Alhamisi, 28 Januari 2016

KUPATA NEEMA MACHONI PA BWANA


MWANZO 6:8 “Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.”

Katika Mwanzo 6:5-7 Biblia inatufundisha kuwa Mungu aliona kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kila kusudi analoliwaza moyoni mwake ni baya siku zote na Mungu akakusudia kumfutilia mbali mwanadamu akiwa amehuzunishwa sana na mwenendo wa wanadamu wote katika nyakati hizo, lakini Katika Mwanzo 6:8 tunapata habari za kutia moyo, Kwamba Nuhu akapata neema Machoni pa Bwana!

 Gharika

Swali moja kubwa sana la kujiuliza kwetu ni kuwa kwanini Nuhu alipata neema Machoni pa Bwana? Na tunawezaje kujiweka katika mazingira yatakayotupa neema na kibali, Kwa Bwana kama ilivyokuwa kwa Nuhu? Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

1.       Maana ya Neema
2.       Kwa nini Nuhu alipata Neema Machoni pa Bwana
3.       Jinsi ya Kupata Neema machoni pa Bwana

Maana ya Neema

Kibiblia neno Neema maana yake kwa Ufupi ni Upendeleo wa Kiungu pasipo kustahili, kupewa kibali na Mungu, kuheshimiwa na Mungu, kutenganishwa na kufanywa wa kipakee na Mungu mwenyewe kupewa Upendeleo na Mungu pasipo Kustahili.
Katika Agano la Kale Neno neema liliandikwa Kiebrania “CHESED” ambalo maana yake kulindwa na Mungu kutoka katika mikono ya adui au hukumu au mitego au vita dhidi ya maadui zako au kuongozwa na Mungu katika shughuli zako za kila siku.
Katika Agano Jipya Neno neema linaandikwa kwa Kiyunani “CHARIS” ambalo maana yake ni Upendo wa Mungu wa kupita kawaida uonekanao katika vitendo vya kuwahurumia na kuwaokoa na kuwapendelea wanadamu wasiostahili kwa vyovyote vile kuhurumiwa na Mungu, ni kibali ni msamaha ni wokovu nakadhalika lakini unaopatikana kwa imani katika yeye, Na wakati mwingine ni vigumu kuielezea Neema maana iko katika uwezo, na utendaji na maamuzi ya Mungu hata kwa wale tusioweza kuwafikiria!

Kwa nini Nuhu alipata Neema Machoni pa Bwana

Biblia inaelezea sababu kadhaa ambazo zilipelekea Nuhu kupata Neema Machoni pa Bwana Mwanzo 6:9 inasema “Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu, Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake, Nuhu alikwenda pamoja na Mungu”

Ni wazi kuwa Biblia inaeleza wazi kuwa yako maswala yaliyopelekea Nuhu kupata Kibali Mbele za Mungu
1.       Tunaambiwa kuwa alikuwa mtu wa Haki, Biblia nyingine zinasema He was “Righteous” na nyingine “A just Man” ni muhimu kuyaangalia maneno hayo kwa makini ili kupata tafasiri njema ya kibiblia
Righteous neno hili katika Kamuzi ya kiingereza ya Oxford linasomeka Morally right and good yaani maana yake alikuwa na Uadilifu unaokubalika kwa Mungu alikuwa mwema na neno Just maana yake Exactly yaani aliyeweza kwenda sawa na Mungu alivyopenda. Hivyo Nuhu alikuwa Mtu wa haki, ilimaanisha alikuwa Muadilifu na aliyefanya sawa na Mapenzi ya Mungu kumbuka kuwa sio kwamba Nuhu hakuwahi kufanya dhambi, hapana Lakini hata ilipotokea amaefanya alijua Mapenzi ya Mungu, alisongeza sadaka za kuteketeza kama njia ya toba sawa na jinsi Mungu alivyoelekeza. Nataka kuwakumbusha wakristo Jambo moja la Muhimu sana kuwa mwenye haki kibiblia hakumaanishi kuwa Hakimu kwa wengine, hakumaanishi kuwanyooshea kidole wengina hakumaanishi umeitwa kuhukumu, Namkumbuka Mtumishi mmoja wa Mungu, aliyekuwa akisema “kuwa Yeye ni Mkamilifu na hana dhambi, na aliweza kuwahakikishia wengine kuwa Mtumishi wa Mungu Fulani amefanya dhambi na kuwa yeye hamuonei na anazungumza ukweli tupu na hivyo mtumishi hyo hafai” Katika mtazamo wa kitoto anaweza kuonekana mtu huyu kuwa yuko sahii na kuwa anachukizwa na dhambi na ni kweli anaishi maisha ya haki lakini Kibiblia mtu huyu si mwenye haki na hayuko sahii na wala hachukii dhambi bali anamchukia mtumishi Yule mwingine na anachokifanya ni kuharibu kibali chake kwa kuwathibitishia wengine kuwa Yule ni mwenye dhambi na kujitangaza kuwa yeye ni mwenye haki!
Lugha ya Kibiblia ya mtu mwenye haki haiku namna hiyo angalia Maandiko haya kwa makini Mathayo 1: 18 – 19 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa MTU WA HAKI, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.
Angalia Mistari hii kwa Makini Yusufu anatajwa katika biblia kuwa walikuwa MTU WA HAKI Lakini kuwa kwake mtu wa haki hakukuwa katika kusimamia Mariamu ahukumiwe kwa kupigwa mawe na kufa kwa vile alipata mimba kinyume na taratibu za kawaida na mila za kiyahudi, Biblia inasema kwa vile alivyokuwa mtu wa haki Hakutaka Kumwaibisha Mariamu.
Ndugu zangu unajiitaje mtu wa haki, huku umejichagua mwenyewe kuwa hakimu? Nuhu hakuwa mtu wa aina hivyo alikuwamtu ambaye njia zake zilifuata maelekezo ya Mungu.
2.       Tunaambiwa kuwa alikuwa mkamilifu katika Vizazi vyake, Mwanzo 6:9 Perfect in His Generation Biblia ya NASV na NIV zinatumia neno “Blameless” Asiyelaumika au asiye lawama hii haimaanishi kuwa hakuwa na dhambi tafasiri nyingine za kiingereza za Neno Blameless zinatumia neno “Blatant Faults” ambalo maana yake Matukio yanayofikirika kuwa mabaya au yanayofanyika waziwazi bila kujali kuwa watu watajisikiaje Maana yake alithibitika kuwa mwenye uadilifu mbele za watu. Aliwapendeza wanadamu wenzake.
3.       Tunaambiwa kuwa alikwenda pamoja na Mungu Walked with God Mwanzo 6:9 Nuhu alifuata uadilifu wa Babu na baba zake Mwanzo 5:24, kutembea na Mungu kunamaanisha kufuata maagizo yake hii ilijumuisha Kuabudu, kuomba yaani kuliitia jina la Bwana sawa na ilivyokuwa wakati wa kaini na Habil Mwanzo 4:3-4 na ilivyokuwa kwa Seth Mwanzo 4:26
4.       Nuhu alikuwa Mtii alifanya yote ambayo Mungu alikuwa amemuagiza Mwanzo 6:22; 7:5 Biblia inathibitisha wazi kuwa Nuhu alikuwa mtii Waebrania 11:7 alimuhofu Mungu alimcha yeye “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake”
5.       Nuhu alihubiri haki 2Petro 2:5 sio tu kuwa aliishi maisha ya haki lakini pia alihubiri haki licha ya kuishi katika ulimwengu uliozungukwa na uovu alihubiri kuwaelekeza njia ya haki alikuwa mwalimu wa haki ya Mungu kwa sababu hizi zote tulizoziona hapo juu Nuhu aliweza kuwa mtu alkiyepata kibali Machoni pa Mungu.
Jinsi ya kupata neema Machoni npa Mungu

·         Neema inapatikana kwa Imani  na ahitokana na haki tunayojipa sisis wenyewe ni lazima tuendelee kumuamini Mungu na kuishi kwa kumtegemea yeye na neno lake hata kama tunazungukwa na ulimwengu ulioharibika
·         Lazima tuendelee kuiamini injili ambayo kupitia hiyo tunatambua haki yetu ipatikanayo kwa njia ya imani katika Kristo Warumi 5:8-9, tuliomwamini Yesu tumeepushwa na Ghadhabu ya Mungu hatutahukumiwa pamoja na ulimwengu kamwe
·         Tuwe tayari kuyatii na kuyalinda na kuyahifadhi na kuyafundisha Mapenzi ya Mungu siku zote kwa vizazi vyote Lazima tuwajulishe watu wokovu, upatikanao kwa Damu ya Yesu, Tuwajulishe Neno lake kwa Ufasaha, Tuwajulishe Baraka ya Ujazo wa Roho Mtakatifu, tuwajulishe neema ya kuishi maisha ya ushindi tukimtegemea Bwana Mathayo 28:20
Hitimisho
Kwa nini tunahitaji Neema
1.       Ili tusiangamizwe pamoja na Dunia
2.       Mungu hependi mtu yeyote apotee 2Petro 3:9: 17:30-31
3.       Ni muhimu sana katima maisha yetu ya kila siku
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba Mwenyezi na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe nasi siku zote na hata milele amen

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima
Rev.Innocent Kamote.

Hakuna maoni: