Alhamisi, 28 Januari 2016

UJUMBE: KUTAFUTA AMANI KWA BIDII


Waebrania 12:14 “Biblia inasema hivi, Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”
Watu wengi sana duniani wanaishi maisha ya uchungu, na majuto na wakati mwingine kuzikosa Baraka za Mungu kwa sababu hawana ufahamu wa umuhimu wa kuwa na amani na watu wote, kukosa kuwa na amani na watu wote kunatukosesha Baraka nyingi sana ambazo Mungu amekusudia kwetu, leo tutazungumzia kwa undani sana umuhimu wa kuitafuta amani, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vya msingi vifuatavyo.


  • ·         Maana ya amani
  • ·         Maana ya neno bidii
  • ·         Kutafuta amani kwa bidii.



      Maana ya amani.
Neno amani linalotajwa katika Biblia ni tofauti sana na neno amani linavyotumika katika mazingira tuliyoyazoea, Kibiblia neno amani lina maana pana zaidi, Katika lugha ya Kiebrania neno amani maana yake ni SHALOM sawa na neno Salaam la kiarabu na Salama la Kiswahili, kwa kiyunani Irene neno hili linamaanisha ni kuwa na ustawi katika mazingira yote ya mwili nafsi na roho na kutokuwa na vita pande zote yaani vita vya kimwili na kiroho na nafsi ni kuwa na utulivu au SOLOMON kwa kiibrania yaani kuwa na amani pande zote au kutokuzungukwa na mazingira ya uadui au kuwa na maadui, wengi wetu tutakuwa tunafahamu kihistoria kuwa hata Mji wa “Dar es Salaam” una uhusiano na tafasiri ya kiarabu ya Amani ambapo Sultani Baraghash aliuona mji wa Mzizima kuwa ni bandari ya utulivu kuliko Zanzibar na kwa sababu alipewa ukanda wa Pwani ya Afrika mashariki kuutawala alihamishia makazi yake Mzizima na kupaita Dar es Salaam kwa kiarabu  ikiwa na maana ya Bandari ya salama, Jina Yerusalem kiibrania pia humaanisha mji wa Amani.
Msgingi mkubwa wa mafanikio ya mwanadamu awaye yote ni amani, ili Familia, Ndoa, taasisi, na hata taifa liweze kuwa na ustawi linahitaji amani, na shetani anajua wazi kabisa kuwa amani ikiwako kila kitu kitafanikiwa hivyo ili aweze kuvuruga Ndoa, Familia, taasisi au Taifa shetani atakachokifanya ni kuiiba amani kwanza kumbuka kuwa yeye anaitwa mwivi katika maandiko na kazi yake ni kuiba, kuchinja na kuua Yohana 10: 10 Biblia inasema hivi “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele”. Shetani wakati wote atatafuta kuiiba amani ili kuharibu kila kitu yakiwamo mafanikio na baraka Mungu alizokusudia kwetu na amani inapotoweka kila kitu hupoteza maana na hata maisha huonekana kama hayana umuhimu tena.

Maana ya neno Bidii
Neno bidii au juhudi Katika kiingereza Biblia ya NIV inatumia neno “Make every Effort” na Biblia ya kiingereza iitwayo Amplified inatumia neno “Strive” ambalo maana yake ni  “try very hard to achieve” kwa maana nyingine Biblia inasema fanya kila juhudi, au jitihada au kila liwezekanalo, au kwa gharama yoyote au juu chini au hakikisha au pambana kwa namna yoyote ile kuhakikisha kuwa unakuwa na amani na watu wote, kama biblia inasisitiza hilo basi ni muhimu kuzingatia kuwa amani na watu wote ni jambo la muhimu sana sana

Kutafuta amani kwa Bidii 
Yakobo ni moja ya mfano muhimu sana wa kibiblia ya mtu aliyetatufa amani kwa bidii, wote tunafahamu historia yake na kaka yake pacha wake aliyeitwa Esau, wao walikuwa ndugu tena mapacha walikuwa pamoja kwa upendo na hawakuwahi kuwa na ugomvi wakati wowote mpaka tunaposoma kisa cha ajabu kuwa ndugu hao walifikia hatua ya kjuwa na uadui wa hali ya juu kiasi cha mmoja kutamani kumuua mwenzi wake kutokana na Yakobo kuuchukua Mbaraka wa Esau kwa hila, jambo hili lilivuruga kabisa mahusiano yao Mwanzo 27:41-45 Biblia inasema hivi
“Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.  Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua.  Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani;  ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke;  hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?”
Unaona ndugu msomaji wangu uhusiano wa ndugu hao wa karibu inaweza kuwa picha yaw ewe na rafiki yako, au mpendwa mwenzako au mumeo au mkeo chuki inaingia kiasi cha kutaka kumalizana, hii ndio ilikuwa hali ya Esau na Yakobo waliachana vibaya na sio kwa amani, na kutokana na hiki alichokifanya Yakobo ukweli ni kuwa Yakobo alikabiliwa na maisha ya taabu na dhiki na matesoi mengi sana kuliko mtu yeyote katika Biblia aliteseka na kupata fadhaa nyingi sana kwa sababu aliuacha moyo wa kaka yake ukiwa hauna amani naye, hata ingawa alifanya kazi kupata mke na mali alizipata kwa shida nyingi yeye mwenyewe anakiri mbele ya Farao kuwa Maisha ya kusafiri kwake yamekuwa ya dhiki na mateso mengi kuliko ya kusafiri kwao baba zake unaweza kuona  Mwanzo 31:4-7 Biblia inaonyesha haya kuwa Yakobo hata huko Ujombani aliamua kutoroka kutokana na shida na taabu alizozipata
 Mwanzo 31:4-7 “Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia, Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru.”
Mwanzo 31: 22-29, 39-42 “Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala. Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku. Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu. Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi. Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu”.
Unaweza kuona maisha ya Yakobo hayakuwa Rahisi licha ya Baraka alizokuwa amezipora alipitia shida mateso na maumivu mengi na sasa ni kama yuko Hatarini anaachana na mjomba wake katika mazingira magumu na sasa ni kama anakotoka kubaya na anakorudi kubaya ameteseka kwa takriban miaka 20 alipopoteza mnyama alilipishwa na sasa maisha yake yako hatarini alitambua kosa lake ni kwa sababu moyo wa kaka yake hauna amani na yeye
Mwanzo 32:3-8  Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu.  Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako.  Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.  Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka.”
Unaweza kupata picha katika mistari hii sasa Esau anapata habari kuwa Yakobo anakuja na anamkabili na askari wapatao mia nne ulikuwa wakati mgumu sana kwa Yakobo na hivyo aliamua kumuomba Mungu Mwanzo 32:9-12 biblia inasema wazi
 “Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, BWANA, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema;  mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili.  Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.”        
Pamoja na maombi ya kuonyesha kumuogopa Esau yak obo alitambua kuwa maombi pekee hayaytoshi na hivyo alilazimika kuandaa zawadi za kutosha ili aweze kupata suluhu na kuurejesha tena moyo wa kaka yake, wapendwa wengi hawafikiri kuwa unapoujeruhi moyo wa ndugu yako unahitaji kuutafuta tena kwa gharama yoyote, Ndugu yako akiwa na kinyongo nawe na uchungu nawe maisha yako yatakuwa ya taabu na mateso na uchungu mwingi na huwezinkufanikiwa sasa Yakobo alikuwa tayari amekwisha pata somo kuhususwala hili na alikuwa na uelewa kuwa Mungu sio wakwake pekee alitambua kuwa anapaswa kunyenyekea aliytambua kuwa Esau ni Bwana na Yeye ni mtumwa tu! Alikubali kujishusha nili kupata kibali kwa kaka yake
Wako wapendwa wengine wanaweza kukutukana na kukunenea maneno mabaya nay a kukubomoa na hata kufanya hila na uzushi ili uharibikiwe na kisha wakafikiri wako sahii mbele za Mungu, ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika upendo wake hafurahii udhalimu sasa Yakobo alibadilika na kuwa mtu mwingine akinyenyekea  angalia hatua alizochukua
Mwanzo 32:13-21 “Biblia inasema hivi Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye; mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini;  ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi.  Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi. Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako?  Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu. Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta.  Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu. Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini”.
Yakobo alifanya jitihada kubwa sana katika kurejesha amani ni jambo la kushangaza kuona kuwa wako watu wanapoteza amani na ndugu zao jamaa zao na wanashindwa hata kutumia ujumbe wa shs 50 kwa simu kuomba radhi, kila mmoja anapokuwa na kiburi na kukataa kujishusha ni wazi kuwa amani haiwezi kupatikana Yakobo alijirudi kwa kweli alikuwa amebadilika si mwenye kupenda makuu tena
Mwanzo 33 :1-11 unaonyesha mafanikio ya jitihada ya kutuatuta amani kwa bidii bilia inasema hivi “Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao.  Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho.  Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia.  Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama.  Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama.  Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako.  Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea”.

Biblia inaonyesha juhudi za Yakobo zilizaa matunda na hatimaye alipokelewa vema na Ndugu yake na wote wakalia machozi na kusameheana moyo wa Esau ukawa na amani na Yakobo!
Ni kupitia mfano huu wa Yakobo Biblia inasema tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote je unafanya jitihada gani kuhakikisha unakuwa na amani na watu wote, unawezaje kuendelea kusali na kuomba na kuabudu huku hauna amani na ndugu yako, mfanya kazi mwenzako,mkeo , mumeo nduguzo mwanasiasa mwenzako na kadhalika. Tukitafuta amani Mungu ataondoa huzuni zote na uadui na kutupa faraja na tutafurahia kila kinachotuzunguka

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

JINSI YA KUSTAWI KAMA MTENDE.(Flourishing like a palm tree)



Zaburi 92:12-15.

     Nyakati hizi tulizo nazo kumekuwepo na wimbi kubwa sana na shauku ya watu kutakakufanikiwa,   na watu wengi sana wanafanikiwa kwa vile wana nia ya kufanikiwa, hata hivyo, mafanikio ya watu wengi sana hustawi kwa muda mfupi na baada ya muda hufilisika na kuishiwa kabisa au kubakiwa na historia ya jinsi walivyofanikiwa!

     Mungu katika mapenzi yake anataka tufanikiwe sana, lakini zaidi anataka tufanikiwe na mafanikio yetu yaweze kudumu kizazi na kizazi, Biblia inapozungumzia ustawi wa kudumu inazungumzia miti miwili yaani mtende na Mwerezi wa Lebanon, hii ni miti inayotumiwa na biblia kutufundisha mafanikio ya kudumu, lakini katika somo hili leo tunauangalia zaidi MTENDE tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo

                                                                          Mtende!


  • ·         Ufahamu kuhusu mti wa Mtende
  • ·         Mambo ya kujifunza kutokana na Mtende
  • ·         Jinsi ya kusitawi kama Mtende.


Ufahamu kuhusu mti wa Mtende.

Kwa kawaida miti jamii ya mitende iko Mingi sana, kuna jamii zaidi ya 2600 ya mitende, lakini iliyo maarufu ni miwili, acacias palm tree na coconut palm tree kwa msingi huo miti jamii ya minazi ni jamii ya mitende, Mawese ni jamii ya mitende. Kama utataka kujua kwa undani kuhusu miti hii unaweza kutafuta google Palm tree/Wikipedia. Kwa Kiaramu na Kiethiopia mtende unaitwa “TAMAR” Kiarabu “Date” na wengine huiita Phoenix.

Mti huu katika Biblia umetajwa kama moja ya miti Maarufu sana ambao hutumika kuelezea Ushindi, amani na Ustawi. Katika Israel mti huu huhesimika sana na unatumika kama moja ya nembo ya Taifa ukihusihwa na Taa ya vinara Saba. Biblia inautaja mti huu kwa sababu ya mafundisho kadhaa
1.       Ushindi na amani na Ustawi  Kutoka 15:27  watu wa Mungu waliburudika baada ya Ushindi
2.       Ni Malimbuko ya Canaan Mji wa kwanza kupewa na Mungu kwa Israel Yeriko ulikuwa na mitende mingi sana na uliitwa mji wa mitende Kumbukumbu 34:1-3, Waamuzi 1:16
3.       Mtende unazungumzia Faraja na furaha na kurejeshwa 2Nyakati 28:15
4.       Katika Biblia kama mtende umekauka ilihesabika kuwa Furaha imeondokwa kwa wanadamu Yoeli 1:10-14 na ilihitajika maombi na toba kurejesha furaha hiyo
5.       Mitende ilitumika kama mapambo na sifa ya uzuri 1Falme 6:28,32, wimbo bora 7:7
6.       Ni alma ya Ushindi wa sasa na ujao Yohana 12:12-12, Ufunuo 7:9-10

Mambo ya Kujifunza kutoka na Mtende.
1.       Jamii ya mitende ni miti inayostawi popote na hustahimili ukame Inazungumza kuhusu Uvumilivu.
2.       Miti jamii ya mitende haina muda wa kubughudhi miti mingine, inakua kuelekea juu
3.       Mitende Haiweki kinyongo inapukutisha Majani ya zamani na kuzalisha Mapya Inazungumzia kusonga mbele bila kujali ni magumu gani unayapitia
4.       Miti ya mitende inawafanya watu waangalie juu, inakumbusha kuabudu, inaelekeza kwa Mungu inakumbusha watu kumtegemea Mungu.
5.       Mitende inawapa watu Burudani, inawapa watu makazi, inafunika inazungumzia Amani
6.       Miti mingi ya mitende Imenyooka Straight,Upright Inazungumzia Unyofu wa Moyo,Ayubu 1:1 na Joshua 1:7-10

Jinsi ya Kustawi kama Mtende
1.       Ishi maisha ya Haki, unaweza kujiuliza mtu wa haki ni Mtu wa namna gani
a.       Hawana muda wa Kuaibisha wengine Mathayo 1:19
b.      Hukaa katika maagizo ya Bwana bila lawama Luka 1:5-6
c.       Anakuwa Mcha Mungu Luka 2:25
d.      Utamtegemea Mungu katika hali zote ziwe njema au mbaya na hatima yako ni suhindi
Warumi 8:33-39. (Yesu alipoingia Yerusalem alishangiliwa kwa matawi ya miti ya mitetende kumaanisha Ushindi, utawala na Amani ya Mungu wa Kweli)
Mwisho wa Yote, Utaishi Maisha Marefu, ukiwa na Matunda wakati wote, na hutayumbishwa na upepo wakati wote bila kujali ukame au mvua utazaa matunda na haya ndio mafanikio ya Mtende.

KUPATA NEEMA MACHONI PA BWANA


MWANZO 6:8 “Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.”

Katika Mwanzo 6:5-7 Biblia inatufundisha kuwa Mungu aliona kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kila kusudi analoliwaza moyoni mwake ni baya siku zote na Mungu akakusudia kumfutilia mbali mwanadamu akiwa amehuzunishwa sana na mwenendo wa wanadamu wote katika nyakati hizo, lakini Katika Mwanzo 6:8 tunapata habari za kutia moyo, Kwamba Nuhu akapata neema Machoni pa Bwana!

 Gharika

Swali moja kubwa sana la kujiuliza kwetu ni kuwa kwanini Nuhu alipata neema Machoni pa Bwana? Na tunawezaje kujiweka katika mazingira yatakayotupa neema na kibali, Kwa Bwana kama ilivyokuwa kwa Nuhu? Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

1.       Maana ya Neema
2.       Kwa nini Nuhu alipata Neema Machoni pa Bwana
3.       Jinsi ya Kupata Neema machoni pa Bwana

Maana ya Neema

Kibiblia neno Neema maana yake kwa Ufupi ni Upendeleo wa Kiungu pasipo kustahili, kupewa kibali na Mungu, kuheshimiwa na Mungu, kutenganishwa na kufanywa wa kipakee na Mungu mwenyewe kupewa Upendeleo na Mungu pasipo Kustahili.
Katika Agano la Kale Neno neema liliandikwa Kiebrania “CHESED” ambalo maana yake kulindwa na Mungu kutoka katika mikono ya adui au hukumu au mitego au vita dhidi ya maadui zako au kuongozwa na Mungu katika shughuli zako za kila siku.
Katika Agano Jipya Neno neema linaandikwa kwa Kiyunani “CHARIS” ambalo maana yake ni Upendo wa Mungu wa kupita kawaida uonekanao katika vitendo vya kuwahurumia na kuwaokoa na kuwapendelea wanadamu wasiostahili kwa vyovyote vile kuhurumiwa na Mungu, ni kibali ni msamaha ni wokovu nakadhalika lakini unaopatikana kwa imani katika yeye, Na wakati mwingine ni vigumu kuielezea Neema maana iko katika uwezo, na utendaji na maamuzi ya Mungu hata kwa wale tusioweza kuwafikiria!

Kwa nini Nuhu alipata Neema Machoni pa Bwana

Biblia inaelezea sababu kadhaa ambazo zilipelekea Nuhu kupata Neema Machoni pa Bwana Mwanzo 6:9 inasema “Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu, Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake, Nuhu alikwenda pamoja na Mungu”

Ni wazi kuwa Biblia inaeleza wazi kuwa yako maswala yaliyopelekea Nuhu kupata Kibali Mbele za Mungu
1.       Tunaambiwa kuwa alikuwa mtu wa Haki, Biblia nyingine zinasema He was “Righteous” na nyingine “A just Man” ni muhimu kuyaangalia maneno hayo kwa makini ili kupata tafasiri njema ya kibiblia
Righteous neno hili katika Kamuzi ya kiingereza ya Oxford linasomeka Morally right and good yaani maana yake alikuwa na Uadilifu unaokubalika kwa Mungu alikuwa mwema na neno Just maana yake Exactly yaani aliyeweza kwenda sawa na Mungu alivyopenda. Hivyo Nuhu alikuwa Mtu wa haki, ilimaanisha alikuwa Muadilifu na aliyefanya sawa na Mapenzi ya Mungu kumbuka kuwa sio kwamba Nuhu hakuwahi kufanya dhambi, hapana Lakini hata ilipotokea amaefanya alijua Mapenzi ya Mungu, alisongeza sadaka za kuteketeza kama njia ya toba sawa na jinsi Mungu alivyoelekeza. Nataka kuwakumbusha wakristo Jambo moja la Muhimu sana kuwa mwenye haki kibiblia hakumaanishi kuwa Hakimu kwa wengine, hakumaanishi kuwanyooshea kidole wengina hakumaanishi umeitwa kuhukumu, Namkumbuka Mtumishi mmoja wa Mungu, aliyekuwa akisema “kuwa Yeye ni Mkamilifu na hana dhambi, na aliweza kuwahakikishia wengine kuwa Mtumishi wa Mungu Fulani amefanya dhambi na kuwa yeye hamuonei na anazungumza ukweli tupu na hivyo mtumishi hyo hafai” Katika mtazamo wa kitoto anaweza kuonekana mtu huyu kuwa yuko sahii na kuwa anachukizwa na dhambi na ni kweli anaishi maisha ya haki lakini Kibiblia mtu huyu si mwenye haki na hayuko sahii na wala hachukii dhambi bali anamchukia mtumishi Yule mwingine na anachokifanya ni kuharibu kibali chake kwa kuwathibitishia wengine kuwa Yule ni mwenye dhambi na kujitangaza kuwa yeye ni mwenye haki!
Lugha ya Kibiblia ya mtu mwenye haki haiku namna hiyo angalia Maandiko haya kwa makini Mathayo 1: 18 – 19 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa MTU WA HAKI, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.
Angalia Mistari hii kwa Makini Yusufu anatajwa katika biblia kuwa walikuwa MTU WA HAKI Lakini kuwa kwake mtu wa haki hakukuwa katika kusimamia Mariamu ahukumiwe kwa kupigwa mawe na kufa kwa vile alipata mimba kinyume na taratibu za kawaida na mila za kiyahudi, Biblia inasema kwa vile alivyokuwa mtu wa haki Hakutaka Kumwaibisha Mariamu.
Ndugu zangu unajiitaje mtu wa haki, huku umejichagua mwenyewe kuwa hakimu? Nuhu hakuwa mtu wa aina hivyo alikuwamtu ambaye njia zake zilifuata maelekezo ya Mungu.
2.       Tunaambiwa kuwa alikuwa mkamilifu katika Vizazi vyake, Mwanzo 6:9 Perfect in His Generation Biblia ya NASV na NIV zinatumia neno “Blameless” Asiyelaumika au asiye lawama hii haimaanishi kuwa hakuwa na dhambi tafasiri nyingine za kiingereza za Neno Blameless zinatumia neno “Blatant Faults” ambalo maana yake Matukio yanayofikirika kuwa mabaya au yanayofanyika waziwazi bila kujali kuwa watu watajisikiaje Maana yake alithibitika kuwa mwenye uadilifu mbele za watu. Aliwapendeza wanadamu wenzake.
3.       Tunaambiwa kuwa alikwenda pamoja na Mungu Walked with God Mwanzo 6:9 Nuhu alifuata uadilifu wa Babu na baba zake Mwanzo 5:24, kutembea na Mungu kunamaanisha kufuata maagizo yake hii ilijumuisha Kuabudu, kuomba yaani kuliitia jina la Bwana sawa na ilivyokuwa wakati wa kaini na Habil Mwanzo 4:3-4 na ilivyokuwa kwa Seth Mwanzo 4:26
4.       Nuhu alikuwa Mtii alifanya yote ambayo Mungu alikuwa amemuagiza Mwanzo 6:22; 7:5 Biblia inathibitisha wazi kuwa Nuhu alikuwa mtii Waebrania 11:7 alimuhofu Mungu alimcha yeye “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake”
5.       Nuhu alihubiri haki 2Petro 2:5 sio tu kuwa aliishi maisha ya haki lakini pia alihubiri haki licha ya kuishi katika ulimwengu uliozungukwa na uovu alihubiri kuwaelekeza njia ya haki alikuwa mwalimu wa haki ya Mungu kwa sababu hizi zote tulizoziona hapo juu Nuhu aliweza kuwa mtu alkiyepata kibali Machoni pa Mungu.
Jinsi ya kupata neema Machoni npa Mungu

·         Neema inapatikana kwa Imani  na ahitokana na haki tunayojipa sisis wenyewe ni lazima tuendelee kumuamini Mungu na kuishi kwa kumtegemea yeye na neno lake hata kama tunazungukwa na ulimwengu ulioharibika
·         Lazima tuendelee kuiamini injili ambayo kupitia hiyo tunatambua haki yetu ipatikanayo kwa njia ya imani katika Kristo Warumi 5:8-9, tuliomwamini Yesu tumeepushwa na Ghadhabu ya Mungu hatutahukumiwa pamoja na ulimwengu kamwe
·         Tuwe tayari kuyatii na kuyalinda na kuyahifadhi na kuyafundisha Mapenzi ya Mungu siku zote kwa vizazi vyote Lazima tuwajulishe watu wokovu, upatikanao kwa Damu ya Yesu, Tuwajulishe Neno lake kwa Ufasaha, Tuwajulishe Baraka ya Ujazo wa Roho Mtakatifu, tuwajulishe neema ya kuishi maisha ya ushindi tukimtegemea Bwana Mathayo 28:20
Hitimisho
Kwa nini tunahitaji Neema
1.       Ili tusiangamizwe pamoja na Dunia
2.       Mungu hependi mtu yeyote apotee 2Petro 3:9: 17:30-31
3.       Ni muhimu sana katima maisha yetu ya kila siku
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba Mwenyezi na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe nasi siku zote na hata milele amen

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev.Innocent Kamote.

HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU


Mathayo 27:50-54
Biblia inasema hivi “ Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.                Natazama,pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;  nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.  Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU.”  

Ndugu mpendwa ni imani yangu kuwa unalisoma neno hili si kwa bahati mbaya Mungu ana makusudi mema kwaajili yako, Hususani kwa kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, kuna faida nyingi sana zipatikanazo kutoka na kufa kwake pale msalabani, hapa nitaeleza chache tu kutokana na aya hizo hapo juu, kuna matukio kadhaa ya kutisha yaliyoambatana na kifo cha Yesu, yaliyotokea dhahiri na wazi lakini pia yakiwa na maana kubwa sana za Rohoni ambazo nataka kushirikiana nawe leo kama mjenzi mwenzangu. Matukio haya yalimfanya askari wa kikosi cha ulinzi na uongozi wa mateso ya Yesu kukiri kwamba Hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.

1.       PAZIA LA HEKALU LILIPASUKA VIPANDE VIWILI Mathayo 27:51-54.
Ni muhimu kufahamu kuwa Nyakati za Biblia Saa tisa ilikuwa saa muhimu sana katika mapokeo ya wazee wa kiyahudi saa hii ilijulikana pia kama saa ya kupunga Upepo ni saa ya utembeleo ambapo Mungu alikuwa akimtembelea Adamu na Mkewe katika Bustani ya Aden. Aidha saa hii pia ilitumiwa kama saa ya kusali na kutoa dhabihu ya jioni katika Torati ya Musa na ni katika saa hii ndipo Yesu alikata roho Mathayo 27:45. Saa hii Yesu alipokata roho ndipo matukio ya ajabu nay a kutisha yalijitokeza moja wapo likiwa ni tukio la Kupasuka kwa Pazia la Hekalu.
     Wengi wetu tunaposikia kuhusu kupasuka kwa pazia la hekalu, huwa tunawaza kuwa ni pazia la kawaida kama yale tuliyonayo majumbani mwetu Hapana! Pazia hili lilikuwa na Urefu wa futi sitini na upana wa inchi Sita yaani sawa na unene wa Tofali la block, Pazia hili lilipasuka katikati kutoka juu hata chni na kufunguka, na kusababisha mahali patakatifu sana kuonekana, Hapo ni mahali alipoingia kuhani mkuu mara moja kwa mwaka kuwaombea watu wa Mungu na yeye mwenyewe wasamehewe dhambi (Waebrania 9:1-3, Kutoka 26:33) Pazia lilitumika kutenga Mahali hapa Patakatifu pa patakatifu au Patakatifu sana ambayo ilikuwa ni sehemu ya Tatu ya mgawanyiko wa hekalu ndani zaidi, Hapo palikuwa na sanduku la agano lililokuwa likiwakilisha Uwepo wa Mungu asiyeonekana, sehemu ya pili iliitwa patakatifu hapa Makuhani walifanya huduma zao za kila siku na kulikuwa na uwa wa nje, ambapo wayahudi waliomcha Mungu walikaa na Pazia linguine liliwatenga wayahudi na Mataifa waliomcha Mungu. Mtu ambaye angeingia patakatifu au hata kupaona hukumu yake ilikuwa ni Kifo (HESABU 4:17-20). Kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka akiwa na damu ili kufanya upatanisho kati ya watu na Mungu na yeye mwenyewe (WAEBRANIA 9:6-7). Tendo la Kupasuka kwa hekalu lilikuwa jambo la kutisha sana kwa vile patajkatifu palionekana bila watu kupata madhara
Tendo hili linaashiria kuwa kila mtu duniani anao uwezo wa kumfikia Mungu na kumuomba Mungu bila ya kupitia kwa Kuhani, Mchungaji au Padre, mtu awaye yote asijiinue juu yako na kuchukua utukufu wa Mungu kwa kujifanya kuwa yeye ndiye mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu Biblia inaonyesha kuwa mpatanishi ni mmoja tu “1Timotheo 2:5” Biblia inatufundisha kuwa tunaweza kumuendea Mungu na kujipatanisha naye kupitia damu ya Yesu kristo bila msaada wa Mwanadamu mwingine,
Watu wote ni sawa Mbele za Mungu, WAEBRANIA 10:19-20; WAEFESO 2:14-18. Pazia lililopasuka linaonyesha kuwa Mungu hana upendeleo, na kuwa Mungu si wa watu fulani tu, wala si wawayahudi tu Mungu ni wa kila mmoja hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu sio wa wamarekani, au waarabu au wachina na wahindi, wala kipimo cha mafanikio ya kimwili duniani sio kipimo cha kuwa Mungu yuko pamoja nawe, Pazia linapopasuka ni udhihirisho wa Kuwa neema ya Mungu imefunuliwa kwa watu wote, kila mmoja anapaswa kufurahia na kuushangilia utukufu wa Mungu na kuabudu, tunapokosea tunaweza kumuendea Mungu kwa furaha na kujipatanisha naye bila kuanika mambo yako kwa wanadamu ambao nao wana yao na Mungu anayajua huhitaji kujidhalilisha mwendee Mungu, pazia limepasuka ni wazi kuwa nawe utatambua jinsi Yesu alivyo mwena na utakiri hakika kweli huyu alikuwa Mwana wa Mungu.

2.       NCHI IKATETEMEKA  -  Hili ni tukio linguine lililoambatana na Kifo cha Yesu pale Msalabani ni ukweli uliowazi kuwa inchi iliogopa kwa vile mtu mwema amaekufa  na huenda atazikwa na kulazwa katika ardhi ambayo ililaaniwa kutokana na dhambi za Adamu, Mara kwa mara watu walipofanya dhambi Mungu aliilaani ardhi isiwape mema wanadamu kuanzia Adamu Mwanzo 3:17,4:10-12 mara kwa mara ardhi imefanyika laana kwa wanadamu kutokana na kuzidi kwa dhambi wakati Huu Yesu anapokata Roho wema wake unaifanya ardhi ikombolewe kutoka katika mikono ya Ibilisi na laana na sasa iwe na faida kwa kila anayemtumaini ardhi iliyozea kupokea watu walioasi Hesabu 16:27-34 Sasa inampokea mtu mwema anayebadilisha mfumo zmima tabia laana ya ardhi na kutuleta katika mfumo uliobarikiwa Dunia yote sasa ni salama na Mungu anauwezo wa kukubariki popote ulipo, Kristo anauwezo wa kuwafanya adui zako kutetemeka, majini na mapepo yote na kila aina ya shida na matatizo Yesu Kristo Mnazareth aliye hai ndio kiboko cha laana, wachawi, majini, mapepo, na kila aina ya hofu za kishetani. Mungu atetemeshe adui zako wote katika maisha yako wapigwe hofu kuu watetemeke.

  1. MIAMBA IKAPASUKA  - Kifo cha Yesu kiliambatana na kupasuka kwa miamba lilikuwa ni tukio la kutisha mmno hii ilikuwa ni miamba halisi ya ardhi na nchi, lakini ni picha iliyowazi kuwa ugumu wa wanadamu katika kuamini ambao ulipandikizwa na shetani sasa uliharibiwa katika saa hii ya utembeleo wa Mungu, ni wazi kuwa hata moyo wa askari waliokuwa wanahakikisha Yesu anafia msalabani wakiwa na mioyo migumu sasa wanakiri kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, ni wazi kuwa hakuna jambo gumu la kumshinda Mungu, kila kitu kinachoonekana kuwa ni kigumu katika maisha yako ni kama mwamba kitapasuliwa kwa nguvu ya Damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani, Bwana na apasue kila kinachoonekana kuwa kigumu katika maisha yako,

  1. MAKABURI YAKAFUNUKA  - Makaburi ya Watakatifu waliojulikana Yerusalemu, yalifunuka wakati wa kufa kwa Yesu na kuleta utisho mkuu.  Hata hivyo, walitoka makaburini mwao BAADA YA KUFUFUKA KWAKE YESU kwa kuwa Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, limbuko lao waliolala (1 WAKORINTHO 15:20; UFUNUO 1:5).  Baada ya Yesu kufufuka, watakatifu hawa walifufuka nao na kuwatokea wengi Yerusalemu, Tukimwamini Yesu, kama alivyokwenda mbinguni, sisi nasi tutakwenda huko.  Kama alivyofufuka, sisi nasi tutafufuliwa katika Ufufuo wa Uzima (YOHANA 5:28-29).  Akida, yaani mkuu wa kikosi, na maaskari wenzake walipoyaona haya, NDIPO wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Nguvu ya mauti na Damu ya Yesu ni alama ya wazi mkuwa Mungu anauwezo wa kuhuisha kila kitu kwa upya katika maisha yetu, anauwezo wa kufufua, atafufua Uchumi wako, Ndoa yako, Huduma yako ,Kazi yako, biashara yako, rafiki zako, uhusiano wako,Masomo yako, mashamba yako anauwezo wa kufufua kila kilichofariki katika maisha yako.

Hatupaswi kusubiri mpaka dakika ya mwisho ndipo tumkiri Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu ni vema tukichukua uamuzi huu sasa, akidana wenzake walichelewa sana kukumkubali Yesu walisubiri alipokuwa amakata roho, Hakuna sababu ya kuchelewa kumkiri Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu ni muhimu kuamini kuwa Yeye ni mwema na ni Mwana wa Mungu na yuko tayari kutusaidia naye atakusaidia.

“Watu wengine hawajui kama Mungu yuko nawe mpaka wakione cha Moto ndipo wakiri”

Ndimi Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.