Zaburi 23:1-6 Biblia inasema
“1. Bwana ndiye
mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 2. Katika malisho ya majani mabichi
hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. 3. Hunihuisha nafsi yangu; na
kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4. Naam, nijapopita kati
ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 5.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa
watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. 6.
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa
nyumbani mwa Bwana milele.”
Bonde la Wadi Quelt linalotajwa na daudi kama Bonde la Uvuli wa Mauti katika Zaburi 23.
Zaburi hii ni moja ya zaburi
muhimu sana na Yenye maneno ya maana sana yenye usalama, Ingawa maandiko yake
ni machache lakini yamebeba maana pan asana na nzito mno isiyoweza kupimika
kuhusu Upendo wa Mungu kwa watu/mtu wake, Ni zaburi ambayo inaweza kutufunulia
kwa kina upana na urefu wa Hali halisi ya uhusiano wa Mfalme Daudi na Mungu.
Tutajifunza Zaburi hii kwa kutafakari vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Historia ya Zaburi hii
·
Bwana ni Mchungaji wa Ajabu
·
Sitaogopa Mabaya
Historia ya Zaburi hii:-
Zaburi ziko za Aina mbalimbali,
lakini zaburi hii inaangukia katika Kundi la Zaburi za kujitia moyo, Katika
moja ya chanzo yaani Commentary ambayo niliiisoma, inatuhakikishia wazi kuwa
zaburi hii ni ya Daudi aliyekuwa mfalme wa Israel, Lakini sababu ambazo
zilipelekea Daudi kuandika zaburi hiii ambayo inaonekana aliiandika kabla ya
kuwa mfalme inazungumzia mazingira ya Bonde liitwalo kwa Kiarabu Wadi Quelt unaweza kugoogle jina hilo
katika wikipidia, Bonde hili liko katika ukanda wa Magharibi yaani West Bank wa
Mto Jordani Karibu na Yerusalem njia ya kuelekea Yeriko karibu na bahari ya
Chumvi, Eneo hilo lilikuwa ni eneo hatari sana na lenye majabali ambapo kama
mtu angeangukia huko kifo tu ndio kingekuwa zawadi yake, ni Bonde la Kutisha
sana na njia yake pia ilikuwa na vibaka na majambazi na huenda ilikuwa ni
simulizi na maonyo kutokupita eneo hilo hatari lililoogopewa sana, Bonde hilo
lenye kutisha lilikuwa ni halisi na ni halisi hata sasa kwa vile liko hata leo,
Kwa vile lilikuwa ni Bonde lenye kuogopesha wengine waliliita Pango la Jabali
au Bonde la Mauti, kuna uwezekano kuwa watu wengi walipoteza Maisha katika eneo
hilo na hata wachungaji walipoteza mifugo yao huko na walishindwa kuiokoa.
Bwana Ni Mchungaji wa Ajabu:-
Daudi anataka kumfunua Mungu
anayemjua Yeye na mwenye uhusiano naye Jinsi alivyomkuu na alivyo na ujasiri
kumtegemea, anataka kuionyesha jamii kuwa yeye anaweza kupita katika Bonde hilo
lenye harufu ya kifo na akatoka salama, kule ambako jamii nzima inaogopa yeye
angeliweza kupita tu kwa sababu hakuna
jambo lolote lenye kuogopesha linaweza kulinganishwa na Mungu wa Daudi na
Mchungaji mwema, Kuweza kufahamu kila Daudi anakizungumzia ni lazima tufanye
uchambuzi wa Maneno mazito yaliyomo katika zaburi hii.
1. Bwana ni Mchungaji wangu – Kwa ufupi
sana Daudi anatumia Mfano huu (Metaphor)
ambao mara nyingi umetumiwa sana na waandishi wa Biblia hususani katika Agano
la kela kuonyesha jinsi Mungu anavyojali na kujihusisha na watu wake (Zaburi 28:9, 79:13,
80:1, 95:7 Isaya 40:11Yeremia 31:10 na Ezekiel 34:6-19) Yesu mwenyewe alikuja kuuweka
wazi kabisa kuwa Yeye ndiye huyu Mchungaji mwema anayetajwa katika zaburi hii
na maandiko mengine Yohana 10:11-16, Ukweli unaofunuliwa
hapa ni sisi ni watoto wa Mungu Mungu ni Baba na ni mwangalizi mkuu wa Maisha
yetu, Yeye hutujali na kutuangalia kwa upendo mkubwa sana kuliko wachungaji
wanavyoangalia mifugo, Jambo kubwa la Msingi ili kunufaika na Bwana kama
ilivyokuwa kwa Daudi ni lazima uwe na uhusiano wa kudumu na Mungu wetu.
2. Sitapungukiwa kitu – Mungu kama
Mchungaji mwema yuko tayari kurupatia malisho, huu ndio ulikuwa wajibu mkuu wa
wachungaji wa wanyama walipaswa kuhakikisha kuwa Konndoo wanashiba ipaswavyo,
ni wazi kuwa Mungu hushughulkika na mahitaji yetu kiasi ambacho hatutapungukiwa
na kitu
3. Kando ya malisho ya majani mabichi hunilaza
– Ulikuwa ni wajibu mwingine wa Mchungaji kuhakikisha kuwa anawapa raha mifugo
yake, ikiwa Mungu ni Mchungaji mwema na sisi tu Kodnoo zake yeye hutupa
kustarehe pia Yesu alisema Njooni kwangu ninyi nyote wenye kuelemewa na Mizigo
nami nitawapumzisha “Mathayo 11:28” haingekuwa hekima ya kawaida common
wisdom kwa Mchungaji kuwazungusha mifugo kutwa nzima bila kuwapa pumziko, Mungu
anajua kuwa tunahitaji pumziko, ingawa tunapitia changamoto za aina mbalimbali
katika ulimwengu huu, Mungu atatupa nyakati za Kuburudika, Acha kusema kuwa
utapumzika Kaburini, au au Heri wafu wafao katika Bwana, hayo maneno Daudi
hakuyatamka hata kidogo yeye alljua kuwa Mungu atampa pumziko sawa kuna hilo la
baadaya lakini hapahapa duniani pia tutafaidika na kazi za Mchungaji mwema,
Mungu atalitumia neno lake kama chakula kutulisha na kututia nguvu,Yohana 6:32
4. Kando ya maji ya utulivu huniongoza. –
Ni wazi kuwa Maji yanawakilisha uwepo na faraja ya Roho Mtakatifu, kwa wale
wakristo amabao wamejazwa Roho mtakatifu wanafahamu jinsi anavyoburudisha na
kuleta utulivu mioyoni mwetu hata kama twapitia majaribu ya aina mbalimbali,
Yeye ndio Chemichemi ya uzima acha kujichimbia visima vyako Yeremia 2:13
Roho wa Mungu yuko kutupa faraja ya kweli, ambayo haipatikani kwa Pombe au
zinaa au uvutaji wa Bangi kila aina ya burudiko na bubujiko lililo bora
utalipata kwa Roho wa Mungu
5. Hunihuisha nafsi yangu – katika
ulimwengu huu tulio nao yako mambo mengi ya kukatisha tamaa na kuvunja Moyo na
kuifanya nafsi kuinama, Mungu wa Daudi aliweza kumtia nguvu alimtia Moyo, Zaburi 42:11,
Tunapokutana na wakati mgumu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali kama
tumemfanya Yehova kuwa Mchungaji wetu atatufariji na kuzihuisha nafsi zetu,
Daudi alilifahamu hilo vema aliona wema wa Mungu ukifanya hayo katika maisha
yake
6. Huniongoza Katika njia za Haki – Ni
muhimu kufahamu kuwa ni Mungu kupitia Roho wake mtakatifu ndiye anayetuongoza
katikia njia ya haki Warumi 8;14, Kwaasili mwanadamu havutiwi sana na
kutembea katika haki, moyo na nia ya kuhakikisha kuwa tunatembea katika haki
hupatikana kwa msaada wa Roho Mtakatifu, na ndio maana ni muhimu ikaeleweka
wazi kuwa haki tuliyo nayo haitokanani na uweza wetu na uamuzi wetu ni haki ya
Yesu Kristo na tunatembea katika hiyo kwa neema na uongozi wake Daudi alilijua
hili wazi,Warumi
8:5-14, alitambua nia ya mwili siku zote inafanya uadui dhidi ya
Mungu na kuwa kama anatembea katika haki ni kwa sababu ya utii wake wa kukubali
kumsikiliza Mchungaji mwema na so sauti ya Mgeni Yohana 10:3-4, 5.
7. Kwaajili ya Jina lake:- Mungu hutufanyia miujiza mikubwa na kutisha na
kushangaza kwaajili ya jina lake, wema wote anaotutendea Mungu hufanya ili
apate utukufu Zekaria 2:8 “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu
amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa
mboni ya jicho lake” Mungu hututetea kwaajili ya Utukufu wake Daudi
alijua wazi kuwa kuna kitu cha ziada ndani yake jina la bwana linatukuzwa na
hivyo kamwe Mungu hataacha kumuongoza katika njia za haki kwa sababu ya Jina
lake takatifu aliloliweka ndani ya Daudi, Mungu akiweka kitu ndani yetu
atatuongoza kwaajili yake
8.
Naam,
nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe
upo pamoja nami:- Daudi sasa analitaja lie Bonde la Wadi Quelt Bonde lenye kutisha sana, ni wazi kuwa Daudi analitumia
Bonde hilo kuonyesha kuwa kuna magumu katika ulimwengu huu kuna mambo ya
kutisha katika ulimwengu huu, Mungu hatatuacha tusipitie katika magumu, na
majaribu, kwamba iwe ni nyakati za hatari, Magumu au hata hatari za kifo Yeye
hataogopa mabaya kwa sababu Mungu atakuwa npamoja nayeYeye ni Mlinzi wetu,na ni
Mwaminifu kamwe hawezi kutuacha Mathayo 28:20 Nami nitakuwa pamoja nayi hata
ukamilifu wa Dahari Mungu ataendelea kuwa pamoja nasi
9.
Gongo
lako na fimbo yako vyanifariji.:- Fimbo na gongo vinawakilisha Mamlaka na silaha
za Mungu pia humaanisha kutia nidhamu, au kurudi, kuadhibu, pia inawakilisha
nguvu na utendaji wa Mungu Kutoka 21:20,
Ayubu 9:34 fimbo ilitumika katika kumrudisha kondoo katika njia au kundi
sahihi na iliwaadhibu pale walipokuwa kinyuma na matakwa ya Mchungaji, Mungu
huwadhibu wale wampendao ili kuwapa nidhamu yeye mwenyewe lakini pia huwalinda
na kuwatetea Gongo liko kwaajili yanulinzi na Usalama wa Kondoo.
10.
Waandaa
meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na
kikombe changu kinafurika.:- Ukweli ni kuwa wanadamu hawafurahii mafanikio
ya wanadamu wengine hata siku moja, kutokana na ubinadamu wao ndani yao kuna
wivu na hivyo ni rahisi kuwa na maadui unapobarikiwa na Mungu, Lakini sio hivyo
tu Mashetani majini na mapepo hayafurahii uhusiano wetu na Mungu, Daudi
alifahamu wazi swala hilo lakini kutokana na ukuu na wema wa Mungu Daudi
anamuona mungu kuwa ni mwenye kujali sana , ni mwenye kujali na kulata usalama
kiasi ambacho pamoja na hatari ya mashetani na majini na mapepo na madui wa
kibinadamu, Bado Mungu anatoa neema na Baraka za Kutosha anakubariki na
kukufanikisha mbele ya wanaokuchukia, na hata wale waliokubali kutumiwa na
shetani kututesa, Licha ya Baraka zake dhidi ya wanaotuchukio Mungu aliendelea
kuonyesha kuwa Daudi ni Mtumishi wake tu ni mtumishi maalumu aliyemchagua
amempaka mafuta! Hii ilikuwa ni Dalili ya wazi kuwa yeye amechaguliwa na Mungu
na ana upendeleo maalumu na wa kipekee ana uhusiano na Roho Mtakatifu ulio wa
Pekee na kwa sababu hiyo hapungukiwi na
kitu, Kikombe kilichofurika kinazungumzia mabalasi yenye uwezo wa kuchukua
Galoni 40 za maji, Daudi alimaanisha kuwa kombe lake linafurika ukiwa na Mungu
huna shaka maana Balasi lako halipungui, Ukimtegemea Mungu hutapungukiwa na
kitu neema na rehema na kufurika roho wa Bwana kutaendelea kububujika siku zote
za maisha yetu.
11.
Hakika
wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani
mwa Bwana milele:- Mchungaji siku zote aliandamana na kondoo kila
walikokwenda uhusiano ulistawi waliwapenda na kuwa kitu kimoja, Daudi amabaye
ana ujuzi mkubwa wa Kuchunga anaelewa wazi kuwa Mungu yuko pamona naye
anafuatana naye akiwa na uso wa wema akiwa yuko tayari kufadhili,alijua kuwa
Mungu akiambatana nawe siku zote atatoa msaada wenye kudumu, wema na fadhili
bila kujali nini kitatokea mbele yako, Mchungaji hufanya shughuli zake zote
kwaajili ya kondoo wake, daudi anamalizia kwa kuonyesha kuwa Lengo lake kuu la
kuambatana na mchungaji huyu mwema ni ili siku moja autazame uso wake amtumikie
na kumuabudu yeye milele.
Nataka
kuhitimisha ujumbe huu kwa kukazia kuwa ukimjua Mungu katika viwango ambayo
Daudi alimfahamu Mungu, Hutaogopa chochote katika maisha yako, Mungu ndio
zindiko letu, yeye ndie Mwamba ngao na kimbilio hatupaswi kuogopa lolote unapotamka
Neno hilo Bwana ndiyo Mchungaji wangu! Kifurushi hicho cha Bwana ndiye
Mchungaji wangu kinabeba maswala kadhaa
Nina uhusiano wa kipekee na Mungu, Yeye ndio anayenitunza, yeye ndiye
starehe yangu na faraja yangu, Yeye ni faraja yangu, yeye ndiye mlinzi wangu,
yeye ni mwaminifu, atanishindia majaribu, nimewekwa wakfu kwake, amanibariki,
amanipa upako, ananitosheleza, niko naye milele mpango wangu ni kutokumuacha
haya yote yatakufanya usiogope kitu chochote katika maisha yako na yeyote
atakayejifanya kuwa ni adui yako atashangaa ukiandaliwa Meza machoni pake,
kwaajili ya utukufu wake.
Ujumbe na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote!
Maoni 2 :
TUMSIFU YESU KRISTO!!
Ahsante sana na mungu mwenyezi akubariki.
Amina ubarikiwe mtumishi
Chapisha Maoni