Ufunuo
1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake
kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope,
Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na
tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”
Utangulizi:
Leo ni sikukuu ya Pasaka, ambapo
wakristo nchini wanaungana na wakristo wote duniani kuadhimisha kuteswa, kufa
na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kulikotokea zaidi ya miaka 2000
iliyopita Huko Yerusalem Nchini Israel, Katika wakati huu wa Pasaka Leo ni
Muhimu kujikumbusha kuwa Mungu ametupa maisha
yasiyozuilika, Kristo Yesu alipofufuka ametufundisha na kutukumbusha kuwa kuna maisha yasiyozuilika, Yesu
anatufundisha kupitia kufufuka kwake kuwa yako maisha yasiyozuilika, na kuwa uko uwezekano wa kuishi maisha yasiyozuilika,
Haya ni maisha ambayo Mungu alikusudia kila mmoja ayaishi katika ulimwengu huu
ambao una vikwazo vingi sana, Lakini kama mtu akiwa na Yesu ataweza kuishi
maisha yasiyoweza kuziilika! Maisha
yasiyozuilika ni maisha ya kushinda vikwazo:-
1Yohana
5:11-13 “Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu
alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye
Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia
ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina
la Mwana wa Mungu.”
Unaweza kujiuliza kuwa Mchungaji
anataka kuzungumzia nini? Je maisha yasiyozuilika nini Ni uzima wa milele? Ama
ni kitu gani na kwa vipi maisha hayo yana uhusiano na Yesu aliyefufuka? Tutachukua muda kujifunza kwa ufupi na kwa
kina ili tuweze kuelewa maisha hayo yasiyozuilika kwa kuzingatia vipengele viwili
tu vifuatavyo:-
·
Maana ya
maisha yasiyozuilika
·
Maisha
yasiyozuilika
Maana
ya Maisha yasiyozuilika!
Tunapozungumzia kuhusu Maisha
yasiyozuilika, tunazungumzia kuwa na maisha yasiyo na mipaka, au maisha
yanayoshinda vikwazo, maisha ya uhuru na na yaliyojaa neema ya Mungu inayotusaidia
kufikia ndoto zetu huku tukishinda kila aina ya kikwazo kinachowekwa na shetani
au wanadamu, Maisha yanayoweza kuwa na
ushindi, bila kujali nguvu kutoka nje inasema nini, Unapoyasoma maandiko
yanaonyesha wazi kuwa Mpango wa Mungu kwa mwanadamu tangu mwanzo ilikuwa ni
aina hii ya maisha na Yesu aliyefufuka anatukumbusha kupitia hatua yake ya
kufufuka kuwa yako maisha yasiyozuilika!, Mapena na mara kadhaa Yesu alikuwa
amesema atafufuka na alisema kuwa
atafufuka siku ya tatu na mpango huu Yesu alitaka ueleweke wazi kwa wanafunzi
wake na hata kwa adui zake na ndio maana alirudia tena na tena maneno yake hayo
ona:-
-
Mathayo
16:21-23 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya
wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa
wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.
Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.
Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana
huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
-
Marko
8:31-32a “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa
Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa
makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa
akinena neno hilo waziwazi.”
-
Luka
9:21-22 “Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu
neno hilo; akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa
na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”
-
Mathayo
17:22-23 “Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu
akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao
watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana.”
-
Marko
9:30-32 “Wakatoka huko, wakapita katikati ya
Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi
wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao
watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini
hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. “
-
Luka
9:43-45 “Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu.
Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi
wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda
kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao
wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.”
Kwa hiyo huu ulikuwa ni mpango wa
Mungu, Na Bwana Yesu aliusema mapema kwamba kifo hakiwezi kumzuia, hakuna kitu
kinaweza kuzuia mpango wake wa kufufuka kutoka kwa wafu, huu ndio ulikuwa
ujumbe mkuu wa Yesu, Lakini katika namna ya kushangaza shetani pamoja na
majeshi yake yote walikuwa na mpango wao wa kuzuia ili yamkini ikiwezekana Yesu
asifufuke ona
Mathayo
27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya
Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema,
Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya
siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya
tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika
wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna
askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi
salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”
Unaona njama zilipangwa na viongozi wa
kidini wakishirikiana na serikali ya kirumi kuhakikisha kaburi la Yesu
linalindwa salama, Kulindwa salama maana yake ni kulinda kwa uhakika,
kuhakikisha kuwa hakuna linalobatilika, lindeni kwa kukakisha kuwa haibiwi,
lindeni kwa kuhakikisha kuwa hafufuki!
Kwa hiyo wayahudi walitaka kuhakikisha Yesu anabaki kaburini na hatoki
tena na hachomoki kabisa kutoka katiia mpango wake huo, walimuwekea ulinzi
waliweka mipaka, waliweka kizuizi, walitaka kuakikisha kuwa hakubadiliki neno,
Hata hivyo hawakujua kuwa Yesu aliishi maisha yasiyozuilika na hakuna kitu
ambacho kingeweza kumzuia asitoke kaburini, hata kifo hakiwezi kumzuia na
kumfanya abaki kaburini, Kristo alikuwa na maisha yasiyozuilika, na kifo
kisingeliweza kumzuia hakuna cha kumzuia Yesu katika mpango wake.
Maisha
yasiyozuilika
Mathayo
28:1-7 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku
ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda
kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu
malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe
akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.
Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu,
akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta
Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni,
mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake,
Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona.
Haya, nimekwisha waambia.”
Yesu alisema atafufuka, na wapinzani
wake walitaka kuhakikisha kuwa Yesu hafufuki, waliweka walinzi katika kaburi
lake, waliweka muhuri kuhakikisha kuwa hakuna neno linalobatilika lakini
Yesu/Mungu akisema neno lake hakuna mtu anaweza kusimama kinyume na makusudi na
mpango wa Mungu, Yesu alikuwa akituonyesha wazi kuwa tunaweza kuishi maisha
yasiyozuilika, kila anaemwamini Yesu na kuiamini kazi aliyoifanya pale msalabani,
atakuwa na maisha yasiyozuilika, sio kifo tu lakini kila kitu kinachojaribu
kusimama kinyume na kile unachokusudia kukifanya, au biashara zako, au ndoa
yako, au mafanikio yako, au kazi yako, au vyovyote vile, unapaswa kukumbuka
kuwa Yesu anatuonyesha njia kuwa hakuna anayeweza kukuwekea mipaka katika
maisha yako, Kristo aliyefufuka ni mfano mzuri wa maisha yasiozuilika, tangu
mwanzo Mungu alikusudia kuwa watu wake wawe mashahidi wa kazi zake na wakati
wote kazi zake na mpango wake hakuna anayeweza kuzuia
Isaya
43:12-13 “Nimetangaza habari, nimeokoa,
nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni
mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi
ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye
ni nani awezaye kuizuia? ”
Kufufuka kwa Yesu Kristo ndio ulikuwa
ushindi mkubwa sana dhidi ya shetani maajenti wake na kazi zake zote, na
ilikuwa ndio kilele cha utekelezaji wa kazi ya ukombozi wa Mwanadamu, kwa hiyo
shetani alikuwa anataka kuzuia na kuiwekea mipaka kazi iliyofanywa na Bwana,
wakati wote unapokaribia katika mafanikio yako, au inapokaribia kuwa Mungu
anataka kubadilisa kabisa mpango wa maisha yako na kukuinua, Kuzimu inataharuki
na itahakikisha inapambana na kuzuia
mpango wa Mungu katika maisha yako, wakati huo shetani anasahau kuwa
Yesu amekupa maisha yasiyozuilika, Kila mtu aliyeokolewa yuko upande wa Mungu
yuko na Bwana na Mungu ametupa maisha yasiyizuilika, Kama hakuna kitu cha
kututenga na Upendo wa Mungu ni wazi vilevile kuwa hakuna kitu kitaweza
kutuzuia katika jambo lolote lile zingatia kuwa Yesu aliyefufuka anaza mamlaka
za mauti na kuzimu na zaidi ya yote yeye ndiye huo ufufuo na uzima sasa jaribu
kuwaza na kifikiri nini kinaweza kuzuia maisha yako ? angalia maandiko:-
Warumi
8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu
akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake
mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo
yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye
kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa;
naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa
Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je!
Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama
ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa
kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na
zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya
kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala
yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo
chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu
ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Unaona maandiko yanaonyesha ukimuamini
Yesu unapewa maisha yasiyozuilika na hakuna cha kutuzuia, hakuna wa
kutushitaki, maana wako watu watatafuta mambo ya kukushitaki, walimshitaki Yesu
mbona! tena kwa ushahidi wa uongo, watatafuta kukudhihaki, watakufanyia kila
kitu kibaya ili yamkini ikiwezekana ukate tamaa, wanaweza kutuhukumu, wanaweza
kutupangia aina ya adhabu, wanaweza kutupangia aina ya hukumu, wanaweza
kukadiria aina ya maisha yetu, wanaweza kujifanya wana hatima ya maisha yetu
kwa vyovyote vile lakini kumbuka kuwa
hawajafa kwaajili yetu, Yesu ndiye
aliyekufa na zaidi ya hayo amefufuka katika wafu, na yuko mkono wa kuume
anatuombea, maombi ya Yesu kwaajili yako na yangu hayawezi kukataliwa, yuko
mkono wa kuume wa baba kwa sababu hiyo kumbe kufufuka kwake kuna umuhimu mkubwa
sana kwa sababu kunatupa maisha yasiyozuilika, kila anayepambana na kusudi la
Mungu ndani yako anapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa sababu huenda anataka
vita na Mungu, na akipigana na Mungu atajikuta yuko kwenye madhara makubwa kwa
sababu tumepewa maisha yasiyozuilika, Wayahudi sio tu walitaka kuzia Yesu
asifufuke lakini pia walitaka kuizua kazi yake mtu mmoja mwenye hekima
akawaonya wayahudi kuwa waache kupambana na kazi za Yesu, kama walimsindwa Yeye
waachie kazi yake ona
Matendo
5:33-39 “Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao;
wakafanya shauri kuwaua. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli,
mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza,
akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli,
jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi
aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne
wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si
kitu.Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa
orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote
waliomsadiki wakatawanyika.Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa,
waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu,
itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana
kuwa mnapigana na Mungu.”
Pasaka hii ni onyo dhidi ya watu wote
wanaokusudia na waliokusudia kushindana na mapenzi ya Mungu, kwa kanisa, kwa
watumishi wake, na kwa maisha yako kwamba wajihadhari waache kushughulika na
watu wenye maisha yasiyozuilika, mtu aliyeokolewa na kumuamini Bwaa Yesu kuwa
bwana na mwokozi wa maisha yake hakuna cha kumzuia hata ukimuua, anapita tu kutoka
mautini na kuingia uzimani,
Yohana
5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”
Hakuna raha kama kuishi maisha
yasiyozuilika maana kuna faida nyingi sana, na hatuwezi kuzimaliza zote lakini
lakini zote hizi tunapewa kwa sababu Mungu alitaka tuwe na maisha yasiyozuilika
-
Watashindana nawe na hawatakushinda – Yeremia 1:18-19 “Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma,
na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu
wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe;
lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”
-
Kila silaha itakayofanyika juu yako
haitafanikiwa – Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila
ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi
wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
-
Hakuna uchawi wala uganga utakuweza – Hesabu 23:23 “Mungu
amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana
uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo
na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! ”
-
Adui atakuja kwa njia moja atatawanyika kwa
njia saba - Kumbukumbu 28:7 “Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa
mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia
saba.”
Ndugu yangu unapoadhimisha
sikukuu ya pasaka leo, Nakuombea kwa Mungu, na ni maombi yangu kuwa kila mmoja
wetu aweze kuishi maisha yasiyozuilika, Yesu Kristo aliyefufuka ana mamlaka ya
kuzimu na mauti, hivyo kila amuaminiye maana yake hakuna mtu anakuweza, sio
mauti sio kuzimu, wala lolote linaweza kuyafanya maisha yako yakawa na kizuizi,
Alipomwambia Yohana asiogope anakuambia na wewe na mimi tusiogope
Ufunuo
1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake
kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope,
Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na
tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”
Pasaka hii Mungu akuondolee
vikwazo vya kila aina katika maisha yako na vile utakavyokutana navyo Mungu
akupe kuvishinda, Mimi nilikutana na vikwazo vingi na vizuizi vyingi sana
katika maisha yangu, huduma na utumishi, lakini hakuna hata kimoja kiliweza
kuyazuia maisha yasiyozuilika Bwana anaweza hata kuandaa meza Machoni pa watesi
wako na kukupaka mafuta mpaka kikombe chako kikafurika, Ubarikiwe na usihi
maisha yasiyozuilika, kukiwa na maji tembea juu ya maji, wakitaka kukukamata
pita katikati yao wende zako, wakikutupa katika makanwa ya simba hutatafunwa,
wakikutupa katika tanuru la moto hutatekeketa, bahari ikiwa kikwazo bwana
atafanya njia, kila iana ya dhiki na mateso na majaribu utayapitia lakini,
utatoboa, wakikuzika na kulilinda kaburi ili usifufuke tetemeko na malaika wa
bwana atawafanya aduinzako wawe kama wafu nawe utatoka. Kwa nini kwa sababu
Yesu ametukirimia Maisha yasiyozuilika, na kwa jina lake kila kikwazo
kinachisimama mbele yako kitabomolewa na kusawazishwa katika jina la Yesu.
Nakutakia msimu mzuri wa sikukuu ya Pasaka Mungu akutunze!
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni