Jumatatu, 8 Julai 2024

Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo


Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”                



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya Silaha yenye nguvu kubwa sana kuliko zote duniani katika ulimwengu wa roho ni pamoja na damu ya Yesu. Bila damu ya Yesu hata Imani yetu isingeweza kuendelea kuwepo duniani, Damu ya Yesu Kristo inawakilisha kila kitu ambacho Yesu Kristo alikifanya pale msalabani, Kuhesabiwa haki, ukombozi, upatanisho, Msamaha, utakaso,Uhuru kutoka katika adhabu na hasira ya Mungu, na agano, Yote haya ni marupurupu yanayopatikana katika damu ya Yesu, kwa msingi huo basi, kuwa na ufahamu kuhusu utendaji wa Damu ya Yesu ni muhimu sana kwetu kama wakristo, kwaajili ya kuelewa haki zetu zipatikanazo kwa Damu ya Yesu ili tuweze kuwa na ushindi siku zote za maisha yetu. Tutajifunza somo hili Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.

·         Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano jipya.

·         Wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo.

Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.

Ni muhimu kufahamu, kwamba ili tuweze kuelewa vema Kazi ya Damu ya Yesu Kristo, uweza wake na nguvu zake ni muhimu kwetu kuchukua muda kidogo, kujifunza matumizi ya damu jinsi yalivyokuwa nyakati za agano la kale, ili tuweze kujua utendaji huo namna unavyokuwa sasa katika agano jipya, Nyakati za agano la kale Damu zilizotumika zilikuwa damu za wanyama na kazi ya damu ilikuwa ni moja ya ishara muhimu sana ya msingi sana katika ibada za agano la kale kwa sababu zifuatazo:-

1.       Ilikuwa sehemu muhimu ya dhabihu ya upatanisho – Damu ilikuwa ni kiini muhimu cha ibada za dhabihu ambayo iliagizwa katika torati ya Musa. Dhabihu/Kafara za wanyama zilikuwa zinatolewa na damu ya wanyama hao zilikuwa zinanyunyizwa katika madhabahu kama njia ya upatanisho kwaajili ya dhambi.

 

Mambo ya walawi 17:10-12 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.”

 

Damu ilikuwa ni nyenzo muhimu ya kufanya upatanisho, yaani kwa kuwa mwanadamu anapotenda dhambi mara moja dhambi huharibu uhusiano wao na Mungu na kudai kifo, kwanini kifo kwa sababu Mungu alikuwa amemuonya mwanadamu wa kwanza kuwa siku atakapofanya dhambi hakika atakufa, kwa hiyo Damu kama uhai inamwagika kwa niaba ya mwanadamu na kugeuka kuwa sadaka ya kumpatanisha mwanadamu na Mungu, Kwa hiyo Damu hufanya kazi ya upatanisho. nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; Nafsi za wanadamu hupatanishwa na Mungu kwa njia ya Damu, uadui wetu na Mungu unapoozwa au kufunikwa kwa sababu ya Damu.

 

Upatanisho ni nini? neno upatanisho katika Biblia ya kiingereza limetumika neno atonement karibu mara 71 katika lugha ya kiebrania neno atonement linasomeka kama neno Kphar  ambalo hutamkwa Kaw-far sawa na neno la Kiswahili KAFARA ambalo maana yake ni kuwaleta pamoja watu waliokuwa maadui au waliotengana kwa kuwapatanishan, kwa hiyo neno atonement  at- one- ment  is reparation, au reconciliation ambalo maana yake ni bringng together into harmony of those who heve been separated or enemies, kwa hiyo damu ina nguvu ya kuvunja uadui  uiotokana na dhambi zetu kati yetu sisi wanadamu na Mungu na kumpa Mungu nafuu, uhalali, kibali, cha kukubali kutuachilia, na kuwa rafiki yetu.

 

2.       Alama muhimu ya agano – Damu katika agano la kale vilevile ilitumika kama alama ya agano kati ya watu na Mungu, Damu iliponyunyizwa juu ya watu iliwafanya wanadamu, kupata kibali kwa Mungu na kuzuia hasira za Mungu zisiwake juu ya watu wake, Damu iliwafanya watu hao kuwa mali ya Mungu, na kuwa na urafiki wa kudumu na Mungu!

 

Kutoka 24:7-11 “Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.”

 

Agano ni nini? Neno agano katika biblia ya kiingereza linatumika neno Covenant ambalo limetumiwa katika biblia mara 264 katika lugha ya kiibrania neno Covenant linatumika neno Beriyth ambalo maana yake ni muungano wa ushirikiano wa kirafiki au kisiasa confederation au alliancethe permanent union  yaani muungano wa kudumu mfano nchi zipatazo 50 au zaidi za America zilikubaliana kuwa kitu kimoja na kupatikana United States of America, kwa hiyo Damu husababisha watu na Mungu kuwa na serikali moja, jeshi moja, na ushirikiano wa kudumu wa kirafiki na kisiasa na Mungu

 

3.       Alama ya utakaso na wakfu – Damu katika agano la kale ilitumika kama alama ya utakaso na kuweka wakfu kwa Bwana, Mfano makuhani wale waliochaguliwa kwa kazi ya utumishi walitakaswa na kuwekwa wakfu ili watumikie Mungu kwa damu ya wanyama angalia:-

 

Kutoka 29:20-21 “Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.”

 

Sio hivyo tu Damu ilitumika kama nyenzo katika ibada kama njia ya kusafisha na kutakasa kwa kutumia damu. Na pasipo kumwagika Damu hakuna ondoleo la Dhambi.

 

Waebrania 9:19-22 “Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”          

 

Kutakaswa au kuwekwa wakfu ni kitendo cha kutengwa na Mungu kwaajili ya Mungu na kufanywa mtakatifu jambo ambalo pia linafanywa na Damu ya Yesu

 

Waebrania 13:11-12 “Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.”

 

4.       Alama ya Pasaka – Ukombozi mzima wa wana wa Israel kutokuuawa kwa wazaliwa wao wa Kwanza na kuruhusiwa kutoka utumwani, na kumtiisha Farao kulikuwa ni matokeo ya kazi ya Damu ya ukombozi ambayo mwanakondoo wa Pasaka alichinjwa na damu yake ikanyunyizwa katika miimo ya milango, na kwa tendo hilo na utii wake wana wa Israel waliokolewa kutoka pigo la mwisho, walipata ulinzi na waliokolewa kutoka utumwani na kutembea kwa ujeuri kurudi katika inchi yao.

 

Kutoka 12:3-13 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani.  Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”

 

Neno Pasaka katika lugha kiingereza linatumika neno Passover sawa na neno la kiibrania Pesach na kiswahili Pasaka neno hilo katika tafasiri ya kiingereza linaweza kutamkwa “passed over” maana yake Skipping au Passing over yaani Mungu alikuwa napita katika inchi ya Misri kuhukumu kwa kuua wazaliwa wa kwanza wa kila mlango usiokuwa na alama ya Damu, lakini kila mlango uliokuwa na akama ya damu aliiruka au kupita juu yake bila kuhukumu, kwa sababu damu ilifanya tukio liitwalo Propitiation yaani kuacha kukasirikia au kuhukumu kwa hoyo damu husababisha tuache kukasirikiwa na Mungu.

 

5.       Alama ya uzima na mauti – Damu katika agano la kale ilitumiwa na Mungu kama alama ya uzima na mauti, Damu ilitumika kuyatakasa maisha ya mwanadamu, na ndio maana Mungu aliwakataza wana wa Israel na wanadamu wote mpaka leo kutokuitumia damu kama chakula kwa sababu inawakilisha uhai, Damu ilikuwa ikitolewa kama mbadala wa dhambi yaani uhai unatolewa ili mwingine apate uzima asiuawe.

 

Walawi 17:10-14 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga. Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”             

 

Kwa hiyo unaweza kuona kuwa nyakati za agano la kale Damu ilikuwa ni alama au ishara muhimu kwaajili ya upatanisho, agano, utakaso, maisha na uhai, na ilitumika kumpa mwanadamu haki zake zote kutoka kwa Mungu ambazo alizipoteza kwa sababu ya kuweko kwa dhambi, damu ilisimama mahali palipobomoka kuwapatanisha wanadamu kwa Mungu na lakini hata hivyo ilikuwa ni alama au ishara inayoonekana na ambayo ilisimama kama kivuli cha damu halisi na safi na kamilifu itakayokamilisha maswala hayo yote katika agano jipya.

Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano jipya

1.        Damu ya Yesu inatupa Ondoleo la dhambi - Damu aliyoimwaga Bwana Yesu kupitia mateso yake pale msalabani inafanya kazi ya kufuta, kuondoa, kumaliza kabisa, kulipa kabisa Deni la dhambi, Damu ya Yesu inazifutilia mbali dhambi zote ambazo tumewahi kuzifanya jana, leo na hata milele.

 

Mathayo 26:27-28 “Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”

 

Ufunuo 1:5-6 “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”

               

1Yohana 1:7 “bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”

 

Neno Ondoleo la dhambi linalotumika katika Mathayo 26:28  katika biblia ya kiingereza linasomeka kama neno for remission of sins yaani katika kiyunani ni Aphesis ambalo maana yake ni Msamaha wa dhambi, au kufutiwa deni kwa kiingereza the cancellation of debt, charge or penalty yaani kufutiwa deni, au kufutiwa kesi au kuondolewa adhabu, Kwa hiyo Mtu anapomwamini Bwana Yesu kwa kazi yake aliyoifanya pale msalabani dhambi zako zote zinasamehewa na anahesabika hana cha kulipa, hawezi kuadhibiwa tena hakuna tena hukumu ya adhabu juu yake  Warumi 8:1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”

 

Neno ondoleo la dhambi katika kiyunani linasomeka kama Aphesis – ambalo linaweza kutafasiriwa kwa maneno ya kiingereza kama Pardon, Deliverence, Forgiveness, Liberty and Remission, Lakini neno Remission linatumika kimahakama zaidi na neno Liberty linatumika kiutawala Neno lililotumika katika maandiko ni neno Remission ambalo limetumika zaidi ya mara tisa neno hili la kimahakama linahusiana na kumuachilia mfungwa mwenye hatia kwamba awe huru mbele ya sheria bila kubadili asili ya mashitaka yake Remission is to reduce without changing the nature of the sentence where by the prisoner is released with or without condition and in the eyes of the law he/she will be free man or woman, Na neno Liberty – is a state of civil or political freedom – ni Hali ya kuwa huru kiraia au kisiasa, ni kama vile Rais anapoamua kuwaachia watu huru wakati wa sikukuu za muungano au uhuru, kuna wafungwa ambao wanaachiliwa huru kwa matamko ya kisiasa, Kwa hiyo Damu ina mtindo huo wa kumtangaza au kumfanya mtu awe huru mbele za Mungu kwa mujibu wa sheria au kiutawala na kuhesabika kuwa raia wa kawaida bila kutumikia adhabu iliyokusudiwa au bila kulipa kodi.

 

Damu ya Yesu pia inaosha – neno kuosha katika kiyunani ni “Louō” ambalo maana yake ni kufua au kuogesha ni tendo la kumsafisha mwanadamu katika ukamilifu wake kwa jinsi ya mwili, nafsi na roho, kwa hiyo damu ya Yesu inawasafisha wale wanaomuamini, kuna maneno mawili yanayotumika kuhusu kuosha kuna neno kuosha “Louō” na “Katharizō” washed and Cleanses ambalo maana yake kutakasa au kufanya safi.(Purify)

 

2.       Damu ya Bwana Yesu pia inasababisha watu wahesabiwe haki - kuhesabiwa haki ni lugha ya kimahakama yenye maana ya kutokuonekana na hatia, ingawa sisi tulikuwa wenye hatia halisi lakini Mungu kwa amri ya kimahakama anakutangaza kuwa na haki kana kwamba hujawahi kukosea kwa sababu ya kumuamini Mwana wake kwa kazi aliyoifanya pale msalabani  Justification –  kwa kiyunani “Dikaioō” yaani kutangazwa kutokuwa na hatia you are innocent , free justify ni lugha ya kimahakama ya kukutangaza kuwa huna hatia. 

 

Warumi 5:1-2 “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.”

               

Warumi 5:8-9 “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.”

 

Wagalatia 3:10-14 “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

 

Tito 3:5-7 “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.”

 

3.       Damu ya Yesu pia inatupa ukombozi - Neno ukombozi katika maandiko ya kiingereza ni Redemption neno hili katika lugha ya kibiblia Neno hilo Redemption kwenye kiyunani linatumika neno “Apolutrōsis” ambalo maana yake kwa kiingereza ni Ransom in full ambalo tafasiri yake  a sum of money demanded or paid for release of a captive,  lugha hii inaweza kutumika katika mazingira ya mfano, watekaji nyara wanamteka mtu na kumuweka kizuizini, kisha wanadai kiwango fulani cha gharama kilipwe ili mateka huyo aweze kuwa huru, lugha hiyo ya kulipia deni ili mtu huyo mfungwa au aliyetekwa aweze kuachiwa huru ndio lugha ya ukombozi inayotajwa katika maandiko, kwa hiyo adui hana uwezo wa kukumiliki tena kwa sababu madai yake yamelipwa yote kwa ukamilifu hawezi tena kukuweka kizuizini na hana madai tena, Kwa hiyo Damu ya Yesu pia hufanya kazi ya kutukomboa yaani kututoa kifungoni, au kutuweka huru bila madai yoyote kutoka kwa aliyekuwa anatuzuia yaani shetani.

 

Waefeso 1:6-8 “Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;”

 

Wakolosai 1:14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”

 

1Petro 1:18-19 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.”

 

Wagalatia 5:1 “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.”

 

Kwa hiyo tunaweza kuona kuwa Damu ya Yesu inafanya kazi ya ukombozi, ambao unajumuisha kusamehewa dhambi, urejesho kutoka katika nguvu za kitu chochote kile ambacho kilikuwa na haki ya kukushikilia, zikiwemo nguvu za giza, unapomjia Yesu nguvu hizo hazina mamlaka ya kukushika kwa sababu zozote zile, hauko tena chini ya utumwa, au ufungwa au mateka ya adui kwa kuwa sasa wewe ni mali ya Yesu.

 

4.       Damu ya Yesu inatuhuhisha tena na kutuweka karibu na Mungu -  Kabla ya kumuamini Yesu kila mkristo na asiye mkristo ambaye hajaokolewa anahesabika kuwa alikuwa mbali na alikuwa ni adui wa Mungu, hatungeweza kuwa karibu na Mungu na kupata msaada kwake kwa sababu dhambi humweka mtu mbali na Mungu, lakini baada ya kazi aliyoifanya Yesu pale Msalabani sisi tuliokuwa mbali sasa tunaletwa karibu na Mungu kwa damu ya Yesu

 

Waefeso 2:11-13 “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono; kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.”

               

Wakolosai 1:21-22 “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;

 

5.       Damu ya Yesu inatupa kibali na ujasiri wa kupaingia patakatifu pa patakatifu – wote tutakuwa tunakumbuka ya kwamba Hekalu lilikuwa na maeneo makuu matatu, yaani uwa wa nje, kisha uwa wa ndani na ndani kabisa, uwa wa nje ni mahali ambapo watu walifika na kufanyiwa ibada za upatanisho za kila siku, na uwa wa ndani ni mahali ambapo makuhani waliingia kwa zamu kwaajili ya kufukiza uvumba kila siku, na uwa wa ndani kabisa mahali palipoitwa patakatifu pa patakatifu kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka na kuweka damu katika madhabahu ya Mungu ambacho ni kiti cha rehema kwaajili ya kuwaombea watu, eneo hili kuhani mkuu aliingia baada ya kuwa amejitakasa kwa siku saba, palikuwa ni mahali ambapo palikaa uwepo wa Mungu nyakati za agano la kale, hapa palitengwa kwa pazia maalumu lenye unene wa inchi sita sawa na unene wa tofali, lakini siku Yesu anakufa msalabani kwa kuimwaga damu yake Pazia hili lilipasuka vipande viwili na watu wakapaona mahali patakatifu ambapo ilikuwa sio rahisi kupaona, pazia hili liliwakilisha mwili wa Kristo uliosulubiwa na damu yake imetupa rehema na neema ya kuweza kumfikia Mungu moja kwa moja bila kizuizi wala bila kuhitaji mtu wa kuingia kwa niaba yako kwa kuwa wewe nawe umefanyika kuhani kwa nafsi yako.

 

Mathayo 27:51-54 “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu

 

Waebrania 10:19-21 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;       

 

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Maandiko yanapotualika kukaribia kwa ujasiri katika kiti cha Rehema au patakatifu maana yake tunaalikwa kumkaribia au kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo hofu sisi wenyewe mahali ambapo tutapokea msamaha na rehema na upendo wa Mungu, hii ni kwa sababu zamani kabla ya Yesu kufa Msalabani hakuna mtu aliruhusiwa kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo kuhani au kuitwa na Mungu mwenyewe na ukikaribia ilikuwa ni kifo, kwa hiyo katika nyakati za agano jipya baada ya kifo cha Bwana Yesu sasa tunaweza kwenda kwa uwazi, kwa uhuru, pasipo hofu, wala pasipo kuhani au mpatanishi, bila woga, bila kuhukumiwa na kukabiliana na Mungu sisi wenyewe na kujielezea kwake bila mtu kuingilia kati na kumwaga mizigo yetu, mashaka yetu, fadhaa zetu na hatutauawa kwa sababu ya rehema zake na upendo wake mkubwa kwetu atatusaidia, kwa sababu ya rehema zake atatupokea bila kujali ukubwa wa makosa yetu, hatuhitaji kuigiza kuwa sisi ni wakamilifu, hatuhitaji kujitafutia haki kwa sababu hatuwezi kuwa na haki yetu wenyewe, Sadaka pekee na kibali pakee kinachotupa ujasiri huo ni Kazi ya Yesu iliyofanyika pale Msalabani. Yaani Damu yale aliyoimwaga, na kwa njia ya Imani damu hii iakupa ruhusa, kibali au tiketi ya kumfikia Mungu

 

6.       Damu ya Bwana Yesu inatupa Amani na Mungu – Damu ya Yesu Kristo inatupa Amani ya kweli, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama hujasamehewa dhambi, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama uko chini ya ufalme wa giza, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama una uadui na Mungu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama huna ujasiri wa kupaingia patakatifu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama u mfungwa na mateka katika utawala wa ibilisi hivyo tunapomuamini Bwana Yesu, ambaye aliteseka kwa niaba yetu tunapata Amani ya kweli.

 

 Waebrania 9:12-14 “wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”                                                             

Wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo!

Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”                

Katika kifungu hiki cha maandiko tunapewa taarifa ya mfumo wa vita kubwa iliyoko katika ulimwengu wa roho na namna ya kuishinda vita hiyo, hii ni vita kati ya nuru na giza ni vita kati ya nguvu za uovu na wema wa Mungu, Kifungu kinafunua siri kubwa ya ushindi wa watu wa Mungu, kushinda kwa damu ya mwana kondoo kunajumuisha maswala yote muhimu ambayo tumeyapata kupitia damu hiyo ambayo yalikuwa yanampa nafasi shetani kutumia mfumo wa kimahakama na kibunge kutushinda kama mshitaki au mwendesha mashitaka na kwa sababu hiyo anapoteza haki na uwezo wa kutushitaki kwa sababu Damu ya Yesu Kristo imemaliza kila hati yake ya mashitaka anayotaka kuitumia ili tuharibiwe;-

Zakaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”

Nyakati za agano la kale Shetani aliendelea kufanya kazi zake za kushitaki wateule wa Mungu hata sasa bado anaifanya kazi hiyo na ndio maana anaitwa mshitaki wetu

1Petro5:8-10. “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.”

Kwa hiyo shetani alipata haki ya kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu kulikuwako hakuna damu ya Yesu, alimshitaki kuhani mkuu Yoshua kwa sababu kweli alikuwa mchafu na Bwana alimkemea, lakini sasa katika agano jipya damu ya Yesu inafanya kazi ya kumkemea ibilisi kwa niaba yetu kama tutaitumia kwa Imani kwa hiyo andiko la msingi linaonyesha kutupwa kwa Mshitaki huyu na sababu kubwa ya kutupwa kwake na ushindi mkubwa kupatikana ni Damu ya mwanakondoo na neno la ushuhuda.

a.       Ametupwa chini Mshitaki wa Ndugu zetu – Ibilisi hufanya kazi katika ulimwengu wa roho kwa mfumo wa kimashitaka na kwa kweli tuna haki ya kushitakiwa kutokana na ukweli ya kuwa tuna dhambi, lakini mashitaka ya shetani hupoteza haki kwa sababu  damu ya Yesu iliyopatikana kwa kazi iliyofanyika msalabani  inafanya kitu cha tofauti

 

i.                    Inatunenea mema – Waebrania 12:22-24 “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”

 

Damu ya Yesu inauwezo wa kuzungumza maneno mema mazuri kwaajili yetu kuliko mashitaka ya adui, kupitia ushindi wake pale Msalabani, Yesu amechukua ushindi dhidi ya nguvu za giza, Kwa hiyo Kazi ya damu hii ni kutunenea mema na kwa sababu hiyo huwezi kuhesabiwa kuwa na hatia, au u mtumwa ama vyovyote vile huwezi kuangamizwa kwa sababu ya damu ya Yesu, kwa hiyo neno hilo ni mjumuisho wa ushindi tulio nao kupitia damu ya Yesu ambayo kwayo inatupa neema juu ya neema, sio hivyo tu Damu ya Yesu inamkemea shetani asiwe na nguvu ya kutushitaki wala kufanya uonevu wa namna yoyote katika nafsi mwili na roho zetu.

 

Wakolosai 2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”

 

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

Ni hatari sana kumshitaki au kumuhukumu mtu anayemuamini Yesu kwa sababu anahesabiwa haki na Mungu, Andiko katika Warumi 8:33 katika kiingereza NIV mstari huo unasomeka

 

Who will bring any charge against those whom God hase chosen? It is God who justifies.”

 

Maana yake ni nani atakaye wahesabia kuwa wana hatia watu ambao Mungu amewachagua “Charge against” (KATA) kiyunani. Na swala hili jibu lake Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki Justifies anouced Innocent (DIKAIOŌ) kiyunani.  yaani wale waliotangazwa na hakimu kuwa hawana hatia INNOCENT maandiko yanaonyesha kuwa kupitia kazi aliyoifanya Yesu pale Msalabani kwa kumwaga damu yake (Kristo Yesu Ndiye aliyekufa) alafu yeye ndiye kuhani mkuu anayefanya upatanisho kwaajili yetu (Tena ndiye anayetuombea) kwa hiyo awaye yote ambaye anatuhesabia hatia au kutuhukumu kuwa hatufai ili hali Yesu amefanya kazi ya ukombozi na anatuombea huyu anaunganishwa na ibilisi katika kushindwa

 

Alaaniwe mtu awaye yote anayekuhesabia kuna na dhambi wakati Yesu amekufia msalabani na kumwaga damu yake nasema alaaniwe, aharibikiwe mtu awaye yote anayeongea maovu yako ili hali Mungu amekutangaza kuwa huna hatia, Bwana na amkemee kila mtu anayeipuuzia kazi ya damu ya Yesu iliyofanyika kwaajili yetu pale msalabani na kujidhani kuwa yeye ndiye yuko sawa, Ni damu ya Yesu inayotupa kiburi cha kuuliza ni nani atakayetushitaki?  Ni damu ya Yesu ndiyo iliyotuleta katika neema hii, kwa hiyo mtu yeyote anayehubiri kinyume na kazi ya damu Amelaaniwa.

 

Wagalatia 1:6-9 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”          

 

ii.                  Na kwa neno la ushuhuda – Ushuhuda huu unaotolewa na waamini ni ushuhuda gani? Ushuhuda wetu ni kuhusu kazi iliyofanywa na damu ya Yesu katika maisha yetu, tunapozungumza habari za ukombozi mkubwa unaosababishwa au uliosababishwa na Damu ya Yesu katika maisha yetu, tunaposhuhudia habari za ukombozi huu tunaendelea kueneza habari mbaya katika ufalme wa ibilisi kwa jinsi Damu hii inavyoleta neema na wepesi wa kila mwanadamu kukubali njia hii sahihi ya ukombozi iliyowekwa na Mungu Msalabani, na ushuhuda huo unatia hasara kubwa sana kwa upande wa shetani na kumletea kushindwa, kumbuka wakamshinda kwa Damu ya mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda. (Injili).

 

1Wakorintho 1:17-18 “Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”

 

Warumi 1:16-17 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”

 

iii.                Damu ya Yesu ni silaha – Damu ya Yesu inasimama kama silaha kubwa ya kivita ya hatari sana katika ulimwengu wa roho, inatumika kama ulinzi kwaajili yetu na silaha ya kumshinda shetani, anakosa nguvu kabisa tunapoikumbuka kazi aliyoifanya Yesu Pale msalabani, Damu hii ni ngao, damu hii inatulinda dhidi ya mashambulizi yote ya ibilisi, tunapokumbuka tu na kujua umuhimu wake na kazi yake ambayo imefanyika kila kitu katika ulimwengu wa roho hasa wa giza unaachia, kama liko giza haliwezi kusimama kwa kazi ya Msalaba, kila kikwazo chochote duniani ambacho kinatokana na mashambulizi ya ibilisi kinasambaratiswa kupitia Damu ya Yesu, tunachotakiwa ni kuitumainia Damu ya Yesu kwa Imani na kuendelea kuzungumzia utamu wa ushindi tunaoupata kupitia Damu ya Yesu, Nisikilize kazi yote ya msalabani na tangazo la Yesu Kristo kuwa imekwisha inakamilishwa katika Damu, ile iliyomwagika msalabani kwaajili yetu. Damu hii ni kitambulisho ya kuwa tuna uhuru, tumekombolewa, mfame ametangaza kuwa tuko huru, tuna ushirika wa kudumu na Mungu, hatudaiwi kodi, ni wageni tulioruhusiwa kufanya kazi zetu kwa kibali cha mfaome hapa duniani, tuna muungano wa kisera, kisiasa na ushirika na Mungu, tuna kibali, hatuna hatia, hatuna mashitaka, tumewekewa alama ya kutokuuawa, tuna utambulisho wa uhuru kwa sababu tumemuamini Mungu na tumeikubali kazi yake ya ukombozi.

 

Yoshua 2:18-19 “Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako. Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu, mkono wa mtu ukimpata.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumapili, 30 Juni 2024

Na tuvuke mpaka ng'ambo


Marko 4:35-41 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.  Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?


Utangulizi:

Kaka zangu, Dada zangu:- Ni muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuliamini kila neno, lililotoka katika kinywa cha Mungu bila kutia shaka yoyote hata kidogo! Wakati mwingine ni ngumu kufahamu kila hali inayokutokea katika maisha yako, kwanini jambo Fulani limechelewa, kwanini ulikutana na mwisho mbaya? Kwanini mligombana na ndugu yule, kwanini mtu yule alikufanyia ubaya? Kwanini maisha ni kama yamerudi nyuma, ni kama ulikuwa mbali na ni kama umerudishwa nyuma hatua mbili, Wakati mwingine Mungu hatuchukui katika kile tunachokitamani moja kwa moja, na wakati mwingine ili kuifikia ile hatima inayokusudiwa na Mungu, basi ni lazima, upitie katika changamoto kadhaa wa kadhaa. Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa mambo yote hutenda kazi kwa kusudi la kutimiza mapenzi yake, hata hivyo yeye anapotamka haijalishi ni hali gani inajitokeza kati kati lakini neno la Mungu litasimama vile vile bila kujali mazingira, kwani Mungu hutumia mambo yote katika kuwapatia watu wake mema!

Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Wakati mambo yanapokuwa mazuri huwa tunafurahia,  na tunaweza kukubali na kumuona Mungu ni mwema lakini mambo yanapoenda mrama tunaweza kuchanganyikiwa na tunasahau kuwa Mungu ndiye bwana mipango mkubwa, wakati mwingine anaweza kukurejesha nyuma, ili kwamba akupeleke mbele zaidi, anaweza kufunga milango na kutulazimisha kubadilika, au kubadilisha mitazamo yetu, inawezekana tulijisikia poa pale tulipokuwa, lakini Mungu hakujisikia poa, kwa sababu anakitu kikubwa zaidi kwaajili yako na yangu, ana kitu ambacho akili zetu haziwezi kuelewa, Leo tutachukua muda kuchambua kwa kina na mapana na marefu Marko 4:35-41 chini ya kichwa “Natuvuke mpaka Ng’ambo” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

1.       Nguvu ya maneno ya Yesu.

2.       Natuvuke mpaka ng’ambo!

3.       Hamna Imani bado?

 

Nguvu ya maneno ya Yesu.

Marko 4:35-39 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.”

Mojawapo ya jambo la Msingi tunalopaswa kufahamu ni kukubali ya kwamba maneno ya Bwana wetu Yesu yana nguvu ya ajabu sana kuliko tunavyoweza kufikiri, Yesu katika kifungu hiki anataka tuamini katika neno lake, na kujua ya kuwa akiagiza kitu au akisema kitu ni lazima kitatimia kama kilivyo bila kujali kuwa kutatokea nini mbele ya agizo lake au neno lake, Neno la Kristo likishatamkwa limetamkwa, neno lake linauwezo wa kugeuza machafuko kuwa Amani, kwa amri nyepesi tu Nyamaza na utulie, neno lake lina mamlaka ya kiungu, inayothibitisha kuwa yeye hakuwa tu Mwalimu wa kawaida bali alikuwa na mamlaka na amri, kila mtu aliyemsikiliza Yesu alikiri kuwa maneno yake na mafundisho yake hayakuwa ya kawaida bali yalijaa uwezo, yalijaa mamlaka, na yalikuwa amri, au sheria!

Luka 4:32 “wakashangaa mno kwa mafundisho yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo.”

Marko 1:21-22” Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.”

Maneno hayo Uwezo, na Amri katika lugha ya kiyunani linatumika neno “Exousia” ambalo kwa kiingereza linaweza kuwa na maana ya Power, Authority, Right, Liberty, Jurisdiction and strength ambalo linaweza kuelezewa kama sense of ability, force capacity,  hii inaonyesha kuwa maneno ya Yesu yalikuwa na nguvu, yalionyesha ushawishi, uweza wa kuhukumu kimahakama, nguvu ya maamuzi, nguvu ya kutenda, nguvu ya kuleta matokeo,  Nguvu ya kisheria, amri ya kijeshi, matokeo ya kiserekali, hii maana yake ni nini Yesu anapotamka jambo, ni kama hakimu anapokuwa ametamka hukumu, na kinachofuata Polisi hupiga saluti na kumchukua mtuhumiwa na kumpeleka magereza, yaani kwa lugha nyingine mamlaka yake inapotamka mara moja kinachotokea ni utekelezaji halali wa Amri halali ya neno hilo, yaani amri yake ni ya kifalme anaposema kile kilichosemwa ni amri, ni sheria, ni mamlaka halali imetamka na hivyo ni lazima kitekelezwe kile kilichotamkwa! Yesu alikuwa anataka wanafunzi wake wafikie ngazi ya kuamini ya kuwa atakachokisema kitatimia au ni lazima kitimizwe bila kujali ni mazingira gani yanajitokeza mbele ya neno lake na mfano mkubwa wa kutufundisha hilo ni amri yake kwa wanafunzi wake pale alipowaagiza kuwa Na tuvuke mpaka ng’ambo.

Na tuvuke mpaka Ng’ambo

Marko 4:35-38 “Siku ile kulipokuwa jioni, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?

Yesu alipoamuru wanafunzi wake na kuwaambia na tuvuke mpaka Ng’ambo na kisha yeye mwenyewe akapumzika na kulala, kisha dhuruba zikaanza kukipiga chombo na wanafunzi wake wakaanza kuhangaika, kulikuwa na kitu cha muhimu cha kuwafunza na kutufunza ya kwamba je tunasadiki maneno yake ?  na je tunaweza kuyasadiki maneno yake hata tukiwa katika taabu?  Yeye amesema na tuvuke mpaka ng’ambo, amri ya mfalme ni sheria tayari mazingira yote yanaratibiwa kuhakikisha ya kuwa neno lake linatimizwa, kumbuka chochote anachokuambia Yesu kitakuwa vile vile kama alivyosema na sio vinginevyo.

Marko 11:13-23 “Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.  Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.”

Yesu aliwahi kuuambia mtini, tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako, na katika macho ya nyama mtini ule ulionekana ni kama bado uko vile vile, Lakini Kristo hakuwa na shaka, asubuhi yake Petro aliuona ule mtini umenyauka toka shinani, na alimkumbusha Yesu maneno yake, Yesu aliwaonyesha ya kuwa sio maneno yake tu hata na ya kwetu tukiyatamka pasipo shaka huku tukimuamini Mungu yatatuklioa vile vile.             

Yohana 11:23-26 “Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

Yesu aliwahi kumwambia Martha kwa habari ya kaka yake Lazaro ambaye alikuwa amekufa na kuzikwa alimwambia ndugu yako atafufuka. Martha alianza kujieleza kwa mambo mengi, najua atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho na kadhalika na kadhalika, mpaka wakati huu Martha alikuwa hajajua mamlaka ya neno la Yesu, Yesu anapotamka neno ni wajibu wetu kusadiki bila kujali ya kuwa kuna mazingira gani 

Yesu akiisha kutamka neno hata kama mazingira yanaonekana kukataa, au kutokukubali au kuonyesha matumaini hiyo haisaidii kulifanya neno lake lisiwe Dhahiri, changamoto zozote zitakazojitiokeza zinasaidia kutusafirisha kutufikisha katika kulitimiza neno la Bwana, Changamoto haziko hapo kutuzuia, lakini changamoto ziko pale kutupeleka katika kiwango cha juuu zaidi  lakini je tunaweza kumuamini yeye wakati mambo yanapoonekana kwenda ndivyo sivyo? Je tunaweza kuwa na Amani wakati mambo yanapoonekana kuwa sio?  Lazima tuamini katika kile alichokizungumza kumbuka yeye alisema na tuvuke mpaka ng’ambo hii maana yake ni kuwa tutafika nga’mbo hata bila kujali ni nini kinajitokeza katikati ya maneno ya Bwana Yesu ni kwa sababu ya tukio hili Yesu aliwakemea kuwa hawajaamini Bado kwa sababu wao walipoona changamoto waliogopa na kuanza kulia na kumuona mwalimu kama mtu asiyejali dhuruba walizokuwa wakizipitia lakini kimsingi Yesu alikuwa na utulivu mkubwa sana kwa sababu aliamini katika neno lake na kuwa hakuna jambo lolote linaweza kusimama kinyume na neno lake natuvuke mpaka ng’ambo.

Hamna Imani bado?  

Marko 4:39-41 “Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Yesu anaweza kutuagiza tuelekee mahali ambapo kuna changamoto, maandiko mengine yanasema akawashurutisha na tuvuke mpaka ngambo, ni wazi kuwa pale walipokuwepo walifurahia sana Baraka za Mungu na hawakutaka kuondoka, Palitendeka miujiza mingi, hata hivyo walihitaji kupumzika, na vilevioe kuwafikiwa watu wengine, hivyo aliwalazimisha wavuke Ng’ambo kwanini  lakini ?  Mungu hawezi kutulazimisha hivi hivi tu, anaweza kukuondoa katika eneo ambalo unakula raha na akataka uelekee eneo lingine lenye Baraka zake kubwa zaidi, wakati mwingine ni ngumu kuona na kufurahia maagizo ya kiungu na kuyaamini lakini Mungu hawezi kukulazimisha uende mahali ambapo, anajua utakutana na dhuruba ambazo zitayaangamiza maisha yetu, sababu kubwa ya kukutuma kwenye dhoruba ni kwa sababu anajua utatoboa na iko njia iliyonyooka, yeye ndiye anayefanya njia, na ni yeye ndiye anayeyaongoza maisha yako na yangu  hakuna sababu ya kujitahidi kuyaokoa maisha yetu,  hakuna sababu ya kuogopa,  wala kuhofia kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Yesu, yeye anajua yupo na anajua kuwa ametamka neno lake na itakuwa salama  anajua pia anauwezo wa kunyamazisha kila aina ya dhoruba inayoyakabili maisha yako, Basi unachopaswa kukifanya wewe ni kuamini katika kile ambacho Mungu amekisema, upepo uliwaleta mahali pazuri zaidi ya kule jangwani walikokuweko

Yesu anapozungumza maneno yake hayawi bure yanatimiza makusudi yake makuu na hakuna kinachoweza kuzuia neno lake katika mazingira yoyote

Mawimbi  yanapokuja yanajaribu tu uwezo wetu wa kuamini, yanapima kwamba tunamuelewa Yesu kwa kiwango gani na tunayachukulia vipi maneno yake, Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kuamini katika maneno yake na mamlaka kubwa aliyokuwa nayo, Changamoto ni kipimo kuwa tunamsadiki yeye kwa kiwango gani, na sio hivyo tu changamoto hizo zinamfunua Yesu pia kwa undani zaidi, wanafunzi walikuwa wanamuona Yesu ni wa kawaida tu, lakini sasa sio tu aliwakema kwa kutokuamini kwao lakini alijifunua kwao katika kiwango cha juu zaidi, yeye aliukemea upepo na bahari na kuziamuru kunyamaza na kutulia na wanafunzi waliacha kuogopa hilo na sasa walimuogopa Yesu na kujiuliza kuwa huyu ni  mtu wa namna gani hata bahari na uepo unamtii ?

Hitimisho

Yesu aliwahoji wanafunzi wake Mbona mmekuwa waoga hamna Imani bado?  Nini maana yake muitikio wetu kwa neno la Kristo unapaswa kuwa usiojawa shaka na hofu wala kujali mazingira  hatuna budi kuendelea kuamini nguvu yake mamlaka yake na neno lake, tujue ya kuwa Mungu wakati wote ni mwema na kila anakotupeleka hutupeleka kwa kusudi lake,  anaposema kitu ni lazima tutii, lakini sio hivyo Yesu alikuwepo pale, wanafunzi wake walipaswa kuamini pia katika uwepo wake  hii inatukumbusha kuwa na Amani tunapokuwa katika uwepo wa Mungu  yeye yuko kwaajili yetu, neno lake sio tu linaleta utulivu wakati wa dhuruba lakini pia linatuhakikishia Amani ya maisha yetu, hivyo wajibu wetu kwa neno lake ni kuamini, kutii na kuwa na Amani katika uwepo wake.

 

Na Rev.Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana

 

Kumbukumbu 18:9-12 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.”


Utangulizi

Kaka zangu na dada zangu wapenzi katika Bwana, Leo tunachukua muda kuzungumzia kwa masikitiko makubwa Swala zima lenye kusikitisha na kutisha na linaloashiria kuwa jamii yetu bado tuko nyuma sana  na tuna safari ndefu sana ya kujiondoa katika ujinga na ufahamu finyu, kuhusu Mapenzi ya Mungu na upendo wake mkubwa kwa wanadamu, kwa kupambana na swala zima la mauaji ya wanadamu kwa dhana potofu za aina mbalimbali ambazo bado zinaendelea kujitokeza katika jamii, Dhana hizi ni pamoja na kutoa kafara za wanadamu, kuua wanawake vikongwe kwa kufikiri ya kuwa ni washirikina au wachawi, na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaani watu wenye u-albino na kuwakata viungo vyao ili kuvitumia kwa ushirikina kwa kufikiri ya kuwa, viungo vya watu hao inaweza kusababisha mafanikio, vyeo, heshima na utajiri, Dhana hii ni dhambi na machukizo makubwa sana mbele za Mungu, na ni kinyume na Amri za Mungu na njia zake za kweli za kutuletea Baraka  wale wanaoamini katika njia ya ushirikina kwaajili ya kujiletea Heshima, vyeo, utajiri na mafanikio wamefuata njia ya mauti yao wenyewe.

Mithali 14:11-12 “Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa. Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”   

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-


·         Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana!

·         Albino hafai kwa dhabihu

·         Njia ya kweli ya Mafanikio


Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana!

Ni muhimu kufahamu, kuwa ziko imani nyingi potofu na ambazo ziko kinyume na maagizo ya Mungu na mafundisho yake na imani hizo zinaelekeza kutoa dhabihu za kuua wanadamu kama kafara eti ili kuleta mafanikio ya kibiashara, cheo, heshima na utajiri kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, imani hizi zimejikita pia katika kuwashambulia na kuwaua ili kwa kutumia damu zao na baadhi ya viungo watu hao waweze kutoa kafara kwa kuamini kuwa watajiletea mafanikio Jambo hilo ni chukizo kwa Mungu na ni kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, na siku za karibuni watu hao wamekuwa wakiwashambulia watu wenye ulemavu wa ngozi wajulikanao kitaalamu kama Albinos, njia hiyo sio njia sahihi ya kuleta Baraka na mafanikio na badala yake inaleta laana, Hatuwezi kupata Baraka kwa kuziarifu amri za Mungu, na kwa kujikita katika ushirikina njia hiyo ni machukizo makubwa sana kwa Mungu:-

-          Kumbukumbu 12:28-32 “Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa Bwana, Mungu wako. Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao; ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo. Usimtende kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto. Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.”

 

Mungu wa kweli, Mungu mwenyezi aliyeziumba mbingu na nchi Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo, alikuwa amewaokoa wana wa Israel kutoka utumwani Misri na kuwaleta katika inchi ya Mkanaani, Mungu alikuwa anataka wana wa Israel wafanikiwe kama anavyotaka wewe na mimi leo vile vile tufanikiwe, lakini Mungu aliwafundisha mojawapo ya njia ya mafanikio ni pamoja na kutenda yaliyo mema machoni pake ikiwa ni pamoja na kutokuwatoa wana wao na binti zao kafara au dhabihu kwa kuwaua na kuwateketeza kwa moto,  jambo hili Mungu alichukizwa nalo na ndilo ambalo watu walioishi Kanaani walikuwa wakiyafanya hayo na Mungu akachukizwa nao na kuwafutilia mbali.  Kwa hiyo kuwatoa wanadamu kama sadaka au dhabihu ni machukizo kwa Mungu. Lakini pia kukata viungo vya watu wenye u albino ni machukizo makuu.

 

2Wafalme 21:1-9 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli. Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia. Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana. Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha. Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele; wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa. Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.”

 

Inawezekana katika jamii yetu watoto hao wasiteketezwe kwa moto, lakini matendo yanayofanyika ya kuwaua kuwakata baadhi ya viungo kwaajili ya sababu za kishirikina yanafanana kwa kiasi kikubwa na matukio ambayo yameorodheshwa katika machukizo mabaya ambayo Mungu anachukizwa  nayo sana, Matendo ya jinsi hii yalikuwa yakifanywa na wakazi wa Kanaani na ndio mojawapo ya sababu zilizopelekea Mungu kuwaondoa na kuwakataza Israel wasifanye kwa mfano wa matendo hayo ambayo kwa Mungu ni dhambi wafalme na watu wengi sana walioishi Kanaani walitegemea kufanya machukizo hayo kwaajili ya kuabudu miungu na kwaajili ya ushirikina wakifikiri kuwa watabarikiwa kwa kufanya mambo hayo.

 

2wafalme 3:26-27 “Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.”

 

Walawi 18:21 “Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapitisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi BWANA.”

 

Watu wote na ibada yoyote ile inayohusisha kuwatoa watoto wa kike au wa kiume na kuwateketeza, au kwa kukata viungo vyao na kwa njia zozote za kishirikina ibada za namna hiyo ziko kinyume na mapenzi ya Mungu na wote wanaofanya hivyo hufanya hayo kwa mashetani au mapepo na wanasababisha laana badala ya Baraka, nchi inalaanika na kutiwa unajisi na kuichochea hasira ya Bwana na kujitia utumwani kwa hiyo badala ya kuleta mafanikio wanayodhani, wanajiletea laana na sio wao tu na nchi zima inatiwa laama kwa sababu hizo uko ulazima wa viongozi wa dini, na imani zote na viongozi wa kimila na kisiasa kwa sababu zozote zile na kwa nia moja kusimama sawasawa na neno la Mungu na kukemea vikali swala zima la mauaji ya Albino na matendo yote ya ushirikina na upigaji ramli na utazamaji wa nyakati mbaya ambayo kimsingi yote yamekemewa katika maandiko  na ndio sababu kubwa ya mauaji ya wenye u albino na kukatwa kwa viungo

 

Zaburi 106:37-42 “Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu. Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao. Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake. Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala. Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.”       

 

Albino hafai kwa dhabihu

Katika siku za miaka ya karibuni na hata majuzi hapa kumeibuka tena tabia za watu wenye mawazo ya kishirikina ambao wamekuwa wakiwaandama watu wenye ulemavu wa ngozi na kuwaua na kuwakata viungo vyao, kwa Imani za kishirikina wakifikiri kuwa wanaweza kujijengea umaarufu, kufanikisha biashara, kupata vyeo vya kisiasa na kutajirika au kujiletea mafanikio mbalimbali, lakini kama tulivyoona katika kipengele hapo juu, Dhabihu ya namna hiyo haipokelewi na Mungu aliye hai na ni dhabihu iliyo machukizo kwa Mungu, na Mungu mwenyezi amekataa kuwa yeye hapokei sadaka za aina hiyo, na hivyo maandiko yako wazi kuwa kazi hizo zinafanywa na washirikina, wachawi na wapiga ramli,  hata hivyo pia nataka kukazia wazi kuwa hata kama Mungu angelitaka sadaka za wanadamu, Mungu asingeliwatumia albino kwa dhabihu, kwa nini kwa sababu ualbino ni ulemavu wa ngozi na hivyo watu hao hawafai kwa dhabihu! Kama wasingelifaa kwa dhabihu kwa Mungu basi hawawezi kufaa kuwa dhabihu kwa miungu.

Ualbino ni changamoto ya kuzaliwa inayotokana na mvurugiko wa vinasaba vya kuzaliwa na kumfanya kiumbe anayezaliwa, kuzaliwa akiwa na changamoto ya ukosefu wa kemikali ya rangi ya ngozi ambayo kitaalamu inaitwa “Melanin” Kemikali hii ndiyo inayoamua kuwa mwili wa mwanadamu uwe na rangi gani katika ngozi, nywele na macho, kwa hiyo mtu mwenye ualbino kimsingi anakosa kirutubisho hicho na hivyo kumuweka katika mazingira yasiyo rafiki kwa jua, na hivyo kuweza kuandamwa na tatizo la saratani ya ngozi, Melanin pia ni kemikali inayohusika na kazi za uoni, na inapokosekana pia husababisha tatizo la uoni hafifu, ualbino hutokea kwa Waafrika, Wazungu, Waarabu na Waasia  na mara chache pia kwa baadhi ya wanyama. Neno Albino limetokana na neno la asili la kilatini Albus ambalo maana yake ni Nyeupe kwa hiyo watu hawa huwa na ngozi nyenye weupe usiokuwa wa kawaida, ualbino wenyewe sio ugonjwa lakini ni ulemavu wa ngozi, kwa hiyo kuna changamoto katika ngozi, nyele na macho inayowafanya wao wasiwe na ukamilifu kimaumbile, lakini wana akili, uwezo na hufanya kazi zao kama wanadamu wengine.  Kwa hiyo wao sio watu wenye ngozi nyeupe bali wao ni watu wenye ulemavu wa ngozi.

Kwa sababu ya ulemavu huu wao hawaingii katika kundi la wanyama au watu wanaotakiwa kutumika kwa dhabihu au kafara, Mwana kondoo wa kafara alitakiwa asiwe na maraka raka wala dosari ya aina yoyote ile nahii ilikuwa ikimzungumzia Yesu Kristo pekee ambaye alikuwa ni sadaka kamili isiyo na dhambi, Mwanakondoo wa sadaka ya dhabihu alikuwa na sifa zifuatazo ambazo kinabii zilimuhusu Yesu Kristo asiyekuwa na dhambi.

1.       Asiwe na Dosari -  Mwanakondoo wa Sadaka ya dhabihu alipaswa kuwa asiye na dosari wala doa la aina yoyote hii maana yake aliwakilisha ukamilifu na usafi ikiwakilisha picha ya Bwana Yesu pekee

 

Kutoka 12:5 “Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.”

 

2.       Alichaguliwa kwa uangalifu sana  kuhakikisha kuwa ni mkamilifu -  Mwankondoo wa sadaka ya dhabihu alichaguliwa kwa uangalifu mkubwa  ili kumpatia Mungu kitu kilicho bora, kumbuka sadaka hiyo pia ilitakiwa kuwa kondoo mume aliye mamilifu, hii maana yake ni kuwa haikutakiwa kuwa ya kike pia

                 

Walawi 1:10 “Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu.”

               

3.       Sadaka ya dhabihu haikupaswa kuwa na ulemavu – Ulemavu unawakilisha mapungufu ya kawaida ya kibinadamu na wanyama kwa hiyo mnyama wa dhabihu hakupaswa kuwa mwenye ulemavu hii maana yake ni kuwa chochote chenye ulemavu hakiwezi kufaa kuwa sadaka ya dhabihu kwa Mungu au miungu

 

Kumbukumbu 17:1Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.”

 

4.       Dhabihu ya Albino sio dhabihu kamilifu – Mungu alitoa agizo kwamba dhabihu zinapaswa kuwa kamilifu, bila dosari, dhabihu yoyote iliyokuwa na dosari ilikuwa ni machukizo kwa Mungu, ile tu mtu kuwa Albino yaani kuwa na ulemavu wa ngozi, na ile tu kuwa Mungu amekataza mwanadamu asitolewe dhabihu tayari kuwatoa wanadamu na zaidi sana wenye ualbino ni kumtolea Mungu au miungu dhabihu isiyofaa, Mungu alikataa dhabihu za wanyama waliokuwa na ulemavu, na alikataa kutumikiwa na makuhani waliokuwa na ulemavu na hii itupe picha ya kuwa mwanadamu mwenye ualbino ni marufuku kutolewa dhabihu na sio wao tu ushirikina ni marufuku, nahata mwanadamu wa kawaida ni marufuku kutolewa dhabihu na kuabudu miungu au kuabudu mizimu, au kufuata maelekezo ya waganga, au wachawi haya yote ni machukizo kwa Bwana Mungu wetu na ni kinyume na maelekezo yake na mwelekeo wa kidhabihu.

 

Malaki 1:8 “Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi.”    

 

5.       Dhabihu ya Albino ni dhabihu ya udhalimu -  Mungu anachukizwa sana na watu wanaotoa dhabihu ya udhalimu, unapomtoa mtu huyu mwenye haki ya kuishi, huku ukiwa umedhulumu maisha yake hiyo ni dhambi, umeua na amri ya Mungu imesema usiue kwa hiyo huwezi kupata Baraka kwa kudhulumu maisha ya mtu hiyo ni dhambi na ni machukizo kwa Mungu, ni dhambi kwa sababu ni ushetani, ni ushirikina, mganga aliyeagiza ana dhambi, yeye aliyeagizwa ana dhambi na wale wanaohusika katika kuitekeleza dhabihu ya aina hiyo wana dhambi kwa hiyo huwezi kupata mafanikio na badala yake unavuna laana, sadaka hiyo inakuwa ni sadaka ya wasio haki na ni sadaka isiyotokana na melekezo ya kiungu ni sadaka au dhabihu ya watu wenye nia mbaya na moja kwa moja inakataliwa na Mungu. Huo ni uchawi na ushirikina kinyume na mapenzi ya Mungu, Kanisa ni lazima lisimame kinyume na uovu huu ambao sio sifa ukasikika katika jamii.  

 

Mithali 21:27 “Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!

 

6.       Dhabihu ya Albino ni dhabihu batili  -  Dhabihu ya watu wenye ualbino ni dhabihu ambayo haikuwahi kuagizwa na Mungu wala miungu wala hata mashetani, kwa hiyo ni machukizo na ni batili, kwa hiyo Mungu anachukizwa nazo, wala hazifurahii, watu wanaofanya hayo watapata laana badala ya Baraka wanazozifikiria kuwa watazipata, sio tu wanajiletea laana kwa familia zao lakini pia wanajiletea laana kwa taifa lao.

 

Isaya 1:10-16 “Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;”

 

7.       Dhabihu ya kichawi au za watu wanaoabudu miungu mingi - Mungu anachukizwa na dhabihu zote za kishirikina zinazotolewa kwa miungu na ibada zote za kishirikina na sanamu zilizo kinyume na Imani ya kweli ibada hizo zote ni machukizo kwa Mungu

 

Yeremia 7:9-10 “Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?

 

Mungu hataki ibada zenye michanganyo, ibada zote za namna hii zinaitwa ibada za kishirikina, kimsingi watu wanaotoa sadaka hizo au dhabihu hizi mbaya wana dini zao ambazo zinaweza kuwa zinamtaja Mungu na wakati huo huo wanashiriki maswala ya uchawi na uchafu mkubwa unaohusisha kuwaua watu wa Mungu.

Kwa hiyo kimsingi kwanza wote tunafahamu kuwa Mungu hakubaliani na sadaka ya dhabihu ya kuwatoa wanadamu, lakini pili tunakubaliana kuwa Mungu hapokei sadaka yenye dosari, au yenye kasoro au isiyokamilika, au isiyofaa, au yenye dosari au ulemavu wa aina yoyote, kwa msingi huo hata kama wanadamu wangekuwa wanatolewa dhabihu kwa Mungu basi mtu mwenye u albino hafai kwa dhabihu, sio hivyo tu hata mtoa dhabihu hakupaswa kuwa na ulemavu wa aina yoyote ile katika nyakati za agano la kale kwa hiyo kama sheria ya Musa ingelikuwa inafanya kazi hata sasa basi mwenye ualboni hangeweza kufaa kuwa mtumishi wa Mungu au kuhani, Hapa lengo langu sio kuwabagua wenye ualbino lakini nataka kunyesha kimaandiko ni namna gani Albino wasingeliweza kufaa kwa kafara

Walawi 21: 17-21 “Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili, au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono, au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za BWANA kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.”               

Lengo langu hasa ni nini hapo, kwa kawaida miungu mingi na hata shetani ameigiza kila kitu kutoka kwa Mungu mwenyezi, kwa hiyo kama unavyoona tabia ya Mungu mwenyezi kutaka kitu kisicho na mawaa wala doa wala dosari na wala kisicho na kilema; Hali kadhalika miungu na mashetani pia hutaka au hutembea katika kanuni hizo hizo kwa sababu hiyo, kwa kuwa watu wenye ualbino ni wanadamu kamili lakini wana ulemavu wa ngozi, kwa mujibu wa torati hawafai kwa dhabihu, Maana yake ni nini? Wale wanaowaua na kuwakata viungo watu wenye ulemavu wa ngozi, wanafanya makosa makubwa sana kwa sababu hakuna ibada ya aina yao inayoweza kukubalika na miungu ya aina yoyote.

Lengo langu ni nini hapa watu wenye changamoto ya ualbino wanapaswa kuachwa, na kuwa watu huru wasitishiwe kwa sababu zozote zile kwa sababu hawafai kwa huo ushirikina, lakini wanafaa katika jamii, mchango wao katika jamii unahitajika, Mungu hakuwaumba wao wawe maalumu kwaajili ya dhabihu hapana, waganga wanaotaka viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni waongo na kamwe hawajui kabisa kanuni za utendaji wa maswala ya kiroho yawe ya Mungu au ya kienyeji, wenye kushiriki zoezi hili ni washirikina kamili na ni wachawi na wapiga ramli na ni watu wasioelimika na waliopitwa na wakati au wako nyuma sana, wanasababisha mashaka, na huzuni na kuwafanya watu hao wa waishi kwa hofu, na wazazi wao na jamii isiwe mahali salama ni jambo la kusikitisha ya kuwa mtu mwenye tatizo anaongezewa tatizo badala ya kuwafariji na kulia nao katika changamoto hii ya ukosefu wa melanin katika maisha yao.

Namuomba Mungu kuwa tiba ya kuweza kurejesha melanini katika jamii hii igunduliwe lakini pia watu wa maombezi, tumuombe Mungu ili aweze kuwaponya watu wenye changamoto hii, aidha mimba zote na  watu wote walio wajawazito waombewe na kuwekwa katika mikono ya Bwana na wazingatie kanuni zote za kiafya na kitabibu ili kuzuia uwezekano wa kuzaliwa kwa watu wenye ulemavu huu.

Imani yangu ni kuwa kama sababu zinaanza kueleweka hatutashindwa kupata majibu ya kushughulika na changamoto hii, naungana na wanajamii wote duniani, na Afrika na katika ukanda wetu kukemea na kusimama kinyume na matendo yote ya kijinga ikiwepo tendo hili la kuwatoa walemavu wa ngozi na kuwafanya dhabihu kwa miungu nalaani kitendo hiki na wote wanaojihusisha na matendo haya na naiombea serikali kuwa ifanikiwe kumkamata kila mtu aliye kwenye mnyororo wa matendo haya maovu katika jamii, matendo haya ukiacha ya kuwa yanamuudhi Mungu lakini ni ishara ya jamii jinga isiyoelimika wala kustaarabika yanaposikilizika  katika masikio yetu matukio kama haya hasa katika nyakati za karibu na chaguzi za serikali za mitaa na serikali kuu, Mungu atuepushe na kuwa na jamii na viongozi wanaoamini katika ushirikina na Mungu awanyime mamlaka zozote zile zinazopatikana kwa njia ya kishirikina na wananchi wasimchague mtu yeyote yule anayekisiwa kujihusisha na ushirikina kwani hawezi kutuletea maendeleo ya kweli wakati yeye yuko nyuma kimaendeleo!

Naelezea haya kwa uchungu mkubwa kwa sababu sitaki kuamini kuwa katika jamii zetu bado tunao watu wanaosadiki mambo ya kijinga na huku wengine wakiwa ni viongozi wa kidini!, Hebu tuwaache ndugu zetu, kaka zetu na dada zetu wenye ualbino wawe huru waishi kwa Amani na utulivu, tuwaache wapambane na hali zao badala ya kuwaongezea maumivu mengine, na kila kiongozi wa ngazi yoyote kuanzia ya familia ahakikishe ya kuwa matendo haya hayatajwi na wala kusikika katika taifa letu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufunguka macho na kuondoka katiia ujinga huu katika jina la Yesu Kristo amen.

Njia ya kweli ya Mafanikio

1.       Mungu kwanza – Mungu aliahidi katika neno lake ya kuwa tukimtanguliza yeye na kumuweka yeye mbele yeye atayafanikisha maisha yetu, hakuna mafanikio ya kweli nje ya Mungu, Mungu ndiye mwenye neema ya kutufanikisha, hivyo ni muhimu kwetu kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na hakli yake naye na mengine tutazidishiwa.

 

Zaburi 84:11 “Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.”

 

Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

 

Tunapomuweka Mungu mbele yeye hutupatia mahitaji yetu yote, na huu ni msingi mmojawapo muhimu wa mafanikio, Mungu ndiye anayetupa akili za kupata utajiri.

 

Kumbukumbu 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”

 

2.       Utii kwa maagizo ya Mungu – Mafanikio ya kweli yana uhusiano mkubwa sana na utii kwa amri za Mungu au maagizo yake, tunapoyatii maagizo yake yeye hutuongoza na kutuletea Baraka kubwa ambazo zinatuletea mafanikio

Yoahua 1: 8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

 

1Wafalme 2:1-3 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”  

 

3.       Mwamini Mungu, mtumainie yeye kwa moyo wako wote  – unapoamini katika Mungu kwa moyo wako wote na kudumisha uhusiano wake nay eye anakuwa msaada mkubwa katika kila aina ya dhuruba tunayokutana nayo

 

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

 

Warumi 8:32 “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?

 

4.       Kufanya kazi kwa bidii   - Maandiko yanatufundisha umuhimu wa kufanya kazi kwa bidi, na kwa uaminifu, Mafanikio hayaji kwa uvivu, bali ka juhudi na uaminifu na kujituma tunapofanya hivyo Mungu yeye hubariki kazi za mikono yetu hii ndio kanuni mojawapo muhimu ya kibiblia ya mafanikio na kwa uvumilivu

 

Mithali 10:4 “Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.”

               

Kumbukumbu 28:11- 12 “Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa. Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.”

 

5.       Ni heri kutoa kuliko kupokea -  Matendo ya ukarimu kwa wengine na utoaji ni mojawapo ya njia inayofungua milango ya Baraka, wanadamu wote bila kujali Imani zao wanapoishi katiika kanuni hii wanabarikiwa, maandiko yanashuhudia kwamba ni vema kutoa na kutoa kwetu kunafungua mlango wa Baraka na mafanikio makubwa sana

 

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”

 

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

 

Matendo 10:1-4 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”

 

Tunapoishi maisha ya ukarimu na kujitoa kwa watu wenye mahitaji tunamkopesha Mungu na kutuweka katika njia ya Baraka na mafanikio ya aina mbalimbali kutoka kwa Mungu

 

6.       Maombi na kudumisha uhusiano na Mungu – Kwa kuwa Mungu ndiye chanzo cha mafanikio ya kweli ni vema kwetu kuhakikisha ya kuwa tunadumisha uhusiano  wetu nay eye,  kwa kusali na kuomba, huku tukikumbuka ya kuwa wakati wote Mungu anatuwazia mema

 

Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”

Hitimisho:

Ndugu zangu, Mafanikio ya kweli nay a kudumu yanapatikana kwa kuutafuta uso wa Mungu na kumpa yeye kipaumbele, kutii amri zake na kwa neema yake tukimtumaini yeye kwa moyo wetu wote na kufanya kazi kwa bidi, na kwa uaminifu, na kuonyesha matendo ya ukarimu kwa wengine Mungu atatupa mafanikio makubwa sana, Mafanikio ya kishirikina sio ya kudumu, na hayawezi kukupa Amani ya kweli, inasikitisha sana kuona au kusikia kuwa bado kuna watu wana akili za kizamani za wakati wa ujinga kwa kutoa sadaka ya viungo vya binadamu na zaidi sana wenye tatizo la Albinism kwa kuwaua na kuchukua baadhi ya viungo vyao hiyo haiwezi kutupa mafanikio ya kweli nay a kudumu, Mungu ametupa njia iliyo bora zaidi ni sadaka moja tu ya Mwanadamu aliyemwaga damu yake Msalabani ilitolewa kwa niaba yatu na hiyo tu ndiyominayokubaliwa na Mungu kwaajili ya mafanikio yote ya kimwili na kiroho kwa wanadamu wote ulimwenguni na sio vinginevyo:-

Isaya 53:4-6 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.”

2Wakorintho 8:7-9 “Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”  
           

Jamii inapaswa kuelimisha watu na kukemea swala hilo vikali, Watu wenye ulemavu huu wa ngozi wamekuwa wakinyanyasika kwa sababu ya misimamo inayochangiwa na wagaganga wa kienyeji wenye madai kuwa uchawi unaohusisha viungo vya Albino una nguvu sana Imani hii potofu imechangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya watu hao, n ahata kuchimbwa kwa makaburi yao na kukatwa viungo vyao, dhana hii inajitokeza zaidi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza, aidha watu wenye ualbino wananyanyasika wakati mwingine wakifikiriwa kuwa ni watu wasiotakiwa katika familia au jamii Ndugu zangu ni lazima tubadilike, utafiti mdogo unaonyesha kuwa Tanzania huenda labda ndio inchi inayoongoza kwa kuwa na albino wengi duniani, Hata hivyo wakati mwingine pia albino wametekwa na kusafirishwa mpaka katika inchi jirani, au kuuawa na wahusika kukimbilia katika inchi za jirani, ni aibu kwa Taifa lenye kuehsimika kama Tanzania kuwa na sifa ya mambo ya kijinga hivi, injili ihubiriwe na dini na imani za kweli zikifishwe katika maeneo yote ambayo yanazingirwa na imani hizi potofu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!