Jumapili, 30 Juni 2024

Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana

 

Kumbukumbu 18:9-12 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.”


Utangulizi

Kaka zangu na dada zangu wapenzi katika Bwana, Leo tunachukua muda kuzungumzia kwa masikitiko makubwa Swala zima lenye kusikitisha na kutisha na linaloashiria kuwa jamii yetu bado tuko nyuma sana  na tuna safari ndefu sana ya kujiondoa katika ujinga na ufahamu finyu, kuhusu Mapenzi ya Mungu na upendo wake mkubwa kwa wanadamu, kwa kupambana na swala zima la mauaji ya wanadamu kwa dhana potofu za aina mbalimbali ambazo bado zinaendelea kujitokeza katika jamii, Dhana hizi ni pamoja na kutoa kafara za wanadamu, kuua wanawake vikongwe kwa kufikiri ya kuwa ni washirikina au wachawi, na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaani watu wenye u-albino na kuwakata viungo vyao ili kuvitumia kwa ushirikina kwa kufikiri ya kuwa, viungo vya watu hao inaweza kusababisha mafanikio, vyeo, heshima na utajiri, Dhana hii ni dhambi na machukizo makubwa sana mbele za Mungu, na ni kinyume na Amri za Mungu na njia zake za kweli za kutuletea Baraka  wale wanaoamini katika njia ya ushirikina kwaajili ya kujiletea Heshima, vyeo, utajiri na mafanikio wamefuata njia ya mauti yao wenyewe.

Mithali 14:11-12 “Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa. Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.”   

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-


·         Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana!

·         Albino hafai kwa dhabihu

·         Njia ya kweli ya Mafanikio


Dhabihu iliyomachukizo kwa Bwana!

Ni muhimu kufahamu, kuwa ziko imani nyingi potofu na ambazo ziko kinyume na maagizo ya Mungu na mafundisho yake na imani hizo zinaelekeza kutoa dhabihu za kuua wanadamu kama kafara eti ili kuleta mafanikio ya kibiashara, cheo, heshima na utajiri kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, imani hizi zimejikita pia katika kuwashambulia na kuwaua ili kwa kutumia damu zao na baadhi ya viungo watu hao waweze kutoa kafara kwa kuamini kuwa watajiletea mafanikio Jambo hilo ni chukizo kwa Mungu na ni kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, na siku za karibuni watu hao wamekuwa wakiwashambulia watu wenye ulemavu wa ngozi wajulikanao kitaalamu kama Albinos, njia hiyo sio njia sahihi ya kuleta Baraka na mafanikio na badala yake inaleta laana, Hatuwezi kupata Baraka kwa kuziarifu amri za Mungu, na kwa kujikita katika ushirikina njia hiyo ni machukizo makubwa sana kwa Mungu:-

-          Kumbukumbu 12:28-32 “Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa Bwana, Mungu wako. Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao; ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo. Usimtende kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto. Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.”

 

Mungu wa kweli, Mungu mwenyezi aliyeziumba mbingu na nchi Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo, alikuwa amewaokoa wana wa Israel kutoka utumwani Misri na kuwaleta katika inchi ya Mkanaani, Mungu alikuwa anataka wana wa Israel wafanikiwe kama anavyotaka wewe na mimi leo vile vile tufanikiwe, lakini Mungu aliwafundisha mojawapo ya njia ya mafanikio ni pamoja na kutenda yaliyo mema machoni pake ikiwa ni pamoja na kutokuwatoa wana wao na binti zao kafara au dhabihu kwa kuwaua na kuwateketeza kwa moto,  jambo hili Mungu alichukizwa nalo na ndilo ambalo watu walioishi Kanaani walikuwa wakiyafanya hayo na Mungu akachukizwa nao na kuwafutilia mbali.  Kwa hiyo kuwatoa wanadamu kama sadaka au dhabihu ni machukizo kwa Mungu. Lakini pia kukata viungo vya watu wenye u albino ni machukizo makuu.

 

2Wafalme 21:1-9 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli. Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia. Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana. Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha. Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele; wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa. Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.”

 

Inawezekana katika jamii yetu watoto hao wasiteketezwe kwa moto, lakini matendo yanayofanyika ya kuwaua kuwakata baadhi ya viungo kwaajili ya sababu za kishirikina yanafanana kwa kiasi kikubwa na matukio ambayo yameorodheshwa katika machukizo mabaya ambayo Mungu anachukizwa  nayo sana, Matendo ya jinsi hii yalikuwa yakifanywa na wakazi wa Kanaani na ndio mojawapo ya sababu zilizopelekea Mungu kuwaondoa na kuwakataza Israel wasifanye kwa mfano wa matendo hayo ambayo kwa Mungu ni dhambi wafalme na watu wengi sana walioishi Kanaani walitegemea kufanya machukizo hayo kwaajili ya kuabudu miungu na kwaajili ya ushirikina wakifikiri kuwa watabarikiwa kwa kufanya mambo hayo.

 

2wafalme 3:26-27 “Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.”

 

Walawi 18:21 “Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapitisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi BWANA.”

 

Watu wote na ibada yoyote ile inayohusisha kuwatoa watoto wa kike au wa kiume na kuwateketeza, au kwa kukata viungo vyao na kwa njia zozote za kishirikina ibada za namna hiyo ziko kinyume na mapenzi ya Mungu na wote wanaofanya hivyo hufanya hayo kwa mashetani au mapepo na wanasababisha laana badala ya Baraka, nchi inalaanika na kutiwa unajisi na kuichochea hasira ya Bwana na kujitia utumwani kwa hiyo badala ya kuleta mafanikio wanayodhani, wanajiletea laana na sio wao tu na nchi zima inatiwa laama kwa sababu hizo uko ulazima wa viongozi wa dini, na imani zote na viongozi wa kimila na kisiasa kwa sababu zozote zile na kwa nia moja kusimama sawasawa na neno la Mungu na kukemea vikali swala zima la mauaji ya Albino na matendo yote ya ushirikina na upigaji ramli na utazamaji wa nyakati mbaya ambayo kimsingi yote yamekemewa katika maandiko  na ndio sababu kubwa ya mauaji ya wenye u albino na kukatwa kwa viungo

 

Zaburi 106:37-42 “Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu. Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao. Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake. Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala. Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.”       

 

Albino hafai kwa dhabihu

Katika siku za miaka ya karibuni na hata majuzi hapa kumeibuka tena tabia za watu wenye mawazo ya kishirikina ambao wamekuwa wakiwaandama watu wenye ulemavu wa ngozi na kuwaua na kuwakata viungo vyao, kwa Imani za kishirikina wakifikiri kuwa wanaweza kujijengea umaarufu, kufanikisha biashara, kupata vyeo vya kisiasa na kutajirika au kujiletea mafanikio mbalimbali, lakini kama tulivyoona katika kipengele hapo juu, Dhabihu ya namna hiyo haipokelewi na Mungu aliye hai na ni dhabihu iliyo machukizo kwa Mungu, na Mungu mwenyezi amekataa kuwa yeye hapokei sadaka za aina hiyo, na hivyo maandiko yako wazi kuwa kazi hizo zinafanywa na washirikina, wachawi na wapiga ramli,  hata hivyo pia nataka kukazia wazi kuwa hata kama Mungu angelitaka sadaka za wanadamu, Mungu asingeliwatumia albino kwa dhabihu, kwa nini kwa sababu ualbino ni ulemavu wa ngozi na hivyo watu hao hawafai kwa dhabihu! Kama wasingelifaa kwa dhabihu kwa Mungu basi hawawezi kufaa kuwa dhabihu kwa miungu.

Ualbino ni changamoto ya kuzaliwa inayotokana na mvurugiko wa vinasaba vya kuzaliwa na kumfanya kiumbe anayezaliwa, kuzaliwa akiwa na changamoto ya ukosefu wa kemikali ya rangi ya ngozi ambayo kitaalamu inaitwa “Melanin” Kemikali hii ndiyo inayoamua kuwa mwili wa mwanadamu uwe na rangi gani katika ngozi, nywele na macho, kwa hiyo mtu mwenye ualbino kimsingi anakosa kirutubisho hicho na hivyo kumuweka katika mazingira yasiyo rafiki kwa jua, na hivyo kuweza kuandamwa na tatizo la saratani ya ngozi, Melanin pia ni kemikali inayohusika na kazi za uoni, na inapokosekana pia husababisha tatizo la uoni hafifu, ualbino hutokea kwa Waafrika, Wazungu, Waarabu na Waasia  na mara chache pia kwa baadhi ya wanyama. Neno Albino limetokana na neno la asili la kilatini Albus ambalo maana yake ni Nyeupe kwa hiyo watu hawa huwa na ngozi nyenye weupe usiokuwa wa kawaida, ualbino wenyewe sio ugonjwa lakini ni ulemavu wa ngozi, kwa hiyo kuna changamoto katika ngozi, nyele na macho inayowafanya wao wasiwe na ukamilifu kimaumbile, lakini wana akili, uwezo na hufanya kazi zao kama wanadamu wengine.  Kwa hiyo wao sio watu wenye ngozi nyeupe bali wao ni watu wenye ulemavu wa ngozi.

Kwa sababu ya ulemavu huu wao hawaingii katika kundi la wanyama au watu wanaotakiwa kutumika kwa dhabihu au kafara, Mwana kondoo wa kafara alitakiwa asiwe na maraka raka wala dosari ya aina yoyote ile nahii ilikuwa ikimzungumzia Yesu Kristo pekee ambaye alikuwa ni sadaka kamili isiyo na dhambi, Mwanakondoo wa sadaka ya dhabihu alikuwa na sifa zifuatazo ambazo kinabii zilimuhusu Yesu Kristo asiyekuwa na dhambi.

1.       Asiwe na Dosari -  Mwanakondoo wa Sadaka ya dhabihu alipaswa kuwa asiye na dosari wala doa la aina yoyote hii maana yake aliwakilisha ukamilifu na usafi ikiwakilisha picha ya Bwana Yesu pekee

 

Kutoka 12:5 “Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.”

 

2.       Alichaguliwa kwa uangalifu sana  kuhakikisha kuwa ni mkamilifu -  Mwankondoo wa sadaka ya dhabihu alichaguliwa kwa uangalifu mkubwa  ili kumpatia Mungu kitu kilicho bora, kumbuka sadaka hiyo pia ilitakiwa kuwa kondoo mume aliye mamilifu, hii maana yake ni kuwa haikutakiwa kuwa ya kike pia

                 

Walawi 1:10 “Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu.”

               

3.       Sadaka ya dhabihu haikupaswa kuwa na ulemavu – Ulemavu unawakilisha mapungufu ya kawaida ya kibinadamu na wanyama kwa hiyo mnyama wa dhabihu hakupaswa kuwa mwenye ulemavu hii maana yake ni kuwa chochote chenye ulemavu hakiwezi kufaa kuwa sadaka ya dhabihu kwa Mungu au miungu

 

Kumbukumbu 17:1Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.”

 

4.       Dhabihu ya Albino sio dhabihu kamilifu – Mungu alitoa agizo kwamba dhabihu zinapaswa kuwa kamilifu, bila dosari, dhabihu yoyote iliyokuwa na dosari ilikuwa ni machukizo kwa Mungu, ile tu mtu kuwa Albino yaani kuwa na ulemavu wa ngozi, na ile tu kuwa Mungu amekataza mwanadamu asitolewe dhabihu tayari kuwatoa wanadamu na zaidi sana wenye ualbino ni kumtolea Mungu au miungu dhabihu isiyofaa, Mungu alikataa dhabihu za wanyama waliokuwa na ulemavu, na alikataa kutumikiwa na makuhani waliokuwa na ulemavu na hii itupe picha ya kuwa mwanadamu mwenye ualbino ni marufuku kutolewa dhabihu na sio wao tu ushirikina ni marufuku, nahata mwanadamu wa kawaida ni marufuku kutolewa dhabihu na kuabudu miungu au kuabudu mizimu, au kufuata maelekezo ya waganga, au wachawi haya yote ni machukizo kwa Bwana Mungu wetu na ni kinyume na maelekezo yake na mwelekeo wa kidhabihu.

 

Malaki 1:8 “Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi.”    

 

5.       Dhabihu ya Albino ni dhabihu ya udhalimu -  Mungu anachukizwa sana na watu wanaotoa dhabihu ya udhalimu, unapomtoa mtu huyu mwenye haki ya kuishi, huku ukiwa umedhulumu maisha yake hiyo ni dhambi, umeua na amri ya Mungu imesema usiue kwa hiyo huwezi kupata Baraka kwa kudhulumu maisha ya mtu hiyo ni dhambi na ni machukizo kwa Mungu, ni dhambi kwa sababu ni ushetani, ni ushirikina, mganga aliyeagiza ana dhambi, yeye aliyeagizwa ana dhambi na wale wanaohusika katika kuitekeleza dhabihu ya aina hiyo wana dhambi kwa hiyo huwezi kupata mafanikio na badala yake unavuna laana, sadaka hiyo inakuwa ni sadaka ya wasio haki na ni sadaka isiyotokana na melekezo ya kiungu ni sadaka au dhabihu ya watu wenye nia mbaya na moja kwa moja inakataliwa na Mungu. Huo ni uchawi na ushirikina kinyume na mapenzi ya Mungu, Kanisa ni lazima lisimame kinyume na uovu huu ambao sio sifa ukasikika katika jamii.  

 

Mithali 21:27 “Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!

 

6.       Dhabihu ya Albino ni dhabihu batili  -  Dhabihu ya watu wenye ualbino ni dhabihu ambayo haikuwahi kuagizwa na Mungu wala miungu wala hata mashetani, kwa hiyo ni machukizo na ni batili, kwa hiyo Mungu anachukizwa nazo, wala hazifurahii, watu wanaofanya hayo watapata laana badala ya Baraka wanazozifikiria kuwa watazipata, sio tu wanajiletea laana kwa familia zao lakini pia wanajiletea laana kwa taifa lao.

 

Isaya 1:10-16 “Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;”

 

7.       Dhabihu ya kichawi au za watu wanaoabudu miungu mingi - Mungu anachukizwa na dhabihu zote za kishirikina zinazotolewa kwa miungu na ibada zote za kishirikina na sanamu zilizo kinyume na Imani ya kweli ibada hizo zote ni machukizo kwa Mungu

 

Yeremia 7:9-10 “Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?

 

Mungu hataki ibada zenye michanganyo, ibada zote za namna hii zinaitwa ibada za kishirikina, kimsingi watu wanaotoa sadaka hizo au dhabihu hizi mbaya wana dini zao ambazo zinaweza kuwa zinamtaja Mungu na wakati huo huo wanashiriki maswala ya uchawi na uchafu mkubwa unaohusisha kuwaua watu wa Mungu.

Kwa hiyo kimsingi kwanza wote tunafahamu kuwa Mungu hakubaliani na sadaka ya dhabihu ya kuwatoa wanadamu, lakini pili tunakubaliana kuwa Mungu hapokei sadaka yenye dosari, au yenye kasoro au isiyokamilika, au isiyofaa, au yenye dosari au ulemavu wa aina yoyote, kwa msingi huo hata kama wanadamu wangekuwa wanatolewa dhabihu kwa Mungu basi mtu mwenye u albino hafai kwa dhabihu, sio hivyo tu hata mtoa dhabihu hakupaswa kuwa na ulemavu wa aina yoyote ile katika nyakati za agano la kale kwa hiyo kama sheria ya Musa ingelikuwa inafanya kazi hata sasa basi mwenye ualboni hangeweza kufaa kuwa mtumishi wa Mungu au kuhani, Hapa lengo langu sio kuwabagua wenye ualbino lakini nataka kunyesha kimaandiko ni namna gani Albino wasingeliweza kufaa kwa kafara

Walawi 21: 17-21 “Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili, au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono, au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za BWANA kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.”               

Lengo langu hasa ni nini hapo, kwa kawaida miungu mingi na hata shetani ameigiza kila kitu kutoka kwa Mungu mwenyezi, kwa hiyo kama unavyoona tabia ya Mungu mwenyezi kutaka kitu kisicho na mawaa wala doa wala dosari na wala kisicho na kilema; Hali kadhalika miungu na mashetani pia hutaka au hutembea katika kanuni hizo hizo kwa sababu hiyo, kwa kuwa watu wenye ualbino ni wanadamu kamili lakini wana ulemavu wa ngozi, kwa mujibu wa torati hawafai kwa dhabihu, Maana yake ni nini? Wale wanaowaua na kuwakata viungo watu wenye ulemavu wa ngozi, wanafanya makosa makubwa sana kwa sababu hakuna ibada ya aina yao inayoweza kukubalika na miungu ya aina yoyote.

Lengo langu ni nini hapa watu wenye changamoto ya ualbino wanapaswa kuachwa, na kuwa watu huru wasitishiwe kwa sababu zozote zile kwa sababu hawafai kwa huo ushirikina, lakini wanafaa katika jamii, mchango wao katika jamii unahitajika, Mungu hakuwaumba wao wawe maalumu kwaajili ya dhabihu hapana, waganga wanaotaka viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni waongo na kamwe hawajui kabisa kanuni za utendaji wa maswala ya kiroho yawe ya Mungu au ya kienyeji, wenye kushiriki zoezi hili ni washirikina kamili na ni wachawi na wapiga ramli na ni watu wasioelimika na waliopitwa na wakati au wako nyuma sana, wanasababisha mashaka, na huzuni na kuwafanya watu hao wa waishi kwa hofu, na wazazi wao na jamii isiwe mahali salama ni jambo la kusikitisha ya kuwa mtu mwenye tatizo anaongezewa tatizo badala ya kuwafariji na kulia nao katika changamoto hii ya ukosefu wa melanin katika maisha yao.

Namuomba Mungu kuwa tiba ya kuweza kurejesha melanini katika jamii hii igunduliwe lakini pia watu wa maombezi, tumuombe Mungu ili aweze kuwaponya watu wenye changamoto hii, aidha mimba zote na  watu wote walio wajawazito waombewe na kuwekwa katika mikono ya Bwana na wazingatie kanuni zote za kiafya na kitabibu ili kuzuia uwezekano wa kuzaliwa kwa watu wenye ulemavu huu.

Imani yangu ni kuwa kama sababu zinaanza kueleweka hatutashindwa kupata majibu ya kushughulika na changamoto hii, naungana na wanajamii wote duniani, na Afrika na katika ukanda wetu kukemea na kusimama kinyume na matendo yote ya kijinga ikiwepo tendo hili la kuwatoa walemavu wa ngozi na kuwafanya dhabihu kwa miungu nalaani kitendo hiki na wote wanaojihusisha na matendo haya na naiombea serikali kuwa ifanikiwe kumkamata kila mtu aliye kwenye mnyororo wa matendo haya maovu katika jamii, matendo haya ukiacha ya kuwa yanamuudhi Mungu lakini ni ishara ya jamii jinga isiyoelimika wala kustaarabika yanaposikilizika  katika masikio yetu matukio kama haya hasa katika nyakati za karibu na chaguzi za serikali za mitaa na serikali kuu, Mungu atuepushe na kuwa na jamii na viongozi wanaoamini katika ushirikina na Mungu awanyime mamlaka zozote zile zinazopatikana kwa njia ya kishirikina na wananchi wasimchague mtu yeyote yule anayekisiwa kujihusisha na ushirikina kwani hawezi kutuletea maendeleo ya kweli wakati yeye yuko nyuma kimaendeleo!

Naelezea haya kwa uchungu mkubwa kwa sababu sitaki kuamini kuwa katika jamii zetu bado tunao watu wanaosadiki mambo ya kijinga na huku wengine wakiwa ni viongozi wa kidini!, Hebu tuwaache ndugu zetu, kaka zetu na dada zetu wenye ualbino wawe huru waishi kwa Amani na utulivu, tuwaache wapambane na hali zao badala ya kuwaongezea maumivu mengine, na kila kiongozi wa ngazi yoyote kuanzia ya familia ahakikishe ya kuwa matendo haya hayatajwi na wala kusikika katika taifa letu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufunguka macho na kuondoka katiia ujinga huu katika jina la Yesu Kristo amen.

Njia ya kweli ya Mafanikio

1.       Mungu kwanza – Mungu aliahidi katika neno lake ya kuwa tukimtanguliza yeye na kumuweka yeye mbele yeye atayafanikisha maisha yetu, hakuna mafanikio ya kweli nje ya Mungu, Mungu ndiye mwenye neema ya kutufanikisha, hivyo ni muhimu kwetu kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na hakli yake naye na mengine tutazidishiwa.

 

Zaburi 84:11 “Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.”

 

Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

 

Tunapomuweka Mungu mbele yeye hutupatia mahitaji yetu yote, na huu ni msingi mmojawapo muhimu wa mafanikio, Mungu ndiye anayetupa akili za kupata utajiri.

 

Kumbukumbu 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”

 

2.       Utii kwa maagizo ya Mungu – Mafanikio ya kweli yana uhusiano mkubwa sana na utii kwa amri za Mungu au maagizo yake, tunapoyatii maagizo yake yeye hutuongoza na kutuletea Baraka kubwa ambazo zinatuletea mafanikio

Yoahua 1: 8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

 

1Wafalme 2:1-3 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”  

 

3.       Mwamini Mungu, mtumainie yeye kwa moyo wako wote  – unapoamini katika Mungu kwa moyo wako wote na kudumisha uhusiano wake nay eye anakuwa msaada mkubwa katika kila aina ya dhuruba tunayokutana nayo

 

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

 

Warumi 8:32 “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?

 

4.       Kufanya kazi kwa bidii   - Maandiko yanatufundisha umuhimu wa kufanya kazi kwa bidi, na kwa uaminifu, Mafanikio hayaji kwa uvivu, bali ka juhudi na uaminifu na kujituma tunapofanya hivyo Mungu yeye hubariki kazi za mikono yetu hii ndio kanuni mojawapo muhimu ya kibiblia ya mafanikio na kwa uvumilivu

 

Mithali 10:4 “Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.”

               

Kumbukumbu 28:11- 12 “Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa. Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.”

 

5.       Ni heri kutoa kuliko kupokea -  Matendo ya ukarimu kwa wengine na utoaji ni mojawapo ya njia inayofungua milango ya Baraka, wanadamu wote bila kujali Imani zao wanapoishi katiika kanuni hii wanabarikiwa, maandiko yanashuhudia kwamba ni vema kutoa na kutoa kwetu kunafungua mlango wa Baraka na mafanikio makubwa sana

 

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”

 

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

 

Matendo 10:1-4 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”

 

Tunapoishi maisha ya ukarimu na kujitoa kwa watu wenye mahitaji tunamkopesha Mungu na kutuweka katika njia ya Baraka na mafanikio ya aina mbalimbali kutoka kwa Mungu

 

6.       Maombi na kudumisha uhusiano na Mungu – Kwa kuwa Mungu ndiye chanzo cha mafanikio ya kweli ni vema kwetu kuhakikisha ya kuwa tunadumisha uhusiano  wetu nay eye,  kwa kusali na kuomba, huku tukikumbuka ya kuwa wakati wote Mungu anatuwazia mema

 

Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”

Hitimisho:

Ndugu zangu, Mafanikio ya kweli nay a kudumu yanapatikana kwa kuutafuta uso wa Mungu na kumpa yeye kipaumbele, kutii amri zake na kwa neema yake tukimtumaini yeye kwa moyo wetu wote na kufanya kazi kwa bidi, na kwa uaminifu, na kuonyesha matendo ya ukarimu kwa wengine Mungu atatupa mafanikio makubwa sana, Mafanikio ya kishirikina sio ya kudumu, na hayawezi kukupa Amani ya kweli, inasikitisha sana kuona au kusikia kuwa bado kuna watu wana akili za kizamani za wakati wa ujinga kwa kutoa sadaka ya viungo vya binadamu na zaidi sana wenye tatizo la Albinism kwa kuwaua na kuchukua baadhi ya viungo vyao hiyo haiwezi kutupa mafanikio ya kweli nay a kudumu, Mungu ametupa njia iliyo bora zaidi ni sadaka moja tu ya Mwanadamu aliyemwaga damu yake Msalabani ilitolewa kwa niaba yatu na hiyo tu ndiyominayokubaliwa na Mungu kwaajili ya mafanikio yote ya kimwili na kiroho kwa wanadamu wote ulimwenguni na sio vinginevyo:-

Isaya 53:4-6 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.”

2Wakorintho 8:7-9 “Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”  
           

Jamii inapaswa kuelimisha watu na kukemea swala hilo vikali, Watu wenye ulemavu huu wa ngozi wamekuwa wakinyanyasika kwa sababu ya misimamo inayochangiwa na wagaganga wa kienyeji wenye madai kuwa uchawi unaohusisha viungo vya Albino una nguvu sana Imani hii potofu imechangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya watu hao, n ahata kuchimbwa kwa makaburi yao na kukatwa viungo vyao, dhana hii inajitokeza zaidi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza, aidha watu wenye ualbino wananyanyasika wakati mwingine wakifikiriwa kuwa ni watu wasiotakiwa katika familia au jamii Ndugu zangu ni lazima tubadilike, utafiti mdogo unaonyesha kuwa Tanzania huenda labda ndio inchi inayoongoza kwa kuwa na albino wengi duniani, Hata hivyo wakati mwingine pia albino wametekwa na kusafirishwa mpaka katika inchi jirani, au kuuawa na wahusika kukimbilia katika inchi za jirani, ni aibu kwa Taifa lenye kuehsimika kama Tanzania kuwa na sifa ya mambo ya kijinga hivi, injili ihubiriwe na dini na imani za kweli zikifishwe katika maeneo yote ambayo yanazingirwa na imani hizi potofu. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!      

Hakuna maoni: