Alhamisi, 1 Januari 2026

Nyakati za kuburudishwa!


Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”




Utangulizi:

Kwa kawaida mojawapo la hitaji kubwa la kila mwanadamu duniani ni pamoja na kupata wakati wa kupumzika au kuburudishwa, Mwanadamu anapopata pumziko na kuburudishwa anapata nafasi ya kuwa na utulivu na kujijenga upya kimwili, kiakili, kihisia, kiroho na kisaikolojia, hivyo kumwezesha kupata nafasi ya kujijenga na kujitia nguvu kwa upya, Mwanadamu sio mashine au robot kwa sababu hiyo anaweza kuchoshwa na mambo mengi na hivyo anahitaji kupumzika, wakati huo wa mapumziko mwanadamu anahitaji kuburudishwa ili aweze kuwa vizuri kwaajili ya majukumu mengine mazuri zaidi, Mungu anafahamu sana kuwa wanadamu wanahitaji mapumziko ili waweze kujijenga upya.

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Mapumziko ya mwanadamu yanaweza kumsaidia mwanadamu kuwa na nguvu katika maeneo yote ya maisha, kuwa na uwezo wa kustahimili migandamizo ya mawazo, kujenga mawazo mapya, kuwa na uwezo wa kutafakari, kupunguza mawazo, kuabudu, kupumzisha akili, kupokea mtazamo mpya, kuwa na mitazamo chanya, kusahau maumivu, na kuleta ufanisi unaomuondoa mwanadamu katika kuishi maisha ya mambo yanayojirudia rudia tena na tena kwa hiyo kuburudika ni hitaji kubwa la kiroho la Mwanadamu na ndio maana wanadamu wana likizo, mapumziko na usingizi n.k. ili kujikarabati, hata hivyo leo tutaangalia kwa undani na kwa kina namna ambayo Mungu huleta nyakati za kuburudishwa kwa wanadamu hasa pale wanapotubu na kurejea na kupokea msamaha wa Mungu kwa imani katika Kristo Yesu. Tutajifunza somo hili Nyakati za kuburudishwa kwa kuzingatia maswala muhimu yafuatayo:-

·         Maana ya nyakati za kuburudishwa.

·         Mwanadamu na nyakati za kuburudishwa.

·         Jinsi ya kuwa na nyakati za kuburudishwa.

Maana ya nyakati za kuburudishwa.

Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”

Tunaona katika kifungu hiki neno la Mungu likizungumzia na kuwaita watu watubu na kurejesha uhusiano wao na Mungu ili kwamba wapate nyakati za kuburudishwa kwa uwepo wa Bwana, ni muhimu kwetu sasa kujiuliza kwamba neno kuburudishwa hasa lina maana gani?, Neno kuburudishwa kimsingi linalotajwa hapo katika neno la asili la Kiyunani linasomeka kama “Anapsuxis” au “Anapaύō” kwa kiingereza “refreshing” – Properly a recovery of breath ambalo maana yake ni kupumzika, kuhuishwa, kutulia ili kupata nguvu kwa upya, kujipa unafuu, kujituliza, kupunga upepo, kutuliza akili, kutuliza roho mwili na nafsi,  au kuvuta pumzi, kuburudika, kujipa nafasi, raha, kupata pumzi mpya, kurejeshea nguvu zilizopotea, kurudishia pumzi kwa usawia!.

Kutoka 23:12 “Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.”

2Samuel 16:13-14 “Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.”

1Wakorintho 16:17-18 “Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu. Maana wameniburudisha roho yangu, na roho zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao.”

Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.”

Kwa hiyo kimsingi kupumzika kwa mwanadamu kuna uhusiano mkubwa sana na uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu, Mwanadamu anaweza kujipa raha au pumziko la kimwili tu lakini pumziko hilo sio pumziko la uhakika likilinganishwa na pumziko analolitoa Bwana wetu Yesu Kristo endapo mtu atampokea, tunafunuliwa katika andiko hilo kwamba, mwanadamu awapo dhambini yuko katika wakati wa kutumikishwa, yuko matesoni, anafanyishwa kazi bila hiyari yake, anatumikishwa na Shetani bila kupenda anateseka na kuelemewa na mizigo  na mateso ya aina mbalimbali na kuwa Pumziko la kweli linapatikana kwa kukubali mwaliko wake Yesu Kristo pekee, aidha mwanadamu anapokuwa katika magonjwa pia yuko vitani mwili wake unapigana kupambana na magonjwa lakini anapopokea uponyaji wa mwili wake nafsi yake na roho yake anapata nafasi ya kupumzika na Yesu Kristo anauwezo wa kutoa pumziko hilo kuanzia nasfini mwetu anauwezo wa kutupumzisha.

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa nyakati za kuburudishwa ni wakati ambapo Mungu anampa mwanadamu pumzi mpya ya uhai, na kuuhisha roho yake iliyochoka na kukata tamaa kwa sababu ya mapito ya dunia baada ya kukubali toba na kumuamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi.

Mwanadamu na nyakati za kuburudishwa.

Kila mwanadamu anahitaji nyakati za kuburudishwa aliyeokoka na hata asiyeokoka wote wanahitaji burudiko la kweli kwa sababu ya uchovu wa safari za duniani, Mwanadamu aliumbwa awe na nyakati za kuburudika na kupumzika kila wakati na kila siku, Mungu alipomuweka mwanadamu katika bustani ya Edeni alimuwekea mwanadamu mazingira ya mapumziko na wakati wa kuwa na ushirika na yeye, anguko la mwanadamu limesababisha upungufu mkubwa katika maisha ya mwanadamu, Mwanadamu ni kiumbe na ni kiumbe cha kibaiolojia, chenye utashi na akili na hisia lakini zenye mipaka, baada ya anguko mwanadamu amewekewa mazingira magumu ya kula kwa jasho, kushambuliwa na adui zake, uadui wetu mapepo na na shetani, michongoma na miiba kutuzalia na kuzaa kwa uchungu adhabu zote zile zilizotamkwa na Mungu zimemwekea mwanadamu mazingira ya kuchoka kiroho, kimwili, kiakili, kisaokolojia na kibailojia, hivi vyote vinamfanya mwanadamu kuwa mchovu katika safari ya maisha na kumfanya mwanadamu awe mwenye kuhitaji mapumziko.

Mwanzo 3:9-19 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.

Tangu baada ya anguko la mwanadamu, hitaji la kupumzika limekuwa ni sehemu ya uhitaji mkubwa wa mwanadamu, sio kimwili tu na hata kiroho na nafsi, hitaji la kupumzika na kuburudika linaonyesha kuwa mwanadamu sio kiumbe mkamilifu na wala hajitoshelezi bila Mungu, na kama mtu anaweza kushindana na hitaji la kuburudika na kupumzika ni wazi kuwa anashindana na asili, kwani hata zaidi ya maisha ya asili mwanadamu anahitaji kuburudika kiroho na hapo ndipo anapopata Amani, kugundua kusudi la kuwepo kwake na kujikuta anakamilika kwa hiyo katika ulimwengu wa anguko tunahitaji pumziko, Dhambi imeleta uhitaji mkubwa wa mapumziko, wanadamu walianza kutafuta faraja kila wakati katika safari ya maisha mara baada ya anguko ona

Mwanzo 4:20-22 “Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.”

Wanadamu walioanguka walijaribu kufanya mambo mbalimbali ya kuwaletea burudani ikiwa ni pamoja na kugundua na kutengeneza vyombo vya muziki kama kinubi na filimbi ili kujaribu kujituliza lakini hata hivyo faraja hizo zote walizojibunia wanadamu hazikuweza kuwaletea amani             ya kweli.

-          Utumwa wa dhambi unachosha - Dhambi ilikuwa imemtenganisha mwanadamu na Mungu, maovu yetu yaliuficha uso wake roho ya mwanadamu ikakumbwa na ukavu na kukosekana kwa utoshelevu bila utoshelevu wa kiungu kwa kweli mwanadamu anakabiliwa na uchovu na ukavu na hitaji la burudiko la mwili nafsi na roho

 

Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”

 

Zaburi 32:3-4 “Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu mchana kutwa. Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.”       

 

Moyo wa mwanadamu ni kama ardhi kavu wakati wa joto au kiangazi, uwepo wa Mungu ni kama maji, wakati roho zetu zinapokaukiwa tunahitaji nyakati za kuburudishwa na burudiko hili na kiu hii inaweza kutimizwa na Mungu peke yake na haiwezi kupozwa na mwanadamu wala katika mazingira ya kibinadamu.

 

-          Kila mwanadamu anachoka – Ukiwa mwanadamu katika safari hii ya maisha kuna kuchoka, watu wanachoka kimwili kiroho na Kisaikolojia, nafsini mwao na wanaumia kwa hiyo kila mwanadamu anahitaji kutiwa nguvu kwa upya na anayeweza kuwapa nguvu wanaochoka na kuzimia ni Bwana mwenyewe kupitia uwepo wake.  

 

Isaya 40:29-31 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”

 

-          Mateso yanachosha sana – Kwa kuwa mwanadamu hakuumbiwa shida anapopita katika changamoto na shida za aina mbalimbali hatimaye anachoka, unapokuwa mtumwa wa mazingira, unapokosa uhuru wako mwenyewe, unapotumikishwa na kutumiwa unazidiwa na mateso na kwa sababu hiyo unachoka na kujikuta unahitaji kupumzika

 

Maombolezo 5:1-5 “Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.”

 

-                Hata kutenda mema kunachosha - Mwanadamu anapotenda mema na wakati mrefu ukapita bila kuona matokeo pia anaweza kuchoka, unaomba, unatoa, unamlilia Mungu, unafunga unakesha lakini huoni matokeo wakati mwingine pia unaweza kuzimia moyo, unatendea mema watu wanakulipa maovu, unafadhili watu wanakuchukulia poa au kukutumia kwa faida hii nayo inachosha kutokana na hali hii watu pia huweza kuchoka kutenda mema.

 

Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.”

Kutokana na changamoto za aina mbalimbali anazokuwa amezipitia mwanadamu kila wakati changamoto hizo zinakuchosha na hivyo unajikuta kuwa unahitaji wakati wa kuburudishwa, ukiishi maisha ya utauwa utaudhiwa, ukiishi maisha ya anasa na dhambi utatumikishwa na shetani kwa ujumla duniani tunayo dhiki hata hivyo habari njema ni kuwa ziko nyakati za kuburudishwa hizi ni nyakati zinapatikana kwa toba na kufutiwa dhambi na kupewa wakati wa kuburudishwa, yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu, Petro ndiye anatufunulia swala hili katika hutuba yake sikuya Pentekoste anaonyesha kuwa katika Bwana kuna kuburudishwa kila mwanadamu anahitaji nyakati hizi anahitaji burudiko la mwili wake, nasi yake na roho.  Na burudiko hili linapatikana kwa kurejesha uhusiano wetu na Mungu, baada ya toba Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya mwamini anamwezesha kuishi maisha yenye burudiko

Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”

Jinsi ya kuwa na nyakati za kuburudishwa.

Mungu katika hekima yake anafahamu kuwa wanadamu wanahitaji nyakati za kuburudhishwa na kwa sababu hiyo neno lake limejaa ahadi za kuburudishwa.

Yeremia 31:23-25 “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; Bwana na akubariki, Ee kao la haki, Ee mlima wa utakatifu. Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao. Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.”

Zaburi 68:8-10 “Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.”

Petro anaunganisha toba kama njia ya kuleta amani na burudiko la kweli kwa mwanadamu, lakini zaidi sana anazungumzia ile ahadi ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu aliyeamini kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha na kuzijutia, ni ukweli ulio wazi kwa kila mtu kuwa ukijazwa Roho Mtakatifu unakuwa na wakati wa kuburudisha, Petro alikuwa anamzungumzia Roho Mtakatifu ndani ya mwamini anakuwa ni kama maji ya kunywa  na kuoga wakati wa joto, aliyeokoka anakuwa ni kama maji ya mito inayotiririka, Hakuna jambo linaleta furaha na amani kama kumpokea Roho Mtakatifu muulize kila mtu ambaye amejazwa Roho Mtakatifu atakuelezea jinsi ilivyo furaha kubwa sana hata unapopita katika magumu yeye anakupa burudiko lisiloweza kuelezeka.

Matendo 4:24-31. “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

2Wakorintho 4:8-9 “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;”

Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu aliyemwamini Yesu unayafanya maisha kuwa burudani kila wakati unamfanya mtu aliyemwamini Bwana asitikiswe na lolote, awe na nguvu ya kustahimili kwa sababu hata kama kwa nje anateseka kwa ndani kuna bubujiko la burudiko kubwa ndani yake, Roho Mtakatifu anatoa nguvu ya kustahimili, anatoa msaada wa uungu ndani yetu kushinda kila vikwazo vya kibinadamu na vya asili anatutia nguvu analihuisha neno la Mungu ndani yetu na kulifanya liwe na uhai na kukuwezesha kustahimili anakupa neema ya kuliona pendo la Mungu katika mateso na magumu na anakupa kuwacheka na kuwahurumia wanaodhani wanaweza kukukwaza kwa sababu zozote zile ndani yako maneno haya yanakuwa hai na halisi ndani ya mtu aliyeokoka.

Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”                                

Waebrania 12:26-29 “ambaye sauti yake iliitetemesha nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia. Lakini neno lile, Mara moja tena, ladhihirisha kuhamishwa vile viwezavyo kutetemeshwa, kama vitu vilivyoumbwa, vitu visivyoweza kutetemeshwa vikae. Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho; maana Mungu wetu ni moto ulao.”

Uwepo wa Mungu ukitembea pamoja nawe ni lazima utapoata raha, raha maana yake refreshment yaani kuburudishwa ni katika uwepo wa Mungu kila mmoja wetu ataweza kubudurika hakuna namna nyingine tunapouanza mwendo wa mwaka huu mpya wa 2026 kila mmoja wetu ajikite katika kuutafuta uwepo wa Mungu, Kufanya kazi kwa bidii kutafuta fedha kwa njia za halali bila kuacha kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii ili atupe raha, Bwana Mungu na atembee pamoja nawe katika mwaka huu na akupe nyakati za kuburudishwa katika jina la Yesu Kristo aliye hai, ulivyotembea katika nyakati ngumu na za majaribio imetosha sasa ni wakati wako wa kuburudishwa Mungu yuko tayari kutoa raha, na burudiko kwa wanadamu wote waliookolewa n ahata wasiookolewa kila mmoja wetu anahitaji kuburudishwa nami kama Petro alivyotangaza zikujie nyakati za kuburudishwa nakutangazia kuwa tayari kwa kuburudishwa, Pokea uwepo wa Bwana maishani mwako uwe na wakati wa kuburudishwa, mtii Mungu na itii sauti yake zipate kuja nayakati za kuburudishwa kwako katika jina la Yesu Kristo aliye hai. 

Kutoka 33:14-17 “Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”             

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.