Jumanne, 7 Juni 2016

Kuzaliwa kwa Masihi na Mioyo ya watu


Leo ni sikukuu ya CHRISTIMAS  Wakristo wote Nchini tunajiunga na wakristo wengine Duniani katika kuadhimisha siku kuu hii ya Kuzaliwa kwa Mwokozi, Zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko Bethelehemu, Katika siku hii muhimu namna hii ni muhimu sana kwetu pia kujifunza na kutafakari kwa pamoja kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Ingawa kiini kikuu ni kuzaliwa kwa Yesu Kristo eneo kubwa tunatafakari mioyo mioyo ya watu kadhaa wakati wa kuzaliwa kwa Masihi, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:

 Wise man means a man versed in magic, witchcraft, or astrology
(Mamajusi maana yake ni mtu anayejishughulisha na Uganga, Uchawi na Unajimu)

·         Maana ya CHRISTIMAS
·         Kuzaliwa kwa Masihi na mioyo ya watu

Maana ya CHRISTIMAS

Neno CHRISTMAS ni muungnaniko wa Maneno mawili ya KILATINI CHRIST na MASS ambapo maana zake ni kama ifuatavyo
Christ maana yake KRISTO au MASIHI
Mass Maana yake ni Jumuiya au mjumuiko au Ibada misa au Kuadhimisha
Kwa hiyo neno Christ na Mass yanapounganishwa tunapata neno CHRISTMAS ambalo maana yake ni Kumuadhimisha Kristo, au kumuabudu Kristo au jumuiya ya Kristo, maana muhimu zaidi ni KUMUABUDU KRISTO.

Kuzaliwa kwa mashi na mioyo ya watu.

Ni muhimu kufahamu kuwa leo tunapoadhimisha kuzaliwa kwa Masihi Biblia inatufunulia kuwa wakati Yesu anazaliwa huko Bathelehemu. Mioyo ya watu iligawanyika katika makundi kadhaa ambayo huenda hata leo makundi hayo yakawepo na huenda hata Yesu Kristo atakaporudi tena mara ya pili atayakuta

1.       Mioyo ya walimwengu 

Yohana 1:10-11 Biblia inasema hivi “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Biblia inapozungumzia ulimwengu inazungumzia mfumo wa kawaida wa uharibifu wa Dunia kiyunani Cosmos ni njamii inayojiendesha bila kujali uwepo wa Mungu, Neno lake wala utawala wake, Ulimwengu siku zote ni mpinzani mkubwa sana wa Historia ya wokovu, kuifuata dunia hii au mfumo wa ulimwengu huu ni kujifanya adui wa Mungu Yakobo 4:4 Biblia inasema hivi “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” Biblia inamuagiza kila mtu anayemfuata Yesu Kristo kutokuifuatisha namna ya dunia hii Warumi 12:2Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Awaye yote ambaye anaifuatisha namna ya dunia hii yaani mfumo wa ulimwengu huu au kawaida ya ulimwengu huu au kufanya urafiki na dunia au kuipenda ni wazi kuwa mtu huyo yuko nje na kusudi na mpango wa Mungu wa kuokoa, Yesu ni mwokozi na alikuja Duniani ili awaokoe wanadamu lakini awaye yote ambaye hamuanimi ama amesikia habari za Yesu lakini bado anaupenda ulimwengu huu, huyo amemkataa Yesu, 1Yohana 2:15 Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia Mtu akiipenda Dunia , kumpenda Baba hakumo ndani yake” Unaona! Kumbe watu wanaofuata kawaida za ulimwengu huu ni raia wa ulimwengu huu wale wanaomfuata Yesu sio raia wa ulimwengu huu kufuata kawaida ya ulimwengu huu ni dhambi Yesu alipozaliwa alikuta mioyo ya watu ikiwa iko katika kawaida zao za kila siku za kijamii na kisiasa na hakukuwa na mtu aliyeonyesha kujali kama Yesu amezaliwa Luka 2:1-7 Biblia inasema “Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi;  ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba.  Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia,  akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.”  Wakati Yesu anazaliwa watu wa ulimwengu walikuwa katika sense na agizo la kifalme ili kuandikishwa hakuna mtu aliyekuwa na wazo la kufikiri kuhusu kuzaliwa kwa masihi. Watu wengi leo wamekuwa busy na shughuli zao za kila siku za biashara, kazi kilimo na shughuli nyingine za utafutaji jambo ambalo si baya lakini hawatoi nafasi ya mioyo yao kufatakari mambo ya Mungu au hata kuhudhuria Ibada jambo kama hili lilipelekea Yesu kuzaliwa katika hori ya kulishia Ng’ombe kwani alikosa nafasi kwa walimwengu.

2.       Mioyo ya wanasiasa.

Kundi hili la pili ni kundi la wanasiasa kundi hili nalo wakati Yesu alipokuwa anazaliwa lilishindwa kumpokea, kundi hili katika biblia linawakilishwa na mfalme Herode Mathayo 2:1-7, 12-16 1. “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. 7. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota.”

“12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. 13. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. 14. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;

unamuona Herode? Huyu alikuwa ni mtu wa namna gani

  • Alikuwa mtu wa Idumeya na Hakuwa Myhahudi Idumeya ni eneo la Edom watu wa Esau
  • Alikuwa Mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa, warumi walimfanya awe kiongozi kibaraka wa Kaisari na mfalme wa jimbo la Galilaya na  Uyahudi au Yuda
  • Alioa mtoto wa kuhami mkuu
  •  Na ili aweze kukubalika na wayahudi alijenga Hekalu, Hili ndilo Hekalu ambalo yesu alilitumia alipokuwa duniani

Pamoja na hayo yote kama tulivyosoma maadniko na sifa za Herode mwanasiasa huyu hakufurahi aliposikia Yesu amezaliwa, aidha alikusudia kumuua Yesu ingawa ilionekana kama anampenda Mungu wa wayahudi kwa kuwajengea hekalu, lakini moyo wake haukumfurahia Mungu hii ndio tabia ya wanasiasa wanaweza kujenga nyumba za ibada kwa kusudi tu la kuiteka mioyo ya watu kisiasa lakini mioyo yao haiku tayari kumkaribia Mungu wanaweza kuonekana kama wema wanaposalimia salama za kidini lakini wanachokitaka sio Mungu sio Yesu bali wanataka mioyo ya kuwapigia kura kutokana na hali hii neema ya Mungu ilikuwa mbali nah erode na akafa bila kumshuhudia Masihi, aidha alikuwa tayari kumiza na kuua watoto wengi sana kwaajili ya kulinda cheo chake na faida yake ni mara ngapi tumeshuhudia, utu ukitoweka karibu na uchaguzi watu wenye ualbino wakiuawa kama hapa Tanzania kwa kusudi la watu wajinga na washirikiana kujipatia kibali cha kisiasa Bwana aliangalie hili na kulikemea!

3.       Mioyo ya Viongozi wa Kidini

Mathayo 2:1-6 Biblia inasema “1.Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, 2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. 3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. 4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? 5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, 6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.”

Biblia inaeleza kuwa Herode aliposikia habari ya kuzaliwa kwa Masihi kutoka kwa Mamajusi alikusanya Makuhani pamoja na waandishi akatafuta habari kwao Kristo azaliwa wapi, Makuhani ni viongozi wa dini na waandishi walikuwa ni walimu wa torati hawa walikuwa ni watu wenye ujuzi sana kuhusu neno la Mungu na unabii lilikuwa ni kundi la watumishi wa Mungu Mungu anirehemu hapa maana na mimi pia ni kiongozi wa kidini kundi hili linanihusu na maonyo yake pia yananihusu, Kundi hili walipouliszwa swali kuwa Masihi azaliwa wapi ilikuwa rahisi kwao kujibu kutokana na ujuzi wao katika maandiko walitafuta na walimjulisha mfalme kuwa Masihi anazaliwa bethelehemu kama anenavyo nabii bila shaka walinukuu unabii katika Mika 5:2Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” Unaona watu hawa wa Mungu yaani watumishi walikuwa na ujuzi mkubwa sana kuhusu maandiko, walijua kuwa masihi ni kiongozi mkubwa ambaye matokeo yake yaani asili yake ni tangu milele walitambua kuwa kiongozi huyu mkubwa sana na wa kuheshimika sana Duniani anazaliwa Bethelehemu lakini jambo la kusikitisha viongozi hao wa dini pia mioyo yao ilikuwa mbali na Mungu, hakuna hata mmoja aliyeonyesha shauku ya kutaka kumuona Masihi ambaye walikuwa na taarifa zake kuwa ameshazaliwa na walijua wapi anazaliwa

Ni dhahiri kuwa kuwa na ujuzi wa maandiko hakuwezi kutupa nafasi ya kuwa na uhusiano wa kweli na Yesu Kristo, aidha kuwaelekeza wengine neno hakumaanishi kuwa ndio nafasi ya sisi kukubaliwa na Mungu, kama kwa matendo yetu tutamuabudu Mungu na kumuadhimisha lakini mioyo yetu iko mbali naye tutakataliwa katika ufalme wa Mungu Mathayo 15:7-9Enyi wanafiki ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu akisema watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami, Nao waniabudu Bure wakifundisha mafundisho yakiyo maagizo ya wanadamu Paulo mtume alikuwa muhubiri wa ngazi yajuu sana lakini alijionya Ole wangu mimi nisije nikawahubiri wengine kisha mimi nikawa mtu wa kukataliwa  1Wakoritho 9: 26-2726. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;27. bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” Kumbe uko uwezekano wa wahubiri wengi kukataliwa katika ufalme wa Mungu kutokana na mkao wa mioyo yetu, leo hii wako watumishi wa Mungu wana kesi ziko mahakamani wameshitakiana wakidaiana mali na hawataki kusameheana, yako matumizi mabaya ya sadaka, uzinifu, Mafarakano, choyo uadui ugomvi kusemana vibaya na maswala kedekede ni muhimu kujikumbusha kuwa kuwa na Elimu kubwa za kidini, kutumiwa na Mungu kwa karama mbalimbali kutoa Pepo na na kufanya unabii kamwe sio tiketi ya kutufanya tuingie katika ufalme wa Mungu ni jambo la kustaabisha kuwa viongozi wa dini ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kumpinga Yesu Kristo na hata kutafuta namna ya kumuua Mungu unikumbuke na kunisamehe na kamwe usinipite na kuniacha

4.       Mioyo ywa watu Masikini na waliokata tamaa
Ni jambo la Kushangaza kuwa Mungu anawaangalia sana wanyonge masikini na waliokata tamaa wakati dunia haijali na mfumo wa dunia hauwajali watu masikini Mungu aliwapa neema watu duni, walikuwa hawana ujuzi wa maandiko wala hawako karibu na ikulu, na huenda walikuwa wamejikatia tamaa Mungu aliwatuma malaika zake kutoa habari maalumu kwa kundi hili kuwa masihi amezaliwa

Luka 2:8-20 Biblia inasema hivi “8. Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. 10. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11. maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. 13. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, 14. Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. 15. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. 16. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. 17. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 18. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 19.Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 20. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa”. Ni jambo la kushangaza kabisa kuwa malaika aliwaambia wachungaji hao kuwa Leo hii katika mji wa Daudi amezaliwa kwaajili yenu Mwokozi ndiye Kristo Bwana natamani kabisa Mungu angenifanya maalumu kama wachungaji hawa ni watu wanyenyekevu wenye mioyo iliyopondeka hawakuwa na ujuzi wa neno hawakuwa wanasiasa lakini Mungu hakuwanyima vyote aliwapa habari njema na hili likawa kundi la kwanza kwenda Bethelehemu na kujionea kundi hili likatoa habari ya kuzaliwa kwake Yesu kristo na kushangaza watu, hii ndio ilikuwa iwe kazi ya makuhani lakini mioyo yao iliwanyima kumjua masihi mioyo iliyopondeka aidha hawa waliishuhudia kundi la malaika wakiimba kwa furaha na kumtukuza Mungu kuhusu kuzaliwa kwa masihi mwe Mungu ni Mungu wa waliotupwa wanyonge na waliohesabika kuwa si kitu, Mungu huwapinga wajikwezao bali huwapa neema wanyenyekevu.

5.       Mioyo ya watu wenye subira.

Kundi hili linawakilishwa na Simeon na Anna Binti Fanuel Simeon alikuwa mtu Mcha Mungu na nabii alikuwa mwenye haki na alikuwa akisubiri kwa shauku kuzaliwa kwa masihi alikuwa ni mzee mmno lakini Roho Mtakatifu alikuwa amemwambia kuwa hatakufa mpaka amemwona masihi, huyu alikuwa mtu mvumilivu umri wake ulikuwa umekwenda lakini bado alikuwa akiutazamia ukombozi, alipomuona masihi Roho Mtakatifu alimuonyesha wazi habari za Mtoto huyo kule hekaluni na sasa alifurahi na kutoa unabii kuhusu Mateso ya Yesu lakini sasa alikuwa tayari kufa kwa amani kwa vile Mungu alikuwa amemtimizia ahadi, Anna binti Fanuel mjane alikaa ujane miaka 84 aliishi na mume miaka 7 tu alidumu katika maombi mwanamke huyu pia alikuwa nabii yeye naye aliwaeleza wazi wote waliokuwa wakisubiria habari zake na kuwathibitishia kuwa huyu ni masihi
Luka 2 25-38 “ 25. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 27. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, 28. yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, 29. Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; 30. Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, 31. Uliouweka tayari machoni pa watu wote; 32. Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. 33. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. 34. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. 35. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. 36. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 37. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. 38. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.  Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuwa mtu mwenye subira na mwenye uvumilivu huku tukimtazamia masihi bila shaka hatuataibika atakapofunuliwa Bwana wakati wa kuja kwake mara ya pili, watu wa rohoni kama ilivyo kwa Simeon na Anna wataelewa wazi Kristo atakapokuja na halitakuwa fumbo kwao hawa walikuwana mioyo yenye kusubiri

6.       Mioyo ya watu wasiotegemewa.

Kundi hili linawakilishwa na jamii ya Mamajusi hili nimeliita kundi la watu wasiotegemewa kwa vile hawakuwa wanamjua Mungu kabisa, hawakuwa na ujuzi wa neno la Mungu, walitokea nchi ya mbali sana na ndio watu wa kwanza kugundua kuwa Kuna Mfalme mkubwa sana wa Wayahudi amezaliwa na kwa vile wafalme huzaliwa ikulu walisafiri kutoka Ukaldayo au mashariki ya mbali yaani Iraq kwa kuchunguza nyota mpaka wakagundua kuwa masihi amezaliwa,\

Ni muhimu kufahamu kuwa watu hawa walijulikana kama watu wenye Hekima na walikuwa ni watu wenye ujuzi na maswala ya nyota yaani wanajimu walihusika na maswala ya uchawi pia Daniel 2: 2 huko ukaldayo kulipotokea jambo gumu sana wao zamani walikuwa ni watu waliotegemewa kutoa majibu Daniel 2: 2 inasema hiviNdipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme.” Wakristo wengi na wataalamu wa maandiko hufikiri nkuwa Mamajusi walikuwa watu wazuri na watakatifu Hapana lilikuwa ni kundi la Waganga, wachawi na wasihiri yaani wapiga lamri hawa sasa walikuwa wanajimu kama ilivyokuwa kwa Marehemu Yahaya Husein kwa hapa Afrika mashariki ndio maana hili ni kundi la watu wasiotegemewa Mungu aliruhusu katika ufahamu wao na unajimu wao kuona Nyota iliyomuhusu Masihi na kwa moyo waliokuwa nao walijua kuwa wanapaswa kumsujudia na kumuabudu na cha kushangaza zaidi ni kuwa Mungu alisema nao na kuwaonya wasiende kwa Herode maana anataka kumuua mtoto nao wakarudi kwao kwa njia nyingine 

Mathayo 2:10-12 10. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. 11. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. 12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.”

Ni wazi kuwa kundi hili linawakilisha watu watakaoingia katika Ufalme wa Mungu bila sisi kuwatarajia, Mungu haukumu wala hatazami kama wanadamu watazamavyo, sikun ya hukumu na katika ufalme wa Mungu tunaweza kabisa kushangaa wale tunaowadhani ndio wakawa sio na wale tunawadhani sio wakawa ndiyo, Mioyo iliyopondeka Mungu huiangalia sana , unyonge na kutokujihesabia haki ni wazi kuwa kama  mioyo yetu itafanana na makundi makuu matatu ya awali tunaweza tukajikuta tumekataliwa katika ufalme wa Mungu, ni jukumu letu kuangalia na kujiangalia na kujipima namna tunavyoeneda ni mioyo ya makundi matatuya mwisho ndio ambao waliweza kupata nafasi ya kumuadudu Yesu yani kusheherekea CHRISTMAS jihoji je wewe utaweza kuisherekea siku hii na unaisheherekea katika mkao upi wa Moyo?

Ujumbe. Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: