Jumanne, 26 Januari 2016

SOMO: JINA LA BWANA MUNGU WETU



Na Mchungaji: Innocent Kamote.
    Kuwa na Ufahamu kuhusu jina La Bwana Mungu wetu na kisha namna ya kulitumia ni kwa muhimu sana hususani katika kizazi chetu, Jina la Bwana Mungu linafunua uweza Mamlaka na asili ya Mungu wetu (Mithali 18: 10). Nyakati za Agano la kale watu wachache sana walifahamu siri na matumizi ya jina la Mungu na hivyo waliweza kufanya mambo makubwa nay a kupita Kawaida, Hata hivyo jina hili la Bwana Mungu wetu Bahati mbaya sana lilifichwa kabisa kwa watu wa agano la Kale kwa vile Mungu hakupenda walitumie kwa nyakati zao. Mungu alilificha jina hilo kwa faida kubwa sana ya watu wa Nyakati za Agano Jipya.

Tuta jifunza somo hili kwa kuzingatia Vipengele vifuatavyo:-
·         Jina la Bwana wakati kabla ya sheria
·         Jina la Bwana wakati wa Nabii Musa
·         Jina la Bwana wakati wa Manabii
·         Jina la Bwana wakati wa Agano Jipya

Jina La Bwana wakati Kabla ya Sheria
Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za kale kabla ya sheria ya Musa Jina la Bwana Mungu wetu lilifichwa, ilikuwa ni siri kubwa sana ambayo haikuweza kufunuliwa kwa kila mtu, kuna ushahidi wa kimaandiko kuwa watu wachache sana huenda walilifahamu jina la Bwana Mungu wetu na kulitumia hata hivyo walilitumia mara chache tu wakati wa kuabudu Mwanzo 4:25-26, baadhi ya wataalamu wa Biblia hudai kuwa Mstari huu unazungumzia kuhusu kuabudu kwa wazi jambo ambalo halikuweko wakati wa Adamu Hata hivyo mimi nina mtazamo tofauti kuwa Uzao wa Seth hawakulipuuzia jina la Bwana Mungu bali ulikuwa ni uzao uliolitaja na kulitumia kwa wazi, ni imani yangu kuwa Adamu alilijua jina hilo na Seth pia na Uzao wake jina hili lilihifadhiwa hata katika kizazi cha Shem na huenda Ibrahimu alilijua na kulitumia katika Ibada Mwanzo 12:8 ni ushahidi ulio wazi kuwa Ibrahimu alilijua jina hilo. Jina hili hata hivyo lilikua siri kuubwa sana.

Kulijua jina la Mungu lilikuwa ni shauku kubwa sana nyakati za Biblia katika Agano la kale  inawezekana kuwa ni wazi kabisa watu walisikia kua liko jina la Mungu na kuwa ukilijua na ukalitumia lina uweza mkubwa sana lakini ilikuwa siri kuu kulijua jina hilo Yakobo alikuwa mtu wa kwanza kumbana Malaika ili aweze kumwambia jina hilo hata hivyo hakufanikiwa Mwanzo 32:22-30, Musa alikuwa miongoni mwa watu waliochunguza sana na kutaka kulijua jina hilo na mara alipokutana na Mungu hili lilikuwa swali lake kuu na la kwanza, kwa ujumla Musa alitumia ujanja sana kutaka Mungu amwambia jina lake Kutoka 3:13, kwa nini hawa walitaka kujua Jina la Mungu walijua nguvu ya jina hili siri na utajiri uliomo katika jina hili na walitambua kuwa jina hili lilikuwa ni siri mmo, Inaonekana kwa namna Fulani Mungu alimfunulia Musa Jina hilo lakini kwa vila jina hilo ni siri Musa alilificha sana ni wazi kuwa Mungu mara kadhaa alimfunulia Musa jina hilo nah ii inaonekana ni kwa sababu huenda Musa aliendelea kudadisi sana akitaka kulijua jina hilo

Ø  Kutoka 6:3
Ø  Kutoka 33: 19
Ø  Kutoka 34:5-6

Jina hili ni jina lenye utukufu mwingi na ni jina lenye kuogopwa sana, Waebrania walitambua jina hili kama jina takatifu sana na waliogopa kulitaja jina hilo hovyo kiasi cha kulifanya likapotea Kumbukumbu 28:58-61. Uko ushahidi ulio wazi katika agano la kale ya kuwa mashujaa wengi wa imani waliotenda mambo makubwa nay a kushangaza walilijua jina hilo na kulitukuza 2 Samuel 22: 50-51. Daudi alitabiri kuwa Mataifa yote yataleta utukufu kwaajili ya jina hilo na Kumuabudu Zaburi 86;9.

Nyakati za agano la kale watu walikatazwa kulitumia jina hili hovyo au kulitaja pasipokuwa na sababu hii ikiwa ni pamoja na kutokuapa au kusema uongo au kuweka nadhiri kwa jina hilo na kutokuitimiza Kutoka 20:7
Haikuruhusiwa kulinajisi jina hili Walawi 18:21
Haikuruhusiwa kulikufuru jina hili Walawi 24:16
Jina hili linapaswa kutukuzwa Mathayo 6: 9

Kuna faida nyingi sana zinazoambatana na Matumizi ya jina hili Zaburi 20:1-7 Kwaajili ya jina hili ni vigumu sana Mtu kuachwa na Mungu kama analifahamu Mungu mwenyewe hawezi kukuacha kama unalijua jina lake 1 Samuel 12: 20 -22, Daudi aliweza kuiondoa aibu ya Isarael dhidi ya Goliath mfilisti kwaajili ya Jina hilo 1 Samuel 17: 45-47.

Pamoja na kujifunza mambo yote haya ya thamani kama mtu akilijua jina la Bwana Mungu swali kuu linabaki katikati yetu lipi ni jina Halisi la Bwana Mungu wetu? Yafuatayo ni majina kadhaa ambayo yanatumika au yametumiwa kumuelezea Bwana Mungu katika mafunuo ya aina mbalimbalinyakati za agano la kale Mungu alijifunua kwa Herufi nne tu YHWH (Yahweh), jina hili linasimama kumfunua Mungu kama Mwokozi, hata hivyo kifurushi cha wokovu kina marupurupu Mengi sana kwa msingi huo Mungu alijifunua kama mwokozi wa mazingira kadhaa ambayo kwa hayo watu walimuita Mungu jina hilo

1.      ELOHIM
Jina ELOHIM ni lenye asili ya Kiibrania ambalo hutafasiriwa Mungu anapojifunua kama Mungu Muumba Creator God na kwa asili ni jila lenye uwingi hivyo lina uhusiano na Utatu wa Mungu jina hili limetumika sana katika kitabu cha Mwanzo.

2.      YEHOVAH
Jina hili Yehova pia lina asili ya kibrania na lilitokana na jina ambalo Mungu alijifunua kwa Musa kwa Herufi kuu nne tu za Kiibrania cha zamani YHWH ambalo hutafasiriwa kama BWANA Hata hivyo jina YHWH linasimama kutokana na shughuli za wokovu jina hili lilibadilika kutokana na kukua kwa Lugha kwani wazee waliotafasiri Biblia toka katika kiebrania kuja katika kiyunani waliweka Herufi za silabu zilizopelekea jina hilo kusomeka YEHOVAH jina hili hata hivyo sio ufunuo kamili wa jina la Mungu kwani haliwezi kusimama pekee hivyo liliunganishwa na sehemu ya wokovu aliotoa Bwana kwa wakati na kwa watu maalumu mfano
*      YEHOVAH – RAPHA – Kutoka 15: 26 Mungu Mponyaji
*      YEHOVAH – NISSI- Kutoka 17:8-15 Mungu Bendera yetu
*      YEHOVAH – SHALOM – Waamuzi 6:24 Mungu amani yetu
*      YEHOVAH – RA’AH- Zaburi 23:1 Bwana Ndiye Mchungaji wangu
*      YEHOVAH – TSDIKENU – Yeremia 23:6 Mungu ndiye haki yetu
*      YEHOVAH – JIREH – Mwanzo 22:14 Mungu atatupatia
*      JEHOVAH – SHAMMAH – Ezekiel 48:35. Mungu yupo
3.      EL
Jina hilo la Mungu El lilikuwa na maana hiyo tu ya Mungu iliyotumika pia nyakati za agano la kale ni jina ambalo pia halikuwa na utoshelevu kwa vile kama Yehova halikuweza kutumika peke yake, jina hilo lilitumika pia kwa kuunganisha El na neon linmgine mfano
*      El – Elyon – ikiwa na maana ya MUNGU aliye juu sana Mwanzo 14:18 – 20
*      El – Shaddai- ikiwa na maana Mungu mwenye kutosheleza Kutoka 6:3
*      El – Olam – ikiwa na maana ya Mungu wa Milele Mwanzo 21:33

4.      ADONAI
Mungu pia alijifunua kwa jina la Adonai wakati wa agano la kale jina hili kwa asili ya nkiibrania ni BWANA au MWALIMU au mmiliki wa mashamba makubwa au mwenye serikali au utawala au mwenye serikali linatumika kuzungumzia ubwana wa Mungu Sovereign Kutoka 23:17
Hata hivyo siri kuhusu jina hili bado ilikuwa imefichwa

Jina la Bwana wakati wa Manabii
Bado kwa Muda mrefu watu walikua na kiu ya kutaka kulijua jina la Mungu iliaminika kabisa kuwa kulijua jina la Mungu kungeweza kutatua kabisa mateso na matatizo yaliyoweza kuisumbua jamii walitambua kuwa kulifahamu jina la Mungu sio tu kungeleta ulinzi na usalama kwao lakini pia kungesababisha kuwashinda adui zao Isaya 7:14 Ishara ya ushindi dhidi ya adui ilitolewa kuwa ni kuzaliwa kwa motto wa kiume ambaye angekuwa anaashiria kuwa Mungu yuko pamoja na wanadamu ni wazi kuwa nabii Isaya alionya kwa wazi kuwa Masihi angezaliwa na kuwa yeye anabeba majina yote ya Mungu lakini angezaliwa kama aina binadamu na kuishi nasi na kututambulisha jina hivyo majina yote ya Mungu sasa yangeweza kupatikana kwa jina moja tu ndani ya Mtoto tutakayepewa sisi wanadamu angalia Isaya 9:6-7
Isaya 9:6-7 ni kifurushi kamili cha wokovu ambacho Isaya anakiona lakini anashindwa kupata wazi kabisa jina la Mungu ingawa anayaona yote ni wazi kuwa ukiichunguza mistari hii utaona Mungu anatajwa kama 

Mungu mwenye nguvu – El shaddai
Mungu wa Milele – El Olam
Mfalme wa Amani – Jehovah Shalom
Uweza wa kifalmeUtawala na Nguvu  – Adonai
Utawala wa haki – Tsdekenu
Kuustawisha - Yire
Kuusimamisha – Rapha
Bwana – aliyeko aliyekuwako na atakayekuwako Niko ambaye niko
Isaya ni kama anaonyesha ya kuwa Mungu ambaye amejifunua kwa namna nyingi na kwa majina mengi akiokoa katika mazingira mbalimbali atakwenda kujidhihirisha katika namna moja au kwa jina moja litakalokuwa na utoshelevu kwa wanadamu, Naye nabii Yoel anathibitisha kuwa wakati Fulani Mungu angeachilia Roho wake kwa watu wote wenye mwili katika wakati huo Mungu atafanya mambo makubwa na kuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataponywa Yoel 2:28-32,Mungu aliwaficha manabii kuhusu mambo haya kwa ajili ya nyakati zetu 1Petro 1: 10-12.


Jina la Bwana wakati wa Agano jipya
Agano jipya ni habari njema kwa watu wote duniani ni habari kuhusu maisha na mafundisho ya Bwana wetu Yesu ni wakati ambao Mungu alitimiza ahadi zake alizonena kwa vinywa vya manabii hii inadhihirika pale malaika alipoleta habari njema ya kuzaliwa kwa motto wa kiume, Malaika alikuja na jina maalumu yaani YESU jina hili linatimiza wazi unabii ya kuwa huyu ndiye Mungu pamoja nasi ni wazi kabisa kuwa jina hili linabeba wokovu wote wa mwanadamu unaohusu kusamehewa Dambi na mahitaji mengine Mathayo 1:20-23. Ni wazi kuwa Jina hili ni jina la Mungu na yesu mwenyewe aliweka wazi kuhusu hilo Yohana 17:11-12, jina Hili Yesu ni jina lenye asili ya kiyunani lakini likitokana na asili ya kiibrania “Ye-ho-shua” au “Yesa” Kwa kiyunani Ieosus au Jesus kwa Kiingereza jina hili lina maana ya  Mungu mwokozi au Mkombozi ni wazi kabisa jina hili kwa kiibrania ndio Yoshua ni wazi kabisa kuwa Musa alilijua jina hilo na kusudi lisisahahulike aliliweka kwa mtumishi wake mwenyewe aliyeitwa HOSHEA Musa aliliweka jina hili kwa Mtumishi wake muaminifu ambaye pia angekuja kuwa mrithi wake na nabii ajaye baada yake Hesabu 13:16  jina Hoshea lilikuwa na maana ya wokovu lakini jina Yoshua lina maana ya WOKOVU WA MUNGU jina hili ndilo jina la YESU ni jina ambalo limeinuliwa juu kuliko majina yote Paulo mtume analiona wazi katika ulimwengu wa kiroho na ufunuo aliopewa kuwa hili sasa ndio jina la Mungu wetu Wafilipi 2:9-11 Jina hili linaashiria kuwa Mamlaka na cheo cha Yesu Kristo kipo juu zaidi.

·         Kila atakayeliitia jina hili ataokoka Matendo 2:21, Warumi 10:13.
·         Hakuna jina lingine tulilopewa litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa jina hili Matendo 4:10-12
·         Jina hili liko juu kuliko majina ya malaika wote Waebrania 1:4.
·         Ukiomba lolote kwa jina hili utapata Yohana 16:23-24.Yohana 14:13-14
·         Asiyeliamini jina hilo atahukumiwa na kuukosa Uzima wa milele Yohana 3:16-18
Jina la Yesu lilipoanza kutumika lilileta athari kubwa sana nyakati za Karne ya kwanza na kuufanya ulimwengu wa wakati huo kutaharuki, viongozi wa dini za kiyahudi waliwaonya sana mitume kuacha kulitumia jina hilo mara moja kwani lilikuwa limeleta mapinduzi makubwa na kuathiri dini zao Matendo 4:5-20, 5:17-33, kumbe ukitaka kuuudhi ulimwengu wa kidini na upinzani wa kiibilisi tumia jina la Yesu, Fundisha kuhusu Yesu hubiri kuhusu Yesu. Matendo 8:4-13,
Na Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima 
Rev Innocent Kamote

Ujumbe: Baraka Katika Mambo magumu


Ujumbe: BARAKA KATIKA MAMBO MAGUMU!
Andiko la Msingi:- Mathayo 14:22-33
“Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.  Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.     
 Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.  Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.  Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.  Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.  Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.  Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”

 Bahari ya Galilaya

Utangulizi:
Katika kifungu hiki cha maandiko, tunaona wanafunzi wa Yesu wakilazimishwa na Yesu mwenyewe waende nga’mbo, na baada ya muda wanajikuta wako katika dhuruba kali na msukosuko mkali, Lakini kumbuka hili wameamriwa na Mungu mwenyewe wavuke ngambo! Hii maana yake ni kuwa wako katika mapenzi ya Mungu, lakini pamoja na hilo wanapata misukosuko, wanajaribu kufanya kila wawezalo lakini inashindikana kupata suluhu

Biblia inatufundisha kuwa hili ni jambo la kawaida! Unaweza kujikuta uko katika wakati mgumu na ukaona mambo hayaendi, ama huduma haiendi, unajaribu kutumia akili na uwezo uliopewa na Mungu kutatua tatizo lakini hali ni kama ndo inazidi kuwa mbaya ni kama huwezi kutoka! Lakini uko katika mapenzi ya Mungu, ndugu msikilizaji wangu na msomaji wangu mpendwa wote huwa tunakutana na wakati kama huu, wote tunapitia haya uko wakati unahisi kama mambo hayawezi kumalizika, Ndoa zinapigwa hakuna amani, mafarakano, watoto hawasikii lakini eti ulimuomba Mungu uwe nao, Mke au Mume ambaye uliamini ni Mungu amekupa, Kazini, na biasharani, hakuna ushirikiano, umejaribu katika siasa na ukaomba na Mungu, hukutumia hata uchawi lakini umekatwa!, Unafiwa na mumeo au mkeo huku bado akiwa kijana na anahitajika zaidi mpaka unajiuliza nini mpango na makusudi ya Mungu? Mungu alikuwa wapi, yuko wapi je hangezuia hali hii?

Waebrania 12:11 “ Kila adhabu wakati wake haionekani  kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni, lakini  baadaye huwaletea wao aliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani” Ni muhimu tu kufahamu kuwa Magumu katika maisha yako yapo kwa sababu yanaambatana na Baraka zilizofichika, tunaweza tukawa wakati mwingine hatujui hili kwa dhati, lakini Mungu huruhusu, dhuruba katika maisha yetu na huenda kusudi likaeleweka baadaye! Katika maisha yangu mimi nimejifunza mambo kadhaa japo wakati mwingine nami hukata tamaa maana ni binadamu kama wengine na pia sikujiita katika ukristo au huduma ni Mungu ndiye aliyeniita, amenitunza katika hofu yake tangu utoto hivyo namcha yeye namuogopa sana japo ziko nyakati natamani kama kuwa huru  kutoka katika mikono ya Mungu niishi kama wanadamu wengine niwe huru kufanya lolote nitakalo nje ya sheria za Mungu, lakini hata hivyo siwezi kwa sababu nimezoezwa katika hofu ya Mungu na neno lake, katika uzoefu wangu wa Kutembea na Mungu na kutokana na ujumbe wa neno katika kifungu kile pale juu nimejifunza yafuatayo:-

1.       Magumu ni njia ya Mungu ya kututokea!
Wakati ambapo wanafunzi wa Yesu walikuwa wakipiga mayowe juu ya dhuruba ya bahari na upepo wake, ni juu ya dhoruba hiyohiyo Yesu alikuwa akiitumia kuwaendea, kumbuka kuwa pia ilikuwa gizani Biblia inatuambia ilikuwa yapata zamu ya nne usiku yaani ni kati ya saa tisa na saa kumi na mbili alfajiri ni usiku wa kutisha na dhoruba kali lakini Bwana alikuwa akija kutumia giza hilo na dhoruba hiyo.
2.       Mungu hututokea tunapokuwa tumekata tamaa!
Wanafunzi wa Yesu wengine walikuwa na ujuzi wa kupiga makasia kwani walikuwa wavuvi walikuwa na ujuzi na Bahari na ziwa, lakini walifikia ukingoni, walipigania maisha yao kwa njia zote walizozijua wao, na sasa inaonekana kila mmoja anakubali kwamba siku ile ndio siku yao ya kuiaga dunia, ndio mwisho wa kila kitu, Marko 6:48 inasema Akawaona  wakitaabika kwa kuvuta Makasia…… akataka kuwapita” kumbe Mungu huwa anaoona tunapojisumbua kwa namna mbalimbali kuhusu maisha na hutumia dhuruba hiyo kutujia, hata hivyo pia hutuonyesha kama anataka kutupita kama hajali, tukiwa tumekata tamaa hututokea, hatakuacha usipite katika magumu, lakini atatoa msaada wakati wa Magumu
3.       Mungu ni mkuu kuliko dhoruba unazopitia!
Kumbuka kuwa Mungu alipanga, alisema wavuke nga’ambo na aliwaona walipokuwa wakitaabika anajua hali walizokuwa wakipitia na hatari yake Mungu alitaka kuwafundisha kuwa yeye ni Mkuu kuliko Dhoruba, dhoruba zinatisha sana Lakini Mungu anatisha zaidi ya dhoruba anaweza kuzitumia dhoruba kupitisha neema yake magumu katika maisha haya ni njia ya Mungu iliyongumu kueleweka na kujua kusudi lake lakini neema yake ni kuu na huleta utukufu mkubwa 2Wakoritho 12;1-10 Hatupaswi kuogopa dhoruba za maisha wala kukata tamaa ni Mungu ameziruhusu na kuziratibu na kuzipanga na matokeo ni mema wakati wote Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa  katika mambo yote Mungu hufanya kazi na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake”
4.       Mungu anayo haki ya kutujaribu ufahamu wetu na imani yetu!
Yesu ni mwalimu, ni Rabbi alikuwa amedhihirisha uwezo wake kwa namna nyinyi na kuwafunza mambo mengi ya msingi, kumbuka aliwaambia na “TUVUKE MPAKA NGAMBO!” wanafunzi walipaswa kuamini, inatupasa kumuamini Mungu tu, ni lazima tuyaamini maneno yake, tuendelee kuamini hata kama twafa katika kuamini, wako watu ni waaminifu katika kutoa zaka, lakini hali zao ni duni na ni kama hawafanikiwi, wako watu waaminifu katika kumtumikia Mungu lakini  maisha yao magumu hakuna uzazi, mimba zinaharibika, wanajifungua kwa visu, ndoa mbaya, hakuna tendo la ndoa, watoto hawasikii wana tabia ambazo hata wewe na jamii yako hamkuwahi kuwa nazo, lakini ni lazima tuendelee katika kumuamini Mungu, tuamini kuwa hatimaye atatokea na kutupatia mema, Yesu alipokuwa anawajia wanafunzi wake waliogopa sana walidhani ni Mzimu, walilia kwa hofu kuu zaidi ashukuriwe Mungu Yesu alisema maneno matatu ya kutia nguvu
a.       Changamkeni/ Jipeni Moyo!
b.      Ni mimi
c.       Msiogope
Ni vigumu kuchangamka wakati wa mambo magumu, maana tunajihurumia na tunataka watu pia watuhurumie, Yesu anasema changamkeni, anajifunua kwao kuwa ni Yeye, hatimaye utatambua katika shida yako na mapito yako baadaye kumbe alikuwa ni yeye, na mwisho atakutia nguvu usiogope, Yeye aliyeiumba bahari na kuruhusu dhuruba yupo kuikemea na kuituliza.

Tembea juu ya Jaribu lako:

Mmoja wa wanafunzi Jasiri alipokundua kuwa ni Yesu na kuwa kila kitu kimetulizwa, alitaka kuonja utamu wa kutembea juu ya kile kilichowasumbua, Mungu anapokuwa amekufungua utatamani itokee tena ahaa kumbe ni Bwana! Utatamani ulikanyage tena jaribu lako Yesu alimruhusu Petro njoo kanyaga kile kilichokuonea, tembea juu yake hakina nguvu tena, umeinuliwa juu ya Jaribu lako, nakuhakikishia kuwa utatembea juu ya Jaribu lako, nimeona mara nyingi Mungu akinishika mkono na kunitia nguvu na kunipa ujasiri wa ajabu wakati wa majaribu, Mungu atafanya hivyo kwako leo!

Alichokifanya Yesu tunaweza:
Mungu ametupa uweza wa ajabu, chochote na lolote ambalo umemuona Yesu akikifanya ni kielelezo kwetu, ikiwa alishinda tutashinda pia, ikiwa alistahimili, tutastahimili tunaweza kufanya kile alichokifanya Yesu, Petro alisema Bwana kama ni wewe niamuru nije! Kama Bwana anaweza kutembea juu ya maji, juu ya majaribu yetu na mapito yetu twaweza kufanya kile alichikifanya Bwana!, twaweza kusamehe adui zetu, twaweza kufanya nao tena kazi, twaweza kuonyesha upendo hata kama walituonyesha chuki, kile alichokifanya Yesu tunaweza kukifanya, Yeye ni kiongozi mkuu nwa wakovu wetu na ametufundisha njia zake tunaweza kuzifuata!

Dhorouba ni njia ya Ushuhuda:
Utakapovuka watu wengi watatamani Baraka zako, ni muhimu wakajua kuwa ulipitia nini, Yesu aliwauliza Yakobo na Yohana Mtaweza kukinywea kikombe nikinyweacho mimi? Maana yake unataka kuwa kama mimi? Pitia mapito niliyopitia, kukua kwetu katika imani kunategemea na jinsi tunavyostahimili magumu mengi, aibu, kuzomewa na kuchekwa, kutukanwa na kukejeliwa ni sehemu ya upako wa Baraka zetu, ni sehemu ya Ushuhuda na Historia, Mapito unayopitia ni Historia ni ushuhuda, Dhoruba hiyo ni shuhuda, Mungu atakapo kukumbuka atakufuta machozi, atanyamazisha adui zako na wote waliokushutumu na kukudhulumu, na kukukandamiza na kufikiri kuwa Mungu hayuko nawe tena! Mungu atakapokutokea Dhoruba yako itageuka kuwa Ushuhuda, uwezo wako wa kumjua Mungu na Utendaji wake utaongezeka

Hitimisho
Ni vigumu kutambua Baraka zilizoko katika majaribu, ni vigumu kutabiri nini kitazaliwa na jaribu lako, wakati mwingine haijulikana litamalizwa lini kwa vile siku zinaenda, Hatujui asili ya Jaribu na tatizo unalolipitia, Lakini tunaweza kujua kuwa wewe unayepitia katika dhoruba Mungu atakutokea, atapitia katika jaribu lako,atakujia hata gizani zamu ya nne, nani ajuaye ataukemea upepo, atakuambia Changamka! Atajitambulisha kwako ni MIMI atakuambia usiogope atakuruhusu utembee juu ya jaribu lako na kulikanyaga!
“Yesu ni Yeye Yule jana leo na hata milele”

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote

JAMAA AKAANZA KUPONDA HASA.

Imepita miaka mine sasa tangu nilipopatwa na mkasa huu , wakati huo nilikuwa mkoani ambako nilikwenda kusalimia ndugu na jamaa kufuatia kupata vijisenti kidogo kwani nilikuwa sijakwenda huko kwa mia karibu mitano, kwa sisi wengine ambao maisha yetu ni ya kubahatisha kwa kiasi Fulani  inabidi ujiwekee vijiakiba vya kubahatisha kwa muda mrefu  kabla hujapata kiasi ambacho kwa hicho unaweza kwenda kusalimia nacho kwenu bila kuadhirika, kuna wakati inaweza kukulazimu kukomba hata nauli ya kurudia  huko sasa ndo kuadhirika kwenyewe.

wasema kweli huitwa wapondaji/wanafiki

Ninaishi Dar es Salaam kwa muda wa miaka 16 hivi sasa na shughuli zangu ni kubangaiza. Lakini kijijini kwetu wote wanajua kuwa kwamba mimi ni mfanya biashara maarufu huku Dar.Kwa hiyo ninapoenda  najitahidi kuwaonyesha wana kijiji kuwa mambo yangu si haba , ingawa kwenye familia yetu wanajua kuwa mimi nimechoka vilivyo, siku hyo nikiwa hapo kijijini nimewanunulia jamaa bia  huku nikiwa natamba sana  mara akatokea jamaa mmoja ‘ Du umekuja lini mshikaji mimi niko hapa tangu wiki jana alisema’ jamaa huyu huwa tunabangaiza wote kule mjini lakini sikuwa na jua kuwa ni mwana kijiji wa pale ingawa najua kuwa ni mwenyeji wa wilaya yetu, siku hizi mimi ni mwana kijiji mama aliolewa hapa na mzee, alimtaja moja ya wazee hao, Sasa mzee lete stori maana ngalambe zetu mjini tunazijua wenyewe alianza kusema na taratibu nilihisi hatari ikija halafu aliendelea , Washikaji huyu jamaa yangu kabisa wiki iliyopita tu  tulikuwa tuna kabiliana na mwenye nyumba ,Jamaa akaanza kuponda hasa, kwani tumepewa notisi geto yetu si unajua maisha ya bongo yalivyo mtu sita chumba kimoja  mambo magumu washikaji msije mjini kabisa asiwadanganye mtu…’ Kila nikifanya bidii ya kumzuia asizungumzie naona mwenzangu anazidi kuchanja mbuga na kumwaga siri za maisha yetu kule Dar , mwsho wale wapambe wangu wakaanza kuhoji kuhusu anachosema Yule jamaa, jamaa aliendelea  kusema ukweli kuhusu maisha yetu kule mjini, nilipoona vile na kwa sababu namjua ni mgomvi niuliona bora niondoke badala ya kubishana naye kwa kweli kesho yake  nikakuta taarifa zimeenea kijiji kizima kwamba huko Dar niliko ninabangaiza tu ilibidi niondoke siku hiyohiyo na kwenda kulala kijiji kingine na kusafiri siku iliyofuata  kurudi Dar Lakini nashukuru jamaa alinisaidia kwani baada ya pale niliamua  kuwa mkweli, leo hii hata hivyo maisha yangu yamebadilika na yamekuwa mazuri kiasi cha kutosha lakini siku zote sasa nimejifunza kuwa mimi tu na sitaki kujipandisha zaidi ya nilivyo katika hali halisia 
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima

NIKABWEDELA LIFTI KWA SAA TATU NZIMA.


Sitaki kutaja jina langu ingawa sio vibaya kufanya hivyo, Mimi ni kijana wa miaka 33 hivi Nilikuja Dar es Salaam kutoka Rufiji mwaka 1999 wakati huo nikiwa na miaka 27, kwa hiyo naweza kusema kwamba siifahamu Dar es Salaam vizuri, hata hivyo kutokufahamu Dar haina maana ya kutokufahamu mambo mengine ya kawaida ambayo kwa dunia ya sasa mtu anayeishi mjini kuyajua ni jambo muhimu, lakini pia la kawaida


Siku ninayotaka kuizungumzia ni Machi mwaka 2001 siku hiyo mjomba wangu ambaye ndiye aliyenilea  aliniita na kunituma , aliniambia niende mjini kwa jamaa yake mmoja nimpelekee fomu zake Fulani, huyo jamaa azishughulikie, alinielekeza ofisi za huyo jamaa zilipo, mjomba alinipa maagizo na kumtaja  huyo rafiki yake  ambaye nikimtaja pengine hata wewe utamfahamu ukifika pale’Panda lifti ghorofa  ya kumi ulizia ..’, Nilimkubalia na kuondoka ,nataka nikuambie jambo moja ni kwamba tangu kuja kwangu Dar nilikuwa nimepita majengo kadhaa wa kadhaa na kuona lifti Nasema kuona, basi nilipojua ni ghorofa ya kumi nilisema iko kazi, nilijiambia kuwa badala ya lifti ningetumia ngazi tu,Nilipofika kwenye jingo lenyewe ambalo lilikuwa bado jipya kabisa  wakati huo ilikuwa 2001 nilikwama baada ya kugundua kuwa hata njia ya kupandia ngazi kwa miguu sikuweza kuiona, Niliona aibu kuuliza kwa hofu ya kuonekana mshamba, Basi ilibidi nijiunge na watu wengine waliokuwa wakisubiri lifti na kupanda, sikuwa najua kuwa , nilifikiri labda kungekuwa na dereva na kondakta au mtu Fulani aliyeniendesha.

                                                                      lift Jamani !


Nilioona watu wanadandia name nikadandia, niliona watu wanaboinyeza kitu Fulani kasha taa inawaka, Nilijinyamazia, na kiroho kilianza kunidunda, Lifti ikapanda watu wana shuka na kuingia, mwisho watu wote wakashuka na wakapanda wengine , nilihisi kama lifti ilikuwa inashuka lakini sikuwa na uhakika nilienda nayo huku nikijaribu kujiuliza maswal, Niliona watu waliopanda wakishuka tena na wengine wapya waliingia na lifti ikaondoka kuelekea  huko inakoelekea , Mimi nilibana tu,nilikuwa naangalia watu wanavyobonyeza lakini sikuwa na uhakika ni kitu gani hasa kinachofanyika , Nilitembea na hiyo lifti mpaka nikahisi  kama vile ninjaumwa  maradhi ya moyo au kitu kingine kibaya zaidi Nilikwenda na kurudi kwenda na kurudi  tangu kwenye saa tano na nilikuwa na uhakika kuwa imefika saa nane .

Nikiwa nimefikia hatua ambayo sasa siwezi kuendelea kuwa bwege yaani kutaka kuuliza, Bwana mmoja mwenye mavazi ya kaki na bluu aliniuliza vipi hufiki unakokwenda? Tangu asubuhi uko ndani ya lifti, abiria wa lifti walivunja shingo zao kunitazama kama unavyojua watanzania masikio yako juujuu kama sungura kutaka kusikiliza ya watu, Nilibabaika lakini nilijikaza na kusema naenda ghorofa ya kumi lakini sipajui…” Yule jamaa ambaye kumbe alikuwa ni mesenja kwenye moja ya ofisi kwenye jingo lile alicheka na kusema ndio maana tangu saa tano hivi nakuona umo humu, naenda narudi nakuona mzee umo humu, nikadhani unataka kubwedela...” Abiria waliangua kicheko
Nilitazama chini hasa kwa kuzingatia kwamba kulikuwa na mademu wengi wakati huo mle kwenye lifti, Yule mesenja alikuwa kama amepata pa kuonyesha ujuaji wake ‘Ona ukitaka kwenda ghorofa ya kumi unabonyeza hapa..’ Halafu aliendelea kunifundisha mambo mengine ya lifti ni tuisheni ya bure lakini!

Nilishuka ghorofa ya kumi na kuulizia ofisi za Yule jamaa, Nilikuwa nahisi kizunguzugu mtindo mmoja, Niliambiwa huyo jamaa yake mjomba alikuwa ametoka Ilibidi nimsubiri hadi kwenye saa kumi aliporejea, Nilimkabidhi fomu na aliponiuliza sababu ya kuchelewa nilimwambia nilikuwa nimepotea jengo, unadhani wakati narudi nilipanda tena lifti? Kama unadhani hivyo shauri yako unadhani mbumbumbu niko peke yangu tuko chungu nzima

AKAJIFANYA ANA MAGARI YAMEKODIWA NA LOWASA.



Nilikaa mahali pale kwa muda mrefu sana nikimsubiri, Hatimaye alitokea, Alikuwa amevaa suti nzuri sana na alikuja na gari aina ya Corrola.Nilimsogelea na kumsalimia aliitikia na kuniambia nipande garini huyu alikuwa ni rafiki yangu mpya wa kiume, Kwa kweli ndio nilikuwa nimemaliza kidato cha sita  na nilikuwa kwenye maisha yangu, Huyu nilimkubalia kwa sababu nilihisi nampenda, siku hiyo ndiyo ilikuwa outing yetu ya kwanza  tangu tukutane naye nayeye kunitaka.

Niliingia kwenye gari na kabla sijasema lolote alisema samahani tunatumia  haka kagari ambako najua sio ka hadhi yako, kwani gari zangu mbili ziko katika kazi maalumu, zimeazimwa na ofisi ya waziri mkuu (WAKATI HUO NI EDWARD LOWASSA), haka ndiko kagari kangu ka awali kukanunua huwa anakatumia mdogo wangu kwendea chuoni, nilisema mbona ni gari zuri tu, tena linaonekana jipya, alicheka  kama vile nilikuwa nimezungumza lugha kutoka kwenye sayari nyingine “hapana hili ni gari wanalotumia watu ambaokidogo bado wako kwenye kujifunza kutafuta vijisenti vya kula, nilicheka kwa kujilazimisha  kwani nilijisikia vibaya  sana.

                                                                 Edward Ngoyai Lowassa

Tulikwenda hadi kwenye klabu moja maarufu kando ya bahari ya Hindi hapo tuliingia na kuamua kula na kunywa, mwenzangu aliagiza pombe na mimi juisi kwa sababu sinywi pombe, Hapo alianza kunielezea jinsi ambavyo ana malengo yake , Muda wote alikuwa anaongea yeye tu tena kwa kujisifu sana.Kwenye saa mbili hivi usiku waliingia watu watatu pale ukumbini na kuja moja kwa moja  pale tulipokuwa tumekaa, walipofika mmoja ambaye alionekana kuwa Baunsa  alisema ulidhani hutapatikana eh! Leo utakunaya hela yetu kutokea mdomoni au kokote ndio maana tulikataa kufanya kazi na mtu wa kula kulala…’

Yule jamaa yangu alikuwa ameshaanza kulewa, hivyo alipandisha na kusema hajui watu wale wanachokisema , ilibidi kuzuke vurugu, watu wale watatui walimshika jamaa yangu pamoja na mimi  na kutupakia ndani ya gari tuliyokuwa nayo, wewe ni mjinga sana  tunakupa gari  unasema una mteja kumbe unakuja kutanulia leo utatuambia udongo unaitwa nini kwa kizaramo mmoja wao alisema halafu aliongeza umepewa helka na …(Alimtaja mtu) unadai umetufikishia  kumbe ndio hizo unakwenda kutanulia na mademu zako..’Yule jamaa yangu alikuwa amenyamaza. Yule jamaa aliniambia anaishi sinza  lakini tulielekea Tandale na kufika kwenye nyumba moja gari, lilisimamishwa  na wale jamaa wakamshusha kwa nguvu, jamaa yangu na mimi  pamoja waliingia  kwenye ile nyumba  ‘fungua  tujue nini kimebeki tusipoteze kila kitu’ jamaa yangu alifungua mlango unajua nini nkilikuwa ni chumba chake.
Haki ya Mungu huwezi kuamini kulikuwa na kitanda cha futi nne, stuli nne, ndoo ya maji na redio kubwa (music system). Hakuwa na kitu kingine, wale wenzake walianza kupekua chumba na kuchukua hela zilizokuwa kwenye godoro chini halafu walimuomba funguo za gari aliwapa.
Mmooja wao alisema  hatuna haja ya kufanya dili na mtu wa dizaini yako.Sister kama unadhani umepata hapo jua kuwa utalia kilio cha mbwa, Nilishangaa kwamba jamaa yangu hakuweza hata kujitetea , wakati huu sikusikia tena habari ya magari yake mawili yaliyokuwa yamekodiwa kwa Ofisi ya waziri mkuu wakati ule Lowasa, kwa kweli sikumuaga niliondoka kimya kimya,huku umati wa watu ukiwa una tukodolea mimacho nashukuru Mungu kuwa ilikuwa usiku kama ningelikuwa sijaolewa hadi sasa niliapa nikimwona mwanaume mwenye kujipa misifa  na kujivuna hata kama angekuwa vipi  na ningemtemea mate. Nikakumbuka ule usemi wa Masiha kuwa kweli ajikwezaye atashushwa!

KAKAJIFANYA KAPAKA KUMBE NI CHUI.


Nilipokea msichana mzuri sana wa kazi hausigeli ambaye nilimpata kupitia rafiki yangu, Huyu rafiki yangu alikuwa na uhitaji wa hausigeli kwa siku nyingio kwa hiyo alitumia watu mbalimbali ili kupata hausigeli, wakati mmoja majibu yalipokuja alipata mahausigeli watatu, kwa kuwa alijua kuwa na mimi ninahitaji alinipa na mimi mmoja kati ya hao
 Chui akiwa Mawindoni

Binti huyu alikuwa anatokea Tanga wilayani Handeni, Alikuwa anataja vijiji tofauti tofauti kila akiulizwa kijiji anachotokea, mara Kwedizinga, kwediboma, kwedibangala, kwedibago,kwedikwazu n.k Hilo halikutusumbua kwani kuna watu wengine ni waongo mpaka wanajidanganya wenyewe.
Alianza kazi juni mwaka 2004, na hakuwa anajua kupika vyakula vingi, lakini nilijitahidi kumfundisha, pamoja na maswala ya chooni matumizi ya friji na jiko la umeme kwani kwake vilikuwa vitu vipya nilimfundisha vyote

Kumbe mwenzangu alikuwa anajua kila kitu hadi kucheza na intaneti kwa nini sasa akaja kufanya kazi za uhausigeli hapo ndipo penye habari  Msichana huyu ambaye kweli kwa umbo alikuwa mzuri kumbe kazi yake ilikuwa ni kuajiriwa kwenye nyumba ambazo anaziona ni alihamdulilah kiuchumi, halafu baada ya muda  anaanza kuwatongoza baba wenye nyumba , tulikaa naye mwezi mmoja  na mume wangu akaniambia hapa hauna mtoto wa kazi, Awali sikumuelewa alikuwa anamaanisha nini kumbe binti huyu alishaanza kumuwangia, baadaye tulikuja kuambiwa kwamba binti huyu akimtafuta mwanaume akishindwa  huzua visa  vikubwa, alipoona mume  wangu ana msimamo  alianza visa, siku moja aliniambia kuwa angependa kuondoka kwa sababu hakuja hapo kuvunja ndoa  yangu, nilipomuuliza ana maana gani aliniambia mama wewe ni mtu mzima najua unaelewa, vitu vingine ni aibu  hata kuvisema, kwa kweli niliumia sana , Nilimwambia avumilie kidogo, Mume wangu alipokuja nilimvaa, Nilipomvaa kwamba kamtongoza hausigeli mume wangu alicheka na kusema yaani huyo naye ni wa kutongozwa?

Kama ameshindwa mbinu zake sasa ndo anataka kutuvunjia ndoa, nitamsweka ndani mwambie’Mume wangu aliniambia lakini hakunishawishi, vya kutosha, Hatimaye mume wangu aliniambia visa ambavyo huyu binti alishawahi kumfanyia ikiwemo kumfuata chumbani na kumfunulia nguo akijidai eti ameumwa na nge kwenye mapaja ili eti mume wangu ajaribu kumtoa mwiba wa nge huyo, aidha wakati mwingine alijaribu kumshika mabega  wakati mume wangu alipoingia jikoni, aidha mara nyingi alikuwa akimkalia vibaya na kumkonyeza kila wakati

Ilibidi nimfungishe virago siku hiyo hiyo, Kesho yake nilimfuata Yule rafiki yangu  na kuulizia kwa undani kuhusu binti Yule, akasema ilikuwa leo nikuulize habari za huyo binti  maana nimepata habari zake juzi tu  hadi nikashindwa kuamini nikasema nikuulize leo ili ufanye uamuzi nilibaki nimeduwaa Niliambiwa binti huyo alishavunja ndoa tatu za watu hapa dar  katika moja ya hizo alishaolewa yeye  badala ya mama mwenye nyumba  na akamfilisi kabisa mwanaume Yule na kumwacha kwa hiyo ndoa yangu ilikuwa iwe ya nne kufisadiwa  “lo kumbe kalijifanya kapaka kumbe ni chui”

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote