Ijumaa, 15 Julai 2016

Mwana wa faraja!



Andiko: Matendo 4:36. “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,”

 "Ndani ya Yesu Kristo kulikuwa na huduma ya Faraja, watu walifurahi kumsikia kumgusa na kumuona, ilikuwa Huzuni kwa wanafunzi wake alipowaambia kuwa ataondoka, lakini aliwaahidi kuwaletea mfariji yaani Roho Mtakatifu, ambaye hufanya kazi ya kuwahudumia watu waliomuamini"

UTANGULIZI:

Kufariji maana yake ni tendo endelevu la kuendelea kutia moyo, kutia matumaini, kutia nguvu, kila mtu duniani anahitaji kutiwa moyo, kuishi kwa matumaini, na kutokukata tamaa katika maisha yetu ya kila siku, Tunaishi katika ulimwengu wenye changamoto nyingi sana na bila huduma ya kutiana moyo ulimwengu hauwezi kuwa mahali pa kupendeza sana kuishi, Tunahitaji watu wenye huduma ya kutia moyo wawepo kila mahali, Nyakati za Kanisa la Kwanza Mungu alilipa Kanisa zawadi ya mtu mwenye karama ya kutia moyo wengine, Mtu huyu alijulikana kama Yusuphu Mlawi mzaliwa wa Cyprus.

·         Mitume walimuita mtu huyu “Barnabas” kuonyesha umuhimu wa huduma hii ya faraja
·         Tunawezaje kutiana moyo kila mmoja na mwingine? Ni kwa kujifunza kutoka kwa “Barnaba” na kuangalia kila alichokifanya:-

Huduma ya Barnaba.
I.       Alitia moyo kanisa kwa kuonyesha mfano wa matendo yake.
·         Aliuza shamba lake  na kutoa fedha Matendo 4:37 alionyesha mfano katika kanisa, Kutoa kwake ulikuwa ni moyo wenye kuonyesha kuwa anawajali wengine, lilikuwa ni jambo gumu sana kuuza shamba Yerusalem kwa ajili ya umuhimu wa kumiliki ardhi katika jiji hilo lakini Barnaba alifanya akionyesha kujali wengine.
·         Aliwatia moyo waliokataliwa katika jamii na kanisa Matendo 9:26-30, Paulo mtume ambaye ndiye Sauli alipookoka na kujiunga na wanafunzi pale Yerusalem watu walikuwa na mashaka naye Lakini Barnaba alikuwa na ujasiri wa ajabu alimchukua Sauli na kumtambulisha kwa mitume, Je tufanyeje kwaajili ya watu wanaokataliwa katika jamii au kanisani lazima wawepo wenye huduma ya kufariji na kutia moyo kama Barnaba.
·         Aliwatia moyo washirika kukaa katika kweli kwa Bwana Matendo 11:22-24, kudumu kwetu katika wokovu pia kunahitaji watu wa kukujenga na kukutia Moyo Barnaba alikuwa mtu wa namna hiyo alilitoia moyo kanisa la Antiokia kudumu katika imani
·         Alimtia moyo Muhubiri mwenye kipawa na kuhudumu naye Matendo 11:25-26, wakati jamii inawapiga vita watu wenye vipawa the talented people na wakati mwingine kuwachukia ni rahisi kuwapoteza watu wa aina hii kama hakuna huduma ya kutia moyo Paulo mtume alikuja kuwa muhubiri mkubwa sana na mwenye huduma kubwa sana lakini ilifanyiwa malezi na kutiwa moyo na Mchungaji Barnaba, watumishi wengi wa Mungu wameshindwa kulea watu wenye vipawa kwa kuhofia kuwa watameza huduma zao, au wameshindwa kuwasaidia waimbaji kwa kufikiri kuwa ni watu wasiochungika, kama tukiwaelewa na kuwatia moyo na kuwajenga watakuwa wenye kufaa sana katika kazi na ujenzi wa ufalme wa Mungu
·         Alitumika kuyatia moyo makanisa yaliyopata shida kwa kupeleka zawadi Matendo 11;27-30, Wakati kanisa la Uyahudi linapitia shida Kanisa la Antiokia lilimtuma Barnaba kupeleka msaada na kanisa likafarijiwa kwa nini Barnaba kwa sababu alikuwa na moyo wa kweli wa kujali na kuwajenga wengine.
·         Alilitia moyo Kanisa kwa ibada za kufunga na kuomba pamoja na mafundisho Matendo 13:1-3,  Namna nyingine ya kulitia moyo kanisa ni kukaa katika maombi, kufunga na kuabudu na kufundisha Barnaba alikuwa mstari wa mbele kufanya hayo mimi naamimi kwa vyovyote vile aliutafuta uso wa Bwana na kuwaombea wengine, alitumiwa na Mungu pia kwa ishara na miujiza maana yake aliwaponya watu wengine na pia kujitoa katika kazi ngumu sana ya umisheni.
II.       Alilitia moyo kanisa kwa kutumia neno la Mungu
·         Alilitia moyo waamini kukaa katika imani bila kujali dhiki Matendo 14:21-22 Barnaba na Paulo walilikumbusha kanisa kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi, waliwakumbusha kuvumilia na kuwatia moyo, fikiria kama unapitia majaribu ya aina mbalimbali na hakuna wa kukutia moyo, je ungedumu katika imani?
·         Alilitia moyo kanisa kwa kutafuta suluhu ya kanisa la mataifa kuhusu tohara Matendo 15:1-2 Injili mbaya ya kutahiriwa kwanza ndipo uokoke ilipolivamia kanisa Barnaba akiwa na Paulo walibishana na waalimu hao wa uongo, lakini pia walikwenda Yerusalem kwaajili ya kutafuta suluhu ili kanisa liweze kufarijika
·         Alilitia moyo kanisa kupitia shuhuda za matendo makuu ya Mungu Matendo 15:12
·         Alilitia moyo kanisa kupitia waraka na maneno Matendo 15:31-32 baada ya maamuzi ya mitume waliyarudia makanisa yaliyosumbuliwa na fundisho baya na kuyaimarisha kwa misimamo ya mafundisho sahii na maamuzi ya kanisa kutoka mkutano wa Yerusalem
III. Alilitia moyo kanisa kupitia kuwepo kwake
·         Ulimwengu huu ni ulimwengu wa changamoto mbalimbali una dhiki nyingi Yohana 16:33
·         Ayubu ni moja ya mfano wa watu waliokutana na mambo magumu sana kiasi ambacho hata waliokuja kumfariji walikaa kimya kwa siku saba Ayubu 1;13-19,2;7-11-13
·         Kuwa na watu kama kina Barnabas ni kwa muhimu sana kwa sababu ziko nyakati ambazo kama wanadamu tunahitaji faraja kwani yako mambo yanatuelemea Majukumu ya kifamilia, watoto wasiosikia na kutii, mikwaruzo katika ndoa, Hofu za kupoteza ajira, mishahara isiyotosheleza mahitaji yetu, hasara za kibiashara, kazi nyingi nyumbani, upweke, kuvunjika kwa uchumba, lawama kutoka kwa ndugu, lawama kazini, lawama kwa bosi, mahitaji ya ada za wanafunzi, Bili za umeme, bili za maji, kodi ya mwenye nyumba mahitaji ya wazee kijijini, mahitaji ya palizi au maandalizi ya mashamba kupanda kwa bei ya vyakula, nguo za watoto, kusengenywa, mafarakano, visa vya majirani, mashambulizi ya wachawi, kuuguliwa, madeni ya vikundi vya mikopo saccos, kupigwa nyundo Kanisani, shida za washirika na wachungaji hali kama hizi na nyinginezo nyingi ndizo zinazopelekea Kuweko na hitaji la kufarijiwa au kutiwa moyo hili ni jambo muhimu sana na linahitajika sana katika wakati huu tulionao kuliko nyakati nyingine zozote, Huduma za watumishi kama Barnaba zinahitajika sana wakati wa maswala mzito kama hayo.

Hitimisho:                
Tafadhali kuwa mtu mwenye kutia moyo wengine na kuwafariji, usiwe mtu wa kuwaponda tu na kuwasema wengine vibaya utakuwa mwana wa uharibifu, Mungu anataka kina barnaba wawepo kila mahali , katika taifa, familia, mashuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali
Jihadhari kuwa mkosoaji na mvunjaji moyo watu yako maswala mazuri ambayo wanadamu wanayo hayo ndio vema yakajadiliwa kwa mujibu wa fundisho la kibiblia “Wafilipi 4:8
Uwepo wetu uwe na thamani kwa sababu kupitia kuwatia moyo wengine na kuwafariji dunia itakua mahali pazuri pa kukaa salama, utakumbukwa duniani kutokana na mchango wako mkubwa kwa jamii na dunia itaona ni afadhali umeondoka endapo utakuwa mtu mwenye kuharibu wengine

·         Barnaba alikuwa mwenye kujali wengine Caring
·         Barnaba alikuwa mwenye kutia matumaini wengine wasikate tamaa Consoler
·         Barnaba alikuwa ni mwenye kuwahurumia wengine Compassionate
·         Barnaba hakuwa mtu wa kubadilika badilika katika huduma aliyokuwa nayo Consistent
·      Alikuwa jasiri katika kile alichokiamini kuwajenga wengine na kuwatetea kwa gharama yoyote ile Convictions

Katika kuhudumia kwangu kanisa la Mungu mtu anayefanana na Barnaba ambaye mimi nimewahi kumuona ni rafiki yangu mmoja anaitwa Raphael Sallu Yeye ni Mchungaji wa TAG Mkanyageni huko Muheza huyu jamaa ni kama Barnaba siongei kumtetea kwa sababu ni rafiki yangu hapana lakini ndivyo alivyo.

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: