Jumanne, 11 Aprili 2023

Naona Kiu - Nina kiu!

 

Yohana 19:28-30 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, NAONA KIU. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.”


Utangulizi

Hivi karibuni Wakristo wote duniani tunaingia katika moja ya Majuma muhimu sana katika kukumbuka mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye aliteseka na kufa kwaajili yatu pale msalabani, Katika wakati huu moja ya maswala ya msingi ambayo huwa tunayakumbuka kwa Pamoja ni pamoja na maneno ya Yesu Kristo pale Msalabani wakati alipokuwa anateseka, kwa ujumla katika injili zote nne unapokusanya maneno yote aliyoyatamka Yesu kabla kidogo ya kukata roho ni Pamoja na maneno haya saba ya mwisho ambayo wakristo huyachukulia kwa uzito mkubwa, Moja ya maneno ambayo tutayatafakari kwa pamoja leo ni pamoja na neno Naona kiu, au Nina kiu,ambalo ni neno la tano katika manenio hayo muhimu, Pamoja na neno hili, lakini maneno yote saba aliyozungumza Kristo ni Pamoja na :-

1.       Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

2.       Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

3.       Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

4.       Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

5.       Naona kiu au Nina kiu Yohana 19:28

6.       Imekwisha Yohana 19:30

7.       Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Tutajifunza somo hili Naona kiu au Nina kiu kwa kuzingatia maswala mawili ya msingi yafuatayo:-

·         Maana ya neno KIU

·         Naona kiu

Maana ya neno Kiu.

Neno kiu kwa kiingereza THIRST ni hali ya  kuhisi au kutaka kunywa kitu Fulani na hasa maji, ni Hali yenye msukumo wenye nguvu wa kutaka kutimiza kitu au jambo Fulani, hali hii wakati mwingine kama ni katika mwili wa mwanadamu inatokana na umuhimu wa mwili kuhitaji maji, kutokana na umuhimu wake na pia kutokana na joto au ukavu Fulani unaojitokeza katika mwili, Neno hilo Kiu katika biblia ya kiyunani linasomeka kama “DIPSAO” kimatamshi  “DIP – SAH – O” Ambalo maana yake kiu halisi au kiu ya jambo Fulani  (to thirst for LITERALLY or FIGURATIVELY) Kwa hiyo Yesu alipozungumza kuhusu kiu kimsingi inaweza kuwa ilikuwa kiu halisi ya kutaka kunywa maji au kiu ya kutaka kuyatimiza mapenzi ya Mungu, nani wazi kuwa kiu aliyokuwa nayo Yesu haikuweza kutimizwa na dunia kwani badala ya kumpa maji wao walimpa divai, na sifongo jambo lililopeleka Yesu kutokunywa, kwa kuwa hiyo haikuwa kiu yake sahihi, Leo tunapotafakari kiu aliyokuwa nayo Yesu Msalabani ni Muhimu kula mmoja wetu kujihoji ana kiu  ya namna gani na je kiu yake inaweza kutimizwa na dunia au inaweza kutimizwa na Mungu? Kiu ya Yesu ilitimizwa na Mungu na haikuweza kutimizwa na wanadamu! Marko 15:23 “Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.” Kile alichokitamani Kristo katika shauku na kiu yake hakikuwa kile ambacho dunia imempa, Mungu atupe neema ya kuweza kutimiza kiu sahihi tuwapo ulimwenguni katika jina la Yesu!

Naona kiu!

Yohana 19:28 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.”   

Moja ya namna ya kuadhimisha Pasaka ni pamoja na kukumbuka Mateso na siku ya mateso ya Bwana wetu Yesu ambayo yametuletea ukombozi, katika siku ile ya mateso Kristo alizungumza maneno Saba muhimu sana katika maisha ya kila Mwanadamu, Katika maneno hayo saba Neno Noana kiu ndio neno la Msingi sana na kiini kikubwa sana cha Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na katika uhitaji wa Mwanadamu wakati tunapopitia mateso kutoka kwa wanadamu wenzetu huku tukiwa na lengo la kudumisha uhusiano wetu na Mungu!, Hapo ndipo Kiu ya kila jambo tulilonalo inapokutana na shida na changamoto mbalimbali,  maneno yote sana yana umuhimu wake na kila moja lina ujumbe wake ingawa leo tutalipa uzito neno la Tano NAONA KIU ;-  bila kupuuzia jumbe katika maneno mengine:-

1.       NENO LA MSAMAHA – Tunapopitia katika wakati Mgumu hasa unaosababishwa na wanadamu wenzetu hatuna budi kufahamu kuwa wakati huo wao wanaona kuwa wako sahihi katika lile wanalokufanyia nan i wewe ndio unaonekana kuwa mkosaji, wakati hio wao huwa dhaifu sana na wewe unayepelekwa matesoni ndio unapaswa kuonyesha ukomavu hivyo kwaajili ya mafanikio Yako samahe – Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo

2.       NENO LA UHAKIKA – Wakati tunapopitia mateso tunapaswa kukumbua ya kuwa wako watu wanaoona umuhimu wetu, na bado wanatutegemea wana wanapaswa kuhakikishiwa kuwa wanakuwa na wakati mzuri hata pamoja na kuteseka kwetu au kuteseka pamoja nao, wahakikishie ya kuwa Mateso ni njia ya kutupeleka katika hali iliyo bora zaidi – Leo hii utakuwa pamoja nani peponi

3.       NENO LA HESHIMA – Wako wale wanaodhalilika unapodhalilika, wako wanaoteseka unapoteseka wako wanaokutegemea ni muhimu kwetu kufahamu kuwa Yesu alikuwa anategemewaa na Ndugu zake na wazazi wake, wakati akiwa katika mateso alitaka kuhakikisha kuwa wazazi wake wanakuwa salama na hivyo alikabidhi Majukumu ya usimamizi wa familia kwa mwanafunzi aliyeaminika kuwa anaweza kumsaidia – Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako

4.       HALI YA UPWEKE – Kila mwanadamu anahitaji kuwa na watu wa kumtia moyo, upweke ni moja ya changamoto kubwa sana kwa mwanadamu hasa anapokuwa mtu mzima lakini zaidi sana tunapopitia katika mateso, wanadamu kwa kawaida hudhani ya kuwa Mungu amemuacha  hsusani anapopita katika magumu au anapokuwa amelemewa na dhambi, - Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha

5.       NAONA KIU – kiu inawakilisha kiini kikuu cha mateso, kila mwanadamu anateseka kwa sababu ya kiu, kila mwanadamu ana kiu anayotaka kuiona inatimizwa katika maisha yake, Kwa bahati mbaya wakati mwingine kiu zetu huharibiwa na watu wenye nia mbaya ambao wanataka kuona kiu yetu ikitimizwa kwa mlango mwingine, Yesu Kristo katikati ya mateso na katika kilelel cha mateso alijisikia kiu bila shaka ilikuwa ni kiu nzuri kiu ya maji safi lakini tunaambiwa watesi walimpa siki badala ya maji, jambo lililopelekea yeye kukataa kunywa Mathayo 27:33-34 “Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa, wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa.” Dunia haita kubali utimize kiu yako, na wakati mwingine utapewa  kitu mbadala kinyume na kiu yako, na kama kiu yako imetoka katika kwa Mungu ni dhahiri kuwa dunia haitakubali uitimize kiu hiyo na badala yake watataka unywe kitu kingine Kiu ya Kristo ilikuwa ni kuwakomboa wanadamu na kuona kuwa watu wote wanaishi kwa amani huku yeye akiwa ni mfalme wa amani, lakini badala yake Dunia ilimfanyia mambo mengine, katika wakati huu tulio nao ni lazima tuwe wakali ili kwamba kiu yetu sisitimizwe kwa njia nyingine, Mapenzi ya Mungu yasikataliwe, Baraka za Mungu zisigeuzwe kuwa laana,

-          Wengi walikuwa na kiu ya kuolewa na kuoa ili wawe na amani katika ndoa zao lakini dunia imewapa machungu badala ya amani

-          Mungu alikusudia tuishi kwa furaha na amani lakini leo hii dunia imewapa vilio na mateso kiu yao ya kuwa na furaha duniani imeharibiwa badala ya maji wamepewa sifongo

-          Wengi wamelima na kupanda wakitarajia mvua itanyesha wapate mazao, lakini dunia imewanyima mvua na imawapa ukame na hali ya uchumi imakuwa sio

-          Mungu alikusudia dunia iwe kama paradiso ka ma watu wangeitunza lakini watu wameharibu mazingira  na hatimaye leo dunia inashuhudia mabadiliko mabaya ya hali ya hewa na ukiharibika kwa anga linalozuia miali mikali ya jua kutufikia moja kwa moja Ozone layer, kuongezeka kwa hewa ya ukaa na hali joto ma mabadiliko makubwa

-          Dunia ilitarajiwa iwe ni sehemu ya ustaarabu, uadilifu na yenye kutunza utamaduni lakini leo tunashuhudia uharibifu mkubwa wa ustaarabu na mmomonyoko mkubwa wa uadilifu, kuharibika kwa tamaduni zenye manufaa na badala yake dunia leo inataka kuwe na ndoa za jinsi moja na kuzalishwa kw agenda ya tatu isiyo ya kiume wala ya kike, Haya pamoja na mambo mengine ni uharibifu wa kiu ya Yesu Kristo unaofanywa na wanadamu

-          Mungu alikuwa na kiu ya kuona haki ikitendeka na dunia ikifanikiwa kila mahali, maana haki huinua taifa lakini dhambi ni aibu ya taifa zima, leo hii wote tunashuhudia haki ikipindishwa kwa rushwa na upendeleo na hukumu zikipotoshwa huo nao ni uharibifu wa kiu ya Mungu

-          Wewe una kiu gani na dunia imekupa maji ya namna gani? Hatuna bhudi kujiweka katika neema ya Mungu na kumuomba Mungu atufanikishe ili kiu yetu na kiu yake isiharibiwe katika maisha yetu tuwapo duniani

6.       KILIO CHA USHINDI – Imekwisha, Yesu alitimiza majukumu yake yote duniani kwa ushindi mkubwa TETELESTAI  Neno hili Imekwisha TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, kila mmoja wetu analo jukumu la kutimiza awapo duniani

7.       KILIO CHA UTII – baba mikononi mwako naiweka roho yangu, Yesu alitii mambo yote ambayo Mungu alikuwa amemuagiza ayatende, usikubali kuondoka duniani bila kutimiza ndoto ambazo Mungu amekukabdihi uzitimilize

Hitimisho!

Kwa hiyo unapoangalia maneno haya saba ya Bwana wetu Yesu Krist utagundua kuwa yote yana umuhimu mkubwa sana lakini neno la tano lina umuhimu mkubwa sana katika swala zima la matarajio ya mwanadamu na kile ambacho dunia inatupa kwa msingi huo basi usalama wetu na kutimia kwa kiu yetu vinaweza kupatikana kwa Mungu mwenyewe

-          Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa” Kama kiu yetu itakuwa ni ya haki na bila shaka hii ni kiu yenye kutaka kuyatimiza mapenzi ya Mungu basi kiu hiyo itatimizwa

-          Yohana 7: 37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.”  Yesu anatoa mwaliko wa kila mtu mwenye kiu aje kwake anywe unaona ni dhahiri kama kiu aliyoisema Yesu ingekuwa kiu HALISI literal Maandiko yasingeweza kuzungumza katika hali kama hii haba ni uhitaji wote wa kimwili na Kiroho Dunia haiwezi kututimizia kiu halisi tuliyo nayo Lakini Yesu anaweza na ametyuahidi kuwa atatimiza hivyo kiu yetu atatupa maji halisi tunywe

Ni maombi yangu kwako katikka pasaka hii kuwa Mungu akutane na kiu yako hamu yako na shauku yako inaweza kutimizwa na Yesu aliyegharimika kufa kwaajili yako pale Msalabani

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!


Hakuna maoni: