1Timotheo 3:11 “Vivyo hivyo wake zao na
wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.”
Utangulizi
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
mwili wa Kristo, Mchungaji ana nafasi ya muhimu sana katika kuongoza na
kufundisha huku akililisha na kulichunga kundi la kondoo wa Bwana, lakini hata
hivyo ni muhimu kuelewa kuwa Mchungaji sio kisiwa peke yake, anahitaji msaada
wa wale walio karibu naye, na miongoni mwao ni Mama Mchungaji. Mama Mchungaji
ni mwenzi wa Mchungaji na ana nafasi ya kipekee sana katika kuisaidia huduma ya
mumewe kusimama au hata kudhoofika, Leo basi tutachukua muda kujifunza jinsi
mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma ya kichungaji kudumu kwa mafanikio au
jinsi tabia zake zinavyoweza kuathiri huduma vibaya, tutajifunza somo hili
Huduma ya kichungaji na Mama Mchungaji kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Nafasi ya Mama Mchungaji katika huduma ya
Kichungaji
·
Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kudhoofisha
huduma.
·
Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma
kusimama.
Nafasi ya Mama Mchungaji katika huduma ya Kichungaji.
Ni muhimu kufahamu kuwa wake wa
viongozi wa kiroho wanahusika moja kwa moja kwa namna moja ama nyingine na kwa
njia tofauti katika kazi ya Mungu, Mwanamke anayekuwa mke wa mtumishi wa Mungu
ana athari ya moja kwa moja katika huduma ya mumewe aidha kuifanya huduma hiyo
kuwa na mafanikio makubwa na au kuifanya huduma hiyo kusambaratika, kwa bahati
mbaya wakati mwingine watumishi wa Mugu wameandaliwa kwa muda mrefu na kwa muda
wa kutosha kwaajili ya kuuhudumia mwili wa Kristo. Wakati mama wachungaji wengi
hasa hapa Afrika, wameachwa wakiwa hata hawaitambui nafasi kubwa na muhimu
waliyo nayo katika utumishi wao na waume zao, unapokuwa umepata nafasi ya
kuolewa na Mchungaji, aidha kabla au baada ya yeye kuitwa katika huduma basi
mama Mchungaji unapaswa kutambua kuwa Mungu hajamtuma mumeo peke yake na kwa
sababu hiyo wote wawili mnahusika katika kumtumikia Mungu.
Luka 10:1-3 “Basi, baada ya hayo Bwana
aliweka na wengine, sabini, AKAWATUMA WAWILI WAWILI wamtangulie kwenda kila mji
na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi,
lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda
kazi katika mavuno yake.Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya
mbwa-mwitu.”
Muhubiri 4:9-12 “Afadhali kuwa wawili
kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka,
mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala
hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto;
lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? Hata ikiwa mtu aweza
kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu
haikatiki upesi.”
Kila mama Mchungaji anapaswa
kuelewa kuwa Mungu amewaita wote wawili, hapa haimaanishi kuwa ni lazima kila
mama mchungaji ajihusishe moja kwa moja na huduma ya madhabahuni hapana, lakini
ufahamu wa mama Mchungaji kuhusu umuhimu wa huduma ya kichungaji na nafsi yake
kama msaidizi wa mumewe una nafasi kubwa sana katika kuifanya huduma ifanikiwe,
umoja wa wanandoa wenye utumishi ndani yao una mafanikio makubwa sana katika
ulimwengu wa roho kuliko yanapokuwepo mafarakano kati yao, na shetani analijiua
hilo vizuri, watu wawili wanapoungana na kukubaliana na kutengeneza kemia ya
umoja katika ulimwengu wa roho hutokea mambo makubwa sana, Maandiko wakati wote
yanaonyesha nguvu kubwa wanapohusika wawili katika utumishi ona
Kumbukumbu 32:29-30 “Laiti wangekuwa na
akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao. Mmoja angefukuzaje watu
elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama
Bwana asingaliwatoa?”
Mathayo 18:19-20 “Tena nawaambia, ya kwamba
wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba,
watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu
wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”
Kama mama Mchungaji na Mchungaji
hawatakaa vizuri na kuwa kitu kimoja na kupatana, maombi yao yatazuiliwa na
mafanikio yao katika huduma yataanza kudhoofika na kuathiri kazi za kichungaji
1Petro 3:6-9 “Kama vile Sara alivyomtii
Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa
kwa hofu yo yote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa
mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya
uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia
moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu,
wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye
kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi Baraka”
Kila mama Mchungaji awe mwenye
huduma au asiye na huduma kwa maana ya wale wanaohudumu Madhabahuni na hata
wale wasio na huduma ya madhabahuni, lakini kile kitendo tu cha kuwa mke wa
Mchungaji kinamaanisha kuwa Mungu amekusudia jambo kwaajili yako, Mungu
amekuita uwe na msaada kwa kazi ya mumeo, kwa hiyo ni muhimu ukajitambua hivyo
na kusaidia wito wa Mumeo:
1. Wewe ni Msaidizi katika huduma.
Mwanzo 2:18 “ BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu
awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”
Mungu alimuumba
mwanamke kama Msaidizi wa mwanaume, na hii inamaanisha ni katika kila kusudi
ambalo mumeo ameitiwa wewe ni msaidizi wake, kwa hiyo kama mumeo ameitwa katika
huduma wewe ni msaidizi wa huduma hiyo, kama mumeo ameitwa kwenye huduma ya
kichungaji basi mke wa Mchungaji au mama mchungaji anahusika kwenye huduma hiyo
moja kwa moja na anaweza kuwa msaada
mkubwa kwa Mchungaji au mume wake na kuleta faraja kubwa sana kwa ushauri,
maombi, utulivu na busara, na kadhalika, kwa bahati mbaya wako baadhi ya mama
wachungaji hawaungani na utumishi waliopewa waume zao na wao huishia kubweteka
au kuwa mzigo wakifikiri kwamba hawana wito au hawakuitwa katika huduma hiyo na
hawahusiki, na ni kazi ya mumewe na wao kuishi kama watu waendao kushoto
ilihali waume zao wakienda kulia, iwapo ma Mchungaji atabweteka kiroho atakuwa
mzigo na kama ilivyokuwa Eva ataleta mauti kwake na kwa mumewe na ama shetani
atapitia kwa mama Mchungaji na kusababisha madhara makubwa kihuduma.
Mwanzo 3:6 “Mwanamke
alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa
kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na
mumewe, naye akala.”
1Timotheo 2:13-14 “Kwa
maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa,
ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”
Prisila alikuwa
ni mwanamke aliyekuwa msaada mkubwa sana kwa mumewe Akila pamoja na mtume Paulo
katika kazi ya injili, Yeye alishiriki moja kwa moja sambamba na mumewe na kuwa
na mchango mkubwa sana katika mwili wa Kristo.
Matendo 18:24-26 “Basi
Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika
Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia
ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha
kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena
kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua
kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”
2.
Wewe
ni msaidizi katika tabia na mwenendo.
1Timotheo 3:11 “Vivyo
hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu
katika mambo yote.”
Tabia ya mama
mchungaji mke wa Mchungaji inaathiri kwa kiwango kikubwa sana kazi ya huduma na
injili, kila mama Mchungaji akijitambua na kujenga japo mazingira ya Amani ili
kumpa mchungaji namna nzuri ya kutumika bila ya mgandamizo wa mawazo basi
Mchungaji atakuwa na nguvu za kutosha kwaajili ya huduma
Mama Mchungaji
mwenye Hekima atakuwa anajua wajibu mkubwa sana alionao mumewe na kwa sababu
hiyo hata kama liko jambo atamueleza mumewe kwa hekima ya kiungu na kujitahidi
kumuepushia migogoro isiyo na maana ya nyumbani kwa masalahi ya ufalme.
Kila mama
Mchungaji ni lazima aelewe kuwa tabia na mwendo wake una maana pana sana katika
huduma ya kichungaji, wajibu wa kuishi maisha ya maombi, kuwa kielelezo, kuwa
mfano wa utii na utakatifu unaanzia nyumbani na mama Mchungaji anapaswa kuwa wakwanza
kuigwa kwa wamama wote na hata mabinti, yeye anatakiwa kuwa kielelezo katika
njia ya wokovu, na hapaswi kusema shauri zake kwani tumeitwa wote?! Mwenye
huduma si ni yeye tu atajijua mwenyewe! Kushindwa kwa mama wachungaji kuwa
kielelezo kikuu katika kanisa la Mungu ni kupunguza mamlaka ya kichungaji
katika usimamizi wa familia na nyumba nyingi zilizoko katika kanisa lake na
zile ambazo Mungu amempa ili kuwatunza.
1Timotheo 5:2-5. “Basi
imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na
busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea
ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye
kupenda fedha;mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika
ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje
Kanisa la Mungu?)”
3.
Wewe
ni msaidizi katika kutia moyo
Wito wa
kichungaji ni wito wa ajabu sana kuna wakati katika huduma za kichungaji
unaweza kukutana na mambo magumu sana kuna majaribu, kuna upweke, kuna vitisho,
kuna hatari, kuna kusakamwa, kuna kuchanganyikiwa, kuna kutokufurahishwa na
kutokuridhika, kwa hiyo Mchungaji anahitaji kutiwa moyo na mtu aliye karibu, na
mtu huyo ni mke wake, kwa kweli mtu anayeweza kuuinua moyo wa mchungaji ni mke
mwenye upendo, unyenyekevu na uadilifu na mwenye uvumilivu mke wa jinsi hii anaweza
kusaidia kuutimiza vema wito wa kichungaji na mama mchungaji ndiye mtu sahihi
wa kufanya hayo, itakuwa inasikitisha sana kama ni mtu wa pembeni ndiye
atagundua kuwa mchungaji amechoka, anahitaji kunywa maji anahitaji kupewa pole na
hata kutiwa moyo, au kama tai yake imekaa vibaya, ameumizwa, na kadhalika kwa
kweli hilo lilitakiwa kuwa labda jicho la tatu lakini jicho la kwanza
lilitakiwa kuwa mama Mchungaji mwenyewe, Maandiko hayajawahi kueleza moja kwa
moja wajibu wa mama Mchungaji wa kihuduma, lakini ukweli unabaki wazi kuwa ni
mama Mchungaji ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuamua huduma ya mumewe iwe bora kwa
kiwango gani na anaweza kufanya hivyo hata kwa kuwa mnyenyekevu na mtii kwa
mumewe kwa sababu niliaminilo ni hili kuwa kama Mungu amemuita mume katika
huduma anamuita katika ukamilifu wake yaani amemuita na mkewe hivyo utii wako
kama mama mchungaji ni wa muhimu kwa mumeo na utumishi wake kwa masalahi ya
ufalme wa Mungu.
Waefeso 5:22-24 “Enyi
wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha
mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini
kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika
kila jambo.”
4.
Wewe
ni msaidizi katika maombi.
Kila mama
Mchungaji ni anapaswa kuwa mwana maombi namba moja katika kuitia nguvu huduma
ya kichungaji na kuitegemeza kwa maombi, mama Mchungaji anapaswa kuwa mwanamke
wa maombi au mwanamke muombaji, kuna uwezekano wa kuwepo kwa watu wengine ambao
Mungu anaweza kuwainua, kuiinua huduma ya kichungaji hata hivyo hilo sio swala
la kutiliwa maanani ukilinganisha na nafasi aliyo nayo mama Mchungaji ombea
huduma, mwenendo na maisha ya mumeo, lolote gumu kama likimpata wewe utakuwa
mtu wa kwanza kuumia na wengine watafuata, kwa hiyo kuna umuhimu kwako kuwa
muombaji.
Yeremia 9:17-20 “Bwana
wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje;
mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; na wafanye haraka na
kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike
maji. Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa!
tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao
yetu. Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee
neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani
yake kulia”
Waefeso 6:18 “kwa
sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na
kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”
Neno la Mungu
linawatambua wanawake kama watu wenye uwezo mkubwa sana wa kulia na kuomboleza,
kuliko hata wanaume na kama kuna wanawake wanapaswa kuwa waombaji ni wazi kuwa
mama wachungaji wanapaswa kuwa wa kwanza, maombi yao yana uwezo mkubwa wa
kuibeba huduma ya waume zao na kusababisha ufanisi mkubwa wa kihuduma.
5.
Wewe
ni Mlinzi wa Mchungaji kwa Mungu na wanadamu.
Yeremia 31:22 “Hata
lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya
duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.”
Nyakati za zamani
ilikuwa ni wajibu wa Mwanaume kumlinda mkewe, na ndivyo ilivyo Mume ni mlinzi
wa mkewe, Mungu alikuwa anazungumza na Israel kwa sababu yeye alikuwa mlinzi
wao, alikuwa akijisikia wivu sana Israel walipokuwa wanamuacha, alikuwa hataki
wamuache aliwalinda na kuwatetea lakini Mungu alisema ataumba jambo jipya yaani
sasa Israel itaona wivu kuachwa na Mungu, watampenda Mungu kiasi ambacho wao
ndio watakuwa walinzi wa Mungu wakiwa hawataki tena kufanya mabaya ili Mungu
asije akawaacha ni katika dhana kama hii Mwanamke anawajibika kumlinda mumewe,
uwe sambamba naye, usipendelee kumuacha acha, wako wanawake wengine hukosa
hekima na kuwacha waume zao mara kwa mara, hawashikamani na na waume zao wala
hawaambatani nao, Mumeo anapokuwa ni mtumishi wa Mungu basi ujue ya kuwa wewe
una wajibu mkubwa kwa kumlinda ili awe salama kwa Mungu na kwa wanadamu, mlinde
kwa kumkumbusha wajibu wake na maswala muhimu anayopaswa kuyatekeleza kwa
Mungu, lakini mlinde pia dhidi ya wanadamu wanotaka kumuharibia huduma,
mkumbushe mumeo wajibu wake kwa Mungu, mwamshe katika kuomba, hakikisha anakula
kwa wakati, kuwa karibu naye katika huduma na wakati anapofanya ushauri wa
kichungaji kama muhusika haoni shaka kujieleza chini ya uwepo wa mama Mchungaji,
ambatana naye anapokwenda kutembelea washirika, hakikisha hafanyi jambo
litakalopelekea apigwe na Mungu, Sipora mke wa Musa alimuokoa Musa kwa kufanya
wajibu ambao Musa alikuwa ameupuuzia, Musa hakuwa amewatahiri watoto wake kwa
hiyo Mungu alimkasirikia Musa na kutaka kumuua kwa kutokulishika agano la
tohara, Lakini Sipora kwa haraka alijua nini kifanyike na kumuokoa Musa asiuawe
na Mungu.
Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa
walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo
Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga
miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi
akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya
kutahiri.”
6.
Wewe
ni mshiriki mwenza katika huduma.
Mama Mchungaji
kama mshiriki mwenza katika huduma atashirikiana na Mchungaji katika huduma
mbalimbali za kikanisa, anaweza kuwa sio muhubiri, lakini kama mchungaji
anafundisha wana ndoa, au kama wanawake wanachama chao kanisani, mama Mchungaji
anaweza kuhusika kwa namna fulani katika utelekezaji wa majukumu hayo aidha Ni
muhimu kwa mama mchungaji kuwa mstari wa mbele katika mahudhurio ya ibada,
kuwahi ibada, kusaidia usimamizi wa kanisa katika nyanja mbalimbali na maswala
yahusuyo wanawake na watoto, usafi wa madhabahu na maswala mengineyo kwa kadiri
ya neema ya Mungu, lakini zaidi sana kufundisha wanawake wa makundi yote
kanisani na wanawake wachanga
Tito 2:3-5 “Vivyo
hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji,
wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake
vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye
kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao
wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”
Aidha mama
Mchungaji anapaswa kuishi maisha matakatifu sawasawa na Mchungaji, kumekuwa na
changamoto kwa watumishi wengi wa Mungu kuwa wa kiroho zaidi huku upande wa
pili mke akiwa wa mwilini sana, matokeo yake wakati Mchungaji anashinda ofisini
akiwa na shughuli (busy) na maombi na
huduma mama wachungaji wao wanabaki kuchati, na kupiga umbeya na kubadilishana
mawazo na watu wasio faa, kufuatilia tamthilia, na kupeana ubuyu, hivyo kuleta
tofauti kubwa ya ukuaji wa kiroho kati
ya mume na mke, wakati Adamu akiwa
anashughulika (busy) mahali Fulani, Eva alikuwa akichati na shetani na
kushawishiana kula matunda aliyokataza Bwana kwa vyovyote vile kulikuwa na hitilafu
Fulani wakati Eva alipokuwa anachati na shetani ni wazi kuwa Adamu huenda
alikuwa mahali akichati na Bwana au kwenye huduma nyinginezo,wangelikuwa pamoja
shetani angekimbia.
Mwanzo 3:1-4. “Basi
nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu.
Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti
yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini
twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema,
Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika
hamtakufa,”
Elizabeth mama
yake Yohana mbatizaji aliishi kwa haki na utauwa sawasawa na Mumewe Zekaria
aliyekuwa kuhani maandiko yanawataja kuwa wote waliishi maisha ya utakatifu na
ya haki, wote walishika maagizo ya Bwana na amri zake bila ya lawama je wewe
mke wa Mchungaji na mumeo mnamcha Mungu kwa pamoja? Au ndio ile mmoja atwaliwa
mmoja aachwa?
Luka 1:5-6 “Zamani
za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa
zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake
Elisabeti. NA WOTE WAWILI WALIKUWA WENYE HAKI MBELE ZA MUNGU, wakiendelea
katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.”
Mke na mume
wanaweza kuishi maisha ya haki mbele za Mungu, lakini pia mke na mume wanaweza
kila mtu kuishi anavyojisikia, unadhani Lutu alikuwa na mke wa namna gani?
Wakati maandiko yanatueleza kuwa Lutu alikuwa mwenye haki, maandiko yanaonya
kumkumbuka mkewe Lutu ambaye aligeuka nguzo ya chumvi kwa sababu aliishi maisha
aliyoyataka mwenyewe
2Petro 2:6-7. “tena
akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya
iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu,
yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu;”
Luka 17:28-36 “Na
kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa,
walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu
aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza
wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika
siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili
kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu.
Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote
atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika
kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa
wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Watu wawili watakuwa
shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]”
Unaweza kujiuliza
ni kwanini mkewe Lutu aliachwa na maandiko yanamuhesabia Lutu kuwa alikuwa
mwenye haki, Je mkewe hakuwa mwenye haki? Lutu alichukia ufisadi, je mkewe
hakuchukia? Lutu alisema mpaka na wakwe zake lakini sikio la kufa halisikii
dawa waliangamia katika moto ule na Lutu tu na wanawe walipona, mmoja atawaliwa
mmoja aachwa, Familia za watumishi wa Mungu ni lazima wahakikishe wanaenda
mbinguni wote
Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kudhoofisha huduma
Wakati maandiko yakituonyesha
wajibu wa mama mchungaji katika huduma ya kichungaji, maandiko pia hayaachi kutuonya
na kutufundisha kuwa wako wanawake wa baadhi ya watumishi wa Mungu ambao
walihusika kuleta aibu kubwa katika huduma za waume zao na kuwaletea usumbufu
mkubwa na hata kuwafanya wawe na wakati mgumu katika shughuli zao za
kimaongozi, sitaki kuamini kuwa tunaweza kuwa na wanawake wa jinsi hiyo leo
lakini kama maandiko yanaonyesha kuwa walikuwepo hata leo wanaweza kuwepo
wanawake wanaofanana na hao.
1.
Gomeri
– Mama Mchungaji huyu aliolewa na Mchungaji Nabii Hosea lakini mama huyu
alimkimbia mumewe ambaye alikuwa nabii na kwenda kujihusisha na wanaume wengine
wengi, aliishi maisha ya kikimbizi na alimsababishia mumewe hasara kubwa ya
fedha na kiuchumi, alijiuza kama kahaba, alisababisha madeni, alimsaliti Hosea kwa
ujumla mwanamke huyu alikuwa mzinzi, Japo Hosea alimuonyesha upendo wa kweli,
Lakini alimpa taabu sana Mumewe huyu, Maisha ya nabii yana mengi ya
kutufundisha kuhusu uhusiano wa Israel na Mungu au kanisa na Mungu lakini leo
tunajifunza kuwa Gomeri alikuwa ni mama Mchungaji lakini alikuwa Malaya na
kahaba, mumewe ni nabii Mcha Mungu lakini mke anafanya mambo ya kikahaba, ni
aibu sana kwa mtumishi wa Mungu kuwa na mwanamke wa aina hii, hata ingawa
hatutiwi moyo kuvunja ndoa, lakini ni swala la kusikitisha kuwa leo wako mama
wachungaji wanazini na wanatongoza na vijana wanajifanyia wanayotaka huku
watumishi wakiwa aidha hawajui au wamemuachia Mungu, au nao wako busy na kazi
ya Mungu, kila kitu kinahitaji kiasi naweza kuwafokea wachungaji lakini leo
nimetumwa kusema na mama wachungaji, Mama Mchungaji aina ya Gomeri ni wengi
sana nyakati za leo.
Hosea 1:2-3 “Hapo
kwanza Bwana aliponena kwa kinywa cha Hosea, Bwana alimwambia Hosea, Enenda
ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi
mwingi, kwa kumwacha Bwana. Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye
akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume.”
2.
Mke
wa Lutu – Alikuwa ni mke wa mtumishi wa Mungu Lutu, ambaye alihudumu katika
miji ya dhambi ya Sodoma na Gomora, Lutu alikuwa mtu wa haki na anatajwa katika
maandiko kuwa hakufurahia dhambi za Sodoma na aliumizwa na uchafu uliokuwa
ukiendelea huko
2Petro 2:6-8 “tena
akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya
iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu,
yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu;
maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa
roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria;”
Hata hivyo
Pamoja na Lutu kuwa mtu wa haki jambo la kusikitisha ni kuwa walipoonywa
waikimbie miji ya Sodoma na Gomora ili Mungu apate kuwaangamiza waovu, Yeye mke
wa Lutu hakuwa miongoni mwa waliotii agizo hilo na hivyo aligeuka kuwa nguzo ya
chumvi, Yeye aliachana na familia yake iliyokuwa imeokolewa na kuitamani
familia ya kwao waliokuwa wakiishi maisha ya dhambi na hivyo aliangamia,
Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana kama mume na watoto watakuwa wanamtii
Mungu kisha akawepo ma Mchungaji ambaye yeye ni mkaidi kwa neno la Mungu huku
akivutwa na dunia Yesu alionya sana kuwa na tujifunze kwa kumkumbuka mkewe Lutu
Luka 17:28-33 “Na
kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa,
walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu
aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza
wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika
siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili
kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu.
Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote
atakayeiangamiza ataiponya.”
3.
Delila
– Alikuwa ni mama Mchungaji wa mchungaji mwenye nguvu nyingi sana za Mungu
na upako mkubwa, lakini alisaliti kwa kukubaliana na maadui wa Samsoni akitoa
siri ya asili ya nguvu zake, alijifanya kuwa anampenda sana lakini alijiunga na
maadui wa Samsoni na kushiriki mpango mbaya wa kumuuza kwa sababu ya tamaa za
kupata mali na ushawishi, hakujali usalama na ustawi wa mumewe, hakujali kuwa
amechaguliwa na Mungu, hakuona umuhimu wa wito wa mumewe na badala yake
alihatarisha mpango wa Mungu uliokuwa ukifanya kazi ndani ya Samsoni, yeye ni
mfano wa mwanamke asiyejali usalama na ulinzi wa mumewe wala mpango wa Mungu
juu ya mumewe hakuwa mwaminifu, alikuwa ni mwenye tamaa, alijichukulia maamuzi,
alikula njama na kumuweka mumewe matatani, yeye ni mfano wa mama wachungaji
wanaopoteza mwelekeo wa waume zao kihuduma na kuua huduma!
Waamuzi 16:18-21 “Delila
alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita
wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote
aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile
fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu
akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua,
nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka
katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na
kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. Wafilisti wakamkamata,
wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya
shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”
4.
Mikali
– Mikali Binti Sauli aliyekuwa mke wa Daudi Mchungaji wa Israel, Mchungaji
alikuwa na moyo wa kupenda ibada alimpenda Mungu sana lakini Mikali alimdharau
mumewe alipokuwa anajituma kuabudu, ni jambo la kusikitisha kuwa Mikali moyo
wake haukuungana na mumewe katika ibada na badala yake alimsanifu mumewe na
kuona kama mtu anayefanya mambo ya kipuuzi, mwanamke huyu kutokana na dharau
iliyokuwa ndani yake na ya kutokumjali Mungu wala kujali ibada alipigwa na
utasa siku zote za maisha yake.
2Samuel 6:16-23 “Ikawa,
sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi, Mikali, binti Sauli, akachungulia
dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za Bwana;
akamdharau moyoni mwake. Wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali
pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa
sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. Kisha Daudi
alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu
kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli,
wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate
wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake. Ndipo Daudi
akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka
nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo
namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano
wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na
haya! Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za Bwana, aliyenichagua mimi juu
ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa
Bwana, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za Bwana. Kisha nitakuwa
hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa
wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa. Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa
na mtoto hata siku ya kufa kwake.”
5.
Yezebeli
– alikuwa ni mwanamke aliyehusika sana kumpotosha mumewe Ahabu kwa kiwango
kikubwa sana na kuharibu huduma ya Mumewe, alichangia kwa kiwango kikubwa sana
ibada za sanamu, tamaa, kujipamba kulikopitiliza na kuelekeza familia nzima
katika uovu, Yezebeli alijihusisha na ibada za sanamu na kueneza zinaa ya
kimwili na kiroho, alikuwa ni mwanamke mpotoshaji aliyelelea manabii wengi wa
uongo
1Wafalme 21:25-26 “(Lakini
hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye
Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na
yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”
Ufunuo 2:19-23 “Nayajua
matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo
yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba
wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi
wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.
Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama,
nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia
matendo yake; nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya
kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa
kadiri ya matendo yake.”
6.
Vashti
– Anasimama kama mfano wa mama Mchungaji asiye na heshima na aliyekosa
adabu na utii kwa mume wake, Mumewe alitoa amri kwa watumishi wake kwamba
wamlete Vashti ili aweze kuwatambulisha watu wake mke wake (malkia) ambaye
kimsingi alikuwa mzuri sana, Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida Vashti
alikataa kuja kwa amri ya mfalme (Mchungaji) jambo ambalo lilimghadhibisha sana
Ahasuero, Jambo hili lilipelekea mwanamke huyu kuachwa, sababu kubwa ni kuwa
alikataa kumuheshimu mumewe tena mbele ya rafiki zake na watu maarufu
waliokuwako, alishindwa kumstahi, alishindwa kumuheshimu, alishindwa kunyesha
adabu, alishindwa kuonyesha utii, alionyesha mfano mbaya kwa taifa zima, wako
mama wachungaji ambao ni mfano wa Vashti, hawana adabu kwa waume zao, hawataki
kuonyesha heshima kwa waume zao hata wanapokuwa mbele za watu wengine au rafiki
zake, wanawake wa jinsi hii wakati wote huwakosoa waume zao hata mbele za watu
na kuwaaibisha unaweza kusikia mshaurini mwenzenu huyu, au hujifunzi kutoka kwa
wenzako, anaweza hata kuwasifia wanaume wengine mbele ya mumewe au kugoma kukaa
na waume zao au kuambatana nao sehemu wanakotakiwa kuwa pamoja, unaweza
kushangaa kuona sehemu ambayo mchungaji alipaswa kuwepo na mkewe, mkewe hayupo
na badala yake Mchungaji yuko peke yake, ni jambo baya sana kukosa hehima kwa
mumeo na kumdhalilisha mbele za watu au kufanya mambo yatakayosababisha kutia
aibu mbele za mume wako, kumvunjia heshima mumeo kwa hadhi yake ya kichungaji
kunaweza kudhoofisha kabisa utumishi wake mbele ya jamii, Jambo alilolifanya
Vashti lilikuwa ni mfano mbaya kwa nchi nzima na jamii nzima na kwa sababu hiyo
wenye hekima walitoa ushauri asiitwe tena na kwa ujumla alikataliwa! Na umalkia
wake alipewa mtu mwingine mwema kuliko yeye
Esta 1:5-21.“Hata
siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko
Shushani ngomeni, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika behewa la
bustani ya ngome ya mfalme. Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawi,
yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na
nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu
ya marumaru, mawe mekundu, na meupe, na ya manjano, na meusi. Wakawanywesha
kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai
tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme; kunywa kulikuwa kama
ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza
watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo. Tena Vashti, malkia, naye
akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero. Hata
siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani,
Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale
wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti,
malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na
maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa
kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme
akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia
wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya
mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena,
Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba
wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme;
akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama
vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi
Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa
mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika
majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na
wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa
mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata
na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za
tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea
dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya
kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba
Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe
mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga
itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu
waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida;
naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.”
7.
Mke
wa Ayubu - Ni mfano wa mama
Mchungaji ambaye alisimama na mumewe wakati wote wa mafanikio na wakati wa matukio mabaya, hata
hivyo aidha kwa kujua au kwa kutokujua, kwa kuchoka au kwa kukosa uvumilivu
alitoa ushauri mbaya kwa Mumewe kuwa kutokana na mateso anayoyapitia hana sababu
ya kuendelea kushikamana na uadilifu wake ni afadhali amkufuru Mungu ili afe,
Huu ni mfano wa mama mchungaji ambaye anaweza kutoa ushauri wa kukosa Imani, au
kuangalia mambo mengine badala ya kumuangalia Mungu, wakati mwingine mtu
anaweza hata akakushauri ugeukie maswala ya kishirikina ili uachane na uaminifu
wako kwa Mungu huu uikuwa mojawapo ya ushauri ambao ayubu kwa msimamo wake
aliuupuuzia na kuuiona kama wa
kipumbavu, kimsingi Ayubu alishangaa kuwa mkewe ameshindwa kujifunza hekima
wakati wote wa kaisha yao ya pamoja na badala yake anazungumza ujinga kama
wanawake wapumbavu tunajifunza kuwa wakati wa changamoto mdomo wa mama
Mchungaji unaweza aidha kuleta msaada au kuleta uharibifu
Ayubu 2:7-10 “Basi
Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu
wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi
majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu
wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa
hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi
tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo
yake.”
8.
Safira
– Mke wa Anania ni wazi kuwa hakumshauri vema mumewe na badala yake alikubaliana naye kwamba
wadanganye kanisa na mitume kuwa wamefanya utoaji mkamilifu ilihali ziko fedha
ambazo walikubaliana kuzificha walifikiri kuwa wanacheza mchezo wa kitoto kumbe
walikuwa wanamdanganya Roho Mtakatifu kuhusiana na mali waliyokuwa wameuza
matokeo yake waliacha watoto yatima kwa sababu Anania na mkewe walikufa kifo
cha kimwili na kiroho kwa sababu walikubaliana kudanganya na yhakuna aliyekuwa
na akili ya kumshauri mwenzi wake kuwa jambo hilo sio jema, kama mke wa
mtumishi una haki ya kuuliza vema kama jambo hili linalofanyika ni halali au la
na kumshauri mumeo kwa tahadhari na upendo ili aweze kufanya vema
Matendo 5:1-11 “Lakini
mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa
siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja
akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza
moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani
ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha
kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno
hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia
maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.
Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika. Hata muda
wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea. Petro
akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa
thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa
Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje
wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta
amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu nyingi ikawapata
kanisa lote na watu wote walioyasikia haya.”
9.
Eva –
Mama Mchungaji wetu mkubwa kabisa kwa baba yetu Adam, alifanya makosa
makubwa sana kwa kumsikiliza shetani kuliko kumsikiliza Mungu na mumewe,
hakuamini kuwa yale aliyoyasema Mungu ndio yalikuwa ya kweli, hakuambatana na
mumewe katika huduma, alibaki akichati na shetani na matokeo yake alisababisha ugumu mkubwa
sana katika huduma na maisha ya mumewe na kuleta mauti hata leo, na wakapotea
kwenye uwepo wa Mungu Adamu alijaribu kujitetea sana na alitaka kujieleza kuwa
ni mwanamke ndiye aliyesababisha Lakini hukumu ikawakuta na mabaya yakawapata
wote wakaumia
Mwanzo 3:9-12 “BWANA
Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako
bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani
aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza
usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa
matunda ya mti huo, nikala.”
Je wewe ni mama
mchungaji wa aina gani? Huduma ya mume wako inatiwa nguvu? au anadhoofika kila
iitwapo leo na wewe ukiwa ni sababu? Je unataka kuwa Baraka kwa kanisa la Mungu
na mwili wa Kristo? au unataka kuwa laana na chanzo cha kukosesha?, andiko
linatuonya kuwa Makwazo hayana budi kuja lakini ole wake yeye asababishaye, je
unataka kuwa mama Mchungaji wa aina gani? Kusudi kubwa la somo hili ni wewe ujitambue
na kuwa Baraka kubwa kwa huduma ya mumeo! Na usiwe mzigo na sababu ya uovu
katika huduma
Luka 17:1-2 “Akawaambia
wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja
kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni
mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.”
Mama Mchungaji
anayechangia uharibifu katika huduma ya mumewe katika maandiko anafananishwa na
mwanamke mpumbavu anayeiharibu nyumba yake kwa mikono yake miwili, je unataka
kuwa ma Mchungaji wa namna gani mbele za Mungu atakayehukumu matendo ya kila
mmoja? uwe na hekima jenga huduma yako mche Mungu. Muombe Mungu akupoe hekima
yake kwani iko hekima ya Mungu na iko pia ya kibinadamu nay a shetani
Mithali 14:1 “Kila
mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa
mikono yake mwenyewe.”
Yakobo 3:14-17 “N'nani
aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake
mzuri, katika upole wa hekima. Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi
mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile
ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.
Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.
Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari
kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina
unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”
Jinsi mama Mchungaji anavyoweza kusaidia huduma kusimama
Kila mama Mchungaji anaweza kuwa
msaidizi mzuri sana wa mumewe katika huduma na kumsaidia Mchungaji kufanya
vizuri, Mama Mchungaji unahusika na huduma na wajibu mzima wa kumtia moyo,
kumuombea, kumsaidia, kutengeneza mazingira mazuri ya kiroho kwake ili aabudu,
aandae neno, aombe, apumzike na maswala mengine mengi hapa kuna mambo kadhaa
unayoweza kufanya kusaidia huduma ya mume wako kusimama.
1. Maombi – Ma Mchungaji tenga muda wa
kila wiki au kila siku kumuombea mumeo, kuombea huduma yake, kuombea jumbe
zake, kumuombea ukuaji wake wa kiroho na kihuduma, unaweza kutengeneza
mazingira ya kuomba naye na mengineyo, ziko nyumba za watumishi wengine wa
Mungu mama anapiga bongo fleva na hakuna nyimbo za kwaya wala za kuabudu,
nyumba inakuwa na kelele wakati wote Mchungaji akitaka kuomba ni mpaka aende
porini nyumbani hakuombeki, hata kama ma Mchungaji anamuona mumewe anaandika
jumbe au anahangaika kupata jumbe za kibiblia yeye na watoto ndio kwanza wako
kwenye kelele, Nyumbani kwenu lazima kuwe na mazingira ya kiibada wakati wote
muombee mumeo, Nyumba ya Mchungaji ni nyumba ya ibada, Nyumba ya mchungaji ni
nyumba ya maombi, Nyumba ya Mchungaji ni ofisi ya dharula, Maombi yako
yatamuinua sana Mchungaji na kurahisisha mambo kwenda.
Yakobo 5:16 “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate
kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”
2. Tia moyo ukuaji wa kiroho – mtie moyo
kujisomea Biblia, muulize maswali magumu ya kibiblia ili aweze kujibu kama
anayefundisha, mnaweza kuwa na muda wa pamoja wa kujisomea Biblia
Mithali
27:17-18 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo
uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye
bwana wake ataheshimiwa.”
3. Mtie moyo kujihusisha na jamii – Mtie
moyo kuandaa mazingira ya kuzifikia jamii, kujihusisha na matukio ya kihuduma,
kujiunga na jamii inapokuwa na huzuni au furaha, mpe taarifa mbalimbali,
mpigishe stori, jiunge naye katika shughuli mbalimbali mtie moyo kutumika kwa
nguvu, epuka kumlinganisha na watu wengine acha mumeo awe nuru, usimfungie
ndani, mchekeshe na mkande kande anapokuwa amechoka.
Mathayo 5:14-16
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika
ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu
ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na
iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu
aliye mbinguni.”
4. Mpende na kumuheshimu mumeo – Moja ya
wajibu mkubwa na wa msingi wa mama Mchungaji ni pamoja na kumpenda, kumlinda,
kumuheshimu, kumtii na kumsaidia mumeo, mama wachungaji wana wajibu wa
kuwatosheleza waume zao pia katika tendo takatifu la ndoa kesi nyingi
wanazopokea watumishi wa Mungu makanisani ni pamoja na kuweko wanandoa ambao hawawajibiki
kutoshelezana katika tendo la Ndoa kwa msingi huo itakuwa ni fedheha na aibu
kubwa kama Mama Mchungaji ambaye anatakiwa kumsaidia mumewe kusimama imara
katika huduma na utumishi kwa Mungu kisha yeye akawa mfano mbaya kwa kina mama
wa kanisani kwa kushindwa kuwajibika ipaswavyo wao ndio wanapaswa kuwa mstari
wa mbele katika kuwafundisha wanawake vijana wajibu wao, mama wachungaji wengi
wamesababisha neno la Mungu kutukanwa kwa sababu badala ya kuwa rafiki wa waume
zao wamekuwa ndio maadui wakubwa wa waume zao, na kushindwa kuwatimizia ulio
wajibu wao, kufanya hivyo ni kumpa ibilisi nafasi
Tito 2:3-5 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa
utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao
mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda
watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa
wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”
Waefeso 2:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.”
5. Zijue fikra za Shetani – 2Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi
kuzijua fikira zake.”
Ni muhimu kufahamu kuwa shetani anapokuwa ameshindwa
kusambaratisha huduma ya Mchungaji njia pekee na rahisi anayoweza kuitumia ni
kupitia mama Mchungaji kama tu jinsi alivyopitia wanawake mbalimbali katika
maandiko kuwa sababu ya anguko kubwa la waume zao na hata huduma, mwanamke
asiye na akili hataelewa mbinu anazozitumia shetani, shetani atafanya mambo
kadhaa ili kuua huduma, na kukumaliza na wewe, Mchungaji akipata changamoto za
kihuduma wewe mama Mchungaji na familia yako pia mtaathirika hivyo usikubali
kumpa shetani nafasi ya kuharibu jambo la kiungu ndani yako!
a.
Atachoma
sindano ya migogoro ya ndoa anajua wazi kuwa kwa kupandikiza migogoro,
ugomvi, kutokuelewana kiburi na ubishi kikipandwa kati ya Mchungaji na mkewe
huduma itakosa Amani na moyo wa mchungaji utakosa Amani na kuchoka na maombi na
dua zenu zitazuiliwa na mfumo wa ibada utaharibika
1Petro 3:7 “Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo
kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu
kusizuiliwe.”
Waebrania 12:14 “Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
b.
Uchonganishi
na washirika – Ma mchungaji anapaswa kuwa makini asitumike kama chombo cha
kupanda chuki, fitina na maneno maneno ya uchonganishi kati ya mchungaji na
washirika, shetani anaweza kutumia udhaifu wa kibinadamu kukufanya wewe uwe
chombo cha kupeleka taarifa hata zisizo rasmi nakukuharibieni huduma
Mithali 6:16-19 “Kuna
vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya
kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao
mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye
uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”
c.
Moyo
wa utawala – Shetani anaweza kumuingia mama mchungaji kisha yeye akataka
kuwa ndiye mdhibiti wa kila jambo na kila kitu kinachoendelea kanisani kiasi
cha kufikia hatua ya kupingana na mume wake na kuleta mkanganyiko, washirika
hasa wanawake wanachukizwa sana wanapoona mama mchungaji ni kama anadhibiti
kila kitu au anakuwa na sauti kubwa kanisani na dhidi ya mumewe, ni vema kuwa
na moyo wa unyenyekevu kama pambo kwako
Ufunuo 2:20 “Lakini
nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye
nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu
vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.”
Mwanzo 3:16 “Akamwambia
mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa
watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”
Yezebeli alikuwa
ni mwanamke mwenye ushawishi aliyemsukuma mumewe na watu katika dhambi, Tamaa
yako itakuwa kwa mumeo ni tamaa ya utawala ambayo wanawake watajaribiwa kuwa
nayo, Mama mchungaji mwenye hekima atatumika kwa unyenyekevu mkubwa na hataweza
kuwa sababu na chanzo cha dhambi kwa mumewe kwa kupunguza maombi, ibada na au
kumsukuma mchungaji kwenye maamuzi mabaya
d. Moyo wa kuangalia nyuma - Mama mchungaji anapaswa kukumbuka agano
la ndoa na kuhakikisha kuwa anaambatana na mumewe, Neno la Mungu limeeleza kuwa
mtu atamwacha babaye na mamaye ataambatana na mkewe/mumewe na hao wawili
watakuwa mwili mmoja, kwa bahati mbaya wako mama wachungaji ambao moyo wao
hauko tayari kuambatana na mumewe na kila siku au kila mara na kila wakati moyo
wake uko kwao, urafiki mkubwa hauko kwenye huduma wala kwa mumewe lakini uko
kwa wazazi wao, kuwatunza na kuwajali na kuwaheshimu wazazi ni swala
linaloungwa mkono kimaandiko lakini kukosa kiasi katika swala hili ni dhambi,
wazazi wenye akili watamtima moyo mke wa Mchungaji na kumtaka aambatane na
mumewe kwa sababu jukumu alilo nalo ni la tofauti na watu wengine kaa na mumeo
wazazi msiwatenganishe wana ndoa, kama unaona kwenu ndio kwa maana zaidi kuliko
huduma na ndoa yako ujue utasababisha ajali za kihuduma kwa mumeo acha kukimbia
majukumu yako, kaa na mumeo mume wa agano lako mtumikieni Mungu.
Mathayo 19:4-6 “Akajibu,
akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na
mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana
na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena,
bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”
Moja ya sababu
ya mke wa Lutu kugeuka nyuma ni pamoja na ile hali ya kutokutaka kuambatana na
mumewe na badala yake aliwaangalia wazazi wake ambao kimsingi wala hawakuwa
wanamcha Mungu bali walikuwa raia wa kawaida wa Sodoma ambao walikataa ofa ya
wokovu
Mwanzo 19:12-26 “Basi
wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti
zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; maana
tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA;
naye BWANA ametupeleka tupaharibu. Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa
binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu BWANA
atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze. Hata
alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti
zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. Akakawia-kawia; nao
wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili,
kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji.Ikawa walipomtoa
nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika
hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. Lutu akawaambia, Sivyo,
bwana wangu! Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha
rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia
mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie,
nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi.
Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji
huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata
uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa
limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo BWANA akanyesha juu ya
Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa BWANA. Akaangusha
miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea
katika nchi ile.Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.”
Swala la
kumfuata mume halina tofauti kabisa na swala la kumfuata Yesu, mke wa Mchungaji
ni lazima amuwaze mumewe na kumjali kuliko baba yake na mama yake na nchi yake na huko alikotoka, mke
wa Mchungaji Lutu pamoja na neema kubwa aliyopewa yeye aliwaangalia ndugu zake
ambao wao walikataa neema na wala hawakuwa wanajali mambo ya Mungu na hivyo
aliangamia, kila mama mchungaji anapaswa kujiatafakari kwa upya anajitoa wapi
na kwa kiwango gani, na wazazi ambao binti yenu anakuwa mama mchungaji basi
mwacheni aende kwa mumewe na aungane na mumewe wamtumikie Mungu hivi mnadhani
Ruthu hakuwa na wazazi na ndugu? Alipoamua kuambatana na Naomi?
Ruthu 1:16-18 “Naye
Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako
nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu
wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo
nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.”
Luka 14:26-27 “Kama
mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na
wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi
kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma
yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”
Kila mama
Mchungaji akumbuke kuwa kumfuata mume ni sawa na kumfuata Yesu, kama unapenda
sana kwenu hufai kuwa mke wa Mchungaji, wako mama wachungaji wengine huwaacha
waume zao na ma - house girl au peke yao wakiwa wanataabika na njaa kisha wao
huenda kufurahia maisha ya huko kwao alikotoka, kufanya hivyo ni kumpa ibilisi
nafasi, kama ukipewa nafasi ya kuona yanayotokea huko nyuma ukiwa haupo nadhani
ungecha mara moja kutoka na kumuacha Mchungaji akitaabika peke yake wewe
ukiinjoy kwenu.
Waefeso 5:22-24 “Enyi
wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha
mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.Lakini
kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika
kila jambo.”
Kila Mama Mchungaji akumbuke kuwa
ana nafasi muhimu sana ikiwa atakuwa na busara na hekima ya kiungu atakuwa
Baraka kwa Mchungaji na Kanisa, lakini akiwa vinginevyo anaweza kuwa sababu ya
migogoro na mafarakano, dharau na kudhoofisha kazi ya Mungu na kupoteza heshima
yake binafsi ni imani yangu ya kuwa kila mama mchungaji atakayesimama katika
zamu yake kwa uaminifu na kujitoa kwa kadiri ya neema ambayo Mungu amewapa na
mumeo katika huduma kazi yako haitakuja iwe bure kwani imeandikwa ampokeaye
nabii kwa kuwa ni nabii atatapata thawabu ya nabii Mungu atawabariki sana mama
wachungaji watakaosimama katika zamu zao kuinua huduma ya kichungaji bila shaka
mama wachungaji watakaozingatia haya watakuwa na kiti chao mbinguni. Maandiko
pia yameahidi kuwa watang’aa kama mwangaza wa jua wale waongozao wengi kutenda
haki, na mama mchungaji ana nafsi kubwa katika kuongoza wengi kutenda mema
Daniel 12:3 “Na walio na hekima watang'aa
kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota
milele na milele.”
Mathayo 10:40-42 “Awapokeaye ninyi,
anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii
kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa
kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote
atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa
kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni