Jumatatu, 24 Aprili 2023

Raha Nafsini mwenu !


Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”




Utangulizi:

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Mojawapo ya maneno muhimu sana aliyowahi kuyazungumza Yesu Kristo ni Pamoja na maneno haya tuliyoyasoma katika kifungu hiki cha maandiko, Mstari huu una maana pana sana na unaweza kutufunza maswala mengi sana, Kwa mwanafunzi wa maandiko anayepita hapa haraka haraka anaweza kupoteza maana muhimu sana inayopatikana katika mistari hii, Leo tutachukua Muda hata hivyo kuangalia kwa undani sana Ahadi ya kumfuata Yesu ambayo matokeo yake ni Kuapata raha nasfini, Kila mwanadamu duniani  anahitaji raha, Mapumziko, au kustarehe na kuondoa msongo wa mawazo, kusoma kwetu, kazi zetu maisha yetu, na lolote lile tunalolifanya hata kumuabudu Mungu kwetu kilele chake ni kuwa na Raha, Duniani na kuwa na raha mbinguni, kwa hiyo kila mmoja anahitaji raha, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-

·         Maana ya neno raha:-

·         Aina tano za raha katika maandiko:-

·         Nanyi mtapata raha nafsini mwenu

Maana ya neno raha:-

Neno raha linalotumika hapa na Bwana wetu Yesu Kristo, linatokana na neno la Kiyunani  “ANAPAUO” ambalo kwa kiingereza ni repose  au rest ambalo tafasiri ya kiingereza ni Freedom from activity, or freedom from daily struggle, Ni hali ya kuwa mbali au kuwekwa huru kutoka katika mahangaiko ya maisha ya kila siku, au usumbufu au msongo au kitu chenye maumivu, au mzigo wenye kuelemea kwa mujibu wa Biblia unafuu huu hauwezi kutolewa na mwanadamu bali unaweza kutolewa na Mungu mwenyewe ona ;-

Kutoka 33:12-14 “Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”

Ushahdi wa kimaandiko unaonyesha kuwa raha hii ni ya kinabii na pia ilikuwa inatarajiwa na watu wengi wa Mungu asili ya hii raha haitokani na mwanadamu bali inatolewa na Mungu mwenyewe  raha hii pia inaitwa utulivu, au starehe  au usalama au amani ya Mungu raha hii inaitwa “Margoa” katika lugha ya Kiebrania

 Yeremia  6:16 “Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo.”

Mungu amekusudia kumpa raha kila mmoja kama atakaa katika kanuni zake, na raha hii ilitabiriwa katika maandiko kwa muda mrefu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu aweze kuifurahia raha hii katika jina la Yesu Kristo Ameen!

Aina tano za raha Katika maandiko!

Kwa mujibu wa maandiko kuna aina tano za Raha zinazotajwa katika maandiko n azote ni unabii wa raha halisi tutakayoipata mbinguni, rah azote ni za Muda na zina changamoto mbalimbali ukilinganisha na raha ya milele hata hivyo katika raha hizi raha nafsini ni ya muhimu kwaajili ya kustahimili majaribu ya aina mbalimbali tunayoyapitia tukiwa hapa duniani nitazielezea kwa ufupi lakini ndani zaidi nitaizungumzia raha nafsini mwenu!

1.       Raha ya Sabato -  Mungu alikusudia kuwa watu wake wawe na siku sita za kufanya kazi wakipambana na shughuli za kila siku za maisha na siku ya saba walitakiwa kuwa na utulivu ili Mungu aweze kuwahudumia, na kuziganga na kuziponya nafsi zao, lakini waalimu wengi wa kiyahudi walikaza sana sheria ya  Musa na sharia ya sabato na kupata jumla ya sheria 613 zilizopatikana na kuifanya sharia ya Mungu kuwa ngumu mzigo na kongwa la kuwasumbua watu, siku ya sabato yenyewe ilikuwa ngumu, Wayahudi hawakutakiwa kufanya  jambo lolote siku hiyo hata kuponywa kwa wagonjwa siku ya sabato kwao ilikuwa ni tatizo, kuokoa uhai na kuhudumia roho, mwili na nafsi  ya mwanadamu kwa huruma  lilikuwa ni tatizo ona

 

Luka 6:1-10 “Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.”

 

Kwa hiyo raha ya sababto haikuwa na manufaa mpaka Yesu Kristo mwenyewe ambaye ndiye Bwana wa sabato alipokuja na kuleta pumziko la kweli, kila raha iliingiliwa na changamoto za kumnyima mwanadamu raha kamili iliyokusudiwa na Mungu.

 

2.       Raha ya Kanaani – Mungu alipowaokoa wana wa Israel kutoka katika nchi ya utumwa kule Misri alikuwa na kusudi kubwa la kuwapa raha, raha hii iliitwa raha ya kanaani, nchi iliyosifiwa kuwa ina wingi wa maziwa na asali,  raha hii aliyepewa jukumu la kuhakikisha anawaingiza katika raha hii ni Yoshua ona :-

 

Yoshua 21:43-44 “Basi Bwana aliwapa Israeli nchi hiyo yote, ambayo aliapa kwamba atawapa baba zao; nao wakaimiliki, na kukaa mumo. Kisha Bwana akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao.”

 

Hata hivyo raha hii kwa mujibu wa historia ya kimaandiko inaonyesha kuwa bado wana wa Israel hawakuwa na raha kamili katika ardhi ya kanaani, badala yake walisumbuliwa mara kwa mara na wenyeji wa inchi ile na hivyo hawakuweza kuwa na amani maandiko yanaonyesha ile haikuwa raha kamili iko raha, ayahudi walisumbuliwa mara kwa mara na adui zai, wenyeji wa kanaani, Mungu wakati mwingine aliinua waamuzi ili kuwasaidia katika taabu yao kwa hiyo Raha ya kanaani  inayokusudiwa na Mungu kwa wana wa Israel iliingia dosari na mushikeli na kuwafanya wasiwe na amani ona  kwa hiyo maandiko yalitabiri kuwako kwa raha nyingine ya watu wa Mungu nje ya raha ya kanaani:-

 

Waebrania 4:8-9 “Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye. Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.”             

 

Raha ya kanaani pia ilikuwa ya Muda na Mungu kupitia manabii na watumishi wake alitabiri kuja kwa raha nyingine, Israel hawakupata raha kamilifu katika nchi ya kanaani hata leo!

 

3.       Raha ya ndoa -  ni Neno lililotumiwa na Naomi katika kitabu cha Ruthu kuonyesha kuwa Ndani ya ndoa watu waliooana wakiishi kwa kanuni zilzokudsudiwa na Mungu ndani ya ndoa kuna raha zake, tunafahamu kuwa raha zote hizo ambazo Mungu amekusudia kuwapa wanadamu zina vita lakini hata hivyo ndani ya ndoa kuna raha, kuna raha ya ajabu sana na Naomi  alitamani Ruthu aolewe ili apate raha hii ni raha ya ndoa  Ruthu 3:1 “Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?”

 

raha hii inatamaniwa na kila mwanadamu mwenye akili timani, wanawake wote kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea ndoto hii hujengeka kwao ukiacha kuwa na mafanikio mengine wanataka raha, Lakini kama ilivyo kwa raha nyingine shetani anaipiga vita sana Raha ya ndoa na kutaka kuiharibu, ndoa nyingi zinavunjika na makusudia yaliyokusudiwa na Mungu yanaondoka, leo hii watu waovu wantaka kuziharibu ndoa kabisa hata kuleta ndoa zisizo katika mpango wa Mungu ili kuharibu taasisis hii muhimu iliyokusudiwa na Mungu, wana ndoa wakiomba pamoja kunakuwa na nguvu kubwa sana katika maombi na wakizozazna maombi yao yanaharibiwa!

 

4.       Raha ya wokovu – Hii ni raha inayopatikana kwa kumwamini Yesu na kumfanya Yesu kuwa Bwana na Mwokozi, katika mstari wetu wa Msingi Yesu anapotoa Mwaliko wa kwenda kwake kwa wote wanaolemewa na Mizigo na kujivika nira yake hii ilikuwa ni wito wa  wa kumuamini yeye na kupokea wokovu, Raha hii, pia huwapa wanadamu tiketi ya kuingia Mbinguni kwa hiyo tunaweza kuiita raha ya wokovu kama raha ya kuingia mbinguni  na ni raha ya milele

 

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

 

Yesu anatoa mwaliko wa starehe na pumziko kwa watu wote wanaomuamini na kwa hakika atawaleta katika wokovu na ukombozi wa mwili nafsi na roho na hatimaye atawaingiza mbinguni kwenye raha ya milele

 

Raha hii ya wokovu na ambayo itatufikisha mbinguni ni raha ya milele na ni raha ambayo itawafutilia mbali maadui wote wa wanadamu ikiwemo kifo na pia Mungu atakomesha uonevu wote na kufuta machozi ya taabu zote za  wanadamu walizokutana nazo duniani ona

Ufunuo 21:4 “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

 

Unaweza kupata raha hii sasa kwa kumkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako na kwa kuamini kazi yake yote aliyoifanya pale Msalabani, kwani kwa kupigwa kwake sisi tumepona! Unapomuamini Yesu anaitwaa mizigo yako, anakusamehe dhambi zako unapata raha ya msamaha wa dhambi, Daudi akasema Heri mtu yule ambaye Bwana hamuhesabii dhambi, raha ya namna hii inapatikana kwa kukubali neema ya Yesu na kama umeikubali kamwe usikubali kabisa kumuacha Yesu!

 

5.       Raha nasfi – Raha hii pia kwa bahati nzuri ni raha ambayo Yesu ameitaja pia katika mstari ule ule wa msingi ona Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

 

Raha hii ni raha inayopatikana pia ndani ya nafsi ya Mwanadamu, kama tutaweka tegemeo letu kwa mwokozi wetu Yesu Kristo, katika mstari wa Msingi kuna starehe, pumziko linalopatikana kwa kukubali mwaliko wa kumfuata Yesu,  na ambayo pia inatufikisha katika raha ya milele, lakini Yesu anaitaja raha Nasfini mwenu, raha hii inakuja kwa kumfuata Yesu, kujitia nira na kujifunza kutoka kwake raha hii ni raha ya namna gani hilo sasa linatuleta katika kutafakari kiini cha somo letu leo katika kipengele cha mwisho!

Nanyi mpatata raha nafsini mwenu!

Hakuna jambo la msingi duniani kama kuwa na Raha nasfini mwako, hii ni raha ambayo haiwezi kuondolewa na mtu, ni raha anayotupa Kristo mwenyewe na raha hii haijali mazingira wala hali ya hewa ni raha inayopatikana kwa kumtegemea Mungu, kwa kumfanya Mungu kuwa ndio msaada wako na raha hii hata Mungu akuache upite katika shida au mateso haiondolewi na mazingira ya aina yoyote, wanadamu wa kawaida na shetani hawezi kuiondoa raha hii inakaa ndani inakaa nafsini, haiondoki kwa sababu eti ndoa imevunjika, haiondoki eti kwa sababu umeondoka kazini, haiondolewi kwa sababu, eti hauna fedha, haondolewi eti kwa sababu unateswa, hii ni raha ambayo haitikisiki kwa lolote, kwamba umeolewa hujaolewa una raha, kwamba u tajiri au umasikini una raha, kwamba una majaribu au huna una raha ni raha ambayo hata ukipita katika mateso unaweza kujawa na tabasamu na kufurahi,

-          Ni raha  ambayo haisababishi upungukiwe na kitu zaidi ya kukukamilisha ona Yakobo 1:2-4  kwamba Mungu anaporuhusu changamoto za aina yoyote ile wewe wala hauauzuniki unajua ya kuwa unanolewa na Mungu kwaajili ya utumishi uliokusudiwa na Mungu, unakamilishwa na hutapungukiwa na kitu

 

Yakobo 1:2-4 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”

 

-          Ni raha ambayo hata kama maadui wanakusumbua na kutaka kukutesa au kukudhaklilisha bado hawawezi kufanikiwa kwa sababu wewe unafurahia kuteseka kama Yesu au kwaajili ya Yesu Matendo 5:41-42 “Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.” Wakati mwingine hata kama unauawa bado adui zako wakikukazia  macho watauona uso wako uko kama uso wa malaika watu walifikiri wanaweza hata kumuua Stefano na wakadhani kuwa watamfadhaisha lakini walipomkazima macho kutokana na raha ya nasfi uzo wake ukawa kama uzo wa malaika ona

 

Matendo 6:8-15. “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.  Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza.  Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.”

 

-          Raha ya nasfi inatokana na upendo wa Mungu kwetu, upendo aliouonyesha kupitia kumtoa Bwana wetu Yesu Kristo hivyo ukiwa na raha ya nafsi hakuna mazingira,  hakuna mwenye mamlaka, wale malaika wala lolote linaloweza kukutenga na upendo wa Kristo Yesu ataendelea kuwa ni bwana katika mazingira yoyote yale his love never fails at all

 

 Warumi 8: 33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

Yesu alikuwa anatambua umuhimu wa raha ya nafsi hii ukiwa nayo, hakuna kitu kitakusumbua duniani, utatoboa katika mazingira ya aina yoyote, na utatoboa katika maneno yoyote na mipango yoyote mibaya, kila mtu anayekusudia kukuondolea raha ya nasfi hatafanikiwa utadunda kila mahali ukiwa na raha moyoni, raha hii inapatikana kwa kumfanya Yesu kuwa tegemeo lako na sio wanadamu!                Tumfuate Yesu tufuate njia yake nasi tutapata raha nsfini mwetu!

 

Nyimbo za injili Namba 73: Ushirika mkuu, Furaha yangu!.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: