Alhamisi, 4 Februari 2016

Kujaribiwa Kwa Imani ya Mtu aliyeokoka !



Mstari wa Msingi  1Petro 1;6-7 “Mnafurahi sana wakati huo ijapokuwa kwa kitambo kidogo ikiwa ni lazima mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu ambayo ina thamani  kuu kuliko dhahabu ipoteayo ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto kuonekane kuwa kwenye sifa  na utukufu na heshima katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo”


                                                    Mateso ya Wakristo nyakati za Karne ya Kwanza

Imani ya mtu aliyeokoka ni ya thamani kuu kuliko dhahabu. ili kuijaribu dhahabu na kuithibitisha kuwa ni dhahabu safi hupitishwa katika moto, dhahabu safi inapopitishwa katika moto mkali hutoka ikiwa inang’aa zaidi, Vivyo hivyo kwa wokovu ili kuijaribu imani ya mtu aliyeokoka na kuithibitisha kuwa ni imani safi  imani hiyo hujaribiwa katika maudhi na mateso  mtu anayestahimili na kushinda kwa kuvumilia maudhi na mateso  yoyote yakayoletwa kwake kwa sababu ya wokovu ndiye atakayeonekana mwenye sifa na utukufu na heshima wakati wa kuja kwake Yesu Kristo, Maudhi haya na mateso ni ya kawaida kwa kila mtu aliyezaliwa kiroho au aliyezaliwa mara ya pili  yaani kuokoka na hivyo hatupaswi kufikiria kuwa ni kitu kigeni Soma 1Petro 4;12 kimsingi majaribu haya hutoka kwa Yule mwovu shetani ambaye yeye anajua sana uzuri wa mbinguni kule tunako kwenda na kwa sababu hiyo anajaribu kuleta vikwazo ili tukate tamaa na kushindwa kwenda mbinguni ambako yeye alifukuzwa kutokana na wivu alio nao  hufanya juu chini ili kuhakikisha kuwa  hatuendelei na wokovu na kujiunga naye kule anakokwenda yaani motoni Mathayo 25;41, Mbinu kubwa anayoitumia ni kuleta makwazo na mateso na maudhi  ili tuvunjike moyo na hapo ndipo anapo furahia, ni muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuhakikisha kuwa tunasonga mbele  bila kujali ni vikwazo vya namna gani shetani anatuletea tukisimama imara namna hii mbele za Mungu tutakuwa tunang’aa kama dhahabu iliyopitishwa katika moto.

Waliozaliwa kwa mwili huwaudhi wale waliozaliwa kwa Roho.
Tangu zamani hata sasa watu waliozaliwa kwa mwili yaani watu ambao hawajaokoka huwaudhi na kuwatesa na kuwanenea mabaya watu waliozaliwa kwa roho yaani waliookoka hivyo sio kitu kigeni mambo haya yakimpata mtu aliyeokolewa katika nyakati hizi Wagalatia 4;29 “Lakini kama vile siku zile Yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomuudhi Yule aliyezaliwa kwa Roho ndivyo ilivyo na sasa”

Yesu Kristo alichukiwa aliudhiwa, alinenewa mabaya tena aliteswa.
Kiongozi mkuu wa wokovu wetu Yesu Kristo alikamilishwa kwa njia ya mateso Waebrania 2;10
·         Aliudhiwa Yohana 5;16
·         Walimuita ana Pepo Yohana 8;48 Yohana 7;20
·         Ulimwengu yaani watu ambao hawajaokoka walimchukia  na kutafuta njia ya kumuua Yohana 7;19 Yohana 8;37,Yohana 7;1,7.
·         Yesu alichukiwa bure yaani bila ya sababu yoyote Yohana 15;24-25
·         Walimuita maerukwa na akili Marko 3;21
Vivyo hivyo katika nyakati zetu sio jambo la kushangaza kuona tukichukiwa kwaajili ya wokovu, mtu aliyeokoka atachukiwa ataudhiwa na kuteswa na watu wasiookoka na kupewa kila aina ya majina ya dhihaka Yesu alitujulisha mambo hayo mapema Yohana 15;18-21 .

Watakatifu waliotutangulia waliudhiwa kudhihakiwa na kuteswa.
Tangu zamani watu wa Mungu walipitia maudhi na mateso
-           Yusufu aliudhiwa na kutendwa machungu Mwanzo 49;22-23
-          Musa alishutumiwa na kuteswa Waebrania 11;24-25 watakatifu wengi waliumizwa vibaya , hata kupigwa mawe na kukatwa na misumeno Waebrania 11;32-38
-          Ayubu aliyekuwa mwenye haki  na mtimilifu alichekwa sana na majirani zake na kufanywa kicheko Ayubu 12;4 alikuwa machukizo kwa ndugu zake na hata wadogo walimdharau na kumdhihaki Ayubu 19;13-19,30;9-10
-          Watakatifu nyakati za kanisa la kwanza walifanywa kuwa takataka ya Dunia 1Wakoritho 6;4-10 Mtume Paulo alipitia kila aina ya mateso na maudhi na kuendelea  katika imani 2Wakoritho 11;23-27.

Wafuasi wa Bwana Yesu ni wale wanaoendelea kulishika neno katika dhiki.
Mtu aliyeokoka ambaye ataamua kuacha wokovu kutokana na kukwepa dhiki au udhia Yesu anamuita mtu aliyepandwa  penye miamba  na hamfurahishi Mungu kabisa Mathayo 13;20-21 wafuasi halisi wa Bwana Yesu ni wale ambao watatendelea katika wokovu pamoja  na dhiki wanazokutana nazo 1Wathesalonike 1;6 “ Imetupasa kuingia mbinguni kwa njia ya dhiki nyingi” Matendo 14;21-22

Kutakuwa na maudhi toka kwa wazazi, ndugu au mume
Kama tulivyoona kutoka kwa Bwana Yesu na watakatifu waliotutangulia sisi sote hatuna Budi kuudhiwa kwaajili ya imani ya wokovu, wakati mwingine ni kawaidia kuona ndugu wazazi hata mume akichukizwa kwaajili ya wokovu, utaitwa kila aina ya majina uliyechanganyikiwa au umerukwa na akili n.k haya yasikufadhaishe ikiwa tunaitwa tumerukwa na akili ni kwaajili ya Mungu  kumbuka hata watu wa nyakati za kanisa la kwanza walipewa majina hayo 2Wakoritho 5;13, Unaweza kupigwa makofi na mumeo na fimbo kwa ajili ya wokovu au kusingiziwa mambo mengi ili kusudi uache wokovu haya yasikufanye uache wokovu ukiteswa kwa ajili ya mema huu ndio wema hasa mbele za Mungu 1Petro 2;19-21 unaweza ukapigwa pia  na ndugu au wazazi, kunyimwa fedha za ada, chakula  au fedha za matumizi kutoka kwa mumeo, na kukatishwa tamaa kwa kila namna  vumilia kwaajili ya Mungu kwani itakusaidia nini kuupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi yako ukatupwa katika ziwa la moto? Marko 8;36 unaweza kuwekwa vikao ukaambiwa unavuruga ukoo au kutishiwa kutengwa na ndugu kwaajili ya imani mpya ya wokovu uliyoipokea haya yote yatoka kwa Yule muovu ili uiache imani Yesu alikuwa wa kwanza kuokoka katika familia yake  na nduguze walikuwa bado soma Yohana 7;2-5 Baadaye nduguze nao walipofahamu siri ya wokovu waliokoka na miongoni mwao alikuwa Yakobo aliyekuwa mtume Wagalatia 1;19  Mungu amekupa wewe neema ya kuwa wa kwanza na wengine watakufuata , ni jambo la kushangaza akiwa mtu ni wa kwanza kwenda chuo kikuu katika ukoo wao asisumbuliwe lakini aliyeokoka anasumbuliwa jipe moyo ulimwenguni tunayo dhiki lakini kama Bwana Yesu alivyoshinda sisi nasi tutashinda Yohana 16;33.

Watatuita tumepotea
Baada ya kuokoka itatulazimu kuyaacha mafundisho manyonge tuliyokuwa tunayatumikia katika madhehebu yetu ya mwanzoni yasiyohubiri wokovu Wagalatia 4;9 hatuwezi kuendelea kuabudu na sanamu na kushiriki divai inayolevya katika meza ya bwana .n.k. ni kwasababu hizi na nyinginezo nyingi inatulazimu kuachana na madhehebu hayo amabayo watu wake wanapinga wokovu na kushindwa kulisimamia neno la Mungu Wagalatia 1;14-16, Tunapofanya hivyo huko sio kutangatanga kwani mitume pia walifanya hivyo ,Yesu alitufundisha kuwa kama mfanya biashara anayetafuta luliu nzuri  akiiona huuza kila alicho nacho na kuinunua Mathayo 13;45-46 dhehebu lolote ambalo sio lulu nzuri halituwezeshi kujifunza neno la Mungu hilo sio lulu nzuri , wako watu wengie wanashindwa kuyaacha kwa sababu tu ya kutafuta utukufu kwa wanadamu Yohana 12;42-43 Luka 14;33  ili tuweze kushinda katika jaribu hili la imani  tunapaswa kutambua kuwa hatujapotea  bali tumetoka upotevuni  na tunaingia uzimani yaani katika njia halisi ya kwenda mbinguni kwao wanaotuita tumepotea ni ishara ya kupotea bali kwetu sisi ni ishara ya wokovu wafilipi 1;27-28.

Tafasiri za kibiblia za maana ya mtu aliyepotea
·         Mtu awaye yote anayesitasita katika mawazo mawili kumtumikia Bwana Yesu au Kumtumikia shetani au ulimwengu huyo amepotea Waebrania 10; 37-39, 1Wafalme 18;21.
·         Mtu awaye yote asiyeijua njia ya Mungu bali anafuata mapokeo ya wanadamu Zaburi 95; 10; Marko 7;6-8.
·         Watu waliokwenda mbali na maagizo ya Mungu siyo maagizo ya wanadamu  yaani maagizo yoyote yaliyo kinyume na Neno la Mungu zaburi 119;21
·         Watu wasiyoyajua maandiko hivyo kuyapotosha  na kuyatafasiri visivyo Mathayo22;29
·         Watu waliokwenda mbali na kweli ya neno la Mungu Yakobo 5;19
·         Watu wanaotetea divai na kumsingizia Mungu kuwa amehalalisha  wakati mbele za Mungu ni matapiko na uchafu Isaya 28;7-8
·         Watu wanaoacha kulisikia na kulifuata Neno la Mungu  linalofundishwa na watumishi wanaoisimamia kweli yote ya injili 1Yohana 4;6
·         Watu ambao injili imesitirika kwao yaani imefichwa na Ibilisi ambaye ndiye mungu wa dunia hii anayefanya kazi ndani yao wakimtumikia na kusema kuwa hakuna wokovu 2Koritho 4;3-4
·         Watu wasiopata maonyo yaliyo katika neno la Mungu bali hutafuta kufarijiwa  hata kama maisha yao hayaendani sawa na injili Mithali 5;23
·         Watu wanaoiacha njia iliyonyooka yaani Neno la Mungu na kufuata njia zao wenyewe 2Petro 2;15.
·         Watu wanaofuata vinyago vyao yaani dhehebu Fulani au mwinjilisti fulani badala ya neno la Mungu Ezekiel 44;10.

Watatuambia kwamba tumedanganywa na manabii wa uongo;
Baada ya kuchukua uamuzi wa kuifuata kweli ya injili  na hatimaye kuamua kuokoka  na vilevile kukutana na nguvu za Mungu zilizobadilisha maisha yetu kabisa  baada ya kufanyiwa maombezi na watumishi wa Mungu  walio tofauti na viongozi wetu wa kidini wa zamani  tuliokuwa tumewazoea ndipo sa utasikia maneno ya kukukatisha tamaa  kuwa hizi ni nyakati za mwisho na manabii wengi wa uongo watatokea  na kudanganya watu wengi Mathayo 24;11 ikiwa hatufahamu maana ya manabii wa uongo ni rahisi  kuanza kubabaika na kuwa na mashaka kwa msingi huo ni muhimu kufahamu  maana ya manabii wa uongo  tangu mapema katika hatua za mwanzoni kabisa za wokovu wetu.

Neno nabii maana yake ni nini? Ni muhimu kufahamu kwanza kuwa Biblia ililetwa kwetu katika lugha kuu mbili Kiebrania na kiyunani na sehemu chache kiaramu  kwa msingi huo Neno nabii katika Kiswahili limetokana na neno la kiebrania Nabiy ambalo maana yake ni Yeye anenaye maneno ya mwingine kwa kuongozwa na Roho wake huyo aliyemtuma  kutokana na maana hiyo sasa tunapata maneno nabii wa kweli na nabii wa uongo nabii wa kweli wa Mungu huyanena maneno ya Mungu siyo maneno yao wenyewe hawazungumzi kwa mapenzi yao  wenyewe  2Petro 1;21 hunena maneno kutokana na uongozi wa Roho matakatifu ambaye Yesu alisema atatutia katika kweli nyote Yohana 16;13 Kweli ni nini? Kweli ni neno la Mungu Yohana 17;17 kwa maana hiyo nabii wa kweli huubiri neno la Mungu kila wanalolifundisha huthibitishwa kwa neno la Mungu  kwa kusema kama yanenavyo maandiko 1Wakoritho 15;3-4 wao watahubiri wokovu na kuonyesha wazi kuwa Mungu anataka tuishi maisha matakatifu hapa duniani Zaburi 16;3 manabii wa uongo watadai kuwa hakuna kuokoka duniani watasema haiwezekani kuishi maisha matakatifui ukiwa duniani  tofauti na Biblia inavyotufundisha kuhusu wokovu ona Tito 2;11-12, manabii wa uongo watafundisha watu kuwa Mariamu ni mama wa Mungu wakati neno linasema ni majakazi yaani mtumwa wa kike Luka 1;38 hawa ndio manabii wa uongo watafundisha watu kusali kwa kutumia Rozari wakati biblia haifundishi aina hiyo ya maombi, watafundisha kuwa mtu akifa anakwenda pugatori au toharani. Watafundisha kuomba wafu au kuwaombea wafu na kutumia mvinyo au divai katika meza ya bwana haya ndiyo mafundisho ya manabiiwa uongo watazuia watu wasioe au kuolewa na kuacha kula aina Fulani za chakula hawa ndio wanaofundisha uongo kinyume na Biblia.

Wajibu wetu tunapoudhiwa au kuteswa na kudhihakiwa kwaajili ya wokovu.
·         Kuendelea na wokovu na kuwaacha waseme huku sisi tukikaa kimya Ayubu 21;3
·         Hatupaswi kurudishia matukano au kulipiza  kisasi bali tujikabidhi kwa Mungu katika maombi yanapotukuta hayo 1Petro 2;23,Warumi 12;18-19 Inatupasa kuushinda ubaya kwa wema warumi 12;20-21
·         Inatupasa kuwapenda na kuwaombea wanaotuudhi na kututesa Mathayo 5;44-45
·         Hatupaswi kuwaogopa wauao mwili kisha wasiwezi kuiua roho inatupasa kumuogopa Mungu awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu Mathayo 10;28,1Petro 3;14
·         Kamwe tusijaribu kutafuta amani kwa  kwa kuamua kuacha wokovu na kufuata masharti yao  huko ni kumkana Yesu Mathayo 10;33-39 wakiona tumesimama imara baada ya mateso yao mwishoni hawataendelea kutuonea na tutawavuta  katika wokovu.
·         Hatupaswi kumtii mzazi au mume  wanapotuelekeza kufanya mambo yaliyokinyume na wokovu au neno la Mungu  kama kuacha kuomba kusali na kuacha wokovu, laki tuyatii yale yote yalio sawa na neno la Mungu  Tito 3;1;Waefeso 6;1 Mke anapaswa kumtii mume sawasawa na maagizo ya Neno la Mungu  Waefeso 5;24 hata hivyo tunahitaji sana kumuomba Mungu hekima katika wakati kama huu wengi wamepoteza ndoa zao kwa sababu ya kukosa hekima na kujikuta wakiachika huu sio mpango wa Mungu  Biblia inatuagiza kuwajibu kwa upole na kwa hofu soma 1Petro 3;15 “ Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari ya tumaini lililo ndani yenu lakini kwa upole na kwa hofu, ni jawabu la upole linaloweza kugeuza hasira  na sio neno liumizalo au linalochochea Mithali 15;1
·          Inatupasa kuamini kwamba hatimaye Mungu atatuepusha na maudhi hayo kwani kwa kila jaribu kuna mlango wa kutokea, Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo yote inatupasa kudumu katika maombi bila kukoma 1Wakoritho 10;13, Zaburi 34;19 1Petro 5;10-11 1Wathesalonike 5;17-18.

Dhehebu linalosimamia Neno la Mungu vema hunenwa vibaya.
Kumbuka kuwa dhehebu linalosimamia kweli ya wokovu hunenwa vibaya kila mahali hivyo hatupaswi kubabaika tunapoona pale tunapohamia pananenwa vibaya kila mahali na kuzushiwa kila aina ya uongo hii ni kawaida hata kanisa la kwanza lilinenwa vibaya kila mahali Matendo Matendo 28;22. 

Aina nyingine ya kujaribiwa kwa imani
Wakati mwingine mara baada ya kuokoka kunaweza kutokea hali mbaya ya kibiashara, kiasi cha fedha kupungua namaisha kuwa magumu unaweza pia kufukuzwa kazi, kuibiwa au kuandamwa na hali ambazo ni nzito na sio za kawaida hii ni kwa sababu ya Shetani kujaribu kufanya kila namna ili uiache imani hii yote ni kujaribiwa kwa imani yako 2Wakoritho 4;8-11 ni mitihani tu lakini tunapoendelea kushikilia misimamo Mungu hufurahishwa nasi na mambo huwa shwari

Thawabu kubwa kwa wote washindao baada ya kujaribiwa kwa imani yao
Kuna thawabu kubwa kwa kila mtu ambaye ataendelea na wokovu pamoja na kujaribiwa kwa imani yake huko ndiko kweli kumpenda Mungu Yeye akupendaye wakati wa dhiki ndiye rafiki Mathayo 5;10-12, 1Petro 4;12-14 jambo la kuangalia ni kwamba siyo sahii kuudhiwa na kuteswa kwa sababu ya kufanya dhambi huko siyo kujaribiwa kwa imani 1Petro 4;15-16.

Yeye Ashindaye !



Mstari wa msingi Ufunuo 21;7 “Yeye ashindaye atayarithi haya nami nitakuwa Mungu wake naye atakuwa mwanangu”
                                                                       Yeye ashindaye


Safari ya mbinguni ni safari ya mashindano;

Mara baada ya kuokoka unapaswa kuwa na Ufahamu kuwa umeingia katika mashindano  ni yeye atakayeshinda ndiye atatakayeipokea taji  ya milele na milele  kila siku katika wokovu itakuwa ni siku ya mashindano  na vita lakini ni lazima tushinde  na kuumaliza mwendo kwa kuilinda imani 2Timotheo 4;7-8

“Nimevipiga vita vilivyo vizuri mwendo nimeumaliza imani nimeilinda baada ya hayo nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana muhukumu mwenye haki atanipa siku ile wala si mimi tu bali na watu wote waliopenda kufunuliwa kwake”

Kwa msingi huo ni lazima kuvipiga vita vya imani maana pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu Waebrania 11; 6 maisha ya wokovu ni maisha ya imani na kumtegemea Mungu katika kila jambo katika maombi na neno la Mungu kinachotakiwa katika mashindano haya ni kujizuia katika kila jambo linalokuja kinyume na mapenzi ya Mungu 1Koritho 9;25 “Na kila ashindanaye katika michezo  hujizuia katika yote  basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo bali sisi tupokee taji isiyoharibika”

Unaweza kushangaa kwamba wakati unajiandaa kwenda ibadani ndipo wageni wanakujia tena wa muhimu ili usihudhurie mafundisho kumbuka haya ni mashindano ni vita na inakupasa kupambana wageni waambie twendeni kanisani pamoja kwa nini waje wakati unakwenda kanisani? Wakati mwingine siku za ibada ndo kunatokea kila aina ya vikwazo na vizuizi jua hiyo ni vita na kuwa adui yetu shetani yuko kazini kutuzuia tusiende kubarikiwa kupitia maneno ya Mungu, uwe radhi kwenda ibadani hata kama ni mbali au kama hauna nauli na utashangaa Baraka za Mungu zinamiminika kwako.

Siku zote kuanzia sasa lenga kukua zaidi kiroho na katika wokovu usikose vipindi vya mafundisho kanisani  kila unapopata nafasi soma Biblia na kufanya maombi japo mafupi mafupi  kwamba bwana Yesu akusaidie kudumu katika wokovu na kushindana  1Timotheo 6;12 “Piga vita vile vizuri vya imani  shika uzima ule wa milele ulioitiwa ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi” Tumia bidii uliyo nayo usiwe mlegevu katika kujifunza  uwe na bidii yote Nunua daftari la kuandikia mafundisho yote na kuyatendea kazi na uwe na tabia ya kuyapitia , uliza lolote kwa viongozi ambalo hujalielewa vema  Warumi 12;11 “ Kwa bidii si walegevu mkiwa na juhudi katika roho zenu mkimtumikia Bwana” lolote utakalojifunza lisiiishie katika dafatari bali ulifanyie kazi kwa vitendo , usiwe msikiaji wa neno tu bali mtendaji Yakobo 1;22-24  ni muhimu kustahimili siku hadi siku  kwani tukistahimili tutamiliki pamoja naye 2Timotheo 2;12 Kama tukimkana yeye naye atatukana sisi.

Hatimaye tusikubali kabisa kurudi nyuma katika wokovu tulioupokea usimkane Yesu halafu naye aje atukane sisi, shindana hadi mwisho, Yako mengi mmno ambayo utazidi kujifunza kila siku kanisani yashike na kuyatendea kazi , siku chache zijazo nawe utakuwa mwalimu ukiwafundisha watu wengine  waliookoka nyuma yako  ili nao wasimame katika wokovu, simama  kiume  ni lazima ushinde katika jina la Yesu, zidi kwenda kanisani kwa mafundisho mengine zaidi kumbuka Ufunuo 2;7 Yeye ashindaye  nitampa kula matunda ya mti wa uzima ulio katioka Bustani ya Mungu. Ubarikiwe sana Amen.

Mfahamu Adui Shetani !



Mstari wa msingi 1Timotheo 5;15 “Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka nyuma na kumfuata shetani”
Mtu aliyeokolewa anaweza kugeuka nyuma na kumfuata shetani kama hatamfahamu shetani ni nani na Fikra zake 2Wakoritho 2;11 Shetani ni adui yetu Luka 10;19 Ni adui wa watu waliookoka kama alivyo adui wa Mungu Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vikuu vifuatavyo;-


·         Historia ya shetani
·         Mbinu za shetani   anazozitumia kutuletea upinzani

Historia ya shetani
 Shetani hapo kwanza hakuwa adui wa Mungu, Yeye aliumbwa na Mungu kama walivyoumbwa malaika wengine, alifanywa kuwa malaika mkuu na kupewa utukufu mwingi na Mungu. Hatimaye alikuwa na tamaa na kiburi cha kutaka kuwa sawa na Mungu na hata kumpindua Mungu aliyemuumba. aliwashawishi malaika wachache kupigana na majeshi ya Mungu na matokeo yake walishindwa vibaya na kutupwa nje ya mbinguni hivyo akawa siyo malaika mkuu tena aliyekuwa na jina Lucifer ambalo maana yake ni mwenye kutoa mwanga kama nyota ya alfajiri na tangu wakati huo aliitwa shetani Ezekiel 28;13-19, Ufunuo 12;7-9 Isaya 14;12. Jina shetani maana yake ni  Adui , mpinzani, mshindani mwenye kuleta vizuizi kazi zake kubwa ziko sawa na majina yake ni adui wa watu wa Mungu ni mshindani ,huleta upinzani  na vizuizi kwa watu wa Mungu hususani waliookolewa  katika hali ya chuki kabisa  ili ikiwezekana waache imani  na njia ya wokovu  ya kweli ya kumfikisha mtu mbinguni  Yeye anaijua njia hiyo ya kweli lakini kwa kusudi anataka kupotosha watu wamuache Yesu ambaye ndiye njia na kweli na uzima  ni shetani anaye waambia watu kuwa hakuana wokovu  na kuwa watu wanaweza kumuona Mungu bila Yesu  na kwa kutumia udanganyifu anawakosesha wengi.Matendo 16;16-18 Shetani anamfahamu Yesu kuwa ni  mwana wa Mungu  na kuwa ndiye wa kuhubiriwa  na kuleta wokovu na kuwa wanaohubiri injili ya wokovu wana nguvu kubwa  na ufalme wa Mungu unawasubiri Marko 3;11 Matendo 19;13-16.

     Shetani baada ya kuasi mbinguni yeye na malaika zake  wamekwisha kuhukumiwa  na mahali pao ni katika ziwa la moto wa Milele na hawana nafasi ya kutubu tena Mathayo 25;41 Ufunuo 20;10  na kwa sababu uzuri wa mbinguni anaufahamu  anachokifanya ni kuwadanganya watu  na kushindana na watu waliookoka  ili wamfuate na kuteswa pamoja naye katika ziwa la moto milele, anaweza kuwafanya waliookoka kuwa na wokovu vuguvugu na hatimaye waweze kutapikwa Ufunuo 3;15-16 safari ya mbinguni ni kama mpira wa miguu katika dunia ambapo mtu anayekwenda kufunga goli huzuiwa kwa namna zote hata kupigwa ngwala  na viatu ilimradi tu asifanikiwe kufunga goli 

Mbinu za shetani anazozitumia kutuletea upinzani.
Ni muhimu kufahamu kuwa shetani wakati wote haji katika njia ambayo utafahamu kuwa ni shetani  kwani kwa njia hiyo watu watashituka upesi , Mara nyingi huja kama malaika wa nuru akiwatumia wachungaji wengine wanaosema kuwa wameokoka  au watu wanaosema kuwa wameokoka  kututoa katika kweli ya wokovu 2Wakoritho 11;14-15 baada ya kushindwa kuuzuia wokovu wako unapokuwa umeokoka shetani kama Farao huwa hakati tama yeye na majeshi yake hujaribu tena na tena  kukurudisha nyuma kama farao alivyo jaribu kuwafuatailia wana wa Isarael shetani atajaribu kufanya hivyo ili turudi nyuma na kumtumikia yeye tena Kutoka 14;5-8 wakati ulipookoka shetani alishindwa  vibaya  kushindana na nguvu za Yesu aliye Bwana na mwokozi wetu na akasalimu amri Kutoka 12;30-36 kwa msingi huo shetani atatumia mbinu mbalimbali kukufanya uache wokovu hususani ukiwa bado mchanga  katika wokovu kwani kuua kitu kichanga ni rahisi zaidi alijaribu kuwaua Yesu na Musa katika uchanga wao Kutoka 1;15-22,2;1-10, Mathayo 2;13 mbinu zote za shetani zinajumuishwa katika kukushawishi uuache wokovu Biblia inasema katika 1Nyakati 21;1 “Tena shetani akasimama akamshawishi Daudi kuwahesabu Israel “ Kushawishi ni kubadili nia ya mtu kwa kumuumbia mawazo mengine  juu ya jambo kinyume na mawazo yale aliyokuwa nayo  mwanzoni kabla ya kushawishiwa shetani  atatumia mbinu mbalimbali katika kushawishi ikiwemo

1.       Kukushawishi yeye mwenyewe ili uache njia ya kweli
Unaweza kuona katika akili yako kunaumbika mawazo yaliyo kinyume na wokovu ulioupokea na hatimaye kukufanya usipige hatua yoyote ya ziada tangu ulipookolewa  mawazo ya aina hii yanatokana na shetani, endapo utayafuata mawazo hayo unakuwa umefuata mawazo ya ibilisi na mawazo yako mwenyewe  na huo ni uasi kwa Mungu Isaya 65;2 Ni lazima ukatae kuafikiana na kila wazo lililo kinyume na njia ya wokovu.

2.       Atatumia watu kukushawishi uiache njia ya kweli
Mara baada ya wokovu utaona watu wanaoandamana kukushawishi kurudi dhambini utashangaa marafiki wa zamani  wakikujia na kukualika katika uvutaji wa sigara bangi na ulevi na dhambi nyinginezo  watakuambia kuwa wana hela nyingi na wahahitaji watu wa kutumia nao , utashangaa watu wanakulaumu kuwa umepotea au kukucheka na kudharau uamuzi wa Busara ulioamua na wanaweza hata kukutenga au kukuchukia kabisa  inakupasa kuwa mwangalifu watu wakikuvuta kurudi dhambini  usiwasikilize wala usiwajali na ujitahidi kujiepusha nao ili wasije wakainyonya nguvu yako  ya wokovu mistari ifuatayo ni muhimu kwako Mithali 1;10-16, Torati 13;6-8 Mithali 24;1 na Hosea 7;8-9

     Shetani atatumia kila njia kuhakikisha kuwa unakosa mafundisho ili ubaki umedumaa bila kukua katika wokovu ili hatimaye urudi nyuma na kuiacha kweli ya wokovu kwa sababu hiyo  utaweza kuona siku za mafundisho  ndio wageni wanakutembelea  nyumbani pamoja na hayo usikubali kuacha kwenda kanisani  na kukaa na wageni  kama watataka uende nao itakuwa vema.

 Wakati mwingine unaweza kuona kama unafanya biashara majira ya siku na saa za ibada ndio biashara inachanganya sana hilo pia ni kusudi la ibilisi kukufanya utafute mapato na kukosa ibada, aidha watu wanaweza kukushawishi na kulaumu kuwa siku hizi umekuwa bise huonekani vyovyote iwavyo ni heri ukose kipato lakini usiikose mbingu Yohana 12;25 ni muhimu kujikana nafsi unaweza kukutana na watu wanaokudhihaki kuwa siku hizi mbona maswala ya ibada yanazidi au watu wanaomsema vibaya mchungaji wako au askofu wako  na kutaka kukutoa katika imani  jihadhari  wajibu watu hao kama nikodemu alivyowajibu wale waliokuwa wakimsema vibaya Yesu mchungaji wetu Yohana 7;45-51 unaweza kuona pia siku za mafundisho na ibada ndio homa zinacharuka na hali za kujisikia vibaya au kuona uvivu au kuumwa kichwa au tumbo la kuhara n.k kemea hali hiyo na chukua hatua ya imani kwenda ibadani utashangaa jinsi ambavyo shetani atakavyokimbia na hali hiyo kutoweka katika dakika usiyoijua Yakobo 4;7,1Petro 5;8-9.

Usimuamini au kumfuata mtu awaye yote ambaye anasema ameokoka lakini anakuvunja moyo kwenda ibadani au kuendelea na wokovu au kuenda katika kanisa linalohubiri wokovulililo tofauti na kanisa au dini yako ya kwanza isiyohubiri wokovu fahamu kuwa huyo ni mpinzani anayetaka kukutoa kwenye kweli akiwa amekuja kama malaika wa nuru au mtumishi wa haki 2wakoritho 11;14-15

Kwa ujumla jihadahari na jambo lolote lile linalokunyima kuenda katika ibada bila sababu za msingi au kukukosesha wokovu, shetani anajua kuwa ukipata mafundisho utaimarika na kuwa askari utakayemdhibiti vilivyo

Usikubali kwenda kwenye mikesha ambayo itakufanya kesho yake ushindwe kulisikia Neno la Mungu vema, Neno la Mungu linauwezo wa kumbadilisha mtu wala usikubali mialiko ya kuhubiri huku wewe ukiwa mchanga kiroho kwani kwa sasa unahitaji kujifunza neno kwanza  na kuwa na muda mrefu wa kujifunza neno kabla ya kuhudumu 1Tomotheo 1;7 Yakobo 3;1 kila jambo linalokuzuia kusikia au kujifunza neno likatae na kujihadhari nalo usikubali kuiacha kweli ya wokovu kaa katika imani uliyoipokea na kudumu katika fundisho hii ndio itakuwa siri ya kukufanya uwe mshindi na zaidi ya mshindi Warumi 8;35-37.