Jumapili, 2 Juni 2024

Mwanadamu siku zake zi kama majani


Zaburi 103:14-16 “Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi. Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo. Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.”




Utangulizi:

Ni muhimu kujikumbusha tena na tena Japokuwa haipendezi ya kuwa maisha ya mwanadamu duniani yamefupizwa sana, Kimsingi maisha ya mwanadamu ni mafupi mno ukilinganisha na maisha ya milele, ambayo Mungu amekusudia kuwapa wanadamu kama watamuamini Bwana Yesu,

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Kufupishwa kwa maisha ya mwanadamu kumetokana na Mungu mwenyewe kuyapunguza kama adhabu Baada ya kuongezeka kwa maasi yaani dhambi zetu wanadamu hapa ulimwenguni!

Mwanzo 6:1-3 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.”

Mwanzoni mwanadamu alikuwana uwezo wa kuishi kwa karne tisa (9) yaani miaka mia tisa na zaidi, na Mwanadamu aliyepata kuishi sana kuliko wanadamu wote aliitwa Methusela ambaye aliishi miaka 969 (mia tisa sitini na tisa)

Mwanzo 5:22-27 Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano. Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa. Methusela akaishi miaka mia na themanini na saba, akamzaa Lameki. Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na miwili, akazaa wana, waume na wake. Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda na sitini na kenda, akafa.”

Hata hivyo maisha ya mwanadamu siku za leo yamekuwa mafupi zaidi kama maua au majani au mvuke, japokuwa kila mwanadamu anatamani kuishi milele, Kwa msingi huo haijalishi mwanadamu ataishi muda mrefu kiasi gani bado maisha hayo ni mafupi kwa nini kwa sababu maandiko yanasema pia yanaenda kwa kasi sana yaani kama kivuli, kwa hiyo maisha haya hayatoshi, bado uko uhitaji wa maisha ya milele, na ndio maana Mungu katika hekima yake alituumba tuishi milele na kwa sababu hiyo kila mwanadamu kwaasili hapendi kifo milele iko katika mioyo yetu.

Muhubiri 3:11-14 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho. Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi, na kufanya mema maadamu wanaishi. Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote. Najua ya kwamba kila kazi aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye.”

Kwa nini tunajifunza somo hili? Kujikumbusha ufupi wa siku zetu sio kitu kibaya kwani kunatupa hekima ya kujua namna ya kuishi kwa Amani na kutumia siku zetu kwa hekima tuwapo hapa duniani Zaburi 90:12 “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.” Kwa hiyo somo hili lina baadhi ya mwaswala Muhimu yanayotuongoza jinsi na na mna ya kuzitumia siku zetu chache duniani kwa hekima, uchahce huu pia unachangiwa na kuwa zinapita haraka sana hata kama utaishi miaka mia, bado utaona ni kama zimepita haraka sana, Na kule kujifunza somo hili hakuna uhusiano wowote na unabii wa kifo cha mtu hapa, hapana ni kwaajili ya kuishi maisha mazuri tuwapo duniani!. Tutajifunza somo hili Mwanadamu siku zake zi kama majani kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-


·         Mwanadamu siku zake zi kama majani

·         Jinsi ya kutumia muda tuliopewa Duniani


Mwanadamu siku zake zi kama majani.

Moja ya mifano ya asili inayoonyesha ufupi wa maisha ya Mwanadamu ni pamoja na majani na maua katika miti na mimea ya kondeni, majani na maua huishi kwa muda mfupi sana na ndio maana utaweza kuona katika maandiko majani na maua yakitumiwa kama mfano halisi au mfano hai wa kufananisha maisha mafupi ya mwanadamu

1Petro 1:24 “Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;”       

Kwa msingi huo maandiko yanatumia majani na maua kama mfano wa asili wa kuonyesha kitu kinachodumu kwa muda mfupi zaidi. Kwa kiyunani kitu kinachodumu kwa muda mfupi zaidi kinaitwa Ephemeral Neno hilo Ephemeral kwa kiyunani yaani Greek ni Muunganiko wa maneno mawili EPI na HEMEROS, EPI kwa kiingereza maana yake ni Upon or For na HEMEROS kwa kiingereza maana yake ni Day kwa hiyo neno Ephemeral maana yake ni “For a day” “kwa siku tu” ikiwa na maana kitu kinachoishi kwa muda mfupi sana. Ephemeral is something that lasting for a very short time yaani ni kama mwendo wa kivuli cha jua, Kwa hiyo Ephemeral maana yake ni kitu kinachoishi kwa muda mfupi sana! Kama majani, au kama maua, na pia kinachopita kwa kasi sana kama kivuli!

Zaburi 102:11-12 “Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani. Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.”         

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.”

Muhubiri 6:12 “Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua?

Zaburi 39:4-6 “Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu. Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.”

Kwa hiyo katika mtazamo wa kifalsafa, maisha ya mwanadamu hutazamwa kuwa mafupi sana bila kujali mtu ameishi maisha ya miaka mingapi hapa duniani, hii inathibitisha ukweli ya kuwa tunapaswa kujua namna na jinsi ya kutumia wakati wetu huu mfupi tulio nao kwa busara zaidi sana tukijifunza kuacha majivuno na maringo kwa sababu zozote.

Zaburi 90:10-12 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara. Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”            

Jinsi ya kutumia muda tuliopewa Duniani

Tunawezaje kutumia kwa busara muda huu mfupi sana tuliopewa duniani? Ili kutumia muda huu vema tunapaswa kufikiri katika maana nzima kuhusu maisha na kulenga kutimiza kusudi kuu la maisha tulilopewa na Mungu, Maisha ni dhamana kwa hiyo:-

1.       Ishi sawa na kusudi la Mungu - Tambua ni jambo gani la Muhimu duniani ambalo Mungu anataka ulifanye?, Mungu alikuumba ili iweje? Mungu amekuleta ufanye nini? Ukiisha kutambua simamia katika siku zako zote za kuishi, kumbuka kila mwanadamu hapa duniani ana kusudi lake ambalo Mungu amemkusudia kulifanya basi kaa katika kusudi hilo, huku ukihakikisha unadumisha uhusiano wako na Mungu mapema!

 

Mhubiri 12:1-7 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.”

 

Kumkumbuka Mungu maana yake ni kulitumikia kusudi la Mungu au kutumikia shauri la Mungu yaani kufanya kile ambacho Mungu amateka tukifanye katika maisha yetu na kubwa zaidi tukiwatumikia watu na kuacha alama katika maisha yao, na moyo wa Mungu baba yetu aliyetuumba. Utatufurahia

 

Matendo 13:36 “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.”

               

2.       Tengeneza mahusiano mazuri – Ni muhimu katika maisha haya kuwekeza katika mahusiano, usiwe na maadui wala uadui na mtu wala usiwe na uadui na Mungu na watu, Neno la Mungu linatutaka tuwe na mahusiano mema na watu wote lakini na Mungu pia, Neno la Mungu limekazia sana uhusiano mwema, baba zetu wa Imani Ibrahimu na Isaka na Yakobo wakati wote katika maisha yao walitafuta amani kwa bidii hata baada ya kufanya makosa makubwa sana ya kibinadamu walitafuta Amani!

 

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

 

Marko 12:29-31 “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”               

 

1Yohana 2:9-11 “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”

 

Wekeza katika ujenzi wa uhusiano mzuri kwa familia ndugu, jamaa na marafiki na katika jamii, tengeneza mtandao mwema wa uhusiano mzuri, tia moyo watu, furahisha watu, jenga jamii, onyesha kujihusisha. Salimia majirani, jichanganye katika jamii, jihusishe katika harusi zao, kama una nafasi na katika misiba yao nafasi ikiruhusu, sema na watu vizuri, cheka na watu vizuri hata wasipokutendea mema usijali wewe tenda, cheka na wanaocheka na lia na wanaolia, usiwe na maadui, uwe rafiki wa kila mtu na wa kila rika!

 

3.       Jaa shukurani – iweni watu wa shukurani, shukuru kwa kila jambo liwe kubwa au dogo na lolote lile ambalo ulimwengu unatoa

 

1Thesalonike 5:18 “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”

 

Zaburi 106:1, “Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.”           

Zaburi 100:4 “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake;”   

 

Wakolosai 3:15 “Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.”       

 

4.       Tia moyo ustawi – wakati wote hakikisha kuwa ustawi unakuwa, yaani wakati wote ongeza maarifa, ongeza ujuzi na mbinu mbalimbali za kuhakikisha unakua katika kutafuta mbinu za kujiongeza kiimani, kiuchumi na kimaisha !

 

Luka 2:40-52 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”

 

1Nyakati 4:9-10 “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”          

 

5.       Ni heri kutoa kuliko kupokea – hakikisha ya kuwa unajitoa kwaajili ya wengine, fanikisha maisha ya wengine, furahia mafanikio ya wengine, rudisha katika jamii, Kwa matendo ya ukarimu, na utu wema, weka misingi ya kudumu kuwa mwema katika jamii yako kwa kadiri Mungu alivyokubariki utakumbukwa Daima na Mungu na watu pia.

 

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”

               

Matendo 9:36-41 “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.”

               

Matendo 10:1-8 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.”             

 

6.       Yafikirie yaliyo juu

Ni muhimu kufikiria kuhusu mambo yajayo, yanayohusiana na uzima wa milele, hata kama tutakuwa tumebarikiwa kwa kiasi gani tukiwa hapa duniani hii isiwe sababu ya kupoteza urafiki wetu na Mungu, Mafanikio yasikutoe katika kufikiri kuhusu Mungu na maswala ya milele!, Mche Mungu, fanya kila kitu huku ukijali sana maswala ya maisha ya milele usiyapuuzikie, watu wenye akili ni wale wanaomcha Mungu!

 

Mwanzo 13:2 “Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.”  

 

Waebrania 11:10 “Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.”             

 

Wakolosai 3:1-4 1. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.”   

 

Yakobo 4:13-16 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya.”           

 

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”

 

7.       Tunza afya yako - Ni muhimu sana pia kuhakikisha unatunza afya yako, Afya ya mwili akili na roho yako, hatuwezi kufurahia maisha yote ya kimwili na kiroho kama hatutatunza afya zetu, hili ni jambo la muhimu sana !

 

3Yohana 1:2 “Maana nalifĂ„rahi mno walipokuja ndugu na kuishuhudia kweli yako, kama uendavyo katika kweli.”                

 

1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”         

 

8.       Ishi kwa kiasi  - Maisha yanahitaji uwiano, yaani kiasi, jaribu kuweka kila kitu katika kiasi ridhika,  Neno kiasi katika maandiko ya kiingereza ni Soberly au Modarate  na katika kiyunani ni Sophronos ambalo maana yake ni Self possessed/Self control yaani kujidhibiti, au kujikana nafsi kwa hiyo ni muhimu kuwa na kiasi ni muhimu kujidhibiti, usipitilize mipaka katika kila jambo ulifanyalo

 

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”

 

Hitimisho:

 

Tukijikita katika mambo hayo hapo juu tutajikuta tunaishi katika utoshelevu, unaotengeneza maana kamili ya maisha bila kujali urefu au ufupi wa maisha yenyewe!

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!     

Hakuna maoni: