Jumapili, 26 Julai 2026

UMUHIMU WA SHULE YA HUDUMA.


 

Waefeso 4:11-12 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kusudi kubwa la shule ya huduma ndani ya kanisa ni kwaajili ya kukumbushana wajibu wetu wa kulijenga kanisa la Mungu, Mungu alitoa wengine kuwa Mitume, wengine kuwa Manabii, wengine kuwa Wainjilisti, wengine kuwa Wachungaji na Walimu kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, na kuhakikisha kazi ya huduma inatendeka na mwili wa Kristo unajengwa kwa hiyo kila mtenda kazi ni mjenzi katika nyumba ya Mungu Kanisa la Mungu linafananishwa na shamba, linafananishwa na jengo na sisi ndio wafanyakazi pamoja na Mungu kwa hiyo kila mtenda kazi ni mjenzi katika nyumba ya Mungu na tunapaswa kuifanya kazi yetu vema na kwa usahihi kwa sababu Mungu ataipima kazi ya kila mtu kwa hiyo kila mjenzi anapaswa kuwa makini namna anavyojenga katika jengo la Mungu.

1Wakorintho 3:6-15 “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Katika nyumba ya Mungu kuna maeneo mbalimbali ambayo yanatutaka sisi kama watenda kazi kuwa makini, kuwa macho na kuyasimamia endapo tunataka kanisa letu likue kiroho na liwe kubwa lenye maelfu ya watu, ikumbukwe kuwa kadiri kanisa linavyokuwa kubwa linahitaji wahudumu wengi zaidi watakaotoa macho na kuhudumia maeneo mbalimbali na kumbuka kila tunapohudumu tunahudumia pamoja na Mungu kwa hiyo Baraka za Mungu huwa kubwa kwa kila mtenda kazi anayeifanya kazi yake kwa uaminifu, watenda kazi wengi wanapotupia macho maeneo mbalimbali ya kihuduma tunawapa watumishi wa Mungu nafasi kubwa ya kuomba na kulihudumia neno badala ya kushughulika na maswala ambayo yangeliweza kuangaliwa na watu wengine, aidha kanisa linapokua linatakiwa kuwa na wahudumu wengi zaidi ili kuzuia manung’unuiko miongoni mwa jumuiya ya  washirika katika kanisa la Mungu.

Matendo 6:1-4 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Kwa msingi huo basi tutachukua muda kujifunza somo hili UMUHIMU WA SHULE YA HUDUMA kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-


  • Sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu
  • Jinsi tunavyoweza kujenga pamoja na Mungu
  • Vema mtumwa mwema na mwaminifu

 

Sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu.

Paulo mtume anaelezea wazi kuwa sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu, anasema hayo kwa kusudi la kuweka mkazo kuwa kazi ya Mungu haiwezi kwenda mbele bila wanadamu, Mungu alimuumba mwanadamu kwa kusudi la kuwa na ushirika na yeye na kwa sababu hiyo sisi tunabeba kusudi lote la Mungu hapa duniani, jukumu hili kamwe Mungu hajawahi kuwapa malaika lakini ametupa sisi, kwa hiyo ni jukumu la kila mtu aliyeokolewa kulijemga kanisa la Mungu na kuifanya kazi ya Mungu kazi hii iliyo njema.

1Wakorintho 3:9 “Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.”

2Wakorintho 6:1-2 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)

Mungu amempa mwanadamu jukumu zima la kuihubiri injili na kuieneza na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi, hii ni heshima kubwa sana kwani tunapoifanya kazi hiii Mungu huwa hakuachi anakuwa pamoja nawe kwa sababu kazi hii sio yetu ni ya kwake kwa hiyo wewe kama mtoto wake unashirikiana naye katika kuikamilisha hakuna mahali popote ambapo Mungu alimuagiza mtu kazi kisha akamuacha, wakati wote mtu anapoifanya kazi ya Mungu neno la Mungu linaonyesha kuwa Bwana akawa pamoja naye

Marko 16:19-20. “Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]

Paulo anatumia mfano wa shughuli za kilimo kama kupanda na kumwagilia na hata maswala ya ujenzi kuonyesha kuwa katika mwili wa Kristo kila mmoja wetu ana majukumu mbalimbali, kutokana na vipawa mbalimbali na karama mbalimbali  lakini wote sisi tunaifanya kazi moja, kwa hiyo katika shule hii ya watenda kazi tunaainisha maeneo mbalimbali ya kiutendaji , hata kama wote tunajifunza hizi ili kumtumikia Mungu kwa pamoja baadae utaweza kuona kuwa tutamtumikia Mungu sehemu mbalimbali na kufanya huduma mbalimbali lakini katika mwili huu huu mmoja.

1Wakorintho 12:12-27 “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa;ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.”

Kwa hiyo tutafanya kazi katika maeneo tofauti tofauti wakati mwingine kwa kupangiwa au wakati mwingine kutokana na kile kitu ambacho Mungu amekiweka ndani yako lakini sisi sote tu watenda kazi na tufahamu kuwa tunaifanya kazi moja, asitokee mtenda kazi akafikiri kuwa hajaheshimiwa kwa kupangiwa eneo fulani, kokote tutakakoenda kumbuka Bwana yuko pamoja nawe na anajua kuwa unaujenga mwili wa Kristo, aidha tunafanya huduma hizi kwa neema ya Mungu kwa hiyo neema zinatofautiana kinachotakiwa kwetu ni uaminifu, usitake kuwa na huduma kama ya fulani kwa sababu kila mmoja ana neema tofauti na hivyo tutatumia neema hizo kwa kufaidiana

Waefeso 4:7-8 “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.”

1Petro 10-11 “kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.”

Warumi 12:3-5 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.”               

Kwa hiyo utaweza kuona Mungu ametuita kutenda kazi pamoja naye kwa neema na vipawa na karama tofauti tofauti, tutumie kila alichotupa Mungu kumtumikia bila kuumiza mwili wa Kristo kwa migawanyiko na manung’uniko mbalimbali kwani wote tutaifanya kazi hii kwa kufikia lengo moja kuufikia ulimwengu na kuwaleta watu kwa Yesu na kulijenga kanisa lake ili baada ya utumishi wetu duniani tukakae naye kule mbinguni

Jinsi tunavyoweza kujenga pamoja na Mungu

Katika kanisa la Mungu kuna namna mbalimbali za utumishi ambazo kwazo tunaweza kuzitumia katika kumtumikia Mungu, Ni muhimu kwetu kufahamu kuwa tukiifanya kazi hii ya Mungu kwa hiyari, kwa moyo na kwa uaminifu Mungu mwenyewe atakupa thawabu na kukupongeza na kukufuta machozi kwa kazi hii ambayo ina upinzani kutoka kwa adui shetani lakini simama kwa uaminifu kwaajili ya Bwana kama alivyofanya mtume Paulo ambaye alivumilia

Mathayo 25:21-23. “Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.”

Washirika wanapohudumiwa vema na kufikiwa katika mazingira yote hasa katika makanisa makubwa wanaona kuwa wanajaliwa hata kama hawamuoni mchungaji kiongozi kutokana na majukumu yake umoja wa kanisa utaimarika, kanisa letu litakuwa kwa kasi kwa ukuaji wa aina zote nazungumzia ukuaji wa kiroho, ukomavu na wa kiidadi na kuwa kanisa la maelfu, umoja utaimarika hata pamoja na ukubwa wa kanisa, na wingi wetu utageuka utajiri na afya ya kila mmoja wetu na miujiza haitakoma umati utavuta umati na Mungu atataka kujidhihirisha kwenye kusanyiko la watu wengi, sasa haya ndio maeneo na mazingira tunayoweza kumtumikia Mungu wetu:-

  1. Kuwahudumiwa waamini wapya – Mojawapo ya eneo Muhimu sana ambalo watenda kazi wote, wanafunzi wote na wenye hekima wote tunapaswa kulipa uzito mkubwa sana sana ili tupate kanisa lililobora ni kuwahudumia waamini wapya, au kuwahudumia watoto wachanga kiroho, kuwafuatilia, kuwalisha kwa neno la Mungu na kufanya malezi, Kama tunampenda sana Yesu upendo wetu utaonekana kwa jinsi tunavyowalisha kondoo zake

 

Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”

 

Agizo hili ni pana kwani linahusu ulishaji mzima wa kondoo, watumishi wa Mungu walioitwa katika wito maalumu wataifanya kazi ya kuwalisha kondoo katika ibada, tulizojipangia na katika semina zitakazojitokeza na kadhalika, lakini watenda kazi, wanafunzi na wenye hekima (Wiseman) wao watapaswa kuhakikisha kuwa wanawahudumia na kuwalisha watoto wachanga kiroho kwa kuwafundisha masomo ya mwanzo ya wokovu, ukiwaimarisha waamini wapya katika wokovu, kwa kuwaombea, kwa kuwafundisha kuisoma Biblia, na kuwaelekeza kuhusu maisha  tamaduni na Misingi  ya imani ya kanisa letu

 

  1. Kuwahudumia waamini wote ibadani    - Eneo lingine la huduma zetu kama watendakazi, wanafunzi na wenye hekima ni kuwahudumia watu wote wanaohudhuria ibada katika kanisa letu, watu waliopitia shule hii ya huduma watawahudumia watu kwa kuwapokea vizuri na kwa heshima, kuwapokelea vitu vyao, watoto na kuwaongoza mahali sahihi pa kuketi, sio hivyo tu kama ni mgeni utafanya kila jitihada kutambua anaitwa nani namba zake za simu na atakuwa pamoja nasi kwa muda gani, kama ni wadhaifu tutawatia nguvu, na tutaanza kuwapandisha imani kuwa umefanya uamuzi wa busara kuja kuabudu katika kanisa letu hili zuri, hakikisha kuwa kila mtu ana mazingira salama ya kuabudu, atajua vyoo viko wapi, wasaidie kujua mambo muhimu wanayopaswa kuyajua, tutakuwa tayari kuhudumu pamoja na Muhubiri katika ibada kuu na maombezi na kusawaidia watu wanaoanguka kwa mapepo au nguvu za Mungu na wale wanaofunguliwa na kuhakikisha kuwa tunawahifadhi kwa nguo maalumu safi na kuwafunika, Pia kuwapeleka mahali salama na sahihi zaidi na katika ibada nyingine maalumu kama ubatizo, meza ya Bwana, kubariki watoto, na kadhalika

 

Yohana 10:14 “Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi

 

1Wathesalonike 5:14 “Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.”

 

Waefeso 4:1-3 “Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.”

 

  1. Kusaidia huduma ya kichungaji – Watendakazi wote, wanafunzi na wenye hekima wanapaswa pia kufanya kazi ya kutoa msaada wa huduma ya kichungaji, ikumbukwe kuwa Mchungaji hawezi kufanya kila kitu peke yake, na akilazimika kufanya yote muda wa kukaa katika neno la Mungu na maombi utafilisiwa na kuathiri huduma za kiroho za jumla  na ndio maana mitume waliona vema kuwa na mashemasi kwaajili ya majukumu

 

Matendo 6:1-7 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.”

 

Warumi 16:3-4. “Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.”

 

Kutoka 18:17-22 “Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.”

 

Wasaidizi wa huduma ya kichungaji watafanya majukumu ambayo yangewezwa kufanywa na mchungaji katika kanisa, majukumu hayo ni pamoja na kuwatembelea washirika, kuwasaidia katika maombi, kufanya ufuatiliaji, na kufanya uashauri wa kichungaji, huduma hizi zote zinafanyika chini ya utumishi wa mchungaji kiongozi katika kanisa

 

  1. Kuwahudumia wale wanaotokwa na pepo – watenda kazi, wanafunzi na wenye hekima ni wajibu wao kuhakikisha kuwa mambo yote katika nyumba ya Bwana yanafanyika kwa kufuata utaratibu, Mungu ni Mungu wa utaratibu na anataka mambo yote yafanyike kwa utaratibu, kwa msingi huo, moja ya huduma wanayotakiwa kuifanya ni kuwahudumia wenye kuteswa na mapepo hasa katika ibada za maombezi, wanaousumbuliwa na pepo kama ni wakati ibada inaendelea ni lazima wahamishiwe kwenye vyumba maalumu vya maombezi, lakini kama machungaji yuko katika kuwashughulikia na wanaangushwa au kusumbua miongoni mwa watu watolewe na kupelekwa mbele au sehemu maalumu wanakoweza kuwa na nafasi ya kuhudumiwa na kufunguliwa kanisa linapokuwa tayari na watendakazi wanapokuwa tayari kuhudumu pamoja na Mchungaji na kuhudumu pamoja na Roho wa Mungu kwa utaratibu maalumu, Mungu Roho Mtakatifu atafanya miujiza mikubwa zaidi, kama pepo watasumbua wakati neno la Mungu linaendelea, wenye pepo wapelekwe sehemu nyingine ili neno la Mungu lihubiriwe kwanza, na wasipoteze usikivu!

 

1Wakorintho 14:39-40 “Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.”

 

Waefeso 6:11-12 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

 

Mapepo yanaweza kuwaathiri watu lakini kumbuka kuwa watu sio pepo, kwa hiyo utu wa aliyeathiriwa uthaminiwe na atunzwe kwa heshima zote, tusiwakasirikie wala tusiwe na msisimko ni lazima tuwe wapole na waungwana tuwahifadhi tuwasaidie kufunguka, tuwapeleke sehemu maalumu zilizoainishwa, tuwafute vizuri na tuchukue taarifa zao kwaajili ya ufuatiliaji na kwaajili ya kutunza muujiza na ushuhuda wa baadae

 

Mwondoe mwemye pepo katikati ya umati wa watu, kama ikiwezekana, tumia mamlaka kwa ustaarabu kuyakemea na sio kelele, usitumie nguvu kumbuka pepo wanatoka kwa jina la Yesu na kwa nguvu za Roho Mtakatifu wewe na mimi sio tunaotoa pepo, Pepo wanatolewa na Roho, sisi wajibu wetu ni kuwapa imani na kuwasaidia wao kupokea muujiza wao, msikemee watu wengi pepo mmoja mamlaka moja inatosha.

 

Mathayo 12:28-29 “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake.”         

 

2Timotheo 2:24 “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;”

 

  1. Kuwahudumia watu wanaoangushwa chini – uwe na uwezo wa kutambua ni aina gani ya sababu imempeleka mtu chini, sio kila anayeanguka chini ni kwa sababu ya pepo, wengine wanaweza kuigiza tu, na wengine wanaweza kuwa wamehemewa na hisia kali, na wengine ni kwa sababu ya nguvu za Mungu anaangushwa chini lakini anaweza asiwe na pepo, kwa hiyo usikimbilie kukemea pepo, kwa sababu wengine huangushwa tu na nguvu za Mungu na anaweza kujisikia vibaya kudhaniwa kuwa ana pepo.

 

Luka 5:16-17 “Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.”

 

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”

 

Wahudumu, watendakazi, wanafunzi na wenye hekima kumbuka ya kuwa lolote linaweza kutokea wakati wa maombezi, na wakati wa ibada jiandae kusimama nyuma kwa huduma, kwa wale wanaohudumiwa,  jiepushe kusukuma watu, tunza heshima ya watu hususani wanawake, wafunike wanapokuwa wamekaa vibaya, hakikisha kunakuwa na utulivu na amani tengeneza mazingira ya Amani, wasaidie kwa upole, omba kimya kimya, na usiwakasirikie wala kuwaudhi wao ni kama wagonjwa wetu na sisi ndio wahudumu wao, jua ya kuwa Mungu ndiye anayewahudumia pamoja nawe kwa sababu hiyo tuwahudumie kwa huruma na upendo

 

  1. Kuwahudumia wageni ambao ni mara yao ya kwanza – Wakristo wanahimizwa kuwa wakarimu, unapowapokea watu vizuri kwa tabasamu la upendo na kuwapa muongozo mzuri, bila papara na kwa kuwaonyesha upendo wao watajua kuwa kweli hapa ni kanisani, kanisani ni mahali ambapo watu wanapaswa kupokelewa kwa upendo kuliko mahali kokote kule, kanisani ni zaidi ya dukani, hotelini, gengeni  na kadhalika waonyeshe watu uungwana mkubwa, msalimie vizuri, mpe ratiba na muelekeo wa ibada,  usimuache akajitenga, zungumza kwa lugha za kawaida, waonyeshe shukurani waonyeshe kuwafuatailia baada ya ibada, wageni wangependa kuagana na mtu yule yule aliyempokea mwanzoni hasa kama ulimpokea vizuri, kwa hiyo yule utakayempokea mwanzoni ni mteja wako mpaka mwisho usimpoteze

 

Waebrania 13:1-2 “Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.”

 

Yohana 13:34-35 “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”

 

1Wakorintho 9:19-23 “Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.”          

 

  1. Kuwahudumia viongozi wa serikali – Viongozi wa serikali na viongozi wakubwa wa kitaifa wanaweza kuwa wakristo wenzetu katika kanisa la Mungu lakini pia wanaweza kuwa rafiki zetu na wanaweza kutembelea kanisa letu kwa taarifa au ghafla watendakazi katika kanisa tunapaswa kuwahudumia kwa heshima na ustaarabu pia, heshimu nafasi waliyo nayo lakini usiwaabudu, usilichuje neno la Mungu kwaajili yao, weka heshima sawa na maelekezo ya injili, Mungu hana upendeleo, lakini anayestahili heshima heshima, viongozi wahudumiwe vizuri na kukaribishwa na kama iko sehemu maalumu ya wageni maalumu wanaweza kuelekezwa hapo, kama ni kiongozi mwenye itifaki (Protocol) kadhaa wasikilize viongozi wa itifaki walioambatana naye na shirikiana nao katika utaratibu mzuri, mawasiliano mazuri na kadhalika, kauli za kisiasa kanisani haziruhusiwi, unabii unaohusu wanasiasa, haufai, isipokuwa kama Mungu amesema hivyo, na hakuna sababu za kulazimisha maombi ya kitaifa kama hakukuwa na programu hiyo msibadili gea angani, jiamini, tunza heshima jiepushe na mizaha inayoweza kutafasiriwa vibaya maneno yako yajae neema.

 

Warumi 13:7-8 “Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.”

 

1Petro 2:17 “Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme

 

Wakolosai 4:5-6. “Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.”  

 

  1. Kuwahudumia watumishi wa Mungu – Watenda kazi, wahudumu, wanafunzi pamoja na wenye hekima katika kanisa wanawajibu pia wa kumuhudumia mchungaji, wakati wote huduma inapoendelea pamoja na shughuli nyingine tutakuwa katika maombi ya kimya kimya tukiendelea kuhudumu pamoja na mtumishi wa Mungu, wafunikwe kwa kuwaombea, uwe na karama ya kupambanua roho na kung’amua kwa haraka watu wanaotaka kuwashambulia watumishi wa Mungu, angalia kama amechoka, angalia kama amekata tamaa, angalia kama anapingwa, angalia kama anahitaji kitambaa cha jasho, maji ya kunywa ama kama analetewa kitu kibaya, wekeni utaratibu wa ulinzi na usalama kwaajili ya kanisa zima na kwaajili ya mtumishi wa Mungu, dhibiti watu kumfikia kwa haraka bila utaratibu, au wale wanaotaka kumshambulia, wekeni timu ya itifaki ya namna ya kumfikia mtumishi wa Mungu, kataza wanaomsengenya, wasahihishe wasiomuelewa, mlinde bila kupigana, muheshimu bila kumuabudu, heshimu mipaka, wajibika kwake, lindeni kile Mungu ameweka ndani yake,  Mke wake na familia yake na kadhalika, tunapowahudumia watumishi wa Mungu tunamuhudumia Mungu pia.

 

Yohana 12:20-21. “Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.”

 

Zaburi 105:14-15”Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.”

 

1Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha

                 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima       

Hakuna maoni: