Jumatano, 4 Juni 2025

Kwa hiyo hatulegei!

 

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika dunia hii iliyojaa changamoto, maumivu, majaribu, mateso, uonevu, dhuluma, kukosekana kwa haki, wivu, majungu na kuumizana, maneno ya kuumiza, na vita vya kila aina ni rahisi sana kwa baadhi ya watu hususani wale walio na moyo wa unyonge kulegea na kukata tamaa, na wakati huohuo kupoteza tumaini kwa sababu ya kuwako kwa vikwazo mbalimbali katika maisha, Paulo mtume yeye anasema na kutangaza kwa ujasiri “Kwa hiyo Hatulegei” ujumbe wake Paulo mtume kwa kanisa ni ujumbe wa matumaini na ushindi na nguvu kwa kila anayemwamini Yesu Kristo Bwana wetu, kwamba sisi ni watu wa tofauti na kamwe hakuna awaye yote aliyemwamini Yesu anayeweza kukata tamaa, au kuzimia moyo “Kwa hiyo hatulegei” tunaendelea kukaza mwendo kwa kadiri tunavyokutana na changamoto na majaribu ya namna mbalimbali.

Wafilipi 3:12-14. “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

Leo basi tutachukua muda kujifunza sababu zilizopelekea Paulo mtume kuelezea “Kwa hiyo Hatulegei” na tutajifunza ujumbe huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo yafuatayo:-

·         Maana ya kutokulegea.

·         Sababu za kutokulegea.

·         Kwa hiyo hatulegei.

Maana ya kutokulegea:

2Wakorintho 4:15-17 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana

Neno kwa hiyo hatulegei katika Biblia ya kiyunani linasomeka “dio ekkakeō ou”  kwa hiyo neno hatulegei kwa kiyunani ni “ekkakeō”  ambalo kwa kiingereza linaweza kutafasirika to become weak, to fail, to faint, to become weary, or to fail in heart, or we do not give up. kwa hiyo kwa Kiswahili maana yake hatuwi dhaifu, hatushindwi, hatuzimii, hatuchoki, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo.

Maana yake hata pamoja na magumu kiasi gani tunayokutana nayo, hata pamoja na dhiki kubwa tunayokutana nayo, hata pamoja na changamoto kubwa tunazokutana nazo, hata pamoja na vipingamizi vikubwa tunavyokutana navyo iwe ni katika imani, iwe ni katika huduma, iwe ni ugumu katika jambo lolote unalokutana nalo, vyovyote vile visisitishe huduma yako, wokovu wako, ndoa yako biashara yako, juhudi zako katika masomo, uwezo wako wa kumtumainia na kumtegemea Mungu, utumishi wako, juhudi yako ya kupambana na umasikini, jitihada zako za kujikwamua, mpango wako wa biashara, mpango wako wa kilimo, mpango wako wa uwekezaji, mpango wako wa ufugaji, mpango wako wa maendeleo, na msimamo wako katika Bwana haupaswi kuzimia kwa sababu zozote zile kwa sababu ya ujuzi wako na maarifa yako ya kina kuhusu Mungu na kazi yake anayoifanya ndani yako! Kamwe Mungu hawezi kukuangusha! Kwa hiyo hatulegei

Hakuna jambo baya sana kama kuzimia, kukata tamaa, kuvunjika moyo, kuchoka, au kuwa dhaifu, adui mkubwa sana wa mwanaridha yoyote yule ni pamoja na kuzimia, au kulegea, kuvunjika moyo, kuogopa, wasiwasi na mashaka, na kufikiri kuwa umezidiwa, wakati wowote mwanadamu anapokata tamaa anazuia maendeleo yake, anatengeneza ugumu wa kushinda vikwazo na kutokusonga mbele mtu awaye yote aliyeokoka hapaswi kamwe kulegea, kulegea na kukata tamaa na kuzimia moyo kunaashiria kuwa uweza wako na nguvu zako ni chache, Jeshi lolote lile halina haja na Askari ambaye anazimia moyo au kukata tamaa.  Mithali 24:10 “Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.”

Kulegea kunafananishwa na mwanamke aliyebeba mimba kwa miezi tisa akipitia shida na taabu mbalimbali kisha akaanza kusikia uchungu alafu muda wa kujifungua unafika wakati anataka kujifungua mwanamke huyu anachoka kusaidia kumsukuma mtoto ili atoke huo unakuwa wakati mgumu sana, unakuwa ni wakati wa dhiki, unakuwa ni wakati wa aibu, kuwa mwanamke huyu amebeba mimba lakini ameshindwa kuzaa, mwanamke huyu atashutumiwa kuwa alipoteza ujasiri na nguvu wakati wa kujifungua, kwa hiyo ni lazima Mwanamke asukume zaidi ili aweze kujifungua kama hakuna nguvu ya kuweza kujifungua maana yake hakuna nguvu ya kushinda kwa hiyo kushindwa kunakuja, aibu inakuja, fedheha inakuja, na jambo gumu zaidi linakabili:-

Isaya 37:1-3. “Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.”

Kwa hiyo kulegea maana yake ni kuzimia, ni kukaribia kushindwa ni kukosa msaada, ni kuchoka, ni kupoteza nguvu ni uwezekano mdogo wa kushinda vikwazo na changamoto mbalimbali zinazokukabili, kwa hiyo watu wa Mungu au watu waliookoka hawalegei, hatukati tamaa, hatuvunjiki moyo, wala hatusitishi juhudi wakati wa mambo magumu tunasonga mbele kama askari wema na waaminifu walioko vitani na ziko sababu kadhaa za kutufanya tusilegee!

Sababu za kutokulegea.

1.       Kwa sababu tunaongezewa neema – Mst 15

 

2Wakorintho 4:15 “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.”

 

Mtu wa Mungu anapopita katika changamoto za aina mbalimbali kwa kadiri ya  mateso na majaribu yanavyozidi Mungu aliyemfufua Bwana Yesu anatuongezea neema ya kupita kawaida ya kutusaidia kushinda majaribu, kwa hiyo ndani yetu moyo wa kukata tamaa unabomolewa na Neema inazidi na kutuinua juu zaidi, tunapewa neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

 

Yakobo 4:5-6 “Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

 

Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

2Wakorintho 12:8-10 “Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.”

 

2.       Kwa sababu mtu wa ndani hachakai        Mst 16

 

2Wakorintho 4:16 “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.”

 

Paulo mtume anasema hatulegei wala hatuishiwi nguvu wala kukata tamaa kwa sababu utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku, wakati kila mkristo anapokutana na majaribu na mateso na machungu ya aina mbalimbali utu wetu wa ndani unapata uzoefu na mabadiliko na ukuaji wa kiroho, kwa hiyo hata kama kwa nje tunaonekana kuchoka, kuugua na kuchakaa utu wetu wa ndani unafanywa upya na kuimarishwa katika imani kupitia uhusiano wetu na Mungu, Imani, maombi, neno la Mungu na uzoefu wa kiroho tunaoupata kila iitwapo leo, wakati wa majaribu unachangia kwamba akili zetu zinakuwa, ujuzi wetu unaongezeka, tunazidi kumjifunza Mungu kutoka katika pito moja kuelekea katika pito lingine  na kama ni hivyo sasa kukatatamaa kunatokea wapi, kuchoka kunatokea wapi, kupoteza nguvu kunatokea wapi, unafungwa gerezani, magereza inaachia, unapigwa mawe mpaka kufa unafufuliwa na unaendelea na injili, unapigwa bakora na kuteseka unazidi kuongezewa neema, unaviziwa getini unashushwa kwenye kikapu na injili inaendelea, utachokaje kwa mfano  unapata ujuzi unapata hekima unajengewa ujasiri na unagundua kuwa hakuna kitu kinaweza kukutenga na wewe na upendo wa Mungu

 

Warumi 8: 38-39 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

3.        Kwa sababu mateso ya sasa ni mepesi na ya muda tu. Mst 17

 

2Wakorintho 4:17 “Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;”      

 

Paulo mtume anayaona mateso ya sasa na dhiki hizi ni nyepesi na za muda tu na kuwa dhiki hizi zinatutengenezea utukufu mkubwa sana na wa milele, watu waliookoka ni askari, askari ili awe na utukufu mkubwa na cheo kikubwa sana lazima akasotee katika chuo cha maafisa wa kijeshi ili kuongezewa nyota begani mwake, wakati wote dhiki huwa zinatujaribu na kutukomaza kupata ujuzi wa kiroho na kutufanya tuwe imara zaidi kwa sababu hiyo hatulegei tunapata uzoefu kutoka kwa dubu na simba ili kumpiga Goliathi.

 

Ayubu 23:10-12 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,”

 

1Petro 1: 6-7 “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”

 

Paulo mtume alikuwa anaangalia hitimisho kubwa lenye utukufu mwingi baada ya dhiki hizi za muda mfupi, Kule mbinguni Mungu atamtukuza kila mmoja kwa kadiri ya neema na mapito aliyoyavumilia kwa sababu hiyo hatupaswi kuangalia hivi vinavyoonekana ambavyo ni vya muda mfupi bali tuviangalie vile vya milele, mateso na dhiki na maumivu ni vitu vinavyoonekana lakini thawabu na utukufu mkuu Mungu aliotuwekea ni kitu kisichoonekana kwa sasa lakini katika uzima wa milele kuna mambo makubwa yanakuja mbele yetu.

 

2Wakorintho 4:18 “tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.”

 

4.       Kwa sababu huduma hii tumeipata kwa rehema Mst 1

 

2Wakorintho 4:1 “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei;”

 

Mungu aliyetuita katika wokovu na kisha kutupa wito wa kumtumikia ametuheshimu sana ni rehema kwa wewe na mimi kufanywa watumishi wa Mungu, angeweza kumtumia mwingine au hata kuwatumia malaika ambao ni wajumbe wake, lakini kwa rehema kubwa ametupa sisi huduma hii  tunawezaje kulegea? Tunawezaje kukata tamaa, Mungu ametukabidhi sisi kazi ya kuieneza injili ametupenda ametuhurumia ametuheshimisha tupeleke ujumbe wa Mwanae kwa watu wote, huduma hii ni ya rehema tu si kwa saababu tunastahili kwa hiyo kwa vipi tukate tamaa, kwa vipi tuzimie, kwanini tulegee?  Kama ni Mungu ameturehemu tumtumikie ni yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa chanzo cha nguvu zetu , kwa sababu hiyo ni lazima tushinde vizuizi vyote na changamoto zote na kamwe tusizimie moyo, kazi yetu ni kazi njema na ni kazi ya Mungu kwa hiyo tusizimie, Yeye aliyetutuma ana mamlaka yote Mbinguni na duniani kwa sababu hiyo hatupaswi kamwe kuogopa!

 

Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”

 

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”         

 

Kwa hiyo hatulegei.

Ni muhimu maneno haya yakawa kauli mbiu katika utumishi wetu na maisha yetu ya wokovu, kila wakati unapohisi kuchoka au kuvunjwa moyo ni lazima tukiri kuwa Hatulegei, hatuzimii moyo hatuanguki, tunasonga mbele, kutokulegea kwetu ni ishara ya kuwa tunamjua Mungu kwa kina na mapana na marefu, na tunamwamini, Paulo alipokuwa anasema kuwa hatulegei yeye alikuwa anajua hakunamtu aliyepitia mateso kama yeye lakini hakuwahi kulegea hata siku moja.

2Wakorintho 11:23-33 “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?  Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.”

Mungu hatatuacha katika mapito ya aina yoyote ile aliahidi kuwa atakuwa pamoja nasi na kwa sababu hiyo atatutia nguvu kwa hiyo hata kama tunazingirwa na mazingira magumu kiasi gani hatutaangamia, wala hatutakata tamaa, kila jaribu linao mlango wa kutokea.

2Wakorintho 4:6-10 “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo. Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.”

Kwa hiyo Hatulegei.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: