2Wakorintho 6:14-18. “Msifungiwe nira
pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani
kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana
ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani
pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na
sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya
kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao
watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana,
Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi
mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”
Utangulizi:
Mojawapo ya fundisho muhimu sana
katika maisha ya Ukristo ni pamoja na fundisho hili Msifungiwe nira pamoja na
wasioamini! Fundisho hili kimsingi linawaonya wakristo kutokuwa na ushirika wa
karibu sana na mtu asiyeamini, uhusiano huu ni ule unaoweza kuathiri uhusiano
wetu tulio nao na Mungu, hii ikiwa na maana ya ushirikiano wa kibiashara,
kindoa, uchumba na urafiki wa karibu wenye ushawishi mkubwa wa kimaadili na
kimwenendo! Pamoja na maswala ya kiibada au maswala ya kiroho. Kimsingi kuna
aina ya maisha ambayo wakristo tunapaswa kuyaishi katika mazingira ya maisha
yetu ambayo yatasababisha uhusiano wetu na Mungu kuwa wa karibu na wa kudumu.
2Wakorintho 6:17-18 “Kwa hiyo, Tokeni kati
yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami
nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na
wa kike,”
Leo tutachukua muda kujifunza
somo hili la msingi na la muhimu sana katika maisha ya wokovu Msifungiwe nira
pamoja na wasioamini kwa kuzingatia vipengele vikuu muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
kufungiwa Nira.
·
Madhara
ya kufungiwa Nira na wasioamini.
·
Faida za
kutokufungiwa Nira na wasioamini.
Maana ya kufungiwa Nira
2Wakorintho 6:14-15 “Msifungiwe nira pamoja
na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya
haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu
gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye
asiyeamini?”
Ni muhimu kuwa na ufahamu wa
kutosha kuhusiana na somo hili, ili hatimaye tuweze kuyatumia maandiko haya kwa
faida ya ufalme wa Mungu bila kuathiri uwepo wetu katika jamii, jambo la msingi
na la muhimu kwanza ni kuhakikisha ya kuwa tunakuwa na ufahamu wa maana ya neno
“Nira”, Neno Nira katika Lugha ya
Kiebrania linasomeka kama neno “Motah”
na katika lugha ya kiyunani linasomeka kama neno “Zygos” yote yakiwa na maana ya kifaa cha mbao au cha chuma
kinachofungwa au kuwekwa juu ya shingo za wanyama wawili wanaofanana wa kazi
ili waweze kufanya kazi kwa pamoja aidha ya kulima au kuvuta mzigo, kwa
kiingereza “Yoke”, lakini katika
maana ya kiroho neno hili linamaanisha kufanya agano, au kuingia mkataba wa
ushirika wa karibu sana na mtu, nchi, biashara au ndoa, au patano au agano kwa
hiyo kufungiwa nira ni uhusiano wa karibu sana na mtu mwingine ili kushirikiana
katika maswala nyeti na ya ndani kiimani, kimaisha, kindoa, kibiashara au
ushirika wa kiroho au udhamini, au kupana mikono, au kuambatana, au kutoa
udhamini wa kisheria mahakamani. Ushirika wa aina hii kimaandiko umekatazwa na
tunaonywa kujihadhari nao kwa gharama yoyote ile kwa faida yetu! Na kwa faida
ya ushirika wetu na Mungu.
Agizo la kutokufungiwa nira
katika andiko hili maana yake ni maneno ya fumbo “metaphor” lenye kumaanisha kuwa mtu anayemuamini Mungu ni tofauti
na mtu asiyemuamini Mungu na kwa sababu hiyo hawawezi kutekeleza lengo moja
lenye kumuhusisha Mungu kwa pamoja, Mtu alieyemuamini Mungu ni kama na mnyama
kazi aliyefundishwa kufanya kazi, na yule asiyeamini ni kama mnyama asiyefundishwa
kufanya kazi kwa hiyo lengo la kuifanya kazi iliyokusudiwa haiwezi kutimia au
kufikia malengo ni sawa na kuvalishwa Nira kwa wanyama wa aina mbili tofauti
jambo ambalo linaweza kusababisha maumivu kwa mmoja kwa sababu hawalingani
uwezo na hawafanani na nguvu zao pia
haziko sawa! Au umri wa wanyama kazi hao au vimo vyao vinatofautiana sana! Na
hivyo kum-athiri mwingine
Walawi 19:19 “Mtazishika amri zangu.
Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba
lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili
zilizochanganywa pamoja.”
Kumbukumbu 22:9-10 “Usipande shamba lako la
mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu
ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako. Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota
jembe pamoja.”
Zaburi 1:1-3 “Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala
hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na
sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani
lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.”
Watu walioamini ni aina nyingine
ya mbegu na haiwezi kuchanganywa na watu wasioamini, ambao ni mbegu nyingine, watu
wa Mungu hawawezi kuwa na ushirika wa karibu au wa kiagano au wa kiibada au wa
kindoa na watu wasioamini, kuwaunganisha hivyo ni sawa na kuweka wanyamakazi
Punda na Ng’ombe ambao kimsingi hawafanani wala hawalingani na hawawezi kufanya
kazi moja kwa pamoja, na sio haki
kuwafunganisha pamoja, watu waaminio wana sheria na wasioamini hawana sheria,
waaminio wanaishi kwa maelekezo ya Mungu wasioamini wanaishi watakavyo,
walioamini wanajifunza na kufundishwa namna na jinsi ya kutembea na Mungu
wasioamini ni tofauti wanafuata kawaida ya ulimwengu huu kwa hiyo hakuna
ulinganifu wa kimzani kati ya mtu aliyemuamini Mungu na yule asiyeamini. Mmoja
ni hekalu la Mungu mwingine ni hekalu la sanamu, hii ni lugha ya hali ya juu na
ya ndani yenye kusisitiza utofauti ulioko kati ya mtu aliyeokoka na mtu
asiyeokoka, aaminiye na asiyeamini, lugha zinazotumika kuelezea ushirika huu
katika kiingreza “Be ye not unequally
yoked together with unbelievers” kisha kuna maneno fellowship, communion,
concord, part, agreement. kwa hiyo kuna maneno unequally, fellowship, communion, concord, part, agreement ambayo
katika kiyunani yanasomeka kama Heterozugeo,
(Associate), Motechē
(Participation or intercourse), sumphonēsis
(Concord, Harmony, a state of agreement), Meris (Share, Patakers),
sugkatathesis – soong-kat-ath’-es-is (in company) kwa hiyo ukiyaangalia
maneno hayo yote yanayotumika katika kifungu hiki cha 2Wakorintho 6:14-18 yanamaanisha kuwa hatupaswi kamwe kuambatana,
kushirikiana, kuingiliana, kukubaliana nao, kushirikisha, kufanya urafiki,
kufanya kazi moja, kuchanganyika nao katika jambo moja mfano kama vyombo vya
muziki vinapopigwa gitaa, ngoma, na kinanda, kisha vikatoa mziki wa aina moja, “a simultaneous cccurence of two or more
musical tones that produce an impression of agreeableness or resolution on a
listener” kwa hiyo wakristo wanapofanya ushirika wa aina hii unaokatazwa na
maandiko yanatufundisha kuwa kitakachotokea kitaalamu kinaitwa “DISCORD” – “a lack of agreement or harmony
as between persons, things or ideas, active
quarrelling or conflict resulting from discord among person or function” “harsh or unpleasant sound” hali
itakayozalishwa itakuwa ni kelele za kutokukubaliana, kutokufikia muafaka,
kupingana kimawazo na kimtazamo, kutokea kwa migogoro na ugomvi, kukosekana kwa
amani na utulivu, kukosekana kwa utaratibu na ustaarabu, ugomvi endelevu, chuki
na sauti zisizopendeza, kwa sababu hiyo
uwepo wa Mungu hauwezi kuwepo mahali pa namna hiyo ni mpaka mtu wa Mungu ajiondoe kwenye patano
la aina hiyo.
Nira huwaunganisha wanyama wawili
wa aina moja na kuwafanya wafanye kazi moja wanyama hao ni kama ng’ombe kwa
ng’ombe na punda kwa punda, Wanyama hao wanapokuwa hawafanani kuna uwezekano
mkubwa wa kuumizana na kumuathiri mmoja
kwani wanaweza kuwa na tofauti ya nguvu na kimo, (horse power) Nguvu ya punda na ng’ombe zinatofautiana, aidha hata
kiumri wakati mwingine wanatakiwa kufanana kama, hawafanani kunakuweko
uwezekano mkubwa wa kuifanya kazi isiwe na ufanisi au kazi inakuwa ngumu sana
na kusababisha maumivu na makwazo kwa kila mmoja. Lakini mbaya zaidi ni kuondoa
uwepo wa Mungu, kwa hiyo agizo la Msifungiwe nira na wasioamini lina faida
kubwa sana kwa Mkristo, mtu wa Mungu, kuliko tunavyoweza kufikiri. Kwa hiyo hata mtu aliyeokoka akishiriki
mapenzi na mtu asiyeokoka ni sawa na kuchukua viungo vya Kristo na kuvifanya
vya kahaba
1Wakorintho 6:15-17 “Je! Hamjui ya kuwa
miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya
viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili
mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja
naye.”
Amosi 3:3 “Je! Watu wawili waweza kutembea
pamoja, wasipokuwa wamepatana?”
Neno la Mungu hapo linaonya
kutokuingia katika ushirika wa karibu au uhusiano wa ndani sana na kujifunga na
watu mnaotofautiana kiimani au hata kimafundisho, kimsingi tunaonywa kutokuchukuliana
na wasioamini katika imani kwani imani yao na uadilifu wao na akili zao ni
tofauti na kwa sababu hiyo upande mmoja unaweza kusababishiwa makwazo, majuto,
maumivu na machungu na kuondoa ufanisi katika utii na uchaji wa Mungu. Hii
haimaanishi kutokuweko kabisa duniani, au kutokushirikiana na watu wa dunia hii
katika kuleta maendeleo, hapana bali neno la Mungu hapa linatoa tahadhari ya
kutokujifunga kiagano, kipatano na kirafiki, na ushawishi na walimwengu kwani
kimsingi badala ya wewe kuwavuta na kuwashawishi wewe mtu wa Mungu ndiye
unayeweza kuathiriwa. “Believers should
not be in close partnership with non- believers” Waamini hawapaswi kuwa na
ushirika wa karibu na wasioamini. Ili kuwaepushia na madhara yanayoweza kuumiza
mioyo yao na kupoteza ushirika na uwepo wa Mungu.
Madhara ya kufungiwa Nira na wasioamini.
Biblia iko makini sana na ushirikiano
wa kiroho na muungano wa kiroho na agano la kiroho kati ya watu waaminio na
wasioamini, kwa sababu Mungu anajua wazi kuwa kuna madhara makubwa sana katika
muungano huo na shughuli zake haziwezi kwenda kwa ufanisi unaohitajika, ili
Mungu atembee katikati yetu kwa uhuru na Baraka, Kimsingi hakuna kitu kinaweza
kumzuia Mungu kutekeleza kutimiza kusudi, lake hata hivyo kwa kanuni ya neno lake
Mungu ni kwamba kutofungiwa nira kuna:-
a.
Kuepusha
migogoro ya kimaadili na kiimani – Watu wasioamini hawana Msingi wa Neno la
Mungu, sawa na mnyama asiyefunzwa au kuandaliwa kama mnyama kazi na hivyo
mtazamo wao kuhusu Ndoa, Biashara au maisha ya kiroho unapingana na ule msimamo
wa maelekezo ya neno la Mungu, kwa sababu hiyo neno la Mungu linaagiza kwa
ukali kuacha mahusiano nao, kwa maana nyingine kufanya maamuzi magumu ya
kujiepusha nao (kuua, au kukata). Kuvunja na kuharibu kabisa mahusiano na wale
wanaoweza kukukosesha.
Kumbukumbu 13:6-10 “Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako,
au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako,
akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;
katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe,
tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; usimkubalie wala
usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;
mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye
mikono ya watu wote. Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na
Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.”
Mathayo 18:8-9 “Basi
mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali
kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono
miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako
likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima
una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.”
Maandiko
yanatumia lugha ya mkazo au mkuzo kitaalamu inaitwa “Hyperbole” kufundisha au kusisitiza msimamo mkali (Radical Action) kuhusiana na maisha ya
dhambi na madhara yake, kwa hiyo katika maandiko hayo juu, maana yake sio
katika uhalisia wa lugha iliyotumika lakini ni kuchukua hatua madhubuti au
kufanya maamuzi magumu ya mabadiliko ya kitabia au kijamaa au kirafiki na watu
wanaokukosesha au wenye kukupa ushawishi kuelekea katika maisha ya dhambi, ni
afadhali kuua urafiki huo au ni afadhali urafiki huo ufe kuliko kuwa na mtu au
watu au ushirika unaokufanya uende motoni, kwa hiyo Musa anaposema ndugu yako
akikushawishi muue, na Yesu anaposema mkono wako au mguu wako ukikukosesha
uukate wote wanaanisha kufanya maamuzi magumu kwaajili ya uzima wa milele kuliko
kuchukuliana (Compromising) ambako
kutakusababishia uende jehanamu ya moto kwa hiyo fundisho la kutokufungiwa nira
hali kadhalika ni mkazo wa kufanya maamuzi magumu kujiondoa au kujitoa katika
ushirika unaotushawishi kuishi maisha ya dhambi na yenye tofauti za kimtazamo
na kiitikadi. Nuru na giza, au haki na uasi. Kwa hiyo neno la Mungu linatutaka
tuache uhusiano unaotupelekea kumkosea Mungu au kujitia unajisi.
Waebrania 12:3-4 “Maana
mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao
dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya
vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;”
b.
Huduma
na maisha ya Imani hudhoofika – Kufungiwa nira na wasioamini kunasababisha
mtu akosane na Mungu na Mungu asitembee pamoja naye, Huduma ya mtu aliyefungiwa
nira na wasioamini hudhoofika na kumfanya mtu kudhoofika kiimani na kihuduma na
kuwa mbali na Mungu, au badala ya kumtumikia Mungu kwa furaha na moyo mweupe
unaishi maisha ya maumivu mengi, kurudi nyuma kukwazwa, kudhoofishwa,
kuchukizwa, kukosa amani na kukata tamaa badala ya kutiwa moyo, kuambatana na
kushikamana na watu wa Mungu kunaleta uchochezi mkubwa wa kusonga mbele katika
maisha ya wokovu na ustawi badala ya kudhoofika na kusinyaa au kupoa. Jambo
hili linapunguza uwepo wa Mungu katika maisha yetu, Mfalme Suleimani aliyekuwa
anampenda Mungu kiasi cha kutokewa na Mungu mara mbili katika maisha yake na
kupewa akili na hekima nyingi kuliko mtu yeyote kbla yake au baada yake alipoa
sana kiroho kiasi cha kuabudu miungu mingine kutokana na kushikamana na wake
zake na kuwasikiliza na kuwatii ili kuwapendeza na wakamfanya apoe kiroho na
kuabudu miungu mingine jambo ambalo lilimuhuzunisha sana Mungu!.
2Wakorintho 6:17-18.“Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana,
Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi
mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”
1Wafalme 11:1-4 “Mfalme
Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake
wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa
mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie
kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani
akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na
masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa
mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake
haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”
c.
Kufanyika
mtego na mjeledi kwa watu wa Mungu - Mungu aliwaonya Israel kuwa endapo
wataungana na wenyeji na kuoana na watu hawa wasiomcha Mungu watu hao watakuwa
mtego kwao, watakuwa kwazo na mtego na mzigo mzito shingoni mwao, lakini pia watakuwa
mjeledi yaani watasababisha maumivu makali katika maisha yao watakuwa miiba, na
Mungu hatawaondoa, itakuwa kama adhabu ya ukaidi kinyume na agizo la Mungu. Kwa ujumla kumpenda Mungu kunaenda
sambamba na kujitenga na uovu na watu waovu
Yoshua 23:11-13 “Jihadharini
nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu. Lakini mkirudi nyuma kwa njia
yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki
kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya
kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu,
bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni
mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu
wenu, amewapa ninyi.”
Kumbukumbu 7:1-6 “Bwana,
Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa
mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na
Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe;
wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo
ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao;
binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa
kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine;
ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. Lakini
watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni
maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. Kwa maana wewe u
taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu
wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”
Ezra 9:10-12. “Na
sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako, ulizoziamuru
kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili
kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa
ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa
uchafu wao. Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake
za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa
hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa
milele.”
Nehemia 13:23-26 “Tena
siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na
Amoni, na Moabu; na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala
hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo.
Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao;
nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae
binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe. Je! Sulemani, mwana
wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa
na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu
akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata
yeye.”
Vifungu hivi
vyote vinatukumbusha wazi kuwa watu wa Mungu ni tofauti na watu wa dunia hii,
watu wa Mungu wana utamaduni wao, utamaduni wao ni neno la Mungu, mtu wa dunia
hii anaweza kujiunga na utamaduni huo kwa kuokoka, au kwa kuona na kuvutiwa na
maisha yetu ambayo ni nuru ndani ya Kristo, kwa kweli jaribio lolote la kuwaoa
au kuoana nao na kutarajia mabadiliko kutoka kwao ambayo hayatokani na Mungu
kunaweza kuwa mtego kwetu na kwa watoto wetu, Musa aliliona hilo na Nehemia na
Ezra pia walilikemea na Paulo anatukumbusha juu ya maamuzi haya Nehemia
anawakumbusha Israel kuwa huwezi kutumia Hekima, kwani hata mtu mwenye Hekima
aliyependwa na Mungu yaani Suleimani alibadilishwa moyo kwa mtego huu, Mungu
anamtarajia mtu wake kuwa tofauti na watu wa dunia hii, na kutokuishi sawa na
watu wa dunia hii wasiojali sheria na maadili ya kiungu ambayo ni Muhimu kwa
uwepo wa Mungu, hii haina maana ya kuwa Mungu ni mbaguzi la hasha hata kidogo,
lakini Mungu anataka kupitia sisi watu wa mataifa yote wageuzwe moyo na
kumuelekea Mungu aliye hai na wa kweli.
Mathayo 5:14-16 “Ninyi
ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu
hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza
wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate
kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”
d.
Kuzuia
ukuaji wako wa kiroho – Kufungiwa nira pamoja na wasioamini hukufunga wewe
katika hali yako ya kiroho na kuzuia ukuaji wako wa kiroho, Mtu aaminiye
anapounganishwa na asiyeamini ushawishi wake wa kiroho unaathiriwa na
kukengeushwa kwa ujumla kunakuwa na ugumu mkubwa kuishi maisha ya kumuheshimu
Mungu, Mtu aliyeokoka anamwamini Kristo, Mtu asiyeokoka anamwamini Beliari,
ubaradhuli, Mtu aliyeamini ni Hekalu la Mungu, mtu asiyeamini ni Sanamu, Mtu
aliyeamini ni Nuru, mtu asiyeamini ni Giza, hawa ni wanyama wasiofanana
hawawezi kwenda pamoja maumivu makali sana yatatokea, watu wengi waliokiuka
kanuni hii wameumia sana, hakuwezi kuwako mafanikio ya kiroho na mafanikio ya
kihuduma kwa watu ambao wamefungiwa Nira na wasioamini hakuna patano! Hapo wala
hakuna shirika!
2Wakorintho 6:14-16 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo
sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika
gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari?
Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano
gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye
hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao
nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”
e.
Kuharibika
kwa tabia njema – 1Wakorintho 13:33-34 “Msidanganyike;
Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala
msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.”
Kanuni ya
kutokufungiwa nira na wasioamini pia inakwenda kugusa urafiki wa karibu,
kuingia katika kufanya biashara au kuingia katika agano au kumdhamini mtu muovu
waamini wanaaswa na maandiko kujihadhari kwani inaweza kukuweka matatani katika
maswala ya imani yako kinyume na wasioamini, Neno mazungumzo mabaya katika Biblia
ya kiingereza yanasomeka “Bad Company” neno
la kiyunani linalotumika hapo ni “Homilia”
ambalo ni sawa na neno la kiingereza “Companionship”
au “intercourse” hii ikiwa na
maana ya ushirika wa karibu na mtu muovu au watu waovu unamchango mkubwa sana
katika kuharibu tabia njema, kwa
hiyo waaminio hawapaswi kamwe kuwa na ukaribu wa kina na watu wenye ushawishi
wa kutenda uovu, au wenye tabia mbaya ondoa watu wote wenye kusudi tofauti na
lako kwa Mungu.
Mithali 1:10-16 “Mwanangu,
wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi,
Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; Tuwameze hai
kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. Tutapata mali yote ya
thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka.Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na
vitu vyote shirika. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako
usiende katika mapito yao.”
f.
Kulinda
utamaduni wa kikanisa – Kanisa ni chombo chenye utamaduni wake, tabia na
maisha na mwenendo wetu ni tofauti na watu wa dunia hii, kufungiwa nira na
wasioamini kunauwa utamaduni wa kanisa na kulifanya kanisa kupoteza ushawishi
wake duniani, unaposoma yale yaliyomkuta Nehemia utagundua kuwa Mungu alikuwa na
Mpango wa kulitunza Taifa la Israel ili liweze kuwa taifa la mfano na liwe
Baraka kwa ulimwengu, kusudi hilo hilo limeletwa kwa kanisa, Kanisa leo
limekuwa na utamaduni mchanganyiko kama ilivyokuwa kwa Israel, tabia nyingi
sana zisizo za kiadilifu zimeingia makanisani, kuna kanisa moja katika mji fulani
nilifika na kukuta hakuna mikesha huko, na kiongozi wa mahali hapo akaniambia
anaogopa kufanya mikesha kwa sababu mikesha hiyo inatumiwa na vijana kufanya
uovu, mikesha ni njia ya kanisa kupata muda mrefu wa kuomba pamoja lakini kama
kanisa linafikia hatua ya kuogopa kukesha kwa sababu ya uasherati basi hakuna
tofauti na wale wanaokwenda kukesha katika disco na ngoma utamaduni wa
kumtafuta Bwana umetoweka, utamaduni wa kumcha Mungu na kuutafuta uso wake kwa
bidi umetoweka na tabia za ajabu zimaingia, lugha na mwenendo umeathiriwa na
mchanganyiko mkubwa wa kitabia umeingilia kati.
Nehemia 13:23-25 “Tena
siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na
Amoni, na Moabu; na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala
hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo.
Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao;
nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae
binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.”
1Petro 2:9-10 “Bali
ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya
Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa
la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”
Warumi 12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Kanisa ni taifa
ni mzao mteule ni ukuhani wa kifalme, ni taifa takatifu, ni wtu wa miliki ya
Mungu, Mungu amelitenga kanisa na dunia kwa sababu hiyo ni lazima kanisa likae
katika utamaduni wake, kufungiwa nira na wasioamini kutalifanya kanisa kupoteza
utaifa wake na utamaduni wake kwa hiyo badala ya waamini kuchukuliwa na
tamaduni za ulimwengu huu, maandiko yanasisitiza kutokuenenda kwa viwango vya
watu wa dunia hii, kwa hiyo ni lazima tujitoe kwa ukamilifu kwa Mungu na kuyatoa maisha yetu kwake na kujihadhari
sana na kujaribu kufuata tamaduni za ulimwengu huu, Mungu anataka iwe hivyo kwa
wake zetu, waume zetu na watoto tutakaowazaa baadae wote waifuate njia ya Mungu
na neno lake, sasa tukikubali kufungiwa nira tutapoteza hilo utamaduni wa
kibiblia na wa kikanisa ambao Mungu ametuandaa sisi kuwa watu wa tofauti.
Kumbuka wakati Israel waliposhuka Misri, Mungu aliugusa moyo wa Farao kuwapa
nchi ya Gosheni, ili wasichangamane na Wamisri, kwani tamaduni zao zilikuwa
tofauti na wamsiri hawachangamani na wafugaji jambo hili lilisaidia katiia
kuwafanya Israel kuwa taifa la kipekee waliokuwa na kuongezeka katika inchi ya
Misri, na kuwa na utamaduni wao na bila ya kupoteza utaifa wao na upekee wao
kama Waebrania.
Mwanzo 46:31-34 “Yusufu
akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi
nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba
yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. Na watu hao ni wachungaji,
maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe
zao, na yote waliyo nayo. Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu
ni nini? Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na
hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila
mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.”
Faida za kutokufungiwa Nira na wasioamini
Paulo anapotukumbusha au
kuwakumbusha Wakorintho kutokufungiwa Nira na wasioamini alikuwa anataka watu
wa Mungu wawe na uhuru wa kumtumikia Mungu kwa ukamilifu, kujiwekea mipaka ya
utakatifu, kuwa na amani ya moyo, kukua kwa haraka kiroho na kuepusha mivutano
isiyo na ulazima, na zaidi sana kuruhusu uwepo wa Mungu katika maisha yetu,
haya ni maswala ya msingi sana kama tulivyojifunza ya kuwa kuna madhara ya
kufungiwa nira na wasioamini, Lakini kuna faida kubwa za kutokufungiwa nira na
wasioamini. Moja ikiwa pamoja na kufurahia uwepo wa Mungu hususani katika ndoa
zetu, urafiki wa karibu, ushirika wa kibiashara na ufikiaji wa malengi ya
kiungu.
1Wakorintho 7:35 “Nasema hayo niwafaidie,
si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate
kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine.”
Kuoa au kuolewa au kufanya agano
na kuwa na ushirika wa karibu au kupatana yaani kufungiwa nira kwa kuwa na
mahusiano ya karibu na mtu asiyemjua Mungu au kupata mafundisho ya kutosha
kuhusu huduma ya Mungu kunatengeneza mazingira ya mgawanyiko na migogoro inayoathiri
utumishi wako kwa Mungu, muelekeo wako kwa Mungu unaathiriwa na mtu asiyemjua
Mungu, kama mtu anataka kumtumikia Mungu kwa uhuru ni vema ukajitoa katika nira
hiyo na kama umeshaingia ni ngumu kujitoa utalibeba, lakini kama hujaingia
chukua tahadhari za kibiblia
2Wakorintho 6:17-18 “Kwa hiyo, Tokeni kati
yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami
nitawakaribisha.Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na
wa kike,”
Kanisa limeitwa au lina wito wa
kuishi maisha matakatifu, maandiko yanakiri kwamba pasipo utakatifu haiwezekani
kumuona Mungu, maisha ya Utakatifu yanahusisha kutengwa na kujitenga, Kwamba
Mungu anakutenga wewe na mimi kwa kazi maalumu, sisi nasi tunawajibu wa
kujitenga na dunia kwa sababu Mungu aliyetuita ni Mtakatifu kwa hiyo wito wa
kutokufungiwa nira na wasioamini unamuita kila mmoja wetu kuishi maisha Matakatifu.
1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita
alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa
maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo
utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”
Kufukia malengo ya kiroho kwa Amani – Kimsingi watu wanapokuwa
wamefungiwa nira maana yake wanatengeneza mwelekeo mmoja na kwa sababu hiyo
lengo lao la kimwili na kiroho linakuwa moja kwa msingi huo inakuwa rahisi kwao
kutimiza makusudi yao kwa Amani na utulivu na hivyo lengo lao linakuwa rahisi
na lenye kuzaa matunda, sawa na ng’ombe ambao wamefunzwa kulima maana yake wote
wataifanya kazi ya kulima au kusukuma mkokoteni wa kizigo kwa ufanisi kwa
sababu wote wana mafunzo yanayolingana, lakini wanyama kazi hao wanapokuwa
hawana ulinganifu mambo huharibika mwenendo hauwezi kuwa sawa na kunatokea
maumivu makali, kuumizana na kukwazana na kusababisha kutokufikiwa kwa malengo
yanayokusudiwa, Nilielezewa na Marabi wa Kiyahudi kuhusu habari za Iditi “Idit” kwa
mujibu wa maelezo yao katika vitabu vya masimulizi ya kiyahudi kiitwacho Midrash Aggadah, Idit lilikuwa jina la
mke wa Lutu, Biblia hailelezi mengi kuhusu mke wa Lutu na wala haitaji jina lake,
Lakini Marabi wa kiyahudi wanaeleza ya kuwa mwanamke huyu hakuwa mkarimu kwa
wageni tofauti na ilivyokuwa na mumewe, Marabi wanasema mwanamke huyu alikuwa
na tabia sawa na watu wengi walioishi Sodoma, ni wazi kuwa huenda Lutu alimpata
mwanamke huyu katika miji hii, Mwanamke huyu hakuwa mwema na inaelezwa kuwa
hata malaika wale wagani walipowatembelea ni Mumewe ndiye aliyeonekana
kuwachangamkia, mke wa Lutu yaani Idit
alitoka nje na kweneda kuomba chumvi kwa wanawake wa Sodoma, sio kuwa hakuwa na
chumvi nyumbani kwake lakini alikuwa anataka watu wa mji ule wajue kuwa
nymkbani kwake kuna wageni na kuwa aliandaa chumvi ya kuwatosha wao tu lakini
kwa kuwa wamekuja wageni aliamua kutoka kuomba chumvi, kwa kusudi la kuwasengneya
wageni na mumewe kuwa amepokea wageni, hata pamoja na ukarimu wa malaika ambao
walimuokoa nayeye na kuwaonya wasitazame nyuma yeye aligeuka nyuma na
akahukumiwa kuwa nguzo ya chumvi, hii ndio sababu iliyopelekea yeye kuachwa,
Tabia ya mke wa Lutu inaweza kuonekana katika nyumba nyingi leo ambapo mwanaume
anaweza kuwa mkarimu lakini mkewe akawa mchoyo au mwanamke anaweza kuwa mkarimu
na mcheshi lakini mumewe akawa tofauti, mkali na hacheki na yeyote, wakati
kanisa litakaponyakuliwa watu wengi wataachwa katika mtindo kama huu mmoja
atwaliwa mmoja aachwa hii ni kwa sababu ya watu wengi kufungiwa nira katika
ndoa moja na asiyeamini, au mtu mwenye tabia mbaya, kwa hiyo swala la kuhukumiwa
kwa mke wa Lutu haikuwa swala la kugeuka nyuma pekee, lakini alikuwa ni mtu
mwenye kudharau maagizo ya Mungu na kuyapuuzia wakati mumewe na watoto walikuwa
waelekevu waliotii walichofundishwa
Mwanzo 19:25-26 “Akaangusha miji hiyo na
Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi
ile. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzi ya chumvi”
Ni mpango wa Mungu kutuokoa wote
pamoja na familia zetu, lakini tunapofunguwa nira na wasioamini tunaweza
kujiletea maumivu sisi wenyewe, nadhani mojawapo ya maumivu yaliyomkuta Lutu
sio kupoteza kila kitu lakini alimpoteza me wake mpendwa ambaye alimvumilia
ijapo kuwa alikuwa na tabia mbaya ambazo malaika hawakuzivumilia, Malengo ya
kuokolewa kwa familia yake hayakuweza kutimia.
Kupoteza furaha na utulivu wa kifamilia. – Pamoja na Baraka zote
walizokuwa nazo Isaka na Rebeka tunataarifiwa katika maandiko kuwa maisha yao
yalitiwa uchungu na kuhuzunishwa sana na wake wa Esau, Esau wakato wote
alionyesha kuvutiwa sana na maswala ya dunia kuliko mambo ya Mungu kwa hiyo
bila kujali wala kuchukua ushauri wa wazazi alioa wanawake wawili wa Kihiti,
hawa walikuwa waabudu miungu, kwa sababu hiyo moyo wa Isaka na rebeka haukuweza
kufurahia na wanawake hao pia waliondoa utulivu wa kifamilia katika maisha yao
Mwanzo 26:34-35 “Esau alipokuwa mwenye
miaka arobaini, akamwoa Yudith, binti Beeri, mhiti na Basemathi, binti Eloni
Mhiti, Roho zao Isaka na rebeka zikajaa uchungu kwaajili yao”
Isaka na Rebeka walikumbuka jinsi
Mungu alivyohusika katika upatikanaji wa mke wa Isaka Abrahamu alimuagiza
mtumishi wake na mtumishi huyu aliomba na kuweka nadhiri, Mungu alihusika moja
kwa moja katika upatikanaji wa Rebeka lakini sio ilivyokuwa kwa kijana wao yeye
alijiolea tu sijui kama Isaka na Rebeka walihudhuria harusi hii, lakini
ilitengeneza mgogoro na kuondoa furaha na utulivu wa kifamilia Biblia ya
kiingereza inasema “Esau marriages with unbeliever
wives made life bitter for Isaac and Rebekah” Isaka na Rebeka hawakuwa
wabaguzi wa rangi, wala hawakuwa na nia ya kumkataza Esau kuoa mke zaidi ya
mmoja kwa sababu yakobo pia alioa zaidi, lakini changamoto hapa ilikuwa
tamaduni tofauti, na wakaanani walikuwa waovu na wasiomcha Mungu hivyo swala la
kiroho kwao ndilo lilipewa kipaumbele
Kuweka usalama wa maisha ya kiroho – Watu wa Mungu wanapoharibu
nira yao na Mungu na kujiunga na wale wasiompenda Mungu kimsingi wanaharibu
usalama wao na kwa sababu hiyo wanakaribisha mashambulizi makubwa ya aina
mbalimbali katika maisha yao ya kiroho, hakuna jambo tunaloweza kulifanya ili
tumpendeze Mungu kila kitu kwa Mungu tunakipata kwa neema ya Mungu lakini hata
hivyo naada ya kuokolewa neno la Mungu linatutaka tutembee katika utii wetu kwa
Mungu ili adui aweze kutukimbia, Mungu kamwe hawezi kuubariki uhusiano ambao
unakwenda kinyume na mapenzi yake, kufungiwa nira na wasioamini kunatunyima
watu wa Mungu kuzifikia usalama unaokusudiwa na Mungu kwa sababu upande mmoja
utakuwa unaharibu na upande mwingine utakuwa unajaribu kutengeneza, ulinzi wa
kiungu unaharibiwa pale mtu wa Mungu anapojiungamanisha na mahusiano ambayo
kimsingi ni machukizo kwa Mungu
Yeremia 5:3-6 “Ee Bwana, macho yako je!
Hayaangalii uaminifu? Umewapiga, lakini hawakuhuzunika; umewakomesha, lakini
wamekataa kurudiwa wamefanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba wamekataa
kurudi. Ndipo nikasema, Hakika, hawa ni maskini; ni wajinga hawa; maana
hawaijui njia ya Bwana, wala hukumu ya Mungu wao; nitawaendea watu wakubwa,
nami nitasema nao; kwa maana hao wanaijua njia ya Bwana, na hukumu ya Mungu
wao. Bali hawa kwa nia moja wameivunja nira, na kuvikata vifungo. Basi, kwa
hiyo, simba atokaye mwituni atawaua, mbwa-mwitu wa jioni atawateka, chui
ataivizia miji yao, kila mtu atokaye humo atararuliwa vipande vipande; kwa
sababu makosa yao ni mengi, na kurudi nyuma kwao kumezidi.”
Kwaajili ya kuepusha migogoro na migongano – Mkristo kuoa au
kuolewa na mtu asiyeamini ni nira inayoweza kusababisha migongano ya kiimani,
kiibada, kimaadili na kimaamuzi katika familia, Aidha kushirikiana kibiashara
na mtu asiyeamini kunaweza kuleta maamuzi yanayopingana na kanuni za kiroho, rushwa,
wizi, udanganyifu, tamaa, kujitafutia na
ushawishi wa tabia mbaya, Ushirika wa kiroho au kujiunga ma makundi yenye
mafundisho potofu ni hatari kwa mustakabali wa kiimani ni kwaajili ya haya Neno
la Mungu linatuagiza kuacha kufungiwa nira na wasioamini, aidha ukiacha ukweli
kuwa ni hatari kwa imani, inaharibu baraka za Mungu, inaharibu hatima ya mtu,
inaharibu uhuru wa mtu kuabudu na kumtumikia Mungu inaathiri uwepo wa Mungu na
uhusiano wetu, Nira na wanaoamini inakuhakikishia usafi wa kiibada na kiimani
na usalama, Kujifungia nira na wasioamini kunatuletea uchafu wa kiroho na
kiimani kwa hiyo ni muhimu kujiepusha na ndoa za kisheria na wasioamini,
kujiepusha na mikataba au mapatano yatakayokulazimu kufanya dhambi, kujiepusha
na kumuwekea dhamana mtu ambaye haamini asije akakuliza na kukuweka matatani, ili
uwe safi chagua marafiki na watu wa karibu ambao wanakuleta karibu na Mungu na
sio vinginevyo, chagua watu ambao mna kusudi moja lenye kuwiana na ufalme wa
Mungu.
Kumbuka kuwa fundisho hili
halihusiani na kujiepusha kabisa na watu wa dunia hii, kwani kwa sehemu sisi ni
sehemu ya jamii, lakini fundisho hili lina mkazo katika watu tunaowaleta
karibu, wenye ushawishi, kikazi, kimkataba, kiagano, kiimani, kindoa na
urafiki, hao ni lazima wawe watu wa Imani moja na wewe na wengine tunaishi nao
katika hali ya kawaida kwa sababu ingelitulazimu kuhama ulimwenguni
Yohana 17:14-16 “Mimi nimewapa neno lako;
na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa
ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule
mwovu.Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”
Hitimisho:
Mji wa Korintho ulikuwa ni kitovu
kikubwa sana cha utamaduni wa Kigiriki, Uchumi na ibada za kipagani, sawa tu na
dunia tuliyo nay oleo, na Wakristo wa Korintho walikuwa wameokolewa kutoka
katika mazingira ya kuabudiwa kwa miungu mingi kama Aphrodite na zeuz, tamaduni
mchanganyiko na biashara lakini pia ulikuwa mji mchafu kingono na ndoa zisizokuwa
na uadilifu, mahusiano ya kijamii yalikuwa na machanganyiko wa kitamaduni
ambazo kimsingi haikuwa zinajali lolote kuhusu Mungu, Kwaajili ya kuwalinda
watu hususani Wakristo ili wasirudi nyuma. Paulo anakataza waamini
kujiungamanisha katika fungano la ukaribu sana na watu wa Dunia ile, Paulo
alikuwa akionyesha wazi kuwa watu waliookolewa wana nguvu tofauti, hatua
tofauti, mwenendo tofauti, hisia tofauti, malengo tofauti na mazigo tofauti kwa
hiyo Paulo anatumia fundisho lile lile la kiyahudi katika Torati akiwataka
wakorintho wasijunganishe katika uhusiano wa karibu na amaagano na ushirika wa
maisha na urafiki na watu waovu baada ya wao kuokolewa, huu ulikuwa ni wito wa
kuishi maisha matakatifu lakini pia wa kujilinda kwa mujibu wa tamaduni na
maisha ya Ukristo, Paulo alitaka watu wakuze uhusiano wao na Kristo maana yake
kujitoa katika nira ya Kristo kwa hiyo wakristo wanaonywa kuhusu ndoa, biashara
na urafiki wa karibu na watu wanaoweza
kuleta ushawishi wa uharibifu wa uadilifu katika maisha yao hii itaweka sawa
ushirika wa kimaadili, kutiana moyo katika ukuaji wa kiroho, Kuimarisha na
kuifanya kazi ya Mungu kwa Amani na Kukaribisha uwepo wa Mungu na Baraka zake katika
maisha yake kwa hiyo ingawa wito huu u naonekana kuwa mkali lakini ni wenye
manufaa makubwa kwa mustakabali wa furaha ya kweli katika maisha ya Ukristo;
Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu,ninyo nyote
msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha.Jitieni nira yangu
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo nanyi mtapata
raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini na Mzigo wangu ni mwepesi.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
.jpg)
Maoni 4 :
Wewe ni MWADVENTISTA MSABATO,
Asante kwa neno, hakika moyo wangu umejawa na furaha nimependa sana.mungu aendelee kukutumia.Amen nait w
Mjenzi kazi yake ni kuujenga mwili wa Kristo
Ubarikiwe sana na uongezewe neema mtu wa Mungu
Chapisha Maoni