Ijumaa, 18 Agosti 2023

Mungu anajua mwanzo -mwisho!


Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.  Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.  Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”



Utangulizi:

Maisha ya mwanadamu yamejaa siri kubwa sana ambayo majibu ya maswali mengi ambayo wanadamu hujiuliza yanajibika tu kwa kuwa na ufahamu wa kutosha katika maandiko na katika kumjua Mungu na kuwa na uhusiano wa kudumu na Mungu, haijalishi umepitia changamoto za aina gani katika maisha au unapitia changamoto gani hata wakati huu somo kama hili linapokujia lakini Roho Mtakatifu amenitaka leo nikujulishe ya kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho, Mungu anayo ramani ya maisha yako na anajua kila kitu kinachoendelea katika maisha yako! Ni yeye pekee mwenye uwezo wa kutangaza mwisho wako tangu mwanzo na sio wanadamu!

 Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

Kwa msingi huo hupaswi kuwa na shaka wala kuogopa katika maisha yako kwamba unapitia changamoto za aina gani, wala hupaswi kuogopa kuwa itakuwaje kesho na kesho kutwa kumbuka tu kuwa Mungu yuko kwenye udhibiti wa kila jambo linalotendeka na linalotokea katika maisha yako yeye pekee ndiye anayejua maisha yako mwanzo mwisho na sio wanadamu, leo tutachukua Muda kujifunza somo hili Mungu anajua mwanzo mwisho kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Mungu anajua yote.

·         Hakuna utakachopoteza.

·         Mungu anajua mwanzo mwisho.

Mungu anajua yote:

Moja ya sifa kubwa ya Mungu aliye hai na wa kweli ni kuwa ANAJUA YOTE tena anajua mwisho wa kila jambo na anauwezo wa kulisema jambo hilo tangu mwanzo hii ni kwa sababu yeye ana sifa ya kuwa mwanzo na mwisho, (Yaani Alfa na Omega).  Hivyo ni wazi kuwa anajua tunakotoka na tunakokwenda! Ramani yote ya maisha yetu iko mikononi mwake na kwa ujumla yeye ndiye mwenye mpango mzima (Master Plan) ya maisha ya kila mtu duniani,

Ufunuo 21:6 “Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.”

Mwanzo 25:21-23. “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo.”

Unaona hapo kalba hajazaliwa Esau na Yakobo Mungu alishajua mwisho wao utakuwaje hivyo ni wazi kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho wa kila mtu, maisha yetu yameratibiwa na Roho wake Mtakatifu tangu itakavyokuwa mwanzo mpaka mwisho! Mungu anajua mwanzo mwisho!          

Kwa ujumla kuna maeneo makubwa matano yanayotumika kuelezea sifa za Mungu ambazo hakuna kiumbe kingine chochote kinaweza kuwa na sifa hizo isipokuwa Mungu peke yake, sifa hizo ni pamoja na:-

-          Mwenye nguvu zote – Omnipotence

-          Mwenye kujua yote – Omniscience

-          Mwenye kuweko mahali kote kwa wakati mmoja – Omnipresence

-          Asiyebadilika – immutability

-          Ni wa Milele na milele – Transcendence

Kwa Mujibu wa wanatheolojia hizo ni sifa ambazo mwanadamu au kiumbe cha kawaida hakiwezi kuwa nazo isipikuwa Mungu peke yake, hata hivyo sio kusudi langu leo kuelezea sifa zote tano za Mungu lakini nataka kuchukua Muda kuelezea sifa moja tu ya MWENYE KUJUA YOTE kwa kusudi tu la kutimiza leongo la somo hili:-

Neno hilo MWENYE KUJUA YOTE Katika lugha ya kiingereza linatumika neno OMNISCIENCE  ambalo kimsingi ni neno la asili ya lugha ya kilatini linalojumuisha muunganiko wa maneno mawili Omnis -  ambalo kwa kiingereza ni ALL ikiwa na maana ya Kiswahili YOTE/WOTE na neno SCIENTIA ambalo kwa kiingereza ni KNOWLEDGE ambalo kwa Kiswahili ni MAARIFA, au UJUZI kwa hiyo linapoungwanishwa pamoja tunapata neno OMNISCIENCE  ambalo kwa kiingereza ni ALL KNOWING na kwa kiwahili KUJUA YOTE  na sasa basi linapotumika kuelezea sifa za Mungu linatumika kuelezea kuwa Mungu anajua yote hivyo hakuna jipya kwake wala hakuna jambo wanadamu watagundua ambalo Mungu hakuwa analijua yeye anajua kila kitu, kwa hiyo kila jambo linalokutokea katika maisha yako haimaanishi kuwa Mungu hakuwa na taarifa nalo, wala Mungu hasahau kitu kwa sababu amekuwepo toka milele na anaendelea kuwepo na yupo hata milele kwa hiyo Mungu anajua kila kitu na hakuna cha kumshangaza !

Katika maisha yetu hakuna bahati mbaya Mungu anaelewa mwisho na mwanzo wa kila kinachoendelea katika maisha yako, hivyo hupaswi kuogopa na badala yake unapaswa kumsubiri Mungu kwa njia ya maombi, Katika andiko la Msingi tulilolisoma tunaona Mungu akizungumza na Abraham kuhusu uzao wake kizazi cha nne ambao wangeshuka Misri na kukaa huko miaka 400 na kuwa kisha atawarejesha tena katika nchi ya mkanaani ona  

Mwanzo 15:12-16 “Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.  Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.  Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado.”

Unaona ni karibu kati ya miaka 1632-2000 hivi kutoka Abraham mpaka wakati Musa anazaliwa na kuitwa kuwakomboa wana wa Israel, Lakini Mungu anayejua yote anamwambia Abrahamu habari za wana wa Israel namna watakavyoshuka Misri na kutumikishwa huko na kuwa angewapandisha tena  Miaka Mingi sana hata Isaka hajazaliwa wala Yakobo hajazaliwa, huo ni uthibitisho ulio wazi kuwa kila kinachotokea katika maisha yetu kimeratibiwa katika mpango na ratiba za Mungu aliye hai, huna sababu ya kujuta wala kulia katika kila jambo unalolipitia Mungu yuko kwenye udhibiti na makusudi yake yatatimizwa tu, na lile ambalo halijakusudiwa halitatimia !

Hakuna utakachopoteza!

Kama Mungu anajua yote ni wazi kuwa anayajua maisha yetu vema na hakuna lolote linaloweza kuharibu mpango wetu kwake, yote yanayotutokea yawe mema au mabaya yote ni kwa makusudi yake na mapenzi yake ni lazima yatatimizwa, kama Mungu amekuahidi jambo fahamu ya kuwa atalitimiza bila kujali nini kinatokea katika maisha yako kwa sasa kitatimia kwani Mungu ni mwaminifu na wanadamu ni waongo!

-          Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?”

-          2Wakorintho 1:20 “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.

-          2Samuel 2:31 “Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia.”

-          Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.”

-          Mithali 19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”             

-          Ayubu 42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”

-          Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”

Mungu anapokuwa amekusudia jambo Fulani katika maisha yako, ni muhimu kufahamu kuwa jambo hilo halitaweza kuzuiliwa na mtu, Mungu ana makusudi na maisha yako, kila kitu katika maisha yako hata aina ya mapito unayoyapitia yanakuandaa kukuleta katika lile kusudi kwa msingi huo lolote lililo jema au lililo baya lisikutishe wala simama katika mapenzi ya Mungu, jitahidi usitende dhambi lakini naam hata ukitenda  maana hakuna mwanadamu atendaye mema asitende dhambi hiyo haimzuii Mungu kutuimiza mpango wake alioukusudia kwako  kwa sababu yeye anajua mwanzo mwisho yeye ni msaada ulio karibu atafanya njia, atarehemu, atasamehe atakuweka panapo nafasi na kusudio lake lililokusudiwa ndani mwako litatimizwa Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”             

Mungu anajua mwanzo mwisho!

Ni muhimu sasa kuwa na ufahamu kuwa Mungu anajua kila kitu, Mungu anajua mambo yote na ya kuwa makusudi yake hayawezi kuzuilika, ikiwa tunafahamu wazi sasa jambo hilo ni muhimu kuelewa kuwa hakuna kitu ambacho kinafanyika duniani katika maisha yetu ambacho Mungu hajui, Mungu ana taarifa ya mambo mengi sana  na anajua vema kila kitu kwa kina na mapana na marefu, Mungu anajua mambo makubwa na madogo, maandiko yanaonyesha wazi maswala ambayo Mungu anayajua na kuyafuatilia na ukijiweka katika ulinganifu wake utakubaliana nami kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ona:-   

-          Anajua idadi ya nywele zetu Mathayo 10:29-30 “Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.” Maandiko tena kupitia Yesu Kristo mwenyewe yananyesha kuwa hata ndege wa angani hawaanguki chini bila mbingu kuwa na taarifa yaani Mungu anajua kuwa kuna ndege amepigwa, ametegwa, ameliwa na kadhalika pamoja na udogo walio nao, lakini sio hivyo tu hata nywele zetu idadi yake inajulikana na Mungu hiii maaana yake nini maana yake Mungu anajali kuanzia vitu vikubwa mpaka vitu vidogo vidogo vingi  na kama ni hivyo anayajali na kuyajua maisha yako na kila unalilopitia na utakalolipitia na namna utakavyotoka na utakavyotimiza mpango wake  na makusudi yake duniani

 

-          Anatujua Mwanzo mwisho Yeremia 1:4-5 “Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”         Mungu anatujua hata kabla hajaruhusu tuzaliwe duniani wewe na mimi tulikuweko katika wazo lake tangu milele Mungu anamwambia Yeremia nabii kabla hajatungishwa mimba kwenye tumbo la mama yake yeye alikwisha kumjua na alikwisha kuchagua kuwa atakuwa nabii kwa mataifa mbalimbali, Kama Mungu anakujua kuumbwa kwako na kuzaliwa kwako na kama anaweka kusudi lake ndani yetu hata kabla hatujazaliwa ni Dhahiri alijua kila utakachokipitia pia anajua siku zetu za kuwepo duniani, anajua matendo yetu yote mema na mabaya kila kitu katika maisha yetu kimeratibiwa Mbinguni  Zaburi 139:13-18 “Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.  Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.”

 

-          Anajua uhusiano wetu na yeye umesimamaje -                 

Nahumu 1:7 “Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao

Warumi 8:16-17 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”    

Yohana 10:27-29 Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”

Mungu anamjua kila mtu anayemtegemea anayemkimbilia anayemuamini anajua umesimama wapi katika uhusiano wako na yeye, anajua anavyotuhudumia na sisi tu mashahidi kwa kuwa Roho wake Mtakatifu hutushuhudia kuwa sisi ni wana wa Mungu hivyo haki zetu zinahifadhiwa ndani yake kwa nini kwa sababu anajua uhusiano wetu tulionao kwake na njia tutakayoipitia na kule atakakotuongoza anajua mwanzo mwisho!

 

-          Anatujua kwa majina yetu -  alimjua Musa Kutoka 33:12 na 17  alimjua sauli na alimjua Koreshi mfalme wa uajemi hata kabla hajazaliwa tena kwa jina lake kabisa wazi wazi

 

Kutoka 33:11-12Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani. Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.” Na

 

Kutoka 33:17’ “BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”               

 

Alimjua Sauli aliyekuwa analiudhi kanisa ona Matendo 9:1-5 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.”

 

Alimjua Koreshi hata kabla hajazaliwa Isaya 45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake,ambaye nimemshika mkono wake wa kuume,ili kutiisha mataifa mbele yake,name nitalegeza viuno vya wafalme;ili kufungua milango mbele yake,hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;”

 

Ni jambo la kushangaza sana Mungu alimjua Musa kwa jina lake, Mungu alimjua Sauli ambaye alikuwa analiudhi kanisa na kumuita ili awe mtume Mungu, alimjua mfalme Koreshi wa uajemi kabla hajazaliwa, Isaya alitaja habari zake na Mungu alijua kuwa atamtumiaje maandiko haya yote ni mjumuisho wa taarifa tu kuwa Mungu anatujua anajua huduma alizotuitia anajua utumishi aliotuitia anajua mapito tunayoyapitia anajua kila kitu kinachoendelea katika maisha yetu.

 

-          Anaijua mioyo yetu. 

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

 

1Falme 8:39 “basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote)”

 

Mungu anaijua mioyo yetu anajua kama uko uovu ndani yetu anajua kama mioyo yetu ni safi, ama ina ugonjwa wa kufisha yaani kama tunayoyawaza yatapelekea mauti ni yeye pia aliye tayari kuitakasa mioyo yetu kama tutakuwa radhi na kuwa na hiyari ya kuyadai na kuyataka mapenzi yake.   

 

-          Anayajua mawazo yetu - Mungu anayajua mawazo yetu anajua kila jambo analoliwaza mwanadamu anajua pia tunapokusudia kutenda uovu anajua Mwanzo 6:5-6 “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.” Mungu aliyasoma mawazo ya wanadamu wakati wa Nuhu na kuona kuwa ayoyakusudia ni maovu tu hii maana yake ni kuwa kila wazo linalotembea katika akili zetu Mungu analiona na hakuna kilichofikichika Zaburi 139: 1-2 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.” Unaona Mungu anajua mwanzo mwisho analiona wazo la mwanadamu tokea mbali, tunaweza kuwatisha watu kwa kujifanya tunajua kila kitu na tunajua kila wanachokifikiri lakini Mungu tayari anajua anaujua ukweli, hakuna kinachoweza kufichika.

 

-          Anajua hofu zetu – achilia mbali kwamba Mungu anayajua mawazo yetu, Mungu anazijua pia hofu zetu na kutuponya nazo zote, Mapema sana Yesu akijua mahitaji Muhimu ya wanadamu ambayo wamekuwa wakihofia aliwaondoa wasi wasi kuwa Mungu anajishughulisha sana na mambo yetu  yawe kwa heri au kwa shari atashughulika katika njia iliyobora na njema zaidi.

 

Mathayo 6:25-34 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.  Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

 

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

 

Baba yetu wa mbinguni anajua tunayoyahitaji kwa sababu hiyo wajibu wetu ni kuomba tu ambako ndiko kumtwika yeye fadhaa zetu zote na tunaambiwa kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu maana yake anashughulika vema na hofu zetu na anajua njia sahihi na namna sahihi iliyo bora ya kutupatia mahitaji yetu

 

-          Anayajua matendo yetu – Kama Mungu anayajua mawazo yetu na anajua hofu yetu sembuse matendo yetu? Mungu anayajua yote hata yale tuyatendayo sirini maandiko yanatueleza kuwa wakati wa hukumu Mungu ataweka wazi kila tendo na kila neno la siri tulilolitenda na pia kazi za wapendwa wote zitapimwa kulinga ana nia ya kila mmoja Mungu anajua Mungu anajua alionya sana katika nyaraka saba kwa makanisa saba kule Asia katika kitabu cha ufunuo kuwa anajua anajua na akatoa maelekezo sasa kwao

 

Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

 

2Wakorintho 5:9-10 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”

 

Ufunuo 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”

 

Mungu hataleta hukumuni mambo asiyoyajua ataleta hukumuni ushahidi ulio wazi wa matendo yetu yote na maneno yetu yote lakini pia waamini watapimwa na Kristo katika kiti cha hukumu so kwaajili ya hukumu bali kwaajili ya kazi tulizozifanya hapa duniani, Mungu anajua pia tuyatendayo na nia yake kwa nini tunayatenda

 

-          Anayajua maneno yetu - Mungu anayajua maneno yetu yote kama Mungu mwenye kujua yote hakuna neno lolote tunalolisema katika ndimi zetu ambalo linampita anayajua vema

 

Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”

 

Mathayo 12:35-37 “Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

 

-          Anazijua njia zetu – Kuna maandiko memngi sana yanayothibitisha au kuonyesha Mungu akizungumza kuhusu njia zetu lakini maandiko hayo yanatutaka tumkabidhi yeye njia zetu kwa kuwa anaijua njia tuiendeayo Ayubu 23:10 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.” Yeye kama Mchungaji mwema wakati wote hutuongoza katika njia inayofaa Zaburi 23:3-4 “Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” Mithali 16:9 “Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.”

 

Kwa kuwa Mungu anajua njia kwa usahihi hii maana yake mipango yetu yote ni vema tukimkabidhi yeye mipango yetu yote au kuomba Muongozo kutoka kwake lakini vyo vyote iwavyo Mungu anajua mwanzo mwisho               .

 

Anayajua madhaifu yetu – Mungu anayajua madhaifu yetu na anajua namna nzuri ya kuchukuliana nasi tofauti na jinsi wanadamu wanavyotuchukulia yeye hutuchukulia kwa rehema kwa sababu anatujua kuwa sisi ni Mavumbi

 

Zaburi 103:8-14 “Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”

 

2Wakorintho 12:9-10 “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

 

-          Anajua siku za uhai wetu Duniani

Wanadamu kwa kawaida hatujui siku za maisha yetu ni ngapi, Mungu ametuficha lakini yeye mwenyewe anajua anajua siku za maisha yetu anaweza kutusaidia kutujulisha ili kwamba tuzitumie kwa hekima ona Zaburi 90:12 “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”

 

Yakobo 4:13-14 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.” Maisha ya uhai wetu uko mikononi mwa Mungu, maisha yetu ni kama mvuke hatujui yatakayokuwako kesho, Lakini Mungu anajua kila kitu anajua mambo yote, unaweza ukafichwa usijue siku yako lakini kwa Mungu hakuna geni wala la kushangaza.

Hitimisho:

Kwa kuwa tumejifunza kwa kina na kuelewa kuwa Mungu anajua mwanzo mwisho ni muhimu kwetu kutokuogopa tunapokuwa  katika mapito ya aina yoyote duniani, ni lazima tuelewe na kukubali kuwa kila linalotutokea katika ulimwengu huu liko chini ya uwezo wa kiungu kazi yetu ni kuomba na kumuacha yeye atimize mapenzi yake, Mungu alimwambia Ibrahimu maswala yote yatakayojitokeza baadaye kizazi chake cha nne ambao walishuka Misri na baada ya miaka 400 kuwa angewapandisha tena walishuka kupitia Yusufu unajua yaliyomkuta Yusufu unajua yaliyowakuta wana wa Israel safari haikuwa nyepesi lakini tumeelewa kuwa Mungu alikuwa kwenye udhibiti, kila linalotutokea kwenye maisha yetu hatupaswi kuogopa tunaye Mungu anayejua yote tukiyajua haya tutafahamu kuwa haupaswi kujisumbua katika jambo lolote lile isipokuwa kwa kila jambo kwa kusali na kuomba na kumuacha  Mungu afanye kazi yake Mungu anajua maisha yetu anajua uendako anajua utokako hakuna lililofichika kwake kuhusiana na maisha yako hivyo usifadhaike! Wala usihuzunike moyoni mwako Mungu anajua Mungu anaona na Yeye atatenda. Mapenzi yake yatimizwe katika maisha yetu kwaajili ya utukufu wake.

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Hakuna maoni: