Marko 4:35-41 “Siku ile kulipokuwa jioni,
akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile
alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea
dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye
mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia,
Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia
bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani
bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na
bahari humtii?”
Utangulizi:
Kaka zangu, Dada zangu:- Ni
muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuliamini kila neno, lililotoka katika kinywa
cha Mungu bila kutia shaka yoyote hata kidogo! Wakati mwingine ni ngumu
kufahamu kila hali inayokutokea katika maisha yako, kwanini jambo Fulani
limechelewa, kwanini ulikutana na mwisho mbaya? Kwanini mligombana na ndugu
yule, kwanini mtu yule alikufanyia ubaya? Kwanini maisha ni kama yamerudi
nyuma, ni kama ulikuwa mbali na ni kama umerudishwa nyuma hatua mbili, Wakati
mwingine Mungu hatuchukui katika kile tunachokitamani moja kwa moja, na wakati
mwingine ili kuifikia ile hatima inayokusudiwa na Mungu, basi ni lazima, upitie
katika changamoto kadhaa wa kadhaa. Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa mambo
yote hutenda kazi kwa kusudi la kutimiza mapenzi yake, hata hivyo yeye
anapotamka haijalishi ni hali gani inajitokeza kati kati lakini neno la Mungu litasimama
vile vile bila kujali mazingira, kwani Mungu hutumia mambo yote katika
kuwapatia watu wake mema!
Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika
mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili,
hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia
haki, hao akawatukuza.”
Wakati mambo yanapokuwa mazuri
huwa tunafurahia, na tunaweza kukubali
na kumuona Mungu ni mwema lakini mambo yanapoenda mrama tunaweza
kuchanganyikiwa na tunasahau kuwa Mungu ndiye bwana mipango mkubwa, wakati mwingine
anaweza kukurejesha nyuma, ili kwamba akupeleke mbele zaidi, anaweza kufunga
milango na kutulazimisha kubadilika, au kubadilisha mitazamo yetu, inawezekana
tulijisikia poa pale tulipokuwa, lakini Mungu hakujisikia poa, kwa sababu
anakitu kikubwa zaidi kwaajili yako na yangu, ana kitu ambacho akili zetu
haziwezi kuelewa, Leo tutachukua muda kuchambua kwa kina na mapana na marefu Marko 4:35-41 chini ya kichwa “Natuvuke mpaka Ng’ambo” kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
1.
Nguvu
ya maneno ya Yesu.
2.
Natuvuke
mpaka ng’ambo!
3.
Hamna
Imani bado?
Nguvu ya maneno ya Yesu.
Marko 4:35-39 “Siku ile kulipokuwa jioni,
akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile
alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea
dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye
mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia,
Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia
bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.”
Mojawapo ya jambo la Msingi
tunalopaswa kufahamu ni kukubali ya kwamba maneno ya Bwana wetu Yesu yana nguvu
ya ajabu sana kuliko tunavyoweza kufikiri, Yesu katika kifungu hiki anataka
tuamini katika neno lake, na kujua ya kuwa akiagiza kitu au akisema kitu ni
lazima kitatimia kama kilivyo bila kujali kuwa kutatokea nini mbele ya agizo
lake au neno lake, Neno la Kristo likishatamkwa limetamkwa, neno lake linauwezo
wa kugeuza machafuko kuwa Amani, kwa amri nyepesi tu Nyamaza na utulie, neno lake lina mamlaka ya kiungu,
inayothibitisha kuwa yeye hakuwa tu Mwalimu wa kawaida bali alikuwa na mamlaka
na amri, kila mtu aliyemsikiliza Yesu alikiri kuwa maneno yake na mafundisho
yake hayakuwa ya kawaida bali yalijaa uwezo, yalijaa mamlaka, na yalikuwa amri,
au sheria!
Luka 4:32 “wakashangaa mno kwa mafundisho
yake, kwa kuwa neno lake lilikuwa na uwezo.”
Marko 1:21-22” Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato
akaingia katika sinagogi, akafundisha.Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa
maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.”
Maneno hayo Uwezo, na Amri katika
lugha ya kiyunani linatumika neno “Exousia”
ambalo kwa kiingereza linaweza kuwa na maana ya Power, Authority, Right, Liberty, Jurisdiction
and strength ambalo linaweza
kuelezewa kama sense of ability, force capacity, hii inaonyesha kuwa maneno ya Yesu yalikuwa
na nguvu, yalionyesha ushawishi, uweza wa kuhukumu kimahakama, nguvu ya
maamuzi, nguvu ya kutenda, nguvu ya kuleta matokeo, Nguvu ya kisheria, amri ya kijeshi, matokeo ya
kiserekali, hii maana yake ni nini Yesu anapotamka jambo, ni kama hakimu
anapokuwa ametamka hukumu, na kinachofuata Polisi hupiga saluti na kumchukua
mtuhumiwa na kumpeleka magereza, yaani kwa lugha nyingine mamlaka yake
inapotamka mara moja kinachotokea ni utekelezaji halali wa Amri halali ya neno
hilo, yaani amri yake ni ya kifalme anaposema kile kilichosemwa ni amri, ni
sheria, ni mamlaka halali imetamka na hivyo ni lazima kitekelezwe kile kilichotamkwa!
Yesu alikuwa anataka wanafunzi wake wafikie ngazi ya kuamini ya kuwa
atakachokisema kitatimia au ni lazima kitimizwe bila kujali ni mazingira gani yanajitokeza
mbele ya neno lake na mfano mkubwa wa kutufundisha hilo ni amri yake kwa wanafunzi
wake pale alipowaagiza kuwa Na tuvuke mpaka ng’ambo.
Na tuvuke mpaka Ng’ambo
Marko 4:35-38 “Siku ile kulipokuwa jioni,
akawaambia, Na tuvuke mpaka ng'ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile
alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea
dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye
mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia,
Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
Yesu alipoamuru wanafunzi wake na
kuwaambia na tuvuke mpaka Ng’ambo na kisha yeye mwenyewe akapumzika na kulala,
kisha dhuruba zikaanza kukipiga chombo na wanafunzi wake wakaanza kuhangaika,
kulikuwa na kitu cha muhimu cha kuwafunza na kutufunza ya kwamba je tunasadiki
maneno yake ? na je tunaweza kuyasadiki
maneno yake hata tukiwa katika taabu? Yeye amesema na tuvuke mpaka ng’ambo, amri ya
mfalme ni sheria tayari mazingira yote yanaratibiwa kuhakikisha ya kuwa neno
lake linatimizwa, kumbuka chochote anachokuambia Yesu kitakuwa vile vile kama
alivyosema na sio vinginevyo.
Marko 11:13-23 “Akaona kwa mbali mtini
wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona
kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata
milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu,
naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na
kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao
wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha,
akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa
yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na
waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa,
kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni
alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka
toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini
ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu,
akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu,
Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba
hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.”
Yesu aliwahi kuuambia mtini,
tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako, na katika macho ya nyama mtini
ule ulionekana ni kama bado uko vile vile, Lakini Kristo hakuwa na shaka,
asubuhi yake Petro aliuona ule mtini umenyauka toka shinani, na alimkumbusha
Yesu maneno yake, Yesu aliwaonyesha ya kuwa sio maneno yake tu hata na ya kwetu
tukiyatamka pasipo shaka huku tukimuamini Mungu yatatuklioa vile vile.
Yohana 11:23-26 “Yesu akamwambia, Ndugu
yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku
ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye
mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa
kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?”
Yesu aliwahi kumwambia Martha kwa
habari ya kaka yake Lazaro ambaye alikuwa amekufa na kuzikwa alimwambia ndugu
yako atafufuka. Martha alianza kujieleza kwa mambo mengi, najua atafufuka
katika ufufuo siku ya mwisho na kadhalika na kadhalika, mpaka wakati huu Martha
alikuwa hajajua mamlaka ya neno la Yesu, Yesu anapotamka neno ni wajibu wetu
kusadiki bila kujali ya kuwa kuna mazingira gani
Yesu akiisha kutamka neno hata
kama mazingira yanaonekana kukataa, au kutokukubali au kuonyesha matumaini hiyo
haisaidii kulifanya neno lake lisiwe Dhahiri, changamoto zozote zitakazojitiokeza
zinasaidia kutusafirisha kutufikisha katika kulitimiza neno la Bwana,
Changamoto haziko hapo kutuzuia, lakini changamoto ziko pale kutupeleka katika kiwango
cha juuu zaidi lakini je tunaweza
kumuamini yeye wakati mambo yanapoonekana kwenda ndivyo sivyo? Je tunaweza kuwa
na Amani wakati mambo yanapoonekana kuwa sio? Lazima tuamini katika kile alichokizungumza
kumbuka yeye alisema na tuvuke mpaka
ng’ambo hii maana yake ni kuwa tutafika nga’mbo hata bila kujali ni nini
kinajitokeza katikati ya maneno ya Bwana Yesu ni kwa sababu ya tukio hili Yesu
aliwakemea kuwa hawajaamini Bado kwa sababu wao walipoona changamoto waliogopa
na kuanza kulia na kumuona mwalimu kama mtu asiyejali dhuruba walizokuwa
wakizipitia lakini kimsingi Yesu alikuwa na utulivu mkubwa sana kwa sababu
aliamini katika neno lake na kuwa hakuna jambo lolote linaweza kusimama kinyume
na neno lake natuvuke mpaka ng’ambo.
Hamna Imani bado?
Marko 4:39-41 “Akaamka, akaukemea upepo,
akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.
Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu,
wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii? ”
Yesu anaweza kutuagiza tuelekee
mahali ambapo kuna changamoto, maandiko mengine yanasema akawashurutisha na
tuvuke mpaka ngambo, ni wazi kuwa pale walipokuwepo walifurahia sana Baraka za Mungu na hawakutaka kuondoka,
Palitendeka miujiza mingi, hata hivyo walihitaji kupumzika, na vilevioe
kuwafikiwa watu wengine, hivyo aliwalazimisha wavuke Ng’ambo kwanini lakini ? Mungu hawezi kutulazimisha hivi hivi tu,
anaweza kukuondoa katika eneo ambalo unakula raha na akataka uelekee eneo
lingine lenye Baraka zake kubwa zaidi, wakati mwingine ni ngumu kuona na
kufurahia maagizo ya kiungu na kuyaamini lakini Mungu hawezi kukulazimisha
uende mahali ambapo, anajua utakutana na dhuruba ambazo zitayaangamiza maisha
yetu, sababu kubwa ya kukutuma kwenye dhoruba ni kwa sababu anajua utatoboa na
iko njia iliyonyooka, yeye ndiye anayefanya njia, na ni yeye ndiye
anayeyaongoza maisha yako na yangu hakuna sababu ya kujitahidi kuyaokoa maisha
yetu, hakuna sababu ya kuogopa, wala kuhofia kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa
Yesu, yeye anajua yupo na anajua kuwa ametamka neno lake na itakuwa salama anajua pia anauwezo wa kunyamazisha kila aina
ya dhoruba inayoyakabili maisha yako, Basi unachopaswa kukifanya wewe ni
kuamini katika kile ambacho Mungu amekisema, upepo uliwaleta mahali pazuri
zaidi ya kule jangwani walikokuweko
Yesu anapozungumza maneno yake
hayawi bure yanatimiza makusudi yake makuu na hakuna kinachoweza kuzuia neno
lake katika mazingira yoyote
Mawimbi yanapokuja yanajaribu tu uwezo wetu wa kuamini,
yanapima kwamba tunamuelewa Yesu kwa kiwango gani na tunayachukulia vipi maneno
yake, Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kuamini katika maneno yake na
mamlaka kubwa aliyokuwa nayo, Changamoto ni kipimo kuwa tunamsadiki yeye kwa
kiwango gani, na sio hivyo tu changamoto hizo zinamfunua Yesu pia kwa undani
zaidi, wanafunzi walikuwa wanamuona Yesu ni wa kawaida tu, lakini sasa sio tu
aliwakema kwa kutokuamini kwao lakini alijifunua kwao katika kiwango cha juu
zaidi, yeye aliukemea upepo na bahari na kuziamuru kunyamaza na kutulia na
wanafunzi waliacha kuogopa hilo na sasa walimuogopa Yesu na kujiuliza kuwa huyu
ni mtu wa namna gani hata bahari na uepo
unamtii ?
Hitimisho
Yesu aliwahoji wanafunzi wake
Mbona mmekuwa waoga hamna Imani bado?
Nini maana yake muitikio wetu kwa neno la Kristo unapaswa kuwa usiojawa
shaka na hofu wala kujali mazingira
hatuna budi kuendelea kuamini nguvu yake mamlaka yake na neno lake,
tujue ya kuwa Mungu wakati wote ni mwema na kila anakotupeleka hutupeleka kwa
kusudi lake, anaposema kitu ni lazima
tutii, lakini sio hivyo Yesu alikuwepo pale, wanafunzi wake walipaswa kuamini
pia katika uwepo wake hii inatukumbusha
kuwa na Amani tunapokuwa katika uwepo wa Mungu
yeye yuko kwaajili yetu, neno lake sio tu linaleta utulivu wakati wa
dhuruba lakini pia linatuhakikishia Amani ya maisha yetu, hivyo wajibu wetu kwa
neno lake ni kuamini, kutii na kuwa na Amani katika uwepo wake.
Na Rev.Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni