Ijumaa, 20 Desemba 2024

Kuzaliwa kwa Masihi na utendaji wa Roho Mtakatifu.


Luka 1:31-35 “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”




Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa Neno la Mungu katika agano jipya limeonyesha wazi namna na jinsi Roho Mtakatifu akihusika kwa kiwango kikubwa sana katika mpango mzima wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, jambo ambalo linatupa kutafakari sana na kupata ufahamu kuwa huwezi kutenganisha habari nzima inayohusiana na kuzaliwa kwa Yesu Kristo na utendaji wa Roho Mtakatifu, Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni mojawapo ya muujiza mkubwa sana ambao unapita akili ya kawaida na utendaji mzima wa ufahamu wa kibinadamu, na Ndio maana hata kitendo cha Mariamu kuwa mjamzito bila tukio la mwanaume kuhusika Malaika alifafanua wazi kuwa ingewezekana kwa uweza wa Roho Mtakatifu, hii maana yake ni kuwa kulikuwa na utendaji wa kiungu uliokuwa unahusika moja kwa moja katika kumleta masihi Duniani. kwa hiyo tunaposheherekea wakati wa kuzaliwa kwa masihi tusimsahau ROHO MTAKATIFU.

Mathayo 1:18-21 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba KWA UWEZA WA ROHO MTAKATIFU. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni KWA UWEZA WA ROHO MTAKATIFU. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”

Hii maana yake ni nini? mpango mzima wa ukombozi wa Mwanadamu ni muujiza ambao umeratibiwa na Roho Mtakatifu kwa muujiza mkubwa sana. Roho Mtakatifu ni wa muhimu mno na anahusika kwa namna ya kipekee katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu kwa sababu hata kuzaliwa kwa Mkombozi mwenyewe tunamuona Roho wa Mungu akihusika katika muujiza huu mkubwa wa kuunganisha kazi za uungu na ukombozi wa Mwanadamu, kwa muujiza mkubwa wa Mungu kufanyika mwanadamu, au mwana wa Mungu kuwa mwana wa mwanadamu ili kuleta ukombozi wa mwanadamu, ikiwa ni hivyo basi ni muhimu kufahamu kuwa tunaweza kufurahia wakati huu wa msimu wa kuzaliwa kwa Masihi kwa kukubali pia utendaji mzima wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni sehemu ya Utatu wa Mungu, na kwa sababu hiyo, tnaposhangilia kuzaliwa kwa Yesu ambaye ni mkombozi wa ulimwengu tunakumbushwa kuwa Utatuwa Mungu yaani Baba na Roho Mtakatifu ulihusika katika mpango wa kumleta Mungu mwana duniani, Tutajifunza somo hili zuri kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa Masihi

·         Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya masihi

·         Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe

Roho Mtakatifu na maandalizi ya kuzaliwa kwa Masihi

Roho Mtakatifu anaonekana kuhusika na ujio mzima wa masihi na maandalizi yake, Kumbuka nabii Yoeli alitabiri kuwa siku za mwisho Mungu angemuachilia Roho wake Mtakatifu kwa wote wenye mwili, kwa hiyo siku za mwisho zinaanzia katika msimu wote wa kuzaliwa kwa Masihi na mpaka atakapokuja mara ya pili katika utawala wake wa miaka 1000 duniani, yaani millennium ambako umwagiko huo utakuwa katika ukamilifu wake au utakuwa katika kilele chake.

Yoeli 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”

Roho Mtakatifu alihusika vipi katika maandalizi mazima ya kuzaliwa kwa masihi?

-          Alihusika katika muujiza mzima wa kutungwa kwa mimba katika tumbo la Mariamu  kwa hiyo tendo zima la Mariamu kupokea ujauzito liliratibiwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu

 

Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”

 

-          Alihusika Katika kumjaza nguvu akiwa tumboni Mtangulizi wa Masihi yaani Yohana Mbatizaji Luka 1:13-16 “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.”

 

-          Alihusika katika kuwaongoza watu waliokuwa wakimsubiria na kuona ahadi ya Mungu ikitimizwa katika maisha yao Luka 2:26-30 “Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako

 

-          Athari za utendaji wa Roho Mtakatifu katika kuzaliwa kwa masihi kunasababisha azaliwe mtu ambaye uungu unakaa ndani yake na kwa sababu hiyo nguvu ya dhambi isingelimuweza, kwa sababu huyu aliyezaliwa angekuwa ni mwana wa Mungu na hii ingeweza kumtofautisha na mwanadamu wa kawaida ambaye asili yake ni Adamu, ambaye asili yake ni udongo, wakati Yesu Kristo asili yake ni ya mbinguni.

 

1Wakorintho 15:47-48 “Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.”

 

Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.”

 

Kitendo cha Yesu Kristo kuzaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kimemfanya kuwa mwanadamu mwenye asili ya mbinguni na kwa sababu hiyo dhambi haingelimuweza na kupitia maisha yake ya ushindi dhidi ya dhambi angeweza kuwa msaada kwa wanadamu wote, Na kwa kufanywa mwenye dhambi ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu kupitia yeye hivyo haya yasingeliwezekana kama sio kazi za Roho Mtakatifu.

 

2Wakorintho 5:21 “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” 
    

Roho Mtakatifu na maisha na huduma ya Masihi

Roho Mtakatifu anaonekana katika maisha na huduma ya Yesu Kristo kuanzia ubatizo wake mpaka kupaa kwake Mbinguni pamoja na ahadi aliyoitoa ya ujio rasmi wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wake na sisi sote tuaminio.

-          Wakati Yesu anabatizwa Roho wa Mungu alishuka juu yake  Mathayo 3:16-17 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

 

Hii ilikuwa ni alama ya kupakwa mafuta kwa mtu huyu aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu sasa anaanza kutumikia kusudi la baba yake, na baba anampaka mafuta kwa Roho wake Mtakatifu ili sasa aweze kuwa kuhani, nabii na mfalme kwaajili ya kuwakomboa wanadamu, uwezo wake wa kufundisha, kuhudumia watu, kufanya miujiza na kila kitu alikifanya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu huku maisha yake yakiongozwa na Roho, kwa hiyo

 

a.       Aliongozwa na Roho MtakatifuMarko 1:12-13 “Mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.”

 

b.   Alifanya huduma zote za kuwafungua watu kama matokeo ya Roho Mtakatifu kuwa juu yake – Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

 

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”

 

c.     Alitoa Pepo kwa Chanda cha Mungu yaani kwa uwezo wa Roho MtakatifuLuka 11:20 “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

 

Mathayo 12:28 “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

 

d.      Nguvu wakati wa kusulubiwa – Roho Mtakatifu aliyehusika katika kuzaliwa kwa Kristo, kubatizwa na kumuongoza na kumtumia katika huduma zake duniani alimtia nguvu vilevile katika huduma yake ya kuukabili Msalaba kwaajili ya ukombozi wetu, alikwenda Msalabani kwa upako ule ule uliomuwezesha kufanya huduma nyingine, Roho alimpa ujasiri, upendo na uvumilivu kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu ili kuyatimiza mapenzi ya Mungu, bila uweza wa Roho Mtakatifu uwezo wa kuvumilia mauti ya msalaba ambayo kwa asili ilikuwa ni mauti mbaya na ya aibu isingeliwezekana au kuwa jambo jepesi.

 

Luka 22:41-43 “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”

 

Waebrania 9:13-14 “Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

e.     Wakati wa kufufuka kwake  - Roho Mtakatifu anatumika pia kama muhusika mkuu wakati wa kuurejesha uhai wa Yesu Kristo, yaani swala zima la kufufuka kwa Yesu Kristo maandiko yanasema Roho Mtakatifu alihusika katika kumfufua Yesu Kristo

 

Warumi 1:3-4 “yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;”

       

Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”        

Roho Mtakatifu na maisha yetu mimi na wewe

Maisha yako wewe na mimi hayawezi kuwa na ukamilifu bila kazi za Roho Mtakatifu kufanyika ndani yetu, Kristo alisema sisi hatuwezi kufanya neno lolote pasipo yeye hii ni Dhahiri kuwa kama Yesu Kristo Mwana wa Mungu alimtegemea Roho Mtakatifu katika maisha yake yote na utumishi wake na uvumilivu wake na kila kitu, ni Dhahiri kuwa, maisha yetu Bila Roho Mtakatifu na kazi zake katika maisha yetu itatufanya tuwe watu wasio na faida maana imeandikwa wala si kwa uweza wala kwa nguvu Bali kwa uweza wa Roho Mtakatifu  yeye ndiye anayetupa uwezo wa kufanya jambo lolote kwaajili ya Mungu.

Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.”

Yohana 16:7-11 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”

Roho Mtakatifu ni msaada ulio karibu katika maisha yetu – Yohana 14:26Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”           

Roho Mtakatifu ni Msaada katika maombi – Warumi 8:26-27Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.”      

Roho Mtakatifu hututia nguvu – Matendo 1:4-8Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”              

Roho Mtakatifu hutupa karama za Rohoni – 1Wakorintho 12:4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.”

Tunaweza kufaidika na maswala yote ya kiroho endapo tu Roho Mtakatifu atakuwa pamoja nasi atatusaidia katika ujuzi, hekima, maarifa na kutuwezesha kutenda mambo kwa uhodari tukiwa na Roho Mtakatifu. Najua wakati huu wa msimu wa sikukuu kuna maswala mengi sana na mada nyingi zitazungumzwa lakini mimi niliongozwa kuwakumbusha watu wote kuwa kuzaliwa kwa masihi nyuma yake uko uratibu mzima wa Roho wa Mungu na kwa sababu hiyo ni vema tukashughulika na Kusheherekea sikukuu hii huku tukijikumbusha kuwa ni kazi zipi Roho wa Mungu anazifanya ndani mwetu je kuna uhai katika maisha yetu? Kuna uhai katika kanisa la Mungu? Iwapo tunataka kufurahia msimu wa sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa furaha ya kweli kutoka mbinguni furaha hiyo itakamilishwa ndani yetu endapo tutaitumia nafasi hii kutafakari na kutubu, na kumuomba Mungu asituondolee Roho wake Mtakatifu, sikukuu ya kuzaliwa kwa masihi itakuwa tamu kama wanadamu watajiandaa kuzaliwa kwa Roho na kijazwa kwa Roho Mtakatifu.

Na. Rev Innocent Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Alhamisi, 12 Desemba 2024

Kuifuata njia ya Balaamu

 

2Petro 2:14-16 “wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule.”




Utangulizi:

Nyakati hizi tulizo nazo ni nyakati za mwisho, tunaishi dakika za mwishoni sana katika dakika za kinabii, na maandiko yametueleza wazi kuwa nyakati hizi za mwisho ni nyakati za hatari, hasa kwa sababu ya uwepo wa mafundisho ya uongo na uwepo wa manabii wengi wa uongo pamoja na uwepo wa mafundisho ya mashetani na roho zidanganyazo, kwa hiyo kila Mkristo anapaswa kulikumbuka hili na kuchukua tahadhari kujihami na uongo wao:-

1Timotheo 4:1-3 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.”

Mathayo24:11-14 “Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”              

Katika nyakati hizi za mwisho ni muhimu kwa kanisa yaani kila mtu aliyeokolewa kuwa makini na kuchukua tahadhari juu ya utendaji wa shetani, hususani kwa kutuingizia mafundisho ambayo kusudi lake ni kututoa katika kweli na usafi wa kiroho ili tuweze kuishi mbali na uadilifu wa kiungu, aina hiyo na njia kama tutaifuata basi tutakuwa tumeifuata njia ya Balaamu, ambaye yeye ni mfano wa manabii wa uongo na walimu wa uongo, leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu juu ya somo hili lenye kichwa “Kuifuata njia ya Balaamu” ili kujiepusha na namna ya kifuata njia ya udanganyifu.Tutajifunza somo hili kuifuata njia ya Balaam kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Ufahamu kuhusu Balaamu.

·         Kuifuata njia ya Balaamu.

·         Onyo la kutokuifuata njia ya Balaamu.

 

 Ufahamu kuhusu Balaamu

Maandiko matakatifu yanatuonya vikali kuacha kuifuata njia ya Balaamu kwa msisitizo mkubwa sana na kwa lugha kali  ya maonyo Petro akionya kuwa kuifuata njia hiyo ni kuacha njia iliyonyooka na kufuata udhalimu, Yuda akitoa onyo kali na akiliita kosa la Balaamu aliyependa ujira wa udhalimu na Yesu mwenyewe katika kitabu cha ufunuo akionyesha kuchukizwa na mafundisho ambayo yanatia watu ukwazo na kuwaongoza katika maisha yasiyo na uadilifu wa Kristo, maonyo haya makali yanatufanya leo tujadili na kutafakari tena huyu Balaamu ni nani na alifanya nini hata kumuudhi Mungu na tahadhari ambayo kanisa linapaswa kuchukua ili kujilinda na mafundisho ya uongo!  

2Petro 2:15 “wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;”

Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora.”

Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”

Jina Balaamu linajitokeza kwa mara ya kwanza katika maandiko mara baada ya wana wa Israel kuvuka bahari ya Shamu na kuanza kuikabili inchi ya mkanaani wakiwa chini ya Musa, Katika wakati huu Israel walikuwa wengi sana na tayari walianza kuogopwa na mataifa yaliyokuwa yakiishi ng’ambo ya Yordani likiwemo taifa la wana wa Moabu, ambalo mtawala wake aliitwa Balaki, akiwa na hofu kubwa sana ya kuwaogopa Israel Mfalme huyu aliamua kwenda kumuita mtu mwenye uwezo wa nguvu za giza kuwalaani au kuwaroga Israel ili ikiwezekana wasiweze kumvamia na kumshinda, mtu huyu aliitwa Balaamu, jina Balaamu kwa kiebrania linasomeka kama “Bā’lam”  au “Bil’ām”  ambalo kwa kiingereza ni “Devourer” a person of thing that eats, consumes, or destroys something greedily, ravenously or voraciously yaani kwa Kiswahili mtu mwenye kitu kinachokula, kinachoteketeza, au kuharibu kitu fulani kwa uroho, mwenye uchu, au mwenye tamaa, kwa hiyo mtu huyu Balaamu ambaye jina lake linafanana sana na tabia zake alialikwa na Mfalme wa Moabu akiwa pamoja na muungano wa wazee wa Midian kuja kuilaani na kuiroga Israel. Balaamu amekuwa ni mfano wa manabii na walimu wa uwongo katika nyakati zote kanisa likiwepo duniani.

Hesabu 22:1-6 “Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”

Balaamu hatajwi kokote kuwa alikuwa nabii, isipokuwa na Petro ambaye amemtaja kama nabii mwenye wazimu lakini tunaweza kusema kuwa alikuwa ni mchawi au nabii wa uongo, alikuwa ni mchawi mwenye uwezo wa kubariki au kulaani, hata hivyo Mungu aliweza  kuingilia kati mara kadhaa na kusema naye, na hata Roho wa Mungu aliingilia mfumo wa maneno yake ili aweze kubariki Israel badala ya kuwalaani, na hivyo mtu huyu mwenye utata mwingi alijikuta akitoa nabii nyingi za Baraka na za kweli kwa Israel na ukiwapo ujio wa Daudi na Masihi, Bwana wetu Yesu.

Hesabu 24:1-4 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani. Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;”

Balaamu alikuwa anamjua Mungu wa kweli au wa Israel wazi wazi, hata baada ya Roho wa Mungu kuingilia mfumo wake, inaonekana tu kuwa mtu huyu alikuwa amezingirwa na kuharibiwa na mazingira ya dunia, tamaa, na ubinafsi ambao ulimfanya ashindwe kutii mapenzi ya Mungu mara kadhaa, kiasi ambacho alitamani kumuendea Balaki, Hata hivyo baada ya kubembelezwa kwa mali nyingi na heshima kubwa na akakaidi katazo la Mungu la kwenda kuwalaani Israel jambo lililopelekea malaika wa Bwana kuingilia kati na punda wake kugomea kwenda na hata kusema naye

Hesabu 22:7-35 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu. Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe? Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa. Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi. Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi. Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza. Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie; maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa. Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza. Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi. Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.”

Mchawi huyu mtata hata hivyo aliruhusiwa kibishi na malaika wa Bwana lakini alilazimishwa kuwa atasema yale tu Mungu atakayoweka katika kinywa chake na sio maneno yake wala makusudio yake kwa hiyo agizo la Mungu kwake ilikuwa ni kubariki wana wa Israel na sio kuwalaani au kuroga. Kama ilivyokusudiwa na mfalme wa wamoabu.

Kuifuata njia ya Balaamu.

Historia inaonyesha ya kuwa Balaamu alipaswa kutamka yale tu ambayo Mungu alikuwa amemwamuru kutamka, wote tunajua mapenzi ya Mungu kwa wanadamu, ya kuwa tangu zamani Mungu ametaka watumishi wake watamke kile tu ambacho Mungu amekikusudia na hata neno lake Mungu anataka litendewe haki katika tafasiri zake, Mungu ametamani watu wote wamtii, watu wote wasikie neno lake kama lilivyo bila kuongeza au kupunguza, na watumishi waiseme kweli yake na ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anachukizwa sana na  manabii na walimu wa uongo ona:-

Hesabu 22:20 “Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.”

Yeremia23:25-29 “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

Kumbukumbu 4:1-2 “Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.”

Ufunuo 22:18-19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”                  

Neno la Mungu linakazia kuwa iko haja ya kusema kile ambacho ni mapenzi ya Mungu na kwa dhamiri iliyo njema, na Mungu alimuamuru Balaamu kufanya hivyo na kwa sehemu alifanya hivyo, Lakini hata hivyo kwa sababu ya tamaa ya fedha na heshima na ujira mkubwa aliokuwa ameandaliwa tunanaarifiwa katika maandiko kuwa baadaye Balaamu alishauri njia itakayoleta madhara kwa wana wa Israel, na hili ndilo jambo walifanyalo manabii na walimu wa uongo.

Hesabu 31:15-16 “Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai? Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana.”

Ni ushauri gani aliutoa Balaamu, inaonekana kuwa baada ya kushindwa kuwalaani Israel na kuwaroga kwa sababu ya karipio la Bwana, Balaamu aliamua kutoa ushauri wa kuwawekea kwazo wana wa Israel, ambao walikuwa wamepiga kambi Shitimu, wanawake wa Moabu waliandaa ibada za Baal Peor na waisrael hasa wanaume walialikwa au kushawishiwa katika ibada hizo na waliruhusiwa kuingiliana na wanawake wanaohudumu katika madhabau za baali,Yaani walizini kiwmili na kiroho, Jambo hili lilimuudhi Mungu na kumpa hasira na kushusha mapigo kwa watu wake Israel kwa maelekezo ya Musa, kwa kuwa ibada hizo za kipagani zilihusisha miungu ya uzazi matukio ya ngono ni sehemu ya ibada hizo  na hivyo Israel yakawakuta, katika tukio hilo watu wapatao elfu 24 walikufa kwa pigo.

Hesabu 25:1-9 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli. Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori. Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake; akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli. Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.”

Kwa hiyo inaonekana wazi kuwa Balaamu, aliposhindwa kuwalaani Israel na kuwaroga, alitoa ushauri, alitoa ushauri huo ili kuwakosanisha watu wa Mungu kwa Mungu mwenyewe na kusababisha madhara makubwa kwa Israel, Balaamu alifanya haya kwa sababu ya tamaa na kutaka kumfurahisha Balaki ambaye alimuahidi mali nyingi sana, na kwa sababu hiyo Balaamu anaingia katika rekodi ya watu waliowakosesha watu wa Mungu, na katika nyakati za agano jipya manabii na walimu wote wa uongo na watu wote wanaopotosha watu na kuharibu uadilifu wetu kwa Mungu nao wanaitwa watu walioifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori, wako watu ambao kwa makusudi kabisa au kwa sababu ya tamaa zao wako tayari kuichuja injili kwa sababu kadhaa kama Balaamu, aidha kwaajili ya mapato ya udhalimu na pia kama watumishi wa shetani, Kanisa la kwanza lilipambana kufa na kupona  na walimu wa uongo.Tabia kadhaa za Balaamu hapa zinaweza kuwasaidia watu wa Mungu kuwatambua wale wanaokwenda katika njia ya Balaamu ona:-

1.       Balaamu alikuwa na tamaa na aliamua kuchakachua - Nyakati za leo, Mitume wa uongo, manabii wa uongo, wainjilisti wa uongo, wachungaji wa uongo, na walimu wa uongo, na washirika wa uongo wako tayari kulichakachua neno la Mungu na uadilifu wa kiroho kwa sababu ya faida za mwilini, wanaingia katika jaribu hilo kwa sababu ya tamaa za mwili na mali na utukufu wa wanadamu, wanafundisha watu na kuwaingizia tamaa za vitu vya mwilini zaidi kuliko vya rohoni, sisemi kuwa vitu vya mwilini havina maana, lakini wanasahu kutoa kipaumbele kwa ufalme wa Mungu na kwaajili ya tamaa na mapato ya aibu wamechuja viwango vya injili na hawakemei dhambi, wala kuwaongoza watu katika mafundisho sahihi na ya kweli. Walimu wa uwongo hujipa mamlaka kubwa kana kwamba wao wako juu ya maandiko na kuwapa watu uhuru usiotokana na Mungu, matokeo yake watu hawataishi maisha matakatifu na watajikuta wanarudi nyuma na kuishi maisha yasiyo na uadilifu kama anavyofafanua Petro:-

 

2Petro 2:15-21 “wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.”

 

2.       Balaamu aliwashawishi watu wazini – Baada ya kushindwa kuwalaani na kuwaroga waisrael alitoa ushauri kwamba wanawake wa Moabu wawashawishi wanaume wa Israel ili wazini na kuabudu miungu, hii inatufundisha kuwa wako watu nyakati za leo badala ya kuwaongoza watu katika kutenda mema wanaichakachua injili na kuwaongoza watu vibaya maandiko yanatuonya kuwa kuifuata njia ya Balaamu ni pamoja na kuwashawishi watu kwenda kinyume na uadilifu, mfano mtu anawezaje kuacha kuikemea dhambi? Leo hii yako makanisa hayakemei dhambi, wala hayaongozi watu katika toba, wala kuishi maisha ya haki, na wala hawahubiri utakatifu na zaidi ya yote zinaa, uasherati, utapeli na uongo, choyo, chuki, wivu, na mafarakano imekuwa ni moja ya maswala au matunda yanayoonekana wazi kwa kanisa kinyume na uadilifu wa Mafundisho ya Yesu Kristo na mitume, aidha watu hawawakemei wale wanaofundisha mafundisho ya uongo. Leo hii uponyaji unanunuliwa kwa viwango vya kifedha na linaonekana kama jambo la kawaida tu.

 

Mathayo 7:15-20 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua

 

3.       Balaamu alikuwa mchawi – Pamoja na kuwa Mungu alimtumia kusema na kutoa unabii, lakini huyu Balaamu alikuwa mchawi, maandiko yanasema alikwenda kutafuta uchawi na pia wazee wa midian walimpa ujira wa uganga, tukio la kutoa ushauri uliokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu unathibitisha wazi kuwa alikuwa nabii wa uongo wala hakusimama katika kweli, swali kubwa la kujiuliza mtu anawezaje kuwa wa kiroho na wakati huo huo akatoa ushauri unaoongoza katika kutenda dhambi? Unabii wa kweli na miujiza ya kweli sio kipimo cha uadilifu wala uthibitisho kuwa Mungu yuko na mtu huyo, tutawatambua kwa matunda yao.

 

Hesabu 24:1 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.”

               

Hesabu 22:7 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.”

 

Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

 

4.       Balaamu aliweka ukwazo - Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”

 

Neno kuweka ukwazo linalotumika hapo katika lugha ya kiyunani ni “Skandalon” ambalo kwa kingereza limetumika neno “Stumbling-block” ambayo maana yake ni kuandaa au kutengeneza mazingira ya kusababisha ugumu, au kumuingiza mtu katika mtego, kuhakikisha kuwa mtu anaingia pagumu, au kusababisha mtu ajikwae, kwa hiyo walimu wa uongo au watu wanaoifuata njia ya Balaamu, mojawapo ya kazi yao ni kutengeneza mazingira yatakayowafanya watu wa Mungu au kanisa wajikute wapo pagumu, waingie mtegoni, Skandalon ni kikwazo, ni kupotosha na kumuondoa mtu katika njia kwa kusudi la kupoteza,ni kumuangusha mtu kutoka katika imani sahihi, Kristo Yesu alikwisha kuonya juu ya changamoto hii ya kukosesha na kutangaza adhabu kali kwa mtu atakayewakosesha watu wa Mungu, ukweli ni kuwa kunaweza kuwepo watu watakaotenda dhambi katika kanisa na wakatubu na kupona, lakini kanisa halipaswi kuvumialia watu wanaoleta mafundisho ya uongo na kuwaingiza watu katika dhambi, au kuwatoa katika Imani ya kweli au kuwaacha wachukuliane na dunia, ikiwa itakuwa hivyo hiyo ni njia ya Balaamu. Yesu Kristo pamoja na mitume wake walikuwa wakali sana lilipokuja swala la kuwapotosha watu kutoka katika njia ya kweli au injili ya kweli, dhambi inaweza kusameheka kirahisi kwa sababu ni tatizo ndani ya mtu, lakini mafundisho ya uwongo hayawezi kusameheka kwa urahisi kwa sababu yataongoza wengi katika uharibifu.

 

Mathayo 18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.”

 

Wagalatia 1:8-9 “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”

 

5.       Balaamu alikuwa na moyo wa kikatili -  Balaamu ni mfano wa watu ambao wanataka mambo yao yaende tu, na kuwatumikisha watu wengine kwa nguvu lakini kwa kusudi la mafanikio yake bila kuwajali wale anaowatumikisha, Balaamu hatajali kuwa wewe unakabiliwa na nini lakini atakulazimisha ufanikishe jambo lake hata kama umemtumikia yeye kwa muda wa kutosha na kwa uaminifu, moyo wa ukatili wa Balaamu unaonekana pale alipompiga punda wake mpaka punda huyo akapewa uwezo wa kuzungumza akionyesha kuwa alikuwa akiyaokoa maisha yake, Balaamu hakutaka hata kumshukuru Punda wake tofauti na malaika wa Bwana ambaye alionyesha kujali kazi ya punda ya kuokoa maisha ya Bwana wake, walimu wengi wa uongo ni makatili, huwatesa na kuwatumikisha watu kwa kisingizo cha kumtumikia Mungu, watataka wewe ujitoe ukiwa na umasikini wako lakini wao wanatajirika kila iitwapo leo, je watu huchuma zabibu katika miiba? Aliwahi kuhoji Bwana Yesu, Mungu hajakuokoa uwe mtumwa wa mtu amekuokoa uwe mtumishi wa Mungu na sisi tuhudumiane kwa upendo kila mmoja akimuhesabu mwenzi wake kuwa bora kuliko nafsi yake

 

Hesabu 22:20-33 “Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!nNdipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.”               

Onyo la kutokuifuata njia ya Balaamu

Habari za Balaamu zinatufundisha na kutuonya kuwa ni lazima wakristo wawe makini wao wenyewe kuyapima mafundisho yaliyojaa ulimwengini katika nyakati za leo, sio kila mtu anaihubiri kweli, na sio kila mtu ni salama, Yesu Kristo alichukizwa na mafundisho ya Balaamu ambayo yalikuweko nyakati za kanisa la kwanza na kimsingi leo pia yapo ulimwenguni hata kama hayaitwi kwa jina lake Balaamu, tamaa zao ziko katika kipato na utajiri wa dunia hii, na hiki ndicho wanachijivunia na kukihubiri wala hakuna mkazo wa kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, Balaamu alianza vizuri lakini alishindwa mwishoni kwa sababu tamaa ilimzidi, na moyo wake ukadanganyika kwa malipo na mapato ya aibu, ya aibu kwa sababu yalipatikana kinyume na mapenzi ya Mungu au kinyume na njia zake

Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”

Maandiko yanatuonya kuwa wala tusifuatishe namna ya dunia hii Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Uko umuhimu mkubwa wa kuishi maisha matakatifu, maisha ya haki na ya uaminifu kwa Mungu, Mafundisho yoyote au mahubiri yoyote yanayotanguliza mahitaji ya kifedha kuliko kushughulika na utakatifu na haki na uaminifu wa Mungu yanaweza kuwa yanaelekea katika njia ya Balaamu, huu ni wakati ambao kanisa linapaswa kukemea kwa nguvu zote na kuwaonya watu wawe makini na ukengeufu ambao sasa umeenea kila mahali duniani, Sehemu yoyote ambayo hakuna upendo, kumejaa ubinafsi, na kujilimbikizia mali, dhambi haikemewi, wenye dhambi hawasaidiwi, wanaibishwa, hawarejeshwi kwa Yesu, watu wanafukuzwa, watumishi hawana mzigo na mshirika wala hawawafuatilii, wenye fedha peke ndio wanaoheshimiwa, wachanga kiroho wanapewa vyeo, matajiri wanapewa vyeo, kuna ugomvi na mafarakano ya kila namna, migogoro haiishi, watu hawasameheani, hizo zote ni dalili za kutokuwepo kwa Mafundisho sahihi na kuwepo kwa mafundisho ya Balaamu, Kanisa ni lazima kujitafakari na kujilinda. Na kukazia kuwa Mungu ni Mtakatifu, na ametuitia utakatifu, ni lazima tufundishe kwa mkazo huo na inawezekana kabisa watu wa Mungu kuishi maisha matakatifu, ikiwa Ayubu aliweza kuishi kwa uadilifu wewe na mimi hatuwezi kushindwa kuishi maisha ya uadilifu. Maandiko yanaonyesha kuwa inawezekana

 

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”  

2Timotheo 4:1-4 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.”

Mwisho

Mungu atawahukumu walimu wa uongo kama alivyomuhukumu Balaamu, Biblia inatuelezea kuwa hatimaye Balaamu aliuawa na wana wa Israel wakikumbuka kuwa aliwakosesha katika tukio la Baal Peor Hivyo waisrael waaminifu walihakikisha kuwa sio uwongo wake tu unafutwa lakini hata na yeye nabii wa uongo anaondoka ili kukomesha mafundisho yasiyo sahihi, pamoja na wale waliomuunga mkono, Kanisa ikiwa liko tunaloliamini kuwa ni sahihi tulisimamie na ikiwa kuna kitu hakiko sahihi tumuombe Mungu na kutumia silaha za kiroho kukiondoa, endapo utabaini kuwa fundisho Fulani sio sahihi usikae kimya badala yake kwa upole na hekima rekebisha kwa mafundisho yaliyo sahihi, wala usimshambulie mtu, lakini shambulia fundisho lisilo sahihi, na utawezaje kujua fundisho lililo sahihi fika katika ibada za mafundisho kwa kusudi la kuijua kweli, na ukitaka kujua watu wanaopenda mafundisho tembelea ibada za katikati za mafundisho ndio utawajua wakristo wa kweli wanaotaka kujifunza na kukua kiroho ili waweze kuwa msaada kwa wengine na kizazi kijacho.

Kumbukumbu 23:3-5 “Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele; kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize. Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda Bwana, Mungu wako.”

Yoshua 13:22 “Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.”

               

Na. Rev Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatano, 4 Desemba 2024

Mzabibu mwema, umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?


Yeremia 2:19-21 “Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi. Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?

 



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu wetu ni Mungu ambaye anatarajia matunda mema kutoka katika maisha yetu, kila mtu aliyeokolewa katika lugha ya mficho ya kimaandiko anatajwa kama mti hususani mzabibu, na Mungu anaturatajia kama mche mzuri wa mzabibu kumzalia yeye matunda yaliyo mema, Haipendezi kama mtu anaweza kusema ya kuwa ameokolewa na kisha matunda yanayotokana na toba yake yasionekane, Haiwezekani kuwa Mkristo aendelee katika wokovu na kukomaa kiroho kisha matunda ya ukomavu wake yasionekane, Mungu alikuchagua wewe na mimi kama mbegu au mche ulio mwema wa Mzabibu na kutufanyia kila linalowezekana kwaajili ya wokovu wetu ili tuweze kumzalia yeye matunda, na kwa sababu hiyo kama hatutamzalia yeye matunda tutajiweka katika hatari ya kukatwa, na kutupwa motoni kama maandiko yasemavyo:-

Luka 3:7-9 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

Yohana 15:1-8 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.”

 

·         Kupandwa kwa mzabibu mwema.

·         Mzabibu mwema, umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?

·         Jinsi ya kuwa mzabibu mwema!

 

Kupandwa kwa mzabibu mwema

Yeremia 2:19-21 “Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi.Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?”

Nabii Yeremia anatoa ujumbe wenye nguvu na wa Muhimu sana kwa watu wa Mungu, Katika wakati huu Mungu alikuwa anazungumza na wana wa Israel utawala wa Yuda kwa kinywa cha nabii Yeremia kuonyesha masikitiko yake na kuumizwa kwake moyo, yeye kama mkulima au mwenye bustani aliyepanda mzabibu mwema, mkulima huyu anaonyesha wazi kuwa alizingatia masharti na vigezo vyote vya kupanda mbegu iliyo njema, kama wote tunavyofahamu kuwa katika uchaguzi wa mbegu ni muhimu na lazima kwa mkulima kuchagua mbegu au mche ulio bora zaidi kwaajili ya matokeo bora zaidi, Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa Mungu alipowachagua Israel kutoka Misri alikuwa amechagua mbegu njema ya uzao wa Ibrahimu, watu ambao walimcha Mungu na kumtii, Mungu alikuwa amewandaa wana wa Israel kwa mkono wenye nguvu ili wamtegemee yeye, Mungu aliwapa sheria na utaratibu na kuwafunza uadilifu kupitia viongozi bora kama Musa na Haruni na wengine na hatimaye kuwaleta katika nchi ya mkanaani, kuchaguliwa kwao na Mungu wakati wote kumefananishwa na mkulima anayezingatia vigezo na masharti katika kuipata mbegu iliyo bora, hakukuwa na kitu chenye upungufu ambacho mkulima huyu hakukizingatia kuanzia na matayarisho ya ardhi, upandaji umwagiliaji, palizi na hata uondoaji wa matawi yasiyo sahihi ili mmea huu uweze kustawi ipaswavyo na kutoa matunda, mazuri na yenye ubora uliokusudiwa!.

Isaya 5:1-4 “Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?       

Zaburi 80:7-11 “Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi. Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.”

Mungu alikuwa amewapanda Israel katika nchi ya mkanaani kwa mfano wa mzabibu, yeye ndiye aliyewatoa katika inchi ya Misri na kuwapanda katika nchi ya mkanaani, huenda Mungu alitumia mfano wa mzabibu kwa sababu Mzabibu ulifikiriwa kuwa ni mti wa Baraka, na mmea huu ulimea katika inchi ya Kanaani kwa miaka mingi sana na kwa karne nyingi sana, kwa hiyo lilikuwa jambo jema na la Baraka kwa Mungu kuwaweka watu wake katika inchi hii, zabibu pia zilikuwa ishara ya Amani na utulivu, Mungu alipowapanda Israel katika Kanaani ilikusudiwa wawe wema na baraka kwa ulimwengu mzima.

Kutoka 15:13-17 “Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu. Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika. Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka. Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua. Utawaingiza, na KUWAPANDA katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako.”

Mungu aliwakusudia Israel na Yuda wawe watu wake watakaokuwa nuru kwa mataifa yote na kuifunua neema ya Mungu ya ukombozi wa mwanadamu duniani pamoja na mfano wa haki na hukumu, na upendo wake kwa ulimwengu mzima, hili halikuwa jambo dogo, ilikuwa ni neema kubwa na upendeleo usio na kifani miongoni mwa mataifa ya dunia

Isaya 49:5-6 “Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

Kuzaliwa kwa zabibu mwitu.

Katika namna yenye kushangaza sana pamoja na ukweli kuwa Mungu anasema alichagua mbegu au mche mwema na kuzingatia vigezo vyote vizuri vya kilimo cha mzabibu, Israel ambao ndio mzabibu wenyewe ulizaa zabibu mwitu, wao walimuacha Mungu na kugeukia ibada za sanamu, waliiacha sheria ya Mungu na kuanza kuabudu miungu, ni ukweli ulio wazi kuwa tunapotenda mema kwa Mungu haiwi jambo la kushangaza kwa sababu tuliumbwa tutende mambo mema, lakini tunapotenda maovu Mungu hushangazwa sana kwa sababu alipotuumba kila kitu kilikuwa chema, lakini watu kwa hiyari yao na utashi walichagua kutokumtii Mungu na kusababisha madhara duniani. Swali kubwa analouliza Mungu ni kuwa imekuaje mzabibu mwema uliohudumiwa kwa vigezo na masharti yote ya mkulima stadi nini kimetokea mzazbibu huo ukazaa zabibu mwitu?

Katika lugha ya kitaalamu mmea uliochaguliwa vizuri, na kuoteshwa katika kitalu kama mbegu iliyo njema kisha ikaoteshwa kwa kuzingatia vigezo vyote kisha ukazaa zabibu mwitu tendo hilo linaitwa “degeneration” kwa kiyunani “ekfylismόs” ni tukio la kutokea kitu kisichotarajiwa na kisichokuwa cha kawaida katika mmea mfano, kunyauka kwa majani, kubadilika rangi ya majani, mizizi kubadilika, kudumaa au kuzorota kwa mmea au kuzaa matunda duni na madogo sana, au kupoteza ubora, tendo hili husababishwa na maambukizi ya virusi kutoka katika ardhi, Katika mfumo wa uzazi wa mwanadamu ni mfano wa Mungu kuweka kizazi kizuri ndani ya tumbo la mwanamke na kisha badala ya tumbo hilo kushika mimba na kuzaa watoto wazuri linatengeneza aina fulani za uvimbe mkubwa ambao ni lazima uondolewe kwa upasuaji na wakati mwingine kulazimika kuondoa na kizazi ili uvimbe huo usijirudie tena, katika hali kama hiyo mzabibu unapopata maambukizi kama hayo wenyewe huondolewa na kuharibiwa ili kuzuia aina hiyo ya ugonjwa kuenea “degeneration” inaweza kusababishwa na aina fulani ya virusi, ambavyo vinauzorotesha mmea halisi na kusababisha matokeo duni, kudumaa, na hata kuzaliwa kwa zabibu zisizo na afya, Katika ulimwengu wa roho kirusi hicho kinaweza kuwa ni utendaji wa shetani na udanganyifu wa mioyo ya wanadamu na kiburi pamoja na tamaa za dunia, Maandiko yanaonyesha kuwa mpanzi anaweza kabisa kupanda mbegu njema lakini adui akapanda magugu.

Mathayo 13:37-43 “Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.”

Tukio hilo la mzabibu kuharibika na kutokuzaa matunda yaliyokusudiwa licha ya Mkulima kujitahidi kuchagua mbegu njema na kuipanda katika udongo mzuri ndio tukio la Israel na Yuda na ndio linalowakuta watu wa Mungu ambao katika siku za leo, Leo Mungu anazungumza na kanisa lake anazungumza na watu waliokoka leo hii watu wengi waliookoka wameharibika bila kujua na mioyo yao imekuwa kinyume na Mungu aliye hai jambo ambalo linamshangaza sana Mungu,  watu wamelelewa vizuri kiroho, waliokolewa kwa neema, wamejazwa na Roho wake Mtakatifu, wamepata mafundisho yote ya wokovu, lakini unashangaa watu wana roho mbaya, wana hasira, wana kiburi, wamejaa majivuno, wanataka kuabudiwa, wachoyo, wakaidi, wanakomeshana, wanaumizana, wanasemana vibaya, wanasengenyana, wachawi wameingia makanisani, watu wanauana, watu wanaharibiana, watu wanafanyiana mabaya, hakuna matunda ya roho, hila na ubaya, ubinafsi na uchoyo,kuna uchafum kuna uasherati, kuna wivu, kuna mafarakano, kuna ubabe, kuna uzushi, kuna husuda, kuna ulafi, anasa, na kupenda fedha kuliko Mungu, kuna mafundisho potofu na uongo, hayo ndio matunda yaliyozaliwa na watu ambao Mungu alitegemea watakuwa na kiasi, wema, wenye furaha, Amani, wenye fadhili, waaminifu, waliojaa upendo, siku hizi kama unataka kuyaona mambo yaliyokinyume na hayo njoo katika makanisa yetu ya kiroho, utashangaa kushuhudia roho ya nubaya ikitawala hata waamini hawana furaha na makanisa yao, chumba za siku hizi hazina uaminifu, Mungu anashangazwa na mbegu hii njema aliyoipanda!. Swali kuu mzabibu mwema umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?

Ezekiel 17:2-8 “Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali; useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi; akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi. Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto. Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko. Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha. Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri..”

Wanadamu wote wamekuwa sawa na mzabibu huu ambao Mungu anausikitikia, ya kuwa alifanya kila kitu kuwa chema lakini uhusiano wa wanadamu na Mungu umezorota, ndoa yako ilikuwa njema lakini imezorota, uchumba wako ulikuwa mwema na mlikuwa mnawasiliana vizuri lakini siku za karibuni uhusiano huo umezorota, ulikuwa unapenda sana ibada lakini siku za karibuni uhusiano wako na Mungu umezorota, ulikuwa muombaji sana lakini siku za karibuni hali ya mzabibu huu umezorota, ulikuwa mtoaji na mkarimu na mwenye upendo mkubwa lakini siku za karibuni umezorota, ulikuwa na biashara inayoenda vizuri, uchumi uliokuwa unastawi, mahusiano yaliyokuwa yanastawi, ulikuwa mchapa kazi, mshuhudiaji mzuri, na mfuatiliaji wa watoto wachanga wa kiroho, ulikuwa unampenda Mungu wakati huo ulikuwa mche mwema lakini sasa mzabibu umezorota, moyo wa ubinafsi, choyo, chuki na wivu, ugomvi, ukatili ni matunda ambayo Mungu anashangazwa kwa kuwa alitarajia matunda mema lakini umezaa zabibu mwitu! Na mizizi yako imeelekea kwingine! Hii maana yake ni nini badala ya kuzaa matunda mema watu wamezaa matunda mabaya mizizi imeenda kujiunga na chanzo kingine cha udongo usio sahihi ona:-

Wagalatia 5:19-23 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

Maandiko yanaonyesha kuwa ni mzabibu mmoja tu ndio umekuwa mzabibu wa kweli na mzabibu huu ni Yesu Kristo, lakini mizabibu mingine yote imezorota na ina mapungufu mbalimbali na kwa kweli sio mizabibu halisi au ya kweli wote tumekuwa mizabibu mwitu, Yesu Peke yake ndiye wa Mzabibu wa kweli, na ili tuweze kuwa mzabibu wa kweli wenye kuzaa matunda hatuna budi kupandikizwa katika Kristo Yesu, na kuendelea kukaa ndani yake kama tawi, hapo ndipo tunapoweza kuzaa matunda mazuri, na tutaendelea kusafishwa, lakini nje ya Yesu, mbingu utazisikia kwa hadithi tu, uwezo wa kuzaa vema hautakuwepo, na uwezekano wa tawi hilo kuondolewa ni mkubwa sana.

Yohana 15:1-2 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”

Jinsi ya kuwa mzabibu mwema!

1.       Tunaweza kumsihi Mungu atupe neema ya kuwa mbali na kiburi, wana wa Israel waliharibiwa na kiburi, walishika dini na sheria za Musa pamoja na mapokeo ya baba zao, wakagoma kabisa kumpa Mungu nafasi ya kushughulika na maisha yao, wakati wote walijifikiria kuwa wako sahihi, hata nyakati za leo wako watu kwa sababu ya kiburi cha kidini, hawana muda wa kujichunguza wanadhani wako sahihi na Mungu, Shetani alikuwa pia mzabibu mwema wakati fulani, lakini moyoni mwake alijaa kiburi na majivuno, alitaka kujiinua kuliko Mungu, aliwaambukiza dhambi yake wanadamu,  wayahudi na bila kujijua wakawa watoto wa shetani, Hebu jaribu kuwaza kuwa wayahudi hawa wenye kuishika sheria ya Musa kwa kiwango hiki ni lini waligeuka na kutokuwa watoto wa Mungu hata Yesu anawaambia ninyi ni wa baba yenu ibilisi? Walikuwa mzabibu mwema lakini hawakujua kuwa wamegeuka kuwa mzabibu mwitu na kwa sababu ya ukaidi wao, wao ndio walikuja kumshulubisha Bwana Yesu na kumsaliti na kumkabidhi mikononi mwa waovu ili asulubiwe!

 

Yohana 8:42-45 “Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu.Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.”

 

Jiulize ni kwanini Yohana alikuja na ubatizo wa toba kwa wayahudi?  Je unadhani watu hawa walikuwa wanahitaji toba? Je walikuwa hawashiki imani? Je walikuwa hawafungi? Je walikuwa hawaepuki dhambi? Nini kiliwaponza wana wa Ibrahimu mche mzuri wakawa wana wa nyoka? Nadhani kanisa tunahitaji kujiangalia vizuri na kwa umakini mkubwa, kama tulizaliwa tukiwa wana wa Mungu inawezekanaje tena tukawa wa uzazo wanyoka?, shetani ni mjanja sana hatatumia zinaa, wala ulevi kutuangusha atatumia kiburi, atatumia majivuno atatumia njia ya kujibebesha utukufu wa Mungu na tukajikuta tumekataliwa kistaarabu.

 

Luka 3:7-9 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”              

 

2.       Tunaweza kurudi kwa Yesu ambaye ndiye mzabibu wa kweli na kuwa tawi linalostawi ndani yake na ambaye tukikaa ndani yake tutazaa sana matunda na kusafishwa zaidi ili tuzidi kuzaa!

 

Yohana 15:4-6 “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.”

 

Endapo tutaacha kiburi na unafiki na kutubu na kukaa ndani ya Yesu Kristo yeye yuko tayari kutupokea na kutusamehe kabisa na kurejesha uhusiano wetu na yeye na tunaweza kumzalia matunda, watu wenye kiburi wakati wote hujifikiria kuwa watakatifu na kuwa hawana dhambi ya kutubia, sio hivyo tu wakati wote wao hunyooshea kidole watu wengine na kukuza makosa ya wengine badala ya kujikagua wewe mwenyewe, kumbuka kila mmoja atalichukua furushi lake mwenyewe!, Matunda unayozaa ndio yanayotambulisha kuwa ani alikuwa mti mbaya na nani alikuwa mti mwema na vile utakavyozaa matunda, matunda hayo ndio yatafunua asili yako hatuwezi kuigiza, mbele za Mungu matunda yatasema

 

1Yohana 1:8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

 

Luka 6:41-45 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri;   kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”

 

3.       Lazima tukubali kuwa wanyenyekevu -  Neema ya Mungu haikai na watu wenye kiburi, neema ya Mungu inakaa na watu wanyenyekevu, uwepo wa Mungu unakaa na watu wanyenyekevu, toba wakati wote inaenda na unyenyekevu, bila unyenyekevu na moyo uliopondeka hatuwezi kufaidi uwepo wa Mungu

 

Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”

 

1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;”

Hitimisho:

Ujumbe wa Yeremia ni ujumbe wa nyakati zote Mungu analionya taifa la Israel, analionya kanisa na kila mmoja wetu, wote tunahitaji toba, wote tunapaswa kuitikia wito wa Mungu na kukubali kuwa Mungu anaumia anapoona tunaacha kuzaa matunda yaliyokusudiwa na kuzaa zabibu mwitu, Mungu anatuvumilia sana vinginevyo tungekuwa tumeshakatwa, Bwana amempa neema kila mmoja wetu kuwa na uwezo wa kuzaa matunda mema yanayokusudiwa katika Ukristo wetu, Mungu alipokuchagua wewe na mimi alituamini, alijua ya kuwa tutamzalia bwana matunda na tutaongoza wengi katika mema na kuwa nuru na Baraka kubwa kwa ulimwengu, mambo yanapokuwa tofauti maana yake ni kuwa Mzabibu mwema umegeuka kuwa mzabibu mwitu, Upewe neema wewe na mimi tusiwe mzabibu mwitu katika jina la Yesu Kristo, wakati huu tunapoelekea kuumaliza mwaka kila mmoja anapaswa kujifanyia tathimini na kuongea na Mungu na kujenga hoja ni kwa nini asikatwe?  Na kama hutaki kukatwa basi tuzae matunda

Luka 13:6-9 “Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.