Matendo 27:14-25 “Baada ya muda mchache
ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu
iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na
tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza
mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza
merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika
fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana
tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa
shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao
wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika,
basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula
chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza
mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.
Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja
miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo
malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama
karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari;
tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume,
changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama
nilivyoambiwa.”
Utangulizi:
Wanaume ni moja ya rasilimali
muhimu sana duniani kama vile ilivyo kwa wanawake, Wanaume wana mchango mkubwa
sana katika jamii, kupitia uwepo wao, kazi zao, ubunifu wao, uongozi wao na
katika mahusiano ya kijamii, wana mchango mkubwa sana katika familia, Wanaume wana Mchango mkubwa katika jamii na
viwandani na katika siasa na hivyo kuwa na mchango mkubwa sana wa maendeleo
endelevu duniani, lakini zaidi ya yote wana umuhimu mkubwa sana katika kanisa
la Mungu!, Mungu aliwatumia wanaume kama makuhani nyakati za Agano la kale,
lakini katika kanisa wana mchango mkubwa sana, wana uwezo wa kuongoza, kufundisha,
kuendeleza mwili wa Kristo na maendeleo mazima ya kiroho, kwa hiyo Kanisa
haliwezi kabisa kuwapuuzia wanaume, Nyakati za Kanisa la kwanza Mitume waliwapa
wanaume kipaumbele kikubwa sana kuna wakati hata kuongoza ibada Paulo mtume
alitamani sana wanaume waifanye kazi hiyo, Katika juma hili ambalo watu
wanawazungumzia wanawake mi nimechagua kujizungumzia, ili pamoja na mambo
mengine tusisisitize mambo tukawaacha nyuma wanaume!
1Timotheo 2:5-8 “Kwa sababu Mungu ni mmoja,
na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye
alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira
yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli,
sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi, nataka wanaume
wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala
majadiliano.”
Paulo hamaanishi kuwa wanawake
hawapaswi kuomba, Lakini yeye anawataka wanaume kuwa mstari wa mbele katika
maombi kila mahali, wawe ndii viongozi wakubwa wa ibada nyumbani na hata
makanisani, wao ni kichwa cha familia,
ni viongozi wa familia na hivyo ni viongozi wa jamii, Nyakati za leo kumekuwako
na wimbi kubwa sana la wanawake kuwa na muitikio mkubwa wa kufika katika ibada
na kumtafuta Mungu hata kuliko wanaume, kwa hiyo wanawake wengi wanafunguliwa
na kufanikiwa, wanaponywa mioyo yao na kuwa mbali na misongo ya mawazo,
wanapata unafuu, wananawiri kuliko wanaume, hii ni kwa sababu wanaume wako
mstari wa mbele kupambana na dhuruma za maisha huku wakiwaachia wanawake
kuutafuta uso wa Mungu, jambo linalopelekea wanaume kushambuliwa zaidi kuliko
wanawake na hata kuwafanya wazimie mioyo, Leo Bwana anataka kuwakumbusha
wanaume kuwa mstari wa mbele na kuchangamkia kuutafuta uso wa Mungu na uwepo wa
Mungu ikiwezekana kuwazidi wanawake, wanaume wengi wamekuwa wakiishi kwa
kutegemea maombi ya wake zao na hata
kufikiri kuwa ni wajibu wa wake zao kuwaombea lakini neno la Mungu linawataka
wanaume kuchangamka na kurejea katika nafasi yao na kusimama na bwana na kwa
kufanya hivi Kanisa litakuwa na nguvu kubwa sana na taifa letu litakuwa na
maendeleo makubwa sana endapo wanaume wataamka na kuchangamka Basi wanaume
Changamkeni! Tunajifunza somo hili wanaume changamkeni kwa kuzingatia vipengele
vitatu vifuatavyo:-
·
Nafasi ya Mwanaume katika moyo wa Mungu
·
Nguvu ya Mwanaume mwenye kumcha Mungu
·
Basi wanaume Changamkeni!
Nafasi ya Mwanaume katika moyo wa Mungu
Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko
matakatifu yamewapa wanaume nafasi kubwa sana na kipaumbele cha hali ya juu
katika kuonyesha kuwa wako katika moyo wa Mungu, wanaume ni wazo la Mungu,
Mungu alipokusudia kuumba ulimwengu katika wazo lake kamili alikusudia kumuumba
mwanaume, hivyo mwanaume ni kiongozi, ni chaguo la kwanza la Mungu bila
kupuuzia wanawake lakini wanaume ni wazo la msingi,
Mwanzo 2:7-17 “BWANA Mungu akamfanya mtu
kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.
BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake
huyo mtu aliyemfanya. BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti
unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya
bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Ukatoka mto katika Edeni wa
kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne. Jina la
wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna
dhahabu; na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham. Na
jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. Na jina la
mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.
BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na
kuitunza. BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa
bustani waweza kula,walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile,
kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”
Mungu alimpa Mwanaume nafasi ya
Kwanza kabla ya kuumbwa kwa mwanamke, maandiko yako wazi kuwa wanaume walikuwa
ni watii, kwa Mungu, walishika maagizo ya Mungu na hawakutenda dhambi, mpaka
alipokuja mwanamke ndipo ilipotokea makosa, na Paulo mtume anaweka wazi kuwa
mwanamume ndiye wakwanza kuumbwa kwa msingi huo wanaume ndio wakwanza kumjua
Mungu na hawakuwahi kudanganywa! Mpaka alipokuja mwanamke na kuwa wala Mwanaume
hakudanganywa! Ona
1Timotheo 2:13-14 “Kwa maana Adamu ndiye
aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke
alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”
Kwa msingi huo utaweza kuona kuwa
wanaume wanapewa kipaumbele kikubwa zaidi katika kujenga mahusiano na Mungu
kama viongozi wa dunia, ni jambo la kusikitisha kuona wanaume wanaachwa, ama
wanapuuzuia hali ya kumcha Mungu, huku nafasi hizo zikienda kwa wanawake,
kitendo cha wanaume kupuzia maswala ya Mungu, hakuna tofauti kabisa na wayahudi
kumpuuzia Kristo, Maandiko yanaonyesha kuwa kama Israel ingemtii Kristo yaani
wayahudi kungekuwa na baraka kubwa sana duniani, hali kadhalika kama kila
mwanaume akisimama katika nafasi yake tutakuwa na dunia ya tofauti sana, muda
usingeliweza kutosha kuonyesha jinsi wanaume wa kwanza katika maandiko
walivyokuwa mstari wa mbele katika kujenga uhusiano na Mungu kuliko wanaume wa
leo, Nuhu, Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Ayubu, Daudi, Sulemani, na wanaume wengi
kadhaa wa kadhaa walisimama na Mungu na kudumisha uhusiano na yeye, Mpaka Mungu
akaitwa Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Je unadhani Mungu hakuwa Mungu wa
Sara, na Rebeka na Raheli? Mungu hana upendeleo alikuwa ni Mungu wao lakini
waume zao ndio waliokuwa mstari wa mbele, katika kujenga madhabahu, kutafuta
uso wa Mungu na kupata miongozo mbalimbali na Mungu aliwatumia na kuwa Baraka
kubwa kwa dunia, leo hii wanaume wakisimama, na kuielekeza mioyo yao kwa Mungu,
Nakuhakikishia Dunia itakuwa ya tofauti na ndio maana Roho wa Bwana leo anasema
Basi wanaume changamkeni! Wanaume ndio waliokuwa wamepewa kipaumbele kikubwa
sana katika ukuhani na baadaye katika maongozi ya Kanisa, Mungu anawaamini
wanaume lakini wanaume wanapozubaa Mungu hashindwi kuwatumiwa wanawake na
akiwatumia wanawake haitawapa heshima wanaume yaani itakuwa aibu kwetu wanaume
kama tutazubaa na kumwachia Mungu nafasi ya kumtumia mwanamke! ona
Waamuzi 4:4-9 “Basi Debora, nabii mke,
mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. Naye alikaa
chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima
ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue. Huyo akatuma mtu akamwita
Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa
Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa
Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? Nami
nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na
magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. Baraka
akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi
pamoja nami, mimi siendi. Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini
safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera
katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka
Kedeshi.”
Tito 1:5-9 “Kwa sababu hii nalikuacha
Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama
vile nilivyokuamuru; ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja,
ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii. Maana
imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU;asiwe
mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala
mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu. bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye
kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile
neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa
mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”
Unaona yaani tukinena kiwazimu ni
kuwa ilikuwa ni mapenzi kamili kabisa Mungu kuwatumia wanaume lakini kama
wanaume hawachangamki na wanazubaa, Mungu kwa shingo upande atawatumiwa
wanawake, Debora alikuwa ni nabii mwamuzi, na alipewa ujumbe na Mungu kuwa Baraka
anapaswa kwenda kumpiga Sisera kwani Bwana amemtia mikononi mwake, Lakini
Baraka alikuwa amezubaa na akasema mimi siwezi kwenda bila wewe Debora, Debora
alimueleza wazi kuwa kama nitekwenda nawe basi ujue ya kuwa Mungu atamtia
Sisera komandoo katika mikono ya Mwanamke nawe hutaheshimika yaani itakuwa ni
aibu kwako, Leo hii wanaume wengi wamepoteza mwelekeo, wameshindwa kusimama
katika zamu zao na kuacha maswala ya Imani katika mikono ya kina mama ili hali
Mungu alikuwa anawategemea wawe viongozi, wa kiroho, kijamii na hata kiuchumi,
Bwana ampe neema kila Mwanaume kuchangamka na kumrudia Mungu katika jina la
Yesu Kristo ameen!
Wanaume katika Nyumba wanapewa
nafasi sawa na Nafasi ya Bwana Yesu Efeso
5:22-28 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii
Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha
Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo
vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni
wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili
makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa
tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu
lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili
yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.”
Unaona Nafasi ya Yesu Kristo
katika familia imewekwa kwa mwanaume, Mwanaume ni mwokozi katika familia, ni
kiongozi wa kiroho na ibada hivo ndivyo maandiko yanavyotaka na kuelekeza ndio
protokali (Itifaki) ya kiroho na kama ikiwa tofauti Mungu hawezi kuuunga mkono
uasi katika familia kwa maana ya kuwa kama mwanamke atachukua nafasi ya kichwa
ni wazi kuwa familia hiyo haitakuwa ikiungwa mkono na Mungu, lakini je si
lazima mwanaume asimame katika zamu yake duty ? lazima mwanaume ashike hatamu,
awe mstari wa mbele, Mungu amekufanya kuwa kuhani wa Familia, mwokozi wa
familia, mtunga shetia na mweka utaratibu wa familia sasa endapo hutasimama
katika nafasi yako nakuhakikishia hautuwezi kufurahia uwepo wa Mungu majumbani
mwetu!
Nguvu ya Mwanaume mwenye kumcha Mungu.
Kwa kuwa wanaume wana nafasi
kubwa sana katika moyo wa Mungu, Ni muhimu kufahamu kuwa kama wao wakitoa
kipaumbele katika maswala ya Mungu wanakuwa na nguvu kubwa sana katika jamii na
familia na kusababisha maendeleo makubwa sana katika taifa, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Mwanaume
akimcha Mungu kunakuwa na mafanikio makubwa sana na uzao wake unabarikiwa ona
Zaburi 112:1-4 “Haleluya. Heri mtu yule
amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake. Wazao wake watakuwa hodari
duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa., Nyumbani mwake mna utajiri na
mali, Na haki yake yakaa milele. Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili
na huruma na haki.”
Neno Heri mtu yule amchaye Bwana – katika Biblia ya kiingereza
linatumika Neno Blessed is the man who
fears the Lord, Neno hilo Man kwa
kiibrania linatumika neno IYSH kimatamshi eesh ambalo tafasiri yake ni male Person kwa hiyo hapo anazungumzwa
mwanamume, Heri Mwanaume yule amchaye
Bwana, na andiko liko wazi kuwa mwanaume akimcha Bwana uzao wake unakuwa
hodari duniani, kizazi chake kinabarikiwa, na zaidi ya yote atakuwa na utajiri
na mali, sasa mwanaume anatafuta nini? Unatafuta nini tena kumcha Bwana ndio
deal kumcha bwana kunakufanya mwanaume uwe na mafanikio, siri hii kama wanaume
wangeijua leo, wangehudhuria ibada kuliko wanawake, wanagekuwa mstari wa mbele
kwenye maombi na ibada, na utoaji usingekuwa ishu uchumi usingekuwa ishu kwa
sababu maandiko yanaonyesha kungekuwa na mafanikio makubwa sana Basi wanaume
changamkeni!
Basi wanaume Changamkeni!
Kutokana na wanaume kuwa na
nafasi kubwa sana katika moyo wa Mungu, na kutokana na ukweli kuwa wanaume
wakiwa mstari wa mbele katika kumcha Mungu kunakuwa na Baraka kubwa sana,
wanaume wamekuwa wahanga wakubwa sana wa mashambulizi ya Shetani katika maisha yao,
wanaume ndio wanaoonewa zaidi na shetani,
wanateswa sana na kutokana na ugumu wao wanaumia na kufa kimya kimya,
wanaume hata kibaiolojia wanazaliwa wachache, mbegu ya uzazi wa kiume hufa
mapema kuliko mbegu ya uzazi wa kike, lakini hata maisha ya wanaume yamekuwa ya
taabu sana na wako nyuma wakipambana na
kutafuta riziki huku wakikosa Baraka za kiroho, wanaume wamekuwa kama Esau na
wanawake wamekuwa kama Yakobo katika habari ya Baraka za Mungu
Katika mstari wetu wa Msingi,
tunaowaona wanaume wakiwa katika chombo ambacho kilikumbwa na dhoruba na maandiko yanaeleza kuwa walipigwa katika
chombo kile mpaka wakakata tamaa ya kuishi, chombo hiki kilikuwa kimejaa
wanaume, kilikuwa kina wanaume wacha Mungu akiwepo Paulo Mtume, na Luka
mwandishi wa habari hii, na wengineo, pia kulikuwa na Manahodha wa meli,
walikuwepo askari, na kulikuwa na wafungwa wote walikuwa wanaume, na shehena za
wafanya biashara bila shaka nao walikuwa ni wanaume, na katika wafungwa kulikuwa na
wafungwa waliofungwa kwa sababu ya uhalifu na wengine kwaajili ya injili, kimsingi chombo hiki kinaonyesha wanaume
wakiwa katika safari yao na dunia yao wakiwa wanapigwa na dhuruba, chombo hiki
chenye dhoruba hakionyeshi dalili ya kuweko kwa wanawake, labda wao walikuwa
majumbani salama lakini wanaume hawa ni wahangaikaji kwaajili ya maswala
mbalimbali ya maisha na haya yamepelekea wakawemo katika chombo hiki
wakikumbana na upepo wa hatari, mawimbi na dhuruba, giza na kupoteza matumaini
ya kuishi!
Matendo 27:6-10 “Na huko yule akida akakuta
merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo.
Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na
kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili
Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari
Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha
kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa
zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari
hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na
ya maisha yetu pia.”
Paulo akawaambia WANAUME naona
kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na
merikebu tu ila na maisha yetu pia, ilikuwa ni safari ya wanaume iliyojawa na
taabu na masumbufu ya kila namna, na wanaume hawa wako hatarini, hatarini
kupata hasara, hatarini kukumbwa na dhuruba, hatarini kupoteza mali na hatarini
kupoteza kila kitu, hii ilikuwa ni safari ya kawaida ya kimisionari kwa Paulo
mtume, ya kiserikali kwa askari, ya kiserikali kwa wafungwa na ya kibiashara
kwa wafanya biashara lakini wote wako hatarini na wote wanakabiliwa na kupoteza
maisha hali ilikuwa ngumu, njaa
iliwapiga, baridi iliwapiga, kila mmoja alinyamaza kimya na ukweli hata kina
Luka na wengineo wote walikata tamaa, hakuna mtu alikula kitu kwa siku 14 wala
aliyeongea kitu!
Matendo 27:15-20 “merikebu iliposhikwa, na
kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na tukipita upesi karibu
na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida.
Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba
chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua
matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile
tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu
wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota
hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata
tamaa ya kuokoka.”
Wanaume hawa walikata tamaa,
walikuwa katika hali mbaya, chombo kimewapiga, upepo umewabishia hawajui
kuogelea wengine, wamepoteza mwelekeo dhuruba inawapeleka kule wanakotaka
wamepoteza mwelekeo wamekata tamaa ya kuokoka, mizigo imepotea, meli
imewavunjikia, kama ni ndoto za kibiashara na kupata faida zimetupiliwa mbali,
kila kitu kimepoteza umuhimu, hutarajii tena kufika Rumi, wala kuiona familia
yako tena, kazi haina maana, ndoto zimekufa umezingirwa na dhoruba hii ndio
hali ya wanaume hawaoni hata chembe ya matumaini ni giza na nuru haiko tena,
matumaini yamekwenda manahodha wamepoteza tumaini, watu wameshusha nanga, na
wanasubiri kifo tu, na katika mkusubiria kifo hata akida alikuwa anawaza kuwaua
wafungwa
Ni Katika mazingira kama hayo
Ndipo Mungu akasema na Paulo mtume kuwakumbusha wanaume kwamba wanapaswa
kuchangamka, uhai wao uko mikononi mwa Mungu aliyeziumba mbingu na nchi na
bahari Ni Mungu yule asiyebadilika, wakati ukutikiswa na mazingira ya aina
yoyote katikati ya giza nene na lenye kukatyisha tamaa na kupoteza tumaini yeye
yuko, Ni Mungu siyeshindwa anaweza asizuie dhuruba lakini hawezi kukuacha
uharibiwe!
Matendo 27:21-25 “Na walipokuwa wamekaa
wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema,
Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata
madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana
hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana
usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye
nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi
kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri
pamoja nawe.Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba
yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”
Yalikuwa ni maneno ya kutia moyo
sana kutoka kwa mtumishi wa Mungu Paulo katika wakati ule na hata leo Bado
Mungu anazungumza na wanaume hawako baharini kama hawa, lakini wako kwenye
mashua zao zenye dhouruba mbalimbali na bahari zao zenye majanga mbalimbali, wengine
wakiwa manahodha wa vyombo vyao na
wanachokiona ni giza tu, wanaume
wamepoteza matumaini lakini leo uko ujumbe kwaajili ya wanaume Bwana amenituma
nikuambie leo, Haijalishi unapitia hali gani, haijalishi umepoteza nini,
umepoteza mizigo, umepoteza kazi, umepata hasara kwenye biashara yako, uko
gerezani, ni mfungwa, ni askari, ni mtumishi wa Mungu, umetia nganga, huelewi
hali itakuwaje ni majanga kwenye ndoa yako, umepoteza mwelekeo katika maisha, umelowa,
unasubiri kufa? Umepigika kisawasawa, huoni hata nyota ya matumaini, giza
limekuzunguka pande zote, unasubiria kifo kikukute hapo hapo ulipo? Changamka,
nasema changamka nasema Basi wanaume changamkeni. Basi wanaume changamkeni, Basi wanaume changamkeni, Mungu yule ambaye
mimi ni wake naye ndiye nimuabuduye amesema msiogope, Ni Mungu aliye karibu ni
Mungu ambaye amenihakikishia kuwa utafika, amenihakikishaia kuwa mko salama
mkononi mwangu, Mungu huyu ni mwaminifu haijalishi unapita katika hali gani
lakini yeye anasema changamkeni, Changamka kwa sababu unayoyahangaikia
utayapata ukimpata Mungu kwanza, Mungu anataka makanisa yajae wanaume, waombaji
wawe wanaume, lunch hour service (ibada za mchana maeneo ya karibu na kazini
yajae wanaume Mungu anataka kukubariki, usikubali Heshima yako ikaenda kwa
mwanamke changamka leo changamka kokote uliko huu ni ujumbe maalumu kwaajili
yako Bwana amekuona nasema changamka wanaume changamkeni tusiogope dhuruba za
aina yeyote kwani Mungu wetu habadiliki ahadi zake ni ndio na kweli, neno lake
limahakikishwa Bwana amekekukusudia mema
naam na naamini ndivyo itakavyokuwa
Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio
na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa
ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake
yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”
Wanaume changamkeni Bwana
amenituma kuwakumbusha kusimama katika nafasi yenu, mko katika moyo wake
mgeukieni yeye yuko tayari kuwabariki, yuko tayari kutoa msaada tele katika
maisha yenu na taabu zenu, hamtaogopa
dhuruba mkiwa na yeye Basi wanaume changamkeni, nasema basi wanaume
changamkeni, nasema basi wanaume changamkeni haleluyaaaaaaaa!
Na. Rev Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni