Jumapili, 29 Machi 2026

Mtoto hajafa Amelala tu !


Marko 5:35-40 “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana.



Utangulizi:

Kila mwanadamu mwenye akili timamu huwa anakuwa na ndoto na matarajio kadhaa wa kadha katika maisha, wengine huwa na matarajio makubwa wengine ya wastani na wengine ya kawaida tu katika maisha, kwa kawaida matarajio fulani yasipofikiwa au kutimia katika maisha husababisha msongo mkubwa wa mawazo na wakati mwingine kupoteza kabisa matumaini, matarajio hayo wakati mwingine yanaweza kuwa ya wazi na wakati mwingine yanaweza kuwa ya siri lakini kwa vyo vyote vile yasipofikiwa anayeumia zaidi ni yule aliyekuwa na matumaini hayo. Neno la Mungu lasema

Mithali 13:12 “Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.”

Hali hii ilimkuta mtu mmoja muhimu sana katika maandiko, huyu anatajwa kama mojawapo ya wakuu wa sinagogi ambaye alimwendea Yesu wakati binti yake mdogo akiwa katika hali ya kufa, ili yamkini ikiwezekana Yesu aweze kumuhudumia na kuokoa uhai wake aendelee na maisha naye

Marko 5:22-24 “Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye; mkutano mkuu wakamfuata, wakimsonga-songa.”

Akiwa katika safari ya kuelekea kumhudumia Yesu alisongwa songwa na watu wengi waliokuwa wakihitaji huduma na zaidi sana tukio la mwanamke mmoja aliyekuwa anatokwa na damu kwa muda wa miaka 13 liliingilia kati na kwa sababu hiyo kuchelewesha safari ya Yesu kufika kwa Yairo, Akiwa katika huduma za dharula zilizokuwa zinaingilia kati, katika huduma za Yesu hapa linakuja kundi la watu na kumpasha habari Yairo kwamba asiendelee kumsumbua Mwalimu kwani binti yake amekwisha kufa!  

Marko 5:35 “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?

Unapopiga picha ya kile kilichokuwa kinaendelea katika moyo wa Yairo utaweza kugundua kuwa kwa vyovyote vile moyo wake uliugua zaidi na nguvu zake zilimuishia na huenda alikata tamaa, hali kama hii huwapata  baadhi yetu pale yale tunayoyatarajia yanapoonekana kutokuwa na uwezo wa kutimia tena, hali ya kupoteza matumaini inatokea, ndoto zinapokufa, mambo yanapoonekana kutokwenda kama vile tulivyotarajia, afya inapokuwa hatarini, kazi inapoonekana kufika mwisho, mkataba unapoonekana kusimama, kazi uliyoitarajia inapoonekana kufikia mwisho, mchongo unaousikilizia unapoota mbawa, uchumba unapovunjika, mtaji unaposambaratika, mkopo unaposhindwa kulipwa, hasara katika biashara, mavuno usiyoyatarajia na kadhalika wakati huu matumaini huonekana kutoweka  na hiyo iko hivyo katika mtazamo wa Binadamu  Yesu anakuambia usilie kuna matumaini


·         Mungu huona tofauti na wanadamu.

·         Kelele za watu hazibadilishi mpango wa Mungu

·         Mtoto hajafa amelala tu    

          

Mungu huona tofauti na wanadamu

Matarajio ya kila mwanadamu anapopitia changamoto mbalimbali ni pamoja na suluhu ya haraka, kukosa faraja kukumbana na mipaka na kutamani kuondoka katika maumivu yanayotusibu, wakati Mungu mtazamo wake ni wa muda mrefu, wa kutukuza kiroho kutukomaza na kutaka tuuone utukufu wake lakini zaidi sana kuimarisha uhusiano wetu na yeye milele, wanadamu tunaona changamoto kama vikwazo njiani  wakati Mungu anaona vikwazo kama njia ya kuonyesha nguvu na utukufu wake, upendo wake na namna anavyotujali  lakini pia kunyamazisha kelele za kipinzani, wakati watu wanaona mauti kama jambo gumu sana na mwisho wa kila kitu, Yesu anaona mauti ni kama usingizi tu

Isaya 55:8-9 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”

Wakati mwanadamu anawaza kuwa amefika mwisho, Mungu ndio kwanza anaanza jambo, wakati wanadamu wanafikiri kuwa haiwezekani, Mungu anaona kivingine wakati mwanadamu anaona mauti na ukavu, Mungu anaona uhai na upako, Mungu hatendi kazi kwa hisia bali kwa imani!

Ezekiel 37:1-3 “Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.”         

Mungu alipomuonyesha Ezekiel bonde lililokuwa limejaa mifupa ya wafu na iliyokuwa imekauka sana katika maono yale yeye hakujua kuwa uko uwezekano wa mifupa ile kufanywa hai, hivi ndivyo inavyokuwa wakati mwanadamu anapopitia mambo magumu na hivyo ndivyo ilivyokuwa katika moyo wa Yairo wakati akitarajia uponyaji wa binti yake anapokea taarifa kuwa asimsumbue Mwalimu (Rabbi) kwani binti yake amekwisha kufa, matumaini yake na ya wale waliomletea taarifa yalikuwa yametoweka na sasa kilichokuwa kinasubiriwa ni mipango ya mazishi ya binti wa miaka 12 akiwa anawaza hilo hata hivyo Yesu alikuwa anaona mambo kwa njia nyingine tofauti sana na mtazamo wa kawaida, alimtia moyo Yairio aamini tu asiogope na sio hivyo tu hata alipofika naye kwenye nyumba ya msiba na kuwakataza watu waache kelele za maombolezo kwani mtoto amelala tu wao walimcheka na kumdhihaki wakidhani labda huenda Yesu hajui hata maiti au mtu aliyekufa  

Marko 5:35-36. “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu.”

Marko 5:38-39. “Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu.”

Je wewe unaona nini katika ndoto zako, unaona nini kazini kwako, unaona nini katika ndoa yako, uchumba wako, biashara zako, na maisha yako kwa ujumla, wakati unaona kuwa umefikia mwisho Mungu kwake yeye anaona ndio kwanza mwanzo unaanza, wakati wewe unaona giza yeye ndio kwanza kumekucha kile kinachoonekana kama mwisho kwako ni mapumziko ya muda tu, kamwe usikubali taarifa na tafasiri za watu ziwe tafasiri ya Mungu juu ya maisha yako! Mwangalie Yesu tu.

Kelele za watu hazibadilishi mpango wa Mungu

Walipofika nyumbani kwa Yairo kulikuwa na kelele, waombolezaji walikuwa wameshajaa tayari, na walilia kwa sauti kuu ya maombolezo na ngoma za maombolezo zilikuwa tayari zimeshawekwa  wakati wao wakifanya maombolezo kweli kweli Yesu alikuwa anaona wanafanya ghasia, na aliwakemea na kuwataka waache ghasia zao, wakati mwingine unapokuwa katika wakati mgumu watu wanaokuzunguka wanaweza kuongezea balaa katika majanga yaliyokupata kwani hata kama wewe ulikuwa na matumaini wao wanayafifisha zaidi, kila mmoja anajua kuwa mwisho wa maisha ya mwanadamu ni kifo na kila mtu anaelewa kuwa kifo ndio mwisho wa mambo yote na kwa sababu hiyo waliendelea na maombolezo na masikitiko na vilio ambavyo Yesu aliona kuwa wanafanya ghasia na alipowanyamazisha walimcheka sana, watu na mazingira yanayokuzunguka yanaweza kusema kuwa wewe uwezi tena, wanaweza kusema muda wako umeisha, wanaweza kusema hii ndio imetoka, Lakini Yesu ni kama alikuwa anamwambia Yairo usisikilize sauti za makelele na ghasia za watu wewe sikiliza sauti ya Yesu kelele za watu hazibadilishi mpango wa Mungu kamwe

Marko 5:38-43. “Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.:”

Yesu alimshika mkono aliyekufa na akamwambia msichana nakuambia inuka, Yesu alitumia maeneno ya Kiaramu “Talitha kum” akimaanisha msichana amka, Yesu hakupiga makelele wala hakutaka kufanya muujiza huu kama maonyesho, alikuwa kazini kuwasaidia watu wenye uhitaji, alikuwa kazini kuahirisha msiba, alikuja kusaidia watu, yuko tayari kukusaidia na yuko tayari kukushika mkono, haijalishi moyo wako umepata ganzi kwa kiasi gani wala hijalishi umevunjika moyo kwa kiwango gani, haijalishi umefikia mwisho wa nguvu zako  yeye akikushika mkono uhai utakurudia wakati watu wanadhani imekwisha Yesu anasema inuka, hakuna hali yoyote ile isiyoweza kubadilishwa na Mungu, tumaini lako na ndoto zako haziwezi kuzikwa mbele za Yesu Krito wa Nazareth aliye hai, wakati watu wanafikiri kuwa hali yako itadumu Yesu anaiona hali yako ni ya muda tu kwa sababu hiyo usilie, wala suiogope, acha kutazama mazingira, wala hali yako wala kushindwa kwako kwa Yesu hakuna kitu kinakufa yeye anauwezo wa kuamsha na leo ataliamsha kwenye maisha yako kila jambo linaloonekana kuwa limekufa na watu wameanza kuzomea wakifikiri mwishi umefika, kwa Yesu Kesi yako sio mwisho, kwa Yesu amini tu usiogope kelele za watu hazibadilishi mpango wa Mungu

Mtoto hajafa amelala tu

Katika uwepo wa Mungu kifo ni jambo la muda na sio la milele, wala sio mwisho wa mambo, na ndio Maana Kristo katika mtazamo wake huona kifo kama usingizi tu, wakati wanadamu wanaona ndio mwisho wa kila kitu, Yesu anakiona kifo kama suingizi tu, sio tatizo kubwa yeye ndio huo ufufuo!

Yohana 11:11-14 “Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha.Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona.Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa.”

Yesu alikuwa akionyesha mamlaka yake kama mwana wa Mungu kuwa anao uwezo wa kufufua na ana mamlaka dhidi ya kifo, ni yeye ndiye anayeshikilia funguo (Mamlaka) ya kifo na uzima kwa hiyo yeye anauwezo wa kuwaamsha waliokufa kama anavyoamsha mtu usingizini, Mungu anatumia usemi huu kuwatia moyo wanadamu kuwa kile wanachokiona kama uzito kwake yeye ni chepesi kuliko wanavyofikiri, wanadamu wanapopoteza tumaini wakati wote wanapaswa wakumbuke kuwa yuko Mungu ambaye kwake mambo ni mepesi tu na ndio maana Yesu aliamua kuwatuliza waombolezaji  na kuwafukuzilia mbali na kuwaamuru kuacha ghasia, aidha Yesu alikuwa anataka kuficha mamlaka yake isijulikane na watu nguvu za Mungu sio kwaajili ya maonyesho bali ni kwaajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji, Yesu alikuwa amekuja kuahirisha msiba amkuja kuondoa ghasia

Yesu alichelewa wakati akiwa njiani kumhudumia mtoto wa Yairo ili kutoa muda wa kifo cha mtoto na habari za kifo ziweze kumfikia Yairo nan a majirani na ndugu na jamaa  pia waombolezaji wajikusanye na kufika  na kuanza kuomboleza, wataalamu wa kifo wathibitishe kuwa mtoto amekufa, mwili uoshwe na watu wasubiri amri ya mazishi kutoka kwa baba mzazi wa binti Yairo

Mathayo 9:23-26 “Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.”

Mungu anapotaka kufanya mambo ya kushangaza huonekana kama amechelewa ili nguvu zake zionekane kwamba muda sio tatizo kwa Mungu, waombolezaji wakuzunguke ili jina la Mungu litukuzwe, wakati mwingine wambeya watapata habari ya yale yaliyokukuta na watasengenya na kusema Mungu atawaacha wazungumze kuwa jamaa amefikia mwisho  mambo yake yameharibika kwisha habaru yake hawezi kuinuka tena na kadhalika, kisha atafanya muujiza  na hapo kila mtu atajua kuwa Mungu ana uwezo anza kuchangamka ndugu yangu kwa sababu mtoto hajafa amelala tu, kinachokutokea ni kwaajili ya utukufu wa Mungu, yanakutokea ili majirani wapate taarifa, ili ndugu na jmaa wajue ili wasengenyaji wasema wakati wanakuza habari zako hapo anatikea mwanaume anaitwa Yesu anatangaza kuwa msifanye ghasia hapa mtoto hajafa amelala tu !

Yesu pia alkuwa akidhihirisha nguvu zake dhidi ya uumbaji kile anachokitamka ndicho kinachokuwa ni vizuri watu wakaamini katika neno la Mungu kuliko kuzitegemea akili zao wenyewe, Neno la Yesu lina nguvu kwa hiyo anapotamka kuwa ndoto zako hazijakufa zimelala tu ataamsha kila kinachoonekana kufa katika maisha yako, kwa uweza wake wa uumbaji, Yesu alimwamsha binti Yairo ataamsha kila kitu chako kinachoonekana kufa katika maisha yako  na watu wanakudhihaki watazuibwa vinywa vyao, anza kuchangamka kwa sababu mtoto hajafa amelala tu, anza kuzungumza lugha ya Bwana Yesu achana na lugha za waombolezaji hizo ni kelele tu mtoto hajafa amelala tu !

 [Korajabasta, para-kashata, roboboboso-kolotam katerrishetapapapa, kastabastariango, korabashandara-kasto, Yesukarabastanda-ding, koroposhotorabalistakarasto, taraka san sando pang-k-satostamanifesto, roborborboroshosta karabasa]

Mtoto hajafa amelala tu, kila kinachoonekana kufa katika maisha yako Katika jina la Yesu Kristo nakutamkia uzima naifukuza roho ya mauti naachilia uzima kila mahali katika mwili wako, katika ndoa yako, katika nyuimba yako,  katika familia yako, katika biashara yako, kazini kwako, katika afya yako nakutangazia uzima katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen! Mungu akutunze!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima  

Hakuna maoni: