Jumanne, 26 Januari 2016

MFULULIZO WA MASOMO YAHUSUYO UTETEZI WA IMANI (APOLOGETICS) 4



UKIRI WA IMANI YA MITUME.
a.       Maendeleo ya kuweko kwa Ukiri wa Imani
 Ukiri wa zamani zaidi wa imani katika kanisa la mapema uliitwa imani ya mitume kwa ujumla haukuandikwa na mitume  lakini ulikuwa ni mkusanyiko wa kiini cha mafundisho yao na ulikusanywa kwa mara ya kwanza kati ya mwaka 140 na ulikuwa ukitumika kama Katekisimo (Catechism) kwa kila mtu mara anapokuwa anakaribia kubatizwa kama ukiri wao wa imani
§  Kumuamini Mungu lilikuwa swala la asili kwa Wayahudi na Wakristo kwa msingi huo kumkiri Kristo katika ukiri wa imani  kulitofautisha kati ya Ukristo na Uyahudi na ubatizo ulikuwa ukifanyika kwa jina la Yesu kama ilivyokuwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume
§  Hata kufikia mwaka 200 A.D. wale waliokuwa wanataka kubatizwa walikuwa wakiulizwa swali Unaamini? Baaday ilibadilishwa na hata ilipofikia Karne ya 12th C ilifikia hatua ya juu  na kukubalika  kwamba anayebatizwa ni muhimu kukiri ukiri wa imani uliosema hivi 

Namwamini Mungu Baba mwenyezi Muumba wa mbingu na Nchi na Yesu Kristo mwana wake wa pekee Bwana wetu aliyechukuliwa mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Mariam, aliyeteswa zamani za Pontious Pilato akasulibiwa, akafa akazikwa siku ya tatu akafufuka akapaa mbinguni ameketi mkiono wa kuume wa Mungu baba, toka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu watu walio hai na wafu na ufalme wake ahauna mwisho, Namwamini Roho MtakatifuKanisa takatifu la Kikristo,Ushirika wa watakatifu Msamaha wa dhambi,ufufuo wa mwili na uzima wa ulimwengu ujao Amen.”

HISTORIA YA BISHANO KUHUSU UTATU WA MUNGU.
Kuenea kwa injili ulimwenguni hususani kwa mataifa kunaifanya injili kuwafikia Wayunani nao wanakuwa sehemu ya kanisa wasomo, watu wenye uwezo wa kufikiri, wanasheria na kadhalika sasa wanaingia kanisani na kuchanganua mambo.
Justin Martyr 100-165.
-          Alikuwa mwanafalsafa kutoka Samaria ingawa wazazi wake waliishi Rumi Kama mwalimu aliuona Ukristo kama Una kitu cha ziada kuliko falsafa  na hivyo aliamini na kuokoka
-          Alifundisha kuwa Yesu ni mwana wa Mungu aliyeumbwa na Mungu kabla ya uumbaji, kwa msingi huo kabla ya hapo Mungu alikuwa peke yake ndani ya Mungu kulikuwa na Neno Logos, kwa hiyo Yesu ni mdogo kwa Mungu na anapaswa kumtegemea Mungu, kwa sababu ya msimamo huo Justin aliuawa mwaka 165 wakati wa utawala wa Marcus Aurelius huyu alikuwa mwana apolojetic wa kwanza.
Turtulian 160-220
-          Alikuwa mtetezi wa imani kutoka Misri.
-          Ibu la tatizo alilokuwa nalo Justin lilitatuliwa na mwanatheolojia huyu alikuwa mtu kutoka Carthage na alikuwa msomi alkuwa mwana Montanists alikazia utakatifu na kukemea udunia ndani ya Kanisa katiliki
-           
-          Alifundisha kuwa Baba na Mwana wanashiriki uungu mmoja na ni nafsi tofauti zikiwa na kazi maalumu hata hivyo alitoa nafasi ya Pili kwa mwana kuwa sio wa milele
-          Alisema Baba na Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu mmoja  na kila mmoja ni nafsi na huu ndio ukawa mwanzo wa msingi wa fundisho hili la utatu kuja kukubalika wakati wa mkutano wa Nicea.

MKUTANO MKUU WA NICEA NA TAMKO LA IMANI (IMANI YA NICEA).
-          Nicea ni moja ya miji katika inchi za asia ndogo
-          Mnamo mwanzoni mwa Karne ya Nne moja ya fundisho muhimu sana liliinuka na kuleta Utata miongoni mwa Kanisa, mijadala iliinuka kupitia wanatheolojia  wakubwa na wenye nguvu, pia kukiwa na utetezi wenye nguvu na mawazo mbalimbali  yaliyopelekea kuitishwa kwa mkutano wa Nicea
a.       Arius wa Alexandria  256-336
Alikuwa ni kiongozi mkubwa wa imani ya Kikristo na mwanzilishi wa imani ya Arianism moja ya imani potofi iliyokuwa inapinga uungu wa Yesu Kristo, Arius alikuwa mwana theolojia aliyesomea huko Antiokia (Antakya ya Leo huko Uturuki) alijifunza theolojia chini ya Msomi aliyejulikana sana aliyeitwa Lucian na huenda ndiko alikotoka na fundisho hilo alijulikana kwa kusisitiza maswala ya kihistoria na njia zanye kujenga na kuzalisha za kidini pamoja na maswala ya utafiti kuhusu umoja wa Mungu na Utatu mtakatifu shule yake ilijulikana pia kama shule iliyokuwa ikimuona Kristo kama  yuko chini ya Mungu Baba,.
Arius alizaliwa Afrika na alikuwa mwangalizi wa Kanisa la Alexandria nchini Misri, alikataa kuweko kwa ushirika wa milele kati ya Yesu na Mungu usemi wake maarufu unasema “kuna wakati ambapo Yesu Hakuweko”na kuwa Mungu alimpitisha Yesu kuwa mwana wake baada ya ufufuo wake na kumpa baadhi ya majukumu ya uungu alisema Yesu alikuwa na mwili wa kibinadamu lakini hakuwa na Nafsi ya Kibinadamu na hivyo hakuwa Mungu wala hakuwa mwanadamu wa kawaida Yuko mahali Fulani hapo katikati.
b.      Athanasius
Mtakatifu Athanasius aliishi kati ya mwaka wa 293-373 B.K. Ni mwanatheolojia mkubwa wa Kikristo na Doctor wa Kanisa Pia alikuwa Askofu ni miongoni mwa watu walioshindana na kusababisha kuundwa kwa Orthodox katika karne ya 4 akishindania imani dhidi ya Arianism alisimikwa kuwa shemasi akiwa kijana  akitumika kama Katibu wa askofu wa Alexandria na ndipo alipopata nafasi muhimu ya kitheolojia ya kuongoza mapambano dhidi ya fundisho la Arius ambalo lilijadiliwa katika mkutano wa Nicea mwaka wa 325 na kwa ujumla alikuwa na nguvu ya ziada ya kupambana na imani hiyo na aliweza kueleza sawia kuwa mwana wa Mungu Yesu Kristo ni sawa na Mungu Baba  ingawa Arius aliendelea kudai kuwa sio sawa kwani Yesu ni kiumbe tu aliye mkamilifu kuliko viumbe wengine na kuwa alitumiwa na Mungu katika uumbaji na kazi nyingine za uumbaji.
Mijadala hii ilipelekea kuzuka kwa mjadala mkubwa kuhusu Utatu wa Mungu mjadala huu ulikuwa umekita miguu yake katka kutaka kujua kuhusu Uungu wa Yesu kwamba je Yesu I Mungu? Na kuna uhusiano gani kati ya Roho na Mwili wa Yesu Je Mungu ni Watatu au mmoja? Na wana uhusiano wa aina gani?

KUITISHWA KWA MKUTANO MKUU WA KWANZA WA NICEA MWAKA 325
Mkutano huu uliitishwa wakati wa Utawala wa Constantine ambaye alifuatilia kwa ukaribu sana mjadala mzima wa maswala ya utatu na uungu wa Yesu ingawa Lengo lake la kuitisha mkutano huu lilikuwa la Kisiasa zaidi yaani katika kuhakikisha kuwa Himaya yake inakuwa na amani aliitisha mkutano huo 19th June 325 mpaka Augosti 25th ni mkutano wa siku kama 67 maaskofu wapatao 300 walihudhuria wengi wao wakiwa ni kutoka Msahariki.




Constantine the Great

Mfalme Constantine mkuu alikuwa Mtawala wa Kwanza wa Kirumi aliyeokoka wakati wa utawala wake, mwanzoni aliwatesa wakristo lakiini baadaye akawa mkristo, alipokuwa Mkristo aliruhusu uhuru wa kuabudu alitoa eneo kubwa sana Estate na zawadi nyinginezo kwa Kanisa alistawisha mji mkuu jimbo la Mashariki na kuliita kwa jina lake Constantinopple ambao kwa sasa unaitwa Instanbul huko Uturuki, aliitisha mkutano mkuu wa Nicea mwaka 325

Mjadala mkuu katika mkutano hu ulikuwa ni kuhusu Fundisho la Arius kuhusu Asili ya Kristo kwamba je ni mwana wa Mungu na kuwa si sawa na Mungu na kuwa aliumbwa na kuwa yuko chini ya Mungu Baba
Neno kuu lilkuwa ni neno la kilatini Homo-Ousios yaani wa wa aina moja Jambo ambalo Arius alikuwa akilipinga
Hitimisho la Mkutano huo lilikubaliana kuwa fundisho la Arius ni la Uzushi na wazo la kuwa kuna wakati mwana hakuwako lilikataliwa na pia swala la kuwa aliumbwa kwanza kabla ya viumbe vingine lilikataliwa na Tamko la Nikea lilikuwa hivi
  “Tunamwamini Mungu Baba Mwenyezi Muumba  wa kila kinachoonekana na kisichoonekana  na Bwana mmoja Yesu risto Mungu kweli kutoka katika Mungu kweli Mwana wa azali asiyeumbwa mwenye uungu mmoja na Baba  ambaye kwa Yeye vitu vyote viliumbwa vya mbinguni na vya Duniani”
Na hii ndio ikawa imani liyonyooka Orthodox, swala la Utatu lilikubalika kwa maneno kama hayo kuwa wote ni ungu katika umoja, Mkutano wa Nicea ulikubaliana kutoa tamko moja ambalo baadaye lilithibitisha katika mkutano wa Constantonople mwaka 381 na hivyo imani ya Arianism ikawa imefikia mwisho katika utawala wa kirumi kwa sababu ya imani iliyonyooka Orthodox.

MASWALA BAADA YA MKUTANO WA NICEA
-          Baada ya mkutano wa Nicea Ukristo ulifanywa kuwa dini ya kitaifa kwa utawala wa Rumi  wakati huu kuliinuka maswala kadhaa yaliyopelekea kanisa  kuwa dhaifu na kulikuweko na mafundisho kadhaa ambayo yaliingizwa na wanadamu zikiwemo baadhi ya Sacrament
Saint Augustine wa Hippo Afrika ya Kaskazini (354-430).
Mtakatifu Augustine, alizaliwa huko Souk-Ahras, Algeria, mwaka 354 A.D.  Ndiye aliyeleta mpangilio wa kifaklsafa wa theolojia ya Kikrisro (a systematic method of philosophy to Christian theology). AugustineAlikuwa mwalimu huko rhetoric mji wa zamani katika miji ya in Carthage, Rome, na Milan Kabla ya kubatizwa na kuwa Mkristo mwaka 387. Alijadili Maarifa kuhusu kweli na kuhusu kuweko kwa Mungu kulimvuta Karibu na Mungu na Biblia na kutoka kwenye Falsafa za kizamani za kiyunani alikuwa mwanasheria wa Roman Catholicism, Augustine aliendeleza mafundisho mengi alipokuwa akijaribu kutatua migogoro mingi ya kitheolojia. Ikiwemo imani za Donatism na Pelagianism, imani kubwa mbili za kizushi zilizokuwa zikiendelea wakati ule.




 Saint Augustine

-          Ni mmoja wa Mababa wakubwa wa kilatini na Daktari wa Kimagharibi wa Kanisa alikuwa Askofu wa Hippo
-          Alizaliwa November 13th mwaka 354 huko Tagaste, Numidia kwa sasa (Souk-Ahras Algeria) Baba yake Paticius alifariki mwaka 371 alikuwa mpagani lakini baadaye aliokoka lakini mama yake Monica alikuwa mkristo aliyejitoa sana  na aliyemsaidia mwanae na hatimaye kukubalika katika kanisa la Roman Catholic, alisoma kati ya umri wa miaka 15-30 huko Madura na Cathage, baadaye aliishi na mwanamke ambaye jina lake halikujulikana kati ya mwaka 372 na alimzalia mwana wa kiume aliyempa jina Adeodatus jina la kilatini lenye maana ya Zawadi ya Mungu
-          Aliishi maisha rahisi naya kimonaki maandishi yake yaliliathiri kanisa  hata katika nyakati za leo
-          Alifundisha kuwa dhambi inatokana na asili ya uovu uliorithiwa kutoka kwa Adamu kwa neema ya Mungu  asili ya dhambi inaweza kuondolewa kwa wale walioandikiwa kuurithi uzima wa milele lakini neema hiyo si kwa wale walioandikiwa kutokuurithi uzima wa milele
-          Fundisho hilo ndio uliokuja kuwa msingi wa mafundisho ya John Calvin, Presybyterian na Baptist katika miaka ya baadaye.
Pelagius aliishi kati ya Karne ya nne na Tano (360? - 420?)
-          Alikuwa mwanatheolojia wa Kiingereza (Romano-British) na mtawa aliyekuja Rumi kati ya mwaka 410, Yeye hakukubaliana na fundisho la Augustino kwa kudai kuwa kila mwanadamu ana utashi Free will na kwa utashi wake aweza kuamua kuokoka au kukataa alikataa juu ya dhambi ya asili kutoka kwa Adamu kuwa ndiyo inayotuamulia alisisitiza kuwa ni utashi ndio unaotuamulia kufanya mema au kufanya uovu
-          Alisisitiza kuwa Yesu alitusaidia kwa kuonyesha mfano namna ya kuupata wokovu lakini matendo ya mwanadamu  ni ya lazima
-          Fundisho la Pelegius lilihukumiwa katika mkutano wa Cathage mwaka 415 na kutangazwa kuwa ni Uzushi na Pope na Mtawala wa Rumi  na fundisho la Augustino lilikubalika kuwa Orthodox mpaka wakati wa Arminius wa Uholanza na John Wesley wa Uingereza.
MKUTANO WA EFESO AD – 431
-          Bishano lingine lilizuka kati ya watawa  wa ki Nestorian, Mababa wa mashariki Constantinople na ki cyxill Mababa wa Alexandria  kuhusu  asili mbili za Kristo Uungu wake na Ubinadamu wake
-          Nestorius alikazia kupita kawaida ubinadamu wa Yersu na kukataa mafundisho kuwa  Mariam ni “theotokos”neno la kiyunani ambalo maana yake ni Mama wa Mungu yeye aliweka wazi kuwa Mama wa Yesu maana yake ni Mama wa mwanadamu Kristo Yesu tu
-          Mkutano wa Efeso ulihukumu fundisho hilo la waanestirism na kumpeleka utumwani Misri jangwani mwaka wa 435.
MKUTANO WA CHALCDON – 451 A.D.
-          Bishano la wa Alexandria na wa Constantinople halikuishia pale kwani mababa wa ki konstantinople waliendelea kusisitiza kuwa Kristo ana asili moja tu baada ya kufufuka na asili hiyo ni ya kiungu tu
-          Huu ulikuwa ni moja ya mikutano ya kanisa ya kihistoria ambapo kanisa liliketi kushughulikia migogoro unaohusu kuilewa asili ya kweli ya Yesu, Mkutano huu ulifanyika kati ya October 08, 451 - November 01, 451 Fundisho lilianzishwa na Bynzantine mtawa wa ki Eutiko walioamini katika Monophysitism ambayo ilikuwa ikisisitiza kuwa asili ya Kristo ni Mungu na sio mwanadamu, fundisho hilo lilitangazwa kuwa ni Uzushi uamuzi ulipelekea kanisa la Kimisri kugawanyika miongoni mwa waliokuwa wakiamini hivyo.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima

MFULULIZO WA MASOMO YAHUSUYO UTETEZI WA IMANI (APOLOGETICS) 3



MISINGI YA KIBIBLIA YA ELIMU YA UTETEZI WA IMANI.

Unaweza kujiuliza swali hili je watu wa nyakati za Biblia walijiingiza katika maswala ya utetezi wa imani? Manabii na mitume je walikutana na changamoto kama hizi tunazokutana nazo leo je waliitetea imani au kwa maana nyingine uko ushahidi wa kimaandiko unaoonyesha swala zima la kuitetea imani? Ni muhimu kwetu kuchukua safari fupi ndani ya maandiko ili kuthibitisha ukweli na maswali yaliyoko juu yetu

1.       Mfano wa Kitabu kizima cha Ayubu, ni wazi kabisa kuwa bi kitabu kinacho halalisha Matendo ya haki ya Mungu kwa wanadamu ni utetezi wa kazi sahii ya Mungu dhidi ya Rafiki ndugu na jamaa waliokuwa wakijaribu kumshawishi Ayubu kuachana na Mungu ni wazai kuwa mwandishi alikuwa akionyesha kuwa Mungu wa Israel ni tofauti na Miungu ya kipagani yeye ni mwaminifu
2.       Mfano katika kitabu cha Zaburi, ni wazi kuwa kwa mifano zaburi ya 19 & 119 zinathibitisha wazi kuwa Mungu yupo  na kuwa amejifunua wazi kupitia Neno lake na kazi zake ni wazi kwa mafano katika Zaburi 19 inaposema Mbingu zatangaza ni wazi kuwa nyota na mbingu ni kazi ya uumbaji wa Mungu uumbaji unatetea kuwekokwa Mungu.

3.       Mfano katika kitabu cha Warumi, sura ya kwanza na ya Pili kuwa kupitia uumbaji na dhamiri mwanadamu anao ushahidi unaomuonyesha kuwa anawajibika kwa Mungu bila kuwa na udhuru
4.       Mfano katika kitabu cha Matendo ya Mitume ni wazi kuwa tunamuona Paulo mtume akiitetea injili chini ya viongozi kama Felix, Festo na agripa, Kwa ujumla kitabu cha Matendo kinazungumza kwa upana namna injili ilivyoweza kutetewa. Kinatetea Ufufuo wa Yesu na uuungu wa Yesu, injili ya neema bila sheria ya tohara ya Musa na Hotuba ya Paulo mbele ya wanafalsafa wa kiyunani Matendo 17 hali yote hiyo ni Apologetics ni utetezi wa Imani
5.       Kwa ujumla hata nyaraka nyingi ziliandikwa kwa kusudi la kuitetea imani na kurekebisha mafundisho potofu na kuonyesha njia kupitia mafundisho halali ya kweli ya injili Wafilipi 1;7 ni wazi kuwa Paulo mtume alifanya kazi ya kuitetea injili, 1Petro 3;15 “Muwe tayari sikuzote kumjibu (Kujitetea) kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu lakini kwa upole na kwa hofu”  Be ready always to make Defense (Apologia) ni wazi kabisa kuwa Mitume waliifanya kazi hii ya kuitetea imani 

Utetezi wa Imani nyakati za Mapema baada ya Mitume.
Tangu nyakati za kanisa la kwanza Mateso yalikuwa yametapakaa na kupamba moto dhidi ya Kanisa  mapaka mnamo mwaka wa 250 hata hivyo watetezi wa imani wengi waliinuka na kuitetea imani, wengi wao walitumia mfumo wa mafundisho katika uandihi na baadhi ya watetezi maarufu wa mapema kabisa ni kama Aristide, Justine Matyr, Tatian, Tertullian, Origen Na Syprian walitoa hoja zao kwa watatwala wa kirumi, katika bunge la senet na kwa watu raia wa Rumi

Wao walitoa miito kadhaa kama miito ya haki.
Mfano Justin Martyr aliyeishi kati ya 100-165 alikuwa ni Mwanafalsafa, Mwanatheolojia na moja ya watetezi wa imani wa mapema sana katika kanisa alikata shauri kuikabili mamlaka kuacha kuwatesa wakristo kwa sababu walikuwa wakristo. Justin alizaliwa huko Flavia Neapolis ambako leo ni Nabulus ukanda wa mashariki wa miji ya kale ya Rumi huko shechem Samaria au Israel wazazi wake walikuwa wapagani, alipokuwa kijana alijitolea kusoma Falsafa kupitia maandiko ya Mwanafalsafa maarufu wa Kiyunani Plato na falsafa za wastoiki alikutana na Ukristo huko Efeso na baada ya kuokoka alikwenda Rumi na kustawisha Shule. Aliuawa huko Rome kama shahidi wakati wa Utawala wa Marcus Aurelius


Marcus Aurelius

Mtawala Marcus Aurelius aliitawala Rumi kati ya 161 na 180 utawala wake ulitawaliwa na maswala ya vita za marakwa mara  ni katika wakati wake ndipo Justin Martyr aliweza kuitetea imani.

Mfano wa mtetezi mwingine ni Tertulian ambaye aliandika miaka 50 baadaye baada ya Justin alukuwa ni moja ya watu muhimu sana katika ukristo na mwandishi wa vitini vingi vya kitheolojia katika lugha ya kilatini ambavyo kati ya hizo 30 zimesalia hata leo aliishi kati ya 190-220 ni mwana wa akida wa kikosi cha jeshi cha kirumi alikuwa amesomea sheria,aliokoka kati ya mwaka 190-95 alirudi kwao Cathage ambaye alioa na baadaye kuwa mwangalizi wa kanisa alikazia maadili na  nidhamu katika kanisa na alikuwa mtetezi wa imani mwenye kupinga uzushi alijaribu kukebehi miungu ya kipagani pamoja na sadaka zao za kuteteketeza zilizotolewa kwa miungu hiyo, aliitetea imani kwa nguvu akithibitisha kuwa Mungu anayetumikiwa na wakristo ndiye Mungu na kuwa tunamuabudu Mungu mmoja ambaye macho ya kawaida hayawezi kumuona ingawa Yupo.
Utetezi wa imani nyakati za karne ya Pili.
Wanatheolojia wa Kanisa la kiorthodox  (Imani ye kweli ya Kikristo) waliitwa watetezi wa karne ya Pili njia yao kubwa ya kiutetezi imekuwa njia kubwa ya muhimu ya kufuatawa na wanatheolojia na watetezi wengi wa kizazi hiki njia yao ilikuwa ni Kutoa Tamko, kutafasiri na kukanusha.

a.       Kutoa Tamko.
Utoaji tamko wakati wa utetezi unajumuisha Imani na kujiuliza mswali  kwamba imani Fulani je inahusiano na kile tunachokifikiri kuwa kweli kwa wakati huo kujiuliza maswali sio swala zima linalohusiana na imani na Imani haimaanishi wakati wote ni kujiuliza maswali Imani ni uhusiano wa mwanadamu na Mungu inampa mtu ujasiri kwa Mungu anayemtegemea hii ni imani endelevu kwa Mungu na ni Binafsi na inapimika kwani unaweza kuwa nayo nyingi au chache lakini imani inayozungumzwa katika Yuda ni imani  ambayo inaonekana ni mjumuisho wa kweli kamili iliyofunuliwa na Mungu katika neno lake yaani Biblia  na inaaaminiwa na wakristo hii ndio imani ambayo watetezi huikusanya pamoja kama misingi ya imani ya kweli ya Kikristo.
Kumbuka kuwa “Haitoshi kujua kile unachoamini, lakini ni muhimu kujua kwa nini unaamini unachokiamini”

b.      Kutafasiri.
Moja ya kazi nyingine ya Muhimu ya elimu ya Utetezi apologetics ni kutafasiri kweli ya Ukristo katika kipimo sahii cha elimu ya kanuni za kutafasiri maandiko.

c.       Kukanusha.
Ni kazi ya tatu ya elimu ya utetezi wakati wote katika historia kumekuweko na madai yaliyo kinyume dhjidi ya kanisa kwa kiwango fulani kwa mfano wayahudi waliifikiri imani ya Kikristo kuwa ni imani iliyokengeuka na kuiasi sheria ya Musa kwa warumi ilikuwa ni kikwazo, kwa wayunani ulikuwa ni ujinga 1Koritho 1; 21-24 kwa waislamu wanakataa kabisa swala la Yesu kuwa mwana wa Mungu na kuwa utatu ni uzushi. Kwa msingi huo uthamani wa Imani ya Kikristo ni Uhakika wa kweli na ulinzi dhidi ya maadui wa imani au mashambulizi ya kiimani.

MABARAZA NA MATAMKO YA IMANI.   (Councils & Creeds)
Matamko ya imani Creeds ni Neno la Kiingereza litokanalo na neno Credo la kilatini ambalo maana yake ni Ninaamini “Ibelieve” Matamko haya ya imani yalitokana na Mikutano au mabaraza ya kikanisa yaliyofanyika kwa nayakati tofauti kushughulikia maswala kadhaa ya kiimani.
1.       Mkutano wa kwanza wa kanisa.
a.       Mkutano mkuu wa kwanza wa kanisa ulifanyika Yerusalem kati ya mwaka wa 49 na 50 ukishughulikia swala la Wokovu kwamba je ni lazima mataifa waliookolewa kuishika sheria ya Musa na kupitia tohara ndipo wahesabike wameokolewa? Paulo na Barnaba walisimama kama watetezi wa imani na walishinda na kwa sababu hiyo kufungua mlango injili kwa ulimwengu kama matokeo ya ushindi huo.
b.      Mfumo wa kuweko kwa mamlaka.
Baada ya kufa kwa mitume Mateso pamoja na mafundisho mengi ya uongo yalijitokeza, Mitume walikuwa wametegemewa sana kama mamlaka ya mwisho kila kulipotokea tatizo na kanisa liliweza kustahimili mafundisho potofu na changamoto nyinginezo. Kwa kuwa mitume walikuwa wamekwisha kufa wote kanisa liliunda mfumo wa mamlaka
1.       Mfumo wa kuwepo kwa Maaskofu
2.       Kupitishwa kwa kanuni ya kupima maandiko
3.       Kustawishwa kwa kiriwa imani na matamko ya kiimani.
Hata kufikia mnamo mwaka 250 Kanisa lilikuwa tayari ni Taasisi yenye viongozi wake yaani Maaskofukatika miji mikuu na majimbo na kutokana na kuweko kwa mafundisho potofu kanisa lililazimika kuwa na Ukiri wa imani kwani kuweko kwa maaskofu na kanuni ya kupimia maandiko hakukusaidia kupambana na imani potofu kama imani ya Gnostics na nyinginezo.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

MFULULIZO WA MASOMO YAHUSUYO UTETEZI WA IMANI (APOLOGETICS) 2



MAFUNDISHO POTOFU WAKATI WA KARNE YA PILI.
Marcionites.

Ni imani iliyoanzinswa na mtu aliyeitwa Marcion  aliyeishi kati ya Mwaka wa 100-160 alizaliwa huko Sinope-Pontus yaani Uturuki ya Leo inaaminika kuwa huenda alikuwa mtoto wa askofu wa mji huo Imani yake ya uzushi ilianzia huko Rome kati ya mwaka 140 hivi  Yeye alisisitiza zaidi sana kuhusu Upendo wa Mungu  kuliko haki yake  na alilipinga vikali agano la kale
Alikuwa mpinzani mkubwa wa wayahudi na pia alikataa sehemu kubwa ya agano jipya ambayo alifikiri kuwa inawapaka mafuta wayahudi au ina uhusiano na imani ya kiyahudi aliamua kuandika Injili yake ambayo ilikuwa ikifanana sana na ile injili ya Luka ingawaje alikuwa ameruka Karibu 1/3 ya injili hiyo.
 Alitengwa na kanisa kama mzushi na alianzisha imani yake hiyo watu wake walijikana na waliacha kuoa ,  imani ilikuwa ana kupata nguvu ikiwa na askofu wake  pamoja na sacrament ya Ubattizo na meza ya Bwana lakini hawakutumia kabisa mvinyo wa divai. Walipinga swala la Incarnation na maswala ya Yesu kusulubiwa, aliamini katika umilele wa vitu vyote, waliendelea kuweko mpaka mnamo karne ya nne na imani hizi zilipingwa vikali na wakristo akiwemo Justin, Irenaeus, and Tertullian.

Montanists.

Ni mojawapo ya imani ya kizushi iliyoanzia wakati wa karne ya pili imnani hii ilianzshwa na Nabii Montanus aliyeishi huko Phyrigia ambayo sasa ni sehemu ya uturuki imani hii ilianza mnamo mwaka 156, Bwana Montanus alitokea katika kijiji kidogo na alianza kutoa unabii akidai kuwa amesikia sauti ya Roho Mtakatifu,Yeye na vijana wawili wa kike Prisca na Maximilla alizunguka akihubiri na kufundisha katika Asia ndogo, alifundisha kuwa mtu akianguka katika neema hawezi kukombolewa tena, waamini walitiwa moyo kuyatafuta mateso na sio kuyakimbia,
Imani hii iliweka mkazo na kukemea ubaridi katika kanisa kwani wakati huu kanisa lilianza kupoa na kuchukuliana na ulimwengu walikuwa wakijiandaa na ujio wa Kristo wa mara ya pili na hawakujali maswala ya kawaida zaidi ya kujiandaa na kuja kwa Bwana mnamo mwaka 177 kiongozi wa kanisa alihofia mgawanyiko wa kanisa na hivyo aliitenga imani ya Montaninism imani hii ilipata nguvu kwa sababu iliungwa mkono na mwanatheolojia wa kipoman Tertulian mpaka karne ya 6 imani hii ilikuwa imetoweka.

Gnosticism.
Ni moja ya imani potofu ya kale na ya zamani zaidi au ya muda mrefu zaidi, Neno Gnosticism lina tokana na neno la kiyunani Gnosis ambalo maana yake ni Maarifa au ujuzi, imani hii ilichanganya maswala ya kipagani na Ukristo.
Walifundisha kuwa baada ya Mungu mkuu kuna miungu mingine mingi midogomidogo ambayo baadhi yao ni mibaya na baadhi ni wema na kuwa kupitia wao ulimwengu uliumbwa ukiwa na Mchanganyiko wa mambo mema na mabaya
Wanafundisha kuwa Kristo ni miongoni mwa miungu hiyo na kuwa uweza wa uungu ulikuwa juu yake kwa muda, waliamini kuwa maandiko ni hadithi na kuwa unaweza kutafasiri maandiko haya kama kila msomaji apendavyo na aonavyo

KWA NINI IMANI POTOFU HUTOKEA?
Jibu moja jepesi kwa nini imani potofu hutokea ni kwa sababu kanuni za kutafasiri maandiko hazikuweko au haizizngatiwi, kwa msingi huo ni Ushauri wa somo hili kwamba kila mwanafunsi wa Biblia ni lazima ajifunze  kanuni za kutafasiri Biblia na kufahamu kuwa maandiko hayawezi kutafasiriwa kama kila mtu apendavyo Paulo alimwambia Timotheo katika 2Timotheo 2;15 kuwa ni muhimu kwake kulitumia neno la Mungu kwa halali kwa msingi huo hapa tunaelekeza maswala kadhaa ya kuzingatia wakati tunapotaka kulitafasiri neno la Mungu.
1.       Ni lazima uzingatie Mazingira.
Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia kwa mfano Agano la kale liliandikwa zaidi ya Miaka 3500 hivi iliyopita na huku wakati Agano jipya liliandikwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita  kwa msingi huo Mtafasiri wa maandiko anapaswa kuzingatia swala zima ka Historia, siasa, Falsafa na Tamaduni za wakati huo kuwa zinatofautiana na za sasa  kwa msingi huo ni lazima Mtafasiri afikiri kuwa kifungu Fulani cha maandiko kliwezaje kuwafaa watu wa nyakati zile na baadaye kuangalia kinawezaje kutumiwa katika wakati tulio nao.

2.       Ni lazima uzingatie Mabadiliko ya Lugha.
Ni muhimu kufahamu kuwa lugha za asili pia zilizotumiwa kuileta Biblia kwetu zilikuwa Kiibrania na kiyunani na sehemu chache kiaramu kwa msingi huo ni muhmu kufahamu lugha hizo zilimaanisha nini kwa wakati ule na ukumbke kuwa maana ya meneo hubadilika baada ya Karne kadhaa.

3.       Ni lazima Uzingatia sheria ya Muktadha Context.
Watu wanaweza kukengeusha maana halisi ya maandiko na kupata mafundisho ya uongo kama Muktadha yaani kifungu cha maandiko hakitazingatiwa unapotaka kuchanganua maana ya aya Fulani lazima uanze kujisomea kutoka juu ya aya hiyo na pia chini ya aya hiyo kwa mfano katika Zaburi ya 116; 11b “Biblia inasema Wanadamu wote ni waongo” lakini unaposoma andiko hilo vema kuanzia 11a utaweza kuona mwandishi akiweka wazi kuwa “Mimi nalisema kwa haraka yangu” unaona?

4.       Ni lazima maandiko unayotumia yawe yanaungwa mkono na maandiko mengine (Harmony).
Mara nyingi waalimu wa uongo hujitungia Mafundisho yao  kwa tafasiri zao kumbuka kuwa 1Petro 1;20-21 Biblia inasema unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu  kwa msingi huo ni lazima maana ya ujumla ya neno la Mung iweze kuzingatiwa na sio kamstari kamoja tu Zaburi 119;160 Unasema Jumla ya Neno lako ni kweli.

5.       Ni lazima ufanye kazi ya kutafuta maana iliyokusudiwa kisha uitumie. (Exegesis)
Neno la asili la kuelezea au kutafuta maana linatokana na asili ya kiyunani Exegeisthai ambalo maana yake ni kuelezea kwa hiyo mtafasiri ni muhimu kutafuata maana iliyokusudiwa na waandishi na andiko na kulinganisha ukweli na maandiko mengine na kasha kuelezea maana inayokusudiwa na Biblia au neno la Mungu na hapo ndipo mtu anakuwa amehubiri neno la Mungu na sio kulisingizia neno la Mungu Eisogesis. Kujitafutia maana yako mwenyewe na kuyasingizia maandiko.

6.       Ni lazima uzingatie swala la kujirudia kwa unabii (Multiple Fullfillment.)
Baadhi ya unabii una tabia ya kujirudia katika kutimizwa kwake kwa zaidi ya mara moja  kwa mfano swala la kurudi kwa Yesu Mara ya pili  liko katika mazingira makuu mawili Unyakuo na Ufunuo, au kunaweza kuwa na wapinga Kristo wengi katika historia lakini hatimaye kutakuwa na mpinga Kristo mmoja tu.

7.       Ni lazima wakati mwingine ukubaliane na maandiko kama yalivyo (Simplicity.)
Wakati wote ni muhimu kuzingatia kwanza Tafasiri iliyowazi katika maandiko kabla ya kuanza kufikiri kuwa ni mafumbo chagua maswala rahisi kuliko kujichagulia maswala magumu.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 
Rev Innocent Kamote