Jumanne, 21 Juni 2016

Mti wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu!



Waamuzi 9:8 – 13. Biblia inasema hivi:- 

“8. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. 9. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 10. Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. 11. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? 12. Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. 13. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?” 

Leo tutachukua muda kutafakari kwa kina na upana na marefu kuhusu mti wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu, Ninazungumza jambo muhimu sana litakaloifaa jamii ya leo ambayo imejaa watu wanaoteseka kwa kukosa maarifa, kama utafuatilia somo hili kwa moyo maisha yako yatabadilika na utakuwa na furaha maishani mwako, Leo nataka kuzungumzia kuhuzu mti wa Mzeituni (Olive Tree) lakini kwanza nataka ufahamu jambo hili

Mwanzo kabisa Mungu alipouumba ulimwengu alitoa zawadi ya mimea na miche pamoja na miti kwa wanadamu kama chakula na zawadi soma Mwanzo 1:29 “ biblia inasema 

29. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; 30. na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. 
  
Miche na miti katika biblia ya kiingereza huitwa Herbs tuangalie Biblia ya Kiingereza tafasiri ya King James Bible inasema:-

"And God said, Behold, I have given you every herb bearing seed, which is upon the face of all the earth, and every tree, in the which is the fruit of a tree yielding seed; to you it shall be foe meal"

Ni wazi kuwa miti na mimea ndio chakula cha kwanza walichopewa wanadamu kabla ya kuongezewa nyama katika Mwanzo 9:3 baada ya gharika wakati wa Nuhu, Moja ya mti muhimu sana unaotajwa katika Biblia ni mti wa Mzeituni na tunda la zeituni na mafuta ya mzeituni huu ni moja ya mti muhimu sana katika uumbaji wa Mungu, Wayahudi na waarabu na wakristo wa zamani sana walifahamu sana umuhimu wa mmea wa mzeituni ukilinganisha na nyakati tulizonazo katika kizazi hiki, ni kwasababu hiyo leo Mkuu wa wajenzi ninataka kuchukua muda kueleza maswala kadhaa muhimu kuhusu mti huu wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu.

Mmea wa Mzeituni ni mmea unaomea kwa wingi sana katika nchi ya Israel, Hata leo, mashamba ya mizeituni yametapakaa kutoka sehemu za chini ya Mlima Hermoni upande wa kaskazini hadi viunga vya Beersheba upande wa kusini. Mizeituni bado inapatikana kwenye pwani ya Uwanda wa Sharoni, vilima vyenye mawemawe vya Samaria, na mabonde yenye rutuba ya Galilaya lakini pia ni mmea unaostawi na kuzalishwa kwa wingi katika inchi ya Hispania (Spain) Nchi hii kwa sasa ndio inayoongoza kwa uzalishaji wa Mafuta ya Mzeituni na sehemu nyingine nyingi duniani, Mungu ameupa mmea huu uwezo wa ajabu sana kama tutakavyoweza kuona mbeleni lakini pia mmea huu kwa tabia zake ni mmea ambao hauwezi kuharibiwa,Unapoukata mzeituni unauwezo wa kutoa machipukizi mapya na ukaendelea kuwepo mara moja, Matunda yake yanauwezo wa kutoa au kuzalisha mafuta mengi ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupikia, kujipaka, kuwashia taa, na kutibu wanadamu, katika shughuli za Ibada mmea huu ni mmea wa kikuhani kwa vile unatumika kutangaza rehema za Mungu na unatumiwa katika ishara ya amani, kuweka wakfu viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini yaani Wafalme, Makuhani na manabii. Aidha mti huu mafuta yake na matawi yake hutumika katika kufukuza Mapepo (Mashetani na Majini) kwa jina la Yesu.

Katika kuwatia Moyo Israel katika safari yao ya kwenda Kanaani moja ya vitu vyenye mvuto sana kwa wana wa Israel ambavyo Mungu alimtumia Musa kuvitaja ilikuwa ni pamoja na Mizeituni yenye mafuta.  Kumbukumbu 8:7-8 biblia inasema 

7. Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; 8. nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;

·         Sifa za Mzeituni
·         Historia ya Kibiblia kuhusu Mzeituni
·         Matumizi ya Mzeituni

Sifa za Mzeituni.

Kwa kawaida Mzeituni ni mti usio na Mvuto ukiuona kwa mara ya kwanza. Si mrefu kama mierezi fulani yenye kuvutia ya Lebanoni. Mbao zake hazina thamani kama mbao za mberoshi, na maua yake hayavutii kama maua ya mlozi ambayo ilitumika kujengea Nyumba katika Israel kama maandiko yasemavyo katika wimbo ulio bora 

Wimbo Ulio bora 1:17 Biblia inasema hivi:- “Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi”. Na Amosi 2:9 9. “Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini”.

Sehemu muhimu zaidi ya mzeituni haionekani—iko chini ya ardhi. Mizizi yake mingi, ambayo hufikia kina cha meta sita chini ya ardhi na kwenda hata mbali zaidi kuelekea upande-upande, ndiyo hasa hufanya mti huo uzae sana na kustahimili hali ngumu.

Mizizi hiyo huiwezesha mizeituni kwenye vilima vyenye mawemawe istahimili ukame wakati ambapo miti iliyo kwenye bonde imekwisha kauka kwa kukosa maji. Mizizi huiwezesha kuendelea kuzaa zeituni kwa karne nyingi, ingawa huenda shina lisilovutia likaonekana kuwa lafaa tu kwa kuni. Mti huo usiovutia huhitaji tu nafasi ya kukua na udongo wenye hewa, bila magugu au mimea mingine inayoweza kuwa na wadudu waharibifu. Mahitaji hayo sahili yakitimizwa, mti mmoja utatoa lita 57 za mafuta kila mwaka.

Historia ya Kibiblia kuhusu Mzeituni.

Kibiblia Mzeituni unatajwa kwa mara ya kwanza katika Kitabu cha Mwanzo 8:6-12 “6. Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 7. akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. 8. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 9. bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. 10. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, 11. njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. 12. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.”

Mzeituni unatajwa kama mti ulioashiria amani baada ya Hasira za Mungu alipoangamiza dunia kwa maji, Nuhu alituma ndege Kunguru ambaye alizurura bila kutoa ripoti na njiwa ambaye alirejea na kijitawi cha jani la mzeituni Tangu wakati huu mzeituni ulipata umaarufu mkubwa sana na kitendo cha njiwa kurudi na Jani bichi la Mzeituni kinywani mwake kuliashiria taarifa ya amani kwa Nuhu na familia yake.

Alama ya “V” ya vidole inayotumika sehemu nyingi sana Duniani ni matokeo ya njiwa huyu aliyekuja na jani la mzeituni katika safina, aidha matumizi ya tawi la mzeituni kama alama ya AMANI/shalom/salaam, yalitumika sana na watu wa Magharibi Karne tano hivi kabla ya Kristo, Wayunani wa kale waliutumia mti huu, kama alama ya uzao na masimulizi na historia zinaonyesha pia waliutumia kufukuzia pepo wachafu, kwa jina la mungu aliyejulikana kama Eirene au Irene ambayo maana yake ni Shalom/Salaam au amani, wapagani wa Kirumi pia walitumia matawi ya Mzeituni kumaanisha mungu mke wa amani ambaye alijulikana kama PAX na katika Coins za zamani za Kirumi iliwekwa nyuma ya fedha maana hizi hazitofautiani sana na maana ya asili iliyotumiwa na waandishi wa Biblia.


Fedha ya zamani sana (Coin) ya Kirumi ikiwa na tawi la Mzeituni

Mara nyingi waandishi wa Biblia walitumia mzeituni kama mfano. Sehemu mbalimbali za mzeituni zilitumika kufananisha rehema ya Mungu, ahadi ya ufufuo, na maisha ya familia yenye furaha. Kuuchunguza mzeituni kwa makini kutatusaidia kuelewa marejeo hayo ya Kimaandiko na kutafanya tuuthamini sana mti huu wa pekee ambao pamoja na uumbaji mwingine wote, ni moja ya mti wenye matunda unaofanya kazi ya kumsifu Mungu Zaburi 148:7,9.

Matumizi ya Mzeituni na Mafuta ya Mzeituni.

Bila shaka, zeituni zilipendwa sana na Waisraeli kwa sababu ya mafuta yake yenye thamani. Walitumia katika nyumba zao taa zenye tambi zilizotumia mafuta ya zeituni. Pia Mungu aliagiza wana wa Israel kuleta mafuta ya mzeituni kwaajili ya Taa yenye vinara saba iliyopaswa kuwaka Daima katika nyumba ya Mungu.


Taa yenye vinara Saba iliwaka katika nyumba ya Bwana Daima ikitumia Mafuta ya Mzeituni

Mambo ya walawi 24:2 “1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2. Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 3. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.”

Mafuta ya zeituni yalikuwa muhimu katika upishi. Yalikinga ngozi dhidi ya miali ya jua, na Waisraeli waliyatumia kutengenezea sabuni. Mazao muhimu ya nchi yalikuwa nafaka, divai, na zeituni. Hivyo, ungekuwa msiba mkubwa kwa familia ya Waisraeli mizeituni ikikosa kuzaa.

Kumbukumbu la Torati 7:13 Biblia inasema. “naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.” Kubarikiwa kwa Divai na Mafuta yanayotajwa hapo ni Mafuta ya Mzeituni Habakuki 3:17 Ilikuwa ni laana nzito ni adhabu kama Bwana ataipiga nchi kiasi cha kufikia Mzeituni kuzaa kwa shida “Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;”
 
Hata hivyo, kwa kawaida mafuta ya zeituni yalikuwa mengi. Yaelekea kwamba Musa aliliita Bara Lililoahidiwa ‘nchi ya zeituni’ kwa sababu mizeituni ilipandwa kwa wingi sana katika eneo hilo. Mtaalamu wa mambo ya asili, H. B. Tristram, wa karne ya 19 aliutaja mzeituni kuwa “mti wa kawaida wa nchi ya Kanaani yaani Israel.” Kwa sababu ya thamani yake na wingi wake, mafuta ya zeituni yalitumika katika eneo lote la Mediterania yakiwa kama fedha ya kimataifa. Yesu Kristo mwenyewe alitaja deni ambalo lilikadiriwa kuwa “vipimo mia vya bathi vya mafuta ya mzeituni.” Luka 16:5-6 “5.Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? 6. Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini”.

“Baraka kuu zililinganishwa Kama Miche ya Mizeituni”

Mzeituni wenye mafaa ni mfano ufaao wa baraka za Mungu. Mtu anayemcha Mungu angethawabishwaje? “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako,” mtunga-zaburi akaimba. “Wanao kama miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako.” Zaburi128:3Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako”.“Miche ya mizeituni” ni nini, na kwa nini mtunga-zaburi anailinganisha na wana?

Mzeituni ni wa pekee kwa kuwa machipukizi mapya huchipuka daima kutoka kwenye shina lake. Wakati shina kuu liachapo kuzaa kama zamani kwa sababu ya uzee, wakulima wanaweza kuacha miche au machipukizi mapya yakue na kuwa sehemu muhimu ya mti huo. Baada ya muda, mti wa awali utazungukwa na mashina machanga matatu au manne yenye nguvu, kama wana wanaoizunguka meza. Miche hiyo inatumia mzizi uleule, nayo hutoa mazao mazuri ya zeituni.
Hali hiyo ya mzeituni ni mfano ufaao wa jinsi imani ya wana na binti iwezavyo kuwa thabiti kwa sababu ya mizizi ya kiroho yenye nguvu ya wazazi wao. Watoto wakuapo, wao vilevile huzaa matunda na kuwategemeza wazazi wao, ambao hufurahi kuona watoto wao wakimtumikia Mungu pamoja nao. Mithali 15:20
 
“Mzeituni Unafundisha kuwa Yako Matumaini ”

Baba mzee-mzee anayemtumikia Mungu hupendezwa na watoto wake wenye kumcha Mungu. Lakini watoto haohao huomboleza wakati hatimaye baba yao ‘anapoenda njia ya ulimwengu wote.’ (1Wafalme 2:2). Ili kutusaidia kuvumilia msiba kama huo wa familia, Biblia hutuhakikishia kwamba kutakuwa na ufufuo. Yohana 5:28-29, 11:25

Aubu, aliyekuwa baba ya watoto wengi, alifahamu vizuri kwamba maisha ya mwanadamu ni mafupi. Aliyalinganisha na maua ambayo hunyauka upesi.  (Ayubu 1:2, 14:1,2). Ayubu alitamani sana kufa ili aepuke maumivu, akiliona kaburi kuwa mahali pa kujificha ambapo angeweza kutoka. “Mtu akifa, je! atakuwa hai tena?” Ayubu akauliza. Kisha kwa uhakika akajibu: “Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie. Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.”Ayubu 14:13-15

Ayubu alionyeshaje imani kwamba Mungu angemwita kutoka kaburini? Kwa kutumia mti ambao kutokana na jinsi anavyoufafanua, yaelekea ni mzeituni. “Yako matumaini ya mti,” Yobu akasema. “Ya kuwa ukikatwa utachipuka tena.” Ayubu 14:7 Mzeituni unaweza kukatwa, lakini kufanya hivyo hakutauharibu. Utakufa tu uking’olewa. Mizizi isipong’olewa, huo mti utachipuka tena ukiwa na nguvu mpya.

Hata ikiwa ukame wa muda mrefu unanyaukisha mzeituni wa zamani, shina lililonyauka laweza kuchipuka tena. “Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, na shina lake kufa katika udongo; lakini kwa harufu ya maji utachipuka, na kutoa matawi kama mche.” Ayubu 14:8-9 Ayubu aliishi katika nchi kavu na yenye vumbi ambako yaelekea aliona mashina mengi ya mizeituni iliyozeeka ambayo yalionekana yamenyauka na bila uhai. Hata hivyo, mvua iliponyesha mti huo “mfu” ulichipuka tena na mizizi yake kutoa shina jipya kana kwamba ni “mche.” Uwezo huo wa kipekee wa kuchipuka tena ulifanya mkulima mmoja wa bustani wa Tunisia aseme: “Kwa kweli mizeituni haiwezi kufa.”

Kama vile mkulima anavyotamani kuona mizeituni yake iliyonyauka ikichipuka tena, ndivyo Mungu anavyotamani kufufua watumishi wake waaminifu. Anangojea kwa hamu wakati ambapo watu waaminifu kama Abrahamu na Sara, Isaka na Rebeka, na wengine wengi watafufuliwa. Mathayo 22:31-32 Itakuwa ajabu kama nini kuwakaribisha wafu na kuwaona wakiishi tena maisha kamili yenye manufaa!

Mzeituni wa Mfano
Sifa ya Mungu ya kutobagua na pia uandalizi wake wa ufufuo hudhihirisha rehema yake. Mtume Paulo alitumia mzeituni kuonyesha jinsi ambavyo Yehova huwarehemu watu bila kujali rangi au malezi yao. Kwa karne nyingi Wayahudi walijivunia kuwa wachaguliwa wa Mungu, “uzao wa Abrahamu.” Yohana 8:33, Luka 3:8
 
Haikuwa lazima uwe mzaliwa wa taifa la Kiyahudi ili kupata kibali cha Mungu. Hata hivyo, wanafunzi wote wa kwanza wa Yesu walikuwa Wayahudi, na walikuwa na pendeleo la kuwa wanadamu wa kwanza kuteuliwa na Mungu kufanyiza mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa Mwanzo 22:18 Wagalatia 3:29. Paulo aliwalinganisha wanafunzi hao Wayahudi na matawi ya mzeituni wa mfano.



Wengi wa Wayahudi wa asili walimkataa Yesu, wakijinyima pendeleo la kuwa washiriki wa “kundi dogo,” au “Israeli wa Mungu.” Luka 12:32: Wagalatia 6:16 Hivyo wakawa kama matawi ya mzeituni wa mfano yaliyokatwa. Ni nani wangechukua mahali pao? Mwaka wa 36 Baada ya Kristo., wasio Wayahudi walichaguliwa kuwa sehemu ya mbegu ya Abrahamu. Ilikuwa kana kwamba Yehova alipandikiza matawi ya mzeituni-mwitu kwenye mzeituni wa bustani. Wale ambao wangefanyiza mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa wangetia ndani watu wa mataifa. Wakristo wasio Wayahudi sasa wangeweza kuwa ‘washiriki wa mzizi wa unono wa mzeituni.’Warumi 11:17

Lingekuwa jambo lisilowazika na lililo “kinyume cha asili” kwa mkulima kupandikiza tawi la mzeituni-mwitu kwenye mzeituni wa bustani.  Warumi 11:24 “Pandikiza mti mzuri kwenye mti wa mwituni, na, kama vile Waarabu wasemavyo, ule mzuri utashinda ule wa mwituni,” chaeleza kitabu The Land and the Book, “lakini huwezi kupandikiza mti wa mwituni kwa mti mzuri ukafanikiwe.” Wakristo Wayahudi hali kadhalika walishangaa wakati ambapo Yehova ‘kwa mara ya kwanza alielekeza uangalifu wake kwa mataifa ili achukue kutoka kwayo watu kwa ajili ya jina lake.’ Matendo 10:44-48, 15:14 Hata hivyo, hiyo ilikuwa ishara ya wazi kwamba kutimizwa kwa kusudi la Mungu hakukutegemea taifa moja tu. La, kwa kuwa “katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” Matendo 10:35

Paulo alionyesha kwamba kwa kuwa “matawi” ya mzeituni ya Wayahudi wasio waaminifu yalikatwa, mtu yeyote aweza kukatwa vivyo hivyo akikosa upendeleo wa Yehova kwa sababu ya kiburi na kutotii. Warumi 11:19,20 Kwa kweli jambo hilo laonyesha kwamba hatupaswi kupuuza fadhili isiyostahiliwa ya Mungu 2Wakoritho 6:1.


Kupaka Mafuta kwa Maombezi ya Mgonjwa

Maandiko yanarejezea kihalisi na kwa mfano matumizi ya mafuta ya zeituni. Zamani, majeraha na machubuko ‘yalilainishwa kwa mafuta’ ili yapone haraka. Isaya 1:6 Kulingana na mojawapo ya mifano ya Yesu, Msamaria aliyekuwa jirani mwema alipaka mafuta ya zeituni na divai kwenye majeraha ya mtu aliyemkuta kwenye barabara ya kwenda Yeriko Luka 10:34.

Mtu huburudika na kupata kitulizo apakapo mafuta ya zeituni kichwani. Zaburi 141:5  Wazee Wakristo wanaweza ‘kumpaka mafuta mtu ambaye hawezi wanaposhughulika na ugonjwa wa mwili na kiroho.na Kuomba kwa Jina la Yesu Yakobo 5:14 Ushauri wenye upendo wa wazee unaotokana na Maandiko na sala zao za kutoka moyoni kwa niaba ya mwamini mwenzao aliye mgonjwa kiroho zinalinganishwa na mafuta ya zeituni yenye kutuliza. Yapendeza kwamba kuna usemi wa Kiebrania ambao wakati mwingine humwita mtu mzuri “mafuta safi ya zeituni.”



‘Mzeituni Unaostawi Katika Nyumba ya Mungu’

Kwa kuzingatia mambo ambayo yametajwa, si ajabu kwamba watumishi wa Mungu wanaweza kulinganishwa na mizeituni. Daudi alitamani kuwa kama “mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu.”  Zaburi 52:8Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.” Kama vile mara nyingi familia za Waisraeli zilivyokuwa na mizeituni iliyozingira nyumba zao, vivyo hivyo Daudi alitaka kuwa karibu na Mungu na kuzaa matunda kwa sifa ya Mungu.

Ufalme wa Yuda wa makabila mawili ulikuwa kama “mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema” wakati walipokuwa waminifu kwa Mungu. Yeremia 11:15-1815. Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha. 16. Bwana alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika. 17. Kwa maana Bwana wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba. 18. Tena Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao.” Lakini watu wa Yuda na Israel walipoteza hali hiyo ya kupendelewa ‘walipokataa kusikia maneno ya Mungu; wakafuata miungu mingine. Yeremia 11:10 “Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.”

Ili kuwa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, ni lazima tumtii Mungu na kuwa tayari kukubali nidhamu ambayo yeye hutumia “kutupogoa” ili tuweze kuzaa matunda zaidi ya Kikristo.Waebrania 12:5-6 Isitoshe, kama vile mzeituni wa kawaida huhitaji mizizi mingi ili kustahimili ukame, twahitaji kuimarisha mizizi yetu ya kiroho kusudi tuvumilie majaribu na mnyanyaso Mathayo 13:21, Wakolosai 2:6-7.

Mzeituni unafananisha vizuri na Mkristo mwaminifu, ambaye huenda asijulikane katika ulimwengu bali anatambuliwa na Mungu. Mtu kama huyo akifa katika mfumo huu, ataishi tena katika ulimwengu mpya unaokuja. 2Wakoritho 6:9, 2Petro 3:13.

Mzeituni ambao ni kama hauwezi kuharibiwa, ambao huendelea kuzaa matunda mwaka baada ya mwaka watukumbusha ahadi hii ya Mungu: “Kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.” Isaya 65:22 Ahadi hiyo ya kiunabii itatimizwa katika ulimwengu mpya wa Mungu 2Petro 3:13.

Jinsi ya Kutumia Mafuta ya Mzeituni kwa shughuli (Mahitaji) Mbalimbali.

1.      Kuweka wakfu Kiongozi Mafuta ya mzeituni hutumika wakati wa kumuweka wakfu Kiongozi wa Kisiasa, Kidini na kijamii, Katika Israel Nabii, Mfalme na Kuhani waliwekwa wakfu kwa ibada maalumu na kupakwa mafuta unapompaka mtu mafuta kwa mujibu wa nafasi aliyo nayo utatangaza kupitia neno la Mungu Je Bwana Hakukupaka Mafuta Ili………………..(Unaeleza Kusudi la kumpaka mafuta hayo) kisha unamiminia na kumuombea neema kwaajili ya kazi hiyo kupitia Jina la Yesu Mfano 1Samuel 10:1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta akayamimina kichwani pake akambusu akasema Je Bwana hakukutia mafuta [Uwe mkuu juu ya watu wake Israel? Nawe utawamiliki watu wa Bwana na kuwaokoa na mikono ya adui zao kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia Mafuta ] uwe mkuu juu ya urithi wake” Unapompaka mafuta kiongozi lazima utangaze kusudi la kupakwa kwake mafuta nay ale yatakayonenwa yatampata.Kama anayepakwa Mafuta ni Mchungaji , Kuhani padre au nabii utasoma Kutoka 29:7 na kumuombea nneema ya majukumu yake na kumpaka mafuta,

 Ibada ya kumpaka mtu mafuta yaweza kufanyika hata Faragha
2.      Ikiwa unahitaji Mafuta haya kwaajili ya kumpokea Roho Mtakatifu utasoma Luka 4:18-19 pia 1Samuel 16:13 kisha ingia katika maombi ya kuhitaji kujazwa Roho mtakatifu na utashangaa nguzu za Mungu zitakushukia na utaanza kusema kwa lugha nyingine
3.      Ikiwa unatumia mafuta kwaajili ya kuondoa msongo wa mawazo, kujilinda na maadui wa kibinadamu na mashetani utachukua mafuta ya mzeituni utasoma Zaburi ya 23 yote na kisha utajipaka au utampaka mtu mwenye stresses Msongo wa mawazo na kisha utaomba neema na rehema huku ukiyasambaza mafuta hayo katika upaji wa uso kwa kutumia jina la Yesu na mtu huyo atapokea amani na furaha tangu wakati huo
4.      Ikiwa ni kwaajili ya kuombea Mgonjwa ambaye hawezi utachukua kichupa cha mafuta ya mzeituni, utaongena na mgonjwa na kumtia moyo na kumfariji kisha utasoma pamoja naye Yakobo 5:14-15 na Marko 16:17-18
5.      Ikiwa ni kwaajili ya kukemea vifungo vya shetani ba kutoa pepo chukua mafuta ya mzeituni kisha soma maandiko yafuatayo na weka mkono wako juu ya mtu mwenye pepo omba rehema kwaajili yake na kukemea kwa jina la Yesu Luka 4:18-19, na Marko 16:17-18
6.      Ikiwa ni kwaajili ya kujilinda na maadui wa aina yoyote yaani wakimwili na kiroho jipake mafuta ya mzeituni na kabla ya kujipaka utasoma maandiko haya kisha utajipaka na kujiombea au kumuombea mwenye uhitaji huo Zaburi 27:1-6, 1Samuel 2:10
7.      Ikiwa ni kwaajili ya nguvu za kiume au za kike utajipaka mafuta hayo ya mzeituni wakati unapokuwa unakwenda kulala katika sehemu ya via vya uzazi kisha utaomba kisha utaisema Zaburi ya 103:1-5 utasubiri kwa dakika tano nguvu zitakushukia kufurahia uumbaji wa Mungu
8.      Kwaajili ya kujitibu Mafua utajipaka katika eneo la pua na tundu zake mara tatu kwa siku ukitumia Marko 16:17
9.      Kwaajili ya kuua wadudu wabaya walioko tumboni utayaombea mafuta hayo na kunywa kijiko cha chai 1X2 kwa siku kwa mfululizo siku saba Marko 16:17-18
10.  Kwaajili ya kutunza kumbukumbu na kuponya ugonjwa wa kusahau chukua mafuta ya zeituni jipake katika paji la uso soma Zaburi ya 103:1-5 kisha muombe Mungu kwa jina la Yesu na utakuwa wa ajabu
11.  Kwa mtu alitepooza atachua eneo lililopooza mara mbili kila siku, mwenye pepo la Degedege atapaka mwili mzima kwa siku mara mbili maombi yatatangulia na Marko 16:17-18 itasomwana kuomba katika jina la Yesu
12.  Kwaajili ya kutunza Ngozi isizeeke kuondoia mikunjo, kuondoa alama za kuungua na jua, kukinga mionzi ya jua kulainisha mishipa, kukinga na saratani ya ngozi, kupambana na sumu kwenye ngozikilinda ngozi kupatwa na sumu,kuondoa mabaka kuondoa ukavu kwenye ngozi soma Zaburi 103:1-5 kisha omba nap aka mafuta haya mwili mzima kama mafuta ya kawaida hutazeeka haraka
13.  Ikiwa una kesi na hoja ngumu zinakukabili Mahakamani soma Isaya 54:17 kisha fanya maombi ya ushindi na ujasiri jipake mafuta ya mzeituni Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya 

14.  Mafuta ya Mzeituni yanaweza kutumika hata kwa kuukanda mwili Massaging na kusababisha mwili ku- relax kupata ahueni nakuondoa uchovu. Pia mizeituni huleta usingizi mzuri  
15. Mafuta ya mzeituni yanaweza pia kutumika kwa kuvunjia mikataba ya aina mbalimbali yaani nira na maagano ambayo ulijiingiza na kama unataka kujikomboa 
Mafuta ya Mizeituni hupatikana katika maduka mbalimbali supermarket, na sehemu nyinginezo kumbuka ni muhimu kupata mafuta Original na sio yaliyochanganyika na kitu kwa vila mengine utaweza kula, kujipaka na kadhalika huitaji msaada wa Mchungaji au kiongozi wa dini kuona matokeo ya mizeituni zaidi ya kujifunza, kuamini na kutendea kazi.


Matumizi ya neno la Mungu na mafuta yanaweza kutumika katika maeneo mengi zaidi ya haya itategemea na ufunuo wako na maandiko utakayoweza kuyatumia utayatumia kulingana nauhitaji wako, Hakuna utata wa kimaandiko kuhusu matumizi ya mafuta,sio lazima upewe na manabii au Mchungaji kanunue mwenyewe hata ndoo nzima kwa matumizi yako ingawa mafuta haya ni ghali, kwa muda mrefu sana nilimtumikia Mungu na kuombea watu bila ya matumizi ya mafuta, sikupanda kabisa kutaka kuyatumia, kwa zaidi ya miaka 20 ya kumtumikia Mungu sikutaka kuamini katika swala hili, nilisubiri kupata ufunuo kamili wa swala hili na dhamiri yangu kuhusu matumizi ya mafuta na Mungu aliponithibitishia kuwa Inatenda kazi naliona vema kama mkuu wa wajenzi kuweka fundisho hili wazi, Jambo kubwa la msingi usiyatumia mafuta kama Biashara, wala usiyatumie kama uganga bali yatumia kwa imani na maombi na neno la Mungu na utaweza kuona Mafanikio, Kwa maandiko zaidi kuhusu Mafuta katika Biblia soma mistari kadhaa ifuatayo:-

Kutoka 25:6, 29:7, 29:2, 29:29,30:3,22-26,40:9, 40:15,  Walawi.8:10,8:12,4:3,5,16,6:20, 
Zaburi.132:10,1Sam.16:13,2Sam.24:4,1Nyakati.16:22;Zab.105:15,1Wafalme-19:16 1Nyakati.16:22Zab.105:15, Isa. 21:5,Luke 7:38-40, Kumb. 28:40, Ruth 3:3,2Samuel 14:2,
Zab.104:15, 109:18, Isaiah 1:6,Mark 6:13, Yakobo. 5:14, Mark 14:8,Luka. 23:56, Zab. 2:2; 
Dan. 9:25, 26, 
Isa. 61:1, Zab. 45:7; Heb. 1:9, John 1:41; Mdo. 9:22; 17:2, 3; 18:5, 28, 1 Yoh. 2:20, Matt. 25:1-13
 

Jumanne, 7 Juni 2016

Kuzaliwa kwa Masihi na Mioyo ya watu


Leo ni sikukuu ya CHRISTIMAS  Wakristo wote Nchini tunajiunga na wakristo wengine Duniani katika kuadhimisha siku kuu hii ya Kuzaliwa kwa Mwokozi, Zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko Bethelehemu, Katika siku hii muhimu namna hii ni muhimu sana kwetu pia kujifunza na kutafakari kwa pamoja kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Ingawa kiini kikuu ni kuzaliwa kwa Yesu Kristo eneo kubwa tunatafakari mioyo mioyo ya watu kadhaa wakati wa kuzaliwa kwa Masihi, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:

 Wise man means a man versed in magic, witchcraft, or astrology
(Mamajusi maana yake ni mtu anayejishughulisha na Uganga, Uchawi na Unajimu)

·         Maana ya CHRISTIMAS
·         Kuzaliwa kwa Masihi na mioyo ya watu

Maana ya CHRISTIMAS

Neno CHRISTMAS ni muungnaniko wa Maneno mawili ya KILATINI CHRIST na MASS ambapo maana zake ni kama ifuatavyo
Christ maana yake KRISTO au MASIHI
Mass Maana yake ni Jumuiya au mjumuiko au Ibada misa au Kuadhimisha
Kwa hiyo neno Christ na Mass yanapounganishwa tunapata neno CHRISTMAS ambalo maana yake ni Kumuadhimisha Kristo, au kumuabudu Kristo au jumuiya ya Kristo, maana muhimu zaidi ni KUMUABUDU KRISTO.

Kuzaliwa kwa mashi na mioyo ya watu.

Ni muhimu kufahamu kuwa leo tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Masihi Biblia inatufunulia kuwa wakati Yesu anazaliwa huko Bathelehemu. Mioyo ya watu iligawanyika katika makundi kadhaa ambayo huenda hata leo makundi hayo yakawepo na huenda hata Yesu Kristo atakaporudi tena mara ya pili atayakuta

1.       Mioyo ya walimwengu 

Yohana 1:10-11 Biblia inasema hivi “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Biblia inapozungumzia ulimwengu inazungumzia mfumo wa kawaida wa uharibifu wa Dunia kiyunani Cosmos ni njamii inayojiendesha bila kujali uwepo wa Mungu, Neno lake wala utawala wake, Ulimwengu siku zote ni mpinzani mkubwa sana wa Historia ya wokovu, kuifuata dunia hii au mfumo wa ulimwengu huu ni kujifanya adui wa Mungu Yakobo 4:4 Biblia inasema hivi “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” Biblia inamuagiza kila mtu anayemfuata Yesu Kristo kutokuifuatisha namna ya dunia hii Warumi 12:2Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Awaye yote ambaye anaifuatisha namna ya dunia hii yaani mfumo wa ulimwengu huu au kawaida ya ulimwengu huu au kufanya urafiki na dunia au kuipenda ni wazi kuwa mtu huyo yuko nje na kusudi na mpango wa Mungu wa kuokoa, Yesu ni mwokozi na alikuja Duniani ili awaokoe wanadamu lakini awaye yote ambaye hamuanimi ama amesikia habari za Yesu lakini bado anaupenda ulimwengu huu, huyo amemkataa Yesu, 1Yohana 2:15 Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia Mtu akiipenda Dunia , kumpenda Baba hakumo ndani yake” Unaona! Kumbe watu wanaofuata kawaida za ulimwengu huu ni raia wa ulimwengu huu wale wanaomfuata Yesu sio raia wa ulimwengu huu kufuata kawaida ya ulimwengu huu ni dhambi Yesu alipozaliwa alikuta mioyo ya watu ikiwa iko katika kawaida zao za kila siku za kijamii na kisiasa na hakukuwa na mtu aliyeonyesha kujali kama Yesu amezaliwa Luka 2:1-7 Biblia inasema “Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi;  ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba.  Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia,  akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”  Wakati Yesu anazaliwa watu wa ulimwengu walikuwa katika sense na agizo la kifalme ili kuandikishwa hakuna mtu aliyekuwa na wazo la kufikiri kuhusu kuzaliwa kwa masihi. Watu wengi leo wamekuwa busy na shughuli zao za kila siku za biashara, kazi kilimo na shughuli nyingine za utafutaji jambo ambalo si baya lakini hawatoi nafasi ya mioyo yao kufatakari mambo ya Mungu au hata kuhudhuria Ibada jambo kama hili lilipelekea Yesu kuzaliwa katika hori ya kulishia Ng’ombe kwani alikosa nafasi kwa walimwengu.

2.       Mioyo ya wanasiasa.

Kundi hili la pili ni kundi la wanasiasa kundi hili nalo wakati Yesu alipokuwa anazaliwa lilishindwa kumpokea, kundi hili katika biblia linawakilishwa na mfalme Herode Mathayo 2:1-7, 12-16 1. “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. 7. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota.”

“12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. 13. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. 14. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;

unamuona Herode? Huyu alikuwa ni mtu wa namna gani

  • Alikuwa mtu wa Idumeya na Hakuwa Myhahudi Idumeya ni eneo la Edom watu wa Esau
  • Alikuwa Mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa, warumi walimfanya awe kiongozi kibaraka wa Kaisari na mfalme wa jimbo la Galilaya na  Uyahudi au Yuda
  • Alioa mtoto wa kuhami mkuu
  •  Na ili aweze kukubalika na wayahudi alijenga Hekalu, Hili ndilo Hekalu ambalo yesu alilitumia alipokuwa duniani

Pamoja na hayo yote kama tulivyosoma maadniko na sifa za Herode mwanasiasa huyu hakufurahi aliposikia Yesu amezaliwa, aidha alikusudia kumuua Yesu ingawa ilionekana kama anampenda Mungu wa wayahudi kwa kuwajengea hekalu, lakini moyo wake haukumfurahia Mungu hii ndio tabia ya wanasiasa wanaweza kujenga nyumba za ibada kwa kusudi tu la kuiteka mioyo ya watu kisiasa lakini mioyo yao haiku tayari kumkaribia Mungu wanaweza kuonekana kama wema wanaposalimia salama za kidini lakini wanachokitaka sio Mungu sio Yesu bali wanataka mioyo ya kuwapigia kura kutokana na hali hii neema ya Mungu ilikuwa mbali nah erode na akafa bila kumshuhudia Masihi, aidha alikuwa tayari kumiza na kuua watoto wengi sana kwaajili ya kulinda cheo chake na faida yake ni mara ngapi tumeshuhudia, utu ukitoweka karibu na uchaguzi watu wenye ualbino wakiuawa kama hapa Tanzania kwa kusudi la watu wajinga na washirikiana kujipatia kibali cha kisiasa Bwana aliangalie hili na kulikemea!

3.       Mioyo ya Viongozi wa Kidini

Mathayo 2:1-6 Biblia inasema “1.Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.”

Biblia inaeleza kuwa Herode aliposikia habari ya kuzaliwa kwa Masihi kutoka kwa Mamajusi alikusanya Makuhani pamoja na waandishi akatafuta habari kwao Kristo azaliwa wapi, Makuhani ni viongozi wa dini na waandishi walikuwa ni walimu wa torati hawa walikuwa ni watu wenye ujuzi sana kuhusu neno la Mungu na unabii lilikuwa ni kundi la watumishi wa Mungu Mungu anirehemu hapa maana na mimi pia ni kiongozi wa kidini kundi hili linanihusu na maonyo yake pia yananihusu, Kundi hili walipouliszwa swali kuwa Masihi azaliwa wapi ilikuwa rahisi kwao kujibu kutokana na ujuzi wao katika maandiko walitafuta na walimjulisha mfalme kuwa Masihi anazaliwa bethelehemu kama anenavyo nabii bila shaka walinukuu unabii katika Mika 5:2Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” Unaona watu hawa wa Mungu yaani watumishi walikuwa na ujuzi mkubwa sana kuhusu maandiko, walijua kuwa masihi ni kiongozi mkubwa ambaye matokeo yake yaani asili yake ni tangu milele walitambua kuwa kiongozi huyu mkubwa sana na wa kuheshimika sana Duniani anazaliwa Bethelehemu lakini jambo la kusikitisha viongozi hao wa dini pia mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu, hakuna hata mmoja aliyeonyesha shauku ya kutaka kumuona Masihi ambaye walikuwa na taarifa zake kuwa ameshazaliwa na walijua wapi anazaliwa

Ni dhahiri kuwa kuwa na ujuzi wa maandiko hakuwezi kutupa nafasi ya kuwa na uhusiano wa kweli na Yesu Kristo, aidha kuwaelekeza wengine neno hakumaanishi kuwa ndio nafasi ya sisi kukubaliwa na Mungu, kama kwa matendo yetu tutamuabudu Mungu na kumuadhimisha lakini mioyo yetu iko mbali naye tutakataliwa katika ufalme wa Mungu Mathayo 15:7-9Enyi wanafiki ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu akisema watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami, Nao waniabudu Bure wakifundisha mafundisho yakiyo maagizo ya wanadamu Paulo mtume alikuwa muhubiri wa ngazi yajuu sana lakini alijionya Ole wangu mimi nisije nikawahubiri wengine kisha mimi nikawa mtu wa kukataliwa  1Wakoritho 9: 26-2726. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;27. bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” Kumbe uko uwezekano wa wahubiri wengi kukataliwa katika ufalme wa Mungu kutokana na mkao wa mioyo yetu, leo hii wako watumishi wa Mungu wana kesi ziko mahakamani wameshitakiana wakidaiana mali na hawataki kusameheana, yako matumizi mabaya ya sadaka, uzinifu, Mafarakano, choyo uadui ugomvi kusemana vibaya na maswala kedekede ni muhimu kujikumbusha kuwa kuwa na Elimu kubwa za kidini, kutumiwa na Mungu kwa karama mbalimbali kutoa Pepo na na kufanya unabii kamwe sio tiketi ya kutufanya tuingie katika ufalme wa Mungu ni jambo la kustaabisha kuwa viongozi wa dini ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kumpinga Yesu Kristo na hata kutafuta namna ya kumuua Mungu unikumbuke na kunisamehe na kamwe usinipite na kuniacha

4.       Mioyo ywa watu Masikini na waliokata tamaa
Ni jambo la Kushangaza kuwa Mungu anawaangalia sana wanyonge masikini na waliokata tamaa wakati dunia haijali na mfumo wa dunia hauwajali watu masikini Mungu aliwapa neema watu duni, walikuwa hawana ujuzi wa maandiko wala hawako karibu na ikulu, na huenda walikuwa wamejikatia tamaa Mungu aliwatuma malaika zake kutoa habari maalumu kwa kundi hili kuwa masihi amezaliwa

Luka 2:8-20 Biblia inasema hivi “8. Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. 10. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11. maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. 13. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, 14. Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. 15. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. 16. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. 17. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 18. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 19.Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 20. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa”. Ni jambo la kushangaza kabisa kuwa malaika aliwaambia wachungaji hao kuwa Leo hii katika mji wa Daudi amezaliwa kwaajili yenu Mwokozi ndiye Kristo Bwana natamani kabisa Mungu angenifanya maalumu kama wachungaji hawa ni watu wanyenyekevu wenye mioyo iliyopondeka hawakuwa na ujuzi wa neno hawakuwa wanasiasa lakini Mungu hakuwanyima vyote aliwapa habari njema na hili likawa kundi la kwanza kwenda Bethelehemu na kujionea kundi hili likatoa habari ya kuzaliwa kwake Yesu kristo na kushangaza watu, hii ndio ilikuwa iwe kazi ya makuhani lakini mioyo yao iliwanyima kumjua masihi mioyo iliyopondeka aidha hawa waliishuhudia kundi la malaika wakiimba kwa furaha na kumtukuza Mungu kuhusu kuzaliwa kwa masihi mwe Mungu ni Mungu wa waliotupwa wanyonge na waliohesabika kuwa si kitu, Mungu huwapinga wajikwezao bali huwapa neema wanyenyekevu.

5.       Mioyo ya watu wenye subira.

Kundi hili linawakilishwa na Simeon na Anna Binti Fanuel Simeon alikuwa mtu Mcha Mungu na nabii alikuwa mwenye haki na alikuwa akisubiri kwa shauku kuzaliwa kwa masihi alikuwa ni mzee mmno lakini Roho Mtakatifu alikuwa amemwambia kuwa hatakufa mpaka amemwona masihi, huyu alikuwa mtu mvumilivu umri wake ulikuwa umekwenda lakini bado alikuwa akiutazamia ukombozi, alipomuona masihi Roho Mtakatifu alimuonyesha wazi habari za Mtoto huyo kule hekaluni na sasa alifurahi na kutoa unabii kuhusu Mateso ya Yesu lakini sasa alikuwa tayari kufa kwa amani kwa vile Mungu alikuwa amemtimizia ahadi, Anna binti Fanuel mjane alikaa ujane miaka 84 aliishi na mume miaka 7 tu alidumu katika maombi mwanamke huyu pia alikuwa nabii yeye naye aliwaeleza wazi wote waliokuwa wakisubiria habari zake na kuwathibitishia kuwa huyu ni masihi
Luka 2 25-38 “ 25. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 27. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, 28. yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, 29. Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; 30. Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, 31. Uliouweka tayari machoni pa watu wote; 32. Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. 33. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. 34. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. 35. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. 36. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 37. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. 38. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.  Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuwa mtu mwenye subira na mwenye uvumilivu huku tukimtazamia masihi bila shaka hatuataibika atakapofunuliwa Bwana wakati wa kuja kwake mara ya pili, watu wa rohoni kama ilivyo kwa Simeon na Anna wataelewa wazi Kristo atakapokuja na halitakuwa fumbo kwao hawa walikuwana mioyo yenye kusubiri

6.       Mioyo ya watu wasiotegemewa.

Kundi hili linawakilishwa na jamii ya Mamajusi hili nimeliita kundi la watu wasiotegemewa kwa vile hawakuwa wanamjua Mungu kabisa, hawakuwa na ujuzi wa neno la Mungu, walitokea nchi ya mbali sana na ndio watu wa kwanza kugundua kuwa Kuna Mfalme mkubwa sana wa Wayahudi amezaliwa na kwa vile wafalme huzaliwa ikulu walisafiri kutoka Ukaldayo au mashariki ya mbali yaani Iraq kwa kuchunguza nyota mpaka wakagundua kuwa masihi amezaliwa,\

Ni muhimu kufahamu kuwa watu hawa walijulikana kama watu wenye Hekima na walikuwa ni watu wenye ujuzi na maswala ya nyota yaani wanajimu walihusika na maswala ya uchawi pia Daniel 2: 2 huko ukaldayo kulipotokea jambo gumu sana wao zamani walikuwa ni watu waliotegemewa kutoa majibu Daniel 2: 2 inasema hiviNdipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme.” Wakristo wengi na wataalamu wa maandiko hufikiri nkuwa Mamajusi walikuwa watu wazuri na watakatifu Hapana lilikuwa ni kundi la Waganga, wachawi na wasihiri yaani wapiga lamri hawa sasa walikuwa wanajimu kama ilivyokuwa kwa Marehemu Yahaya Husein kwa hapa Afrika mashariki ndio maana hili ni kundi la watu wasiotegemewa Mungu aliruhusu katika ufahamu wao na unajimu wao kuona Nyota iliyomuhusu Masihi na kwa moyo waliokuwa nao walijua kuwa wanapaswa kumsujudia na kumuabudu na cha kushangaza zaidi ni kuwa Mungu alisema nao na kuwaonya wasiende kwa Herode maana anataka kumuua mtoto nao wakarudi kwao kwa njia nyingine 

Mathayo 2:10-12 10. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. 11. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. 12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.”

Ni wazi kuwa kundi hili linawakilisha watu watakaoingia katika Ufalme wa Mungu bila sisi kuwatarajia, Mungu haukumu wala hatazami kama wanadamu watazamavyo, sikun ya hukumu na katika ufalme wa Mungu tunaweza kabisa kushangaa wale tunaowadhani ndio wakawa sio na wale tunawadhani sio wakawa ndiyo, Mioyo iliyopondeka Mungu huiangalia sana , unyonge na kutokujihesabia haki ni wazi kuwa kama  mioyo yetu itafanana na makundi makuu matatu ya awali tunaweza tukajikuta tumekataliwa katika ufalme wa Mungu, ni jukumu letu kuangalia na kujiangalia na kujipima namna tunavyoeneda ni mioyo ya makundi matatuya mwisho ndio ambao waliweza kupata nafasi ya kumuadudu Yesu yani kusheherekea CHRISTMAS jihoji je wewe utaweza kuisherekea siku hii na unaisheherekea katika mkao upi wa Moyo?

Ujumbe. Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Jumapili, 5 Juni 2016

Ujumbe: Makusudi ya Bwana Hayawezi Kuzuilika!



Ayubu 42:1Ndipo Ayubu akamjibu BWANA na Kusema Najua ya kuwa waweza Kufanya Mambo yote  Na ya makusudi yakohayawezi kuzuilika.”

 Ayubu alielewa Kuwa makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika
 
Watu wengi sana Duniani wanaishi Maisha ya huzuni na kukata tamaa kwa sababu ya kutokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu Mungu na makusudi ya Mungu katika maisha yao, Na huuzunika zaidi wanapopitia katika Magumu, masumbufu na Mateso ya aina mbalimbali wakati mwingine ikiwa ni magonjwa, kuchukiwa na hata kutendewa mambo mabaya au kupatwa na Mabaya, Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika mambo yoote (Mema au mabaya) anaweza kuyatumia katika kutimiza Mpango wake mwema katika maisha Yetu. 

Warumi 8:28Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema yaani wale walioitwa kwa kusudi lake

Andiko la msingi linatoka katika kitabu cha Ayubu ni kitabu cha kifalsafa kinachojadili dhana kuhusu Mateso kwa wanadamu na Mtazamo wa Mungu, wote tunajua kuwa Ayubu alipatwa na Mateso na mitihani migumu ya kupita kawaida, Muda Hautoshi kuangalia ni hasara gani na mateso gani aliyapitia, lakini wote tunajua kuwa Ayubu hakutenda dhambi, na hata kama angetenda Mungu ni wa rehema na hawezi kutulipa mabaya kwa sababu ya ubaya wetu, Rafiki za Ayubu walimlaumu Ayubu na kumtetea Mungu walionyesha wazi kuwa haiwezekani Mateso hayo yampate Ayubu kama Ayubu hakuwa na Makosa, aidha Ayubu alijitetea sana kuwa hakuna makosa aliyoyafanya, Ayubu ingawa hakufanya dhambi lakini alimlaumu Mungu katika kiwango cha kufikia kuonyesha Kiburi na kuonyesha kuwa Mungu hayuko sawa, ni kama alikuwa akimhoji Mungu kwa nini niyapitia haya
Kutokana na majibu ya Mungu kwa Ayubu hatimaye Ayubu alitambua

1.      Mungu huruhusu mambo yote yatupate kwa makusudi yake mema
2.      Kila jambo ambalo Mungu uliruhusu litokee katika maisha yetu katika hekima yake Mungu huruhusu kwa makusudi
3.      Hata mateso ya Mwanadamu na mapito magumu yana maana katika kusudi la Mungu

Kwa sababu hiyo basi ni muhimu kwetu kuamini kuwa Mungu anaweza kufanya mambo yote, Kuamini kuwa kama tunatembea katika Makusudi ya Mungu basi hakuna cha kutuzuia, wala mtu wa kuzuia kusudi la Mungu kwetu katika maisha yetu.

Ni muhimu kwetu tu kutambua makusudi ya Mungu katika maisha yetu, na kutambua kuwa hakuna jambo linalotokea kwa Bahati mbaya “Socrates alisema maisha yasiyotafakariwa Hayafai kuyaishi” mimi nasema “Kuishi maisha yasiyo na kusudi nikupoteza mwelekeo” Mungu ametuumba kwa Makusudi na ni lazima makusudi hayo yatimizwe.

Mungu akikusudia Jambo katika maisha yako hakuna anyeweza Kulibatilisha

Mungu huyabatilisha Mashauri ya watu waovu Dhidi yako

Yusufu alipewa Ndoto yale yalikuwa ni Makusudi ya Bwana katika maisha yake hata hivyo alipitia changamoto za aina mbali mbali, tunapopitia hayo ni muhimu kutambua kuwa Kusudi la Mungu haliwezi kubatilika.

Daudi alipakwa mafuta kwa kusudi la Kuwasaidia Israel kama Mfalme, Sauli alitaka kumuua mara kadhaa alimtupia mkuki ili kuharibu kusudi na mpango wa Mungu lakini hatimaye Daudi alimiliki na kutawala

Musa alikuwa auawe katika mpango mbaya wa mfalme wa Misri aliyeamuru watoto wa kiume wauawe, Mungu katika hekima yake alimfanya Musa huyohuyo alelewe ikulu na kuwa salama zaidi
Kiko mifano mingi inayothibitisha kuwa Makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika, Adui zetu wanapotufikiria mabaya Mungu hutufikiria mema au kutumia ubaya wao kutuletea mambo mema.

Zaburi 33:10-11“Bwana huyabatilisha Mashauri ya mataifa, Huyatungua makusudi ya watu, Shauri la Bwana lasimama milele. Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi”

Mithali 21:30 - 31 “Hapana Hekima wala ufahamu, wala shauri juu ya Bwana, farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita Lakini bwana ndiye aletaye wokovu” 

Isaya 8:10 “ Fanyeni Shauri pamoja nalo litabatilika, Semeni neno, Lakini halitasimama kwa maana Mungu yu pamoja nasi”

Mungu akikusudia hakuna anayeweza kubatilisha
 
Isaya 14:27 “Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na Mkono wake uliionyooshwa ni nani atakayegeuza nyuma?

Hata wanadamu wafanye hila bado kusudi la Mungu ndio litakalo simama
 
Mithali 19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu, Lakini Shauri la Bwana ndilo Litakalosimama”

Paulo Mtume alikuwa amekusudia kuuona na Rumi pia
Warumi 1:15 “Kwa hiyo kwa Upande wangu mimi ni tayari kuihubiri injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi” 

Lakini Wayahudi walikusudia kwa kila namna kuharibu mpango na makusudi ya Paulo, walitaka kumuua kabla hajafika Rumi Angalia
 
Matendo 23:12-15 “Kulipopambauka,Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo.  Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.  
        
Angalia je hila zao zilifanikiwa?
Matendo 23: 11 “.Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.”

Ni muhimu kufahamu kuwa kama unatembea katika kusudi la Mungu basi hakuna anayeweza kuzuia kusudi hilo na kamwe hupaswi kukata tamaa unapoona mambo magumu, vikwazo na hila za ibilisi na mipango ya kukukatisha tamaa hila na matendo mabaya ya watu dhidi ya ndoto zako hakuna muda wa kumlaumu mtu au kutafuta mchawi ni nani, jambo moja unalopaswa kulitambua ni kuwa “Makusidi ya Mungu hayawezi kuzuilika” Mungu amekupa nguvu na mamlaka ya kubatilisha hata Mashauri ya Adui zako hata kama mashauri hayo yanaonekana kana kwamba yanatoka kwa Mungu angalia.

 2Samuel 16:23, Na shauri lake Ahithofeli alilokuwa akilitoa siku zile lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu, Ndivyo yalivyokuwa mashauri yake Ahithofeli kwa Daudi na Kwa Absalom”

Daudi alitambua kuwa Ahithofeli alikuwa mtu mashuhuri kwa Ushauri na ushauri wake ilikuwa kama kuuliza kwa Mungu na Ahithofeli  alipokuwa ameasi kwa Daudi Dua za daudi kwa Mungu ilikuwa ni kuilaani karama ya ushauri ya Ahithofeli na kuibatilisha 

2Samuel 15:31 “Mtu mmoja akamwambia Daudi ya Kwamba Ahithofeli yu katika hao walioambatana na Absalom, Daudi akasema Ee Bwana nakusihi Uligeuze Shauri la Ahithofeli liwe Batili”

Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kumsihi Mungu ili mashauri mabaya yanayotolewa dhidi yatu yaweze kuwa Batili, mawazo mabaya yanayotolewa dhidi yetu yabatilike maneno mabaya yanayotolewa dhidi yako yabatilike Bwana na abatilishe manuizo yote ya wachawi na laana zote na kila mpango ambao sio makusudi ya Bwana dhidi ya maisha yetu katika Jina la Yesu Amen.

Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.