Jumapili, 20 Agosti 2023

Kuuwa simba bila kitu cho chote mkononi!


Waamuzi 14:5-6 “Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.”


 

Utangulizi:

Mungu wetu tunayemwamini na kumuabudu ni Mungu mwenye nguvu sana, uwezo wake na mamlaka yake haiwezi kulinganishwa na kitu chochote ni Mungu mwenye nguvu ni Mungu mwenye uwezo mkubwa mno na ndio maana tunamtegemea kwa kila jambo.

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU MWENYE NGUVU, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

Maandiko yanatufundisha hivyo na kutuelezea hivyo kuwa Mungu wetu ni mwenye nguvu, kwa msingi huo kila mwanadamu anapaswa kumwamini Mungu na kumtegemea akijua wazi kuwa hakuna jambo lolole linaloshindikana kwa Mungu, Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo linamuudhi Mungu kama kutokumuamini au kama hatuamini nguvu zake maana yake ni kuwa tumemuwekea mpaka (limitations) Jambo hilo ni Uasi, ni jambo la kuhuzunisha la kusikitisha na ni kama tumerudi nyuma na kumwacha au kutokukumbuka matendo yake.

Zaburi 78:40-42 “Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.”

Watakatifu waliotutangulia waliamini katika nguvu za Mungu, na kumtegemea katika maswala mbali mbali ya maisha na wakafanikiwa sana, Lakini wale ambao hawakumuamini walimsikitisha sana na hakupendezwa nao wala kuwafurahia, Mungu hafurahii mtu mwenye kusita sita lakini anamfurahia mtu anayemuamini.

Waebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye”.      

Mungu anataka tumuamini, anataka tuamini uwezo wake na anataka tumuamini Nguvu zake na anataka tuzitafute nguvu zake na kuutafuta uso wake kila siku, tutendapo hayo utaweza kuona tutakuwa na furaha na amani na Mungu wetu atatutendea mambo makubwa katika njia nyepesi sana 1Nyakati 16:11 “Mtakeni Bwana na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote.Tukifanya hivyo uweza ule wa Mungu na utendaji na mamlaka na nguvu za Mungu zitadhihirika ndani yetu katika namna nyepesi sana kuliko tunavyofikiri.

Leo tutachukua Muda kuangalia kwa kina tukio la Samsoni kumuua simba kwa mikono yake bila kutumia chombo chochote na maana yake kubwa ambayo Mungu amekusudia kutufundisha katika siku ya leo! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Mungu hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu.

·         Maana ya kuua simba bila kitu chochote mkononi.

·         Kuuwa Simba bila kitu chochote mkononi.

Mungu hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu.

Wote tutakubaliana kwamba Mungu hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu kwa kadiri apendavyo Roho Yeye Yule, na maandiko yametupa mwongozo, kwa mfano wana wa Israel walipokuwa wanatoka Misri kuelekea katika inchi ya ahadi inchi ya Kanaani Fimbo ya Musa ilitumika sana kama ishara ya mamlaka yake na Mungu aliitumia fimbo ya Musa kufanya Miujiza, mfano walipokuwa wamekutana na kikwazo katika kuivuka bahari ya Shamu, bado tunaona Mungu alimuelekeza Musa kutumia fimbo na ikawa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali.

Kutoka 14:15-16 “BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.”             

Unaona hapa kwa maelekezo ya Mungu wana wa Israel walivuka kikwazo cha bahari ya shamu Musa akipewa maelekezo ya kuitumia fimbo, nasisitiza tena kwa maelekezo Nawe inua fimbo yako unaona! Mungu ndiye aliyemuelekeza Musa kutumia fimbo iliyokuwa mkononi mwake kufanya ishara na miujiza, na ni katika hali kama hiyo wana wa Israel walipokuwa wanapaswa kuvuka ng’ambo ya Mto Yodrani  Mungu alitoa maelekezo mengine kwa kiongozi aliyekuwepo Yoshua Mungu alitoa maelekezo mengine namna watakavyouvuka mto wa Yordani ona.

Yoshua 3:5-8 “Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu. Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu. Bwana akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa. Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani. Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu. Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi. Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani. Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja. Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu.”       

Unaona kwa mara nyingine tena katika matukio yenye kufanana kuvuka bahari ya shamu na kuvuka mto wa Yordan Mungu akiwa ni yule yule lakini wakati wanatoa maelekezo ya kuvuka mto wa Yordani alitoa maelekezo mengine ni katika mtindo huo huo wakati wa waamuzi Mungu aliweza kutoa ushindi kwa waamuzi hao kwa nyenzo mbalimbali ambazo Mungu aliweka mkono wake na kuwapa ushindi mfano:-

1.       Mungu alimtumia Mwamuzi Shamghari kuwapa Israel ushindi kwa kutumia konzo la ng’ombe Waamuzi 3:31Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng'ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.” (Konzo la Ngombe ni mti mgumu unaotumika kuunga gari au kokoteni unaosukumwa na Ngombe)

 

2.       Mungu alimtumia Yael Mwanamke kuleta ushindi kwa wana wa Israel dhidi ya Sisera kwa kutumia nyundo na kigingi  Waamuzi 4:17-21 “Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni. Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti.  Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika. Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana. Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.”

 

3.       Muda usingeweza kutosha kuona namna Mungu alivyotumia watu mbalimbali na nyenzo mbalimbali kutenda miujiza na kuwaletea ushindi watu wake lakini hatimaye tunamuona Samsoni naye baada ya kujiliwa na Roho wa Mungu akiua Simba bila kitu chochote Mkononi ona

 

Waamuzi 14:5-6 “Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.”

Maana ya kuua simba bila kitu chochote mkononi.

Tunajifunza nini katika mifano hiyo hapo juu namna na jinsi Mungu alivyotumia njia mbalimbali katika kuiwasaidia watu wake kupata ufumbuzi na changamoto zilizokuwa zikiwakabili, nikiwa nimetulia zangu natafakari tu kuhusu Mungu ghafla ujumbe huu ulinijia nilimsikia Roho Mtakatifu mwenyewe akiniambia neno HILI KUUA SIMBA BILA KITU CHOCHOTE MKONONI  na mawazoni ilikuja moja kwa moja picha ya Samsoni akikabiliana na mwana simba na kumuua Biblia inasema akampasua mwana simba, nikawaza na kufikiri kwa haraka kuna jambo gani Roho Mtakatifu anataka kuniambia, Mungu kweli alifanya kazi na watu mbalimbali lakini pia na waamuzi mbalimbali kutatua changamoto za wanadamu kwa kutumia vifaa mbalimbali, lakini mwamuzi maarufu zaidi Samsoni katika tukio la kuua simba alitumia mikono tu bila ya kuwa na kitu chochote Mkononi.

Leo hii kumekuwepo na idadi kubwa sana ya matumizi ya vifaa vya kiroho, watu wanaponywa na kuamini katika uponyaji na usuluhishi wa changamoto zao kupitia vifaa vya kiroho, chumvi, mafuta, maji ya Baraka, udongo, vitambaa, sabuni na kadhalika kila mmoja akidai ni muongozo aliopewa na Roho Mtakatifu, hatuwezi kuingilia maelekezo yao na wala hatuwezi kukataa kuwa vinafanya kazi kwa jina la Yesu, vinafanya Lakini tusisahau pia kuwa Mungu ametuagiza kutumia mikono yetu kwaajili ya uponyaji na kwa kutumia jina la Yesu ona kwa mfano:-

Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Maandiko yanatufundisha kuwa tunaweza kukemea pepo na changamoto nyingine na zikaondoka kwa kutumia jina la Yesu tu, na tunaweza kuweka mikono yetu juu ya wagonjwa nao wakapata afya pia tunaweza kutumia vinywa vyetu na tukamuomba Mungu naye akafanya bila haja ya kutumia vifaa vya kiroho, matumizi ya vifaa vya kiroho yanaonyesha udhaifu mkubwa sana wa kiimani katika nyakati tulizonazo, watu wanahitaji sana kuona vitu vinavyoonekana na vitu ambavyo wanaweza kugusa ndipo waweze kuamini Mungu wetu ni mwenye nguvu kubwa sana aliiumba ulimwengu kwa neno tu na kila kitu kikawa kama kilivyokuwa kuua simba bila kitu chochote mkononi ni ishara ya kuwa yako mambo Mungu anaweza kuyafanya bila kuhitaji kutumia vifaa vya kiroho, Roho Mtakatifu anataka kulikumbusha kanisa kurudi katika utukufu wake na kuondoka katika udhaifu kutumia vifaa vya kiroho ni kwa watoto wachanga kiimani ni ishara ya kuwa kanisa limepoteza mamlaka, kanisa limesahau msingi wa matumizi ya Jina la Yesu jina lanye uwezo wa kufanya lolote hata bila msaada wa kitu chochote cha kuonekana  ufike wakati sasa kanisa tubatilishe mambo yote ya kitoto,

1Wakorintho 13:11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.”

 

Kuua Simba bila kitu chochote mkononi

Kama nilivyogusia hapo juu ni kuwa kuua simba bila kitu chochote mkononi kunamaanisha uwezo wa kukabiliana na changamoto zozote kutoka kwa ibilisi kwa kutumia jina la Yesu hata bila kutumia vifaa vya kiroho, Maandiko kinabii yanamtafasiri Shetani kama simba aungurumaye akitafuta mtu aweze kummeza ona 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Shetani pamoja na changamoto zote zinazotokana na yeye ni simba aungurumaye kanisa likirejea katika mamlaka yake na nguvu zake litakuwa na uwezo wake na nguvu zake za awali watakuwa na ufahamu kuwa iko mamlaka kubwa ya kutamka jina la Yesu na likaleta matokeo makubwa jina lenyewe tu peke yake hata bila ya kifaa chochote cha kiroho sio kila wakati tutatumia tu vifaa vya kiroho sio kila wakati Mungu atatoa maelekezo yale yale lakini kukaa katika uwepo wa Mungu kunatusaidia kuwa na mamlaka ya kutosha kutamka neno na ikawa

-          1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.”

 

-          2Wafalme 4:16 “.Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.”

 

-          2Wafalme 7:1 “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.”       

 

-          Matendo 3:6-9 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.”

 

-          Matendo 13:8-12. “Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”

 

-          Mathayo 8:5-10 “Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli.”

 

-          Marko 11:23-24 “Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”

 

-          Matendo 3:6-7 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.”     

Hitimisho.

Maandiko yote hapo juu ni ushahidi ulio wazi ya kuwa kama tukisimama imara katika maombi tutaweza kua simba bila kitu chochote mkononi yaani hatutahitaji sabuni, wala chumvi wala maji ya Baraka wala udongo wa upako tutatamka tu kwa Imani na kwa mamlaka ya jina la Yesu na yale yaliyokusudiwa na Mungu kupitia watumishi wake yatatimia, kuuwa simba bila kitu chochote mkononi ni shara ya ushujaa wa ngazi ya juu sana, kama ilivyo katika jamii ya kimasai,  Neno la Mungu limetaja watu watatu tu  ambao walikuwa na uwezo wa kuua simba bila kutumia silaha ama kitu Mkononi

Samsoni - Waamuzi 14:5-6 “Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.”

Daudi1Samuel 17:34-36 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”          

Benaya - 2Samuel 23:20-21. “Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji. huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.”            

Biblia inaonyesha mashujaa wakubwa watu hodari waliowahi kuua simba ambao ni Samsoni, Daudi na Benaya na benaya ndiye anaonekana kuongoza katika kufanya mauaji ya simba wengi zaidi, kufikia ngazi hii ya juu zaidi ya ushujaa ndilo jambo ambalo Mungu analitazamia, kwa kila mmoja wetu, ifikie wakati hata kama tutasahau kifaa fulani cha kiroho lakini tuwe na uweza na mamlaka ya kiungu na uwezo wa kutumia Jina la Yesu na mamlaka katika jina hilo         kusababisha mambo makubwa ya uponyaji na miujiza na utatuzi wa changamoto mbalimbali wakati mwingine bila haja ya kutumia kifaa chochote cha kiroho, hii ndio ngazi ya juu kabisa ya kimamlaka ambayo tunapaswa watu wa Mungu kuitafuta na kuitumia.

Matendo 4:12 – “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Wafilipi 2:9-1 1 – “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Matendo 2:21 – “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”

Warumi 10;13 – “Kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.”

Kanisa ni muhimu kwetu kukumbuika na kujiimarisha kiimani katika matumizi ya jina la Yesu na kusababisha mamlaka ya kiungu kutokea na kutenda kazi na kupunguza dhana ya matumizi ya vifaa vya kiroho, matumizi ya jina la yesu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali bila kutumia vifaa vya kiroho ndio kuuwa simba bila kitu chochote Mkononi.

Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Ijumaa, 18 Agosti 2023

Mungu anajua mwanzo -mwisho!


Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.  Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.  Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”



Utangulizi:

Maisha ya mwanadamu yamejaa siri kubwa sana ambayo majibu ya maswali mengi ambayo wanadamu hujiuliza yanajibika tu kwa kuwa na ufahamu wa kutosha katika maandiko na katika kumjua Mungu na kuwa na uhusiano wa kudumu na Mungu, haijalishi umepitia changamoto za aina gani katika maisha au unapitia changamoto gani hata wakati huu somo kama hili linapokujia lakini Roho Mtakatifu amenitaka leo nikujulishe ya kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho, Mungu anayo ramani ya maisha yako na anajua kila kitu kinachoendelea katika maisha yako! Ni yeye pekee mwenye uwezo wa kutangaza mwisho wako tangu mwanzo na sio wanadamu!

 Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

Kwa msingi huo hupaswi kuwa na shaka wala kuogopa katika maisha yako kwamba unapitia changamoto za aina gani, wala hupaswi kuogopa kuwa itakuwaje kesho na kesho kutwa kumbuka tu kuwa Mungu yuko kwenye udhibiti wa kila jambo linalotendeka na linalotokea katika maisha yako yeye pekee ndiye anayejua maisha yako mwanzo mwisho na sio wanadamu, leo tutachukua Muda kujifunza somo hili Mungu anajua mwanzo mwisho kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Mungu anajua yote.

·         Hakuna utakachopoteza.

·         Mungu anajua mwanzo mwisho.

Mungu anajua yote:

Moja ya sifa kubwa ya Mungu aliye hai na wa kweli ni kuwa ANAJUA YOTE tena anajua mwisho wa kila jambo na anauwezo wa kulisema jambo hilo tangu mwanzo hii ni kwa sababu yeye ana sifa ya kuwa mwanzo na mwisho, (Yaani Alfa na Omega).  Hivyo ni wazi kuwa anajua tunakotoka na tunakokwenda! Ramani yote ya maisha yetu iko mikononi mwake na kwa ujumla yeye ndiye mwenye mpango mzima (Master Plan) ya maisha ya kila mtu duniani,

Ufunuo 21:6 “Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.”

Mwanzo 25:21-23. “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”

Unaona hapo kalba hajazaliwa Esau na Yakobo Mungu alishajua mwisho wao utakuwaje hivyo ni wazi kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho wa kila mtu, maisha yetu yameratibiwa na Roho wake Mtakatifu tangu itakavyokuwa mwanzo mpaka mwisho! Mungu anajua mwanzo mwisho!          

Kwa ujumla kuna maeneo makubwa matano yanayotumika kuelezea sifa za Mungu ambazo hakuna kiumbe kingine chochote kinaweza kuwa na sifa hizo isipokuwa Mungu peke yake, sifa hizo ni pamoja na:-

-          Mwenye nguvu zote – Omnipotence

-          Mwenye kujua yote – Omniscience

-          Mwenye kuweko mahali kote kwa wakati mmoja – Omnipresence

-          Asiyebadilika – immutability

-          Ni wa Milele na milele – Transcendence

Kwa Mujibu wa wanatheolojia hizo ni sifa ambazo mwanadamu au kiumbe cha kawaida hakiwezi kuwa nazo isipikuwa Mungu peke yake, hata hivyo sio kusudi langu leo kuelezea sifa zote tano za Mungu lakini nataka kuchukua Muda kuelezea sifa moja tu ya MWENYE KUJUA YOTE kwa kusudi tu la kutimiza leongo la somo hili:-

Neno hilo MWENYE KUJUA YOTE Katika lugha ya kiingereza linatumika neno OMNISCIENCE  ambalo kimsingi ni neno la asili ya lugha ya kilatini linalojumuisha muunganiko wa maneno mawili Omnis -  ambalo kwa kiingereza ni ALL ikiwa na maana ya Kiswahili YOTE/WOTE na neno SCIENTIA ambalo kwa kiingereza ni KNOWLEDGE ambalo kwa Kiswahili ni MAARIFA, au UJUZI kwa hiyo linapoungwanishwa pamoja tunapata neno OMNISCIENCE  ambalo kwa kiingereza ni ALL KNOWING na kwa kiwahili KUJUA YOTE  na sasa basi linapotumika kuelezea sifa za Mungu linatumika kuelezea kuwa Mungu anajua yote hivyo hakuna jipya kwake wala hakuna jambo wanadamu watagundua ambalo Mungu hakuwa analijua yeye anajua kila kitu, kwa hiyo kila jambo linalokutokea katika maisha yako haimaanishi kuwa Mungu hakuwa na taarifa nalo, wala Mungu hasahau kitu kwa sababu amekuwepo toka milele na anaendelea kuwepo na yupo hata milele kwa hiyo Mungu anajua kila kitu na hakuna cha kumshangaza !

Katika maisha yetu hakuna bahati mbaya Mungu anaelewa mwisho na mwanzo wa kila kinachoendelea katika maisha yako, hivyo hupaswi kuogopa na badala yake unapaswa kumsubiri Mungu kwa njia ya maombi, Katika andiko la Msingi tulilolisoma tunaona Mungu akizungumza na Abraham kuhusu uzao wake kizazi cha nne ambao wangeshuka Misri na kukaa huko miaka 400 na kuwa kisha atawarejesha tena katika nchi ya mkanaani ona  

Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.  Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.  Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”

Unaona ni karibu kati ya miaka 1632-2000 hivi kutoka Abraham mpaka wakati Musa anazaliwa na kuitwa kuwakomboa wana wa Israel, Lakini Mungu anayejua yote anamwambia Abrahamu habari za wana wa Israel namna watakavyoshuka Misri na kutumikishwa huko na kuwa angewapandisha tena  Miaka Mingi sana hata Isaka hajazaliwa wala Yakobo hajazaliwa, huo ni uthibitisho ulio wazi kuwa kila kinachotokea katika maisha yetu kimeratibiwa katika mpango na ratiba za Mungu aliye hai, huna sababu ya kujuta wala kulia katika kila jambo unalolipitia Mungu yuko kwenye udhibiti na makusudi yake yatatimizwa tu, na lile ambalo halijakusudiwa halitatimia !

Hakuna utakachopoteza!

Kama Mungu anajua yote ni wazi kuwa anayajua maisha yetu vema na hakuna lolote linaloweza kuharibu mpango wetu kwake, yote yanayotutokea yawe mema au mabaya yote ni kwa makusudi yake na mapenzi yake ni lazima yatatimizwa, kama Mungu amekuahidi jambo fahamu ya kuwa atalitimiza bila kujali nini kinatokea katika maisha yako kwa sasa kitatimia kwani Mungu ni mwaminifu na wanadamu ni waongo!

-          Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?”

-          2Wakorintho 1:20 “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.

-          2Samuel 2:31 “Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia.”

-          Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

-          Mithali 19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”             

-          Ayubu 42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”

-          Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

Mungu anapokuwa amekusudia jambo Fulani katika maisha yako, ni muhimu kufahamu kuwa jambo hilo halitaweza kuzuiliwa na mtu, Mungu ana makusudi na maisha yako, kila kitu katika maisha yako hata aina ya mapito unayoyapitia yanakuandaa kukuleta katika lile kusudi kwa msingi huo lolote lililo jema au lililo baya lisikutishe wala simama katika mapenzi ya Mungu, jitahidi usitende dhambi lakini naam hata ukitenda  maana hakuna mwanadamu atendaye mema asitende dhambi hiyo haimzuii Mungu kutuimiza mpango wake alioukusudia kwako  kwa sababu yeye anajua mwanzo mwisho yeye ni msaada ulio karibu atafanya njia, atarehemu, atasamehe atakuweka panapo nafasi na kusudio lake lililokusudiwa ndani mwako litatimizwa Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”             

Mungu anajua mwanzo mwisho!

Ni muhimu sasa kuwa na ufahamu kuwa Mungu anajua kila kitu, Mungu anajua mambo yote na ya kuwa makusudi yake hayawezi kuzuilika, ikiwa tunafahamu wazi sasa jambo hilo ni muhimu kuelewa kuwa hakuna kitu ambacho kinafanyika duniani katika maisha yetu ambacho Mungu hajui, Mungu ana taarifa ya mambo mengi sana  na anajua vema kila kitu kwa kina na mapana na marefu, Mungu anajua mambo makubwa na madogo, maandiko yanaonyesha wazi maswala ambayo Mungu anayajua na kuyafuatilia na ukijiweka katika ulinganifu wake utakubaliana nami kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ona:-   

-          Anajua idadi ya nywele zetu Mathayo 10:29-30 “Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.” Maandiko tena kupitia Yesu Kristo mwenyewe yananyesha kuwa hata ndege wa angani hawaanguki chini bila mbingu kuwa na taarifa yaani Mungu anajua kuwa kuna ndege amepigwa, ametegwa, ameliwa na kadhalika pamoja na udogo walio nao, lakini sio hivyo tu hata nywele zetu idadi yake inajulikana na Mungu hiii maaana yake nini maana yake Mungu anajali kuanzia vitu vikubwa mpaka vitu vidogo vidogo vingi  na kama ni hivyo anayajali na kuyajua maisha yako na kila unalilopitia na utakalolipitia na namna utakavyotoka na utakavyotimiza mpango wake  na makusudi yake duniani

 

-          Anatujua Mwanzo mwisho Yeremia 1:4-5 “Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”         Mungu anatujua hata kabla hajaruhusu tuzaliwe duniani wewe na mimi tulikuweko katika wazo lake tangu milele Mungu anamwambia Yeremia nabii kabla hajatungishwa mimba kwenye tumbo la mama yake yeye alikwisha kumjua na alikwisha kuchagua kuwa atakuwa nabii kwa mataifa mbalimbali, Kama Mungu anakujua kuumbwa kwako na kuzaliwa kwako na kama anaweka kusudi lake ndani yetu hata kabla hatujazaliwa ni Dhahiri alijua kila utakachokipitia pia anajua siku zetu za kuwepo duniani, anajua matendo yetu yote mema na mabaya kila kitu katika maisha yetu kimeratibiwa Mbinguni  Zaburi 139:13-18 “Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.  Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.”

 

-          Anajua uhusiano wetu na yeye umesimamaje -                 

Nahumu 1:7 “Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao

Warumi 8:16-17 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”    

Yohana 10:27-29 Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”

Mungu anamjua kila mtu anayemtegemea anayemkimbilia anayemuamini anajua umesimama wapi katika uhusiano wako na yeye, anajua anavyotuhudumia na sisi tu mashahidi kwa kuwa Roho wake Mtakatifu hutushuhudia kuwa sisi ni wana wa Mungu hivyo haki zetu zinahifadhiwa ndani yake kwa nini kwa sababu anajua uhusiano wetu tulionao kwake na njia tutakayoipitia na kule atakakotuongoza anajua mwanzo mwisho!

 

-          Anatujua kwa majina yetu -  alimjua Musa Kutoka 33:12 na 17  alimjua sauli na alimjua Koreshi mfalme wa uajemi hata kabla hajazaliwa tena kwa jina lake kabisa wazi wazi

 

Kutoka 33:11-12Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani. Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.” Na

 

Kutoka 33:17’ “BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”               

 

Alimjua Sauli aliyekuwa analiudhi kanisa ona Matendo 9:1-5 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.”

 

Alimjua Koreshi hata kabla hajazaliwa Isaya 45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake,ambaye nimemshika mkono wake wa kuume,ili kutiisha mataifa mbele yake,name nitalegeza viuno vya wafalme;ili kufungua milango mbele yake,hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;”

 

Ni jambo la kushangaza sana Mungu alimjua Musa kwa jina lake, Mungu alimjua Sauli ambaye alikuwa analiudhi kanisa na kumuita ili awe mtume Mungu, alimjua mfalme Koreshi wa uajemi kabla hajazaliwa, Isaya alitaja habari zake na Mungu alijua kuwa atamtumiaje maandiko haya yote ni mjumuisho wa taarifa tu kuwa Mungu anatujua anajua huduma alizotuitia anajua utumishi aliotuitia anajua mapito tunayoyapitia anajua kila kitu kinachoendelea katika maisha yetu.

 

-          Anaijua mioyo yetu. 

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

 

1Falme 8:39 “basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote)”

 

Mungu anaijua mioyo yetu anajua kama uko uovu ndani yetu anajua kama mioyo yetu ni safi, ama ina ugonjwa wa kufisha yaani kama tunayoyawaza yatapelekea mauti ni yeye pia aliye tayari kuitakasa mioyo yetu kama tutakuwa radhi na kuwa na hiyari ya kuyadai na kuyataka mapenzi yake.   

 

-          Anayajua mawazo yetu - Mungu anayajua mawazo yetu anajua kila jambo analoliwaza mwanadamu anajua pia tunapokusudia kutenda uovu anajua Mwanzo 6:5-6 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.” Mungu aliyasoma mawazo ya wanadamu wakati wa Nuhu na kuona kuwa ayoyakusudia ni maovu tu hii maana yake ni kuwa kila wazo linalotembea katika akili zetu Mungu analiona na hakuna kilichofikichika Zaburi 139: 1-2 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.” Unaona Mungu anajua mwanzo mwisho analiona wazo la mwanadamu tokea mbali, tunaweza kuwatisha watu kwa kujifanya tunajua kila kitu na tunajua kila wanachokifikiri lakini Mungu tayari anajua anaujua ukweli, hakuna kinachoweza kufichika.

 

-          Anajua hofu zetu – achilia mbali kwamba Mungu anayajua mawazo yetu, Mungu anazijua pia hofu zetu na kutuponya nazo zote, Mapema sana Yesu akijua mahitaji Muhimu ya wanadamu ambayo wamekuwa wakihofia aliwaondoa wasi wasi kuwa Mungu anajishughulisha sana na mambo yetu  yawe kwa heri au kwa shari atashughulika katika njia iliyobora na njema zaidi.

 

Mathayo 6:25-34 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.  Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

 

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

 

Baba yetu wa mbinguni anajua tunayoyahitaji kwa sababu hiyo wajibu wetu ni kuomba tu ambako ndiko kumtwika yeye fadhaa zetu zote na tunaambiwa kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu maana yake anashughulika vema na hofu zetu na anajua njia sahihi na namna sahihi iliyo bora ya kutupatia mahitaji yetu

 

-          Anayajua matendo yetu – Kama Mungu anayajua mawazo yetu na anajua hofu yetu sembuse matendo yetu? Mungu anayajua yote hata yale tuyatendayo sirini maandiko yanatueleza kuwa wakati wa hukumu Mungu ataweka wazi kila tendo na kila neno la siri tulilolitenda na pia kazi za wapendwa wote zitapimwa kulinga ana nia ya kila mmoja Mungu anajua Mungu anajua alionya sana katika nyaraka saba kwa makanisa saba kule Asia katika kitabu cha ufunuo kuwa anajua anajua na akatoa maelekezo sasa kwao

 

Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

 

2Wakorintho 5:9-10 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”

 

Ufunuo 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

 

Mungu hataleta hukumuni mambo asiyoyajua ataleta hukumuni ushahidi ulio wazi wa matendo yetu yote na maneno yetu yote lakini pia waamini watapimwa na Kristo katika kiti cha hukumu so kwaajili ya hukumu bali kwaajili ya kazi tulizozifanya hapa duniani, Mungu anajua pia tuyatendayo na nia yake kwa nini tunayatenda

 

-          Anayajua maneno yetu - Mungu anayajua maneno yetu yote kama Mungu mwenye kujua yote hakuna neno lolote tunalolisema katika ndimi zetu ambalo linampita anayajua vema

 

Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”

 

Mathayo 12:35-37 “Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

 

-          Anazijua njia zetu – Kuna maandiko memngi sana yanayothibitisha au kuonyesha Mungu akizungumza kuhusu njia zetu lakini maandiko hayo yanatutaka tumkabidhi yeye njia zetu kwa kuwa anaijua njia tuiendeayo Ayubu 23:10 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.” Yeye kama Mchungaji mwema wakati wote hutuongoza katika njia inayofaa Zaburi 23:3-4 “Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” Mithali 16:9 “Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.”

 

Kwa kuwa Mungu anajua njia kwa usahihi hii maana yake mipango yetu yote ni vema tukimkabidhi yeye mipango yetu yote au kuomba Muongozo kutoka kwake lakini vyo vyote iwavyo Mungu anajua mwanzo mwisho               .

 

Anayajua madhaifu yetu – Mungu anayajua madhaifu yetu na anajua namna nzuri ya kuchukuliana nasi tofauti na jinsi wanadamu wanavyotuchukulia yeye hutuchukulia kwa rehema kwa sababu anatujua kuwa sisi ni Mavumbi

 

Zaburi 103:8-14 “Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”

 

2Wakorintho 12:9-10 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

 

-          Anajua siku za uhai wetu Duniani

Wanadamu kwa kawaida hatujui siku za maisha yetu ni ngapi, Mungu ametuficha lakini yeye mwenyewe anajua anajua siku za maisha yetu anaweza kutusaidia kutujulisha ili kwamba tuzitumie kwa hekima ona Zaburi 90:12 “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”

 

Yakobo 4:13-14 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.” Maisha ya uhai wetu uko mikononi mwa Mungu, maisha yetu ni kama mvuke hatujui yatakayokuwako kesho, Lakini Mungu anajua kila kitu anajua mambo yote, unaweza ukafichwa usijue siku yako lakini kwa Mungu hakuna geni wala la kushangaza.

Hitimisho:

Kwa kuwa tumejifunza kwa kina na kuelewa kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ni muhimu kwetu kutokuogopa tunapokuwa  katika mapito ya aina yoyote duniani, ni lazima tuelewe na kukubali kuwa kila linalotutokea katika ulimwengu huu liko chini ya uwezo wa kiungu kazi yetu ni kuomba na kumuacha yeye atimize mapenzi yake, Mungu alimwambia Ibrahimu maswala yote yatakayojitokeza baadaye kizazi chake cha nne ambao walishuka Misri na baada ya miaka 400 kuwa angewapandisha tena walishuka kupitia Yusufu unajua yaliyomkuta Yusufu unajua yaliyowakuta wana wa Israel safari haikuwa nyepesi lakini tumeelewa kuwa Mungu alikuwa kwenye udhibiti, kila linalotutokea kwenye maisha yetu hatupaswi kuogopa tunaye Mungu anayejua yote tukiyajua haya tutafahamu kuwa haupaswi kujisumbua katika jambo lolote lile isipokuwa kwa kila jambo kwa kusali na kuomba na kumuacha  Mungu afanye kazi yake Mungu anajua maisha yetu anajua uendako anajua utokako hakuna lililofichika kwake kuhusiana na maisha yako hivyo usifadhaike! Wala usihuzunike moyoni mwako Mungu anajua Mungu anaona na Yeye atatenda. Mapenzi yake yatimizwe katika maisha yetu kwaajili ya utukufu wake.

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Ijumaa, 11 Agosti 2023

Kumwamini Mungu tokea Pangoni!


Zaburi 57:1-3. “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.  Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake




Utangulizi:

Moja ya zaburi zenye utajiri wa kutufundisha kumuamini Mungu katika mazingira magumu na ya aina yoyote ile ni Pamoja na Zaburi hii ya 57, Kihistoria Zaburi hii iliandikwa au kutungwa katika mazingira ya wakati Daudi anamkimbia Mfalme Sauli ambaye alikuwa amekusudia kumuua kwa vile ni kijana aliyeonyesha kuwa anaweza kuwa mfalme baada ya Sauli, Daudi alikimbia katika Pango liitwalo Pango la Adulamu na watu kadhaa wakamfuata huko pamoja na ndugu zake kwaajili ya usalama wao na kulitumia pango hili kama ngome ya kujificha dhidi ya Adui zake ona

1Samuel 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.”     

Unaweza kuona kwa nini maandiko yanasema Daudi akaondoka huko akakimbilia Pango la Adulamu? Sababu kubwa ni kuwa Daudi alikuwa ametiwa Mafuta ili awe mfalme baada ya Sauli kwa mapenzi ya Mungu ona

1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”

Baada ya Daudi kutiwa Mafuta ili aje kuwa mfalme baadaye uweza wa Mungu ulikuwa juu yake, Roho Mtakatifu alikuja juu ya Daudi kwa nguvu na kuanza kumtumia katika kazi zake kwa uhodari Mkubwa ona

1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Maandiko yanatuonyesha kuwa Daudi alianza kuwa Mtu shujaa kutokana na uweza wa Mungu uliokuwa juu yake kupitia Roho Mtakatifu, aliweza kuwalinda kondoo wa Baba yake walipokuwa wakihatarishiwa maisha na Simba na dubu pamoja na wanyama wakali sana bila kujulikana ushujaa wake lakini Zaidi sana alikuja kujitiokeza kama shujaa wa kitaifa pale alipokabiliana na adui wa kutisha wa Israel aliyeitwa Goliati na kujipatia umaarufu mkubwa hata kuliko Sauli jambo lilopelekea kuanza kuwepo kwa wivu na visa vya kutaka kuuawa na Mfalme Sauli:-

1Samuel 17:49-51Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.”

1Samuel 18:6-9 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”               

Ni katika mazingira kama haya sasa ndipo tangu wakati huo Daudi alianza kuwindwa na Sauli ili yamkini akipata nafasi aweze kumuua, na kwa kweli mara kadhaa Daudi alikoswa koswa kuuawa kwa mkuki kupitia  na njia nyinginezo, Sauli ambaye alikusudia kumtenda vibaya  kwa ujumla Sauli alikusudia kumuu a Daudi mara saba

1Samuel 19:10-12 “Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.” 

Ni katika mazingira kama hayo ya kuwindwa kila wakati na kutaka kuuawa ndipo Daudi alipoanza kuishi maisha ya kuhama hama huku na kule akijificha kwaajili ya kuokoa uhai wake ndipo sa tunamuona Daudi pamoja na kundi kubwa la watu wanyonge wakimkimbilia na kumfuata naye akawa kamanda wao hii ndio sababu ya Daudi kukimbilia katika Pango la Adulamu.

Tutajifunza somo hili sasa kumwamini Mungu tokea Pangoni kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Kumkimbilia Mungu wakati wa shida zetu  

·         Kumsifu Mungu wakati wa shida zetu

·         Kumwamini Mungu tokea Pangoni


Kumkimbilia Mungu wakati wa shida zetu.

Baada ya kuwa tumeona changamoto aliyokuwa akikutana nayo Daudi akitafutwa kuuawa na huku akiwa amekoswa koswa kuuawa mara saba kutoka kwa sauli, tunamuona Daudi akikimbia sasa kutoka kwa Sauli na kwenda kujificha katika Pango la Adulamu, tunaweza kujiuliza kuwa ni kwanini Daudi alifanya jambo hili? Ni ukweli ulio wazi kuwa Daudi alikuwa anatafutwa na Mfalme Sauli na Sauli hakuwa peke yake alikuwa na Jeshi kubwa la wateule yaani watu waliochaguliwa kuwa wanajeshi  wenye uzoefu mkubwa na ni hodari katika vita kwa hiyo unaweza kuona wazi kabisa kwamba Daudi alikuwa hatarini kweli kweli kwa ujumla Jeshi alilokuwa nalo Sauli lilikuwa na watu hodari wa vita wapatao elfu tatu (3000) ona  

1Samuel 24:1-2 “Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.”

Kwa bahati mbaya Biblia ya Kiswahili ya (SUV) iliacha neno tatu kwa hiyo inasomeka kama watu hao walikuwa Elfu lakini matoleo mengine ya kiingereza likiwepo toleo la kiingereza cha KJV ambapo ndipo tafasiri ya Biblia ya Kiswahili inakotokea yanaonyesha kuwa lilikuwa jeshi la watu 3000 unaweza kuona mfano:-

NIV inaonyesha 3000 1Samuel 24:1-2 “After Saul returned from pursuing the Philistines, He was told, “David is in the Desert of Engedi. So Saul took three thousand able young men from all Israel and set out to look for David and his men near the Crags of the wild goats

KJV inaonyesha pia 3000 1Samuel 24:1-2 “And it came to pass, when Saul was returned from following the Philistines, that it was told him, saying, Behold David is in the wilderness of Engedi, then Saul took three thousand chosen men out of all Israel and went to seek David and his men upon the rocks of the wild goats

Kwa hiyo utaweza kuona mtu aliyekoswa koswa kuuawa zaidi ya mara saba na sasa anafuatiliwa na Jeshi kubwa la wanajeshi Hodari yaani makomandoo walio na mafunzo ya kivita katika Nyanja mbalimbali za kijeshi wanamtafuta Daudi ambaye alikuwa na kundi la watu wasio na mafunzo kama mia nne tu  wastani kila askari wa Daudi alikuwa na askari wa upinzani saba hivi wa kupigana nao, kwa hiyo kukimbilia Pangoni pekee kulikuwa hakutoshi wala hakukuwa salama kwa sababu wapelelezi walimueleza Sauli kila alikokimbilia Daudi na sasa Daudi anajua kuwa anapaswa kumkimbilia nani katika msiba wake Daudi alijiona kama kwamba anazungukwa na simba wakali na msaada wake ulikuwa ni Mungu tu:-

Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake

Daudi anatufundisha ya kuwa wakati wote tunapokutana na changamoto mbali mbali katika maisha yetu hatuna budi kumkimbilia Mungu, yeye ndiye anayeweza kuturehemu na kusaidia katika shida zetu, kukimbilia Pangoni ni sawa tu na mtu akiwa anaumwa anaweza kwenda Hospitali kwaajili ya msaada wa kawaida wa kibinadamu lakini changamoto nyingine haziwezi kutatuliwa hospitali wala haziwezi kutatuliwa na ujuzi wetu na ushujaa wetu na utaalamu wetu na elimu zetu na vyeti na kadhalika lakini neno la Mungu linatueleza wazi ya kuwa tunaweza kumkimbilia Mungu na tunaweza kulitumainia jina lake na tukawa salama, Daudi alikuwa na uelewa huo kuwa Usalama wake utatoka kwa Mungu tu na hivyo ingawa amekimbilia katika Pango la Adulamu bado anatufundisha kuwa pango pekee halitoshi kwani yuko Mungu anayeweza kutupa uvuli, anayeweza kututimizia mambo yetu anayeweza kutuokoa kwa msaada kutoka mbinguni anayeweza kupeleka fadhili zake kwa watumishi wake huyo tukimtumaini na kumkimbilia tunajihakikishia usalama wa kutosha !.

Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Daudi anakimbilia katika lile Pango akiwa katika hali ya kuvunjika moyo amenusurika kuuawa mara saba na sasa anamkimbia Sauli, anajiona nafsi yake kuwa sasa kwa msala huu anaweza kuuawa anachukiwa mno anapingwa mno, hakuna wa kuweza kumsaidia isipokuwa Mungu peke yake, Kaka zangu na dada zangu tunapopita katika changamoto mbalimbali za maisha haya hakikisha ya kuwa unamkimbilia Mungu, mfanye yeye kuwa kimbilio lako!. Mkimbilie yeye na fungua kinywa chako kuomba mwambie nakuhitaji hakuna wa kunisaidia ila wewe Mungu katika hali yangu naye atakufanikisha.

Kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.

Kuna nguvu kubwa sana katika kumsifu Mungu, Daudi alikuwa na ufahamu mkubwa sana wote tunajua kuwa katika maisha yake Daudi hakuwahi kushindwa vita, moja ya siri yake kubwa ya ushindi ukiacha kupakwa mafuta, ukiacha kumkimbilia Mungu, ukiacha kutafuta uso wa Mungu ili aweze kujua mapenzi ya Mungu katika kila alilokuwa anataka kulifanya  yeye alitangulia kumsifu Mungu kwa Imani akitarajia ushindi mkubwa ya kuwa Mungu atafanya kitu, hii inatufundisha kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.

Zaburi 57:5-11 “Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake! Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi, Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri. Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa. Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni. Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.”

Wako watu wengi sana katika maandiko ambao walipokuwa wakikabiliwa na mambo magumu walimsifu Mungu wakiwa katika shida zao na Mungu akawakomboa mfano mmojawapo ni Paulo na Sila waliomsifu Mungu wakiwa gerezani.

Matendo 16:25-28 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.”

Kumwamini Mungu tokea Pangoni.

Daudi kama tulivyojifunza ya kuwa alikuwa anakabiliwa na jeshi kubwa na zaidi ya yote alijiona kama yuko katikati ya simba kwa ujumla ukiitazama hali halisi utaweza kujua kuwa Daudi alikuwa anawindwa na kuzungukwa na hatari kubwa adui yake alikuwa Sirius sana, alikuwa amemaanisha kumua kama Sauli alijaribu kumuua Daudi mara saba na sasa anamfuatia kwa silaha kali, na Jeshi la watu 3000 ni Dhahiri kuwa alikuwa na msako mkubwa sana wa kumfanya Daudi kuwa kitu kibaya sana 

Zaburi 57:4 “Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.”

Daudi anakubaliana wazi kuwa adui zake walikuwa na nguvu kuliko yeye walikuwa wengi na wenye uzoefu wa vita, walikuwa na umri mkubwa kumzidi, anakumbuka alivyokuwa akikabiliana na simba huko nyikani na anakumbuka alivyoweza kupata usingizi  kati ya simba lakini kwetu sisi kama kanisa tunafahamu Simba huyu ni adui  yetu mkubwa yaani shetani.

 1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Licha ya kuwa maadui hawa walikuwa na nguvu kama simba lakini pia ndimi zao na meno yao yaani nguvu yao ni mikuki na mishale lakini pia walikuwa wakinena maneno mabaya sana dhidi ya Daudi, kwa ujumla walikuwa ni wenye nguvu, hodari wenye silaha kali na maneno yao makali ya kutisha sana lakini pia walimtukana Daudi; Daudi alimuamini Mungu, aliamini kuwa atastarehe kati yao waliowaka moto yaani ni kama adui zake watageuka majivu tu Mungu atawafanya kuwa sio kitu, Mungu atawageuza kuwa kitu kilichoteketea na watakuwa kama mavumbi ya majivu watatoweka wote na hawatakuwako tena!, tunajifunza ya kuwa ni lazima kumwamini Mungu bila kujali unapitia hali gani, hata kama hali hiyo inatisha kiasi gani, hata kama gonjwa hilo linatisha kupita kawaida, hata kama, hata kama  afya yako haijatengemaaa mwamini Mungu ya kuwa anaweza kukusaidia na utakuwa salama atawafutilia mbali adui zako, kikla kinachosumbua katika maisha yako kitafanywa kuwa majivu katika jina la Yesu Kristo.

Hitimisho:

Zaburi hii imeandikwa wakati Daudi akiwa katika mateso ya kumkimbia mfalme Sauli na Daudi alikuwa amekimbilia huko Adulamu, na ni katika kumbukizi hii zaburi ikaandikwa, ni wakati alipokoswa koswa kuuawa mara saba. Zaburi imegawanyika katika makundi makuu mawili aya ya 1-6 anakimbilia rehema za Mungu, na kumuomba na kumlilia ili aweze kumpa msaada aya ya 7-11 Anaonyesha Imani na ujasiri na kumsifu Mungu na kumtukuza kutoka Pangoni kwa Imani akijua kuwa fadhili za Mungu ni kuu na Mungu hatampungukia, tunaweza kumsifu Mungu hata kama tumepungukiwa, hata kama ndoto zetu zinaonekana kupotea au kufifia, Daudi alikuwa amepakwa mafuta kuwa mfalme na sasa anakimbia mbali na kiti cha ufalme anaishi Pangoni mbali na nyumba ya Mungu hakutumia muda huo kulalamika lakini aliamini kuwa Mungu aliye mwema bila kujalisha yuko Mazingira gani atamtoa na kumuokoa na mwaswaibu yanayomkuta Yeye alimuamini Mungu tokea pangoni wewe unamwamini Mungu ukiwa wapi? Kwa wale wenye vita za kiroho na watu wenye wivu siku zote kumbuka kwamba kiwango cha watu wanaokupiga vita kinaonyesha ni kiwango gani cha utukufu Mungu anakupa, kama unapigwa vita na mfalme ujue wewe ni mfalme ajaye.

Na. Rev Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!