Yohana 14:29-30 “Na sasa nimewaambia kabla
halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno
mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya
maswala ya msingi sana yaliyowahi kutamkwa na Yesu Kristo alipokuwa akiwaandaa
wanafunzi wake kwaajili ya kusulubiwa kwake ni pamoja na maneno haya “Yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana
kitu kwangu” maneno haya yalisemwa masaa machache kabla kidogo ya kukamatwa
na maadui zake, kimsingi maneno hayo yalikuwa yanamuhusu Shetani na utendaji
wake na kuhusika kwake moja kwa moja katika swala zima la kusulubiwa kwa Yesu
Kristo, ambapo Yesu alikuwa akiliona tukio hilo hilo kua ni tukio la ushindi la hiyari na kuwa ingawa shetani atahusika
katika kukamatwa na kusulubiwa kwa Yesu Kristo, Yesu Kristo alikuwa na tafasiri
nyingine kuwa litakuwa ni tukio la kuokolewa kwa watu wengi Duniani na ushindi
wa kiroho.
Yohana 12:31-33 “Sasa hukumu ya ulimwengu
huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi,
nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.”
Yohana 13:26-27 “Basi Yesu akajibu, Ndiye
mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa
Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia.
Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi.”
Njama, mipango na usaliti pamoja
na swala zima la kukamatwa kwa Yesu na mpango mzima wa kuteswa kwake na
kusulubiwa msalabani kwa namna Fulani kulionekana kama kufaulu kwa mbinu za
ibilisi kwani kuliratibiwa chini ya uwepo wa shetani, hata hivyo Yesu
anatufungua katika kifungu hiki cha msingi kuwa mpango huo hauna madhara kwake
na kuwa ni ushindi wa kiroho wa hali ya juu. Ni kwa msingi huo basi leo
tutachukua muda kutafakari kwa pamoja somo hili muhimu Yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu!, tutajifunza
somo hili kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya neno
mkuu wa ulimwengu huu.
·
Yuaja
mkuu wa ulimwengu huu.
·
Wala hana
kitu kwangu.
Maana ya neno mkuu wa ulimwengu huu.
Yohana 14:29-30 “Na sasa nimewaambia kabla
halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno
mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
Yesu Kristo aliyazungumza maneno
hayo muda mfupi kidogo kabla ya kukamatwa kwake na kusulubiwa msalabani kwa
mateso mabaya sana, maneno yake hayo yanatufunulia siri nzito kuhusu ushindi
utakaoambatana na mateso yake, ushindi unaotokana na kuzizidi hila za shetani
na njama zake; Maneno anayoyatumia hapo Mkuu wa ulimwengu huu yana maana gani
hasa? Kimsingi neno yuaja mkuu wa ulimwengu huu wala hana kitu kwangu yanasomeka
hivi katika lugha ya Kiyunani ona “yáp
archon toutou kósmos
erchomai, kai echo oύ
oudeis en emoi” na katika kiingereza
cha KJV ambayo ni literal
translation Bible yaani ni biblia iliyotafasiriwa kwa mtindo wa neno kwa neno
andiko hilo linasomeka hivi “for the Prince of this world cometh, and
hath nothing in me” NIV yenyewe
ambayo ni dynamic translation inasomeka
hivi “for the prince of this world is
coming, He has no hold on me” kwa hiyo utabaini kuwa neno Mkuu wa ulimwengu
huu au Prince of this world katika Kiyunani
anaitwa “Archon” ambalo maana yeke
hasa kwa Kiingereza ni “a person in
authority” au “a magistrate” kimsingi
Yesu alikuwa akimtaja shetani hapo ambaye anatajwa kama mwendesha mashitaka na
ushawishi katika mfumo wa ulimwengu huu wa uovu “Ksómos” taratibu zote za uovu za dunia zinaendeshwa
na shetani kwa hiyo kutokana na kazi zake hizo anaitwa mtawala wa dunia hii, au
mungu wa dunia hii au mkuu wa anga anayetamalaki falme na mamlaka za kiovu
duniani.
Waefeso 2:1-3 “Nanyi mlikuwa wafu kwa
sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida
ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye
kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati
yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia,
tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”
Waefeso 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa
hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu
ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili,
juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”
Ulimwengu wa uovu uko chini ya
utawala na ushawishi na uendeshaji wa kishetani, changamoto na mapambano anayokutana
nayo mwanadamu yanayopingana na maisha yetu ya kila siku na mafanikio yetu na
uonevu ni matokeo ya kimwili ya kushindana kwetu katika ulimwengu wa kiroho wa
utendaji wa shetani ambaye pia huitwa Mungu wa dunia hii.
2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu
imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii
amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake
Kristo aliye sura yake Mungu.”
Kwa hiyo Yesu anayasema mambo
hayo akiwaonyesha wanafunzi wake kuwa saa yake imewadia ya kwenda kupambana na
mkuu wa ulimwengu huu, ni wakati wake sasa kwenda kufanya kazi ambayo kwa akili
zake mawazo yake na mpango wake ni kuwa anakwenda kummaliza Yesu Kristo lakini
Yesu Kristo katika hekima yake na mpango wake anaonyesha kuwa mpango na mkakati
mzima wa ibilisi hautakuwa na mashiko kwake!
Yuaja mkuu wa ulimwengu huu.
Kwa nini Yesu anatumia neno
yuaja? Shetani alikuwa wapi na kwanini Yuaja? Neno yuaja katika Biblia ya
kiyunani hapo kama tulivyoona linatumika neno “erchomai” ambalo kwa kiingereza ni “to come” au “to go” ambalo hasa linatumika kuelezea ujio halisi
katika mwili “a Physical movement” kama alikuwa
akizunguka zunguka huko na kule katika ulimwengu wa roho sasa anakuja akiwa
amejikamilisha kwa hiyo anakuja akijitokeza hadharani “to appear in public” “a physical arrival” kwa hiyo Shetani
alikuwa amewapagaa rasmi Yuda, Viongozi wa dini, mahakama na askari wanakuja
rasmi sasa kuendesha mateso na kufanya kazi ya kuua kupitia kusulubiwa
kikatili, ni muhimu kuelewa hapo kuwa shetani anapokuja wazi kama alivyokuja
wakati wa kumkamata Yesu maana yake ni wakati anapowavaa watu na watu hao sasa
wanakuwa hawana huruma wanaingiwa na roho ya kikatili, roho mbaya inawakalia
huruma ya kibinadamu inaondoka sasa wanakukusudia mabaya, kuharibu
kusambaratisha na kuua!
1Petro 5:8-9 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa
kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta
mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa
mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.”
Ayubu 2:7-8 “Basi Shetani akatoka mbele za
uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa
kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.”
Yohana 10:10-11 “Mwivi haji ila aibe na
kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.Mimi
ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.”
Shetani anapokuja wazi wazi madhara yake yanaonekana wazi wazi,
uharibifu mkubwa hutokea, wizi wa Afya mali na uvunjifu mkubwa wa maadili, mafarakano,
ukatili uliopitiliza, anapokuja huwa anachinja ni tofauti na Yesu anapokuja,
wakati Yesu anapokuja anaokoa, anakuja na uzima wa milele, shetani anapokuja
anakuja na kufukuzwa kazi, anakuja na talaka, anakuja na uvamizi, anakuja
kuleta hali mbaya, analeta usaliti, analeta mafarakano, kutokuelewana, anakuja
na majungu, anakuja na matukio ya kuhuzunisha, hasara, na uhaini, mateso,
dharau, matukano na kadhalika hapo
unapoona mambo mabaya yanakuandama kila kitu hakiendi ni kama una nuksi, mikosi
na balaa ujue amekuja, Shetani anapokuja maana yake anakuja na kufikia
kilele cha utendaji wa kazi yake katika
maisha yetu ataharibu kwa kiasi ambacho unaweza kufikiri kuwa Mungu hana
huruma, utashuhudia utendaji wake wa kikatili ambao huwezi kulinganisha na siku
au wakati mwingine wowote katika maisha.
Wala hana kitu kwangu.
Yohana 14:29-30 “Na sasa nimewaambia kabla
halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno
mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
Haleluya, habari njema ni kuwa
Yesu alitoa taarifa hizo Yuaja mkuu wa ulimwengu huu lakini aliwathibitishia
wanafunzi wake kuwa vyo vyote iwavyo hata kama anakuja na saa ile anayokuja
inaonekana kuwa ni ya kutisha sana huyu jamaa hana kitu kwake! Neno wala hana kitu kwangu linasomeka katika
Kiyunani “kai echo oύ oudeis en emoi” kwa kiingereza ESV as “No claim on me” NIV “nothing in me” NASB “ No power over me”
KJV “and hath nothing in me” maana yake ni nini hasa anachokimaanisha Yesu
ni kuwa pamoja na ujio wake huu wenye hatari wa kumsulubisha mwana wa Mungu
Shetani hana udhibiti wowote juu ya Yesu, hana uhalali wowote, hana mamlaka
yoyote, wala hausiki kwa lolote wala hana sehemu katika mpango wa Mungu wa
ukombozi wa mwanadamu kupitia mauti ya Yesu msalabani Yesu haendi msalabani kwa
sababu ya dhambi zake au makosa yake anaenda kwa mpango wa Mungu kwa hiyari yake
mwenyewe, kwani uwezo wa kuutoa uhai anao na uwezo wa kuutwaa anao, hakuna wa
kumshitaki Yesu Kristo, uwezo huo uko kwenye mamlaka ya kimbinguni, na sio
shetani wala serikali wala makuhani
Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa
sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi
nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena.
Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.”
Yohana 19:10-11. “Basi Pilato akamwambia,
Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka
ya kukusulibisha? Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu,
kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi
iliyo kubwa zaidi.”
Yohana 8:46-47 “Ni nani miongoni mwenu
anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi
hamnisadiki? Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi
hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
Waebrania 4:14-15 “Basi, iwapo tunaye
kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana
maungamo yetu.Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo
yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila
kufanya dhambi.”
Kitendo cha Yesu kusulubiwa na
kufa msalabani kwa mateso makali, hakikutokana na uwezo wa shetani bali ulikuwa
ni mpango wa Mungu wa ukombozi wa mwanadamu, kimsingi shetani alihusika kwa
upumbavu wake akiwatumia viongozi wa dunia hii waliopagawa na fikra zake,
Lakini wakati anajihusisha katika mpango huu alijikaanga kabisa
1Wakorintho 2:6-9 “Walakini iko hekima
tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao
wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika
siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu
wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama
wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu; lakini, kama ilivyoandikwa,
Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia
katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.”
Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa na kukataliwa
na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu
humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona.”
Yesu alitaka tuelewe ya kuwa vita
katika ulimwengu wa roho ni halisi, shetani yuko nyuma ya kila linalokupata
anatumia usaliti, mateso na chuki lakini hata hivyo hana kitu kwa Yesu Kristo,
sio tu kwa Yesu Kristo bali na kwa kila aaminiye kila mtu anayemkubali Yesu
Kristo hapa duniani au ulimwenguni anakuwa kama Yesu kwa hiyo kama yeye alivyo
ndivyo tulivyo, kwa hiyo kila yajapo mateso na dhiki za aina yoyote tunajua
kuwa amekuja mkuu wa ulimwengu huu lakini hana kitu kwangu, zikija dhiki hivyo
hivyo yakija magonjwa wewe jua yanakuja tu lakini hayana kitu kwako kwa sababu
wewe ni kama alivyokuwa Kristo hapa duniani una Mungu aliye hai ndani yako
1Yohana 4:15-17 “Kila akiriye ya kuwa Yesu
ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi
tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo,
naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya
hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.”
1Yohana 4:4 “Ninyi, watoto wadogo,
mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu
kuliko yeye aliye katika dunia.”
Ni kutokana na ushindi aliotupa
Yesu Kristo pale msalabani una haki ya kumuambia shetani, magonjwa, dhiki,
shida, changamoto kuwa najua umekuja lakini huna kitu kwangu, wachawi hawana
madhara kwako, wambeya hawana madhara kwako, wafitini hawana madhara kwako chochote
kinachokukabili hapa duniani fahamu amekuja tu lakini hana kitu kwako tembea
katika ushindi huu tangu sasa tambua ya kuwa Yesu amekutetea amekufanya kuwa
mshindi wa changamoto zozote zinazoendelea hapa duniani usikate tamaa wala
usilie unapoteseka wala usimlaani Mungu na kumlaumu na kumuona kama amekuacha
wewe tambua tu kuwa kama una Yesu kama una Mungu aliye ndani yako ni mkuu
kuliko aliye katika dunia hii sema kila wakati na sema na kila changamoto ya
kuwa najua kuwa yu aja mkuu wa ulimwengu huu kwa vyovyote vile hana kitu kwangu
katika jina la Yesu Kristo kumbe kama alivyokuwa Yesu hapa ulimwenguni ndivyo
tulivyo kwa sababu hiyi shetani hana kitu kwako na kwangu katika jina la Yesu
Mwana wa Mungu aliye hai ameen !
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni