Mathayo 21:1-11 “Hata walipokaribia
Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma
wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na
mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee.
Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo
atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii,
akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye
amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao,
wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda,
wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano
wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza
njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti,
wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la
Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki,
watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa
Nazareti ya Galilaya.”
Utangulizi:
Leo 24/3/2024 ni jumapili ambayo
katika makanisa ya Mengi, utaweza kuona watu wakubwa kwa wadogo wakiwa na
matawi ya mitende mikononi mwao, wengine wakifanya maandamano kuanzia nje ya
kanisa na kuingia nayo ndani, wote wakiadhimisha siku ya kuingia kwa Bwana wetu
Yesu Kristo kwa Shangwe katika jiji la Yerusalem, wengine wakiwa wanajua maana
yake na wengine hata hawajui lakini wanafuata tu utaratibu wa kidini,
inawezekana hawajaambiwa, wala haajafundishwa, lakini sasa wakati wa kutokuambiwa
umeisha kila kitu sasa ni wakati wake kuwekwa wazi ili watu waweze kuelewa,
haikuwa tu siku ya kuingia Yerusalem kwa shangwe, wala siku ya kusheherekea
sikukuu ya mitende, lakini kinabii ilikuwa ni ushindi dhidi ya Ukoloni! wa
kiroho ni siku ya Kusimikwa kwa mfalme
mkuu sana mwenye uwezo wa kuwasaidia watu kutoka katika kila aina ya utumwa na
ukandamizaji wa kimwili na kiroho uliowachosha kwa muda mrefu angalia:-
Ufunuo 7:9-10 “Baada ya hayo nikaona, na
tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila
taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi,
na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende
mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye
katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.”
Ni neema kubwa sana kuwa Makanisa
ya mengi hasa ya kizamani, wametunza tukio hili la Muhimu aidha kwa kujua au
kwa kutokujua lakini wanapoadhimisha wanaadhimisha mojawapo ya tukio la msingi
sana katika nabii zinazohusiana na Masihi na kazi aliyoifanya Kwa dunia na ile
atakayoifanya na kuitimiza baadaye, hata kama unaweza usikate matawi ya
mitende, lakini unaweza kufanya ibada ya kusifu na kuabudu ukimuadhimisha
Masihi kwa kazi yake njema aliyoifanya pale Msalabani! Au pia unaweza kuitioa
wakfu jumapili hii kwa kuhubiri ujumbe kuhusu kuingia Kwa Yesu jijini Yerusalem
kwa shangwe, kwa hiyo sio makanisa ya zamani peke yao Lakini hata makanisa ya
uamsho wa kipentekoste na Karismatiki wote tunasheherekea siku hii, lakini kila
mmoja kwa namna yake!, Kimsingi katika maandiko jumapili ya mitende ina maana pana
sana kuliko tunavyoweza kufikiri juu juu:-
·
Ilikuwa
siku ya kutimizwa kwa unabii
·
Ishara ya
matawi ya mitende
·
Hosana
Mwana wa Daudi (Jumapili ya mitende)
Ilikuwa siku ya kutimizwa kwa unabii
Tendo la Yesu Kristo kushangiliwa
na kuingia Yerusalem kwa Shangwe halikuwa tu tukio la bahati mbaya, lilikuja
kutimiza unabii ulionenwa na nabii Zekaria
na bila kuelewa jamii kubwa ya wayahudi waliokuwa wanasogea Yerusalemu
majira ya sikukuu, walimshangilia Bwana Yesu kwa nguvu zao zote ilikuwa ni siku
ya kilele cha Huduma ya Yesu Kristo kwa watu walichoka kuwa watumwa wa ukoloni
wa Kirumi, kimwili na utumwa wa shetani kiroho, wenye shauku na utawala wa
Kisayuni uliokuwa unatarajiwa kuletwa na Mwana wa Daudi, mara kadhaa walikuwa
wametaka kumfanya awe mfalme lakini yeye mwenyewe alikataa, lakini wakati huu
walikuwa wamemkubali na kumsimika kuwa mfalme bila kufanya mapinduzi yoyote,
ilikuwa ni siku ngumu kwa maadui wa Kristo, ilikuwa sio siku rahisi kupinga
wala kunyamazisha watu wasimtukuze Kristo kwa kuwa jamii yote ilikuwa
imemkubali.
Yohana 6:15-22 “Kisha Yesu, hali akitambua
ya kuwa walitaka kuja kumshika ili WAMFANYE MFALME, akajitenga, akaenda tena
mlimani yeye peke yake. Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini
wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha
kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo
mkuu.Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda
juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi,
msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia
nchi waliyokuwa wakiiendea. Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng'ambo ya
bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu
hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake
walikwenda peke yao.”
Zekaria 9:9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni;
Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, MFALME wako anakuja kwako; Ni mwenye
haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto
wa punda.”
Kifungu cha kwanza kinaonyesha
Yesu akikataa kwa sababu watu walitaka kumfanya kuwa mfalme kwa manufaa yao,
walitaka kumfanya mfalme aliyetukuzwa, mwenye nguvu dhidi ya serikali ya
kirumi, mwenye kuwalisha mikate, mfalme mwenye kutenda miujiza, mfalme ambaye
ukiwa naye huhitaji hata kufanya kazi ngumu, anakulisha mikate, anafanikisha,
anabariki kila ulicho nazo kinazidi, samaki wanazidi, mikate inazidi, faida
zinazidi, biashara zinafanikiwa, na zaidi ya yote warumi na serikali yao
itaondolewa, lakini Yesu ni mfalme lakini kwa wakati ule hakuwa mfalme
aliyetukuzwa, alikuwa mfalme mnyenyekevu ambaye kwanza angepigana vita ya
rohoni na kuwakomboa na utumwa mmbaya zaidi wa shetani kuliko utumwa wa
kikoloni wa warumi, Hivyo hangepanda farasi, angepanda punda kama alivyo tabiri
nabii, Kupanda Punda ilikuwa ni ishara
ya ufalme duni, ufalme wa kinyenyekevu, ufalme usiohusu kujikweza, tena sio ufalme wa kimapinduzi, bali ufalme wa
kujishusha, ufalme usiotokana na vita bali wa Amani.
Kwa hiyo kifungu hiki cha pili, unabii
wa nabii Zekaria unatimizwa kwa sababu kubwa zaidi aalitabiri siku hii ambayo
masihi ndiye mfalme aliyeingia kwa Amani, kwa kutumia Punda, ilikuwa ni sihara
ya unyenyekevu na Amani na anatajwa mfalme huyu kuwa anakuja na zawadi ya
wokovu, si kwa fahari ya kifalme bali kwa unyenyekevu alikuwa tayari kuukabili
Msalaba apate kuwakomboa wanadamu, Huu ni ushindi mkubwa zaidi kuliko aina
nyingine yoyote ya ushindi na Hivyo Sayuni ilipaswa kupiga kelele, kwani Kristo
huyu atakuja tena si kwa unyenyekevu huu na kukubali kufa msalabani bali kwa
nia ya kusimamisha utawala wake wa miaka
1000 duniani ambapo kila mtu atafurahia na zaidi sana katika utawala wake na
siku yake ya kusimikwa rasmi katika kiti cha enzi.
Kwa hiyo siku hii ya matawi ya
mitende ilikuwa ni siku ya ushindi na kusimikwa kwa mtawala na mwokozi wa roho
zetu zaidi kabla ya ukombozi wa mwili siasa na uchumi utakaofuata katika
utawala wake, japo matumaini makubwa ya Israel yalikuwa ni katika ufalme wenye
kuonekana, Lakini Mwokozi alikuwa analeta kwanza zawadi ya wokovu wa roho zetu,
na msamaha wa dhambi, na kuuvunja utawala wa shetani na kuharibu kiburi cha
wanadamu!
Matendo 1:6-8 “Basi walipokutanika,
wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli
ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka
katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu
Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Ishara ya matawi ya mitende
Mathayo 21:1-11 “Hata walipokaribia
Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma
wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na
mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee.
Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo
atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii,
akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye
amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao,
wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda,
wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano
wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza
njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti,
wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la
Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki,
watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa
Nazareti ya Galilaya.”
Katika siku hii ya kutimizwa kwa
unabii wa Zekaria, Yesu aliingia Yerusalem kwa shangwe huku kukiwa na matukio
makubwa mawili, ukiacha swala la kupanda Punda watu walichukua matawi ya
mitende na kutoa mavazi yao na
kuyatandaza njiani, lakini kubwa zaidi kupaza sauti zao wakisema Hosanna mwana
wa Daudi.
Kwanini Matawi ya mitende? Ni
kweli kijiografia Israel ni moja ya nchi zenye miti jamii ya mitende ambayo
inasitawi sana katika inchi zote za
mashariki ya kati, kwa hiyo mitende ni moja ya miti iliyokuwako kwa wingi, hata
hivyo ni muhimu kujiuliza kwa nini walichukua matawi ya mitende na sio miti
Mingine? Mitende hii ilikuwa ni ishara Mtende una maana kubwa ya muhimu kiroho,
kwa hivyo watu hawakuchuma tu kwa sababu ni miti iliyokuwepo, kwani iko pia
miti ya mizeituni, mizabibu, tini na kadhalika lakini mti huu ulikuwa na maana
kubwa ya kiroho Mti huu ulikuwa ni alama ya
USHINDI Mti wa mtende ni mti wenye kuvutia sana nyakati za zamani sana
Wagiriki walipokuja kutawala nchi ya Israel waliilita nchi hii PHOENICIA wakimaanisha nchi ya mitende, Mti huu ni alama ya
ustawi, ushindi na Baraka Mtende unastawi hata janwani, ni mti wa ushindi,
unashinda ukame, unaonyesha ukijani bila kujali majira na nyakati na unazaa
matunda wala hauchoki, Kwa hiyo mti huu ulikuwa ni ishara ya kushinda na
kuvumilia magumu!
Zaburi 92:12-14 “Mwenye haki atasitawi kama
mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana
Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.”
Wayahudi walikuwa na kiu ya
ushindi, walikuwa wamechoshwa na utumwa wa Kirumi, na walikuwa wanataka Mwokozi
na mpakwa mafuta kutoka ukoo wa Daudi awarudishie ufalme walioamini kuwa ni
ufalme wa Mungu, ilikuwa ni machukizo sana kwao kutawaliwa na watu
wasiotahiriwa, ilikuwa ni unajisi kuwa hawako huru kutoka katika inchi yao, ilikuwa ni maumivu kuwa hawana mfalme wao wala
manabii wanaoweza kurudisha uhusiano wa kiungu na taifa lao kwa hiyo walimuona
Yesu kuwa mtu maarufu na walijua kuwa ni wa ukoo wa Daudi na waliona ndiye
anafaa kuwa kiongozi wao wa kiroho na kisiasa kama alivyokuwa Daudi, na
walimjua kuwa alikuwa mwana wa Daudi kwa hiyo walikuwa wanataka Yesu awashindie,
walikuwa wanatamani kutolewa katika utumwa ule, hivyo mtende ulikuwa ni alama
ya Ushindi, kile ambacho Yesu anakwenda kukifanya katika mji ule mkuu ni kuleta
ushindi.
Jambo la Pili wimbo waliouimba HOSANNA mwana wa Daudi Ndiye mbarikiwa
ajae kwa jina la Bwana, Hosana juu mbinguni, huu ulikuwa ni wimbo ambao
umeandaliwa kwaajili ya Masihi, siku ile kila mmoja alikubali na kumtambua Yesu
kuwa Ndiye masihi, waliamini pia kuwa amekubalika Duniani na mbinguni na
wakaimba Hosana. Neno Hosana ni neno linalotokana na Neno la kiibrania ambalo
ni la kumsifu Mfalme na la kutaka mfalme afanye kazi yake ya kuokoa, neno hili
linaweza kutamkwa kwa Mungu na kwa masihi wake tu, TAFADHALI TUOKOE ni kilio
cha ukombozi cha kumtaka mfalme aokoe na Mungu aingilie kati kupitia mfalme
awaletee watu wake wokovu, Kwa hiyo Hosana mwana wa Daudi, ni Maombi maalumu ya
kumsihi TAFADHALI TUOKOE EE MWANA WA
DAUDI, WEWE UMEBARIKIWA NA HOSANA JUU MBINGUNI, Yalikuwa ni maombi ya Kumuomba Mungu aokoe kupitia
mpakwa mafuwa wake na kwa kweli Ndicho ambacho Yesu alikuwa anakwenda kukifanya
katika juma lile lakini haikuwa kisiasa.
Hosana Mwana wa Daudi (Jumapili ya mitende)
Kwa hiyo tunapoadhimisha siku ya
Jumapili ya Mitende, haijalishi inaadhimishwaje, yako makanisa wanaadamana huku
wakiwa na matawi ya mitende wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu, wanaweza
kufanya maandamano hayo ndani au nje ya kanisa, Matawi ya mitende yakiwakilisha
mti ule uliotumiwa na wayahudi kumtukuza Mungu na kumuadhimisha Kristo
alipokuwa akiingia Yerusalem, wengine wakibariki matawi hayo ya mitende na
kufanya ibada maalumu jumapili ya mwisho kabla ya jumapili ya pasaka, na kusoma maandiko yanayohusiana na siku
hiyo, na tamaduni mbali mbali kila
kanisa linaweza kufanya ibada ya jumapili ya mitende vile wanavyoo nan a kupendekeza
Hata hivyo siku hii ni siku ya
ushindi, tunaanza kuadhimisha na kusheherekea Kuanza kwa ufalme wa Mungu, Yesu
aliingia Yerusalemu akiwa amebeba wokovu, alikuwa yuko tayari kuyakabili mateso
ya msalaba na kuyatoa maisha yeke kuwa dhabihu kwaajili ya wengi. Siku zote
katika huduma ya masihi hakuna mahali palikuwa pa hatari kama Yerusalem, hii
ilieleweka wazi hata kwa wanafunzi wake, njama zote na mipango yote ya kumuua
mwanaume huyu aliyepata umaarufu mkubwa nchini Israel ilikuwa ikisukwa
Yerusalem angalia :-
Yohana 11:7-8, 16 “Kisha, baada ya hayo,
akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. Wale wanafunzi wakamwambia,
Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe
unakwenda huko tena?, Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe,
Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.”
Hata hivyo Kristo kwa nini
anakubali kwenda katika eneo hatarishi la maisha yake? Yesu alikuwa anajua wazi
kuwa ndipo mahali anapopaswa kufia na wakati wake ulikuwa umefika na alijua
kuwa haimpasi kufia nje ya Yerusalem, kwa hiyo siku hii Yesu aliingia Yerusalem
kwa ujasiri mwingi, akikubali kutukuzwa na watu wote ni siku ambayo kama
kuhatarisha maisha yake aliyahatarisha zaidi, lakini hakuwa na hofu yeye alikua
anajua anachokwenda kukifanya.
Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha
wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu
Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo
na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na
hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa
haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”
Kristo alikuwa amepanga aende
Yerusalem licha ya kuwa kulikuwa na vitisho vya kuuawa kwake, siku hii
alikaribishwa kwa furaha na kwa matarajio makubwa sana, wayahudi walikuwa
wamemkubali kama mfalme, walikuwa wako tayari awaokoe, ilikuwa ni kilele cha
huduma yake kubwa ya ukombozi, Japo Israel walifikiri, atawakomboa dhidi ya
ukoloni wakiwarumi lakini ilikuwa ni siku ya ukombozi kwa ulimwengu wote,
ilikuwa ni siku ya ushindi kwa wote wanaomtazamia kwa wokovu!
Kwa hiyo ni jumapili ya maombi,
ni jumapili ya kusifu, ni jumapili ya kumkubali Yesu, ni jumapili ya kukubali
utawala wa masihi katika mioyo yetu, ni jumapili ya kumwambia bwana okoa kila
eneo la maisha yetu, ni jumapili ya kufutiwa huzuni zetu, ni siku ya kutarajia
ushindi na wokovu katika kila Nyanja ya maisha yetu, ni jumapili ya kumuomba
Masihi mwana wa Daudi aingilie kati maisha yetu, kwa hiyo tunapoadhimisha leo
Jumapili ya mitende, acha kufikiri kuhusu mitende fikiri kuhusu ushindi katika
kila eneo la maisha yako, kama kuna eneo
ulishindwa leo ni siku ya kuomba ukombozi katika maisha yako, kama ulikuwa
unatawaliwa na unaonewa na kukandamizwa ni siku ya kuwaambia wakoloni wa kipepo
kuondoka, ni siku ya kuvunja mikataba na shetani, ni siku ya kumaliza maadui na kuitangaza Amani, kwa kuwa mfalme anakuja,
ni siku ya Amani na furaha ujumbe mkubwa unaobebwa na Mfalme huyu ni Amani,
tabia inayobebwa na Mfalme huyu ni unyenyekevu, tunda linalobebwa na mfalme
huyu ni upole. Na ni hukumu ya namna gani inayobebwa na Mfalme huyu ni haki.
Zekaria 9:9-10 “Furahi sana, Ee binti
Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni
mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam,
mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu,
na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye
atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari
hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.”
Ni siku ambayo Yesu hawezi
kuzuiliwa na kitu chochote, kila kitu ni lazima kimsifu, na kama kuna mtu
atazui siku ile Mawe yangeifanya kazi hiyo, kwa sababu Mbingu nan chi zilikuwa
zimekubali, kwamba ni lazima atimize haki na lazima aokoe hakuna upinzani
unaweza kufaulu siku Yesu anapotukuzwa na kuinuliwa, siku ile Mfarisayo
walitaharuki sana, walipigwa na butwaa mamlaka ya Kristo ilizidi, alikuwa na
nguvu kubwa sana alisifiwa na kutukuzwa kila mahali watu wazima kwa watoto, na
ni siku ambayo hakuna mtu angeweza kuzuia Yesu asitukuzwe!
Luka 19:37-40 “Hata alipokuwa amekaribia
matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi
na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,
wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na
utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia,
Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi,
wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni