Jumanne, 11 Aprili 2023

Mama tazama mwanao


Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”


Utangulizi

Moja ya maneno saba aliyoasema Bwana Yesu pale msalabani ni Pamoja na Maneno haya Mama tazama mwanao, neno hili ni moja ya neno Muhimu sana linalotukumbusha wajibu wetu Muhimu sana wa kuhakikisha kuwa wazazi wetu na jamii yetu na familia zetu zinajengewe uhakika wa maisha ya baadaye hata pale wakati sisi tunapokuwa hatupo, leo tutachukua muda kujifunza kwa undani kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na maana ya maneno haya, hata hivyo ni muhimu kama ilivyo kwa masomo yote ya mfululizo wa maneno saba ya Kristo pale Msalabani kujikumbusha maneno yote sana kwa mfululizo wake kisha tutaendelea na uchambuzi wa neno husika leo, Maneno yote sana ya Msalabani ni pamoja na :-

·         Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34

·         Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani peponi Luka 23:43

·         Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27

·         Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46

·         Nina kiu Yohana 19:28

·         Imekwisha Yohana 19:30

·         Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46

Tutajifunza somo hili, Mama tazama mwanao kwa kuzingatia maeneo makuu matatu yafuatayo:-

*      Utata kuhusu Ndugu wa Yesu Kristo

*      Kwa nini Mariam mikononi mwa Yohana ?

*      Mama tazama mwanao

Utata kuhusu Ndugu wa Yesu Kristo.

Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”

Kabla ya kuzungumzia umuhimu na maana ya maneno ya Bwana Yesu ya awamu ya tatu Mama tazama mwanao… Ni muhimu kwanza tukaondoa utata wa kitheolojia unaotoka na msimamo wa kanisa katoliki na msimamo wa makanisa ya kipentekoste kuhusu Maana ya mstari huu!

Katika mtazamo wa kikatoliki wao wanajenga hoja ya kuwa mstari huu wa Yesu akiwa msalabani kumwambia Mama tazama mwanao Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama mama yako, Na tangu saa ile Mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake, ni suhahidi wazi kuwa Mariamu hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu, wakatoliki wanajenga hoja kuwa ni jambo la kushangaza kumuona Yesu akimkabidhi mama yake kwa Mtu mwingine mbali na watoto wake mariamu kama mama huyo angelikuwa na watoto wengine kwa hiyo kwao mstari huu ni ushidi ulio wazi kuwa Mariamu hakuwa na watoto wengine tofauti na wapentekoste wanavyodai!

Katika mtazamo wa kipentekoste ni wazi na dhahiri kuwa kulikuwepo sababu maalumu za Yesu kumkabidhi mama yake Kwa mwanafunzi aliyempenda sana ambaye kiushahidi mwanafunzi huyu ni Yohana, ukweli wa kuweko ndugu za Yesu kristo sio ukweli na mtazamo wa kipentekoste bali ni ukweli na mtazamo wa Biblia yenyewe Maandiko yanaionyesha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu zake wa kuzaliwa mara baada ya yeye kuzaliwa nao walikuwa ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda pamoja na dada zake wawili ona :-

Mathayo 13:53-56 “Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?

Biblia imeweka wazi kuwa Yesu Kristo alikuwa na ndugu zake na imetueleza kuwa mwanzoni nduguze walikuwa bado hawajamuamini, na pia mara kwa mara walimtembelea kutaka kumuona hata wakati akiwa anawahudumia watu ona

Mathayo 12:46-47 “Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe.”

Marko 3:31-32 “Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

Luka 8:19-20 “Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.”

Yohana 7:1-10 “Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. Kweeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa haujatimia wakati wangu. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.”

Matendo 1:13-14 “Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”

Wagalatia 1:18-19 “Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.    

Kwa hiyo tunapoyachunguza maandiko unaweza kuona kuwa yanabainisha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu wa kibailojia ndugu wa damu ndugu wa kuzaliwa mara baada yaye ye kuzaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kwa msingi huo ni dhahiri ya kuwa Yesu alikuwa na ndugu,  na ndio maana utaweza kuona kwa asili wanapotajwa wanatajwa wakiwa pamoja na mama yao, wakatio mwingine wakatoliki wamefikiri kuwa ndugu hao wa Yesu ni binamu zake lakini iko wazi kuwa hao hawakuwa binamu zake Neno la asili la kiyunani linalotumika katika maandiko kuelezea maana ya Ndugu ni Adelphos au Delphus ambalo maana yake connective particle au Morphological ties Neno hilo Ndugu limetumika mara 346 katika Biblia likimaanisha Ndugu wa damu au ndugu wa tumbo Moja wakati ndugu wa kiimani limetumika mara 226 kwa msingi huo Yesu alikuwa na ndugu wa damu na wa kuzaliwa baada ya kuzaliwa yeye kwa muujiza nduguze wa karibu walizaliwa Nduhu hao wa Yesu wanatajwa katika maandiko baada ya Yesu kuzaliwa na sio kabla kwa kuwa wangeweza kutajwa wakati Yusufu alipoenda Bethelehemu au walipokimbilia Misri au wakati wa kurudi Nazarethi kwa msingi huo Maandiko yanabainisha wazi kuwa Yesu alikuwa na ndugu zake wa damu na wa kuzaliwa mwenye sikio la kusikia na alisikie neno hili.

*      Kwa nini Mariam mikononi mwa Yohana ?

Swali kubwa wanalouliza wengi ni kuwa kama Yesu alikuwa na ndugu zake iweje Yesu amkabidhi Mariama kwa Mwanafunzi wake aliyempenda aitwaye Yohana? Jibu ni rahisi sana Yohana ndiye mwanafunzi pekee aliyekuwa karibu sana na Msalaba pamoja na Mariamu mama yake Yesu wakati wanafunzi wengine walikimbia au walikuwa wakiangalia kwa mbali sana

Mathayo 26:58 “Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.”

Mathayo 27:55-56 “Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.”

Marko 15:40-41 “Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.”

Luka 23:49 “Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.”

Wakati injili zote zikithibitisha kuwa watu wote walikuwa mbali sana na Yesu wakati wa mateso yake habari njema ni kuwa waliokuwako karibu kabisa na msalaba kiasi cha kusikia maneno ya Yesu akizungumza ni Mariamu mama yake Yesu na Yohana mwanafunzi mpendwa wa Yesu Kristo  ona

 Yohana 19:26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.”

Yesu alipokuwa msalabani aliweza kumuona mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu unaona jukumu la kumuangalia Mariamu mama yake Yesu alipewa Yohana na Jukumu la Mama kumuona Yohana kama mwanae walipewa kwa sababu ndio waliokuwa karibu na Yesu na sio vinginevyo, wakati wa mateso  na majaribu watu muhimu ni wale wanaokuwa karibu na wewe na sio wale wanaokuwa mbali na wewe

*      Mama tazama mwanao

Ukiacha sababu ya Yesu kumuona Yohana na mama yake kuwa karibu kiasi cha kuweza kuzungumza nao na kuwapa majukumu ya kutunzana maneno haya mama tazama mwanao na mwana tazama mama yako, ni fundisho lililowazi kuwa Yesu pamoja na mambi mengine alikuwa anaijali famlia yake, Historia ya kimasimulizi ya kale inaona wazi kuwa huenda Yusufu baba mlezi wa Yesu Kristio na baba mzazi wa ndugu zake Yesu huenda atakuwa alifariki kitambo kidogo kabla ya kusulubiwa kwa Yesu na huenda kuwa ni kwa muda Fulani Yesu alikuwa ndio nguzo ya Familia na ndio maana utaweza kuona ndugu zake na mama yake mara kadhaa walikuwa wakimuendea, Sasa Yesu Yuko Msalabani alimkabidhi mama yake kwa Yohana na kumtaka amuangalie na pia alimkabidhi Mariamu kwa Yohana ili wawe na ushirika naye

Agizo hili linatukumbusha wote majukumu yetu ya kuwaangalia wanafamilia wote na kuhakikisha tunawatunza,  kukabidhiwa kwa Mariamu kwa Yohana ni sawa na kukabidhiwa kwa wanafunzi wote na Yesu angeagiza hivyuo kwa owte kanma wote wangekuwa karibu naye Mungu hana upendeleo, baadaye tunamuona Yesu akiwaoa wanafunzi wake majukumu kadhaa akionyesha kuwa amewaamini, mfano alimwambia Petro Lisha kondoo zangu lakini pia aliwaambia wanafunzi wote waihubiri injili na kuwa anagekuwa pamoja nao zaidi ya yote tunawaona wanafunzi wote baadaye wakiwa na Mariamu mama yake Yesu na nduguze wakiwa na ushirika mmoja wote kwa pamoja, 

Matendo 1:13-14 “Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.”

Unaona Katika majira ya Pasaka ni muhimu kila mmoja kukumbuka kuwa karibu na familia na kuangaliana na kutunzana lakini ni wakati wa kujikumbusha umuhimu wa kuwa karibu na wale wanaopitia changamoto za aina mbalimbali, na wakati wote kuhakikisha kuwa tunawakumbuka wazazi wetu na kuwapa msaada wa karibu unaowezekana heshima hii ni ya Muhimu wakati wote tunapokuwa hai.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Hakuna maoni: