Luka 23:44-46 “Hapo ilikuwa yapata saa
sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake;
pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee
Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.”
Utangulizi:
Tunaendelea kujifunza kuhusu
maneno ya Yesu aliyoyasema pale msalabani, ambayo yana maana pana sana kama
utapata nafasi ya kujifundisha moja baada ya jingine, Leo nataka kuzungumzia
kuhusu maneno ya mwisho miongoni mwa maneno saba aliyoyazungumza Yesu pale
msalabani ambalo ni BABA MIKONONI MWAKO
NAIWEKA ROHO YANGU!, Maneno haya ni sehemu ya maombi aliyokuwa akiyaomba
Bwana Yesu Pale msalabani kwa kutumia Zaburi, yeye alipaza sauti kubwa sana na
kuyasema maneno haya na kisha akakata roho, watu wengi sana huyaogopa maneno
haya wakidhani ya kuwa ukiyasema basi utakuwa unajitakia kifo, au unaweza
ukayasema inapofika saa yako ya mwisho, lakini maneno haya yana maana tofauti
kabisa na namna ambavyo wengi wetu tumefikiri kwa siku nyingi, hata hivyo kabla
ya kuyafanyia uchambuzi na upembuzi yakinifu ni vema kwanza tukajikumbusha tena
maneno mengine katika maneno yote saba aliyoyasema Bwana Yesu Pale msalabani,
maneno hayo ni pamoja na :-
·
Baba uwasamehe kwa maana
hawajui walitendalo Luka 23:34
·
Amin nakuambia leo hii utakuwa
pamoja nani peponi Luka 23:43
·
Mama tazama mwanao, mwana
tazama mama yako Yohana 19:26-27
·
Mungu wangu Mungu wangu mbona
umeniacha Mathayo 27:46
·
Nina kiu Yohana 19:28
·
Imekwisha Yohana 19:30
·
Baba mikononi mwako naiweka
roho yangu Luka 23:46
Baba mikononi mwako naiweka roho yangu
Kama tulivyoona ya kwamba maneno
haya BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO
YANGU Yalizungumzwa na Bwana Yesu kama maneno ya mwisho pale msalabani na
kisha Yesu akakata roho na matukio mengi ya kushangaza yakajitokeza wakati
mwana wa Mungu akikata roho, Maandiko haya ya msingi yanatuambia hivi tuone
tena:-
Luka
23:46 “Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba,
mikononi mwako naiweka roho yangu”
kimsingi maneno haya yana asili
ya Lugha ya kiibrania na yanatoka moja kwa moja katika Zaburi ya 31:5 thelathini na moja, mstari wa tano, Na hivyo
kimsingi Mwandishi au waandishi wa agano jipya waliruka maneno muhimu kutoka
katika zaburi hii ambayo yana maana pana sana nay a muhimu linapokuja swala la kufufuka kwa Yesu na
sikukuu ya Pasaka, labda waandishi walikuwa na dhana kama yetu ya kufikiri kuwa
Yesu alikuwa amevuta pumzi yake ya mwisho ya uhai na kuamua kufa kwa kukabidhi
roho yake kwa baba yake, basi. Lakini maneno haya yanasomeka namna hii katika
Zaburi yenyewe ya asili ambayo Yesu alikuwa akiinukuu kama maombi pale
msalabani ona -
Zaburi ya 31:5 “Mikononi mwako naiweka roho
yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.”
Aidha ili ieleweke vema pia
zaburi hii katika kiingereza inasiomeka namna hii hasa kwa tafasiri ya Biblia
ya kiingereza ya ESV yaani “English Standard Version” yanasomeka
hivi Psalm 31:5 “Into your hand I commit my spirit; you have redeemed me, O LORD,
Faithful God”, Kwa msingi huo pale msalabani Yesu alikuwa anasali
kwa kunukuu Zaburi ya 31:5 akiwa
katika hali ya mateso makali mno wakati akiwa katika hali yake ya mwilini
duniani akiteseka maneno aliyoyasema Yesu kwa tafasiri ya ESV yalitakiwa kusomeka hivi MIKONONI
MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU,UMENIKOMBOA EE BWANA, MUNGU MWAMINIFU, Kwa hiyo
utakubaliana nami kuwa kuna maneno ya msingi yalirukwa au yalipoteza maana
wakati wa kufanya tafasiri katika lugha mbalimbali, nataka sasa nikuchukue
taratibu ili iweze kujua kwa uwazi maneno haya na maana yake namna yalivyo na
nguvu kuliko tunavyoweza kufikiri utanielewa tu, kwanza tuangalia neno NAIWEKA kwa undani kisha tuunganishe na
maneno yaliyorukwa katika Luka 23:46
na kuyaona kwa uhalisia wake katika Zaburi
31:5
Usemi huo unakubaliana wazi
kabisa na Lugha za kiibrania na kiyunani ambapo neno NAIWEKA ROHO YANGU kwa kiingereza “I COMMIT” katika lugha ya Kiibrania linatumika neno “AFKID” na kiyunani neno “DIAPRATO”,
Neno la kiibrania AFKID kwa kiingereza
linasomeka kama “I DEPOSIT” ambalo
Kiswahili chake ni kuweka amana au kuacha kitu cha thamani kubwa mfano fedha
kwa mtu au taasisi unayoiamini kwa kusudi la kuja kuchukua kitu hicho baadaye,
mfano ni kama vile tunavyoweka fedha zetu bank na kisha tunakuwa na haki au
uhakika wa kuzichukua wakati wowote unaona!, na neno la kiyunani “DIAPRATO” kwa kiingereza “ENTRUST” ambalo maana yake kukabidhi
jukumu Fulani muhimu kwa mtu unayemuamini kuwa atalifanya, atalinda na
kukuwakuilisha salama, Hatakuangusha. Kama Neema ya Mungu itakuwa
imefunuliwa kwako sasa utakuwa umefahamu kuwa
Yesu aliposema BABA MIKONONI
MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU, kama alinukuu
Zaburi 31:5 Basi Yesu alikuwa akisema maneno haya “BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA AMANA ROHO YANGU, UMENIKOMBOA EE BWANA,
MUNGU MWAMINIFU.
Hii maana yake ni nini maana yake
Yesu alipaza Sauti yake kwa imani pasipo shaka akatamka kwa uhakika kuwa
anaiweka Roho yake amana kwa Mungu mwaminifu na ambaye anaweza kumrejeshea na
sio anaweza kukaa nayo jumla jumla, Yesu aliamini katika uweza wa baba yake ya
kuwa anauweza wa kuirejesha Roho yake tena na sio hivyo tu yeye mwenyewe
anauwezo wa kuichukua atakapokua anaitaka kama wewe unavyoweza kuchukua fedha
zako kutoka katika bank wakati unapotaka, Hii maana yeke ni kuwa Yesu kristo
aliutoa uhai wake yeye mwenyewe na
hakuna mtu anayeweza kumuondolea uhai, lakini licha ya kuutoa mwenyewe yeye pia
anauwezo wa kuutwaa tena uhai wake au roho yake, Aidha tunajifunza kuwa maneno
yale yalikuwa na maana ya kuiweka roho yake kwa muda tu, na kisha ataichukua
tena, kwa hiyo kukata roho kwa Yesu kulikuwa ni kwa muda na kuwa angafufuka
tena !
Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa
sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi
nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena.
Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”
Kwa msingi huo Yesu alimaanisha
kuwa hakuna anayeweza kuuondoa uhai wake hapa inajumuisha kila kitu mbinguni na
duniani hakuna anayeweza kuiondoa uhai wake, kifo cha Msalabani ilikuwa ni
hiyari yake mwenyewe kwaajili ya kuwakomboa wanadamu na ndio maana anapendwa na
baba kwa sababu hakuna aliyemshurutisha,
Yesu anayo mamlaka ya kuyatoa maisha yake na anayo mamlaka ya kuyachukua tena,
hivyo ni kwa hiyari yake mwenyewe kwa kawaida yeye humuheshimu baba yake, na
hafanyi neno Bila kuagizwa na baba hasa alipokuwa Duniani neno linasema:-
Yohana 5;19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona
Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile
vile.”
Yesu anazungumza hii katika hali
ya ubinadamu wake hali ya kumtegemea baba yake akiwa duniani, hali ya
kujinyenyekeza, lakini neno lake baba mikononi mwako naiweka roho yangu
linatufungulia akili kujua uweza na mamlaka kubwa aliyonayo Yesu Kristo, lakini
linatuthibitishia kuwa alikuwa na uhakika wa kufufuka!
Yesu hakufa kama afavyo mchuuzi,
ulikuwa ni mpango wake kamili wa kumuokoa mwanadamu, mpango ambao baba wa
mbinguni alifurahishwa nao, kwa mamlaka hii, tunaweza kukabidhi chochote kwake,
na anauwezo wa kuturejeshea, kama kuna vitu tulipokonywa au kuumizwa au kuibiwa
au kudhulumiwa vyovyote iwavyo tunaye Yesu mwenye uwezo wa kuturejeshea
maradufu yeye anauwezo wa kufisha na kuuhisha, anajeruhi na anaponya, nani yeye
mwenye uwezo wa kuokoa hivyo kama kuna kitu kimepotea katika maisha yetu iwe
amani, furaha na kadhalika Huyu Yesu anauwezo mkubwa ana mamlaka kubwa yeye ni
Mungu na anajitambulisha kuwa hakuuawa isipokuwa ilikuwa kwa hiyari yake ni
sadaka aliyojitoa yeye anauwezo wa kuutoa uhai wake na kuuchukua tena na
anaweza kufanya hivyo na lolote kwa yeyote akimtumainia yeye, Maandiko yanasema!
Kumbukumbu 32:39 “Fahamu sasa ya kuwa Mimi,
naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha
Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,”
Hakuna jambo la Msingi kama
kukabidhi maisha yetu, mali zetu, ndoa zetu, kazi zetu, watoto wetu, waume
zetu, wake zetu, mashamba yetu, magari yetu, afya zetu, na lolote lila katika
mikono salama ya baba wa mbinguni ambaye tunajua anaweza kulinda kile
tunachiomkabidhi, hakikisha kuwa katika maisha yako unamkabidhi Mungu mwaminifu
maisha yako kwa sababu yeye anauwezo wa kutunza, kulinda na kukurejeshea kila
kinachopotea ni kwa Mungu pekee ndipo tunapokuwa na uhakika wa kurejezewa kila
kilichopotea endapo kweli katika maisha yetu tulimkabidhi yeye, watu wengi
wamekabidhi maisha yao na mali zao kwa watu mabaradhuli na wakapoteza Yesu
anatukumbusha kuwa ukijikabidhi kwa Mungu mwaminifu hakuna cha kupoteza ! ni
muhimu wakati huu wa msimu wa Pasaka kukabidhi maisha yetu kwa Mungu mwaminifu
yeye atayarejesha tena yatakapopotea kwa sababu yoyote ile, tukiamini kazi
aliyoifanye Yesu Msalabani hakika yeye naye atatufufua siku ya mwisho
Yohana 6:53-54 “Basi Yesu akawaambia, Amin,
amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake,
hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa
milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
Na Rev Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni