Waamuzi 14:5-6 “Ndipo Samsoni na baba yake
na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na
tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye
akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote
mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.”
Utangulizi:
Mungu wetu tunayemwamini na
kumuabudu ni Mungu mwenye nguvu sana, uwezo wake na mamlaka yake haiwezi
kulinganishwa na kitu chochote ni Mungu mwenye nguvu ni Mungu mwenye uwezo mkubwa
mno na ndio maana tunamtegemea kwa kila jambo.
Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto
amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake;
Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU MWENYE NGUVU, Baba wa milele,
Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe,
Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa
hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio
utakaotenda hayo.”
Maandiko yanatufundisha hivyo na
kutuelezea hivyo kuwa Mungu wetu ni mwenye nguvu, kwa msingi huo kila mwanadamu
anapaswa kumwamini Mungu na kumtegemea akijua wazi kuwa hakuna jambo lolole
linaloshindikana kwa Mungu, Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo linamuudhi
Mungu kama kutokumuamini au kama hatuamini nguvu zake maana yake ni kuwa
tumemuwekea mpaka (limitations) Jambo hilo ni Uasi, ni jambo la kuhuzunisha la
kusikitisha na ni kama tumerudi nyuma na kumwacha au kutokukumbuka matendo yake.
Zaburi 78:40-42 “Walimwasi jangwani mara
ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka
Mtakatifu wa Israeli.Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na
mtesi.”
Watakatifu waliotutangulia
waliamini katika nguvu za Mungu, na kumtegemea katika maswala mbali mbali ya
maisha na wakafanikiwa sana, Lakini wale ambao hawakumuamini walimsikitisha
sana na hakupendezwa nao wala kuwafurahia, Mungu hafurahii mtu mwenye kusita
sita lakini anamfurahia mtu anayemuamini.
Waebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu
ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye”.
Mungu anataka tumuamini, anataka
tuamini uwezo wake na anataka tumuamini Nguvu zake na anataka tuzitafute nguvu
zake na kuutafuta uso wake kila siku, tutendapo hayo utaweza kuona tutakuwa na
furaha na amani na Mungu wetu atatutendea mambo makubwa katika njia nyepesi
sana 1Nyakati 16:11 “Mtakeni Bwana na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku
zote.” Tukifanya hivyo uweza ule wa Mungu na utendaji na mamlaka na
nguvu za Mungu zitadhihirika ndani yetu katika namna nyepesi sana kuliko
tunavyofikiri.
Leo tutachukua Muda kuangalia kwa
kina tukio la Samsoni kumuua simba kwa mikono yake bila kutumia chombo chochote
na maana yake kubwa ambayo Mungu amekusudia kutufundisha katika siku ya leo!
Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mungu
hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu.
·
Maana ya
kuua simba bila kitu chochote mkononi.
·
Kuuwa
Simba bila kitu chochote mkononi.
Mungu hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu.
Wote tutakubaliana kwamba Mungu
hutumia njia mbalimbali katika kutatua changamoto za wanadamu kwa kadiri
apendavyo Roho Yeye Yule, na maandiko yametupa mwongozo, kwa mfano wana wa
Israel walipokuwa wanatoka Misri kuelekea katika inchi ya ahadi inchi ya Kanaani
Fimbo ya Musa ilitumika sana kama ishara ya mamlaka yake na Mungu aliitumia
fimbo ya Musa kufanya Miujiza, mfano walipokuwa wamekutana na kikwazo katika
kuivuka bahari ya Shamu, bado tunaona Mungu alimuelekeza Musa kutumia fimbo na
ikawa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali.
Kutoka 14:15-16 “BWANA akamwambia Musa,
Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo
yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli
watapita kati ya bahari katika nchi kavu.”
Unaona hapa kwa maelekezo ya
Mungu wana wa Israel walivuka kikwazo cha bahari ya shamu Musa akipewa maelekezo
ya kuitumia fimbo, nasisitiza tena kwa maelekezo Nawe inua fimbo yako unaona!
Mungu ndiye aliyemuelekeza Musa kutumia fimbo iliyokuwa mkononi mwake kufanya
ishara na miujiza, na ni katika hali kama hiyo wana wa Israel walipokuwa
wanapaswa kuvuka ng’ambo ya Mto Yodrani
Mungu alitoa maelekezo mengine kwa kiongozi aliyekuwepo Yoshua Mungu
alitoa maelekezo mengine namna watakavyouvuka mto wa Yordani ona.
Yoshua 3:5-8 “Yoshua akawaambia watu,
Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu. Kisha Yoshua
akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao
watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu. Bwana akamwambia
Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya
kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa. Nawe
uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika
ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani. Basi Yoshua akawaambia wana
wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu. Yoshua akasema,
Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa
kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na
Mwamori, na Myebusi. Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka
mbele yenu na kuingia Yordani. Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika
kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja. Itakuwa, wakati nyayo za makuhani
walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya
Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo
yatasimama kama chuguu.”
Unaona kwa mara nyingine tena
katika matukio yenye kufanana kuvuka bahari ya shamu na kuvuka mto wa Yordan
Mungu akiwa ni yule yule lakini wakati wanatoa maelekezo ya kuvuka mto wa Yordani
alitoa maelekezo mengine ni katika mtindo huo huo wakati wa waamuzi Mungu
aliweza kutoa ushindi kwa waamuzi hao kwa nyenzo mbalimbali ambazo Mungu
aliweka mkono wake na kuwapa ushindi mfano:-
1. Mungu
alimtumia Mwamuzi Shamghari kuwapa Israel ushindi kwa kutumia konzo la ng’ombe Waamuzi 3:31 “Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari
mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng'ombe;
yeye naye aliwaokoa Israeli.” (Konzo la Ngombe ni mti mgumu
unaotumika kuunga gari au kokoteni unaosukumwa na Ngombe)
2. Mungu
alimtumia Yael Mwanamke kuleta ushindi kwa wana wa Israel dhidi ya Sisera kwa
kutumia nyundo na kigingi Waamuzi 4:17-21 “Lakini
Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa
maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi,
Mkeni. Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu,
karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa
bushuti. Akamwambia, Tafadhali nipe maji
kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa,
akamfunika. Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye
yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana.
Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi
mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho
kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika;
basi akazimia, akafa.”
3.
Muda usingeweza kutosha kuona namna Mungu
alivyotumia watu mbalimbali na nyenzo mbalimbali kutenda miujiza na kuwaletea
ushindi watu wake lakini hatimaye tunamuona Samsoni naye baada ya kujiliwa na
Roho wa Mungu akiua Simba bila kitu chochote Mkononi ona
Waamuzi 14:5-6 “Ndipo
Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya
mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana
ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala
hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama
yake aliyoyafanya.”
Maana ya kuua simba bila kitu chochote mkononi.
Tunajifunza nini katika mifano
hiyo hapo juu namna na jinsi Mungu alivyotumia njia mbalimbali katika
kuiwasaidia watu wake kupata ufumbuzi na changamoto zilizokuwa zikiwakabili,
nikiwa nimetulia zangu natafakari tu kuhusu Mungu ghafla ujumbe huu ulinijia
nilimsikia Roho Mtakatifu mwenyewe akiniambia neno HILI KUUA SIMBA BILA KITU CHOCHOTE MKONONI na mawazoni ilikuja moja kwa moja picha ya
Samsoni akikabiliana na mwana simba na kumuua Biblia inasema akampasua mwana
simba, nikawaza na kufikiri kwa haraka kuna jambo gani Roho Mtakatifu anataka
kuniambia, Mungu kweli alifanya kazi na watu mbalimbali lakini pia na waamuzi
mbalimbali kutatua changamoto za wanadamu kwa kutumia vifaa mbalimbali, lakini
mwamuzi maarufu zaidi Samsoni katika tukio la kuua simba alitumia mikono tu
bila ya kuwa na kitu chochote Mkononi.
Leo hii kumekuwepo na idadi kubwa
sana ya matumizi ya vifaa vya kiroho, watu wanaponywa na kuamini katika
uponyaji na usuluhishi wa changamoto zao kupitia vifaa vya kiroho, chumvi,
mafuta, maji ya Baraka, udongo, vitambaa, sabuni na kadhalika kila mmoja akidai
ni muongozo aliopewa na Roho Mtakatifu, hatuwezi kuingilia maelekezo yao na
wala hatuwezi kukataa kuwa vinafanya kazi kwa jina la Yesu, vinafanya Lakini
tusisahau pia kuwa Mungu ametuagiza kutumia mikono yetu kwaajili ya uponyaji na
kwa kutumia jina la Yesu ona kwa mfano:-
Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana
na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka
mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Maandiko yanatufundisha kuwa
tunaweza kukemea pepo na changamoto nyingine na zikaondoka kwa kutumia jina la
Yesu tu, na tunaweza kuweka mikono yetu juu ya wagonjwa nao wakapata afya pia
tunaweza kutumia vinywa vyetu na tukamuomba Mungu naye akafanya bila haja ya kutumia
vifaa vya kiroho, matumizi ya vifaa vya kiroho yanaonyesha udhaifu mkubwa sana
wa kiimani katika nyakati tulizonazo, watu wanahitaji sana kuona vitu vinavyoonekana
na vitu ambavyo wanaweza kugusa ndipo waweze kuamini Mungu wetu ni mwenye nguvu
kubwa sana aliiumba ulimwengu kwa neno tu na kila kitu kikawa kama kilivyokuwa
kuua simba bila kitu chochote mkononi ni ishara ya kuwa yako mambo Mungu
anaweza kuyafanya bila kuhitaji kutumia vifaa vya kiroho, Roho Mtakatifu
anataka kulikumbusha kanisa kurudi katika utukufu wake na kuondoka katika
udhaifu kutumia vifaa vya kiroho ni kwa watoto wachanga kiimani ni ishara ya
kuwa kanisa limepoteza mamlaka, kanisa limesahau msingi wa matumizi ya Jina la
Yesu jina lanye uwezo wa kufanya lolote hata bila msaada wa kitu chochote cha
kuonekana ufike wakati sasa kanisa
tubatilishe mambo yote ya kitoto,
1Wakorintho 13:11 “Nilipokuwa mtoto
mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri
kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya
kitoto.”
Kuua Simba bila kitu chochote mkononi
Kama nilivyogusia hapo juu ni
kuwa kuua simba bila kitu chochote mkononi kunamaanisha uwezo wa kukabiliana na
changamoto zozote kutoka kwa ibilisi kwa kutumia jina la Yesu hata bila kutumia
vifaa vya kiroho, Maandiko kinabii yanamtafasiri Shetani kama simba aungurumaye
akitafuta mtu aweze kummeza ona 1Petro
5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki
wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
Shetani pamoja na changamoto zote
zinazotokana na yeye ni simba aungurumaye kanisa likirejea katika mamlaka yake
na nguvu zake litakuwa na uwezo wake na nguvu zake za awali watakuwa na ufahamu
kuwa iko mamlaka kubwa ya kutamka jina la Yesu na likaleta matokeo makubwa jina
lenyewe tu peke yake hata bila ya kifaa chochote cha kiroho sio kila wakati
tutatumia tu vifaa vya kiroho sio kila wakati Mungu atatoa maelekezo yale yale
lakini kukaa katika uwepo wa Mungu kunatusaidia kuwa na mamlaka ya kutosha
kutamka neno na ikawa
-
1Wafalme
17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi,
akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama
mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.”
-
2Wafalme
4:16 “.Akasema, Panapo wakati huu mwakani,
utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie
mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume
wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.”
-
2Wafalme
7:1 “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana
asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli,
na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.”
-
Matendo
3:6-9 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala
dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa
Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na
vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza
kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu
Mungu. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.”
-
Matendo
13:8-12. “Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo
tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa
kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu,
akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi,
adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia,
mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara
kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika
mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini,
akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”
-
Mathayo
8:5-10 “Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja
alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa
kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida
akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;
lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu
niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu,
Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu
aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni,
Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli.”
-
Marko 11:23-24
“Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu,
Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba
hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote
myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
-
Matendo
3:6-7 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala
dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa
Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na
vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.”
Hitimisho.
Maandiko yote hapo juu ni
ushahidi ulio wazi ya kuwa kama tukisimama imara katika maombi tutaweza kua
simba bila kitu chochote mkononi yaani hatutahitaji sabuni, wala chumvi wala
maji ya Baraka wala udongo wa upako tutatamka tu kwa Imani na kwa mamlaka ya
jina la Yesu na yale yaliyokusudiwa na Mungu kupitia watumishi wake yatatimia,
kuuwa simba bila kitu chochote mkononi ni shara ya ushujaa wa ngazi ya juu
sana, kama ilivyo katika jamii ya kimasai,
Neno la Mungu limetaja watu watatu tu
ambao walikuwa na uwezo wa kuua simba bila kutumia silaha ama kitu
Mkononi
Samsoni - Waamuzi 14:5-6 “Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia
Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba
akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba
anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini
hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.”
Daudi – 1Samuel 17:34-36 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga
kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo
wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake;
na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua
simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa
sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”
Benaya - 2Samuel 23:20-21. “Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli
aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia
akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji. huyo naye akamwua
Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye
alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki
wake mwenyewe.”
Biblia inaonyesha mashujaa
wakubwa watu hodari waliowahi kuua simba ambao ni Samsoni, Daudi na Benaya na
benaya ndiye anaonekana kuongoza katika kufanya mauaji ya simba wengi zaidi,
kufikia ngazi hii ya juu zaidi ya ushujaa ndilo jambo ambalo Mungu
analitazamia, kwa kila mmoja wetu, ifikie wakati hata kama tutasahau kifaa
fulani cha kiroho lakini tuwe na uweza na mamlaka ya kiungu na uwezo wa kutumia
Jina la Yesu na mamlaka katika jina hilo
kusababisha mambo makubwa ya uponyaji na miujiza na utatuzi wa changamoto
mbalimbali wakati mwingine bila haja ya kutumia kifaa chochote cha kiroho, hii
ndio ngazi ya juu kabisa ya kimamlaka ambayo tunapaswa watu wa Mungu kuitafuta
na kuitumia.
Matendo 4:12 – “Wala hakuna wokovu katika
mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa
wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Wafilipi 2:9-1 1 – “Kwa hiyo tena Mungu
alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la
Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya
nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu
Baba.”
Matendo 2:21 – “Na itakuwa kila
atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”
Warumi 10;13 – “Kwa kuwa, Kila
atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.”
Kanisa ni muhimu kwetu kukumbuika
na kujiimarisha kiimani katika matumizi ya jina la Yesu na kusababisha mamlaka ya
kiungu kutokea na kutenda kazi na kupunguza dhana ya matumizi ya vifaa vya
kiroho, matumizi ya jina la yesu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali bila
kutumia vifaa vya kiroho ndio kuuwa simba bila kitu chochote Mkononi.
Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni