2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya
upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala
usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya
Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”
Utangulizi
Nyakati
za Kanisa la kwanza kuwa mkristo na kuwa muhubiri wa injili maana yake ilikuwa
ni pamoja na kukabiliana na mateso, maumivu, kukataliwa, kutishiwa, kuonewa,
kukandamizwa na hata kuuawa, Wakristo wengi waliotawanyika duniani wakati ule
waliuawa na kuteswa kwa kutupwa gerezani, kutupwa katika matundu ya simba,
kuchomwa moto na kupingwa vikali kwaajili ya wokovu, kwa sababu hiyo wakristo
wengi na watumishi wengi wa Mungu waliingiwa na hofu au woga, na kwa sababu
hiyo maendeleo yao ya kiroho na kihuduma yalikumbwa na vikwazo kwa sababu
waliingiwa na shaka na hivyo kuogopa kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwaajili ya
haya wakristo wengi waliingiwa na hofu na walihitaji kutiwa moyo kujua tuko
katika njia ya dhiki nyingi
Matendo 14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na
kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya
imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba
imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.”
Ni
katika hali kama hii Paulo mtume akiwa gerezani huko Rumi akiwa mfungwa
aliyehukumiwa kama muhalifu kwaajili ya injili anaandika waraka huu kwa kusudi
la kumtia moyo Mtumishi wa Mungu Timotheo ambaye kwaasili alikuwa mwoga,
akimkumbusha kuwa Mungu hakutupa Roho ya woga, bali ya nguvu na upendo na moyo
wa kiasi, Timotheo ni kama sisi tulivyo leo, Tunahitaji kujikumbusha kuwa
Tunaye Roho wa Mungu ndani yetu ambaye anatupa nguvu katika wakati wa mahitaji
yetu, bila kujali kuwa tunakutana na magumu kiasi gani, au tuko hatarini kiasi
gani, tunauwezo wa kukabiliana na hali yoyote ile inayotishia maisha yetu bila
kuogopa kwa sababu Roho Mtakatifu yuko juu yetu na hivyo Hatuogopi! Kwa
msingi huo basi Leo wakati huu wa juma la Pentekoste tutachukua Muda
kujikumbusha tena na tena umuhimu wa Roho Mtakattifu katika kutupatia ujasiri
unaotusaidia kusonga mbele bila kujali kuwa ni vikwazo gani tunakutana navyo
katika maisha yetu ya Ukristo katika jina la Yesu, tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mungu
hakutupa roho ya woga!
·
Roho
Mtakatifu ni roho wa ujasiri
·
Jinsi
ya kutupilia mbali woga.
Mungu hakutupa roho
ya woga!
Moja
ya adui mkubwa sana wa watu waliookoka ukimuacha shetani ni woga, kwa kweli
woga ni mtego mkubwa sana unaopunguza uwezo wetu wa kutenda mambo makuu pamoja
na Bwana, Maendeleo yetu ya kimwili na kiroho na hata kisaikolojia yanaweza
kuathiriwa kwa kiwango kikubwa sana na woga, wako watu wanaogopa hata kuanza
biashara, wako watu hawaoi kwa sababu wanaogopa wataoaje, wako watu
hawafanikiwi kwa sababu wanaogopa kuingia gharama na kujitosa katika kufanya
majaribio, woga unaleta mashaka, woga unaleta kutokujiamini, woga ni mtego
unaotuzuia kufikia ndoto zetu na kuona ahadi za Mungu zikitimia katika maisha
yetu, woga hutuletea kukata tamaa, woga unaweza kuchelewesha kwa kiwango
kikubwa maendeleo yetu! Wana wa Israel walishindwa kuirithi inchi ya ahadi
mapema kwa sababu zilizochangiwa na woga!
Hesabu 13:25-33 “Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku
arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa
wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao
na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika
nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali,
na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na
miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa
Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na
Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya
ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande
mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu
waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa
maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile
nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza,
ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu
warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao
Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”
Hesabu 14:1-3 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka
machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni;
mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri,
au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.Mbona Bwana anatuleta
mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa
mateka; je! Si afadhali turudi Misri? “
Woga
uliwachelewesha wana wa Israel kuirithi inchi ya Kanaani kwa miaka 40, woga ni adui mkubwa wa Imani, unapokuwa na
woga ni sawa kabisa na kukosa Imani, na unapokosa Imani ni vigumu kabisa
kumpendeza Mungu, huwezi kamwe kuzifurahia ahadi za Mungu na kuziona kwa
uhalisi katika maisha yako, woga unaua maono, woga unachelewesha ndoto zako
kutimia, Paulo mtume alifahamu kuwa kama Timotheo ataruhusu woga, kufungwa na
kutiwa gerezani hata kuuawa kwaajili ya Kristo, atakuwa kikwazo kikubwa kwa
injili kwake na kwa wale anaowaongoza kwa hiyo alimkumbusha kuwa Mungu hakutupa
Roho ya woga, hii pia inatukumbusha na sisi leo kuwa hatukupewa Roho ya woga
kwa jambo lolote lile linalotukabili, kwa kuwa Roho Mtakatifu sio Roho wa woga
yeye atatupa ujasiri kuendelea mbele na injili na kusonga mbele hata kama
tunakutana na magumu na vipingamizi na vitisho na hofu kamwe hatupaswi kuogopa
na tusonge mbele kwa sababu hatujapewa roho ya woga
2Timotheo 1:7-8 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya
upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala
usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya
Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”
Neno
woga linalotumika katika kifungu hiki, linasomeka kama “Deilia” katika lugha ya kiyunani likiwa na tafasiri ya fear au timidity ambalo tafasiri yake ni kukosa ujasiri, au kutikujiamini,
au kuwa na aibu, kutishika na kuingia hofu hasa unapojilinganisha na kile
unachokabiliana nacho ni kwaajili ya woga Israel walishindwa kumkabili Goliathi
hata alipkuwa akiwatukana
1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita,
nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka,
katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika
bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu
ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo
palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya
Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita
na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya
shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba.
Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati
ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha
mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia
ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli
akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si
watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana
nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua,
ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana
leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.nBasi Sauli na Israeli wote
waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”
Roho Mtakatifu ni
roho wa ujasiri
Moja
ya kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ndani ya mwamini, ni pamoja na kutuumbia Roho
ya ujasiri, kila mwanadamu ndani yake kuna aina Fulani ya hofu au woga,
tunaogopa kukosea, tunaogopa kushindwa, tunaogopa majaribio, tunaogopa kuchekwa,
tunaogopa watu, lakini pia tunaogopa magonjwa, tunaogopa njaa, tunaogopa mateso
na kadhalika, Lakini Roho Mtakatifu hutujengea ujasiri usiokuwa kawaida wa kuwa
tayari hata kuwa mashahidi (kufa) wa Yesu Kristo kwaajili ya injili
Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho
Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Warumi 8:15-18 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu;
bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;
na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo;
naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana
nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule
utakaofunuliwa kwetu.”
Roho
wa Mungu ndani yetu hutupa ujasiri wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu bila kujali
vikwazo vya aina yoyote tunavyokutana navyo, anatufanya tushuhudiwe ndani yetu
kuwa sisi ni wana wa Mungu na kuwa hatuna kitu cha kupoteza, ndani yetu, Paulo
anaona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kama ule utukufu
utakaofunuliwa kwetu, kwa sababu hiyo hatuogopi wala hatupaswi kuogopa kwa
sababu ndani yetu uko ujasiri kuwa sisi sio watu wa kawaida, tu wana wa Mungu
na kama Yesu alivyo ndivyo tulivyo, na kama ikiwa sisi tuko kama Yesu je
unaogopa nini hapa duniani?
1Yohana 4:17-19 “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na
ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA
SISI ULIMWENGUNI HUMU. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili
huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa
katika pendo. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.”
Tukijitambua
kuwa sisi ni nani katika Kristo na kuwa hatukupewa Roho wa woga bali ya nguvu na ya upendo, nay a kiasi hatutaogoa
lolote hata ijapotetemeka nchi, ijapobadilika milima, vijapotikisa vilindi vya
bahari bado hatutaogopa Roho Mtakatifu atatukumbusha kumtegemea Mungu,
atatukumbusha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu msaada uonekanao tele
wakati wa mateso, na sio hivyo tu anatukumbusha kuwa sisi ni wana wa Mungu na
kuwa hatuna cha kupoteza duniani, hatutaweza kupoteza ujasiri kamwe ikiwa tu
Roho Mtakatifu atapewa nafasi kubwa ndani yetu, Roho wa Mungu hutupilia mbali
hofu na kutusaidia kukabiliana na hali yoyote ile inayotakiwa kukabiliwa ndani
yetu! Na nje yetu mbele yetu na nyuma yetu!
Matendo 21:10-13 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja
jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo,
akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo
Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia
katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali
pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya
nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari
hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.”
Jinsi ya kutupilia
mbali woga.
Ni
muhimu kufahamu kuwa wewe sio matokeo ya mazingira wala sio matokeo ya kile
watu wanachokisema wewe ni matokeo ya kile Mungu anachokisema kukuhusu, kwa
msingi huo ili kutupilia mbali hofu na woga katika maisha yetu ya kila siku hatuna
budi kujitazama kwa kulitazama neno la Mungu linavyosema kutuhusu Neno la
Mungu linasema:-
Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada
utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka,
Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”
Isaya 41:10-13 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa
maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam,
nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu
yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na
kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu;
watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi,
Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi
nitakusaidia.”
Yoshua 1:9 “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa;
usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila
uendako.”
Neno
la Mungu linatueleza kuwa hatupaswi kuogopa wala hatupaswi kuwa na visingizio
wala sababu za kibinadamu, hakuna sababu zozote za kibinadamu zinazoweza
kuhalalisha sisi kutokutumiwa na Mungu kwa sababu zozote zile, wala hakuna
maumbile yoyote ya kibinadamu yanayoweza kuhalalisha Mungu kuto kutimiza kusudi
lake ndani yetu kwa sababu hiyo hakuna kisingizio huusani pale Mungu anapotutia
Muhuri kwa Roho wake mtakatifu!
Ni
kwa sababu hiyo Paulo mtume alikuwa akimtia moyo Timotheo kuweka mbali hofu na
aibu ili kumshuhudia Yesu Kristo kwa ujasiri, Kila mkristo anapaswa kujiandaa
na kuwa tayari kukabiliana na aina yoyote ya mateso, kukabuliana na vita vya
kiroho na kufungwa nahata kuuawa, au kupigwa na changamoto nyinginezo zote
kwaajili ya injili haya yote yanawezekana ikiwa tutamruhusu Roho Mtakatifu
ambaye ni Roho ya ujasiri na nguvu kutawala maisha yetu na hisia zetu.
Kila
mmoja wetu anamuhitaji Roho Mtakatifu katika wakati huu wa sasa ili atupe
ujasiri tusione haya wala tusiogope kumshuhudia yeye kwa ujasiri hata kama kuna
hatari zinayakabili maisha yetu ni nguvu za Roho Mtakatifu peke yake zinazoweza
kutusaidia na kutubeba kwa neema kuendelea kuwa na nguvu hata wakati ambapo
tunakabiliwa na magumu kwaajili ya injili, na kwaajili ya maisha ya kawaida Roho
Mtakatifu hutusaidia kuwa imara na kutokuogopa kikwazo chochote kinachosimama
mbele yetu kwani kila kitu kinawezekana alipo yeye na sio kwa akili zetu na
nguvu zetu, kwa hiyo kumbuka kuwa woga na hofu sio sehemu ya maisha yetu, woga
na hofu si sehemu ya mtu aliyejaa nguvu za Roho Mtakatifu badakla yake akija
juu yetu hofu zote na woga wa jambo lolote hutupiliwa mbali kabisa, leo hii
tunapoadhimisha sikuu ya Pentekoste kumbuka kuwa Mungu hakutupa roho ya woga! ,
Mwamini Mungu, kabiliana na lolote lile linalokuja mbele yako, kabiliana na
lolote lile kabiliana na kila changamoto na matisho, na mateso, na uhdia, na
adha, na lolote lile linaloonejkana kuwa kama kwazo au kuwa kama mlima mbele
yako jua ya kuwa kwa Roho wa Bwana litasambaratishwa na kuwa tambarare na
makusudi ya Bwana yatatimizwa maishani mwako!
Zekaria 4:6-7 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa
Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu,
asema Bwana wa majeshi. Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa
nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na
vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.”
Na Rev. Innocent
Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni