Wagalatia 6:17-18 “Tangu sasa mtu
asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu
zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.”
Utangulizi:
Wagalatia 6:17-18 “Tangu sasa mtu
asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu
zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.”
Leo tutachukua muda kutafakari
kwa kina maneno ya mkuu wa wajenzi mwenye hekima yaani Paulo mtume alipokuwa anamalizia waraka wake
kwa Wagalatia, Paulo hapa alikuwa akiwaaga Wagalatia na kuwaonya kuwa wakae
katika kweli, Ambayo kwaajili ya hiyo yeye aliitesekea huku akiamini kuwa
watayashika Mafundisho yake “Tangu sasa mtu asinitaabishe kwa maana ninachukua mwilini
mwangu chapa zake Yesu” huenda haya yalikuwa ni maneno yake ya
mwisho na yenye kuonyesha msimamo wake imara kuhusiana na uhusiano wake na
Kristo, endapo Wagalatia hawatajali habari ya injili na njia ile aliyokuwa
amewahubiri, Msimamo anaouweka Paulo hapa unafanana sana na ule Uliowekwa na Yoshua
kwa wana wa Israel katika hutuba yake ya
mwisho kwamba wachague ni nani watakayemtumikia lakini yeye na nyumba yake
wameamua kumtumikia Bwana. Ona:-
Yoshua 24:14-15 “Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie
kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu
waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana. Nanyi kama
mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni
miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya
wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu
tutamtumikia Bwana.”
Ni katika mazingira kama hayo
Paulo mtume alikuwa akiwaonya Wagalatia kuifuata injili iliyo sahihi na
mafundisho yaliyo sahihi ambayo yeye aliwaelekeza, Lakini mwanzoni alionyesha
masikitiko yake vilevile kuwa wako watu waliowafundisha makanisa ya Galatia kushika
sheria kadhaa ikiwemo kutahiriwa jambo ambalo halikuwa na ulazima katika wokovu
wa mwanadamu lakini Wagalatia wengi waligeuka na kusahau mafundisho sahihi na
badala yake wakawa wakirejea kwenye mafundisho manyonge yenye upungufu:-
Wagalatia 4:9-11. “Bali sasa mkiisha kumjua
Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya
kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?
Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda
nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.”
Paulo alionya wazi kuwa wale
wanaohubiri injili inayounga mkono maswala ya sheria kama tohara wanafanya
hivyo kwa kuogopa mateso, Kwani kila mtu anayeihubiri kweli ya injili kama
ilivyo Wayahudi walikuwa wakimuudhi na wakali sana na waliendesha msako mkali
wa mateso ambayo Paulo mtume yalimkuta mara kadhaa
Wagalatia 6:11-14 “Tazameni ni kwa herufi
gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe! Wote watakao kuonekana
ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi
wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe
waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona
fahari katika miili yenu. Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho
chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.”
Ni kwaajili ya hayo Paulo mtume
anaonyesha kuwa amekwisha kuiweka kweli wazi na amekwisha kuwaandikia Wagalatia
na amekwisha kuwapa injili ya kweli na kuwaonya na ni wao ndio wenye maamuzi ya
kuamua kuifuata njia sahihi na mafundisho sahihi ya Kristo au la na yeye kuonyesha msimamo wake kuwa yeye
anaendelea kuubeba msalaba na kuwa yuko tayari kuteseka kwaajili ya Kristo na
hatachuja kwa namna yoyote kiwango cha injili anayoihubiri na kuwa yeye yuko tayari na amekwishateseka na
ataendelea kuteseka kwaajili ya injili
ya Kristo, Yeye anawapenda sana Wagalatia
na ni watoto wake aliowazaa mwenyewe
kiroho, lakini anashangazwa wanapoigeukia injili nyingine! Tutajifunza somo
hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
Maana ya neno chapa.
Kuchukua chapa za Yesu Kristo.
Maana ya neno chapa
Wagalatia 6:17-18 “Tangu sasa mtu
asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu
zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.”
Neno Chapa linalotumika katika
maandiko hapo katika Biblia ya kiyunani linatumika neno STIGMA ambalo asili ya neno hilo ni STIZO ambalo kwa kiingereza linafafanuliwa kama - incised Mark au a punched Mark for
recognition of ownership yaani ni alama isiyofutika au chanjo inayowekwa
katika mwili wa mnyama au mtumwa kwaajili ya kutambua kuwa ni mali ya mtu
Fulani, chapa hii pia hutumika kuelezea alama za huduma ya askari yaani SCAR OF SERVICE yaani majeraha ya
askari aliyeshiriki vita za aina mbalimbali.
Nyakati za Biblia wakati wa zama
za agano jipya lilipokuwa likiandikwa watu waliokuwa na alama au chapa au makovu
walikuwa ni watu wa aina tatu, Watumwa, Askari na Watawa hawa walikuwa na alama
au makovu yaliyotokana na shughuli zao, Askari hususani waliokuwa na uzoefu wa
vita mbalimbali walijulikana pia kwa kuwa na makovu ya aina mbalimbali katika
miili yao, Watumwa nao walikuwa na alama za moto ambapo mmiliki wa mtumwa angeweka
chombo maalumu katika moto na kumuweka alama mtumwa wake kuonyesha kuwa mtumwa
huyo anamilikiwa na Bwana wake na kuwa hana uwezo wa kumilikiwa na mtu
mwingine, lakini na watawa Devotee
watu walioamua kujitoa kwa ajili ya Mungu walikuwa pia na alama za kuonyesha
kuwa wao ni mali ya Mungu,kwa maisha yao ya kujikana mtindo wao wa maisha na
mavazi, ni Katika wazo kama hili Paulo mtume anaonyesha wazi kuwa mwili wake
umejaa majeraha kama askari aliyejeruhiwa katika vita za aina mbalimbali,
lakini vilevile yeye kama mtumwa wa Yesu Kristo anaendelea kuchomwa na kuwekwa
alama hizo kama mtumwa asiyelipwa au mtumwa asiye na faida, akiwa na alama
nyingi za mateso kwaajili ya Yesu Kristo,
alama hizi ni changamoto mbalimbali na upinzani wa aina mbalimbali
aliokutana nao kwaajili ya injili, aidha mtindo wake wa maisha na mwenendo na
tabia zake zinaendelea kukua na kuwa kama za Kristo akidhihirisha ya kuwa yeye
ni mtu aliyejiotoa kwa Yesu Ona:-
2Wakorintho 11:21-27 “Nanena kwa jinsi ya
kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri
kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na
mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia.
Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu
kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika
mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu
nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri
mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari
kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini;
hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara
nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa
uchi.”
Paulo sasa amekuwa mtu mzima kama
ungeweza kumuona hungeweza kufurahia sura yake iliyoharibiwa na iliyojaa
makovu, mikono inayotetemeka kwa vipigo, majeraha ya kuumizwa katika vipigo vya
aina mbalimbali, kule Filipi alipigwa na kutiwa gerezani, huko Listra alipigwa mawe
mpaka akapoteza fahamu, huko Melita alivunjikiwa na jahazi haya yote yalimfanya mtume huyu aliyekuwa
mrefu mwembamba na mwenye macho ya bluu na matege miguuni, na nywele zilizokuwa
zimejisokota kuwa na sura ya Yesu aliyesulubiwa, Paulo hakuwa anatafuta
umaarufu, wala hakuwa mnenaji hodari kama wanafalsafa wa kiyunani,
alidharaulika na kukataliwa, Hakuna mtu katika nyakati za kanisa la kwanza
aliyekuwa anatafuta kuwa maarufu, kila mmoja alikuwa akiihubiri injili na
kuifanya kazi ya Mungu kwa moyo na wengi waliumizwa vibaya walitiwa
magerezani walikuwa kama askari
waliopigana vita nyingi wakiwa na makovu ya mwilini na moyoni, Kimsingi Mtume amekwisha kuiweka kweli
hadharani, ni wajibu wao sasa wagalatia kuyashika aliyowafundisha lakini yeye
anachukua alama za Kristo, yeye anabaki na msimamo mkali wa kumfuata Yesu kama
alivyo hana mpango wa kurejea nyuma bali kushikamana na hatua zake Kristo,
akikubali kuteseka kwaajili ya Kristo lakini vilevile kukua kiimani na
kuendelea kukua kitabia na kiuadilifu kufika kwenye ubora wa tabia na mwenendo
kama aliokuwa nao Kristo!;-
Kuchukua chapa za Yesu Kristo.
Kimsingi kama tulivyoona hapo
awali kwamba waliokuwa na alama hizo walikuwa ni Watumwa, Askari na watawa,
Watumwa waliwekwa alama ya utumwa na Bwana wao kuonyesha kuwa wanamilikiwa
alama hizo zilipatikana kwa chuma kupashwa moto na kisha wakachomwa na kubaki
na alama hiyo kudhihirisha kuwa wao ni watumwa wa mtu fulani milele na hawawezi
kuepuka, Askari nao walikuwa na alama za mkuu wa majeshi yao ili wasiweze
kabisa kujitoa kutoka kwa kamanda wao, lakini vilevile alama za makovu
zilizodhihirisha kuwa walishiriki vita nyingi na wanauzoefu wa vita na
waliojitoa kuishi maisha ya utawa walijitoa kwa Mungu waliwekwa alama hizo na kuhani, wakionyesha kwa maisha yao na mwendo
wao kuwa wao wamejitoa kuishi kwaajili ya Mungu, alama hizo kwa kuwa ziliwekwa
kwa moto ziliacha majeraha au makovu katika miili yao, Kimsingi alama ya utumwa
pia ilikuwa ni alama ya aibu na sio ya heshima,
Paulo anautumia mfano huo kujitangaza kuwa yeye ni Mtumwa wa Yesu Kristo
asiye na faida ni kama hawezi kumtoroka
Kristo yeye ni mfungwa kwake, na zaidi ya yote yuko tayari kuishi kwaajili ya
Kristo akifuata nyayo zake na tabia zake na mwendo wake:-
Filemoni 1:1 “Paulo, MFUNGWA wa Kristo
Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi
pamoja nasi, na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa
kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa
Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.”
2Timotheo 4:7 “Nimevipiga vita vilivyo
vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;”
Unaweza kuona Paulo anajitaja
kama Mtumwa maana yake ni Mfungwa na zaidi ya yote Mpiganani nimevipiga vita
vilivyo vizuri (Askari) anakubali kuaibishwa kwaajili ya Kristo mbele ya macho
ya watu wa dunia hii, alama anazozizungumza Paulo ilikuwa ni Utumwa wa Yesu
Kristo, Askari mwema kama mpiganaji na kama mtu aliyejitoa kwaajili ya Kristo
akikubali kuaibishwa na sio kutafuta heshima, Lakini zaidi ya yote kuonyesha
tabia na mwenendo wa ukomavu wa kuishi kama Kristo mwenyewe na hataki
kutaabishwa katika hilo!
Tuwapo hapa duniani Yesu alisema
tunayo dhiki, na ziko changamoto za aina mbalimbali, kazi yetu kubwa ni
kuihubiri kweli na kuhakikisha tunawaambia watu kile ambacho Mungu ametuagiza,
lakini lazima ufikie wakati tuwe na maamuzi yetu yakuwa hata watu waseme nini
kuhusu maisha yetu au maisha yako jambo kubwa la msingi ni kuchukua chapa za
Yesu, kila mwanadamu anaweza kukosea, kila mwanadamu anaweza kufanya uzembe,
kila mwanadamua anaweza kufanya makosa na wako watu ambao wanabaki na makosa na
uzembe na tabia zetu za zamani kuendelea kuzitumia kama mfano wa kutuchafua na
kujaribu kututaabisha nataka nikuambie:-
-
Kama wako wanaosengenya wasengenye sana lakini
watangazie kuwa tangu sasa mtu asinitaabishe nachukua chapa za Yesu
-
Kama kuna wanaoshutumu na kulaumu walaumu sana
lakini waelewe jana sio leo ziko chapa za Yesu, tunaweza tusibebe chapa za
Kristo katika miili yetu lakini tunawezxa kuzibeba katika mioyo yetu, tumekuwa
makomandoo, tu meumizwa sana, tumekataliwa sana, tumesengenywa sana, tumezomewa
sana, tumeaibishwa sana, tumeshutumiwa sana, tumeonekana kutokufaa sana
tumechakazwa sana, tumedhulumiwa sana, tumesingiziwa sana, lakini haijalishi
kama tumebaki na Kristo na njia ya mateso tulioipitia inakomaza mishipa yetu na
kutufanya tuwe kama Kristo basi ni Dhahiri dunia inatakiwa itambue kuwa
tunachukua chapa zake Kristo!
-
Kama kuna waliopata somo kupitia makosa yetu na
tabia zetu za wakati wa ujinga na wabaki nazona wazitumie kama somo, na
wazitumie kama shuhuda lakini sisi tunachukua
chapa za Yesu, chapa za Kristo ni ukomavu unaoonyesha kuwa tuna uzoefu wa vita,
tunasonga mbele na tunaendelea kuishi maisha ya utauwa, Mungu huwakomaza watu
wake kupitia changamoto mbalimbali jambo kubwa la maana ni kubaki na Kristo na
kudumu katika Imani bila kujali kuwa ni aina gani ya mapito tunapitia!
-
Iwe inili yetu inakubalika au iwe haikubaliki,
maadamu tumehubiri kweli mtu asitutaabishe tunachukua chapa za Yesu, hatudaiwi
mikono tumenawa na mavumbi tu mekun’guta, sasa tunalenga kuwa kama Yesu
-
Wakati mwingine injili inapohubiriwa sio lazima
watu waikubali hata Yesu alifanya miujiza mingi Kapernaumu, Bethasaida na
Korazin lakini hawakumuamini hivyo sisi sio wa kwanza tunachukua chapa za Kristo, tunaishi na
kuigiza tabia na mwenyedno wa Kristo na hiki ndicho tulichoitiwa
-
Tangu sasa mtu asinitaabishe maana nachukua
chapa za Yesu, aidha ionekane nimebarikiwa au ionekana kama nimelaaniwa
haijalishi wa Muhimu ni Kristo, mwenedo wake, tabia zake na uwezo wake mkubwa
wa kuvumilia mateso alipokuwa duniani ni chapa tosha ambazo mkristio anapaswa
kuzichukua
-
Kama ni mateso, Yesu na mitume waliyapitia,
kusemwa vibaya, kushutumiwa kusingiziwa na kadhalika hiyo haiwezi kusababisha
tusimfuate Yesu, au tusiendelee kuwa na tabia na mwenendo kama ule wa Kristo ni
lazima tuitangazie jamii ya kuwa tunachukua chapa za Yesu kwa midomo yetu na
kwa matendo yetu na kwa muitikio katika maswala magumu na changamoto ngumu
tunazozipitia
-
Lazima majamii ifahamu kuwa maneno yao, matusi
yao, masingizio yao, mashutumu yao, uzushi wao na uongo wao hauwezi kuzuia kitu
chochote wala kumshawishi Mungu kufuta jina langu na la wale walio kama mimi
wasichukue kwenye kitabu cha uzima wala tusiache kuchukua chapa za Yesu
-
Wanaotarajia kuwa watatupunguza makali,
watashusha kasi yetu, na kutufanya kuwa somo la lawama ni lazima wajue kuwa
sisi tumekusudia kuchukua chapa za Yesu, Tangu sasa mtu asinitaabishe nachukua
chapa za Yesu!
-
Wewe kama unaona ujanja kuifuata dunia, kuiba,
na kujinufaisha kwa masengenyo na dhuluma na wizi na uasherati na zinaa na
uadui na ugomvi na uchawi, chuki, wivu, hasira, uzushi, uuaji, ulevi, uwongofitina
na majungu, hongera zako hizo ni chapa za Shetani, sisi tutwaonyesha chapa za Kristo,
kwamba tuna uwezo wa kuwa na furaha katika mazingira yoyote, kuwa na Amani,
kuvumilia na kuonyesha utu wema, na uaminifu, na kiasi chapa za Yesu katika
mazingira yoyote yale hakuna kitu chochote duniania nitaweza kutufanya
tusimfuate Yesu
-
Kwanini ? kwa sababu Hakuna kitu kinaweza
kututenga na Upendo wa Kristo! HAKUNA !
Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na
upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari,
au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,
Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote
tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha
kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye
mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu,
wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo
wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Rev. Innocent Mkombozi Samuel Jumaa Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni