Zaburi 57:1-3. “Unirehemu, Ee Mungu,
unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa
mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.
Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka
toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka
Fadhili zake na kweli yake”
Utangulizi:
Moja ya zaburi zenye utajiri wa
kutufundisha kumuamini Mungu katika mazingira magumu na ya aina yoyote ile ni
Pamoja na Zaburi hii ya 57, Kihistoria Zaburi hii iliandikwa au kutungwa katika
mazingira ya wakati Daudi anamkimbia Mfalme Sauli ambaye alikuwa amekusudia
kumuua kwa vile ni kijana aliyeonyesha kuwa anaweza kuwa mfalme baada ya Sauli,
Daudi alikimbia katika Pango liitwalo Pango la Adulamu na watu kadhaa
wakamfuata huko pamoja na ndugu zake kwaajili ya usalama wao na kulitumia pango
hili kama ngome ya kujificha dhidi ya Adui zake ona
1Samuel 22:1-2 “Basi Daudi akaondoka huko,
akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake
waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya
dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao,
wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye
walipata kama watu mia nne.”
Unaweza kuona kwa nini maandiko
yanasema Daudi akaondoka huko akakimbilia Pango la Adulamu? Sababu kubwa ni
kuwa Daudi alikuwa ametiwa Mafuta ili awe mfalme baada ya Sauli kwa mapenzi ya
Mungu ona
1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli,
Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze
pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana
nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli
akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme,
Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami
nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”
Baada ya Daudi kutiwa Mafuta ili
aje kuwa mfalme baadaye uweza wa Mungu ulikuwa juu yake, Roho Mtakatifu alikuja
juu ya Daudi kwa nguvu na kuanza kumtumia katika kazi zake kwa uhodari Mkubwa
ona
1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia
Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama,
anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa
sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao.
Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza.
Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa
pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana
ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake
Rama.”
Maandiko yanatuonyesha kuwa Daudi
alianza kuwa Mtu shujaa kutokana na uweza wa Mungu uliokuwa juu yake kupitia
Roho Mtakatifu, aliweza kuwalinda kondoo wa Baba yake walipokuwa
wakihatarishiwa maisha na Simba na dubu pamoja na wanyama wakali sana bila
kujulikana ushujaa wake lakini Zaidi sana alikuja kujitiokeza kama shujaa wa
kitaifa pale alipokabiliana na adui wa kutisha wa Israel aliyeitwa Goliati na
kujipatia umaarufu mkubwa hata kuliko Sauli jambo lilopelekea kuanza kuwepo kwa
wivu na visa vya kutaka kuuawa na Mfalme Sauli:-
1Samuel 17:49-51 “Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja,
akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo
likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule
Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa
na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti,
akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga
huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.”
1Samuel 18:6-9 “Hata ikawa, walipokuwa
wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka
katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli;
wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana
wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi
Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi
makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa
ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”
Ni katika mazingira kama haya
sasa ndipo tangu wakati huo Daudi alianza kuwindwa na Sauli ili yamkini akipata
nafasi aweze kumuua, na kwa kweli mara kadhaa Daudi alikoswa koswa kuuawa kwa
mkuki kupitia na njia nyinginezo, Sauli
ambaye alikusudia kumtenda vibaya kwa
ujumla Sauli alikusudia kumuu a Daudi mara saba
1Samuel 19:10-12 “Ikawa siku ya pili yake,
roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya
nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye
Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana
alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara
mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila
amemwacha Sauli.”
Ni katika mazingira kama hayo ya
kuwindwa kila wakati na kutaka kuuawa ndipo Daudi alipoanza kuishi maisha ya
kuhama hama huku na kule akijificha kwaajili ya kuokoa uhai wake ndipo sa
tunamuona Daudi pamoja na kundi kubwa la watu wanyonge wakimkimbilia na
kumfuata naye akawa kamanda wao hii ndio sababu ya Daudi kukimbilia katika
Pango la Adulamu.
Tutajifunza somo hili sasa
kumwamini Mungu tokea Pangoni kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kumkimbilia
Mungu wakati wa shida zetu
·
Kumsifu
Mungu wakati wa shida zetu
· Kumwamini Mungu tokea Pangoni
Kumkimbilia Mungu wakati wa shida zetu.
Baada ya kuwa tumeona changamoto
aliyokuwa akikutana nayo Daudi akitafutwa kuuawa na huku akiwa amekoswa koswa
kuuawa mara saba kutoka kwa sauli, tunamuona Daudi akikimbia sasa kutoka kwa
Sauli na kwenda kujificha katika Pango la Adulamu, tunaweza kujiuliza kuwa ni
kwanini Daudi alifanya jambo hili? Ni ukweli ulio wazi kuwa Daudi alikuwa
anatafutwa na Mfalme Sauli na Sauli hakuwa peke yake alikuwa na Jeshi kubwa la
wateule yaani watu waliochaguliwa kuwa wanajeshi wenye uzoefu mkubwa na ni hodari katika vita
kwa hiyo unaweza kuona wazi kabisa kwamba Daudi alikuwa hatarini kweli kweli
kwa ujumla Jeshi alilokuwa nalo Sauli lilikuwa na watu hodari wa vita wapatao
elfu tatu (3000) ona
1Samuel 24:1-2 “Ikawa, Sauli aliporudi
baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya
Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote,
akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.”
Kwa bahati mbaya Biblia ya
Kiswahili ya (SUV) iliacha neno tatu kwa hiyo inasomeka kama watu hao walikuwa
Elfu lakini matoleo mengine ya kiingereza likiwepo toleo la kiingereza cha KJV
ambapo ndipo tafasiri ya Biblia ya Kiswahili inakotokea yanaonyesha kuwa
lilikuwa jeshi la watu 3000 unaweza kuona mfano:-
NIV inaonyesha 3000 1Samuel 24:1-2 “After
Saul returned from pursuing the Philistines, He was told, “David is in the
Desert of Engedi. So Saul took three thousand able young men from all Israel
and set out to look for David and his men near the Crags of the wild goats”
KJV inaonyesha pia 3000 1Samuel 24:1-2 “And
it came to pass, when Saul was returned from following the Philistines, that it
was told him, saying, Behold David is in the wilderness of Engedi, then Saul
took three thousand chosen men out of all Israel and went to seek David and his
men upon the rocks of the wild goats”
Kwa hiyo utaweza kuona mtu
aliyekoswa koswa kuuawa zaidi ya mara saba na sasa anafuatiliwa na Jeshi kubwa
la wanajeshi Hodari yaani makomandoo walio na mafunzo ya kivita katika Nyanja
mbalimbali za kijeshi wanamtafuta Daudi ambaye alikuwa na kundi la watu wasio
na mafunzo kama mia nne tu wastani kila
askari wa Daudi alikuwa na askari wa upinzani saba hivi wa kupigana nao, kwa
hiyo kukimbilia Pangoni pekee kulikuwa hakutoshi wala hakukuwa salama kwa
sababu wapelelezi walimueleza Sauli kila alikokimbilia Daudi na sasa Daudi
anajua kuwa anapaswa kumkimbilia nani katika msiba wake Daudi alijiona kama
kwamba anazungukwa na simba wakali na msaada wake ulikuwa ni Mungu tu:-
Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu,
unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa
mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu
anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule
atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake”
Daudi anatufundisha ya kuwa wakati
wote tunapokutana na changamoto mbali mbali katika maisha yetu hatuna budi
kumkimbilia Mungu, yeye ndiye anayeweza kuturehemu na kusaidia katika shida
zetu, kukimbilia Pangoni ni sawa tu na mtu akiwa anaumwa anaweza kwenda
Hospitali kwaajili ya msaada wa kawaida wa kibinadamu lakini changamoto
nyingine haziwezi kutatuliwa hospitali wala haziwezi kutatuliwa na ujuzi wetu
na ushujaa wetu na utaalamu wetu na elimu zetu na vyeti na kadhalika lakini
neno la Mungu linatueleza wazi ya kuwa tunaweza kumkimbilia Mungu na tunaweza
kulitumainia jina lake na tukawa salama, Daudi alikuwa na uelewa huo kuwa
Usalama wake utatoka kwa Mungu tu na hivyo ingawa amekimbilia katika Pango la
Adulamu bado anatufundisha kuwa pango pekee halitoshi kwani yuko Mungu
anayeweza kutupa uvuli, anayeweza kututimizia mambo yetu anayeweza kutuokoa kwa
msaada kutoka mbinguni anayeweza kupeleka fadhili zake kwa watumishi wake huyo
tukimtumaini na kumkimbilia tunajihakikishia usalama wa kutosha !.
Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome
imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Daudi anakimbilia
katika lile Pango akiwa katika hali ya kuvunjika moyo amenusurika kuuawa mara
saba na sasa anamkimbia Sauli, anajiona nafsi yake kuwa sasa kwa msala huu
anaweza kuuawa anachukiwa mno anapingwa mno, hakuna wa kuweza kumsaidia
isipokuwa Mungu peke yake, Kaka zangu na dada zangu tunapopita katika
changamoto mbalimbali za maisha haya hakikisha ya kuwa unamkimbilia Mungu,
mfanye yeye kuwa kimbilio lako!. Mkimbilie
yeye na fungua kinywa chako kuomba mwambie nakuhitaji hakuna wa kunisaidia ila
wewe Mungu katika hali yangu naye atakufanikisha.
Kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.
Kuna nguvu kubwa sana katika
kumsifu Mungu, Daudi alikuwa na ufahamu mkubwa sana wote tunajua kuwa katika
maisha yake Daudi hakuwahi kushindwa vita, moja ya siri yake kubwa ya ushindi
ukiacha kupakwa mafuta, ukiacha kumkimbilia Mungu, ukiacha kutafuta uso wa
Mungu ili aweze kujua mapenzi ya Mungu katika kila alilokuwa anataka
kulifanya yeye alitangulia kumsifu Mungu
kwa Imani akitarajia ushindi mkubwa ya kuwa Mungu atafanya kitu, hii
inatufundisha kumsifu Mungu wakati wa shida zetu.
Zaburi 57:5-11 “Ee Mungu, utukuzwe juu ya
mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. Wameweka wavu ili kuninasa miguu;
Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake! Ee
Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,
Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri. Ee Bwana,
nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa. Maana fadhili
zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni. Ee Mungu,
utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.”
Wako watu wengi sana katika
maandiko ambao walipokuwa wakikabiliwa na mambo magumu walimsifu Mungu wakiwa
katika shida zao na Mungu akawakomboa mfano mmojawapo ni Paulo na Sila
waliomsifu Mungu wakiwa gerezani.
Matendo 16:25-28 “Lakini panapo usiku wa
manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu,
na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la
nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka,
vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya
kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya
kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema,
Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.”
Kumwamini Mungu tokea Pangoni.
Daudi kama tulivyojifunza ya kuwa
alikuwa anakabiliwa na jeshi kubwa na zaidi ya yote alijiona kama yuko katikati
ya simba kwa ujumla ukiitazama hali halisi utaweza kujua kuwa Daudi alikuwa anawindwa na kuzungukwa na hatari
kubwa adui yake alikuwa Sirius sana, alikuwa amemaanisha kumua kama Sauli
alijaribu kumuua Daudi mara saba na sasa anamfuatia kwa silaha kali, na Jeshi
la watu 3000 ni Dhahiri kuwa alikuwa na msako mkubwa sana wa kumfanya Daudi
kuwa kitu kibaya sana
Zaburi 57:4 “Nafsi yangu i kati ya simba,
Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na
ndimi zao ni upanga mkali.”
Daudi anakubaliana wazi kuwa adui
zake walikuwa na nguvu kuliko yeye walikuwa wengi na wenye uzoefu wa vita,
walikuwa na umri mkubwa kumzidi, anakumbuka alivyokuwa akikabiliana na simba huko
nyikani na anakumbuka alivyoweza kupata usingizi kati ya simba lakini kwetu sisi kama kanisa
tunafahamu Simba huyu ni adui yetu
mkubwa yaani shetani.
1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
Licha ya kuwa maadui hawa
walikuwa na nguvu kama simba lakini pia ndimi zao na meno yao yaani nguvu yao
ni mikuki na mishale lakini pia walikuwa wakinena maneno mabaya sana dhidi ya
Daudi, kwa ujumla walikuwa ni wenye nguvu, hodari wenye silaha kali na maneno
yao makali ya kutisha sana lakini pia walimtukana Daudi; Daudi alimuamini
Mungu, aliamini kuwa atastarehe kati yao waliowaka moto yaani ni kama adui zake
watageuka majivu tu Mungu atawafanya kuwa sio kitu, Mungu atawageuza kuwa kitu
kilichoteketea na watakuwa kama mavumbi ya majivu watatoweka wote na
hawatakuwako tena!, tunajifunza ya kuwa ni lazima kumwamini Mungu bila kujali
unapitia hali gani, hata kama hali hiyo inatisha kiasi gani, hata kama gonjwa
hilo linatisha kupita kawaida, hata kama, hata kama afya yako haijatengemaaa mwamini Mungu ya
kuwa anaweza kukusaidia na utakuwa salama atawafutilia mbali adui zako, kikla
kinachosumbua katika maisha yako kitafanywa kuwa majivu katika jina la Yesu
Kristo.
Hitimisho:
Zaburi hii imeandikwa wakati
Daudi akiwa katika mateso ya kumkimbia mfalme Sauli na Daudi alikuwa
amekimbilia huko Adulamu, na ni katika kumbukizi hii zaburi ikaandikwa, ni
wakati alipokoswa koswa kuuawa mara saba. Zaburi imegawanyika katika makundi
makuu mawili aya ya 1-6 anakimbilia rehema za Mungu, na kumuomba na kumlilia
ili aweze kumpa msaada aya ya 7-11 Anaonyesha Imani na ujasiri na kumsifu Mungu
na kumtukuza kutoka Pangoni kwa Imani akijua kuwa fadhili za Mungu ni kuu na
Mungu hatampungukia, tunaweza kumsifu Mungu hata kama tumepungukiwa, hata kama
ndoto zetu zinaonekana kupotea au kufifia, Daudi alikuwa amepakwa mafuta kuwa
mfalme na sasa anakimbia mbali na kiti cha ufalme anaishi Pangoni mbali na nyumba
ya Mungu hakutumia muda huo kulalamika lakini aliamini kuwa Mungu aliye mwema
bila kujalisha yuko Mazingira gani atamtoa na kumuokoa na mwaswaibu yanayomkuta
Yeye alimuamini Mungu tokea pangoni wewe unamwamini Mungu ukiwa wapi? Kwa wale
wenye vita za kiroho na watu wenye wivu siku zote kumbuka kwamba kiwango cha
watu wanaokupiga vita kinaonyesha ni kiwango gani cha utukufu Mungu anakupa,
kama unapigwa vita na mfalme ujue wewe ni mfalme ajaye.
Na. Rev Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni