Jumanne, 26 Januari 2016

Ujumbe: Baraka Katika Mambo magumu


Ujumbe: BARAKA KATIKA MAMBO MAGUMU!
Andiko la Msingi:- Mathayo 14:22-33
“Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.  Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.     
 Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.  Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.  Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.  Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.  Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.  Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”

 Bahari ya Galilaya

Utangulizi:
Katika kifungu hiki cha maandiko, tunaona wanafunzi wa Yesu wakilazimishwa na Yesu mwenyewe waende nga’mbo, na baada ya muda wanajikuta wako katika dhuruba kali na msukosuko mkali, Lakini kumbuka hili wameamriwa na Mungu mwenyewe wavuke ngambo! Hii maana yake ni kuwa wako katika mapenzi ya Mungu, lakini pamoja na hilo wanapata misukosuko, wanajaribu kufanya kila wawezalo lakini inashindikana kupata suluhu

Biblia inatufundisha kuwa hili ni jambo la kawaida! Unaweza kujikuta uko katika wakati mgumu na ukaona mambo hayaendi, ama huduma haiendi, unajaribu kutumia akili na uwezo uliopewa na Mungu kutatua tatizo lakini hali ni kama ndo inazidi kuwa mbaya ni kama huwezi kutoka! Lakini uko katika mapenzi ya Mungu, ndugu msikilizaji wangu na msomaji wangu mpendwa wote huwa tunakutana na wakati kama huu, wote tunapitia haya uko wakati unahisi kama mambo hayawezi kumalizika, Ndoa zinapigwa hakuna amani, mafarakano, watoto hawasikii lakini eti ulimuomba Mungu uwe nao, Mke au Mume ambaye uliamini ni Mungu amekupa, Kazini, na biasharani, hakuna ushirikiano, umejaribu katika siasa na ukaomba na Mungu, hukutumia hata uchawi lakini umekatwa!, Unafiwa na mumeo au mkeo huku bado akiwa kijana na anahitajika zaidi mpaka unajiuliza nini mpango na makusudi ya Mungu? Mungu alikuwa wapi, yuko wapi je hangezuia hali hii?

Waebrania 12:11 “ Kila adhabu wakati wake haionekani  kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni, lakini  baadaye huwaletea wao aliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani” Ni muhimu tu kufahamu kuwa Magumu katika maisha yako yapo kwa sababu yanaambatana na Baraka zilizofichika, tunaweza tukawa wakati mwingine hatujui hili kwa dhati, lakini Mungu huruhusu, dhuruba katika maisha yetu na huenda kusudi likaeleweka baadaye! Katika maisha yangu mimi nimejifunza mambo kadhaa japo wakati mwingine nami hukata tamaa maana ni binadamu kama wengine na pia sikujiita katika ukristo au huduma ni Mungu ndiye aliyeniita, amenitunza katika hofu yake tangu utoto hivyo namcha yeye namuogopa sana japo ziko nyakati natamani kama kuwa huru  kutoka katika mikono ya Mungu niishi kama wanadamu wengine niwe huru kufanya lolote nitakalo nje ya sheria za Mungu, lakini hata hivyo siwezi kwa sababu nimezoezwa katika hofu ya Mungu na neno lake, katika uzoefu wangu wa Kutembea na Mungu na kutokana na ujumbe wa neno katika kifungu kile pale juu nimejifunza yafuatayo:-

1.       Magumu ni njia ya Mungu ya kututokea!
Wakati ambapo wanafunzi wa Yesu walikuwa wakipiga mayowe juu ya dhuruba ya bahari na upepo wake, ni juu ya dhoruba hiyohiyo Yesu alikuwa akiitumia kuwaendea, kumbuka kuwa pia ilikuwa gizani Biblia inatuambia ilikuwa yapata zamu ya nne usiku yaani ni kati ya saa tisa na saa kumi na mbili alfajiri ni usiku wa kutisha na dhoruba kali lakini Bwana alikuwa akija kutumia giza hilo na dhoruba hiyo.
2.       Mungu hututokea tunapokuwa tumekata tamaa!
Wanafunzi wa Yesu wengine walikuwa na ujuzi wa kupiga makasia kwani walikuwa wavuvi walikuwa na ujuzi na Bahari na ziwa, lakini walifikia ukingoni, walipigania maisha yao kwa njia zote walizozijua wao, na sasa inaonekana kila mmoja anakubali kwamba siku ile ndio siku yao ya kuiaga dunia, ndio mwisho wa kila kitu, Marko 6:48 inasema Akawaona  wakitaabika kwa kuvuta Makasia…… akataka kuwapita” kumbe Mungu huwa anaoona tunapojisumbua kwa namna mbalimbali kuhusu maisha na hutumia dhuruba hiyo kutujia, hata hivyo pia hutuonyesha kama anataka kutupita kama hajali, tukiwa tumekata tamaa hututokea, hatakuacha usipite katika magumu, lakini atatoa msaada wakati wa Magumu
3.       Mungu ni mkuu kuliko dhoruba unazopitia!
Kumbuka kuwa Mungu alipanga, alisema wavuke nga’ambo na aliwaona walipokuwa wakitaabika anajua hali walizokuwa wakipitia na hatari yake Mungu alitaka kuwafundisha kuwa yeye ni Mkuu kuliko Dhoruba, dhoruba zinatisha sana Lakini Mungu anatisha zaidi ya dhoruba anaweza kuzitumia dhoruba kupitisha neema yake magumu katika maisha haya ni njia ya Mungu iliyongumu kueleweka na kujua kusudi lake lakini neema yake ni kuu na huleta utukufu mkubwa 2Wakoritho 12;1-10 Hatupaswi kuogopa dhoruba za maisha wala kukata tamaa ni Mungu ameziruhusu na kuziratibu na kuzipanga na matokeo ni mema wakati wote Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa  katika mambo yote Mungu hufanya kazi na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake”
4.       Mungu anayo haki ya kutujaribu ufahamu wetu na imani yetu!
Yesu ni mwalimu, ni Rabbi alikuwa amedhihirisha uwezo wake kwa namna nyinyi na kuwafunza mambo mengi ya msingi, kumbuka aliwaambia na “TUVUKE MPAKA NGAMBO!” wanafunzi walipaswa kuamini, inatupasa kumuamini Mungu tu, ni lazima tuyaamini maneno yake, tuendelee kuamini hata kama twafa katika kuamini, wako watu ni waaminifu katika kutoa zaka, lakini hali zao ni duni na ni kama hawafanikiwi, wako watu waaminifu katika kumtumikia Mungu lakini  maisha yao magumu hakuna uzazi, mimba zinaharibika, wanajifungua kwa visu, ndoa mbaya, hakuna tendo la ndoa, watoto hawasikii wana tabia ambazo hata wewe na jamii yako hamkuwahi kuwa nazo, lakini ni lazima tuendelee katika kumuamini Mungu, tuamini kuwa hatimaye atatokea na kutupatia mema, Yesu alipokuwa anawajia wanafunzi wake waliogopa sana walidhani ni Mzimu, walilia kwa hofu kuu zaidi ashukuriwe Mungu Yesu alisema maneno matatu ya kutia nguvu
a.       Changamkeni/ Jipeni Moyo!
b.      Ni mimi
c.       Msiogope
Ni vigumu kuchangamka wakati wa mambo magumu, maana tunajihurumia na tunataka watu pia watuhurumie, Yesu anasema changamkeni, anajifunua kwao kuwa ni Yeye, hatimaye utatambua katika shida yako na mapito yako baadaye kumbe alikuwa ni yeye, na mwisho atakutia nguvu usiogope, Yeye aliyeiumba bahari na kuruhusu dhuruba yupo kuikemea na kuituliza.

Tembea juu ya Jaribu lako:

Mmoja wa wanafunzi Jasiri alipokundua kuwa ni Yesu na kuwa kila kitu kimetulizwa, alitaka kuonja utamu wa kutembea juu ya kile kilichowasumbua, Mungu anapokuwa amekufungua utatamani itokee tena ahaa kumbe ni Bwana! Utatamani ulikanyage tena jaribu lako Yesu alimruhusu Petro njoo kanyaga kile kilichokuonea, tembea juu yake hakina nguvu tena, umeinuliwa juu ya Jaribu lako, nakuhakikishia kuwa utatembea juu ya Jaribu lako, nimeona mara nyingi Mungu akinishika mkono na kunitia nguvu na kunipa ujasiri wa ajabu wakati wa majaribu, Mungu atafanya hivyo kwako leo!

Alichokifanya Yesu tunaweza:
Mungu ametupa uweza wa ajabu, chochote na lolote ambalo umemuona Yesu akikifanya ni kielelezo kwetu, ikiwa alishinda tutashinda pia, ikiwa alistahimili, tutastahimili tunaweza kufanya kile alichokifanya Yesu, Petro alisema Bwana kama ni wewe niamuru nije! Kama Bwana anaweza kutembea juu ya maji, juu ya majaribu yetu na mapito yetu twaweza kufanya kile alichikifanya Bwana!, twaweza kusamehe adui zetu, twaweza kufanya nao tena kazi, twaweza kuonyesha upendo hata kama walituonyesha chuki, kile alichokifanya Yesu tunaweza kukifanya, Yeye ni kiongozi mkuu nwa wakovu wetu na ametufundisha njia zake tunaweza kuzifuata!

Dhorouba ni njia ya Ushuhuda:
Utakapovuka watu wengi watatamani Baraka zako, ni muhimu wakajua kuwa ulipitia nini, Yesu aliwauliza Yakobo na Yohana Mtaweza kukinywea kikombe nikinyweacho mimi? Maana yake unataka kuwa kama mimi? Pitia mapito niliyopitia, kukua kwetu katika imani kunategemea na jinsi tunavyostahimili magumu mengi, aibu, kuzomewa na kuchekwa, kutukanwa na kukejeliwa ni sehemu ya upako wa Baraka zetu, ni sehemu ya Ushuhuda na Historia, Mapito unayopitia ni Historia ni ushuhuda, Dhoruba hiyo ni shuhuda, Mungu atakapo kukumbuka atakufuta machozi, atanyamazisha adui zako na wote waliokushutumu na kukudhulumu, na kukukandamiza na kufikiri kuwa Mungu hayuko nawe tena! Mungu atakapokutokea Dhoruba yako itageuka kuwa Ushuhuda, uwezo wako wa kumjua Mungu na Utendaji wake utaongezeka

Hitimisho
Ni vigumu kutambua Baraka zilizoko katika majaribu, ni vigumu kutabiri nini kitazaliwa na jaribu lako, wakati mwingine haijulikana litamalizwa lini kwa vile siku zinaenda, Hatujui asili ya Jaribu na tatizo unalolipitia, Lakini tunaweza kujua kuwa wewe unayepitia katika dhoruba Mungu atakutokea, atapitia katika jaribu lako,atakujia hata gizani zamu ya nne, nani ajuaye ataukemea upepo, atakuambia Changamka! Atajitambulisha kwako ni MIMI atakuambia usiogope atakuruhusu utembee juu ya jaribu lako na kulikanyaga!
“Yesu ni Yeye Yule jana leo na hata milele”

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote

Hakuna maoni: