Jumanne, 21 Juni 2016

Mti wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu!



Waamuzi 9:8 – 13. Biblia inasema hivi:- 

“8. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. 9. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 10. Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. 11. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? 12. Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. 13. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?” 

Leo tutachukua muda kutafakari kwa kina na upana na marefu kuhusu mti wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu, Ninazungumza jambo muhimu sana litakaloifaa jamii ya leo ambayo imejaa watu wanaoteseka kwa kukosa maarifa, kama utafuatilia somo hili kwa moyo maisha yako yatabadilika na utakuwa na furaha maishani mwako, Leo nataka kuzungumzia kuhuzu mti wa Mzeituni (Olive Tree) lakini kwanza nataka ufahamu jambo hili

Mwanzo kabisa Mungu alipouumba ulimwengu alitoa zawadi ya mimea na miche pamoja na miti kwa wanadamu kama chakula na zawadi soma Mwanzo 1:29 “ biblia inasema 

29. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; 30. na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. 
  
Miche na miti katika biblia ya kiingereza huitwa Herbs tuangalie Biblia ya Kiingereza tafasiri ya King James Bible inasema:-

"And God said, Behold, I have given you every herb bearing seed, which is upon the face of all the earth, and every tree, in the which is the fruit of a tree yielding seed; to you it shall be foe meal"

Ni wazi kuwa miti na mimea ndio chakula cha kwanza walichopewa wanadamu kabla ya kuongezewa nyama katika Mwanzo 9:3 baada ya gharika wakati wa Nuhu, Moja ya mti muhimu sana unaotajwa katika Biblia ni mti wa Mzeituni na tunda la zeituni na mafuta ya mzeituni huu ni moja ya mti muhimu sana katika uumbaji wa Mungu, Wayahudi na waarabu na wakristo wa zamani sana walifahamu sana umuhimu wa mmea wa mzeituni ukilinganisha na nyakati tulizonazo katika kizazi hiki, ni kwasababu hiyo leo Mkuu wa wajenzi ninataka kuchukua muda kueleza maswala kadhaa muhimu kuhusu mti huu wenye kuleta Heshima kwa Mungu na wanadamu.

Mmea wa Mzeituni ni mmea unaomea kwa wingi sana katika nchi ya Israel, Hata leo, mashamba ya mizeituni yametapakaa kutoka sehemu za chini ya Mlima Hermoni upande wa kaskazini hadi viunga vya Beersheba upande wa kusini. Mizeituni bado inapatikana kwenye pwani ya Uwanda wa Sharoni, vilima vyenye mawemawe vya Samaria, na mabonde yenye rutuba ya Galilaya lakini pia ni mmea unaostawi na kuzalishwa kwa wingi katika inchi ya Hispania (Spain) Nchi hii kwa sasa ndio inayoongoza kwa uzalishaji wa Mafuta ya Mzeituni na sehemu nyingine nyingi duniani, Mungu ameupa mmea huu uwezo wa ajabu sana kama tutakavyoweza kuona mbeleni lakini pia mmea huu kwa tabia zake ni mmea ambao hauwezi kuharibiwa,Unapoukata mzeituni unauwezo wa kutoa machipukizi mapya na ukaendelea kuwepo mara moja, Matunda yake yanauwezo wa kutoa au kuzalisha mafuta mengi ambayo hutumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupikia, kujipaka, kuwashia taa, na kutibu wanadamu, katika shughuli za Ibada mmea huu ni mmea wa kikuhani kwa vile unatumika kutangaza rehema za Mungu na unatumiwa katika ishara ya amani, kuweka wakfu viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini yaani Wafalme, Makuhani na manabii. Aidha mti huu mafuta yake na matawi yake hutumika katika kufukuza Mapepo (Mashetani na Majini) kwa jina la Yesu.

Katika kuwatia Moyo Israel katika safari yao ya kwenda Kanaani moja ya vitu vyenye mvuto sana kwa wana wa Israel ambavyo Mungu alimtumia Musa kuvitaja ilikuwa ni pamoja na Mizeituni yenye mafuta.  Kumbukumbu 8:7-8 biblia inasema 

7. Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; 8. nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;

·         Sifa za Mzeituni
·         Historia ya Kibiblia kuhusu Mzeituni
·         Matumizi ya Mzeituni

Sifa za Mzeituni.

Kwa kawaida Mzeituni ni mti usio na Mvuto ukiuona kwa mara ya kwanza. Si mrefu kama mierezi fulani yenye kuvutia ya Lebanoni. Mbao zake hazina thamani kama mbao za mberoshi, na maua yake hayavutii kama maua ya mlozi ambayo ilitumika kujengea Nyumba katika Israel kama maandiko yasemavyo katika wimbo ulio bora 

Wimbo Ulio bora 1:17 Biblia inasema hivi:- “Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi”. Na Amosi 2:9 9. “Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini”.

Sehemu muhimu zaidi ya mzeituni haionekani—iko chini ya ardhi. Mizizi yake mingi, ambayo hufikia kina cha meta sita chini ya ardhi na kwenda hata mbali zaidi kuelekea upande-upande, ndiyo hasa hufanya mti huo uzae sana na kustahimili hali ngumu.

Mizizi hiyo huiwezesha mizeituni kwenye vilima vyenye mawemawe istahimili ukame wakati ambapo miti iliyo kwenye bonde imekwisha kauka kwa kukosa maji. Mizizi huiwezesha kuendelea kuzaa zeituni kwa karne nyingi, ingawa huenda shina lisilovutia likaonekana kuwa lafaa tu kwa kuni. Mti huo usiovutia huhitaji tu nafasi ya kukua na udongo wenye hewa, bila magugu au mimea mingine inayoweza kuwa na wadudu waharibifu. Mahitaji hayo sahili yakitimizwa, mti mmoja utatoa lita 57 za mafuta kila mwaka.

Historia ya Kibiblia kuhusu Mzeituni.

Kibiblia Mzeituni unatajwa kwa mara ya kwanza katika Kitabu cha Mwanzo 8:6-12 “6. Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 7. akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. 8. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 9. bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. 10. Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, 11. njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. 12. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.”

Mzeituni unatajwa kama mti ulioashiria amani baada ya Hasira za Mungu alipoangamiza dunia kwa maji, Nuhu alituma ndege Kunguru ambaye alizurura bila kutoa ripoti na njiwa ambaye alirejea na kijitawi cha jani la mzeituni Tangu wakati huu mzeituni ulipata umaarufu mkubwa sana na kitendo cha njiwa kurudi na Jani bichi la Mzeituni kinywani mwake kuliashiria taarifa ya amani kwa Nuhu na familia yake.

Alama ya “V” ya vidole inayotumika sehemu nyingi sana Duniani ni matokeo ya njiwa huyu aliyekuja na jani la mzeituni katika safina, aidha matumizi ya tawi la mzeituni kama alama ya AMANI/shalom/salaam, yalitumika sana na watu wa Magharibi Karne tano hivi kabla ya Kristo, Wayunani wa kale waliutumia mti huu, kama alama ya uzao na masimulizi na historia zinaonyesha pia waliutumia kufukuzia pepo wachafu, kwa jina la mungu aliyejulikana kama Eirene au Irene ambayo maana yake ni Shalom/Salaam au amani, wapagani wa Kirumi pia walitumia matawi ya Mzeituni kumaanisha mungu mke wa amani ambaye alijulikana kama PAX na katika Coins za zamani za Kirumi iliwekwa nyuma ya fedha maana hizi hazitofautiani sana na maana ya asili iliyotumiwa na waandishi wa Biblia.


Fedha ya zamani sana (Coin) ya Kirumi ikiwa na tawi la Mzeituni

Mara nyingi waandishi wa Biblia walitumia mzeituni kama mfano. Sehemu mbalimbali za mzeituni zilitumika kufananisha rehema ya Mungu, ahadi ya ufufuo, na maisha ya familia yenye furaha. Kuuchunguza mzeituni kwa makini kutatusaidia kuelewa marejeo hayo ya Kimaandiko na kutafanya tuuthamini sana mti huu wa pekee ambao pamoja na uumbaji mwingine wote, ni moja ya mti wenye matunda unaofanya kazi ya kumsifu Mungu Zaburi 148:7,9.

Matumizi ya Mzeituni na Mafuta ya Mzeituni.

Bila shaka, zeituni zilipendwa sana na Waisraeli kwa sababu ya mafuta yake yenye thamani. Walitumia katika nyumba zao taa zenye tambi zilizotumia mafuta ya zeituni. Pia Mungu aliagiza wana wa Israel kuleta mafuta ya mzeituni kwaajili ya Taa yenye vinara saba iliyopaswa kuwaka Daima katika nyumba ya Mungu.


Taa yenye vinara Saba iliwaka katika nyumba ya Bwana Daima ikitumia Mafuta ya Mzeituni

Mambo ya walawi 24:2 “1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2. Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 3. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.”

Mafuta ya zeituni yalikuwa muhimu katika upishi. Yalikinga ngozi dhidi ya miali ya jua, na Waisraeli waliyatumia kutengenezea sabuni. Mazao muhimu ya nchi yalikuwa nafaka, divai, na zeituni. Hivyo, ungekuwa msiba mkubwa kwa familia ya Waisraeli mizeituni ikikosa kuzaa.

Kumbukumbu la Torati 7:13 Biblia inasema. “naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.” Kubarikiwa kwa Divai na Mafuta yanayotajwa hapo ni Mafuta ya Mzeituni Habakuki 3:17 Ilikuwa ni laana nzito ni adhabu kama Bwana ataipiga nchi kiasi cha kufikia Mzeituni kuzaa kwa shida “Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;”
 
Hata hivyo, kwa kawaida mafuta ya zeituni yalikuwa mengi. Yaelekea kwamba Musa aliliita Bara Lililoahidiwa ‘nchi ya zeituni’ kwa sababu mizeituni ilipandwa kwa wingi sana katika eneo hilo. Mtaalamu wa mambo ya asili, H. B. Tristram, wa karne ya 19 aliutaja mzeituni kuwa “mti wa kawaida wa nchi ya Kanaani yaani Israel.” Kwa sababu ya thamani yake na wingi wake, mafuta ya zeituni yalitumika katika eneo lote la Mediterania yakiwa kama fedha ya kimataifa. Yesu Kristo mwenyewe alitaja deni ambalo lilikadiriwa kuwa “vipimo mia vya bathi vya mafuta ya mzeituni.” Luka 16:5-6 “5.Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? 6. Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini”.

“Baraka kuu zililinganishwa Kama Miche ya Mizeituni”

Mzeituni wenye mafaa ni mfano ufaao wa baraka za Mungu. Mtu anayemcha Mungu angethawabishwaje? “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako,” mtunga-zaburi akaimba. “Wanao kama miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako.” Zaburi128:3Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako”.“Miche ya mizeituni” ni nini, na kwa nini mtunga-zaburi anailinganisha na wana?

Mzeituni ni wa pekee kwa kuwa machipukizi mapya huchipuka daima kutoka kwenye shina lake. Wakati shina kuu liachapo kuzaa kama zamani kwa sababu ya uzee, wakulima wanaweza kuacha miche au machipukizi mapya yakue na kuwa sehemu muhimu ya mti huo. Baada ya muda, mti wa awali utazungukwa na mashina machanga matatu au manne yenye nguvu, kama wana wanaoizunguka meza. Miche hiyo inatumia mzizi uleule, nayo hutoa mazao mazuri ya zeituni.
Hali hiyo ya mzeituni ni mfano ufaao wa jinsi imani ya wana na binti iwezavyo kuwa thabiti kwa sababu ya mizizi ya kiroho yenye nguvu ya wazazi wao. Watoto wakuapo, wao vilevile huzaa matunda na kuwategemeza wazazi wao, ambao hufurahi kuona watoto wao wakimtumikia Mungu pamoja nao. Mithali 15:20
 
“Mzeituni Unafundisha kuwa Yako Matumaini ”

Baba mzee-mzee anayemtumikia Mungu hupendezwa na watoto wake wenye kumcha Mungu. Lakini watoto haohao huomboleza wakati hatimaye baba yao ‘anapoenda njia ya ulimwengu wote.’ (1Wafalme 2:2). Ili kutusaidia kuvumilia msiba kama huo wa familia, Biblia hutuhakikishia kwamba kutakuwa na ufufuo. Yohana 5:28-29, 11:25

Aubu, aliyekuwa baba ya watoto wengi, alifahamu vizuri kwamba maisha ya mwanadamu ni mafupi. Aliyalinganisha na maua ambayo hunyauka upesi.  (Ayubu 1:2, 14:1,2). Ayubu alitamani sana kufa ili aepuke maumivu, akiliona kaburi kuwa mahali pa kujificha ambapo angeweza kutoka. “Mtu akifa, je! atakuwa hai tena?” Ayubu akauliza. Kisha kwa uhakika akajibu: “Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie. Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.”Ayubu 14:13-15

Ayubu alionyeshaje imani kwamba Mungu angemwita kutoka kaburini? Kwa kutumia mti ambao kutokana na jinsi anavyoufafanua, yaelekea ni mzeituni. “Yako matumaini ya mti,” Yobu akasema. “Ya kuwa ukikatwa utachipuka tena.” Ayubu 14:7 Mzeituni unaweza kukatwa, lakini kufanya hivyo hakutauharibu. Utakufa tu uking’olewa. Mizizi isipong’olewa, huo mti utachipuka tena ukiwa na nguvu mpya.

Hata ikiwa ukame wa muda mrefu unanyaukisha mzeituni wa zamani, shina lililonyauka laweza kuchipuka tena. “Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, na shina lake kufa katika udongo; lakini kwa harufu ya maji utachipuka, na kutoa matawi kama mche.” Ayubu 14:8-9 Ayubu aliishi katika nchi kavu na yenye vumbi ambako yaelekea aliona mashina mengi ya mizeituni iliyozeeka ambayo yalionekana yamenyauka na bila uhai. Hata hivyo, mvua iliponyesha mti huo “mfu” ulichipuka tena na mizizi yake kutoa shina jipya kana kwamba ni “mche.” Uwezo huo wa kipekee wa kuchipuka tena ulifanya mkulima mmoja wa bustani wa Tunisia aseme: “Kwa kweli mizeituni haiwezi kufa.”

Kama vile mkulima anavyotamani kuona mizeituni yake iliyonyauka ikichipuka tena, ndivyo Mungu anavyotamani kufufua watumishi wake waaminifu. Anangojea kwa hamu wakati ambapo watu waaminifu kama Abrahamu na Sara, Isaka na Rebeka, na wengine wengi watafufuliwa. Mathayo 22:31-32 Itakuwa ajabu kama nini kuwakaribisha wafu na kuwaona wakiishi tena maisha kamili yenye manufaa!

Mzeituni wa Mfano
Sifa ya Mungu ya kutobagua na pia uandalizi wake wa ufufuo hudhihirisha rehema yake. Mtume Paulo alitumia mzeituni kuonyesha jinsi ambavyo Yehova huwarehemu watu bila kujali rangi au malezi yao. Kwa karne nyingi Wayahudi walijivunia kuwa wachaguliwa wa Mungu, “uzao wa Abrahamu.” Yohana 8:33, Luka 3:8
 
Haikuwa lazima uwe mzaliwa wa taifa la Kiyahudi ili kupata kibali cha Mungu. Hata hivyo, wanafunzi wote wa kwanza wa Yesu walikuwa Wayahudi, na walikuwa na pendeleo la kuwa wanadamu wa kwanza kuteuliwa na Mungu kufanyiza mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa Mwanzo 22:18 Wagalatia 3:29. Paulo aliwalinganisha wanafunzi hao Wayahudi na matawi ya mzeituni wa mfano.



Wengi wa Wayahudi wa asili walimkataa Yesu, wakijinyima pendeleo la kuwa washiriki wa “kundi dogo,” au “Israeli wa Mungu.” Luka 12:32: Wagalatia 6:16 Hivyo wakawa kama matawi ya mzeituni wa mfano yaliyokatwa. Ni nani wangechukua mahali pao? Mwaka wa 36 Baada ya Kristo., wasio Wayahudi walichaguliwa kuwa sehemu ya mbegu ya Abrahamu. Ilikuwa kana kwamba Yehova alipandikiza matawi ya mzeituni-mwitu kwenye mzeituni wa bustani. Wale ambao wangefanyiza mbegu ya Abrahamu iliyoahidiwa wangetia ndani watu wa mataifa. Wakristo wasio Wayahudi sasa wangeweza kuwa ‘washiriki wa mzizi wa unono wa mzeituni.’Warumi 11:17

Lingekuwa jambo lisilowazika na lililo “kinyume cha asili” kwa mkulima kupandikiza tawi la mzeituni-mwitu kwenye mzeituni wa bustani.  Warumi 11:24 “Pandikiza mti mzuri kwenye mti wa mwituni, na, kama vile Waarabu wasemavyo, ule mzuri utashinda ule wa mwituni,” chaeleza kitabu The Land and the Book, “lakini huwezi kupandikiza mti wa mwituni kwa mti mzuri ukafanikiwe.” Wakristo Wayahudi hali kadhalika walishangaa wakati ambapo Yehova ‘kwa mara ya kwanza alielekeza uangalifu wake kwa mataifa ili achukue kutoka kwayo watu kwa ajili ya jina lake.’ Matendo 10:44-48, 15:14 Hata hivyo, hiyo ilikuwa ishara ya wazi kwamba kutimizwa kwa kusudi la Mungu hakukutegemea taifa moja tu. La, kwa kuwa “katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.” Matendo 10:35

Paulo alionyesha kwamba kwa kuwa “matawi” ya mzeituni ya Wayahudi wasio waaminifu yalikatwa, mtu yeyote aweza kukatwa vivyo hivyo akikosa upendeleo wa Yehova kwa sababu ya kiburi na kutotii. Warumi 11:19,20 Kwa kweli jambo hilo laonyesha kwamba hatupaswi kupuuza fadhili isiyostahiliwa ya Mungu 2Wakoritho 6:1.


Kupaka Mafuta kwa Maombezi ya Mgonjwa

Maandiko yanarejezea kihalisi na kwa mfano matumizi ya mafuta ya zeituni. Zamani, majeraha na machubuko ‘yalilainishwa kwa mafuta’ ili yapone haraka. Isaya 1:6 Kulingana na mojawapo ya mifano ya Yesu, Msamaria aliyekuwa jirani mwema alipaka mafuta ya zeituni na divai kwenye majeraha ya mtu aliyemkuta kwenye barabara ya kwenda Yeriko Luka 10:34.

Mtu huburudika na kupata kitulizo apakapo mafuta ya zeituni kichwani. Zaburi 141:5  Wazee Wakristo wanaweza ‘kumpaka mafuta mtu ambaye hawezi wanaposhughulika na ugonjwa wa mwili na kiroho.na Kuomba kwa Jina la Yesu Yakobo 5:14 Ushauri wenye upendo wa wazee unaotokana na Maandiko na sala zao za kutoka moyoni kwa niaba ya mwamini mwenzao aliye mgonjwa kiroho zinalinganishwa na mafuta ya zeituni yenye kutuliza. Yapendeza kwamba kuna usemi wa Kiebrania ambao wakati mwingine humwita mtu mzuri “mafuta safi ya zeituni.”



‘Mzeituni Unaostawi Katika Nyumba ya Mungu’

Kwa kuzingatia mambo ambayo yametajwa, si ajabu kwamba watumishi wa Mungu wanaweza kulinganishwa na mizeituni. Daudi alitamani kuwa kama “mzeituni mbichi, unaostawi katika nyumba ya Mungu.”  Zaburi 52:8Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.” Kama vile mara nyingi familia za Waisraeli zilivyokuwa na mizeituni iliyozingira nyumba zao, vivyo hivyo Daudi alitaka kuwa karibu na Mungu na kuzaa matunda kwa sifa ya Mungu.

Ufalme wa Yuda wa makabila mawili ulikuwa kama “mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema” wakati walipokuwa waminifu kwa Mungu. Yeremia 11:15-1815. Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha. 16. Bwana alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika. 17. Kwa maana Bwana wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba. 18. Tena Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao.” Lakini watu wa Yuda na Israel walipoteza hali hiyo ya kupendelewa ‘walipokataa kusikia maneno ya Mungu; wakafuata miungu mingine. Yeremia 11:10 “Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.”

Ili kuwa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, ni lazima tumtii Mungu na kuwa tayari kukubali nidhamu ambayo yeye hutumia “kutupogoa” ili tuweze kuzaa matunda zaidi ya Kikristo.Waebrania 12:5-6 Isitoshe, kama vile mzeituni wa kawaida huhitaji mizizi mingi ili kustahimili ukame, twahitaji kuimarisha mizizi yetu ya kiroho kusudi tuvumilie majaribu na mnyanyaso Mathayo 13:21, Wakolosai 2:6-7.

Mzeituni unafananisha vizuri na Mkristo mwaminifu, ambaye huenda asijulikane katika ulimwengu bali anatambuliwa na Mungu. Mtu kama huyo akifa katika mfumo huu, ataishi tena katika ulimwengu mpya unaokuja. 2Wakoritho 6:9, 2Petro 3:13.

Mzeituni ambao ni kama hauwezi kuharibiwa, ambao huendelea kuzaa matunda mwaka baada ya mwaka watukumbusha ahadi hii ya Mungu: “Kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.” Isaya 65:22 Ahadi hiyo ya kiunabii itatimizwa katika ulimwengu mpya wa Mungu 2Petro 3:13.

Jinsi ya Kutumia Mafuta ya Mzeituni kwa shughuli (Mahitaji) Mbalimbali.

1.      Kuweka wakfu Kiongozi Mafuta ya mzeituni hutumika wakati wa kumuweka wakfu Kiongozi wa Kisiasa, Kidini na kijamii, Katika Israel Nabii, Mfalme na Kuhani waliwekwa wakfu kwa ibada maalumu na kupakwa mafuta unapompaka mtu mafuta kwa mujibu wa nafasi aliyo nayo utatangaza kupitia neno la Mungu Je Bwana Hakukupaka Mafuta Ili………………..(Unaeleza Kusudi la kumpaka mafuta hayo) kisha unamiminia na kumuombea neema kwaajili ya kazi hiyo kupitia Jina la Yesu Mfano 1Samuel 10:1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta akayamimina kichwani pake akambusu akasema Je Bwana hakukutia mafuta [Uwe mkuu juu ya watu wake Israel? Nawe utawamiliki watu wa Bwana na kuwaokoa na mikono ya adui zao kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia Mafuta ] uwe mkuu juu ya urithi wake” Unapompaka mafuta kiongozi lazima utangaze kusudi la kupakwa kwake mafuta nay ale yatakayonenwa yatampata.Kama anayepakwa Mafuta ni Mchungaji , Kuhani padre au nabii utasoma Kutoka 29:7 na kumuombea nneema ya majukumu yake na kumpaka mafuta,

 Ibada ya kumpaka mtu mafuta yaweza kufanyika hata Faragha
2.      Ikiwa unahitaji Mafuta haya kwaajili ya kumpokea Roho Mtakatifu utasoma Luka 4:18-19 pia 1Samuel 16:13 kisha ingia katika maombi ya kuhitaji kujazwa Roho mtakatifu na utashangaa nguzu za Mungu zitakushukia na utaanza kusema kwa lugha nyingine
3.      Ikiwa unatumia mafuta kwaajili ya kuondoa msongo wa mawazo, kujilinda na maadui wa kibinadamu na mashetani utachukua mafuta ya mzeituni utasoma Zaburi ya 23 yote na kisha utajipaka au utampaka mtu mwenye stresses Msongo wa mawazo na kisha utaomba neema na rehema huku ukiyasambaza mafuta hayo katika upaji wa uso kwa kutumia jina la Yesu na mtu huyo atapokea amani na furaha tangu wakati huo
4.      Ikiwa ni kwaajili ya kuombea Mgonjwa ambaye hawezi utachukua kichupa cha mafuta ya mzeituni, utaongena na mgonjwa na kumtia moyo na kumfariji kisha utasoma pamoja naye Yakobo 5:14-15 na Marko 16:17-18
5.      Ikiwa ni kwaajili ya kukemea vifungo vya shetani ba kutoa pepo chukua mafuta ya mzeituni kisha soma maandiko yafuatayo na weka mkono wako juu ya mtu mwenye pepo omba rehema kwaajili yake na kukemea kwa jina la Yesu Luka 4:18-19, na Marko 16:17-18
6.      Ikiwa ni kwaajili ya kujilinda na maadui wa aina yoyote yaani wakimwili na kiroho jipake mafuta ya mzeituni na kabla ya kujipaka utasoma maandiko haya kisha utajipaka na kujiombea au kumuombea mwenye uhitaji huo Zaburi 27:1-6, 1Samuel 2:10
7.      Ikiwa ni kwaajili ya nguvu za kiume au za kike utajipaka mafuta hayo ya mzeituni wakati unapokuwa unakwenda kulala katika sehemu ya via vya uzazi kisha utaomba kisha utaisema Zaburi ya 103:1-5 utasubiri kwa dakika tano nguvu zitakushukia kufurahia uumbaji wa Mungu
8.      Kwaajili ya kujitibu Mafua utajipaka katika eneo la pua na tundu zake mara tatu kwa siku ukitumia Marko 16:17
9.      Kwaajili ya kuua wadudu wabaya walioko tumboni utayaombea mafuta hayo na kunywa kijiko cha chai 1X2 kwa siku kwa mfululizo siku saba Marko 16:17-18
10.  Kwaajili ya kutunza kumbukumbu na kuponya ugonjwa wa kusahau chukua mafuta ya zeituni jipake katika paji la uso soma Zaburi ya 103:1-5 kisha muombe Mungu kwa jina la Yesu na utakuwa wa ajabu
11.  Kwa mtu alitepooza atachua eneo lililopooza mara mbili kila siku, mwenye pepo la Degedege atapaka mwili mzima kwa siku mara mbili maombi yatatangulia na Marko 16:17-18 itasomwana kuomba katika jina la Yesu
12.  Kwaajili ya kutunza Ngozi isizeeke kuondoia mikunjo, kuondoa alama za kuungua na jua, kukinga mionzi ya jua kulainisha mishipa, kukinga na saratani ya ngozi, kupambana na sumu kwenye ngozikilinda ngozi kupatwa na sumu,kuondoa mabaka kuondoa ukavu kwenye ngozi soma Zaburi 103:1-5 kisha omba nap aka mafuta haya mwili mzima kama mafuta ya kawaida hutazeeka haraka
13.  Ikiwa una kesi na hoja ngumu zinakukabili Mahakamani soma Isaya 54:17 kisha fanya maombi ya ushindi na ujasiri jipake mafuta ya mzeituni Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya 

14.  Mafuta ya Mzeituni yanaweza kutumika hata kwa kuukanda mwili Massaging na kusababisha mwili ku- relax kupata ahueni nakuondoa uchovu. Pia mizeituni huleta usingizi mzuri  
15. Mafuta ya mzeituni yanaweza pia kutumika kwa kuvunjia mikataba ya aina mbalimbali yaani nira na maagano ambayo ulijiingiza na kama unataka kujikomboa 
Mafuta ya Mizeituni hupatikana katika maduka mbalimbali supermarket, na sehemu nyinginezo kumbuka ni muhimu kupata mafuta Original na sio yaliyochanganyika na kitu kwa vila mengine utaweza kula, kujipaka na kadhalika huitaji msaada wa Mchungaji au kiongozi wa dini kuona matokeo ya mizeituni zaidi ya kujifunza, kuamini na kutendea kazi.


Matumizi ya neno la Mungu na mafuta yanaweza kutumika katika maeneo mengi zaidi ya haya itategemea na ufunuo wako na maandiko utakayoweza kuyatumia utayatumia kulingana nauhitaji wako, Hakuna utata wa kimaandiko kuhusu matumizi ya mafuta,sio lazima upewe na manabii au Mchungaji kanunue mwenyewe hata ndoo nzima kwa matumizi yako ingawa mafuta haya ni ghali, kwa muda mrefu sana nilimtumikia Mungu na kuombea watu bila ya matumizi ya mafuta, sikupanda kabisa kutaka kuyatumia, kwa zaidi ya miaka 20 ya kumtumikia Mungu sikutaka kuamini katika swala hili, nilisubiri kupata ufunuo kamili wa swala hili na dhamiri yangu kuhusu matumizi ya mafuta na Mungu aliponithibitishia kuwa Inatenda kazi naliona vema kama mkuu wa wajenzi kuweka fundisho hili wazi, Jambo kubwa la msingi usiyatumia mafuta kama Biashara, wala usiyatumie kama uganga bali yatumia kwa imani na maombi na neno la Mungu na utaweza kuona Mafanikio, Kwa maandiko zaidi kuhusu Mafuta katika Biblia soma mistari kadhaa ifuatayo:-

Kutoka 25:6, 29:7, 29:2, 29:29,30:3,22-26,40:9, 40:15,  Walawi.8:10,8:12,4:3,5,16,6:20, 
Zaburi.132:10,1Sam.16:13,2Sam.24:4,1Nyakati.16:22;Zab.105:15,1Wafalme-19:16 1Nyakati.16:22Zab.105:15, Isa. 21:5,Luke 7:38-40, Kumb. 28:40, Ruth 3:3,2Samuel 14:2,
Zab.104:15, 109:18, Isaiah 1:6,Mark 6:13, Yakobo. 5:14, Mark 14:8,Luka. 23:56, Zab. 2:2; 
Dan. 9:25, 26, 
Isa. 61:1, Zab. 45:7; Heb. 1:9, John 1:41; Mdo. 9:22; 17:2, 3; 18:5, 28, 1 Yoh. 2:20, Matt. 25:1-13
 

Maoni 7 :

Unknown alisema ...

Nimepata kitu

Bila jina alisema ...

barikiwa sana nimeongeza maarifa nitatumia ii nakala kwa kuwa najiombeazaidi amina

Unknown alisema ...

Barikiwa sana, nimejifunza kitu

Unknown alisema ...

Asantee san

Mtume NYEWE alisema ...


Nimebarikiwa sana na nimefurahi ufafanuzi natamka MUNGU akuinue na akutumie zaidi wewe na uzawa wako akupe baraka in je sus mighty name

Bila jina alisema ...

Naitaji mafuta hayo original

Bila jina alisema ...

Nimepanda mche wa mzeituni hapa nyumbani kwangu toka mwezi March 2023.Mche unaendelea kukua vizuri. Nitarajie matunda baada ya muda gani?