Mwanzo 44:1-5 Biblia inasema Hivi “1. Akamwamuru yule
msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri
wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. 2. Na
kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo
pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. 3.
Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao. 4. Na
walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa
nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini
mmelipa mabaya kwa mema? 5. Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye
hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi.”
kikombe cha uaguzi hakikuhusu maswala ya uchawi bali kilihusu upambanuzi wa Kimungu kuhusu badiliko la Ndugu zake yaani wana wa Israel
Leo
tunataka kuchukua Muda kujifunza kwa undani kutoka katika kifungu hicho hapo
juu cha maandiko, Ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi sana wanapenda sana Mungu
awabariki na kuwafanyia mambo mazuri, huku wanasahau kuwa Mungu naye anahitaji
mambo Fulani ya muhimu kutoka kwetu ili atubariki na kutimiza ahadi zake na
makusudi yake kwetu. “Kama tukimpa Mungu yale anayoyahitaji kwetu, Mungu atatupa
lolote tulitakalo kwake” alisema Muhubiri Mkubwa mwenye asili ya
Afrika TD Jakes.
Katika
kifungu hiki cha maandiko wote tunakumbuka Vizuri Habari ya Yusufu, tunakumbuka
wazi jinsi Yakobo alivyompenda sana Yusufu, tunakumbuka jinsi ndugu zake
walivyomchukia na kumtendea mabaya, tunakumbuka uchungu aliokuwa nao Yakobo kwa
kumpoteza Yusufu, aliomboleza maombolezo makubwa sana kumpoteza Yusufu, na sasa
upendo wake mkubwa umeelekezwa kwa Benjamin, ambaye Yakobo alimtoa kwa shida
sana akihofia kuumia moyo kama alivyompoteza Yusufu aliogopa sasa asimpoteze
Benjamin.Wakati umefika sasa Yusufu aliyetunzwa na Mungu huko Misri kwa muujiza
mkubwa sasa anataka kujifunua kwa ndugu zake amekwisha kuwahoji mengi na
kuwajaribu kwa namna nyingi sasa anataka kujifunua kwao, lakini anataka kujua
Je Ndugu zake wamebadilika? Atajuaje sasa anatumia Kikombe cha Fedha kupambanua
mabadiliko yao huu ndio mpango wake kupitia kikombe hiki je kikombe hiki
kilihusu nini?
1. Mpango wa siri wa kutafuta uhakika
·
Yusufu na Ndugu zake walikuwa na wakati mzuri wa
kufurahi pamoja Mwanzo 43:31-34 Ndugu zake bado hawajamfahamu
kuwa ni Yusufu, lakini yeye amekwisha kuwajua na kupata uhakika, anawajua vilivyo
kuliko wao wanavyo mjua, Mfano walipokuwa wakila aliwapanga kwa kufuata umri
wao kuanzia mkubwa hata mdogo, Mwanzo
43:33, Benjamini alikuwa amependelewa kwa chakula kingi mara tano zaidi ya
nduguze Mwanzo 43:34.
·
Siku ya pili baada ya karamu kila mmoja akiwa na
furaha na uhakika kuwa wamemthibitishia waziri mkuu wa Misri kuwa wao sio
wapelelezi, na kuwa wamefanikiwa kumuokoa Ndugu yao Simeon ambaye alikuwa
amefungwa kwa muda na kuwa wanarudi nyumbani wakiwa na Benjamin ambaye Yuda
alimuapia baba yake kuwa atahakikisha anamrudisha mtoto Mwanzo 43:3-10.
·
Sasa wanarejea nyumbani asubuhi mizigo ikiwa juu
ya punda zao na mbegu na chakula, hawana mashaka wamejawa na furaha wanafikiri kufika nyumbani na kuungana na
familia zao na watoto wao, wanafurahia mafanikio yao nay a safari yao, Lakini
hawakuwa wanajua kuwa Mungu yuko nyumba ya mambo anataka kuwakutanisha na
dhambi yao waliyoifanya miaka 22 takribani iliyopita
·
Wakati wanajiandaa kuondoka Yusufu anamtuma
mtumishi wake kuwaandalia nafaka na kuwapatia kadiri wawezavyo kubeba,
alimwambia pia awarudishie na fedha zao walizolipa kwa nafaka, lakini Yusufu
alimwambia Mtumishi wake afanye jambo geni zaidi, kuweka kikombe chake cha
fedha katika mzigo wa Benjamin mdogo wake wa kunyonya hayo yalifanyika wakiwa
bado hawajaondoka
·
Baada ya kuwa wamefika mbali Yusufu anamtuma
mtumishi wake kuwakabili na kuwahoji kwa nini wamelipa Mabaya kwa mema? Wao walikuwa
na uhakika kuhusu haki yao, walikuwa na uhakika kuwa hawakuwa wezi kwa vile
walirejesha fedha zote ambazo waliwekewa mwanzoni na hivyo hawakuwa na sababu
ya kuiba kikombe cha Yusufu cha fedha na hatimaye kwa kujiamini waliapa kuwa swa atakayekutwa na kikombe chako cha fedha
na afe! Na sisi tutakuwa watumwa wa wamisiri
·
Hili lilikuwa jambo geni sana kufanywa na Yusufu
Mungu alikuwa anamtumia Yusufu kuwarejesha ndugu zake katika toba ya kweli, wao
walikuwa wamemtenda mabaya Yusufu lakini Yusufu alikuwa anawalipa Mema, Ni
lazima tukumbuke kuwa katika maisha haya hakuna jambo linalotokea kwa bahati
mbaya kila jambo linalotokea katika maisha yetu ni mpango kamili wa Mungu nyuma
yake Warumi 8:28 “ Nasi twajua yakuwa
katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia
mema wale walioitwa kwa kusudi lake” Mungu hufanya kazi kwa kusudi
la kutuleta katika mapenzi yake njia zake ziko juu sana Isaya 55:8-9 “ Maana mawazo yangu si mawazo yenu wala njia zenu si njia
zangu asema Bwana kwa maana kama vile mbigu zilivyo juu sana kuliko nchi
kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo
yenu” Jambo hili Mungu hulifanya pia anapojihusisha na tabia zetu
mbaya anapotaka kutubadilisha na kutuleta katika toba
·
Uko wakati ambapo tunaweza kujisahau katika
maisha yetu na tukaendelea kuishi maisha ya dhambi na tukaona Mungu yuko kimya
kama hashughuliki namaisha yetu wala hajatughadhabikia wala kutuonya
tukaendeleza tabia Fulani kama kawaida na tukaona Baraka zake huku
akitufanikisha na kukutana na mahitaji yetu, akitutumia na watu wakibarikiwa na
kila huduma tuifanyayo, Ukweli unabaki kuwa Mungu anajua ni namna gani
atatuagua atatutibu tatizo letu anajua namna anavyoweza kukutana na kuzungumza
na mioyo yetu, na hapo ndipo hufikia wakati nanabana kifungi Fulani maalumu
kutunyenyekesha na kutuleta katika toba
·
Kikombe cha uaguzi cha Yusufu kilikuwa ni kibano
cha dakika za mwisho cha kuwapima wana wa Israel kama wametubu, wamebadilika,
wanampenda baba yao ambaye walikuwa wamemdanganya kuhusu Yusufu, walikuwa
wanampenda Benjamin ambaye sasa anapendwa na baba yao zaidi baada ya Yusufu,
wanampenda Benjamini ambaye ni mtoto wa raheli kama Yusufu, wanawajibika kiasi
gani kwa familia zao, ndugu na baba yao.
·
Mungu anajua namna ya kutuleta katika ukamilifu,
anajua namna ya kupima mioyo yetu kujua tumekuwa kiasi gani na kubadilika kiasi
gani, na ili atupate anajua ni wapi akuweke katika kibano ambacho kitakuleta
katika toba na badiliko la kweli, ni Mungu anayejua namna ya kuweka kikombe
chake cha uaguzi katika gunia lako.
·
Hatuwezi kumficha Mungu maisha yetu kwa muamini
au mkristo anayejua wajibu wake na mwenye kufikiri sawa sawa ni lazima akubali
kutubu haraka Mithali 28:13 afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali
aziungamayena kuziacha atapata rehema, Tukiziungama dhambi zetu yeye ni
mwaminifu na wa haki anatusamehe 1Yohana 1:9, tukikataa toba na kubadilika
gharama itakuwa kubwa kuliko tunavyoweza kufikiri, Waebrania 12:6-11 Mithali
13:15
·
Mungu alikuwa anatafuta uhakika wa mabadiliko
katika maisha ya wana wa Israel, alitaka waonyeshe kuwa wamebadilika toba sio
maneno ni vitendo ni mabadiliko makubwa katika maisha yetu, kama hatubadiliki
kila wakati tutajikuta katika marudio ya mitihani ileile katika nmaisha yetu.
2. Mpango
wa Mungu wa kuwakabili
·
Magunia yalifunguliwa wana wa Israel walikuwa na
uhakika hawana hatia wanasimama wakijiamini na wakiwa na nyuso za furaha kila
mmoja anasaidia kufungua gunia lake kwa
ujasiri na sasa wanafika gunia la Benjamin hali inabadilika wanakuta kikombe
cha fedha cha Yusufu katika namna isiyoweza kuaminika walipigwa na Butwaa!!!
·
Huu ni wakati wa majuto na ukweli sasa ni kipimo
cha mwisho cha Yusufu kwa ndugu zake wakati woote Yusufu alikuwa anawajaribu
ili kuona je kuna mabadiliko?
-
Walimleta Benjamin kama alivyowaagiza Mwanzo 43:15-16
-
Walirejea kwaajili ya kaka yao Simeon Mwanzo 43:23
- Walirejesha Fedha yoote waliyokuwa wamezidishiwa na
kurejeshewa katika magunia yao Mwazno
43:20-22
·
Haya yote yalikuwa ni majaribio, ni mkiaka
karibu 22 imepita walimchukia Yusufu sana walimshambulia walimtupa katika
shimo, walimuuza utumwani, walimuhuzunisha baba yao walimvinja moyo, walimuambia
uongo kuhusu kilichomtokea Yusufu, walifanya msiba pamoja naye kama kwamba amekufa
walipatana kwa nia moja kunyamaza kimya siku zote, walikaa na uongo huo kwa
muda wote huo, sasa wangekuwa na nafasi nyingine ya kufurahia kifo cha mwana
mwingine wa Raheli, Kwa vile sasa ni wazi kuwa Benjamin anapendwa sana na baba
yao kama alivyopendwa Yusufu Mwanzo
42:36, 43:13-14, labda wakati huu wangeruhusu Benjamin kupatwa na mabaya
kama ilivyokuwa kwa Yusufu, wangejirudia tu nyumbani, wangeuumiza tena moyo wa
baba yao ambaye amevumilia maumivu ya kupotelewa na mwanae kwa miaka yote hiyo
bila kujielewa Yusufu alikuwa anapata picha kuwa Ndugu zake wamebadilika sana
wamekuwa watu wengine sasa wako tayari hata kufa hata kuwa watumwa ndugu zao na
baba yao awe na furaha
·
Hawakutaka hata kumuuliza Benjamin kikombe
kimefikaje kwako, hawakutaka hayt kumkemea kwanini umechukua kikombe cha watu,
walikuwa tayari kubeba mzigo wa Benjamin hata ikiwezekana kufa ili kuokoa
maisha yake na baba yao, wako tayari kubeba hukumu bila kujali Benjamin
alifanya nini, wameacha ubinafsi, wameacha uongo, wameacha kupenda fedha,
wanalia kwa huzuni, hawamlaumu yoyote wakati huu
·
Huu ndio wakati ambao Mungu anausubiri kwa kila
mmoja wetu, kuwa tayari kufanya mambo sahihi na kwa njia sahii, wana wa Israel wamekomaa
sasa hawahukumu wengine, hawahukumiani tena, hawachekani, wako tayari kubeba
tatizo lao kama la mtu mmoja, wako tayari kuwa wakeli hata kama ukweli
utawagharimu
·
Ndugu yangu mpendwa Mungu anakusubiri ufikie
wakati ambapo huwezi kumtupia mwingine lawama, wala kumsingizia mwingine tatizo
kwa kushindwa kwetu kuwajibika, anataka tufikie wakati ambapo tutakuwa tayari
kukabiliana na dhambi zetu wenyewe na kuzikiri na kuzitubu na kuziacha na
kubadilika.
·
Mungu anatutaka tufikie wakati ambapo hatutanyoosha
vidole kwa wengine, dhambi zetu sio za wazazi wetu, wala wake zetu, wala waume
zetu, hakuna wa kulaumiwa Mungu anatusubiri tufikie ngazi hii ya kujitambua
ndipo anapoweza kujifunua kwetu, Mungu anataka tufikie ngazi ya kuweza kuwa
wakweli hata kama kweli hiyo itatugharimu
·
Mungu haogopi kuifunua dhambi yetu wazi kwetu
ili kwamba tuweze kufikia toba, Mungu anapotutaka tumgeukie atatumia kila
analoliweza kuhakikisha kuwa anarudisha uhusiano wetu nayeye, Ndugu zanhgu
Dhambi si ya kucheza nayo, sio ya kuirudiarudia ni lazima itubiwe mara moja,
kwa ukamilifu na uaminifu, hapo ndipo Mungu anapoweza kutusamehe, kutubariki,
kujifunua kwetu na kuonyesha nguvu zake
3. Mpango wa Mungu kuwarejesha katika toba
·
Sasa wana wa Israel wanarejea ikulu kwa Yusufu
hapo hajajifunua kwao bado, Yusufu alikuwa anasubiri sasa kujifunua kwao,
anataka kuona mabadiliko, je atamuona Benjamin peke yake? Maana ndiye
aliyewekewa kikombe cha uaguzi, njia hii ilikuwa ni ya kumlinda Benjamin kutoka
kwa ndugu zake kama wanekuwa hawana mabadiliko.
·
Walipotokea wote walimsujudia hata chini
wakiitimiza ile ndoto ya Yusufu alipokuwa kijana Mwanzo 37:5-11, Yusufu anawauliza
kuhusu kikombe chake cha fedha, na anawaambie hamkujua ya kuwa naweza kufanya
Uaguzi?
·
Ni muhimu kufahamu kuwa Yusufu hakuwa muaguzi
wala hakufanya uaguzi kabisa, lakini uaguzi na ramli lilikuwa ni jambo la
kawaida la wamisri na waaguzi walitumia kikombe cha Fedha na kukiweka divai na
shanga za thamani na walitumia kusoma maisha ya watu, Yusufu hakufanya uaguzi
huo lakini hapa alikuwa anawajua ndugu zake vilivyo, alifahamu sana matendo yao
mabaya na tabia zao zilizokuwa za kutomkumjali Mungu, alitaka kujua kuwa Baba
yake sasa amewafunza neno la Mungu na kuwa huenda je sasa wamebadilika au bado
baba hana watu hapo ? Kitendo cha Yusufu kutambua kila kilichokuwa kinaendelea
na wao kutokutambua, kitendo cha wao kuonyesha badiliko kubwa hata wakiwa mbali
ambako watu hawawaoni kilionyesha uaminifu ulio wazi kuwa ni kweli wamebadilika
je ni wangapi wanaweza kufanya uovu hata wakiwa katika miji au nchi ngeni
ambako huko hakuna anayewajua? Yusufu alikuwa akifanya kile ambacho Mungu
alikuwa anamuongoza kuwaleta nduguze katika ukamilifu wake
·
Yuda alikuwa wakwanza kujitokeza mbele na
kuzungumza maneno ya muhimu sana katika neno la Mungu ni maneno yanayoonyesha
kuwa ni moja ya watu waliobadilika sana
·
Alikiri wazi kuwa wamefanya dhambi alisema Mungu
ameona uovu wao, alisema sisi sote nay eye aliyekutwa na kikombe chako ni
watumwa wako, alitambua kuwa Mungu alikuwa akiwahukumu kwaajili ya dhambi,
kitendo cha kuwa Mwenye kikombe anataka aliyekutwa na kikombe awe mtumwa wake,
kilimkumbusha wazi kuwa ni ile dhambi ya kumuuza ndugu yao utumwani Misri sasa
kimewageukia, alikubali kuwa yeye na ndugu zake wote ni watumwa tu Mwanzo 45:16
·
Yusufu alikataa wao kuwa watumwa wake aliwataka
wote kuendelea na safari isipokuwa yeye aliyekutwa na kikombe chake cha uaguzi
tu Mwanzo 45:17
·
Mwanzo 45”18-34 Ni maandiko yenye maneno mazito
ya Yuda, alimkubusha Yusufu kuwa sababu ya kuja na Benjamin ilikuwa ni kwa vile
yeye alikuwa amewaagiza 19-23 Yuda alimueleza Yusufu kuwa Baba yao Yakobo angekufa
tu kama Benjamin atapatwa na mabaya ndiye mwanaye mdogo naye anampenda 24-31,
kisha Yuda alisema yeye yuko tayari kuchukua nafasi ya Benjamin, alikuwa tayari
kubaki Misri kama Mtumwa ili kwamba Benjamin aweze kurudi kanaani na ndugu zake
32-34, Moyo wa Yuda unakuwa kama wa yesu Kristo yuko tayari sasa kubeba adhabu
ili ndugu zake na baba yake wawe na amani na furaha
·
Huu ulikuwa ni kama wakati muafaka ambao Yusufu
alikuwa akiutazamia alithibitisha wazi kuwa wamebadilika sana
·
Wako na umoja kama mtu mmoja, wako tayari
wameiva Yuda yuko tayari kuchukua nafasi ya Benjamin na kumpendezesha baba yake,
hapa ndipo mambo yalipobadilika Ukiri wa Yuda ulionyesha wazi kuwa amebeba
majukumu makubwa ya kuwajibika kwaajili ya familia yake hakuna ubinafsi ndani
yake yuko tayari kupoteza kila kitu, kumbuka alikuwa na watoto na mke na mali
zake lakini alikubali kubaki Misri kama mtumwa ndugu yake awe huru, aidha
amefanya dhambi au hakufanya, na aliweza kuwaza moyo wa baba yake, kutokana na
hali hii Yusufu alishindwa kujizuia na alijifunua kwa Ndugu zake Mwanzo 45:1-4
·
Kwa ujumla kuna jambo la kujifunza kutoka kwa
Yuda ni wazi kuwa dhambi yoyote ile ni matokeo ya ubinafsi na choyo na umimi,
kadiri mtu anavyokuwa mbinafsi ndivyo na dhambi yake ilivyo, dhambi yoyote
inayotendwa na wanadamu ni matokeo ya ubinafsi na kujihurumia, toba halisi
inaonekana pale tunapoanza kujali wengine na kuweza kukubali kuwa tayari hata
kujidhabihu kwaajili yaw engine kumbuka siku zote asili ya dhambi zote ni
ubinafsi Isaya 14:12-15, 1Yohana 2:16
·
Tunapofanya dhambi huwa hatuko tayari kujali
madhara yake tunajitoa kikamilifu kuasi kwa sababu ya ubinafsi, tunaweza wakati
mwingine kutubu au kuogopa dhambi au kunyenyekea kwa sababu ya kuogopa aibu au
kushikwa tu, Mkristo aliyekomaa anaiangalia dhambi kwa mtazamo zaidi ya huo,
kuwa ina madhara kwa jamii, kanisa na familia nay eye mwenyewe na kazi ya mungu
pia njia pekee ya kuikabili dhambi na kukubali kulipa gharama na kuwa wakweli
kwa Mungu na nafsi zetu hata kama itatugharimu hivi ndivyo Yuda alivyofanya
·
Watu wengi wanataka Baraka za Mungu na Mungu
amekuwa mvumilivu kwetu kwa miaka mingi, inawezekana unawacheka hata wale
waliotengwa makanisani kwa kubainika kuwa ni wenye dhambi lakini wewe una za
kwako haijawahi kuonekana lakini kiko kikombe cha uuguzi cha bwana kiko katika
gunia lako atakubana tu ni vema sasa ukabadilika na kuacha dhambi na kuwa
tayari kwa gharama yoyoye kuwa mbali na Ubinafsi na Yesu atajifunua kwako na
kukupa memma ya nchi na kukuhifahdi na kukualika katika furaha yake, Yuda
alitambua kuwa hawakuwa wamemfanyi Yusufu mabaya walijua kuwa wamemkosea Mungu,
ni muhimu kwako kujitathimini yale unayowafanyia wengine kuwa unamkosea Mungu.
·
Je unakua kiriho?
·
Je una dhambi unapaswa kuitubu?
· Je unaogopa hukumu ya Mungu (kikombe cha Fedha cha
uaguzi) Badilika leo na Bwana takaubariki sana na kukustawisha sana.
Na
mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev
Innocent Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni