Jumapili, 22 Juni 2025

Malkia wa Sheba atasimama na watu wa kizazi hiki!


Mathayo 12:42 “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”




Utangulizi:

Moja ya wanawake maarufu katika Biblia ni pamoja na Malkia wa kusini (Malkia wa Sheba) Mwanamke huyu mashuhuri mwenye mikogo isiyokuwa ya kawaida amewahi kusifiwa na Yesu Kristo kama moja ya mwanadamu mwenye maamuzi thabiti ya kutafuta hekima kwa gharama yoyote ile bila kujali umbali, Mwanamke huyu alikataa ujinga na kuona kuliko kubaki na ujinga ni vema akasafiri kwenda mbali kwa gharama kubwa kwenda kuitafuta Hekima, Aliandaa maswali yake magumu na akasafiri mpaka Yerusalem makao makuu ya mji wa Israel kwaajili ya kusikia na kupokea Hekima kutoka kwa mfalme Suleimani, Hekima ambayo Suleimani alipewa na Mungu.

1Wafalme 10:1-13 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani. Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani. Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya Bwana, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo. Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.”

Leo basi tutachukua muda kujifunza kwa habari ya mwanamke huyu mashuhuri katika Biblia ili tuweze kujifunza na kufuata mfano wake wa kutafiti na kutafuta kujua habari za Yesu Kristo ambaye ni mkuu kuliko Suleimani kwa gharama yoyote, Ikiwa yeye alitoka pande za mwisho za dunia kwaajili ya kutafuta Hekima kwa Suleimani sisi kama watu wa Mungu tunajikumbusha kuitafuta hekima ya Yesu Kristo, tutajifunza somo hili Malkia wa Sheba atasimama na watu wa kizazi hiki kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Ufahamu kuhusu malkia wa Sheba.

·         Kujifunza kutoka kwa malkia wa Sheba.

·         Malkia wa sheba atasimama na watu wa kizazi hiki.


Ufahamu kuhusu malkia wa Sheba.

Malkia wa Sheba ni moja ya wanawake maarufu sana katika Biblia, mwanamke huyu alitawala katika eneo la Pembe ya Afrika hususani Ethiopia na sehemu za Asia ya kusini yaani uarabuni au Arabuni ya kusini, wakazi wa eneo lake waliitwa Sheba au Saba, eneo la utawala wake ulikuwa ni sehemu ya Uarabuni ya kusini na pembe ya Afrika ikijumuisha mataifa ya Yemen, Eritrea, Sudani, na Ethiopia, Malkia huyu ni maarufu kwa jina la “Bilqis” katika lugha ya kiarabu akiwa maarufu sana huko Yemen kwa jina hilo, na pia akijulikana kwa jina la “Makeda” katika nchi ya Ethiopia, hata hivyo Malikia huyu hakutajwa kwa jina lake katika Neno la Mungu yaani Biblia, lakini anatajwa tu kama Malikia wa kusini au Sheba au “Malkat Saba” kwa kiebrania na kwa kirumi “Basilissa Saba” katika Biblia ya Septuagint. Habari zake na kuvuma kwake katika historia amekuwa maarufu zaidi katika Taifa la Ethiopia zaidi kuliko Yemen ambao kila mmoja anadai ndiko alikotokea Malkia huyu, hata hivyo tafiti zinaonyesha kuwa waseba au washeba waliishi eneo lote la uarabuni na pembe ya Afrika kwa hiyo huenda utawala wake ulikuwa ni eneo lote la pembe ya Afrika na maeneo ya Arabuni ya kusini, Yemen na Oman yaani arabuni ya kusini ya leo. Lakini anatajwa zaidi katika eneo la Ethiopia ambako watoto wake walitawala badala yake, historia za kale za Kiethiopia  ziitwazo Kebra Negast zinaonyesha kuwa alitembelea Yerusalem na alizaa mtoto na Mfalme Suleimani na mtoto huyu aliitwa Meneleki I ambaye alikuwa baba wa wafalme wote wa Ethiopia wenye nasaba na mfalme Suleimani huko Ethiopia mpaka Mfalme maarufu zaidi Haile Selassie.  Malkia wa Sheba Anajitokeza katika maandiko akisafiri kwa ngamia, akiwa na zawadi ya viungo mbalimbali, dhahabu na mawe ya thamani akisafiri kwa safari ya msafara wa kifahari mpaka kwa Suleimani kwaajili ya kujifunza na kuuliza maswali magumu ya maisha kutoka kwake, vyovyote ilivyo Malkia huyu ana jambo muhimu la kutufunza ambalo ni kubwa kuitafuta Hekima pamoja na mambo mengine.

1Wafalme 10:1-10 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.”

Maandiko yanamtaja mwanamke huyu kwa sifa kubwa tano muhimu sana:-


1.       Alikuwa Mtafiti, mwenye kupenda kujifunza na mwenye busara.

 

Malikia huyu anasifiwa katika maandiko kama mwanamke ambaye licha ya kuwa kiongozi katika taifa lake yeye aliposikia habari za Hekima ya mfalme Suleimani, akapanga kusafiri kutoka nchi ya mbali, Yesu anaita pande za mwisho wa Dunia kwaajili ya kujifunza kutoka kwa Mfalme huyu mwenye hekima na tunaelezwa kuwa alikuwa amejipanga kwani alikuja na maswali magumu sana kwa Mfalme Suleimani ambayo alijibiwa yote na roho yake ikazimia. Napenda sana tafasiri ya kiingereza ya NIV inaeleza hivi “She came to Jerusalem to test him with hard questions” yaani malikia huyu alikuja Yerusalem kumjaribu (Suleimani) kwa Maswali magumu sana na maswali yake yote yalijibiwa.

 

2Nyakati 9:1-9 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga, na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana; roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.”

 

2.        Alikuwa mkarimu mtoaji:

 

Maandiko yamenukuu zawadi alizokuja nazo Malkia wa Sheba kwa  Mfalme Suleimani kuwa ni zawadi za kipekee na nyingi sana kiasi kwamba neno la Mungu linasema kuwa wala hakujawahi kuja tena wingi wa manukato sawa na yale ambayo malkia wa Sheba aliwahi kumletea Suleimani, utoaji huu unatufunza ya kuwa Malkia huyu alikuwa na moyo wa utoaji alikuwa na moyo wa ukarimu, hakutaka kumtembelea mtumishi wa Mungu, huku akiwa mikono Mitupu, alitambua ya kuwa kutokana na umaarufu aliokuwa nao Suleimani na utajiri wake hangehitaji kitu lakini Moyo wa malikia unaonekana tena katika eneo hili, wote tunajua kuwa Mungu ambaye ni mfalme wetu ana kila kitu na hahitaji lolote kutoka kwetu lakini Moyo wetu wa ukarimu kwake unaweza kupelekea yeye aturidhie, na kuipokea sadaka yetu kama alivyofanya Habili. Suleimani aliipokea zawadi na kumpa zawadi mara dufu kuliko zake

 

1Wafalme 10:13 “Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani. Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani. Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya Bwana, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo. Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.”

 

3.       Alikuwa mwenye bidii kuitafuta hekima.

 

Malikia huyu anasifiwa na Yesu Kristo kuwa alitoka pande za mwisho za dunia yaani katika ncha ya bara la Afrika kutoka mbali sana Ethiopia na kuja kuitafiti Hekima ya Suleimani, Yesu anasema Malikia huyu atasimama siku ya hukumu na watu wa kizazi hiki kuwahukumu kwa uzembe, kukosa bidii, moyo wa kujifunza wakati wao wamejaaliwa sana Hekima iliyokubwa kuliko ya Sulemaini, yaani mafundisho ya Yesu Kristo!

 

Mathayo 12:42 “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”

 

Maandiko yanatuasa kuitafuta hekima kwa gharama yoyote ile, kutokana na hekima kuwa na thamani kuliko madini yoyote Malikia huyu aliigundua siri hiyo na kujitajidi sana kuitafuta Hekima, alikuwa na bidii katika kutaka kufahamu na kujifunza tofauti sana na watu wa kizazi hiki, kama yeye alisafiri kwenda mbali sana kutafuta maarifa akiwa na maswali yake magumu je watu wa kizazi hiki unaweza kuwaandalia kila kitu lakini wakawa wavivu wa kusoma tu! Nyakati za leo hekima inapatikana karibu sana, Elimu na ujuzi na maarifa yako katika kiganja cha kila mtu leo, lakini watu hawana hamu wala kiu na shauku ya kujipa muda wa kusoma na kujifunza n ahata kufanya utafiti wa neno la Mungu tu, na unapoandaa mada na ikawa ndefu kwaajili ya kuweka mafafanuzi zaidi kizazi hiki hakitaki, kinafurahia kuperuzi, habari za udaku, koneksheni, siasa, michezo na burudani lakini kiu ya hekima ya kiungu na kuutafuta uso wa Mungu imekuwa ni ndogo sana, malikia anatufundisha kuyatafuta maarifa.

 

Mithali 4:5-7 “Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.”

 

4.       Alikuwa mcha Mungu.

 

Katika lugha yake kumhusu Suleimani malikia huyu anaonyesha ya kuwa alikuwa na ujuzi kuhusu Mungu na alikuwa mcha Mungu, Yeye hakuwa tu amevutiwa na Suleimani pekee bali alikuwa amesikia habari za Mungu wa Suleimani, maandiko yanaonyesha kuwa ni kwaajili ya jina la Bwana alikuja na sio hivyo tu bali pia alimtukuza Mungu wa Suleimani kutokana na umaminifu wake kwake na kwa watu wake Israel.  Na alitambua kuwa Mungu anawapenda Wayahudi.

 

1Wafalme 10:1 “Na malkia wa SHEBA ALIPOSIKIA HABARI ZA SULEMANI JUU YA JINA LA BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.”

 

2Nyakati 9:5-8 “Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. NA AHIMIDIWE BWANA, MUNGU WAKO, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.”           

 

5.       Alitambua kuwa Mungu anawapenda Israel.

 

Malikia huyu alipoona kuwa Mungu amewapa watu wake Israel kiongozi mzuri, mwenye hekima ya kupita kawaida alielewa wazi kuwa hukumu na haki zitafanyika vizuri, maamuzi mazuri ya kumpendeza Mungu yatafanyika kwa manufaa ya taifa la Israel, alielewa wazi kuwa Mungu anawapenda Israel, Mungu akilipenda taifa lolote lile atalisimamishia kiongozi mzuri, Mcha Mungu na mwenye kuchukia rushwa na mwenye kupenda haki na asiye na upendeleo ambaye ataamua mambo kwa haki, Lakini Mungu akitaka kuwahukumu ataachilia kiongozi mbaya awatawale, siri ya mafanikio ya taifa lolote lile kuinuka ni pamoja na taifa hilo kuwa taifa la haki.

 

Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.” Mithali 29:2 “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.”

 

Uwepo wa kiongozi kama Suleimani mwenye akili nyingi na hekima nyingi kulimfanya malikia wa Sheba kutafasiri kuwa Mungu anawapenda watu wake Israel, Kama Malikia wa Sheba angepata nafasi ya kumuona Bwana Yesu akiwa duniani angelisema Mungu ameupenda ulimwengu, kwa kuwa Yesu ni mkuu kuliko Suleimani. Na maamuzi yake na utawala wake ni wa haki

 

Kujifunza kutoka kwa malkia wa Sheba

Umuhimu wa kufanya utafiti – Malikia wa Sheba hakukubali kusikia tu kuhusu Suleimani bali yeye mwenyewe alitaka kuthibitisha na kujipatia ukweli wa Mambo na kuona kama ndivyo ulivyo, wakristo tunajifunza hapa umuhimu wa kufanya utafiti, unaposikia jambo, au mafundisho ya injili hata kama yanatolewa na muhubiri mkubwa kiasi gani ni lazima kufanya utafiti na kujiridhisha ili uone kama mambo ndivyo yalivyo, Utafiti unasaidia kujua mzizi wa jambo lolote iwe ni tukio, fundisho, majungu, masingizio na kadhalika na kutusaidia kupata suluhu ya mambo, Utafiti wa kina unatusaidia kujithibitishia mambo, kupata ushahidi, kujifunza, kupata taarifa, kudhibiti matukio na kadhalika, utafiti unasaidia kujenga usalama wa taifa, Malikia alikuwa na taarifa za kila kinachoendelea ulimwenguni, na sasa alitaka kujionea ukweli wa mambo na kujithibitishia kama hakuna chumvi katika hilo na kupata kweli iliyonyooka

1Wafalme 10:6-7 “Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. LAKINI MIMI SIKUZISADIKI HABARI HIZO, HATA NILIPOKUJA NA KUONA KWA MACHO YANGU; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.”          

Kwa bahati mbaya sana wakristo wa nyakati za leo hawana muda wa kufanya utafiti kuhusu neno la Mungu na mambo mengine na kujithibitiashia kama neno hilo ndivyo lilivyo na kwa sababu hiyo watu wengi leo ni rahisi kudanganyika, kumekuwa na mafundisho mengi potofu katika nyakati za leo, au mafundisho ambayo hayako sawa na kweli za neno la Mungu aidha kwa sababu ya watu wenye hila au kwa sababu ya kutafasiriwa vibaya kwa neno la Mungu bila nia ovu, hata hivyo jambo la kusikitisha ni kuwa watu wengi wa kizazi hiki wamekosa uungwana kwani hawayachunguzi mambo ili kupata uhakika wake Malikia anatufundisha kuwa ni lazima tufanye uchunguzi na utafiti, tusikimbilie haraka hara kuamini kila tunachofundishwa na kuitikia amina lakini tufanye utafiti, tujithibitishie wenyewe, na ikiwezekana kujionea wenyewe!

Matendo 17:10-11 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”

Je wewe huwa unafanya utafiti wa mambo na kujiridhisha kama ndivyo yalivyo? Ukifanya hivyo utakuwa na busara kama Malikia wa Sheba na watu wa Beroya, Yesu alipoagiza wakristo wawe wanafunzi hakutaka tuwe tu watu waamini bali alitaka tuwe shule tujifunze, tuwe na maswali yetu na tutafute namna ya kujibizana, tufanye utafiti na kujithibitishia mambo.Kila kitu duniani kinahitaji utafiti lakini Neno la Mungu linahitaji utafiti zaidi kwa ubora wake na viwango vyake

Uthubutu wa kufanya mambo makubwa – Malikia wa Sheba alithubutu kusafiri safari ndefu sana kwaajili ya kutafuta maarifa na Elimu, Lakini pia kwaajili ya jina la Mungu na kwaajili ya kuitafuta kweli, Neno uthubutu katika kiyunani ni “Afthentikόtita” kwa kiingereza “Authenticity” maana yake ni kanuni ya kujithibitishia, kujihakikishia, kutaka kujionea, kutaka kuweka mambo sawasawa, Mtu anayetafuta hekima na maarifa anataka kuweka mambo sawa, Malikia alithubutu, tunaagizwa katika maandiko kuitafuta sana na kuishika sana Elimu, hekima na maarifa na kuwa na bidii hata kuthubutu kufanya lolote tukitafuta mambo makubwa kwaajili ya Mungu. Malkia alisafiri kutoka mbali sana huu ni uthubutu, wa kufanya mambo makubwa kwaajili ya utukufu wa Mungu na ndio uthubutu uliosifiwa na Bwana Yesu Je wewe unathubutu?

Mathayo 12:42 “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”

Alikuwa mkarimu – Maandiko yanatufundisha kuwa wakarimu, kanuni mojawapo ya mafanikio ya kibiblia ni kutoa au kuwapa watu vitu, na tunapofanya hivyo Mungu hutubariki zaidi, hakuna kanuni ya kumpangia mtu katika utoaji msingi wa agano jipya unawataka watu kutoa kwa ukarimu, au kwa kadiri ya neema waliyojaliwa na Bwana, kwa hiyari na kwa moyo mkunjufu, utoaji na ukarimu ni sehemu muhimu sana ya kuonyesha ubora wa mtu! Upendo wake na kujitoa kwake.

Matendo 20:34-35 “Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

Ni ukweli ulio wazi kuwa kanuni hii ya mafundisho ya Bwana Yesu ilifanya kazi kwa Malikia wa Kushi, kwani ni ukweli usiopingika kuwa wakati anajitoa na zawadi nyingi sana kwa mfalme Suleimani, Mfalme alimpa yeye zawadi zilizo nyingi zaidi kuliko alizotoa yeye, na kututhibitishia ukweli wa lile neno apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu

2Nyakati 9:9-12 “Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba. Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani. Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda. Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.”

2Wakorintho 9:6-7 “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.”                                             

Alimwabudu Mungu wa Israel – Malikia wa Sheba alimuabudu Mungu wa Israel, yeye alitambua wazi kuwa Mungu amempa Suleimani ile hekima kwaajili ya utukufu wake na kwaajili ya upendo kwa watu wake hivyo baada ya kujithibitishia ukweli wa Mambo alimuabudu Mungu wa Israel na kumhimidi. Hakuna jambo muhimu na kubwa sana duniani kuliko yote kama kumuabudu Mungu.

2Nyakati 9:5-8 “Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.”

Malkia wa Sheba atasimama na watu wa kizazi hiki.

Luka 11:31Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani.”

Yesu alimsifia na kumtaja malikia wa Sheba ya kuwa atasimama siku ya hukumu na watu wa kizazi hiki na kuwapa hatia kwa sababu yeye alitoka mbali kwaajili ya hekima ya Suleimani ili hali sisi tunaye Yesu na mafundisho yake ambaye ni mkuu kuliko Suleimani, Sifa kubwa sana aliyo nayo malikia huyu ni moyo wake wa kuitafuta hekima bila kujali kuwa ataipatia wapi lakini alilazimika kusafiri safari ndefu sana ilhali yeye ni mwanamke lakini hakujali kama kuitafuta hekima hiyo kungemgharimu mambo mangapi.

Wako watu wanasikia ujumbe wa Yesu Kristo ambao unahubiriwa kila iitwapo leo, wanaona na kusikia mafundisho kuhusu maswala mbalimbali ya kweli za injili lakini wanapuuzia na hawajali, Malikia aliona kuwa habari za Mungu kupitia Suleimani zilikuwa ni za Muhimu kuliko mali, aliamua kuiacha inchi yake kwa Muda kwa sababu ya kujifunza, aligundua kuwa Mungu ndiye chanzo cha Hekima yote kwani alielewa kuwa hata Hekima aliyokuwa nayo Suleimani inatoka kwa Mungu alikubali kuwa Mungu anawapenda wayahudi, alimtukuza Mungu na kumuabudu.

1Wafalme 10:9Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.”

 

Hitimisho:

Malikia wa Sheba ni miongoni mwa wanawake mashuhuri wa kibiblia, alikuwa ni mwanamke mwenye ujasiri, uthubutu, busara hekima na uaminifu, Yesu alimthibitisha kwa neno lake na kumtumia kama mfano wa kuigwa na kutuonya kwamba ni lazima tumsikilize Yesu ambaye yeye ni Mwana wa Mungu na kwa kumsikiliza Kristo tunajiokoa na hukumu ile ijayo, ni lazima tufanye kila jitihada kujifunza na kuitafuta kweli kama alivyofanya Malikia wa Sheba, tuache uvivu wa kujifunza neno la Mungu, tuache uvivu na kutokuacha kuhudhuria ibada, tuutafute uwepo wa Mungu na kujifunza kutoka kwake kwa gharama yoyote, tumtafute Yesu, tumtafakari, tujifunze kuhusu Yesu na wakati mwingine tuingie gharama hata za kifedha kuyatafuta maarifa sahihi kuhusu Mungu na Neema ya Mungu itatufunika na uwepo wake tutauona na kumhimidi Mungu kwa upendo wake mkubwa kwetu.

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: