Ayubu 42:1 “Ndipo Ayubu
akamjibu BWANA na Kusema Najua ya kuwa waweza Kufanya Mambo yote Na ya makusudi yakohayawezi kuzuilika.”
Ayubu alielewa Kuwa makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika
Watu wengi sana Duniani wanaishi
Maisha ya huzuni na kukata tamaa kwa sababu ya kutokuwa na ujuzi wa kutosha
kuhusu Mungu na makusudi ya Mungu katika maisha yao, Na huuzunika zaidi
wanapopitia katika Magumu, masumbufu na Mateso ya aina mbalimbali wakati
mwingine ikiwa ni magonjwa, kuchukiwa na hata kutendewa mambo mabaya au kupatwa
na Mabaya, Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika mambo yoote (Mema au mabaya)
anaweza kuyatumia katika kutimiza Mpango wake mwema katika maisha Yetu.
Warumi 8:28 “ Nasi twajua ya
kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia
mema yaani wale walioitwa kwa kusudi lake”
Andiko la msingi linatoka katika
kitabu cha Ayubu ni kitabu cha kifalsafa kinachojadili dhana kuhusu Mateso kwa
wanadamu na Mtazamo wa Mungu, wote tunajua kuwa Ayubu alipatwa na Mateso na
mitihani migumu ya kupita kawaida, Muda Hautoshi kuangalia ni hasara gani na
mateso gani aliyapitia, lakini wote tunajua kuwa Ayubu hakutenda dhambi, na
hata kama angetenda Mungu ni wa rehema na hawezi kutulipa mabaya kwa sababu ya
ubaya wetu, Rafiki za Ayubu walimlaumu Ayubu na kumtetea Mungu walionyesha wazi
kuwa haiwezekani Mateso hayo yampate Ayubu kama Ayubu hakuwa na Makosa, aidha
Ayubu alijitetea sana kuwa hakuna makosa aliyoyafanya, Ayubu ingawa hakufanya dhambi
lakini alimlaumu Mungu katika kiwango cha kufikia kuonyesha Kiburi na kuonyesha
kuwa Mungu hayuko sawa, ni kama alikuwa akimhoji Mungu kwa nini niyapitia haya
Kutokana na majibu ya Mungu kwa
Ayubu hatimaye Ayubu alitambua
1.
Mungu huruhusu mambo yote
yatupate kwa makusudi yake mema
2.
Kila jambo ambalo Mungu uliruhusu
litokee katika maisha yetu katika hekima yake Mungu huruhusu kwa makusudi
3.
Hata mateso ya Mwanadamu na
mapito magumu yana maana katika kusudi la Mungu
Kwa sababu hiyo basi ni muhimu
kwetu kuamini kuwa Mungu anaweza kufanya mambo yote, Kuamini kuwa kama
tunatembea katika Makusudi ya Mungu basi hakuna cha kutuzuia, wala mtu wa
kuzuia kusudi la Mungu kwetu katika maisha yetu.
Ni muhimu kwetu tu kutambua
makusudi ya Mungu katika maisha yetu, na kutambua kuwa hakuna jambo linalotokea
kwa Bahati mbaya “Socrates alisema maisha yasiyotafakariwa Hayafai kuyaishi”
mimi nasema “Kuishi maisha yasiyo na kusudi nikupoteza mwelekeo” Mungu
ametuumba kwa Makusudi na ni lazima makusudi hayo yatimizwe.
Mungu akikusudia Jambo katika
maisha yako hakuna anyeweza Kulibatilisha
Mungu huyabatilisha Mashauri ya
watu waovu Dhidi yako
Yusufu alipewa Ndoto yale
yalikuwa ni Makusudi ya Bwana katika maisha yake hata hivyo alipitia changamoto
za aina mbali mbali, tunapopitia hayo ni muhimu kutambua kuwa Kusudi la Mungu
haliwezi kubatilika.
Daudi alipakwa mafuta kwa kusudi
la Kuwasaidia Israel kama Mfalme, Sauli alitaka kumuua mara kadhaa alimtupia
mkuki ili kuharibu kusudi na mpango wa Mungu lakini hatimaye Daudi alimiliki na
kutawala
Musa alikuwa auawe katika mpango
mbaya wa mfalme wa Misri aliyeamuru watoto wa kiume wauawe, Mungu katika hekima
yake alimfanya Musa huyohuyo alelewe ikulu na kuwa salama zaidi
Kiko mifano mingi inayothibitisha
kuwa Makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika, Adui zetu wanapotufikiria mabaya
Mungu hutufikiria mema au kutumia ubaya wao kutuletea mambo mema.
Zaburi 33:10-11“Bwana
huyabatilisha Mashauri ya mataifa, Huyatungua makusudi ya watu, Shauri la Bwana
lasimama milele. Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi”
Mithali 21:30 -
31 “Hapana Hekima wala ufahamu, wala shauri juu ya Bwana, farasi huwekwa
tayari kwa siku ya vita Lakini bwana ndiye aletaye wokovu”
Isaya 8:10 “ Fanyeni
Shauri pamoja nalo litabatilika, Semeni neno, Lakini halitasimama kwa maana
Mungu yu pamoja nasi”
Mungu akikusudia hakuna
anayeweza kubatilisha
Isaya 14:27 “Maana Bwana
wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na Mkono wake
uliionyooshwa ni nani atakayegeuza nyuma?
Hata wanadamu wafanye hila bado
kusudi la Mungu ndio litakalo simama
Mithali 19:21 “Mna hila
nyingi moyoni mwa mtu, Lakini Shauri la Bwana ndilo Litakalosimama”
Paulo Mtume alikuwa amekusudia
kuuona na Rumi pia
Warumi 1:15 “Kwa hiyo kwa
Upande wangu mimi ni tayari kuihubiri injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi”
Lakini Wayahudi walikusudia kwa
kila namna kuharibu mpango na makusudi ya Paulo, walitaka kumuua kabla hajafika
Rumi Angalia
Matendo
23:12-15 “Kulipopambauka,Wayahudi wakafanya mapatano,
wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue
Paulo. Na hao walioapiana hivyo walipata
zaidi ya watu arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema,
Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja
na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka
kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.
Angalia je hila zao zilifanikiwa?
Matendo 23: 11 “.Usiku ule
Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama
ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo
Rumi nako.”
Ni muhimu kufahamu kuwa kama unatembea katika kusudi la Mungu basi hakuna
anayeweza kuzuia kusudi hilo na kamwe hupaswi kukata tamaa unapoona mambo
magumu, vikwazo na hila za ibilisi na mipango ya kukukatisha tamaa hila na
matendo mabaya ya watu dhidi ya ndoto zako hakuna muda wa kumlaumu mtu au
kutafuta mchawi ni nani, jambo moja unalopaswa kulitambua ni kuwa “Makusidi ya Mungu hayawezi kuzuilika”
Mungu amekupa nguvu na mamlaka ya kubatilisha hata Mashauri ya Adui zako hata
kama mashauri hayo yanaonekana kana kwamba yanatoka kwa Mungu angalia.
2Samuel 16:23, Na shauri lake
Ahithofeli alilokuwa akilitoa siku zile lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la
Mungu, Ndivyo yalivyokuwa mashauri yake Ahithofeli kwa Daudi na Kwa Absalom”
Daudi alitambua kuwa Ahithofeli
alikuwa mtu mashuhuri kwa Ushauri na ushauri wake ilikuwa kama kuuliza kwa
Mungu na Ahithofeli alipokuwa ameasi kwa
Daudi Dua za daudi kwa Mungu ilikuwa ni kuilaani karama ya ushauri ya
Ahithofeli na kuibatilisha
2Samuel 15:31 “Mtu mmoja
akamwambia Daudi ya Kwamba Ahithofeli yu katika hao walioambatana na Absalom,
Daudi akasema Ee Bwana nakusihi Uligeuze Shauri la Ahithofeli liwe Batili”
Ni muhimu kwa kila mmoja wetu
kumsihi Mungu ili mashauri mabaya yanayotolewa dhidi yatu yaweze kuwa Batili,
mawazo mabaya yanayotolewa dhidi yetu yabatilike maneno mabaya yanayotolewa
dhidi yako yabatilike Bwana na abatilishe manuizo yote ya wachawi na laana zote
na kila mpango ambao sio makusudi ya Bwana dhidi ya maisha yetu katika Jina la
Yesu Amen.
Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye
Hekima
Rev. Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni