Mathayo 27:46 - 49. “Na kama saa tisa, Yesu
akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu
wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia,
walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo,
akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha;
na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.”
Utangulizi:
Leo tutachukua Muda kujifunza kwa
undani mojawapo ya maneno Muhimu katika maneno yaliyosemwa na Yesu Kristo
wakati wa Mateso yake pale msalabani MUNGU
WANGU MUNGU WANGU MBONA UMENIACHA, tunataka kujifunza maana ya maneno haya
kwa kina na kuangalia uhalisia wa ubinadamu hususani wakati wanadamu wanapopitia
mateso, Pamoja na menono haya muhimu, tutakayoangalia leo maneno mengine kwa
mfululizo katika maneno saba aliyozungumza Kristo pale msalabani kwa mujibu wa
injili zote nne ni pamoja na :-
·
Baba uwasamehe kwa maana
hawajui walitendalo Luka 23:34
·
Amin nakuambia leo hii utakuwa
pamoja nani peponi Luka 23:43
·
Mama tazama mwanao, mwana
tazama mama yako Yohana 19:26-27
·
Mungu wangu Mungu wangu mbona
umeniacha Mathayo 27:46
·
Nina kiu Yohana 19:28
·
Imekwisha Yohana 19:30
·
Baba mikononi mwako naiweka
roho yangu Luka 23:46
Maana ya Maneno Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?
Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu
akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu
wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”
Ni muhimu kufahamu kuwa Mwandishi
wa kitabu cha Mathayo anajaribu tu kufupisha kile ambacho Yesu Kristo alikisema
na pia anajaribu kutafasiri lugha kiaramu ambayo Yesu aliitumia wakati
anazungumza maneno hayo. Maneno hayo Eloi, Eloi, Lamasabakthan, katika lugha ya
asili yanasomeka kama Eli, Eli, Lama Sabachthan ni sehemu ya maneno kamili
ambayo Yesu aliyazungumza ka lugha ya kiaramu, maneno hayo yanatafasirika hivi
Eli, (Adonai) Eli (Adonai) Lama (Why?) kwanini ?, mbona? Sabachthani (You have
left, Abandoned) me) Umeniacha. Kimsingi
ni kuwa katika kini cha mateso yake Yesu Kristo alikuwa anatimiza na kumuomba
Mungu sawa na Zaburi ya 22:1-22
ambapo katika Zaburi hii Daudi ambaye alipendwa sana na Mungu alikuwa akimuomba
Mungu kutokana na Mapito aliyokuwa akiyapitia ambayo kimsingi pia yalikuwa ni
mapito ya kinabii yaliyohusiana na Yesu Kristo Mwenyewe Mwana wa Daudi, Kumbuka
kuwa Yesu alikuja kutimiza maandiko ambayo torati na manabii na maandiko yote
yaliweka bayana kuwa Masihi hana budi kuteseka
Luka 23:13- 27 “Na tazama, siku ile ile
watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau,
kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa
wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia. Ikawa katika
kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao. Macho
yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi
mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao. Akajibu mmoja wao, jina lake
Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui
yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu
wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele
za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia
katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye
ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu
yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu
walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake;
wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na
wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale
wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona. Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye
mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata
mateso haya na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii
wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.”
Unaona kimsingi Yesu alikuwa
ameandikiwa kila atakalokuja kulitenda na kulinena katika Torati, Manabii na
Zaburi au maandiko hivyo Neno Mungu wangu Mungu wangu ilikuwa ni nukuu ya
Zaburi ya 22 ambayo ina mukhtasari wa Mateso ya Bwana Yesu yaliyotabiriwa na
Daudi katika zaburi hiyo hebu tuyaangalie tuweze kuona
Zaburi 22:1-20 “Mungu wangu, Mungu wangu,
Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee
Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.
Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini
Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini
wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa
watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema,
Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe
ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu. Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni
mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana
hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani
wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.
Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama
nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi
wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana
mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.
Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, Bwana, usiwe
mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga,
Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.”
Kimsingi maombi ya Daudi na
Maombi ya Yesu Kristo yanafanana na hatujawahi kuona wakati wowote Mungu
akimuacha Daudi au akimuacha Yesu Kristo lakini kwanini walilia maneno hayo na
kuomba dua hizo wakati wa mateso yao ilihali wote tunajua kuwa maandiko
yanamsifia Daudi kama mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu ona
Matendo 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa
huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona
Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu
yote.”
Aidha katika namna kama hiyo Mungu
katika neno lake vilevile anajivunia Kristo Yesu mwanae kama mtu aliyeupendeza
moyo wake ona
Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha
kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona
Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka
mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”
Inawezekanaje Mungu kuwaacha
awapendao? Mungu anatujali sana katika kiwango ambacho hata mama anaweza
kumsahau mtoto wake lakini sio Mungu wetu ona
Isaya 49:15-16 15. “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata
asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi
sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta
zako ziko mbele zangu daima. Kimsingi kila mwanadamu anapokuwa na mafanikio
watu”
Mungu wetu anatujali mmno lakini
katika hali ya kawaida kila mwanadmu anapopitia mateso na changamoto za aina
mbalimbali kwa kawaida wanadamu wana tabia ya kuwa mbali nawe wanatabia ya
kukuacha ubaki peke yako na wakati huu Mungu hukaa kimya ili mateso yale yaweze
kuleta somo linalokusudiwa kwako hivuo kibinadamu zinakuweko fikra ya kuwa
huenda Mungu amekuacha, Ayubu alipokuwa na mafanikio makubwa sana tunaambiwa
watu wengi sana walimwendea na nyumba yake ilijaa watu wa kila aina maandiko
yanasema na watu wa nyumbani wengi sana ona
Ayubu 1:3 “Mali yake nayo yalikuwa ni
kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda
wake mia tano, NA WATU WA NYUMBANI WENGI SANA; basi hivi mtu huyo alikuwa ni
mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.”
Tunaambiwa kuwa wakati wa mateso
yake Ayubu watu wote waliokuwa nyumbani mwake walimkimbia mpaka pale Ayubu
alipobarikiwa tena ndio tunaelezwa kuwa watu wote wakamwendea ona
Ayubu 42:10-12 “Kisha Bwana akaugeuza uteka
wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili
kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza. Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa
wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika
nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote
Bwana aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu
kila mmoja. Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo
wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za
ng'ombe elfu, na punda wake elfu.”
Ni swala la kawaida kwamba wakati
wa mateso watu wanakukimbia na mara kadhaa inadhaniwa kuwa Mungu amekuacha nani
kilio cha kawaida Pale mtu anapopita katika magumu kufikiri mkuwa ni Mungu
ndiye aliyemtendea hayo, Ndio maana Daudi alilia katika Zaburi ya 22 japo
ilikuwa pia ni unabii kw Mwanaye Yesu Masihi ambaye naye alilia akijua ya kuwa
anaitimiza Zaburi ya 22 yote alitioandikiwa humo yalitokea siku ya mateso yake
maneno mabaya , kugawanywa kwa nguo zake kwa kuzipigia kura, kugomelewa mikono
yake na miguu yake msalabani, kudharauliwa na kuwekwa katika mikono ya watu
wabaya wapate kumdhihaki, na kumdhalilisha, Kifo cha Msalabani hakikuwa kifo
cha kawaida kilikuwa ni kifo cha maumivu ya kila aina kisaikolojia na nafsi na
mwili Yesu ni kama alikuwa amabaki pake yake msalabani, saa ya kujaribiwa huwa
ni kama tunabaki peke yetu, kundi kubwa la watu waliofaidika na huduma yake
hakuna hata mmoja aliyeweza kusogea na kufanya utetezi wakati Masihi alipokuwa
anateseka Msalabani na ndio maana akaisema zaburi ya 22 ambayo hutambulika
zaidi kwa Mstari wake wa kwanza Mungu wangu Mungu wangu mbiona umeniacha!
Msalabani Yesu hakuwa ametundikwa
kwa sababu nya dhambi yake ilikuwa ni kwaajili ya dhambi zetu mimi na wewe, nani
mimi na wewe ndio ambao tulipaswa kuyabeba maumivu yale, lakini Mwokozi alibeba
kwa niaba yetu na kilio kilikuwa kwa ajili yetu na ubinadamu wetu, alilia
kuonyesha kuwa wanadamu wakati wote tunahitaji msaada wa Mungu na kuwa peke
yetu hatuwezi, adui yetu yu aweza kufanya jambo lolote la kutuumiza sana kama
tutabaki bila msaada wa Mungu, Mtu mmoja aliimba wimbo unasema nafikiria
ukiniacha roho yangu itakuwaje Bwana ? itakuwa ni mawindo ya adui kwa wepesi
sana… wakati wote tunapokuwa na maisha yetu bila ya Mungu tunajiweka katima
hatari ya kushambuliwa na kuumizwa na ibilisi, magonjwa matesi na dhiki za
dunia hii, lakini ashukuriwe Mungu kuwa pale msalabani Yesu Kristo alikuwa
anateseka kwaajili yatu na kwaajili ya ukombozi wetu ili kuukaribisha uwepo wa
Mungu katika maisha yetu
Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko
yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na
Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu
yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Na Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni