wasiutupe ujasiri wao kwa sababu una thawabu kubwa sana, na kuwa waendelee kukaza, kuwa imara na kuamini.

Hakuna jaribu gumu duniani kama Kusubiri, kusubiri ndiko kunakowasumbua watu wengi, watu wengi sana wameiacha imani na kukosea kwa sababu walichoka kusubiri najua unaweza kusema mchungaji wewe hujui habari ya subira nisikilize najua sana na najua ugumu wa kusubiri na kuvumilia, yako mambo katika maisha yangu nimevumilia sana na nikamuona Mungu lakini yako mambo yalinishinda, yaliniumiza na yalinifanya ninung’unike, kwa hiyo naelewa habari ya subira na uvumilivu najua kilivyo kitu kigumu, hapa ndipo watu wengi sana wameutupa ujasiri wao, wamefarakana na imani, wamemuacha Yesu, kwa sababu tu walishindwa kusubiri, Imani yetu pia inajengwa katika kusubiri, Yusufu alisubiri miaka 13 mpaka ndoto zake kutimia, Mateso ya  Ayubu yalidumu kwa miaka 13 mpaka kupona na kurejeshewa kila alichokipoteza, Daudi aliusubiri ufalme kwa miaka karibu 14 huku akikataa kulazimisha awe mfalme kwa kumuua Sauli, Ibrahimu alimsubiria Isaka kwa miaka 25 na alishindwa kusubiri akajitafutia Ishamaeli wake, nimeona watu wengi sana wakishindwa kushika ujasiri wao mpaka mwisho japo mwanzoni walikuwa na imani, lakini pale Mungu alipoonekana anachelewa walichoka, Mungu leo anakutaka usichoke, anakutaka uwe na subira, anakutaka uendelee kuvumilia hatimaye utauona mkono wake yeye atakutokea tu, Mungu ameahidi Baraka kubwa sana za kimwili na kiroho kwa kila mwenye subira  na wakati tunaposubiri tuendelee kuyatenda mapenzi ya Mungu kwa uvumilivu mpaka mwisho ili tusipoteze thawabu yetu iliyokusudiwa na zaidi sana tuweze kuifikia ile ahadi ambayo kwayo Mungu ametuahidi, Mwandishi anaonyesha kuwa tunaweza kuifikia ahadi tukiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu !

Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.  Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

Maandiko yanatuonyesha ya kuwa Mungu ni mwema tena ni mwingi wa rehema, na amejaa huruma hawezi kukuacha kama ulivyo, kubali kuendelea kuwa somo ili uwe ushuhuda mzuri, ziko baraka zinakusubiri, kaka zangu na dada zangu, tunakutana na majaribu mengi sana duniani majaribu ya kutisha na kutikisa yanaweza hata kutuondolea ujasiri wetu, lakini tusikubali kuibiwa thawabu zetu kumbuka uaminifu wa Mungu, kumbuka Kuwa Mungu ni mwema katika ahadi zake, watu wengi leo hawako tayari kuteseka kwaajili ya Kristo, wala hawataki kupoteza, wala kusubiri na kuvumilia  Yesu Kristo Bwana wetu ni kielelezo cha uvumilivu aliweza kuvumilia mapingamizi makuu sana kwaajili ya furaha iliyowekwa mbele yake, kaka zangu na dada zangu wapenzi natoa wito kwa kanisa na kila mtu anayesoma ujumbe huu tuvumilie, tuvumilie, tuvumilie, uvumilivu unalipa, Mungu hawezi kutuagiza kitu ambacho yeye mwenyewe hajawahi kukifanya tukishindwa kuvumilia na kuwa na subira maana yake tumeutupa ujasiri wetu, Yesu ni ujasiri wetu mkuu, Imani katika yeye ni ujasiri wetu mkuu hatupaswi kuupoteza tunapokutana na changamoto za aina mbalimbali, suluhu iko wazi kwamba tunapaswa kukumbuka imani yetu mwanzoni, ujasiri tuliokuwa nao mwanzoni wakati tulipomuamini Bwana Yesu, tuendelee kuvumilia na kuendelea kutenda mapenzi ya Mungu, na kuwa na subira kamwe tusiutupe ujasiri wetu una thawabu kubwa sana, ahadi za Mungu ni kweli, tuendelee kuamini katika ahadi zake, neno lake na kujua ya kuwa yeye ni mwaminifu tu naye atatenda lile tunalolisubiri kwa muda.

Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”

Maombi!

Baba katika jina la Yesu;  tunakushukuru kwa somo zuri la mfano kutoka kwa Waebrania hawa, waliovumilia magumu kwa furaha wakiendelea kudumu katika Imani bila kujali ni magumu gani waliyapitia, sisi nasi utupe uvumilivu, na subira ili tuzione rehema zako na wema wako na baraka zilizofichika katika kipimo cha uvumilivu, kwa ulimwengu huu wa sasa na ule ujao,  wako wanaosubiri watoto, wako wanaosubiri kuolewa, wako wanaovumilia mateso na changamoto mbalimbali, wako wanaosubiri kazi, wako wanaoteseka kwa sababu wamekuamini, wako wanaosubiri kutoka kiuchumi na kufanikiwa katika maeneo mbalimbali, wako pia wanaosubiri kuinuliwa kihuduma; Baba Mtumwa wako ninawaombea kwa jina la Yesu Kristo, asante kwa sababu utatupa kuvumilia kwa neema na kila aliyewahi kushindwa kuvumilia msamehe na utupe neema ya uaminifu wako asante kwa sababu nimekuomba kwa ufupi nawe utafanya kwa urefu kwa kadiri ya wingi wa rehema zako, asante kwa sababu utafanya hivyo na kuzidi katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai ameen!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!       

Hakuna maoni: