Alhamisi, 28 Januari 2016

HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU


Mathayo 27:50-54
Biblia inasema hivi “ Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.                Natazama,pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;  nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.  Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU.”  

Ndugu mpendwa ni imani yangu kuwa unalisoma neno hili si kwa bahati mbaya Mungu ana makusudi mema kwaajili yako, Hususani kwa kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, kuna faida nyingi sana zipatikanazo kutoka na kufa kwake pale msalabani, hapa nitaeleza chache tu kutokana na aya hizo hapo juu, kuna matukio kadhaa ya kutisha yaliyoambatana na kifo cha Yesu, yaliyotokea dhahiri na wazi lakini pia yakiwa na maana kubwa sana za Rohoni ambazo nataka kushirikiana nawe leo kama mjenzi mwenzangu. Matukio haya yalimfanya askari wa kikosi cha ulinzi na uongozi wa mateso ya Yesu kukiri kwamba Hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.

1.       PAZIA LA HEKALU LILIPASUKA VIPANDE VIWILI Mathayo 27:51-54.
Ni muhimu kufahamu kuwa Nyakati za Biblia Saa tisa ilikuwa saa muhimu sana katika mapokeo ya wazee wa kiyahudi saa hii ilijulikana pia kama saa ya kupunga Upepo ni saa ya utembeleo ambapo Mungu alikuwa akimtembelea Adamu na Mkewe katika Bustani ya Aden. Aidha saa hii pia ilitumiwa kama saa ya kusali na kutoa dhabihu ya jioni katika Torati ya Musa na ni katika saa hii ndipo Yesu alikata roho Mathayo 27:45. Saa hii Yesu alipokata roho ndipo matukio ya ajabu nay a kutisha yalijitokeza moja wapo likiwa ni tukio la Kupasuka kwa Pazia la Hekalu.
     Wengi wetu tunaposikia kuhusu kupasuka kwa pazia la hekalu, huwa tunawaza kuwa ni pazia la kawaida kama yale tuliyonayo majumbani mwetu Hapana! Pazia hili lilikuwa na Urefu wa futi sitini na upana wa inchi Sita yaani sawa na unene wa Tofali la block, Pazia hili lilipasuka katikati kutoka juu hata chni na kufunguka, na kusababisha mahali patakatifu sana kuonekana, Hapo ni mahali alipoingia kuhani mkuu mara moja kwa mwaka kuwaombea watu wa Mungu na yeye mwenyewe wasamehewe dhambi (Waebrania 9:1-3, Kutoka 26:33) Pazia lilitumika kutenga Mahali hapa Patakatifu pa patakatifu au Patakatifu sana ambayo ilikuwa ni sehemu ya Tatu ya mgawanyiko wa hekalu ndani zaidi, Hapo palikuwa na sanduku la agano lililokuwa likiwakilisha Uwepo wa Mungu asiyeonekana, sehemu ya pili iliitwa patakatifu hapa Makuhani walifanya huduma zao za kila siku na kulikuwa na uwa wa nje, ambapo wayahudi waliomcha Mungu walikaa na Pazia linguine liliwatenga wayahudi na Mataifa waliomcha Mungu. Mtu ambaye angeingia patakatifu au hata kupaona hukumu yake ilikuwa ni Kifo (HESABU 4:17-20). Kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka akiwa na damu ili kufanya upatanisho kati ya watu na Mungu na yeye mwenyewe (WAEBRANIA 9:6-7). Tendo la Kupasuka kwa hekalu lilikuwa jambo la kutisha sana kwa vile patajkatifu palionekana bila watu kupata madhara
Tendo hili linaashiria kuwa kila mtu duniani anao uwezo wa kumfikia Mungu na kumuomba Mungu bila ya kupitia kwa Kuhani, Mchungaji au Padre, mtu awaye yote asijiinue juu yako na kuchukua utukufu wa Mungu kwa kujifanya kuwa yeye ndiye mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu Biblia inaonyesha kuwa mpatanishi ni mmoja tu “1Timotheo 2:5” Biblia inatufundisha kuwa tunaweza kumuendea Mungu na kujipatanisha naye kupitia damu ya Yesu kristo bila msaada wa Mwanadamu mwingine,
Watu wote ni sawa Mbele za Mungu, WAEBRANIA 10:19-20; WAEFESO 2:14-18. Pazia lililopasuka linaonyesha kuwa Mungu hana upendeleo, na kuwa Mungu si wa watu fulani tu, wala si wawayahudi tu Mungu ni wa kila mmoja hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu sio wa wamarekani, au waarabu au wachina na wahindi, wala kipimo cha mafanikio ya kimwili duniani sio kipimo cha kuwa Mungu yuko pamoja nawe, Pazia linapopasuka ni udhihirisho wa Kuwa neema ya Mungu imefunuliwa kwa watu wote, kila mmoja anapaswa kufurahia na kuushangilia utukufu wa Mungu na kuabudu, tunapokosea tunaweza kumuendea Mungu kwa furaha na kujipatanisha naye bila kuanika mambo yako kwa wanadamu ambao nao wana yao na Mungu anayajua huhitaji kujidhalilisha mwendee Mungu, pazia limepasuka ni wazi kuwa nawe utatambua jinsi Yesu alivyo mwena na utakiri hakika kweli huyu alikuwa Mwana wa Mungu.

2.       NCHI IKATETEMEKA  -  Hili ni tukio linguine lililoambatana na Kifo cha Yesu pale Msalabani ni ukweli uliowazi kuwa inchi iliogopa kwa vile mtu mwema amaekufa  na huenda atazikwa na kulazwa katika ardhi ambayo ililaaniwa kutokana na dhambi za Adamu, Mara kwa mara watu walipofanya dhambi Mungu aliilaani ardhi isiwape mema wanadamu kuanzia Adamu Mwanzo 3:17,4:10-12 mara kwa mara ardhi imefanyika laana kwa wanadamu kutokana na kuzidi kwa dhambi wakati Huu Yesu anapokata Roho wema wake unaifanya ardhi ikombolewe kutoka katika mikono ya Ibilisi na laana na sasa iwe na faida kwa kila anayemtumaini ardhi iliyozea kupokea watu walioasi Hesabu 16:27-34 Sasa inampokea mtu mwema anayebadilisha mfumo zmima tabia laana ya ardhi na kutuleta katika mfumo uliobarikiwa Dunia yote sasa ni salama na Mungu anauwezo wa kukubariki popote ulipo, Kristo anauwezo wa kuwafanya adui zako kutetemeka, majini na mapepo yote na kila aina ya shida na matatizo Yesu Kristo Mnazareth aliye hai ndio kiboko cha laana, wachawi, majini, mapepo, na kila aina ya hofu za kishetani. Mungu atetemeshe adui zako wote katika maisha yako wapigwe hofu kuu watetemeke.

  1. MIAMBA IKAPASUKA  - Kifo cha Yesu kiliambatana na kupasuka kwa miamba lilikuwa ni tukio la kutisha mmno hii ilikuwa ni miamba halisi ya ardhi na nchi, lakini ni picha iliyowazi kuwa ugumu wa wanadamu katika kuamini ambao ulipandikizwa na shetani sasa uliharibiwa katika saa hii ya utembeleo wa Mungu, ni wazi kuwa hata moyo wa askari waliokuwa wanahakikisha Yesu anafia msalabani wakiwa na mioyo migumu sasa wanakiri kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, ni wazi kuwa hakuna jambo gumu la kumshinda Mungu, kila kitu kinachoonekana kuwa ni kigumu katika maisha yako ni kama mwamba kitapasuliwa kwa nguvu ya Damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani, Bwana na apasue kila kinachoonekana kuwa kigumu katika maisha yako,

  1. MAKABURI YAKAFUNUKA  - Makaburi ya Watakatifu waliojulikana Yerusalemu, yalifunuka wakati wa kufa kwa Yesu na kuleta utisho mkuu.  Hata hivyo, walitoka makaburini mwao BAADA YA KUFUFUKA KWAKE YESU kwa kuwa Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, limbuko lao waliolala (1 WAKORINTHO 15:20; UFUNUO 1:5).  Baada ya Yesu kufufuka, watakatifu hawa walifufuka nao na kuwatokea wengi Yerusalemu, Tukimwamini Yesu, kama alivyokwenda mbinguni, sisi nasi tutakwenda huko.  Kama alivyofufuka, sisi nasi tutafufuliwa katika Ufufuo wa Uzima (YOHANA 5:28-29).  Akida, yaani mkuu wa kikosi, na maaskari wenzake walipoyaona haya, NDIPO wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Nguvu ya mauti na Damu ya Yesu ni alama ya wazi mkuwa Mungu anauwezo wa kuhuisha kila kitu kwa upya katika maisha yetu, anauwezo wa kufufua, atafufua Uchumi wako, Ndoa yako, Huduma yako ,Kazi yako, biashara yako, rafiki zako, uhusiano wako,Masomo yako, mashamba yako anauwezo wa kufufua kila kilichofariki katika maisha yako.

Hatupaswi kusubiri mpaka dakika ya mwisho ndipo tumkiri Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu ni vema tukichukua uamuzi huu sasa, akidana wenzake walichelewa sana kukumkubali Yesu walisubiri alipokuwa amakata roho, Hakuna sababu ya kuchelewa kumkiri Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu ni muhimu kuamini kuwa Yeye ni mwema na ni Mwana wa Mungu na yuko tayari kutusaidia naye atakusaidia.

“Watu wengine hawajui kama Mungu yuko nawe mpaka wakione cha Moto ndipo wakiri”

Ndimi Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: