Yohana 4:1-10 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu
ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko
Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,)
aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya
Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile
shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha
Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi
kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji.
Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini
kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi
kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani
na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye
ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji
yaliyo hai.”
Utangulizi:
Leo tutachukua muda kujifunza
mojawapo ya masomo ya Msingi sana katika Maisha na mafundisho ya Bwana wetu
Yesu Kristo ili kujifunza jambo moja la msingi sana tunapofanya kazi ya
kuieneza injili, na jambo hili lina uhusiano na kuvunja mipaka ya kijamii,
kiimani, kidini, kisiasa, kiitikadi, kiadui na rangi, na kuhakikisha kuwa
tunasambaza upendo wa Mungu kwa watu wote sawasawa na agizo kuu la Bwana wetu
la kuihubiri injili na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake na kuwabatiza.
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema
nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Katika kujifunza somo hili muhimu
lenye kichwa, Naye alikuwa hana budi
kupita katikati ya Samaria, ambalo kimsingi litazungumzia mazingira mazima
ya mazungumzo ya Yesu na mwanamke Msamaria katika Yohana 4:1-42 pamoja na matokeo ya mazungumzo hayo kwa ujumla, tutaligawa somo hili katika vipengele
vitatu muhimu:-
·
Uhusiano
wa Wayahudi na Wasamaria.
·
Naye
alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.
·
Matokeo
ya kupita kwa Yesu pale Samaria
Uhusiano wa Wayahudi na Wasamaria.
Ni muhimu kuwa na ufahamu, kwamba
moja ya safari Muhimu sana ambayo ina maswala mengi sana ya kutufunza ni pamoja
na safari hii ya Yesu Kristo kupita katika jimbo la Samaria, Kimsingi katika
wakati huu Yesu alikuwa amejipatia umaarufu mkubwa sana kuliko Yohana
Mbatizaji, Na mafarisayo walianza kuchukizwa na Yesu kwa sababu walianza
kupoteza umaarufu wao na mamlaka yao, na
hivyo hawakuwa na furaha sana na uwepo wa Yesu, kwa hivyo Yesu alilazimika
kuondoka kwaajili ya kuepusha migogoro na mafarisayo ambao kimsingi walishaanza
kutafuta namna na njama za kutaka kumuangamiza,kabla ya muda wake halisi wa
kusulubiwa.
Yohana 4:1-3 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu
ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko
Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,)
aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.”
Yesu alikuwa amekwishakuwa
maarufu pande zote Uyahudi na Galilaya na jamii kubwa ya watu walikuwa
wakimfuata kila aliko, kwa hiyo ili kupata nafasi ya kupumua aliazimia kupita
Samaria (Alikuwa hana budi maana yake
ilikuwa lazima) Biblia ya kiingereza inatumia maneno “And he must needs go through Samaria” neno Must
needs katika kiyunani linatumika neno DEI au DEON
kwa kiingereza Necessary yaani
ilikuwa ni muhimu, ilikuwa ni lazima, ilikuwa kuna jambo la msingi la kukutana
nalo, kwa sababu maalumu, ikiwa ni pamoja
na kupunguza kwa kiwango fulani mkakati wa mafarisayo kumuwinda na kutaka
kumwangamiza, lakini kulikuwa na uhitaji wa kiungu.
Marko 3:6-10 “Mara wakatoka wale
Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya
kumwangamiza. Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini.
Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya,
na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia
habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi
wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije
wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia
wapate kumgusa.”
Kwaajili ya hayo Yesu anakusudia
kupita katikati ya Samaria, Samaria lilikuwa mojawapo ya jimbo kati ya majimbo
makubwa matatu katika taifa la Israel, kusini kulikuwa na jimbo la Uyahudi
(Yudea) na Kaskazini kulikuwa na jimbo la Galilaya, na katikati lilikuwepo
jimbo la Samaria, kwa kawaida wayahudi halisi waliishi Yudea na Galilaya na
wale wenye kuishika Imani sana walipotaka kwenda Galilaya au kuja Uyahudi hawakuthubutu
kupita katikati ya Samaria kwani kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kujitia
unajisi, na sababu kubwa ni kuwa kulikuwa na uhasama wa kihistoria kati ya
Wayahudi na Wasamaria, hivyo Wayahudi walipokuwa wakienda Galilaya walilazimika
kupita njia ndeefu kuzunguka nje ya Samaria kuliko kupita kati kati yake yaani
Samaria ambayo kimsingi ilikuwa ndio njia fupi.
Wayahudi na Wasamaria
walichukiana sana na hawakuwa hata na muda wa kuzungumza wao kwa wao, Sababu
kubwa ni kuwa Wasamaria walikuwa ni Wayahudi hapo zamani, Lakini Israel ya
kaskazini ilipovamiwa na Waashuru na watu wengi kuchukuliwa utumwani mwaka wa 722 KK.
Mfalme wa Ashuru aliwaleta wageni wengi sana kuikalia nchi ya Samaria,
na wageni hawa walizaliana na waisrael waliobaki na hivyo kukazaliwa machotara
wa kiyahudi na wageni na kwa sababu hiyo jamii hii ilianza kuabudu miungu na
kujihusisha na tabia za mataifa wasio wayahudi.
2Wafalme 17:23-33 “hata Bwana akawaondoa
Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake
wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe,
waende nchi ya Ashuru, hata leo. Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka
Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya
Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji
yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo
Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia
mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika
miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba
kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.
Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani,
mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa
nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa
katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana. Lakini pamoja na
hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika
nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao
walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa
Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya
Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa
Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha Bwana, nao
wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia
dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha Bwana, na kuitumikia miungu
yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.”
Kitendo cha wasamaria hawa
kumwacha bwana na kuanza kutumikia miungu mingine kilijenga chuki kubwa sana
kati ya wayahudi na wasamaria, lakini hata hivyo mpaka wakati wa Yesu baadhi
walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli, lakini hata hivyo waliabudu katika mlima
Gerizimu na ambapo pia palijengwa hekalu hapo, lakini wayahudi walilibomoa
kabisa na hivyo kuongeza uhasama mkubwa baina yao, kwa hiyo uadui wao ukawa mkubwa, Wayahudi waliwadharau sana
Wasamaria, waliwaona kama watu waliopoteza utakatifu wao kwa kujichanganya na
mataifa mengine, ambao walikuwa washirikina na wachawi na kamwe hawakuwahi
wayahudi kufikiri kuwa Wasamaria wako sahihi, Mlima Gerizimu ni moja kati ya
milima miwili iliyoko nchini Israel katika mji uitwao Nablus leo, lakini zamani
paliitwa Shekemu, Neno Gerizim ni neno la kiarabu kumaanisha Jabal kwa
kiibrania ni Argarizem na mlima mwingine
uliitwa Ebal. Na wasamaria wengi
waliishi chini ya mlima Gerizim, mlima huo ulifikiriwa kuwa mtakatifu.
Yohana 4:20 -23 “Baba zetu waliabudu katika
mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo
kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu
Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi
tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.Lakini saa inakuja,
nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli.
Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”
Uhasama baina ya wayahudi na
wasamaria ukageuka kuwa uhasama wa kiimani, uhasama wa kiitikadi, uhasama wa ki
ubaguzi, uhasama wa kisiasa na hata kijiografia, Wasamaria waliamini vitabu vitano tu vya Musa
na hawakutaka kuamini katika vitabu vingine hivyo walimtambua Musa tu na yule aliyetabiriwa
na Musa tu yaani Masihi na yeye ndiye waliyekuwa wakimsubiria.
Kumbukumbu 18:15 “Bwana, Mungu wako,
atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni
yeye.”
Uhasama wao ulipelekea kuchukiana
kiasi ambacho hata kijiografia ilikuwa ni ngumu sana kwa myahudi wa kawaida
kupita katikati ya Samaria akielekea Galilaya na badala yake walilazimika
kupita njia ndefu ya kuzunguka yaani kuizunguka Samaria badala ya kupita
katikati ya Samaria, sasa basi kwa mara ya Kwanza baada ya miaka mingi sana
ndio tunamuona sasa Yesu akilazimika kupita Samaria kwa sababu maalumu za
kimkakati katika kuwahudumia watu
Naye alikuwa hana
budi kupita katikati ya Samaria.
Yesu Kristo akiwa na moyo wa
tofauti kabisa na wayahudi wengine Yeye aliona iko haja ya kupita katikati ya Samaria,
sio tu kwa sababu, Mafarisayo walikuwa na mpango wa kumwangamiza, bali pia ziko
sababu nyingi sana na mambo mengi sana ya kujifunza kutokana na ziara hii ya
kijasiri ya Yesu Kristo! Ambayo ilikuwa ziara ya kimkakati katika kuifikisha
huduma ya injili kwa watu waliokataliwa lakini pia kwaajili ya kutufunza
maswala kadhaa muhimu sana
1.
Injili
ni kwa watu wote – Yesu alikuwa amekuja ulimwenguni kwaajili ya watu wote
na sio kwaajili ya Wayahudi peke yao, Kupita Samaria na kuzungumza na yule
Mwanamke na hata matokeo yake kunadhihirisha wazi kuwa injili yake na habari
njema zinamuhusu kila mmoja duniani, watu wenye ukomavu kiroho, na kisiasa,
wanashinda kabisa mipaka ya kibaguzi na kuvuka mipaka ya kawaida ya kibinadamu na kumuiita kila mmoja kushiriki neema ya
Mungu bila kujali, itikadi, historia, ukoo, rangi, uchotara, siasa yake na kadhalika
na zaidi ya yote kuufikia ulimwengu mzima hata kwa wale tunaofikiria kuwa ni
maadui zetu.
Tito 2:11-13 “Maana
neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa
ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu
wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;”
Yohana 3:16 -17 “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma
Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”
Kila mtu
anayedai ya kuwa anamfuata Yesu hana budi kuhakikisha ya kuwa anawafikia watu
wote bila ubaguzi, hubiri kila mahali, kuna watu wanadhani iko jamii ya watu
Fulani tu ndio wanaohitaji injili Yesu aliivunja mipaka hiyo na anatufundisha
kivitendo ya kuwa ni lazima injili imfikie kila mtu, awe Mwafrika, awe Mzungu,
awe Muasia, awe Mwarabu, awe muislamu, awe mbudha, awe mhindu, awe Singasinga,
awe Mjapani (Shintoism), awe Mchina (Taoism na Comfucianism) na kadhalika ni
wajibu wetu kuhakikisha injili inapenya na kufika kila mahali hata kwa watu
ambao tuna historia nao mbaya, wanaotuchukia,
hawatupendi, hawatukubali, ni lazima
tutafute njia ya kuwafikia kwa upendo. Ziara ya hii ya Bwana iliweka Msingi kwa wanafunzi wa Yesu
ambao baadaye walishuka Samaria na
kuhihubiri injili na Samaria ikaipokea injili na watu wakatubu na wakajazwa Roho Mtakatifu na kukawa
na uamsho mkubwa sana
2.
Kuleta
Maridhiano – Pamoja na mafundisho kadhaa wa kadhaa Yesu kwa kupita kwake Samaria
kama kiongozi mkubwa sana Duniani na mbinguni anatufundisha umuhimu wa
Maridhiano, Yeye kwa kuonyesha mfano anaonyesha na kufunua ukweli mpya wa
kiroho ya kuwa kupitia injili watu wake wanaweza kuonyesha upendo, yeye akiwa
Myahudi wa mfano anaonyesha ya kuwa sio kuwa karanga moja ikioza ndio zote, anaonyesha
ya kuwa Sasa yeye kama Myahudi halisi na wa kweli anavunja mipaka ya
kibaguzi, na kustawisha uhusiano na
kuvunja ubinafsi na ubaguzi uliokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria. Kila Mkristo aliyekomaa kiroho na mwenye ujuzi wa juu sana anaweza kuwa
njia na daraja la kuwapatanisha watu kwa Mungu, hata bila ya kusubiri adui
akunyenyekee, ni sisi ndio ambao tunaweza kuchukua hatua za kuvunja kuta za
uadui na kuwafikia wengine, Kama Yesu asingelichukua hatua uadui kati ya
wasamaria na wayahudi ungedumu, Lakini aliye na afya nzuri ya kiroho ndiye
aliyekuwa wa kwanza kuuvunja uadui huo na jambo hili lilimshangaza mwanamke
msamaria kwa sababu alijua sio kawaida Myahudi kuchukua hatua ngumu kama hii,
na alijiuliza inakuwaje? Je wewe unasubiri adui yako ndio achukue hatua? Aje
akunyenyekee na kukuomba? Yesu alikuwa wa kwanza kuchukua hatua na ikawashangaza
sana wasamaria
Yoahana 4:9-10 “Basi
yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu,
nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu
akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye,
Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.”
Mungu anataka
tuwashangaze wakati wote wale wanaojifikiria kuwa ni maadui zetu kwa kuwatendea
mema, linapokuja swala la injili hakuna adui, hakuna mtu asiyestahili kufikiwa
na upendo wa Mungu kwa sababu zozote zile, Kanisa ni lazima lijipange
kuhakikisha kuwa injili inawafikia watu wote hata wale ambao tunadhani kuwa
hawastahili, Wayahudi walikuwa ndio watu wa kwanza kuteuliwa na Mungu ili
waweze kuwa Baraka kwa ulimwengu mzima, ingekuwa ni hasara kubwa sana kama
wayahudi wangesahau wajibu wa kuvunja mipaka na kupeleka Baraka hizo kwa
mataifa mengine, Na ashukuriwe Mungu kwamba Yesu kiongozi mkuu wa wokovu wetu
anakuwa wa kwanza kuonyesha mfano huo kwa kuvunja mipaka ya kiadui, kibaguzi,
kikabila, kidini, kitamaduni na kijimbo kwa kuifikisha injili kila mahali
wakiwemo Wasmaria.
3.
Kufunua Mpango wa Mungu – Katika mpango wa
Mungu kulikuwa na umuhimu sana wa ziara ya Yesu kule Samaria, nawe utakubaliana
nami kuwa kulikuwa na mpango mahususi wa kiungu kwa Yesu kukutana na mwanamke
huyu mjadala wao unatupa mafunzo makubwa sana kuanzia na mafundisho ya kweli na
mpaka namna ya kuabudu na mafundisho sahihi ambayo yangeifaa sana jamii ya leo,
Mazungumzo ya Kristo na mwanamke Msamaria yanatufunulia kweli kadhaa za muhimu
katika Imani yetu kama tunavyoweza kuona
a. Mungu ni Roho – Katika mazungumzo ya
Yesu na Mwanamke Msamaria kuna mafundisho mengi ya msingi na moja ya Fundisho
hilo ni kuwa Mungu ni Roho, Wayahudi
waliamini kuwa sehemu sahihi ya kuabudu ni Yerusalem, na Wasamaria waliamini ya
kuwa Mungu anapatikana katika Mlima Gerizimu, Lakini Yesu anaonyesha kuwa
wakati sahihi unakuja ambapo watu watamuabudu Mungu sio kule Yerusalem wala
kule Gerizimu, Lazima ufikie wakati watu wajue ya kuwa Mungu hapatikani katika
mahekalu yaliyojengwa kwa mikono, wala hapatikani milimani, Mungu ni ROHO, mkao
wako wa kiroho bila kujali uko wapi utamfanya Mungu akutembelee sawa na kiu
uliyo nayo moyoni mwako, huitaji leo kwenda mahali Fulani kumtafuta Mungu kwani
Mungu anapatikana kila mahali popote ulipo endapo tu utafungua moyo wako, Mungu
yuko mahali kote na anapatikana kwa kila mtu amtafutaye kwa Moyo
Matendo 7:48-50
“Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba
zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii, Mbingu ni kiti changu cha
enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema
Bwana, Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?”
Matendo
17:24-27 “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote
vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu
zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba
anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu
vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya
uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na
mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa,
wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.”
Ibada ya kweli haitegemei mahali, inategemea mkao wa
Moyo wako, Mungu hawi mbali na yeyote anayemtafuta kwa dhati, uende milimani
usiende, Yesu alitufundisha kupitia mwanamke huyu na kutupa kuelewa namna na
jinsi inavyopaswa kumuabudu Mungu, Sio kwa sababu Ibrahimu na Isaka na Yakobo
waliabudu katika mlima huo, basi na Mungu angepatikana katika mlima huo, Mungu
ni Roho maana yake Mungu hapatikani katika namna ya asili kama wanadamu ambao
wao wanafungwa na mipaka ya kijiografia, Mungu hana mwili kama huu wa
kibinadamu, Yeye kwa kuwa ni roho hana mipaka na hivyo huwezi kumfungia Mungu
katika mahali Fulani maalumu, kwani yeye yuko mahali pote na anapatikana kila
mahali, kwa hiyo kupitia roho yako, na kujitoa kwako kwa moyo unaweza kumpata Mungu zaidi ya yote Msaada wa Roho Mtakatifu ndani
yetu, yeye anayeweza kuiinua dhamiri yetu na kutuvuvia kumtafuta kwa msaada
wake tunaweza kujiungamanisha na Mungu popote tulipo, ikiwa tu tunakuwa na
dhamira ya kweli ya kumtafuta sawasawa na neno lake na kupitia Yesu ambaye
ndiye ufunuo wa kweli, na zaidi ya yote ndani ya mwili wetu ambao ni hekalu la
Roho Mtakatifu, Mungu anaweza kuwasiliana nasi na tunaweza kumuabudu yeye
popote tulipo tukiamua tu kuwa katika roho na kumsikiliza kiibada
Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu
haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yohana 17:17 “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”
1Wakorintho
6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la
Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu
wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili
yenu.”
b. Maji ya Uzima – Mazungumzo ya Kristo na
mwanamke huyu yalianzia kisimani, na yalianza kwa Yesu kuomba maji, Yesu
aliomba maji ya kawaida, Na mwanamke huyu alisita kutokana na ubaguzi
uliokuwepo, na mshangao na ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua
karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye,
naye angalikupa maji yaliyo hai. Maji yaliyo hai kwa kimasai Engare Embuani, Katika lugha ya
kiebrania linatumika neno “Mayim Chayim”
yaani Mayim maana yake maji na Chayim maana yake uzima au uhai, Hii ilikuwa na maana ya maji yasiyo na chumvi
wala magadi, Maji masafi yanayotiririka
maji ya aina hiyo yaliaminiwa kuwa yalikuwa ni maji bora na safi na
salama na anayeweza kuwapa watu maji ya
aina hiyo ilisadikiwa kuwa chanzo chake ni Mungu tu na ndio maana mwanamke
Msamaria alimshangaa Yesu kuwa huenda ni mkuu kuliko Ibrahimu na Isaka na Yakobo
waliowaachia kisima kile.
Yeremia 2:13 “Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili;
wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika,
mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.”
Kwa hiyo Maji ya uzima yalikuwa yanawakilisha Mungu
mwenyewe ambaye ndiye chanzo cha uhai na uzima wa wanadamu wote, Ni Mungu pekee
ndiye anayeitwa kisima cha maji yaliyo hai au chemichemi ya maji ya uzima, Kwa
hiyo kimsingi Yesu alikuwa anajitambulisha kuwa yeye ndiye chemichemi hiyo mya
maji ya uzima. Na unapomuacha Mungu maana yake umeenda mbali na kisima cha maji
yaliyo hai.
Yeremia 17:13 “Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao
watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu
wamemwacha Bwana, kisima cha maji yaliyo hai.”
Katika lugha ya kiyunani (Greek) neno linalotumika kuelezea maji ya uzima ni “Hydor zōn”
“Hydor” likiwa na maana ya maji na zōn ikiwa na maana ya Uzima Kwa hiyo
Yesu alipozungumzia maji yaliyo hai au
maji ya uzima alikuwa anazungumzia kile chanzo cha uzima wa milele, Yesu
alikuwa anamaanisha jambo kubwa sana zaidi ya kiu ya kawaida ya maji ya
kimwili, Yesu alikuwa akizungumzia utoshelevu kwa kiu ya wale wanaomtafuta
Mungu unatoka kwake na yeye ndiye chanzo hicho yeye ndiye anayetoa utoshelevu
huo, kama mtu anahitaji utoshelevu wa kweli wa kiibada na kiimani basi Yesu
ndiye halisi.
Yohana 4:13-14 “Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona
kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu
milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji,
yakibubujikia uzima wa milele.”
Kwa hiyo hapa Yesu anatumia mfano wa maji kuzungumzia
kitu Fulani au chanzo Fulani ambacho ndio chanzo halisi cha maisha ya kiroho na
uzima wa milele. Na ule uzima wa milele unaitwa ZOE kwa kiyunani ambalo kwa kiingereza ni God-Kind of life maisha ya umilele kama Mungu au maisha ya milele
yanayotokana na kuungwa na Mungu. Ni dhahiri kuwa mwanamke yule ingawa alikuwa
mwenye dhambi, lakini ndani yake alikuwa na kiu ya kutaka kumjua Mungu, na kiu
ya kumuabudu Mungu, hakuwa kichwa tupu tu, alikuwa anajua pia kuwa masihi
angekuja na angeweza kuleta majibu ya namna na jinsi iwapasavyo kuabudu, kiu
yake ilikuwa imejibiwa kwa kuwa yeye aliyekuwa akisema naye alikuwa ndiye
Masihi mwenyewe, na ndiye chanzo cha uzima na maji ya uzima, Kwa hiyo unaweza
kuona kuwa ufunuo huu tusingeliupata kama Yesu asingelipita Samaria. Sio hivyo
tu wale watu tunaoweza kuwaweka katika kundi la wat wasiofaa na tukawahukumu
kama makahaba, au Malaya usije ukafikiri ya kuwa kichwani mwao hakuna kitu
kabisa, au usije ukawahukumu na kufikiri kuwa hawastahili habari njema kila
mwanadamu duniani bila kujali shetani amemuharibu kwa kiwango gani ndani yake
iko kiu ya kumuhitaji Mungu na ni wajibu wetu kama wanafunzi wa Yesu kuyafikia
makundi yote bila dharau kama za kifarisayo, na kuwapelekea injili hii ya uzima
bila ubaguzi, wala kuwahukumu paleka habari njema kwao
c. Nenda kamuite mumeo - Kuna kitu cha
Ziada cha kujifunza tena na tena katika mazungumzo ya Yesu na Mwanamke
Msamaria, Yesu alikuwa anayajua maisha ya Mwanamke huyu mwanzo mwisho, na alikuwa anajua mahitaji yake ya kiroho,
mwanamke huyu alikuwa anaishi maisha ya zinaa/alikuwa anaishi katika dhambi,
Lakini alikuwa anajua maswala kadhaa ya kiroho, na ndio maana Yesu Hakumdharau
hata kidogo alikuwa anataka kumsaidia na kuwasaidia na wengine katika siku za
leo, Somo kuhusu maji ya uzima lilikuwa bado halijaeleweka kwa mwanamke huyu na
alikusudia kubadilisha mada, Yesu akiwa anaelewa anachokifanya alimueleza nenda
kamuite mumeo!
Mwanamke huyu hakutaka kuzungumza kuhusu mumewe wa
sasa wala aliyekuweko nyumbani kwa hiyo alidanganya kuwa hana mume! Ni Kama
aliyekuwa anasema shiishi na mume, Lakini pamoja na kuwa mwanamke huyu alikuwa
akijaribu kumdanganya Yesu, ni ukweli ulio wazi kuwa jibu lake lilikuwa ni kweli,
kwanini? Mwanamke huyu alikuwa anaishi na mwanaume ambaye hakuwa mume wake
kihalali, na kwa mujibu wa sheria za Kiyahudi kama mwanamke mume wake wa kwanza
bado yuko hai, na mwanamke huyu akaishi na mwanaume mwingine maana yake
mwanamke huyu anaishi katika uzinzi
Marko 10:11-12
“Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa
mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine,
azini.”
Warumi 7:2-3 “Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa
yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria
ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa
mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si
mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.”
Hatuwezi kumdanganya Mungu kwa sababu zozote zile kwa
sababu Mungu anajua kila kitu, Yesu alikuwa anamjua mwanamke huyu na
asingeliweza kujificha, katika nyakati zetu leo, Ndoa za kikristo zinachukuliwa
poa sana, wako watu wanafanya zinaa, zile za kuibia, lakini ziko zinaa
zimepitishwa kiofisi, wako watu wamefungishwa ndoa kwenye makanisa ya kiroho,
na wengine ni watu wanaoheshimika sana katika imani, watumishi wa Mungu na
kadhalika leo wanaweza kusema kuwa ninawahukumu, mimi simuhukumu yeyote yule
lakini Neno la Mungu linasimama leo na kutukumbusha wajibu wetu ya kuwa
mwanaume na mwanamke wakristo kama uko kwenye ndoa nyingine na mumeo au mkeo
bado yuko hai wewe una kesi ya kujibu kimaandiko na kwa sababu hiyo, unapaswa kurudi kwa mkeo
au mume au ukae hivyo hivyo bila kuoa au kuolewa kama yalivyo mfundisho ya Bwana
ona, yeye Bwana amekataa kuwa hakuna sababu za mtu aliye katika Kristo kumuacha
mkewe, Mungu haamini ya kuwa iko sababu inayoweza kupelekea wewe kama mwamini
ukaacha ndoa yako halisi, au mkeo au mumeo halisi na ukapuuza lile agano na
kuishi kinyumba, kama tu vile unavyoamini kuwa hakuna dhambi Mungu hawezi
kusamehe, Basi Mungu naye anaamini hakuna dhambi inayoweza kusababisha wewe
uachane na ndoa.
Mathayo 19:3-9
“Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu,
wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? Akajibu,
akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na
mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana
na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena,
bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha
wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu
atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine,
azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.”
Safari ya Yesu katika mji wa Samaria pia ilijaa
fundisho hili na inatukumbusha kuhakikisha ya kuwa tunaishi katika ndoa kwa
usafi na mwenendo sawasawa na imani yetu katika Kristo na sio vinginevyo. Mungu
ni Mungu wa utaratibu, inamshangaza Yesu Leo kuona watu wakiachana na wakati
huo huo wakitaka kuoa tena au kuolewa tena ili hali wenzi wao wako hai, Katika
eneo hili ni muhimu kujitafakari.
d. Mavuno – Safari ya Bwana Yesu iliyo
mlazimu kupita Samaria pia ilikuwa na faida kubwa kwa ufalme wa Mungu yaani
kumvunia Bwana nasfi na roho za watu wengi sana, na hivyo kuzungumza na yule
mwanamke ilikuwa ni chanzo tu cha kubadilisha moyo wake ili kisha aweze
kuwaleta wasamaria wengi kwa Bwana
Yohana 4:27-38
“Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa
sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini?
Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake
mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote
niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini,
wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi
wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua
ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu
akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka,
nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno?
Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa
yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.”
Yesu alikuwa na akili sana alifanya kazi ndogo kwa
hekima iliyomletea matokeo makubwa sana, alimfundisha neno la Mungu mwanamke
mmoja tu, lakini kupitia huyo alijikuta anazungumza na mji mzima, alikuwa
akiwaza mavuno, na kwa kuvunja ukuta wa kiitikadi, kuvunja ukuta wa kiimani na
kitamaduni na ubaguzi alifanikiwa kuwapata wengi nao wakamwamini hili lilikuwa
ni jicho la Mavuno, Kristo anatukumbusha hapa kufanya kazi ya Mungu kwa akili
sana na kuhakikisha ya kuwa tunamletea mavuno na katika kulitekeleza hili
hatuna budi kufuata njia ya Mungu na kuacha kuwadharau watu, kwa sababu zozote
zile, tuwaendee watu wa kila kabila na kila mila na tamaduni na kumzaliwa Bwana
matunda, kwa kumletea mavuno hakuna mtu mbaya duniani ambaye hawezi
kubadilishwa na neema
Yohana 4:39-43
“Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa
sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote
niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye
akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake.
Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako
tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi
wa ulimwengu. Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya.”
Matokeo ya kupita kwa Yesu pale Samaria
Kupita kwa Bwana Yesu katika Samaria
kulikuwa na ulazima sana kwa sababu ya mafunuo makubwa na ya muhimu ambayo
tunayapata kupitia safari yake, Na zaidi ya yote kuokolewa kwa nafsi za watu
wengi sana na kuhudumiwa kwa huruma za Mungu, Mungu ametufundisha maswala mengi
sana na ya muhimu kupitia safari hii yenye mafanikio makubwa sana watu wa Samaria
wengi zaidi walimuamini Yesu. Kanisa ni lazima tukumbuke Upendo wa Mungu na
neema yake haina mipaka, tunaweza kuwafikia wengi bila kujali jamii zao,
tamaduni zao, historia zao, ama tofauti zetu, Yesu alitufundisha namna ya
kuvunja mipaka hiyo na kuwafikishia watu huduma inayowastahili
Wagalatia 3:28 “Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu”
Matendo 10:34-35 “Petro akafumbua kinywa
chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila
taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”
Hitimisho
Nimuhimu kukumbuka kuwa injili ni
kwa ulimwengu wote na kwa watu wote na kabila zote, Bwana anatufundisha
kuhakikisha ya kuwa tunavunja vihunzi vyote
vya kijamii, kiutamaduni, kikabila,
na kiimani au kidini na hata kidhehebu, na kuhakikisha ya kuwa tunahubiri
upendo kivitendo, umoja na neema na msamaha wa Mungu kwa watu wote, na kuwa inatupasa kuuiga mfano wake ili
kuwafikia watu wote kwa upendo na huruma bila kujali tofauti zetu, Bwana ampe
neema kila mmoja wetu kuvuka mipaka na vihunzi vya kibaguzi vinavyotufanya
tusiwafikie watu au kuifikia jamii fulani kwa sababu zozote zile katika jina la
Yesu ameen!, Aidha nakukumbusha kuwa Yesu aliongea na mwanamke huyu Kisimani
yaani mahali ambapo hapawezi kuwa na maswala na wakati wowote mtu anaweza kuja,
Yesu hakuongea na mwanamke huyu mafichoni, nalieleza hili mapema, mtu asione
kuwa unaweza kuzungumza na mtu wa jinsi tofauti popote tu hapana, ili
kujiepusha na kasfa na kusingiziwa kaa na ongea na mtu wa jinsi tofauti mahali
pasipo na utata. Mungu akubariki
sana kwa kufuatilia somo hili na kama umebarikiwa kumbuka kuwasiliana nami,
uongezewe neema na Mungu akutunze!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni