Alhamisi, 12 Desemba 2024

Kuifuata njia ya Balaamu

 

2Petro 2:14-16 “wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule.”




Utangulizi:

Nyakati hizi tulizo nazo ni nyakati za mwisho, tunaishi dakika za mwishoni sana katika dakika za kinabii, na maandiko yametueleza wazi kuwa nyakati hizi za mwisho ni nyakati za hatari, hasa kwa sababu ya uwepo wa mafundisho ya uongo na uwepo wa manabii wengi wa uongo pamoja na uwepo wa mafundisho ya mashetani na roho zidanganyazo, kwa hiyo kila Mkristo anapaswa kulikumbuka hili na kuchukua tahadhari kujihami na uongo wao:-

1Timotheo 4:1-3 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.”

Mathayo24:11-14 “Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”              

Katika nyakati hizi za mwisho ni muhimu kwa kanisa yaani kila mtu aliyeokolewa kuwa makini na kuchukua tahadhari juu ya utendaji wa shetani, hususani kwa kutuingizia mafundisho ambayo kusudi lake ni kututoa katika kweli na usafi wa kiroho ili tuweze kuishi mbali na uadilifu wa kiungu, aina hiyo na njia kama tutaifuata basi tutakuwa tumeifuata njia ya Balaamu, ambaye yeye ni mfano wa manabii wa uongo na walimu wa uongo, leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu juu ya somo hili lenye kichwa “Kuifuata njia ya Balaamu” ili kujiepusha na namna ya kifuata njia ya udanganyifu.Tutajifunza somo hili kuifuata njia ya Balaam kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Ufahamu kuhusu Balaamu.

·         Kuifuata njia ya Balaamu.

·         Onyo la kutokuifuata njia ya Balaamu.

 

 Ufahamu kuhusu Balaamu

Maandiko matakatifu yanatuonya vikali kuacha kuifuata njia ya Balaamu kwa msisitizo mkubwa sana na kwa lugha kali  ya maonyo Petro akionya kuwa kuifuata njia hiyo ni kuacha njia iliyonyooka na kufuata udhalimu, Yuda akitoa onyo kali na akiliita kosa la Balaamu aliyependa ujira wa udhalimu na Yesu mwenyewe katika kitabu cha ufunuo akionyesha kuchukizwa na mafundisho ambayo yanatia watu ukwazo na kuwaongoza katika maisha yasiyo na uadilifu wa Kristo, maonyo haya makali yanatufanya leo tujadili na kutafakari tena huyu Balaamu ni nani na alifanya nini hata kumuudhi Mungu na tahadhari ambayo kanisa linapaswa kuchukua ili kujilinda na mafundisho ya uongo!  

2Petro 2:15 “wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu;”

Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora.”

Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”

Jina Balaamu linajitokeza kwa mara ya kwanza katika maandiko mara baada ya wana wa Israel kuvuka bahari ya Shamu na kuanza kuikabili inchi ya mkanaani wakiwa chini ya Musa, Katika wakati huu Israel walikuwa wengi sana na tayari walianza kuogopwa na mataifa yaliyokuwa yakiishi ng’ambo ya Yordani likiwemo taifa la wana wa Moabu, ambalo mtawala wake aliitwa Balaki, akiwa na hofu kubwa sana ya kuwaogopa Israel Mfalme huyu aliamua kwenda kumuita mtu mwenye uwezo wa nguvu za giza kuwalaani au kuwaroga Israel ili ikiwezekana wasiweze kumvamia na kumshinda, mtu huyu aliitwa Balaamu, jina Balaamu kwa kiebrania linasomeka kama “Bā’lam”  au “Bil’ām”  ambalo kwa kiingereza ni “Devourer” a person of thing that eats, consumes, or destroys something greedily, ravenously or voraciously yaani kwa Kiswahili mtu mwenye kitu kinachokula, kinachoteketeza, au kuharibu kitu fulani kwa uroho, mwenye uchu, au mwenye tamaa, kwa hiyo mtu huyu Balaamu ambaye jina lake linafanana sana na tabia zake alialikwa na Mfalme wa Moabu akiwa pamoja na muungano wa wazee wa Midian kuja kuilaani na kuiroga Israel. Balaamu amekuwa ni mfano wa manabii na walimu wa uwongo katika nyakati zote kanisa likiwepo duniani.

Hesabu 22:1-6 “Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”

Balaamu hatajwi kokote kuwa alikuwa nabii, isipokuwa na Petro ambaye amemtaja kama nabii mwenye wazimu lakini tunaweza kusema kuwa alikuwa ni mchawi au nabii wa uongo, alikuwa ni mchawi mwenye uwezo wa kubariki au kulaani, hata hivyo Mungu aliweza  kuingilia kati mara kadhaa na kusema naye, na hata Roho wa Mungu aliingilia mfumo wa maneno yake ili aweze kubariki Israel badala ya kuwalaani, na hivyo mtu huyu mwenye utata mwingi alijikuta akitoa nabii nyingi za Baraka na za kweli kwa Israel na ukiwapo ujio wa Daudi na Masihi, Bwana wetu Yesu.

Hesabu 24:1-4 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani. Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;”

Balaamu alikuwa anamjua Mungu wa kweli au wa Israel wazi wazi, hata baada ya Roho wa Mungu kuingilia mfumo wake, inaonekana tu kuwa mtu huyu alikuwa amezingirwa na kuharibiwa na mazingira ya dunia, tamaa, na ubinafsi ambao ulimfanya ashindwe kutii mapenzi ya Mungu mara kadhaa, kiasi ambacho alitamani kumuendea Balaki, Hata hivyo baada ya kubembelezwa kwa mali nyingi na heshima kubwa na akakaidi katazo la Mungu la kwenda kuwalaani Israel jambo lililopelekea malaika wa Bwana kuingilia kati na punda wake kugomea kwenda na hata kusema naye

Hesabu 22:7-35 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu. Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe? Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa. Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi. Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi. Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza. Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie; maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa. Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza. Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi. Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.”

Mchawi huyu mtata hata hivyo aliruhusiwa kibishi na malaika wa Bwana lakini alilazimishwa kuwa atasema yale tu Mungu atakayoweka katika kinywa chake na sio maneno yake wala makusudio yake kwa hiyo agizo la Mungu kwake ilikuwa ni kubariki wana wa Israel na sio kuwalaani au kuroga. Kama ilivyokusudiwa na mfalme wa wamoabu.

Kuifuata njia ya Balaamu.

Historia inaonyesha ya kuwa Balaamu alipaswa kutamka yale tu ambayo Mungu alikuwa amemwamuru kutamka, wote tunajua mapenzi ya Mungu kwa wanadamu, ya kuwa tangu zamani Mungu ametaka watumishi wake watamke kile tu ambacho Mungu amekikusudia na hata neno lake Mungu anataka litendewe haki katika tafasiri zake, Mungu ametamani watu wote wamtii, watu wote wasikie neno lake kama lilivyo bila kuongeza au kupunguza, na watumishi waiseme kweli yake na ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anachukizwa sana na  manabii na walimu wa uongo ona:-

Hesabu 22:20 “Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.”

Yeremia23:25-29 “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

Kumbukumbu 4:1-2 “Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.”

Ufunuo 22:18-19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”                  

Neno la Mungu linakazia kuwa iko haja ya kusema kile ambacho ni mapenzi ya Mungu na kwa dhamiri iliyo njema, na Mungu alimuamuru Balaamu kufanya hivyo na kwa sehemu alifanya hivyo, Lakini hata hivyo kwa sababu ya tamaa ya fedha na heshima na ujira mkubwa aliokuwa ameandaliwa tunanaarifiwa katika maandiko kuwa baadaye Balaamu alishauri njia itakayoleta madhara kwa wana wa Israel, na hili ndilo jambo walifanyalo manabii na walimu wa uongo.

Hesabu 31:15-16 “Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai? Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana.”

Ni ushauri gani aliutoa Balaamu, inaonekana kuwa baada ya kushindwa kuwalaani Israel na kuwaroga kwa sababu ya karipio la Bwana, Balaamu aliamua kutoa ushauri wa kuwawekea kwazo wana wa Israel, ambao walikuwa wamepiga kambi Shitimu, wanawake wa Moabu waliandaa ibada za Baal Peor na waisrael hasa wanaume walialikwa au kushawishiwa katika ibada hizo na waliruhusiwa kuingiliana na wanawake wanaohudumu katika madhabau za baali,Yaani walizini kiwmili na kiroho, Jambo hili lilimuudhi Mungu na kumpa hasira na kushusha mapigo kwa watu wake Israel kwa maelekezo ya Musa, kwa kuwa ibada hizo za kipagani zilihusisha miungu ya uzazi matukio ya ngono ni sehemu ya ibada hizo  na hivyo Israel yakawakuta, katika tukio hilo watu wapatao elfu 24 walikufa kwa pigo.

Hesabu 25:1-9 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli. Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori. Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania. Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake; akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli. Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.”

Kwa hiyo inaonekana wazi kuwa Balaamu, aliposhindwa kuwalaani Israel na kuwaroga, alitoa ushauri, alitoa ushauri huo ili kuwakosanisha watu wa Mungu kwa Mungu mwenyewe na kusababisha madhara makubwa kwa Israel, Balaamu alifanya haya kwa sababu ya tamaa na kutaka kumfurahisha Balaki ambaye alimuahidi mali nyingi sana, na kwa sababu hiyo Balaamu anaingia katika rekodi ya watu waliowakosesha watu wa Mungu, na katika nyakati za agano jipya manabii na walimu wote wa uongo na watu wote wanaopotosha watu na kuharibu uadilifu wetu kwa Mungu nao wanaitwa watu walioifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori, wako watu ambao kwa makusudi kabisa au kwa sababu ya tamaa zao wako tayari kuichuja injili kwa sababu kadhaa kama Balaamu, aidha kwaajili ya mapato ya udhalimu na pia kama watumishi wa shetani, Kanisa la kwanza lilipambana kufa na kupona  na walimu wa uongo.Tabia kadhaa za Balaamu hapa zinaweza kuwasaidia watu wa Mungu kuwatambua wale wanaokwenda katika njia ya Balaamu ona:-

1.       Balaamu alikuwa na tamaa na aliamua kuchakachua - Nyakati za leo, Mitume wa uongo, manabii wa uongo, wainjilisti wa uongo, wachungaji wa uongo, na walimu wa uongo, na washirika wa uongo wako tayari kulichakachua neno la Mungu na uadilifu wa kiroho kwa sababu ya faida za mwilini, wanaingia katika jaribu hilo kwa sababu ya tamaa za mwili na mali na utukufu wa wanadamu, wanafundisha watu na kuwaingizia tamaa za vitu vya mwilini zaidi kuliko vya rohoni, sisemi kuwa vitu vya mwilini havina maana, lakini wanasahu kutoa kipaumbele kwa ufalme wa Mungu na kwaajili ya tamaa na mapato ya aibu wamechuja viwango vya injili na hawakemei dhambi, wala kuwaongoza watu katika mafundisho sahihi na ya kweli. Walimu wa uwongo hujipa mamlaka kubwa kana kwamba wao wako juu ya maandiko na kuwapa watu uhuru usiotokana na Mungu, matokeo yake watu hawataishi maisha matakatifu na watajikuta wanarudi nyuma na kuishi maisha yasiyo na uadilifu kama anavyofafanua Petro:-

 

2Petro 2:15-21 “wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.”

 

2.       Balaamu aliwashawishi watu wazini – Baada ya kushindwa kuwalaani na kuwaroga waisrael alitoa ushauri kwamba wanawake wa Moabu wawashawishi wanaume wa Israel ili wazini na kuabudu miungu, hii inatufundisha kuwa wako watu nyakati za leo badala ya kuwaongoza watu katika kutenda mema wanaichakachua injili na kuwaongoza watu vibaya maandiko yanatuonya kuwa kuifuata njia ya Balaamu ni pamoja na kuwashawishi watu kwenda kinyume na uadilifu, mfano mtu anawezaje kuacha kuikemea dhambi? Leo hii yako makanisa hayakemei dhambi, wala hayaongozi watu katika toba, wala kuishi maisha ya haki, na wala hawahubiri utakatifu na zaidi ya yote zinaa, uasherati, utapeli na uongo, choyo, chuki, wivu, na mafarakano imekuwa ni moja ya maswala au matunda yanayoonekana wazi kwa kanisa kinyume na uadilifu wa Mafundisho ya Yesu Kristo na mitume, aidha watu hawawakemei wale wanaofundisha mafundisho ya uongo. Leo hii uponyaji unanunuliwa kwa viwango vya kifedha na linaonekana kama jambo la kawaida tu.

 

Mathayo 7:15-20 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua

 

3.       Balaamu alikuwa mchawi – Pamoja na kuwa Mungu alimtumia kusema na kutoa unabii, lakini huyu Balaamu alikuwa mchawi, maandiko yanasema alikwenda kutafuta uchawi na pia wazee wa midian walimpa ujira wa uganga, tukio la kutoa ushauri uliokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu unathibitisha wazi kuwa alikuwa nabii wa uongo wala hakusimama katika kweli, swali kubwa la kujiuliza mtu anawezaje kuwa wa kiroho na wakati huo huo akatoa ushauri unaoongoza katika kutenda dhambi? Unabii wa kweli na miujiza ya kweli sio kipimo cha uadilifu wala uthibitisho kuwa Mungu yuko na mtu huyo, tutawatambua kwa matunda yao.

 

Hesabu 24:1 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.”

               

Hesabu 22:7 “Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.”

 

Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

 

4.       Balaamu aliweka ukwazo - Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.”

 

Neno kuweka ukwazo linalotumika hapo katika lugha ya kiyunani ni “Skandalon” ambalo kwa kingereza limetumika neno “Stumbling-block” ambayo maana yake ni kuandaa au kutengeneza mazingira ya kusababisha ugumu, au kumuingiza mtu katika mtego, kuhakikisha kuwa mtu anaingia pagumu, au kusababisha mtu ajikwae, kwa hiyo walimu wa uongo au watu wanaoifuata njia ya Balaamu, mojawapo ya kazi yao ni kutengeneza mazingira yatakayowafanya watu wa Mungu au kanisa wajikute wapo pagumu, waingie mtegoni, Skandalon ni kikwazo, ni kupotosha na kumuondoa mtu katika njia kwa kusudi la kupoteza,ni kumuangusha mtu kutoka katika imani sahihi, Kristo Yesu alikwisha kuonya juu ya changamoto hii ya kukosesha na kutangaza adhabu kali kwa mtu atakayewakosesha watu wa Mungu, ukweli ni kuwa kunaweza kuwepo watu watakaotenda dhambi katika kanisa na wakatubu na kupona, lakini kanisa halipaswi kuvumialia watu wanaoleta mafundisho ya uongo na kuwaingiza watu katika dhambi, au kuwatoa katika Imani ya kweli au kuwaacha wachukuliane na dunia, ikiwa itakuwa hivyo hiyo ni njia ya Balaamu. Yesu Kristo pamoja na mitume wake walikuwa wakali sana lilipokuja swala la kuwapotosha watu kutoka katika njia ya kweli au injili ya kweli, dhambi inaweza kusameheka kirahisi kwa sababu ni tatizo ndani ya mtu, lakini mafundisho ya uwongo hayawezi kusameheka kwa urahisi kwa sababu yataongoza wengi katika uharibifu.

 

Mathayo 18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.”

 

Wagalatia 1:8-9 “Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”

 

5.       Balaamu alikuwa na moyo wa kikatili -  Balaamu ni mfano wa watu ambao wanataka mambo yao yaende tu, na kuwatumikisha watu wengine kwa nguvu lakini kwa kusudi la mafanikio yake bila kuwajali wale anaowatumikisha, Balaamu hatajali kuwa wewe unakabiliwa na nini lakini atakulazimisha ufanikishe jambo lake hata kama umemtumikia yeye kwa muda wa kutosha na kwa uaminifu, moyo wa ukatili wa Balaamu unaonekana pale alipompiga punda wake mpaka punda huyo akapewa uwezo wa kuzungumza akionyesha kuwa alikuwa akiyaokoa maisha yake, Balaamu hakutaka hata kumshukuru Punda wake tofauti na malaika wa Bwana ambaye alionyesha kujali kazi ya punda ya kuokoa maisha ya Bwana wake, walimu wengi wa uongo ni makatili, huwatesa na kuwatumikisha watu kwa kisingizo cha kumtumikia Mungu, watataka wewe ujitoe ukiwa na umasikini wako lakini wao wanatajirika kila iitwapo leo, je watu huchuma zabibu katika miiba? Aliwahi kuhoji Bwana Yesu, Mungu hajakuokoa uwe mtumwa wa mtu amekuokoa uwe mtumishi wa Mungu na sisi tuhudumiane kwa upendo kila mmoja akimuhesabu mwenzi wake kuwa bora kuliko nafsi yake

 

Hesabu 22:20-33 “Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!nNdipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.”               

Onyo la kutokuifuata njia ya Balaamu

Habari za Balaamu zinatufundisha na kutuonya kuwa ni lazima wakristo wawe makini wao wenyewe kuyapima mafundisho yaliyojaa ulimwengini katika nyakati za leo, sio kila mtu anaihubiri kweli, na sio kila mtu ni salama, Yesu Kristo alichukizwa na mafundisho ya Balaamu ambayo yalikuweko nyakati za kanisa la kwanza na kimsingi leo pia yapo ulimwenguni hata kama hayaitwi kwa jina lake Balaamu, tamaa zao ziko katika kipato na utajiri wa dunia hii, na hiki ndicho wanachijivunia na kukihubiri wala hakuna mkazo wa kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, Balaamu alianza vizuri lakini alishindwa mwishoni kwa sababu tamaa ilimzidi, na moyo wake ukadanganyika kwa malipo na mapato ya aibu, ya aibu kwa sababu yalipatikana kinyume na mapenzi ya Mungu au kinyume na njia zake

Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”

Maandiko yanatuonya kuwa wala tusifuatishe namna ya dunia hii Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

Uko umuhimu mkubwa wa kuishi maisha matakatifu, maisha ya haki na ya uaminifu kwa Mungu, Mafundisho yoyote au mahubiri yoyote yanayotanguliza mahitaji ya kifedha kuliko kushughulika na utakatifu na haki na uaminifu wa Mungu yanaweza kuwa yanaelekea katika njia ya Balaamu, huu ni wakati ambao kanisa linapaswa kukemea kwa nguvu zote na kuwaonya watu wawe makini na ukengeufu ambao sasa umeenea kila mahali duniani, Sehemu yoyote ambayo hakuna upendo, kumejaa ubinafsi, na kujilimbikizia mali, dhambi haikemewi, wenye dhambi hawasaidiwi, wanaibishwa, hawarejeshwi kwa Yesu, watu wanafukuzwa, watumishi hawana mzigo na mshirika wala hawawafuatilii, wenye fedha peke ndio wanaoheshimiwa, wachanga kiroho wanapewa vyeo, matajiri wanapewa vyeo, kuna ugomvi na mafarakano ya kila namna, migogoro haiishi, watu hawasameheani, hizo zote ni dalili za kutokuwepo kwa Mafundisho sahihi na kuwepo kwa mafundisho ya Balaamu, Kanisa ni lazima kujitafakari na kujilinda. Na kukazia kuwa Mungu ni Mtakatifu, na ametuitia utakatifu, ni lazima tufundishe kwa mkazo huo na inawezekana kabisa watu wa Mungu kuishi maisha matakatifu, ikiwa Ayubu aliweza kuishi kwa uadilifu wewe na mimi hatuwezi kushindwa kuishi maisha ya uadilifu. Maandiko yanaonyesha kuwa inawezekana

 

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”  

2Timotheo 4:1-4 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.”

Mwisho

Mungu atawahukumu walimu wa uongo kama alivyomuhukumu Balaamu, Biblia inatuelezea kuwa hatimaye Balaamu aliuawa na wana wa Israel wakikumbuka kuwa aliwakosesha katika tukio la Baal Peor Hivyo waisrael waaminifu walihakikisha kuwa sio uwongo wake tu unafutwa lakini hata na yeye nabii wa uongo anaondoka ili kukomesha mafundisho yasiyo sahihi, pamoja na wale waliomuunga mkono, Kanisa ikiwa liko tunaloliamini kuwa ni sahihi tulisimamie na ikiwa kuna kitu hakiko sahihi tumuombe Mungu na kutumia silaha za kiroho kukiondoa, endapo utabaini kuwa fundisho Fulani sio sahihi usikae kimya badala yake kwa upole na hekima rekebisha kwa mafundisho yaliyo sahihi, wala usimshambulie mtu, lakini shambulia fundisho lisilo sahihi, na utawezaje kujua fundisho lililo sahihi fika katika ibada za mafundisho kwa kusudi la kuijua kweli, na ukitaka kujua watu wanaopenda mafundisho tembelea ibada za katikati za mafundisho ndio utawajua wakristo wa kweli wanaotaka kujifunza na kukua kiroho ili waweze kuwa msaada kwa wengine na kizazi kijacho.

Kumbukumbu 23:3-5 “Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele; kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize. Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda Bwana, Mungu wako.”

Yoshua 13:22 “Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.”

               

Na. Rev Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Hongera sana mtumishi. Hakika ujumbe ni mzuri sana. Mungu aendelee kukulinda ili tuzidi kupata maarifa .

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima alisema ...

Asante sana Mtu wa Mungu Kwa kunitia moyo, endelea kuniombea neema Niko tayari kuendelea kutumiwa kama chombo Kwa ajili ya mwili wa Kristo