Luka 13:1-5 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya
Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba
Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na
mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo
hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua,
mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?
Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa taarifa
(Habari) ni moja ya nyenzo yenye kubwa sana yenye kubeba maana zinazoweza
kujenga au kubomoa jamii, taarifa zina nguvu, zina nguvu zote mbili za kujenga
au kubomoa, Mungu ndiye mwanzilishi wa taarifa, Alipomuumba mwanadamu alimpa
taarifa ya namna na jinsi ya kuutawala ulimwengu alimweleza kama mtu huru namna
anavyoweza kuutumia ulimwengu na alimuelekeza namna nzuri ya kuutumia ulimwengu
lakini pia alimuonya kuwa kama atautumia ulimwengu vibaya angeweza kuleta
madhara makubwa kwa maisha yake na jamii yake yaani kifo. Taarifa inaweza kuwa
ndogo lakini kama ikitumika vibaya inaweza kuleta madhara makubwa sana kwa
jamii kama njiti ya kiberiti inavyoweza kuchoma msitu mzima!
Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati
za Biblia pia kulikuwa na namna ambavyo watu waliweza kupokea na kutoa taarifa
kama unavyoweza kuona katika kifungu hiki Luka
13:1-5 “Na
wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao
Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.
Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa
wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia,
Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na
wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao
walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo;
lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”
Yesu alikuwa
amepokea taarifa au habari kuhusu Wagalilaya waliouawa vibaya na Pilato, na
baada ya kupokea taarifa hizi tunaona namna Yesu alivyozitumia taarifa hizo
sasa kuwafundisha watu wake somo kuhusu toba na pia akiunganisha na taarifa
nyingine ya watu kumi walioangukiwa na mnara huko siloamu, Kutoa na kupokea
taarifa ni haki ya kila jamii, Yesu aliitumia taarifa hii kwa sababu huenda
aliamini au kulikuwa na namna ya uthibitisho kuwa chanzo cha taarifa
alichokipokea kilikuwa ni chanzo cha kuaminika na kwa sababu hiyo taarifa
alizozipokea zilikuwa na ukweli, na hivyo alizitumia kufundisha kama mfano kwa
jamii iliyomzunguka, Unapochunguza kwa kina mafundisho ya Yesu Kristo utaweza
kuona alikuwa na mifano mingi sana na alikuwa na stori nyingi sana na khadithi
nyingi sana na nyingi alizitumia katika kuielimisha jamii na kuijenga kama
jinsi Mungu anavyotaka.
Kutokana na kupanuka kwa
technolojia leo hii kumekuweko na vyanzo vingi sana vya kupokea na kutoa
habari, lakini ni jambo la kusikitisha sana kuwa jamii ya leo haizingatii
uadilifu katika swala zima la kupokea na kutoa habari, Mfano mzuri ni tukio la
hivi karibuni ambapo watangazaji/ waandishi wa habari wa TBC walifariki, lakini
wakati huo huo kulikuwa na taarifa za kufariki kwa Mtangazaji wa shirika hilo
wa habari za biashatra aliyeitwa “Gloria Maiko” aidha kabla ya kuenea kwa
taarifa hii kuhusu kufa kwake iliebnea taarifa kuwa Gloria anaumwa sana tena
ana ugonjwa wa Corona, Mimi napenda habari, mimi ni mwana habari, mimi nimesoma
Introduction to jounalism, napenda kupata taarifa kwa sababu huwa pia natoa
taarifa yaani nazitumia kuijenga jamii, sio hivyo tu unaposoma chuo cha Biblia
kwaajili ya kazi ya uchungaji hausomei Biblia pekee unaandaliwa pia kuwa mwana
habari kwa sababu kanisa linaweza kuwa na gazeti, Kanisa linaweza kuandika
vitabu, kanisa linaweza kuwa na televisheni, kanisa linaweza kuwa na radio,
kanisa linaweza kuwa na ukurasa wa faceboo, instagram, blog na nyenzo nyingine
za utoaji wa taarifa kwa hiyo lazima watu wa Mungu wawe na angalau ufahamu
mdogo tu kuhusu upokeaji na utoaji wa habari, wakati huu nilisoma chanzo
kingine kuhusu Gloria kinasema hivi ngoja nikinukuu
“TBC1 tuliwaonya kukusanyika siku ya msiba wa
Marini Hassan hamkusikia! Haya leo Joseph Kambangwa mfanyakazi wenu kafa kwa
corona na maziko ni kesho saa 4 huko huko Mloganzila! **Gloria Maiko
(anatangazaga habari za biashara) yuko hoi ana dalili zote za corona! RIP
Kambangwa”
mwisho wa
kunukuu, angalia huyu ni mtu mwenye akili timamu, ni mtu ambaye jamii
inamtegemea, jamii inaamini labda katika hiki alichokisema lakini je habari hii
ilikuwa na malengo gani kwa jamii, ilikusudia nini kwa Gloria? Na kwa familia
yake, je ilikuwa inajenga au inabomoa? Kwa sababu baada ya kuenea kwa Taarifa
hii Gloria Maiko alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kuwa yeye
yuko hai na wala haumwi! Lakini mwandishi anajisikiaje? Baada ya Gloria
mwenyewe kutokea je wale walioeneza katika mitandao ya kijamii na kutoa salamu
za astarehe kwa amani wanajisikiaje katika mioyo yao baada ya mtu mliyemzushia
kifo kujitokeza na kuonyesha yuko hai, nimetoa tu mfano huu lakini Jambo hili
limewahi kuwatokea wengi, hapa nchini hata Mheshimiwa Augustin Lyatonga Mrema
alizushiwa mara kadhaa mpaka alipojitokeza na kuionya jamii kuwa yeye ni mzima
na kuwa kuanzia sasa atawafungulia mashtaka watu wanaoanzisha uzushi huu, Huko
ulaya mambo ya aina hii yako sana lakini kwa mujibu wa tamaduni zao, Lakini
sisi ni Watanzania na wana Afrika Mashariki je mambo haya ni sawasawa? Je wale
waliosomea uandishi wa habari jambo hili ni sawa katika utoaji wa taarifa na
upokeaji, Je wale wanaozushia wenzao hujitokeza kuomba radhi? Je wanachukuliwa
hatua gani je ni aina gani ya jamii tunaijenga ya watu wanaosema ukweli au
jamii ya waongo? Mungu ametupa hekima na akili na maendeleo makubwa ya nyenzo
za utoaji wa taarifa lakini ni muhimu zikatumika kwaajili ya utukufu wa Mungu,
kwa wakristo tunaambiwa katika maandiko kwamba lolote tulifanyalo kwa neno au
kwa tendo tulifanye kwa utukufu wa Mungu ona
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika
jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
Swali kubwa
ambalo kila mwana jamii anapaswa kujiuliza na kuhoji ni kuwa kama Yesu
angekuwepo Duniani leo ni habari gani angeikubali na habari gani angeikataa na
je angetumiaje mitandai ya kijamii, na sisi vilevile tujiulize je tunapopata
habari ambazo hazina uhakika haziko sahihi, hazina utu, zina mitazamo hasi,
zinaupendeleo, na kama ni za uongo wanaozitoa hawawajibishwi, habari hazina
kiasi, na ziko kinyume na uadilifu je tungejisikiaje? Nafikiri wote tuna namna
ambavyo tunatarajia jinsi habari au taarifa inavyopaswa kuwa! Mkurugenzi wa
Maadili ya uandishi wa habari aitwaye Aidan White anasema ziko kanuni 400
ambazo wanahabari wanapaswa kuzizingatia lakini ziko kanuni 5 Muhimu zaidi
ambazo kila mwandishi na mtoa habari anapaswa kuzifuata bila kushindwa.
1. Ukweli na Uhakika (Accuracy)
– “the quality or state of being correct or precise” Maana yake kila mtoa
habari na mpokea habari na mtawanya habari au taarifa anapaswa kuhakikisha kuwa
taarifa anayoitoa ina UKWELI na pia IMEHAKIKISHWA. Lakini pia kuzinagatia kuwa habari inaweza
kuwa ya ukweli na imehakikishwa lakini swali je ni wakati muafaka kuitoa? Kwa
sababu inaweza kuwa kweli na ya uhakika lakini wakati ukawa hauruhusu kuisema
au mazingira yakawa hayaruhusu kusema !, tunapohubiri injili watu wa Mungu huwa
hatuleti maneno ya kushawishi, wale yenye ufundi wa kibinadamu tunapopeleka
habari njema tunapeleka habari ambazo ni za kweli na zinathibitishwa na Roho
Mtakatifu, ile Nguvu ya ukweli pekee inauwezo wa kuwaweka watu huru na kuiponya
jamii. Waandishi wa habari ni kama manabii wanapaswa kutia habari za ukweli na
uhakika ona Kumbukumbu
la Torati 18:22 “Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile
wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo
nabii, usimwogope” Biblia liagiza
kuwa kama nabii atatia taarifa na akadai taarifa hiyo imetoka kwa Mungu na
kumbe sivyo yaani haikutimia yaani haina ukweli asiogopwe maana yake achukuliwe
hatua, kwa hiyo kama watu wanaotoa habari na habari zao zikawa sio za uhakika
torati inashauri wachukuliwe hatua katika agano la kale waliuawa, katika agano
jipya wanapaswa kuchukuliwa hatua, Yesu
angelikuwepo leo hangeweza kukubalia habari ambayo haijathibitishwa haina
ukweli na haijahakikishwa!
2. Huru – Independence – yaani taarifa inapaswa kuwa ya haki
isiyopendelea upande wowote, Kila mtoa habari na mpokea habari anapaswa kuwa na
mtizamo wa haki, hapaswi kuwa mwenye kupendelea upande fulani, mfano kama ni
kwa habari ya vyama vya siasa ni vema mtoa habari na mpokea habari wakawa
hawana mtazamo wa kisiasa au mtazamo wa siasa zinazofungamana na upande fulani,
taarifa itolewe kwa uwazi na kwa haki na ihaririwe kwa uwazi na kwa haki,
Maandiko yanatufundisha wale wanaomuamini Yesu kuwa imani yetu katika Kristo
isiwe kwaajili ya kupendelea watu Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu” unaona Yesu angelikuwepo leo hangeweza kupokea au
kutoa habari inayomkandamiza mtu fulani haki ingesimama
3. Usiyo na Masalahi nayo – Impartiality kwa kiingereza neno hili
maana yake “Impartiality is a principle
of justice holding that decisions should be based on objective criteria, rather
than on the basis of bias, prejudice, or preferring the benefit to one person
over another for improper reasons“ yaani kanuni ya haki inayotaka maamuzi yafanyike kwa
mujibu wa vigezo na sio kwa sababu mtu una masalahi fulani, au ukungu fulani
unaotaka mtu mmoja anufaike dhidi ya mwingine kwa sababu zisizo sahihi,
unapopokea au kutoa habari kwa makusudi maovu au kwa uependeleo kwa Mungu hufai
kuwa mtu wa haki, Yesu angekuwepo leo kwa habari ya kupokea na kutoa habari
angehukumu kwa haki Isaya 11:1-5 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi
litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu
yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya
kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa
kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa
masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa
dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya
midomo yake atawaua wabaya.Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu
mshipi wa kujifungia” Mtoa habari au mpokea habari anapaswa kuwa
mwaminifu na kuwa mtu wa haki, wakati mwingine kwa sababu ya mitazamo fulani na
hata kwaajili ya kupokea rushwa tumepokea au kutoa habari kwa maslahi ya upande
fulani kwa sababu tunaletu jambo, Mungu hapendezwi na utaratibu huo na ndio
maana hatua kali sana zinapaswa kuchukuliwa endapo itabainika mwandishi kuwa
ana dalili za kupokea rushwa.
4. Taarifa yenye kujali utu – Humanity Ni muhimu kufahamu kuwa biblia
inasema usiue kuua kuko kwa namna nyingi sana unaweza kuua kwa kutumia maneno,
unamuua mtu kisiasa, umamuharibia mtu au unamchafua mtu huku ni kuua mpokea
habari au mtoa habari anapaswa kuhakikisha kuwa anajali utu, ni dhambi
kuandika, kupokea au kutoa habari yenye kudhuru, yenye kuharibu ubinadamu wa
mtu, au yenye kumvunjia mtu heshima hatupaswi kutoa habari wala kusambaza
habari au habari picha yenye kuharibu maisha ya wengine au kudhalilisha, watu wasiojua
kutumia mitandao ya kijamii wanapiga picha hata za watu waliopata ajali mbaya
na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii, katika nchi nyingi zilizoendelea
hata mwili wa Marehemu anapoagwa haupigwi picha, Picha ya marehemu
inayoruhusiwa kuonekana ni ile ambayo wanafamilia wataiweka juu ya jeneza
kwaajili ya kumbukumbu yake, nchi nyingi zawatu wasiostaraabika utaona mtu
aliyepasuka kichwa kwa ajali, waliovunjika miguu, mtu mwenye ulemavu wa jabu na
picha za kutisha sana zinarushwa kwenye mitandao ya kijamii, je umewahi
kujiuliza kwanini mtu akipata ajali watu hutoa nguo zao na kuufunika mwili wa
marehemu? Ni kwaajili ya kujali utu,
Mungu hawezi kukubali na kufurahia utu wa mtu udhalilishwe, kwa msingi huo kila
mtoa habari na mpokea habari namsambazaji anapaswa mno sana kuzingatia utu,
Yesu alikubali kifo cha aibu pale msalabani ili kutunza heshima ya mwanadamu,
natarajia kuona jamii iliyostaarabika ambayo haitarusha picha ya marehemu
yoyote akiwa na pamba puani, wala hata jeneza ikiwezekana na kama umefiwa weka
picha ya aliyefariki ikiwa katika hali ya ubora na usiiwekee “X” muonyehse mtu enzi za ubora wake,
sikitika kwa kumpoteza mtu huyo lakini usimdhalilishe nduguyo, aidha usisambaze
wala usizikubali picha za watu walio katika hali mbaya za ajali, mwanadamu
ameumbwa kwa sura na utukufu wa Mungu na lazima utu wa kila mtu uheshimiwe,
hali kadhalika picha za ngono na zenye kuonyesha uchi ni mwiko kwa watu
waadilifu, Mtu wa haki huwa hadhalilishi mtu mwingine. Mathayo 1:18-19 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake
alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa
uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki,
asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.” Mtu wa haki huwa
hafanyi mambo kwa kusudi la kumuaibisha mtu mwingine hata kama mtu huyo ni
kweli amefanya jambo hilo Yesu angekuwepo leo hangekubali kupokea au kutoa
taarifa zinazodhalilisha utu wa mwanadamu ambao ni uumbaji wake.
5. Kuwajibika – accountability - In ethics and governance,
accountability is answerability, Maana yake kila mtoa habari na mpokea habari
na msambaza habari wanapaswa kujua na kukubali kuwa wanawajibika kwa habari
wanazotoa au kusambaza, kwa msingi huo kama utatoa habari na ikasababisha madhara
au hata isiposababisha madhara ufahamu kuwa unatakiwa kuwa na utayari wa
kuijibia kuitolea maelezo na kuwa tayari kuomba radhi ikiwa umekosea, au kukubali kukosoelewa na kupokea maoni ya
jamii kuhusiana na ulichokitoa au kukisema na ikiwezekana kuwa tayari
kushitakiwa mahakamani na hata kufungwa na au hata kuuawa na wale
watakaochukizwa na habari ulizozitoa, kila habari unayoitoa ni muhimu kufahamu
kuwa itakugharimu Yesu alisema kila neno lisilo na maana atakalolinena
mwanadamu atatoa hesabu yake Mathayo 12:36-37“Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena
wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako
utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa” Yesu atakapokuja atawahukumu wazishi wote hapa
aliwaonya watu waliokuwa wakitoa habari zisizo sahihi kuhusu utendaji wa Yesu
Kristo, Yesu anatoa pepo kwa Roho wa Mungu wapotoshaji wakesema anatumia nguvu
za mkuu wa pepo Baalzebub, lazima ieleweke wazi kuwa watioa habari watawajibika
sio mbele za wanadamu tu na mbele za Mungu!
Hitimisho!
Biola shaka kuna kitu umejifunza hapo sisi kama
wakristo ndio chumvi ya ulimwengu napenda kila mmoja wetu aelimike na kukubalia
kujifunza kuwa katika wakati huu wa utandawazi wakati ambapo kila mwanadamu
anauwezo wa kutoa taarifa, kupokea taarifa na kusambaza taarifa ni Muhuhimu
kwetu tukaacha kujisahau na kukumbuka kuwa ziko kanuni za neno la Mungu ambazo
zinatuongoza jinsi na namna ya kuitumia mitandao hii ya kijamii,
ninapohitimisha nataka kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yafuatayo:-
a. Tumia mitandao ya kijamii
kuhudumu kwa neno la Mungu na kusambaza habri njema
b. Kumbuka kujitenga kwa muda
na mitandao ya kijamii na kwenda kuomba
c. Kumbuka kuwakumbusha watu
kutubu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu
d. Kumbuka kutia moyo mambo
yaliyo mema kwa ku like na kuweka maoni yako na kukosoa vikali maovu na
kuonyesha wazi jambo au kitu usichopendezwa nacho tumia neno la Mungu
e. Tumia mitandao ya kijamii
kudumisha uhusiano na kutafuta amani na watu wote na sio kuharibu
f.
Tumia mitandao ya kijamii kuonyesha semina, mikutano ya neno
la Mungu na maswala muhimu ya kijamii onya karipia fundisha na jihadhari na
matapeli
g. Zingatia kanuni husika
tulizojifunza na muombe Mungu ziwe kanuni muhimu katika maisha yako, asomaye na
afahamu, ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda
Na.
Mchungaji Innocent Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye hekima
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni